Jumapili, 21 Septemba 2025

Heri aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba!


Mathayo 7:24-27 “Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.”




Utangulizi:

Moja ya maneno ya msingi sana yanayohitimisha hutuba maarufu ya Bwana Yesu, maarufu kama Hutuba ya Mlimani ni pamoja na mfano wa mjenzi mwenye hekima na yule mjenzi mpumbavu, ambao ni mfano alioutumia Yesu Kristo kukazia hutuba yake kuonyesha umuhimu wa kusikia na kulitendea kazi neno lake, kimsingi kulitendea kazi neno kunajenga msingi imara sana wa kiroho, msingi usiotikisika  katika maisha ya kila mwanafunzi wa Yesu, uwezo wa kustahimili  majaribu na magumu, Lakini pia usalama wa kukaa ndani ya Yesu,  sawa na nyumba iliyojengwa juu ya mwamba ambayo inakuwa na uwezo wa kustahimili dhuruba za aina mbalimbali na kukaa kwa usalama na kudumu.

Luka 6:47-49 “Kila mtu ajaye kwangu, na kuyasikia maneno yangu na kuyatenda, nitawaonyesha mfano wake. Mfano wake ni mtu ajengaye nyumba, na kuchimba chini sana, na kuweka msingi juu ya mwamba; na kulipokuja gharika, mto uliishukia nyumba ile kwa nguvu, usiweze kuitikisa; kwa kuwa imejengwa vizuri. Lakini yule aliyesikia ila hakutenda, mfano wake ni mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi pasipokuwa na msingi, mto ukaishukia kwa nguvu, ikaanguka mara; na maangamizi yake nyumba ile yakawa makubwa.”           

Kimsingi neno la Mungu linampa umuhimu mkubwa mtu anayelitendea kazi neno la Mungu, na mfano huu Yesu aliutoa sawa na tu na agizo linalotutaka tuwe watendaji wa neno na sio wasikiaji, moja ya changamoto kubwa katika nyakati za leo, sio kukosekana kwa mafundisho au watu kuisikia injili lakini changamoto kubwa iko kwamba ni nani analifanyia kazi neno la Mungu, uwezo wetu wa kusikia hauko katika kusikia bali kutenda Wayahudi wanaita agizo hilo SHEMA yaani SIKIA Israel.

Marko 12:29-30 “Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, SIKIA, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.”

Mathayo 21:28-32 “Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, Mwanangu, leo nenda kafanye kazi katika shamba la mizabibu. Akajibu akasema, Naenda, Bwana; asiende. Akamwendea yule wa pili, akasema vile vile. Naye akajibu akasema, Sitaki; baadaye akatubu, akaenda. Je! Katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye? Wakamwambia, Ni yule wa pili. Basi Yesu akawaambia, Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu. Kwa sababu Yohana alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini; lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini, nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini.”

Yakobo 1:22-25 “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo. Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake.”

Kimsingi maandiko yote na mifano yote hapo inatolewa kusisitiza ujumbe mmoja wa kulifanyia kazi neno la Mungu, yaani kulitenda au kuliishi, Mtu anayelitendea kazi neno la Mungu huyu anafananishwa na mtu aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba imara na kwa sababu hiyo dhoruba za kimwili na kiroho na kiakili na kisaikolojia na mafundisho potofu, haziwezi kumdhuru kwa sababu amejengwa juu ya Mwamba, Leo tutachukua muda kujifunza juu ya somo hili Muhimu, Heri aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba na kuliangalia somo hili katika vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Maana ya neno Mwamba.

·         Heri aliyejenga nyumba yake juu ya Mwamba. 

·         Jinsi ya kujijenga juu ya Mwamba.


Maana ya neno Mwamba.

Ni muhimu kufahamu kuwa moja ya msamiati muhimu sana ambao umetumika mara nyingi katika neno la Mungu ni pamoja na neno MWAMBA, Neno Mwamba tunalolisoma katika maandiko kwa mujibu wa muktadha wake mara nyingi limetajwa kwa Lugha ya Kiebrania kama neno Sela’, Cr na Kēphīm, sawa na maneno Kēphas na Pétra katika Lugha ya Kiyunani  Katika Kiingereza tunapata maneno Rock au neno Solid Foundation kwa Kiswahili Mwamba au Msingi imara, Pamoja na neno hili kutumika kitaalamu katika maswala ya miamba na ujenzi, katika uhalisia wake, katika Lugha ya kinabii mara nyingi neno Mwamba lilitumika kumtaja Mungu mwenyewe, Kristo au neno la Mungu:-

2Samuel 22:1-4 “Basi Daudi akamwambia Bwana maneno ya wimbo huu, siku ile Bwana alipomwokoa mikononi mwa adui zake zote, na mkononi mwa Sauli; akasema, Bwana ndiye jabali langu, na ngome yangu, na mwokozi wangu, naam, wangu; Mungu wa MWAMBA wangu, nitamwamini yeye; Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, mnara wangu, na makimbilio yangu; Mwokozi wangu, waniokoa na jeuri. Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa; Hivyo nitaokoka na adui zangu.”

Zaburi 71:1-3 “Nimekukimbilia Wewe, Bwana, Nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye, uniopoe, Unitegee sikio lako, uniokoe. Uwe kwangu MWAMBA wa makazi yangu, Nitakakokwenda sikuzote. Umeamuru niokolewe, Ndiwe genge langu na ngome yangu.”

Isaya 17:10 “Maana umemsahau Mungu wa wokovu wako, wala hukuukumbuka MWAMBA wa ngome yako; kwa sababu hiyo ulipanda mashamba yapendezayo, na kutia ndani yake mizabibu migeni.             

Zaburi 61:1-3 “Ee Mungu, ukisikie kilio changu, Uyasikilize maombi yangu. Toka mwisho wa nchi nitakulilia nikizimia moyo, Uniongoze juu ya MWAMBA nisioweza kuupanda. Kwa maana ulikuwa kimbilio langu, Ngome yenye nguvu adui asinipate.”

Kumbukumbu 32:3-4 “Maana nitalitangaza Jina la Bwana; Mpeni ukuu Mungu wetu. YEYE MWAMBA, kazi yake ni kamilifu; Maana, njia zake zote ni haki. Mungu wa uaminifu, asiye na uovu, Yeye ndiye mwenye haki na adili.”

1Wakorintho 10:4 “wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea MWAMBA wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo.”

Unaona kwa msingi huo katika lugha ya kinabii, Neno la Mungu halizungumzii Mwamba wa kawaida au jiwe la kawaida au Msingi mgumu bali inamzungumzia Mungu mwenyewe na sifa zake alizonazo za Uimara, Uthabiti, Usalama na Uwepo wake wa milele, Mungu anapowaita watu wake yaani Kanisa anakuwa amewajenga juu ya Mwamba, na kwa sababu hiyo Shetani hana uwezo, wala kuzimu hakuna uwezo wowote wa kulishinda Kanisa lake, kwa sababu amelijenga juu yake yeye Mwenyewe

Mathayo 16:17-18 “Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya MWAMBA huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.”

Waefeso 2:20-22 “Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.”               

Watu waliomwamini Bwana Yesu wamejengwa juu ya Mwamba ambaye ni Yesu Kristo mwenyewe, na Neno lake, Mtu akilitendea kazi neno la Mungu anafananishwa na mtu aliyejenga nyumba yake juu ya MWAMBA yaani Kristo na neno lake, huyu anakuwa amejijenga juu ya msingi imara usiotikisika, kwa ujumla neno la Mungu linazungumzia maisha yaliyojengwa juu ya Mungu, Kristo wake na Neno lake ambalo halibadiliki, pamoja na na jina lake lenye nguvu, maisha ya aina hii humfanya mtu aishi kwa amani kwa sababu anamjua sana Mungu kwa hiyo hata apitie dhuruba za aina yoyote duniani, dhuruba hizi haziwezi kumtikisa hata kidogo, Kwa hiyo ili mtu awe imara katika maisha haya hana budi, kujijenga katika kumjua sana Mungu, kumfahamu sana Yesu Kristo huu ni ndio utajiri unaoweza kutuhakikishia usalama wa maisha ya kiroho na kimwili!

Yohana 17:2-3 “kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele. Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.”

Ayubu 22:21 “Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.”       

Heri aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba.

Neno Heri maana yake ni Baraka kubwa sana au amebarikiwa mtu yule aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba, Hapa Mungu hamaanishi kujenga nyumba halisi, hapa anamaanisha mtu ambaye maisha yake amewekeza juu ya Mungu, Juu ya Kristo na juu ya Neno la Mungu au jina lake,  mtu wa aina hii Maandiko yanaonyesha kuwa mtu aliyejijenga katika Kristo, kujikita katika kumfahamu Yesu Kristo, kulijua neno lake na kuishi sawa na neno lake  huyu ni mtu asiyeweza kuyumbishwa na lolote hapa duniani na kuzimu pia, Kumbuka wala malango ya kuzimu hayataliweza hii maana yake mtu aliyejijenga katika kumjua Mungu maishani mwake hawezi kutikiswa hata kidogo!

Ni mtu asiyeweza kuyumbishwa – Kwa kawaida Mwamba huwa hauyumbishwi, ni jiwe lenye msimamo, ni gumu ni la kudumu ni la milele, huwezi kulitikisa unaweza kukimbilia juu ya MWAMBA au chini yake na ukawa salama kwa hiyo ukijijenga juu ya Yesu na juu ya neno lake na jina lake lililo takatifu sana unahakikishiwa usalama na uwepo wa kudumu na kutokuonolewa au kutikiswa kwa sababu zozote zile, si kuwa hutapitia magumu kabisa lakini hata ukipitia hayatakutikisa kabisa! Si kuwa hutapatwa na majaribu lakini yakikupata hatutatikiswa, sababu uko juu ya mwamba

Mathayo 7:25 “mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba.”

Mtu aliyejikita katika kumjua Mungu, aliyejikita katika kulijua neno lake mtu anayemtegemea Mungu katika kila jambo sio kuwa hatakutwa na dhuruba, sio kuwa mafuriko hayatampiga, sio kuwa pepo hazitavuma juu yake, hii ikimaanisha kuwa atapitia katika moto, atapita katika dhiki, atapita katika maji, atapigwa na pepo zinazovuma lakini kwa kuwa amejikita juu ya mwamba hakuna kitakachoweza kuufarakanisha uwepo wake na Yesu.

Zaburi 46:1-5 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake. Kuna mto, vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu, Patakatifu pa maskani zake Aliye juu. Mungu yu katikati yake hautatetemeshwa; Mungu atausaidia asubuhi na mapema.”

Zaburi 27:1-4 “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini. Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake

Zaburi 23:4 “Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.”

Isaya 43:1-2 “Lakini sasa, Bwana aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.”

Ulinzi wa kudumu – Nyakati za agano la kale watu wengi sana walitafuta usalama katika miamba, walifahamu kuwa kama kukitokea janga lolote lile mahali salama ni kwenye JABALI au kwenye MWAMBA, ni MWAMBA ndio ulimpa mtu ulinzi na usalama wa kudumu kwa hiyo ujenzi pia unaozingatia usalama unajengwa juu ya Mwamba na sio vinginevyo.

Zaburi 18:1-6 “Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana; Bwana ni JABALI langu, na boma langu, na mwokozi wangu, Mungu wangu, MWAMBA wangu ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu. Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa, Hivyo nitaokoka na adui zangu. Kamba za mauti zilinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu. Kamba za kuzimu zilinizunguka, Mitego ya mauti ikanikabili. Katika shida yangu nalimwita Bwana, Na kumlalamikia Mungu wangu. Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake.”

Mtu aliyejijenga juu ya mwamba ana ulinzi wa kudumu, Maagano ya Mungu wetu sio ya siku moja ni agano la kudumu ni agano la milele, kwa hiyo mtu akimtumainia Yesu Kristo ana ulinzi wa kudumu, Yesu hafanyi jana tu yeye ni wa siku zote jana, leo na hata milele, ulinzi wake ni wa milele, msamaha wake ni wa milele, fadhili zake ni za milele hakuna kitu kitakachoweza kututenga na upendo wake, hatujamjia Yesu kwa majaribio bali tumemjia yeye kwa sababu anastahili kujiliwa, yeye ni usalama wetu wa milele kwa jambo lolote lile na kwa jaribu lolote lile!

Warumi 8:33-39 “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.

Usalama wa milele – Ni mwamba ndio humuhakikishia mtu usalama wa milele, kwa hiyo mtu akijijenga juu ya mwamba anajihakikishia Msamaha, na uzima kulindwa dhidi ya hatari zozote zile ziwe za kimwili na kiroho, mwamba unakupa Amani hata kutokee mafuriko au pepo zinazovuma kama umejenga juu ya mwamba utalala usingizi mtamu

Waebrania 10:10-14 “Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu. Na kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi. Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu; tangu hapo akingojea hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake. Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa.”

Yohana 10:27-29 “Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu.”

Jinsi ya kujijenga juu ya mwamba.

Tumeona faida kubwa sana na Baraka za mtu aliyejenga juu ya Mwamba, hata hivyo ni muhimu kwetu kujifunza kwa kuhitimisha ili kuangalia kuwa tunawezaje kujijenga juu ya mwamba?

1.       Kumtegemea Mungu – Kwa kuwa Mungu ndiye Mwamba maisha ya mtu anayemtegemea Mungu hayategemei mabadiliko ya hali ya hewa au mambo, sisi tunaye Mungu asiyebadilika, Sifa mojawapo ya mwamba ni kutokubadilika, miaka nenda miaka rudi mwamba hubakia vile vile, siku zote, Mwamba ni mgumu una nguvu, mwamba ni wa milele, mwamba ni wa kudumu, mwamba ni ngome, mwamba ni wa kuaminiwa, mwamba ni wa kutumainiwa mwana unaweza kumlinda mtu dhidi ya adui, mwamba unakubeba.

 

Zaburi 62:1-8 “Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya, Wokovu wangu hutoka kwake. Yeye tu ndiye MWAMBA wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana. Hata lini mtamshambulia mtu, Mpate kumwua ninyi nyote pamoja? Kama ukuta unaoinama, Kama kitalu kilicho tayari kuanguka, Hufanya shauri kumwangusha tu katika cheo chake; Huufurahia uongo. Kwa kinywa chao hubariki; Kwa moyo wao hulaani. Nafsi yangu, umngoje Mungu peke yake kwa kimya. Tumaini langu hutoka kwake. Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana. Kwa Mungu wokovu wangu, Na utukufu wangu; MWAMBA wa nguvu zangu, Na kimbilio langu ni kwa Mungu. Enyi watu, mtumainini sikuzote, Ifunueni mioyo yenu mbele zake; Mungu ndiye kimbilio letu.”

 

2.       Kudumu Katika maombi na ibada – Maombi na ibada, kusoma neno la Mungu, kusikiliza mahubiri mbalimbali, kujisomea neno la Mungu kulijadili na kujifunza kunatutengenezea ukaribu wenye nguvu na Mungu na kwa sababu hiyo kwa kufanya hivyo tunajiimarisha juu ya mwamba, tunakuwa na uhusiano wa karibu sana na Mungu, kujitoa kwa Mungu “Devotions” kunatushikamanisha na Mwamba na kwa sababu hiyo sio rahisi kwetu kuyumbishwa kwa namna yoyote ile na mtu yeyote na fundisho lolote!

 

Yeremia 33:1-3 “Tena, neno la Bwana likamjia Yeremia mara ya pili, hapo alipokuwa akali amefungwa katika uwanda wa walinzi, kusema, Bwana alitendaye jambo hili, Bwana aliumbaye ili alithibitishe; Bwana ndilo jina lake; asema hivi, Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.”

 

3.       Kulitendea kazi neno la Mungu – Kristo ameonyesha wazi kuwa kulitendea kazi neno lake kunafananishwa na kujenga juu ya mwamba na kutokulitendea kazi neno lake kunafanyanishwa na kujenga kwenye mchanga, kwa msingi huo hatuna budi kulitendea kazi neno la Mungu kwa kadiri ya neema ili kuimarisha uhusiano wetu na Mungu wetu na kumuelewa au kumjua yeye kwa kina na mapana na marefu.

 

Mathayo 7:24-27 “Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya MWAMBA; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.”

 

4.       Kuishi maisha ya toba – Ni maisha ya toba pekee yanayoweza kumsaidia mtu kudumisha uhusiano wake na Mungu, watu wengi sana wanafikiri kuwa ujumbe kuhusu toba ni ujumbe kwa wasiookoka lakini ukweli ni kuwa ujumbe wa toba unalihusu Kanisa na unawahusu watu wa Mungu, Hakuna namna yoyote ile tunaweza kubaki katika Mwamba yaani Yesu Kristo bila kuwa na toba neno toba katika kiyunani ni “Metanoia” maana yake kugeuka na kuacha njia mbaya, toba inawahusu watu wa Mungu kugeuka na kuacha njia zao mbaya!

 

2Nyakati 7:14 “ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.”

 

Ufunuo 2:2-5 “Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo; tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.”

 

Ufunuo 2:13-15 “Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani; nawe walishika sana jina langu, wala hukuikana imani yangu, hata katika siku za Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu, aliyeuawa kati yenu, hapo akaapo Shetani. Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini. Vivyo hivyo wewe nawe unao watu wayashikao mafundisho ya Wanikolai vile vile. Basi tubu; na usipotubu, naja kwako upesi, nami nitafanya vita juu yao kwa huo upanga wa kinywa changu.”

 

5.       Kuishi maisha Matakatifu – Mungu wetu ni Mtakatifu, hii sifa ya utakatifu ni sifa yake yeye na hakuna awaye yote mwingine ambaye anasifa hii, Yeye kama Mwamba moja ya sifa yake ni utakatifu, kwa hiyo ili mtu aweze kuwa salama juu ya mwamba huu, maana yake maisha matakatifu yanamhusu, na hakuna njia ya mkato, nyakati tulizo nazo imekuwa ngumu sana kusikia watu wakihubiri utakatifu lakini wito wa Mungu kwa kanisa lake ni pamoja na kuishi maisha matakatifu ili kujihakikishia usalama kwa Mungu wetu.

 

2Samuel 2:1-2 “Naye Hana akaomba, akasema, Moyo wangu wamshangilia Bwana, Pembe yangu imetukuka katika Bwana, Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu; Kwa kuwa naufurahia wokovu wako; Hakuna aliye MTAKATIFU kama Bwana; Kwa maana hakuna ye yote ila wewe, Wala hakuna MWAMBA kama Mungu wetu.”

 

Isaya 6:1-3 “Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu. Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka. Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, MTAKATIFU, MTAKATIFU, MTAKATIFU, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake.”


Walawi 20:26 “Nanyi mtakuwa watakatifu kwangu mimi; kwa kuwa mimi BWANA ni MTAKATIFU nami nimewatenga ninyi na mataifa, ili kwamba mwe wangu.”

 

1Petro 1:15-16. “bali kama yeye aliyewaita alivyo MTAKATIFU, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”

Heri yule aliyejenga Nyumba yake juu ya Mwamba, maana yake heri mtu yule aliyewekeza maisha yake kwa Mungu wetu na Kristo wake na Neno lake na jina lake, Mtu wa namna hii ana maisha thabiti yasiyoyumbishwa na dhuruba, wala pepo wala mafuriko wala changamoto za aina yoyote na ana uhakika wa uzima wa milele, Neno la Mungu linatoa wito kwetu kuwekeza katika kristo kwa usalama wa uhakika wa maisha yetu!.

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni: