Jumapili, 31 Agosti 2025

Tazama nimekupa mlango uliofunguliwa!


Ufunuo 3:7-8 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye. Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.”



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa katika maisha yetu kama wanadamu ziko nyakati ambazo tunaweza kujikuta katika dimbwi la mawazo na hali ya kutokufahamu kutokana na mambo kadhaa katika maisha yetu kutokuenenda kama tunavyotaka au kufikiri,  na mara nyingine tumejikuta hatuelewi au kuwa kama watu waendao gizani kwa kupapasa kwa sababu tu ya kutokuyajua mapenzi ya Mungu katika maisha yetu, tunaweza kudhani kuwa labda tuko katika maisha yaliyopoteza mwelekeo, au yaliyopoteza tumaini, na kukosa msaada ya kiungu au hata wa kibinadamu wakati mwingine unaweza kuwaza hata kufikiri kuwa labda una laana, au kuna mtu amekuroga kwa sababu tu huoni mwelekeo wa hatima ile unayoitamani katika maisha yako huu ni ule wakati ambapo tumekwama na kila mlango wa mpenyo tuliojaribu katika maisha yetu unaonekana kama umefungwa au umepata kile ambacho hakilingani na akili yako au mtazamo wako au kile ulichokitarajia! Mlango umefungwa! Unaweza kufikiria kuwa umekataliwa kila mahali na ukadhania kuwa hustahili na ni kama Mungu hausiki na maisha yako tena lakini Mungu anajua uliposimama na ameahidi kufanya kitu kwako!

Isaya 22:19-22 “Nami nitakusukuma na kukutoa katika mahali pako, naye atakushusha utoke hapa usimamapo. Na itakuwa katika siku ile nitamwita mtumishi wangu Eliakimu, mwana wa Hilkia; nami nitamvika vazi lako, nitamtia nguvu kwa mshipi wako, nami nitamkabidhi yeye mamlaka yako; naye atakuwa baba kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa nyumba ya Yuda. Na ufunguo wa nyumba ya Daudi nitauweka begani mwake; yeye atafungua wala hapana atakayefunga; naye atafunga wala hapana atakayefungua.”

Leo tutachukua muda kutafakari mambo haya yanayotokeza katika maisha yetu kwa kuliangalia neno la Mungu linasema nini pale tunapohisi kuwa labda mlango huu umefunga, labda jaribu hili halitatoka, na pale unapohisi umekwama, leo tutajikumbusha kuwa neno la Mungu linaonyesha wazi kuwa hakuna mwanadamu anaweza kukufunga wala mchawi anayeweza kuzuia Baraka zako kwa sababu tunaye Mungu mwenye mamlaka ya kufunga na kufungua milango na hakuna mtu anayeweza kufunga alichokifungulia wala hakuna anayeweza kufungua alichokifunga, Yeye ndiye anayesema leo Tazama nimekupa mlango uliofunguliwa! Na tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Maana ya mlango uliofunguliwa.

·         Tazama nimekupa mlango uliofunguliwa.

·         Na huyu ndiye mwenye mamlaka ya milango yote.   

      

Maana ya mlango uliofunguliwa.

Kwa kawaida neno mlango uliofunguliwa  katika maandiko una maana pana sana neno uliofunguliwa katika lugha ya kiebrania linatumika neno “Pāthah”  na neno lingine la kiebrania ni “Gālāh” kwa kiyunani “AnoigōKwa hiyo neno Mlango uliofunguliwa kwa kiyunani linasomeka “Anoigō thura” neno hili lilitumika kumaanisha kupata mpenyo, kufunguliwa macho, kufunguliwa kinywa, kufunguliwa masikio, kufunguliwa mlango, kupewa macho ya kuona, kufunguliwa mbingu, kuwekewa wazi, kupata nafasi, kutoka, na kupata muelekeo, kwa sababu hiyo Mlango katika lugha ya kiroho unawakilisha Nafasi maalumu anayoitoa Mungu kwa mwanadamu kwaajili ya huduma, kusonga mbele, kutoka katika changamoto inayokukabili katika maisha kwa msaada wa Mungu  na anayesababisha milango hiyo ifunguke ni Mungu mwenyewe na hufanya hivyo kwa watu wake ambao pia ni kondoo wa malisho yake! Yesu alikwisha kutangaza kuwa yeye ndio mlango wa kondoo, awaye yote ambaye anataka upenvyo wa aina yoyote katika maisha yake hawezi kutoka bila kupitia Yesu!

Yohana 10:7-10 “Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. Wote walionitangulia ni wevi na wanyang'anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho. Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.”

Kwa msingi huu katika maisha yetu tunapoona kuwa kuna mambo hayaendi katika maisha yetu ya kila siku hatupaswi kuzimia moyo kwa sababu uko mlango uliofunguliwa kwaajili yetu na yuko mwenye mamlaka ya kufunga na kufungua, hakuna mtu awaye yote anayeweza kuzuia usiolewe, hakuna mtu anayeweza kuzuia usifanikiwe, hakuna mtu anayeweza kuzuia usizae, hakuna mtu anayeweza kuzuia usipate kazi, hakuna mtu anayeweza kuzuia usifanikiwe, hakuna mtu anayeweza kuzuia usipone,  hakuna mtu anayeweza kuzuia usijenge hakuna mtu anayeweza kuzuia usiendelee mbele, hakuna anayeweza kuzuia usifaulu! Mungu wetu sio binadamu, hakuna mnyanyasaji asiyekuwa na mwisho, hakuna adui asiyekuwa na mwisho, hakuna hali ngumu isiyokuwa na mwisho kwa sababu uko mlango uliofunguliwa kwaajili yako, Mungu amekupa mlango uliofunguliwa wengine wanaweza kuona giza lakini sivyo itakavyokuwa kwako wewe na mimi wewe na mimi neno la Mungu linatuambia kuwa tunao mlango ulio wazi nguvu ya mafanikio iko kwetu na Mungu anayeweza kutufanikisha yuko kwetu na yeye ndio mlango wenyewe!

Tazama nimekupa mlango uliofunguliwa

Ni muhimu kuelewa kuwa wakati tunapopitia changamoto na majaribu mbalimbali moja ya kazi kubwa anayoifanya Shetani au adui ni kutufanya tusione njia, yaani ni kutupofusha tusipate ufunuo wa mapenzi na makusudi ya Mungu na hii ndio inayotufanya tufadhaike na kuvunjika moyo au kukata tamaa kwa sababu ya hali unayoipita kwa wakati ule, lakini Neno la Mungu linasema kuwa kwa kila jaribu uko mlango wa kutokea, na Mungu amekupa mlango uliofunguliwa!

2Wakorintho 4:3-4 “Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.”

1Wakorintho 10:13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.”    

Ufunuo 3:7-8 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye. Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.”

Mungu ametupa mlango uliofunguliwa, hakuna mtu wa Mungu ambaye anaweza kukwama milele, Mungu anapofunga mlango mmoja huwa anafungua mlango mwingine, kila mwanadamu anayejitahidi kukuzibia ataula wa chuya kwa uvivu wa kuchambua, hajui nguvu na uweza wa Mungu wetu sisi tunao ufunguo wa Daudi, kila mahali palipofungwa tutatoboa tu, ni lazima ufahamu ya kuwa wakati mwingine unapoona mambo yanakwama sio lazima iwe umerogwa wewe haurogeki sio lazima uwe una laana wewe haulaniki, lakini wakati mwingine ni sauti ya Mungu inafunga mlango mmoja ili kufungua mwingine, na ukisikiliza katika ulimwengu wa roho kwa makini mlango uko wazi kwako na kwaajili yako!

Matendo 16:6-10 “Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia. Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakatelemkia Troa. Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie. Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari Njema.”

-          Walimfanyia fitini Yusufu, walimtupa shimoni, walimuuza utumwani Misri, walimfitini tena na alitupwa gerezani, badala ya mema ilionekana kana kwamba mambo yanamuendea vibaya lakini katika mpango wa Mungu, Mungu alikuwa anatengeneza mlango uliofunguliwa wa kumuweka Yusufu katika ufalme

 

Mwanzo 41:40-44 “Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe. Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri. Farao akavua pete yake ya muhuri mkononi mwake, akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake. Akampandisha katika gari lake la pili alilokuwa nalo. Na watu wakapiga kelele mbele yake, Pigeni magoti. Hivyo akamweka juu ya nchi yote ya Misri. Farao akamwambia Yusufu, Mimi ni Farao, na bila amri yako, mtu asiinue mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri.”

 

-          Walimdharau Daudi na kufikiri ya kuwa hafai kabisa kuwa miongoni mwa watoto anayeweza kuwa mfalme na kupakwa mafuta, alipigwa vita kila mahali, hakukubaliwa na baba wala hakukubaliwa na kaka zake, na mfalme aliyekuwepo madarakani alimkataa na kutaka kumuua, alimwinda katika mapango na kujaribu kwa kila jinsi na kila namna kumzuia asiwe mfalme, njia ilionekana kuwa ngumu milango ilionekana kufunga lakini Mungu alikuwa na sababu, hatimaye Yeye akawa ndiye mtu sahihi aliyeupendeza Moyo wa Mungu na aliyewaongoza Israel kwa ukamilifu wa moyo, Mungu alimpa Daudi mlango uliofunguliwa!

 

Zaburi 78:70-72 “Akamchagua Daudi, mtumishi wake, Akamwondoa katika mazizi ya kondoo. Nyuma ya kondoo wanyonyeshao alimwondoa, Awachunge Yakobo watu wake, na Israeli urithi wake. Akawalisha kwa ukamilifu wa moyo wake, Na kuwaongoza kwa busara ya mikono yake.”

 

-          Walimfukuza Hajiri na Ishamel na kuwatupilia jangwani, waliishiwa na mkate na waliishiwa na maji na hatari ya kifo ilikuwa ikiwakabili, Hajiri alilia na Ishamel alilia Lakini Mungu ni Mungu ambaye hakuwa na upendeleo aliwafungulia mlango wa uhai hata walipokuwa wametaka tamaa jangwani Mungu alijidhihirisha kuwa ni Mungu mwenye kujali ni Mungu mwenye upendo, ni Mungu asiye na upendeleo, Ni Mungu anayebariki na ni Mungu mwenye kukuza sana aliahidi kumfanya Ishamel kuwa Taifa kubwa hakuna upendeleo kwa Mungu!

 

Mwanzo 21:10-21 “Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa. Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako. Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde. Akakaa katika jangwa la Parani; mama yake akamtwalia mke katika nchi ya Misri.”

Ndugu yangu Mungu ametupa mlango uliofunguka, haijalishi sasa unapitia hali ya namna gani, au umesimama katika hali inayoonekana kuwa ni ngumu na kama kila kitu hakionekani kuwa sawasawa huna sababu ya kulalamika wala kunung’unika  Mungu anaweza kukufungulia mlango wa afya yako, masomo yako, visa yako, safari yako, biashara zako, cheo chako, mshahara wako kuongezeka, mapato yako kuchanua, kilimo na biashara kufanikiwa, walikuwa wakifukia visima vya Isaka lakini aliendelea kuchimba vingine hakuna mtu anaweza kukufungia mlango, njia za Mungu sio kama njia za wanadamu wala mawazo yake sio kama mawazo yetu yeye huweza kufanya njia pasipo na njia leo Mungu amenituma nikukumbushe ya kuwa uko mlango uliofunguliwa kwaajili yako, ndoa yako njema inakuhusu, mchumba anakuja na yule aliyeondoka haikuwa mpango wa Mungu Mungu atakufungulia mlango mwingine, kazi iliyopotea haikuwa mahali pako sahihi Mungu amekupa mlango ulio wazi Mungu amekupa mlango uliofunguliwa na hakuna awezaye kuufunga. 

Na huyu ndiye mwenye mamlaka ya milango yote

Ufunuo 3:7 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye.”

Yesu Kristo ndiye aliyejitangaza ya kuwa anao ufunguo na kuwa mwenye kufunga ni yeye na mwenye kufungua ni yeye na akifunga hapana afunguae na akifungua hakuna awezaye kufunga, huna sababu ya kulalamika wala kulia unapoona mambo hayaendi, Yesu anabatiza kwa Roho Mtakatifu, Yesu anamwaga neema juu ya neema, Yesu ndiye anayebariki, Yesu ndiye anayefungua kurasa mpya wakati nyingine inapofunga yeye anayo mamlaka yote, Yesu sio tu anafungua milango yote lakini pia anazo funguo za mauti na kuzimu hakuna wa kukupeleka kaburini bila ruhusa yake na uwezo wake, watu wanaweza kukuona umekwama lakini Yesu anakuona unaelekea anakotaka uko mlango na unaweza kuwekwa wazi kwako katika ndoa yako, katika maisha yako, katika magonjwa yako, katika familia yako, katika uponyaji wako, acha kuangalia milango iliyofungwa mwangalie mwenye funguo mwangalie Yesu ambaye yeye ana mamlaka na wokovu wako, na uponyaji wako na mafanikio yako ukimwangalia yeye kutoboa utatoboa katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai kataa kuona giza, kataa mahangaiko mwombe Bwana akufungulie mlango, Mwambie nipe kuona Malango uliofunguliwa nionapo giza naye amekupa mlango uliofunguliwa tayari!

Ufunuo 1:17-18 “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.”     

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: