Jumatatu, 4 Agosti 2025

Mungu anapoonekana kuwa mbali!


Zaburi 34:18-19 “Walilia, naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.”




Utangulizi:

Wengi wetu tunapokuwa tunapita katika nyakati ngumu za majaribu ya aina mbalimbali, huwa tunakumbwa na mawazo ya kufikiria kuwa huenda Mungu yuko mbali sana, na wako watu wengine duniani hufikiri kuwa haiwezekani kabisa kuwa na ukaribu na Mungu wala hatuwezi kamwe kuwa na ushirika na yeye, na kwa bahati mbaya hata unapokosea watu wengine hufikiri kuwa Mungu hawezi kuwa karibu na wewe na wanadhani Mungu atakuwa amekuacha, Kila mwanadamu aliyeumbwa na Mungu,Mungu huwa karibu naye lakini zaidi sana aaminiye na wale waliovunjika moyo! au wanaojinyenyekeza.


·         Mungu anapoonekana kuwa mbali!

·         Mungu si Mungu aliye mbali

·         Jinsi ya kuwa karibu na Mungu


Mungu anapoonekana kuwa mbali!

Hisia za kuhisi kuwa Mungu yuko mbali zinaweza kuchangiwa na sababu mbalimbali katika maisha ya mwanadamu, wakati mwingine kwa sababu ya mapungufu ya kibinadamu tuliyonayo, Upweke, na changamoto mbalimbali katika maisha zinapokuwa zimetusonga mioyo yetu na hisia zetu huhisi kuachwa na kufikiri kuwa Mungu yuko mbali na wakati mwingine kwa sababu ya kushuka kwa Imani zetu na tafasiri zetu za kimazingira, tunapolemewa na mawazo, mashaka, hofu na kukosa usalama tunaanza kufikiri kuwa Mungu yuko mbali nasi au ametuacha, na wakati mwingine kudhani kuwa wala hajibu maombi yetu pale anapochelewa kutoa msaada, ndani yetu kuna kilio mbona umeniacha

Zaburi 22:1-11 “Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu? Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu Na wakati wa usiku lakini sipati raha. Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli. Baba zetu walikutumaini Wewe, Walitumaini, na Wewe ukawaokoa. Walikulilia Wewe wakaokoka, Walikutumaini wasiaibike. Lakini mimi ni mdudu wala si mtu, Laumu ya wanadamu na mzaha wa watu. Wote wanionao hunicheka sana, Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao; Husema, Umtegemee Bwana; na amponye; Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye.Naam, Wewe ndiwe uliyenitoa tumboni, Ulinitumainisha matitini mwa mama yangu. Kwako nalitupwa tangu tumboni, Toka tumboni mwa mamangu ndiwe Mungu wangu. Usiwe mbali nami maana taabu i karibu, Kwa maana hakuna msaidizi.”

Zaburi 10:1-2 “Ee Bwana, kwa nini wasimama mbali? Kwani kujificha nyakati za shida? Kwa kiburi chake asiye haki mnyonge anafuatiwa kwa ukali; Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza.”

Mungu huonekana kuwa mbali tunapougua na akachelewa kuleta uponyaji, huonekana kuwa mbali tunapolia na akachelewa kuleta msaada, anaonekana kuwa mbali tunapopatwa na aibu ambayo yeye angeweza kuizuia, anaonekana kuwa mbali wakati adui zetu wanapofurahi na kutucheka ilihali yeye yupo, anaonekana kuwa mbali tunaposhutumiwa kwaajili ya uhusiano wetu na Yeye na Yeye haonyeshi nguvu zake upesi, anaonekana kuwa mbali wakati tuna shida na haonekani kufanya kitu au anapochelewa kufanya jambo kwa wakati wa moyo wa kibinadamu unapotamani kufanyiwa ni kawaida tu ya kibinadamu, kiroho na kisaikolojia kufikiria kuwa Mungu amemuacha kwa sababu wakati mwingine tunahitaji msaada wa haraka kisha yeye akaonekana kuwa amechelewa!

Yohana 11:1-6 “Basi mtu mmoja alikuwa hawezi, Lazaro wa Bethania, mwenyeji wa mji wa Mariamu na Martha, dada yake. Ndiye Mariamu yule aliyempaka Bwana marhamu, akamfuta miguu kwa nywele zake, ambaye Lazaro nduguye alikuwa hawezi. Basi wale maumbu wakatuma ujumbe kwake wakisema, Bwana, yeye umpendaye hawezi. Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo. Naye Yesu alimpenda Martha na umbu lake na Lazaro.Basi aliposikia ya kwamba hawezi, alikaa bado siku mbili pale pale alipokuwapo.”

Yesu alipewa taarifa mapema kwamba rafiki yako umpendaye hawezi yaani anaumwa sana Lakini hata hivyo Yesu hakufanya haraka kwenda maandiko yanaonyesha aliendelea kukaa siku mbili zaidi akiendelea na shughuli zake, hii iliwaletea fadhaa sana Martha na Mariamu, kwani walidhani kuwa kama Yesu angewahi hali isingelikuwa mbaya kiasi kile lakini Yesu alionekana kuchelewa, huwa unajisikiaje Mungu anapokawia kujibu maombi yako, unajisikiaje anapokawia kushughulika na yale yanayokusibu, au pale anapoonekana kana kwamba hashughulikii lolote huonekana kana kwamba alikuwa mbali hapo moyo wa mwanadamu husikitika na kuona kama kwamba Mungu yuko mbali!

Yohana 11:20-26 “Basi Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alikwenda kumlaki; na Mariamu alikuwa akikaa nyumbani. Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yo yote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa. Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka. Martha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho. Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?

Mungu alionekana kuwa mbali na familia ya Matha na Mariamu hata pamoja na kuwa ilikuwa ni familia ambayo Yesu alikuwa anawapenda sana, na ni ukweli ulio wazi kuwa kulikuwa na sauti ya lawama kutoka kwa Martha kuwa kama ungelikuwepo hapa ndugu yangu hangalikufa, yaani Yesu hakuwa karibu na kwa sababu alikuwa mbali amechelewa kujihusisha na taabu ya familia hii, huu ndio mtazamo wetu, wengi wetu pale Mungu anapoonekana kuchelewa kutoa mrejesho wa kile tunachokitarajia kutoka kwake, Mungu huonekana kuwa mbali. Lakini Mungu si Mungu aliye mbali!

Mungu si Mungu aliye mbali.

Neno la Mungu linazungumza kinyume na hisia zetu, lenyewe tofauti na mawazo yetu linakanusha kuwa yeye hayuko mbali na Mungu anajitambulisha katika neno lake kuwa ni Mungu aliye karibu:-

Yeremia 23:23-24 “Mimi ni Mungu aliye karibu, asema Bwana, mimi si Mungu aliye mbali. Je, mtu ye yote aweza kujificha mahali pa siri, nisimwone? Asema Bwana. Je! Mbingu na nchi hazikujawa nami? Asema Bwana.”          

Mungu anaweza kufikiwa na mtu yeyote na wakati wowote anaweza kuona hata yale tunayoyawaza kwa siri na kufikiri mioyoni mwetu yeye ni Mungu ambaye yuko mahali kote kwa wakati mmoja  na anaweza kuonekana na kupatikana kwa yeyote yule na anasikia, tunajua tu kuwa hatuwezi kumpangia kile tunachotaka hatuwezi kuingilia mapenzi yake lakini tunaweza kuliitia jina lake na akasikia na kujidhihirisha katika maisha yetu.

Zaburi 145:17-19 “Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote, Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote. Bwana yu karibu na wote wamwitao, Wote wamwitao kwa uaminifu. Atawafanyia wamchao matakwa yao, Naye atakisikia kilio chao na kuwaokoa.”

Mungu ameahidi katika neno lake katika torati ya kuwa hatatuacha atakuwa pamoja nasi na hatatuacha kamwe kwa sababu hiyo hatupaswi kuogopa lolote wala hatupaswi kuacha kumuamini

Kumbukumbu 31:6 “Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha.”

Mungu amehahidi katika neno lake kutoka kwa manabii ya kuwa tusigope yeye ni Mungu wetu na kuwa atatutia nguvu na kutusaidia na kutushika kwa mkono wake wa kuume, hivyo tusifadhaike katu

Isaya 41:10-13 “usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi, Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia.”

Mungu wakati wote anatamani kuingilia kati mfumo wa maisha yetu pale tunaposumbuliwa na yuko tayari kutoa msaada, faraja nguvu, muongozo, uponyaji na hata kuingilia kati kama kuna vita na kukulipia kisasi unachopaswa wewe ni kumkaribia yeye na kuwa na agano naye kupitia mwanaye Yesu Kristo!

Yakobo 4:7-10 “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za Bwana, naye atawakuza.”

Jinsi ya kuwa karibu na Mungu

Neno la Mungu sio tu linatujulisha na kutuhimiza kuwa Mungu ni Mungu aliye karibu lakini vile vile linatufundisha namna ya kumkaribia Bwana Mungu wetu kwa sababu hiyo pale tunapjisikia na kudhani kuwa Mungu ametuacha yako mambo ya kufanya ili tuweze kumkaribia naye yuko tayari kwaajili yetu!

-          Tubia maovu na kuachana na dhambi – Isaya 59:1-2 “Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.”

 

-          Mwamini Yesu aliye kuhani mkuu – Kazi ya kuhani mkuu ni kuomba kwaajili ya makosa ya watu wake kwa sababu hiyo kabla hata hujaanza kufanya lolote Yesu hutuombea kwa baba na kwa sababu hiyo tunayo haki kwa damu yake kumwendea baba kwa ujasiri

 

Waebrania 10:19-23 “Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake; na kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu; na tukaribie wenye moyo wa kweli, kwa utimilifu wa imani, hali tumenyunyiziwa mioyo tuache dhamiri mbaya, tumeoshwa miili kwa maji safi. Na mlishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu;”

 

1Yohana 2:1-2 “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.”

 

-          Mungu anataka tumrudie yeye – Ni maagizo ya neno la Mungu na wito wa Mungu mwenyewe kwamba tumrudie yeye, na tunapofanya hivyo yeye naye anaturudia sisi, hii ni sawa tu na kusema Mungunanataka tumkaribie Yeye na Yeye atatukaribia sisi na ameonyesha ni kwa namna gani tunaweza kumkaribia au kumrudia

 

Zekaria 1:3-4 “Basi, uwaambie, Bwana wa majeshi asema hivi, Nirudieni mimi, asema Bwana wa majeshi, nami nitawarudia ninyi, asema Bwana wa majeshi. Msiwe ninyi kama baba zenu, ambao manabii wa zamani waliwalilia, wakisema, Bwana wa majeshi asema hivi, Rudini sasa, na kuziacha njia zenu mbovu, na matendo yenu maovu; lakini hawakusikia, wala kunisikiliza, asema Bwana.”

 

Yoel 2:12-14 “Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya. N'nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa Bwana, Mungu wenu?                      

 

Kama ulikuwa na hisia ya kuwa Mungu yuko mbali, Neno la Mungu linakukumbusha kuwa Mungu ni Mungu aliye karibu na hayuko mbali na ni Mungu ambaye anajishughulisha sana na mambo yetu, sio tu kuwa Mungu yuko Karibu lakini kwa wale waliomwamini Yesu na kumkubali kuwa Bwana na mwokozi katika maisha yao wafahamu kuwa anaishi ndani yetu na neno la Mungu linasema kuwa ametupa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu kwa sababu hiyo kama yeye alivyo ndivyo na sisi tulivyo hapa ulimwenguni

1Yohana 3:1-3 “Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo. Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu.”

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: