Yohana 3:30-31 “Basi hii furaha yangu
imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua. Yeye ajaye kutoka juu,
huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena
mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.”
Utangulizi:
Moja ya watu waliokuwa na uwezo mkubwa
sana wa kumuelezea vizuri Yesu Kristo na kumtambulisha kwa watu ni pamoja na
Yohana Mbatizaji, huyu ni moja ya manabii waliopata neema ya ajabu sana ya sio
tu kutabiri kuhusu ujio wa Maisihi, lakini kuonyesha moja kwa moja mubashara
kuhusu Yesu Kristo, Mjadala kuhusu Yesu ulikuja baada ya watu kumuhoji kuhusu habari za Yesu ambaye
watu wengi walikuwa wameanza kumuendea, huku wengine wakiendelea kuonyesha
heshima kubwa kwa Yohana Mbatizaji wakifikiri kwa kuwa alitokea nyikani na alikuwa
kama Eliya kimtazamo na kimuonekano kwamba huenda ndiye angefaa kuwa masihi,
Hata hivyo yeye aliendelea kuwasisitizia kuwa huyo anayefanya wanafunzi wengi
ndiye masihi na yeye hana budi kupungua ili huyo aweze kuzidi
Yohana 3:26-31 “Wakamwendea Yohana,
wakamwambia, Rabi, yeye aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Yordani, yeye
uliyemshuhudia, tazama, huyo anabatiza na watu wote wanamwendea. Yohana
akajibu, akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka
mbinguni. Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya kwamba nalisema, Mimi siye Kristo,
bali nimetumwa mbele yake. Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini
rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti
yake bwana arusi. Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali
mimi kupungua. Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia,
asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni
yu juu ya yote.”
Yohana anamuelezea Yesu kwa
ufunuo mkubwa ambao sio rahisi mwanadamu wa kawaida kuwa nao, Yeye anamuelezea
Yesu kama Yeye ajaye kutoka juu, ana
anamfunua hivyo kwa umati mkubwa wa watu akimaanisha kuwa Yesu sio nabii wa
kawaida wala Mwalimu wa kawaida wa duniani bali huyu ashuka kutoka mbinguni, Yohana
alikuwa akiuthibitishia ulimwengu kuwa Yesu ana mamlaka kubwa sana kuliko hata
yeye mwenyewe, Yesu ana asili ya uungu na sio ya kibinadamu tu, Kila Mwalimu wa
kweli wa neno la Mungu ni lazima awe na uhakika wa Yesu ni nani na awe anajua
kumuelezea vizuri, na kutokujaribu kuchukua nafasi yake na kumleta Yesu mzima
mzima kwa jamii ili jamii imkubali na kupata masaada kutoka kwake, leo tutachukua
muda kuijadili kauli hii ya Yohana Mbatizaji Yeye ajaye kutoka juu! kwa
kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Asili ya
Yesu Kristo.
·
Yeye
ajaye kutoka juu.
·
Yeye
ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote!
Asiili ya Yesu Kristo!
Yohana ni moja ya manabii wa
ajabu sana na wa tofauti mno, Kabla ya wanafunzi wa Yesu kutuelezea kwa kina
kuwa Yesu Kristo ni nani Yohana mbatizaji ni mtu wa kwanza kutuelezea ukuu wa
Yesu Kristo Yeye anamuelezea Yesu kama ambaye asili yake si ya dunia kama
alivyo Yohana na manabii wengine na sisi, Yesu anaelezewa na Yohana Mbatizaji
kama ambaye asili yake ni ya mbinguni yaani Yeye ajaye kutoka juu!
Yohana 3:31 “Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu
juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya
duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.”
Yohana anatufunulia hapa kwamba
Yesu amekuja kutoka mbinguni na hivyo asili yake sio ya dunia, ukweli huu
unakubalina na mafundisho ya kibiblia na maneno ya Bwana mwenyewe kwamba Yeye
amekuwepo kabla hata ya Ibrahimu baba wa Imani ya kiyahudi hajakuwepo, Yeye
Ibrahimu asijakuwako mimi niko (“Before
Abraham was born I am!”) yaani kabla Ibrahimu hajazaliwa mimi niko alisema
Yesu Kristo mwenyewe.
Yohana 8:56-58 “Ibrahimu, baba yenu,
alishangilia kwa vile atakavyoiona siku yangu; naye akaiona, akafurahi. Basi
Wayahudi wakamwambia, Wewe hujapata bado miaka hamsini, nawe umemwona Ibrahimu?
Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko.”
Neno la Mungu vilevile
linathibitisha ya kuwa Yesu Kristo kabla ya kuvaa mwili wa kibinadamu alikuweko
tangu milele kama neno la Mungu na alihusika katika kuumba ulimwengu na hapa
Duniani alijifunua kwetu kwa utukufu kama wa mwana pekee wa Mungu.
Yohana 1:1-3,1 4 “Hapo mwanzo kulikuwako
Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo
alikuwako kwa Mungu.Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika
cho chote kilichofanyika. 14 Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi
tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa
neema na kweli.”
Kwa msingi huo neno la Mungu
linabainisha wazi kuwa Yesu Kristo hakuwa mwanadamu wa kawaida, mamlaka yake na
uwezo wake ulikuwa uko juu ya kawaida ya kibinadamu kama anavyoeleza Nabii
Yohana mbatizaji, ufahamu huu kwa kweli sio ufahamu wa kawaida ni lazima uwe
umefunuliwa na Roho Mtakatifu kumfahamu na kumtambua Yesu kuwa ni mtu wa namna
gani, mapema kabla ya kuzaliwa kwake nabii Mika aliyeishi karibu wakati sawa na
nabii Isaya alieleza mpaka mahali atakapozaliwa Masihi na kuutaja mji
atakaozaliwa kuwa ni Bethelehemu, lakini kama haitoshi alieleza kuwa mtu huyu
asiyekuwa wa kawaida asili yake imekuwepo tokea enzi na enzi.
Mika 5:2 “Bali wewe, Bethlehemu Efrata,
uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja
atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani
za kale, tangu milele.”
Nabii Isaya akitabiri kuhusu kuja
kwa masihi Yaani Bwana Yesu yeye naye alitabiri na kuonyesha kuwa Yesu atakuwa
mfalme wa ajabu na baba wa milele, na Mungu mwenye nguvu, kwa ujumla maandiko
yanamuelezea Yesu kwa namna pana zaidi kuliko watu wengine wanavyoweza kufikiri
au kukosoa kwa kukosa maarifa Isaya anasema:-
Isaya 9:6-7 “Maana kwa ajili yetu mtoto
amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake;
Naye ataitwa Jina Lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele,
Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe,
Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa
hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio
utakaotenda hayo.”
Kwa msingi huo sio kuwa wakristo
wanamkuza tu Yesu Kristo na wengine wanadhani kuwa tunakufuru, lakini ni ukweli
ulio wazi manabii walimfunua Yesu Kristo kwetu pamoja na mitume wake ambao
kwaasili ni wayahudi wanatuwekea wazi kuwa Yesu Kristo asili yake ni Mbinguni
na kuwa alikuwako huko toka milele na sio hivyo tu tunaelezwa kuwa alikuwa
Mungu na kwa kuja kwake duniani ililikuwa swala la unyenyekevu mkubwa na
kujidhili au kujishusha kwa namna isiyoweza kufananishwa au labda kuwa sawa na
mtumwa ingawa yeye alijijua kuwa hakuwa mtu wa kawaida, Paulo mtume analiweka
hilo sawa katika waraka wake kwa Wafilipi ona:-
Wafilipi 2:5-8 “Iweni na nia iyo hiyo ndani
yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna
namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha
kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa,
akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu,
alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.”
Kwa sababu hiyo Yohana alimtambua
Yesu kuwa alikuwa mwanadamu wa viwango vingine, mwanadamu asiyekuwa wa kawaida
alisema huyu ni mkuu mno akionyesha ukuu wa Yesu Kriso katika kiwango ambacho
yeye mwenyewe alisema hastahili hata kulegeza gidamu za viatu vyake:-
Luka 3:16-17 “Yohana alijibu akawaambia
wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko
mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; yeye atawabatiza
kwa Roho Mtakatifu na kwa moto; ambaye pepeo lake li mkononi mwake, naye
atausafisha sana uwanda wake, na kuikusanya ngano ghalani mwake, bali makapi
atayateketeza kwa moto usiozimika.”
Yohana anatusaidia wanazuoni
kutokumchukulia Yesu Kristo kama mtu wa kawaida au kama manabii wengine, Yesu Kristo
hafananishwi wala kulinganishwa na kitu chochote, kujishusha kwake na unyenyekevu
wake wa kukubali kudhalilishwa msalabani kusiwanye wanadamu wawe na nafasi ya
kumdhalilisha na kumkufuru badala yake wanapaswa kuogopa na kumchukulia kwa
heshima kubwa kwani ni zawadi ya kipekee ambayo Mungu amewapa wanadamu ili
tuweze kuokolewa Yesu yeye asili yake ni juu, yaani yeye ametokea Mbinguni
ambako alikuweko tangu mwanzo, Yeye yuko juu y asana kuliko ufalme wowote,
mamlaka yoyote, usultani wowote, enzi yoyote, na jina lolote litajwalo
ulimwenguni humu na vitu vyote viliumbwa kwa njia yake na kwaajili yake
Waefeso 1:17-21 “Mungu wa Bwana wetu Yesu
Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua
yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi
lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo;
na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya
utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika
wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko
ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si
ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia;”
Wakolosai 1:16-19 “Kwa kuwa katika yeye
vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana
na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka;
vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya
vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili,
yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba
awe mtangulizi katika yote. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae;”
Kwa msingi huu kwa uchunguzi wa
kimaandiko utakubaliana nami kwamba Yesu, Yu Juu ya yote kama yanenavyo
maandiko!
Yeye ajaye kutoka juu
Wako watu katika nyakati za leo
hususani watu wanaoendesha mijadala ya kidini ambao humchukulia Yesu kwa mchezo
mchezo na wala hawataki kumuelezea Yesu Katika namna ambayo maandiko
humuelezea, mijadala ya aina hii, Nabii Yohana mbatizaji aliizima kabisa kwani
wanazuoni wa wakati huo walitaka kumlinganisha Yeye (Yohana mbatizaji) au nabii
(Yahaya bin Zekaria) na Masihi Bwana Yesu, wao walimtazama kwa mtazamo wa nje
tu na kuona kama Nabii Yohana alionekana wa maana sana labda huenda hata kuliko
Yesu, kwa sababu yeye alitokea Porini/Nyikani/jangwani na alivaa nguo za ngozi
na singa za ngamia akila nzige na asali, akijiepusha na maisha ya kawaida ya
mitaani akiishi nyikani, kujidhabihu kwake kulionekana kimtazamo kuwa alikuwa
nabii kweli kweli na maarufu sana labda
huenda kuliko hata Masihi, Yesu alivyokuja na mtindo wake wa maisha pengine pia
na kuonekana kwake kama kijana mdogo wa miaka 30 hivi, Yohana alitahadharisha
kuwa Yesu sio wa kulinganishwa naye kumlinganisha yeye Yesu ni sawa tu na msimamizi
wa harusi na Bwana harusi mwenyewe, aliwathibitishia kuwa maagizo yote
anayoyatoa Yesu ni muhimu akasikilizwa kwa kuwa Yeye ni wa mbinguni na Yohana
ni wa duniani, Yesu ni wa mbinguni anatoka juu na yuko juu ya manabii wengine
wote ambao asili yao ni ya dunia na wananena mambo ya duniani Lakini sivyo
ilivyo kwa Yesu Kristo ambaye asili yake ni juu na ananena maswala kutoka
mbinguni!.
Yohana 3:25-31 “Basi palitokea mashindano
ya wanafunzi wa Yohana na Myahudi mmoja juu ya utakaso.Wakamwendea Yohana,
wakamwambia, Rabi, yeye aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Yordani, yeye
uliyemshuhudia, tazama, huyo anabatiza na watu wote wanamwendea. Yohana
akajibu, akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka
mbinguni. Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya kwamba nalisema, Mimi siye Kristo,
bali nimetumwa mbele yake. Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini
rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti
yake bwana arusi. Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali
mimi kupungua. Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia,
asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni
yu juu ya yote.”
Yohana alikuwa akiwahakikishia
watu kuwa mamlaka ya Yesu sio ya kawaida
na kuwa iko juu kwa namna ambayo haiwezi kulinganishwa na mamlaka
nyingine yoyote, alisema tena sifa za Yesu zinapaswa kuzidi na za kwake yaani Yohana
mbatizaji zinapaswa kupungua, Yesu ni mwenye mamlaka na nguvu na hekina na
akili na ujuzi na maarifa na ufahamu kuliko mtu mwingine yeyote, hakuna
mamlaka, wala serikali, wala usultani
wala uongozi, wala bosi wala mwenye mamlaka wala mwenye serikali inayoweza
kuzidi mamlaka aliyonayo Yesu Kristo, Yesu mwenyewe anathibitisha kuwa ameshuka
kutoka mbinguni na anatakeleleza mapenzi ya baba yake wa mbinguni:-
Yohana 6:32-38 “Yesu akawaambia, Amin,
amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba
yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. Kwa maana chakula cha
Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima. Basi
wakamwambia, Bwana, sikuzote utupe chakula hiki. Yesu akawaambia, Mimi ndimi
chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye
hataona kiu kamwe. Lakini naliwaambia ya kwamba mmeniona wala hamwamini. Wote
anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. Kwa
kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi
yake aliyenipeleka.”
Yesu anadhihirisha wazi katika
neno lake ya kuwa kama ile mana ilivyoshuka kutoka mbinguni na kuwapa uzima wa
muda baba za wayahudi huko jangwani ambao kimsingi walikufa, yeye alikuwa anamaanisha
kuwa ile mana ilikuwa ni ishara ya kuwa baba anawapa chakula kishukacho kutoka
mbinguni na kuwa kama wakimuamini hawataona njaa tena na ya kuwa hawatakufa
bali watakuwa na uzima wa milele wakati watu waliona kuwa yeye ni mwana wa
seremala tu na wakidhani kuwa masihi atashuka moja kwa moja kwa jinsi ya
kuonekana kimwili kama atakavyokuja mara ya pili duniani, Lakini masihi alikuja
bila wao kuelewa. Ujio wa Yesu Kristo kutoka juu mbinguni una faida kubwa sana
katika maisha ya wanadamu wote kama tutatambua kuwa Yesu yuko juu ya yote na
kumuamini kuna faida lukuki ambazo tutafaidika kwa imani hii, Neno ajaye kutoka
juu katika kiyunani linasomeka “Erchomai
anōthen esti epanō” ambapo
maneno mawili “Anōthen na epanaō”
yana maana “From the beginning he is over
on” yaani mwenye mamlaka au mwenye cheo cha juu cha kijeshi tangu mwanzo,
hii inazungumzia kuwa katika mamlaka za kijeshi Yesu ni jemadari tangu mwanzo
na ni jemadari aliyeko juu ya mambo yote ya mbinguni na duniani, anaweza
kukupigania vita ya aina yoyote ile, na anaweza kuagiza au kuamuru majeshi ya
malaika kama amiri jeshi mkuu.
Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote!
Yohana sio tu katika majibu yake
anataka kuonyesha kuwa Yesu asili yake sio ya dunia na kuwa Yesu asili yake ni
kutoka juu, lakini pia anakazia kuwa yuko juu ya yote, Yohana anapotuelezea
kuwa Yesu yuko juu ya yote anafunua faida kubwa zenye maana pana sana kwa kila
mwamini ulimwenguni, hii inaonyesha kuwa Yesu ana mamlaka yote mbinguni na
duniani, ana heshima ya kipekee na nafasi ya kwanza katika kila jambo, Yesu
kuwa juu ya yote ina maana gani na faida gani hasa
-
Ana
mamlaka yote mbinguni na Duniani – Mathayo 28:18 “Yesu
akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.”
maana yake Serikali yake iko juu ya serikali zote, dola yake iko juu ya
dola zote, mamlaka ya kimwili na kiroho
iko na yeye, kama ni kukata rufaa unakata kwake, kama ni hospitali ya rufaa
yeye ndio hospitali ya mwisho, kama umeonewa yeye ndiye yuko juu ya wale
waliokuonea ana mamlaka yote kama kuna watu wanajitukuza na kujiiinua juu yako
basi kumbuka ya kuwa Yeye ana mamlaka kubwa kuliko hiyo yu juu ya yote, chochote
kinachojiinua dhidi yako kikumbushwe kuwa Yuko aliye juu zaidi yake
-
Jina lake
lina nguvu kuliko majina yote – Wafilipi 2:9-11 “Kwa
hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;
ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani,
na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa
utukufu wa Mungu Baba.”
-
Hukumu
yote ya wanadamu imewekwa chini yake – Matendo 17:31 “Kwa
maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule
aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika
wafu.”
Yohana 5:22-23
“Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana
hukumu yote; ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu
Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka.”
-
Sisi tu
warithi pamoja naye – Warumi 8:16-17 “Roho mwenyewe
hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu
watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam,
tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.”
-
Yeye
ndiye anayehusika na ufufuo – Yoahan 11:25 “Yesu
akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa,
atakuwa anaishi;”
-
Akifunga
hakuna afunguaye, akifungua hakuna afungaye – Ufunuo 3:7-8 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya
ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi,
yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye.
Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao
hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno
langu, wala hukulikana jina langu.”
-
Yeye
ndiye mwanzo na mwisho Alfa na Omega – Ufunuo 1:8 “Mimi
ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako
na atakayekuja, Mwenyezi.”
-
Ana
mamlaka ya kusamehe dhambi – Marko 2:5-10 “Naye
Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu,
umesamehewa dhambi zako. Na baadhi ya waandishi walikuwako huko, wameketi,
wakifikiri mioyoni mwao, Mbona huyu anasema hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye
kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu? Mara Yesu akafahamu rohoni mwake
kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri hivi mioyoni
mwenu? Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au
kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana
wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza)”
-
Ana
mamlaka dhidi ya shetani - Wakolosai 2:14-15 “akiisha
kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na
uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua
enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika
msalaba huo.”
Yesu Kristo kuwa juu ya yote
maana yake ana mamlaka ya kila kitu mbinguni na duniani na kuwa kila kitu kiko
chini yake, yeye ni chanzo cha wokovu wetu wa mwili nafsi na roho, ni kiboko ya
mahitaji yetu yote na ni mwenye nguvu dhidi ya adui zetu wote chochote kinachojiinua
juu yako kikumbushe tu kuwa Yeye ajaye kutoka juu yu juu ya yote, mashetani,
mapepo, wenye mamlaka wenye uwezo, wanajimu na wachawi, wasihiri, wapiga ramli,
waganga wa kienyeji, waonevu, magonjwa
na mateso ya aina mbalimbali yakumbushwe tu kuwa Yeye ajaye kutoka juu huyo yu juu ya yote, dhuruba yoyote
ikikusumbua, mateso yoyote yakikusumbua, magonjwa yoyote yakikusumbua, majungu
yoyote yakikusumbua, mtu yeyote akikusumbua, mwenye mamlaka yeyote akizingua, changamoto
zozote zikikusumbua unapaswa kuzikumbusha tu kuwa AJAYE KUTOKA JUU HUYO YU JUU YA YOTE, Kristo Yesu sio wa kulinganishwa
na nabii yeyote, wala mtume yeyote wa dini yeyote wala mwanafalsafa yeyoye,
wala mwasiasa yeyote, wala msanii yeyote, wala kiongozi yeyote, watambulishe na
kuwajulisha kuwa ajaye kutoka juu huyu yu juu ya yote, kama liko jambo
linajitukuza juu yako, linaonekana kuwa gumu kwa sababu yoyote, lina jina la kutisha, linakuogopesha,
linakunyima usingizi, linakudhoofisha, iwe ni ndoa, watoto, kazini, biasharani,
mdeni na kadhalika wote washitakie kwa Huyu mwamba aliye juu ya yote, aliye juu
ya majeshi yote anayeweza kukushindia vita yoyote ambaye asili yake sio ya
dunia huyu amekuja kutoka juu ana mamlaka yote kwa faida ya mahitaji yetu yu
juu ya yote! Yesu kuwa juu ya yote maana yeke tunaweza kuliitia jina lake kwa
changamoto zozote zile maana yeye yuko juu ya hizo, haupaswi kuogopa, haupaswi
kulia, haupaswi kuhuzunika, haupaswi kusikitika tunaye aliye juu ya yote!
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!
0718990796
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni