Hesabu 27:1-4 “Wakati huo wakakaribia hao
binti za Selofehadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana
wa Manase, wa jamaa za Manase mwana wa Yusufu; na majina ya hao binti za
Selofehadi ni haya; Mala, na Noa, na Hogla, na Milka, na Tirsa. Nao wakasimama
mbele ya Musa, na mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya wakuu, na mkutano wote,
mlangoni pa hema ya kukutania, wakasema, Babaetu alikufa nyikani, naye hakuwamo
katika mkutano wa hao waliojikutanisha kinyume cha Bwana katika mkutano wa
Kora; lakini akafa katika dhambi zake mwenyewe; naye alikuwa hana wana wa
kiume. Kwa nini basi jina la babaetu kufutwa katika jamaa zake kwa sababu
alikuwa hana mwana wa kiume? Tupe sisi urithi pamoja na ndugu zake babaetu.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa katika Jamii
nyingi zamani na hata siku hizi, Mwanamke hakupewa nafasi kubwa katika urithi
wa mali za baba yake hususani ardhi, Kulikuwa na sheria na mila nyingi
zinazompa upendeleo mtoto wa kiume na kumpuuzia mtoto wa kike, Hapa Masaini
Loiborosoit A, Wilayani Simanjirio, Mkoani Manyara niliko pia nimeikuta mila
hii miongoni mwa jamii ya Kimaasai, Mila, Desturi na Sheria kama hii vilevile
lilikuweko katika jamii ya Kiyahudi wakati wa Torati ya Musa, Lakini kupitia
mabinti jasiri sana wana wa
SELOFEHADI yaani Mala, Noa, Hogla, Milka na Tirsa
wao waliwahi kutoa hoja mbele ya Musa na kuhani mkuu Eleazari na
kisha hoja ikapelekwa kwa Mungu na Mungu akalazimika kubadilisha sheria na
kutoa kibali kwamba watoto wa kike wana haki ya kurithi kama ilivyo kwa watoto
wa kiume, ujasiri wao na uthubutu wao wa kuweza kumkabili Musa na hatimaye
Mungu kubadili sheria kwaaji yao unaonyesha kuwa mabinti hawa walikuwa na
ujasiri usiokuwa wa kawaida “uncommon
boldness” katika tafiti zangu wakati wa maandalizi ya somo hili nilimuona
mtu mmoja akiwaita mabinti hawa “Change
Makers” yaani waleta mabadiliko, Hoja yao ilikuwa na mashiko jambo
lililopelekea Mungu kubadili sheria kwaajili ya watoto wa kike
Hesabu 27:5-8 “Basi Musa akaleta neno lao
mbele ya Bwana Bwana akanena na Musa, na kumwambia, Hao binti za Selofehadi
wananena lililo haki; kweli utawapa milki ya urithi pamoja na ndugu za baba
yao; nawe utawapa urithi wa baba yao. Kisha utanena na wana wa Israeli, na
kuwaambia, Mtu akifa, naye hana mwana wa kiume, ndipo utampa binti yake urithi wake.”
Leo basi tutachukua muda
kujifunza kwa njia ya uchambuzi somo hili Urithi
wa Mtoto wa kike kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Sheria
isiyozingatia haki
·
Kuvunjwa
kwa sheria isiyozingatia haki
·
Urithi wa
mtoto wa kike
Sheria isiyozingatia haki
Sheria ya Musa pamoja na Mila
nyingi na Desturi za zamani zilikuwa zimezoeleka ya kwamba urithi wa mali
pamoja na ardhi ulikuwa unaelekezwa kwa watoto wa kiume pekee, mtoto wa kiume
wa kwanza akipokea urithi mara dufu yaani mara mbili kuliko wengine na wengine
kwa kadiri ya sehemu zao, watoto wa kike hawakuhesabiwa, na kuwa kama mtu
angefariki dunia bila kuwa na mtoto wa kiume basi mali zake zingerithiwa na
Ndugu zake wa karibu na mabinti wangeolewa tu na kuwa na jina la familia
nyingine, kimsingi pia wangeachwa bila kurithi lolote
Kumbukumbu 21:15-17 “Akiwa mtu yuna wake
wawili, mmoja ampenda, mmoja hampendi, nao wamemzalia watoto, ampendaye na
asiyempenda wote wawili; na yule mzaliwa wa kwanza akiwa ni wa mke asiyependwa;
ndipo itakapokuwa ya kwamba siku atakayowarithisha wanawe alivyo navyo,
asimweke mwana wa ampendaye kuwa mzaliwa wa kwanza mbele ya mwana wa
asiyempenda, naye ndiye mzaliwa wa kwanza huyu; lakini amkubali mzaliwa wa
kwanza mwana wa yule asiyempenda, kwa kumpa mafungu mawili katika vyote alivyo
navyo; kwa maana ndiye mwanzo wa nguvu zake; haki ya mzaliwa wa kwanza ni yake
yeye.”
Kwa hiyo Mwanzoni Mila na Desturi
na Sheria za Kiebrania hazikuwa zimemfikiria hata kidogo mtoto wa kike, Sheria
hii ilikuwa ni Sheria isiyozingatia haki, ilisababisha huzuni kwa mabinti kwani
mali hususani ardhi ya baba yao ingekwenda kwa ndugu zake na wao wangeachwa
mikono mitupu, Binti za wana wa Selofehadi
yaliwakuta haya, na bila shaka waliyafikiri kwa kina na kuona kuwa hakuna haki
hapo na sheria hiyo ni kandamizi kwao wakadai haki hiyo
Hesabu 27:1-4 “Wakati huo wakakaribia hao
binti za Selofehadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana
wa Manase, wa jamaa za Manase mwana wa Yusufu; na majina ya hao binti za Selofehadi
ni haya; Mala, na Noa, na Hogla, na Milka, na Tirsa. Nao wakasimama mbele ya
Musa, na mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya wakuu, na mkutano wote, mlangoni
pa hema ya kukutania, wakasema, Babaetu alikufa nyikani, naye hakuwamo katika
mkutano wa hao waliojikutanisha kinyume cha Bwana katika mkutano wa Kora;
lakini akafa katika dhambi zake mwenyewe; naye alikuwa hana wana wa kiume. Kwa
nini basi jina la babaetu kufutwa katika jamaa zake kwa sababu alikuwa hana
mwana wa kiume? Tupe sisi urithi pamoja na ndugu zake babaetu.”
Mabinti wa Selofehadi walihuzunika kuona kwakuwa baba yao hakuwa na mtoto wa
kiume, basi ndugu zake baba yao wangerithi mali na ardhi yake na mabinti zake
wakiepo wangeachwa bila kitu, lakini baada ya kuchukua hatua za kijasiri na
kumkabili Musa na Musa akamuuliza Mungu huo ukawa mwisho wa sheria kandamizi
dhidi ya wanawake.
Tunajifunza kutoka kwa Mala, na Noa, na Hogla, na Milka, na Tirsa
kwamba tunaweza kubadili lolote lisilo la haki kwa ujasiri na lolote lililo
kandamizi kwa njia ya maombi na Mungu akasikiliza, Sheria na Kanuni yoyote
iliyokinyume na lile tunalolihitaji na linalosimama kama haki yetu mbele za
Mungu inaweza kuingiliwa kati kwa Sheria ya Kanuni ya kuomba kwa Mungu, Mabinti
hawa kwa imani na ujasiri walimkabili Musa na Musa aliomba kwa Mungu na Mungu
akabadili sheria, tunaweza kuomba lolote kwa jina la Yesu kwenda kwa Baba yetu
wa Mbinguni na kubadilisha Sheria na Kanuni, Mila na Desturi kandamizi na uhuru
wetu ukapatikana katika jina la Yesu Kristo.
Kuvunjwa kwa sheria isiyozingatia haki
Habari ya mabinti hawa
inatufundisha kuwa tunaweza kubadili sheria, endapo tu tutasimama katika haki,
na tunajifunza ya kuwa maombi yana nguvu ya kubadili sheria mila na desturi
ambazo hazitutendei haki katika ulimwengu wa roho na mwili, wakati habari hii
ikizungumzia kubadilishwa kwa sheria iliyopelekea wasichana au wanawake katika
familia kuwa na haki ya kisheria ya kurithi, lakini tunajifunza pia kuwa
tunaweza kubadili sheria za mila na desturi za aina yoyote ile kwa njia ya
maombi ikiwa sheria hiyo au mila hizo au kanuni hizo hazijazingatia haki
Esta 4:15-16 “Basi Esta akawatuma ili
wamjibu Mordekai, Uende ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani,
mkafunge kwa ajili yangu; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala
mchana, nami na wajakazi wangu tutafunga vile vile; kisha nitaingia kwa mfalme,
kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie.”
Daniel 6:10-26 “Hata Danieli, alipojua ya
kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na
madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu ;)
akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake,
kama alivyokuwa akifanya tokea hapo. Basi watu hao wakakusanyika pamoja,
wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake. Ndipo
wakakaribia, wakasema mbele ya mfalme katika habari ya ile marufuku ya mfalme;
Je! Hukuitia sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu
awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako,
Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba? Mfalme akajibu, akasema, Neno hili
ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza kubadilika. Basi
wakajibu, wakasema mbele ya mfalme, Yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale
waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia
sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku. Basi mfalme aliposikia maneno haya
alikasirika sana, akakaza moyo wake ili kumponya Danieli; akajitaabisha
kumwokoa hata jua likachwa. Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja mbele ya
mfalme, wakamwambia mfalme, Ee mfalme, ujue ya kuwa ni sheria ya Wamedi na
Waajemi, lisibadilike neno lo lote lililo marufuku, wala amri yo yote
iliyowekwa na mfalme. Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa
katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako
unayemtumikia daima, yeye atakuponya. Likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa
lile tundu; naye mfalme akalitia muhuri kwa muhuri yake mwenyewe, na kwa muhuri
ya wakuu wake, lisibadilike neno lo lote katika habari za Danieli. Kisha mfalme
akaenda nyumbani kwake, akakesha usiku kucha, akafunga; na vinanda havikuletwa
mbele yake; na usingizi wake ukampaa. Asubuhi mfalme akaondoka mapema, akaenda
kwa haraka mpaka penye lile tundu la simba.Naye alipolikaribia lile tundu,
akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danieli, Ee
Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako, unayemtumikia daima,
aweza kukuponya na simba hawa? Ndipo Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme,
uishi milele. Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya
simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia;
tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno. Basi mfalme akafurahi sana,
akaamuru wamtoe Danieli katika lile tundu. Ndipo Danieli akatolewa katika lile
tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake, kwa sababu alikuwa
anamtumaini Mungu wake. Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki
Danieli, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na
wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika
chini ya tundu. Ndipo mfalme Dario akawaandikia watu wa kabila zote, na taifa
zote, na lugha zote, waliokaa juu ya uso wa dunia; Amani na iongezeke kwenu.
Mimi naweka amri, ya kwamba katika mamlaka yote ya ufalme wangu watu watetemeke
na kuogopa mbele za Mungu wa Danieli; maana yeye ndiye Mungu aliye hai, adumuye
milele, na ufalme wake ni ufalme usioharibika, na mamlaka yake itadumu hata
mwisho.”
Tunaona katika mifano kadhaa hapo
juu ya kuwa maombi yana uwezo wa kuingilia kati sheria za kawaida na mila za
kawaida na hata za Mungu na kubadilisha mambo, mabinti hawa wenye ujasiri
waliomkabili Musa kwa maombo yao na ufuatiliaji waliweza kusababisha mabadiliko
ya sheria, walimrudisha Musa kwa Mungu na Mungu akafanya mabadiliko ya sheria
kwaajili yao na wengine hata leo, kwa tukio lao Mungu alibadili kanuni na
kuamua kuwapa haki
Luka 18:1-7 “Akawaambia mfano, ya kwamba
imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. Akasema, Palikuwa na
kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo
palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki
na adui wangu. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa
simchi Mungu wala sijali watu,lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia
haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima.Bwana akasema, Sikilizeni
asemavyo yule kadhi dhalimu. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake
wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?”
Mungu atampa haki yake kila mtu
anayemkomalia katika maombi, Mungu aliwapa haki mabinti wa Selofehadi ya Kuwa kama mtu akifa bila mwana wa kiume basi urithi
wake utapewa binti zake, asipokuwa na binti au mwana wa kiume basi watepea
ndugu zake walio karibu na sheria hii ikawa agizo la kudumu kwa Israel hata
leo, haya yakawa mapinduzi makubwa na ya kipekee kwa sababu kupitia wao na kwa
mara ya kwanza katika mila na desturi za Kiyahudi wanawake walihesabika kuwa
warithi halali wa mali na ardhi ya baba zao. Sio hivyo tu Mungu aliongezea
baadaye kwamba ili mali hizo zisitawanyike kutoka kwenye kabila lao basi
mabinti hao waolewe ndani ya koo zao ili urithi usihame kutoka kabila moja hadi
lingine na hii haikuwanyima haki ya kurithi bali ilihifadhi urithi ule ndani ya
ukoo na ndani ya kabila husika bila kutawanyika kwa jina na mali za Muhusika
Hesabu 36:1-10 “Kisha wale wakuu wa nyumba
za mababa ya jamaa ya wana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, katika
jamaa za wana wa Yusufu, wakakaribia, na kunena mbele ya Musa, na mbele ya
wakuu walio juu ya nyumba za mababa ya wana wa Israeli; wakasema, Bwana
alimwagiza bwana wangu awape wana wa Israeli nchi kwa kupiga kura iwe urithi
wao; tena bwana wangu aliagizwa na Bwana awape binti za Selofehadi ndugu yetu huo
urithi wa baba yao. Wakiolewa na watu wa wana wa hizo kabila nyingine za wana
wa Israeli, ndipo urithi wao utatwaliwa na kuondolewa katika urithi wa baba
zetu, na hiyo kabila watakayotiwa ndani yake itaongezewa urithi wao; basi
urithi huo utaondolewa katika kura ya urithi wetu. Tena itakapokuwapo hiyo
yubile ya wana wa Israeli, ndipo urithi wa hiyo kabila ambayo wamekuwa ndani
yake utaongezewa huo urithi wao; hivyo urithi wao utaondolewa katika urithi wa
kabila ya baba zetu. Basi Musa akawaagiza wana wa Israeli kama neno la Bwana
lilivyokuwa, akasema, Kabila ya wana wa Yusufu imenena yaliyo haki. Bwana
ameagiza neno hili katika habari ya binti za Selofehadi, akasema, Na waolewe na
waume wawapendao; lakini na waolewe katika jamaa ya kabila ya baba zao. Hivyo
hapana urithi wo wote wa wana wa Israeli utakaotoka kabila hii kwenda kabila
hii; kwa kuwa wana wa Israeli watashikamana kila mtu na urithi wa kabila ya
baba zake. Na kila binti atakayemiliki urithi katika kabila yo yote katika wana
wa Israeli, ataolewa katika jamaa moja ya kabila ya baba yake, ili wana wa
Israeli wapate kumiliki kila mtu urithi wa baba zake. Hivyo hapatakuwa na
urithi uwao wote utakaotoka kabila hii kwenda kabila hii; kwa kuwa kabila za
wana wa Israeli zitashikamana kila mmoja na urithi wake mwenyewe. Basi hao
binti za Selofehadi wakafanya kama Bwana alivyomwagiza Musa;”
Urithi wa mtoto wa kike
Moja ya fundisho lingine la
msingi na la Muhimu tunalojifunza kutoka kwa mabinti wa Selofehadi ni kuwa tunajifunza namna Mungu anavyotaka sheria ya
urithi wa mtoto wa kike kuzingatiwa, Ni kama neno la Mungu olinatoa wito kwa
jamii kutokuwapuuzia watoto wa kike katika maswala mbalimbali ya kijamii, Kamwe
jamii haipaswi kufikiri kuwa Mwanamke ni kiumbe wa daraja la chini, Haki zao
zimendikwa katika Torati na zimethibitishwa na Mungu mwenyewe. Jamii inapaswa
kuondoa dhana potofu ya kufikiri kuwa mwanamke hastahili urithi na kupingana na
hilo ni kupingana na mpango wa Mungu, watoto wa kike wapewe kila wanachistahili
katika familia zao, ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha, kupinga ukatili na ubaguzi
wa kijinsia, kutokuwatahiri wanawake na yote yanayowanyima haki kutokana na
maumbile yao na kuwa jamii inapaswa kuacha mila na desturi za kizamani ambazo
ni kandamizi.
Katika nyakati za agano jipya
Mwanamke ana haki na mwanaume, Mtumwa na muajiri, Myahudi na Myunani wote wana
haki sawa za kiroho, Kwa hiyo anapomuamini Yesu wote wanaonekana kuwa wamoja
katika Kristo
Wagalatia 3:27-29 “Maana ninyi nyote
mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana
mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja
katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu,
na warithi sawasawa na ahadi.”
Habari ya mabinti wa Selofehadi ni fundisho la kipekee
kwamba Mungu ni mtetezi wa haki ya wote walio dhaifu na wanyonge na wale
wanaokandamizwa katika jamii, ni somo kwamba Mungu hakubaliani na mila na
desturi zinazowanyima haki wengine kwa sababu fulani fulani, kila mwanadamu ana
nafasi yake na heshima yake mbele za Mungu na kila mwanadamu anastahili
kushiriki Baraka zote za Mungu, Urithi wa mwanamke ni agizo la Mungu na sio
upendeleo, Lakini ili urithi ubaki katika kabila lao na jina la baba yao
lisipotee waliolewa na binamu zao, kimsingi baadaye watoto hao mabinti
walikabidhiwa urithi ulioahidiwa na Musa mtumishi wa Mungu katika nchi ya Mkanaani
Yoshua 17:3-4 “Lakini Selofehadi, mwana wa
Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, hakuwa na wana
waume ila binti; na majina ya hao binti zake walikuwa wakiitwa Mala, na Noa, na
Hogla, na Milka, na Tirsa. Nao wakakaribia mbele ya Eleazari, kuhani, na mbele
ya Yoshua, mwana wa Nuni, na mbele ya mashehe, wakasema, Bwana alimwamuru Musa
kutupa sisi urithi kati ya ndugu zetu; basi kwa kuiandama hiyo amri ya Bwana
akawapa urithi kati ya ndugu za baba yao.”
Desturi ya kuwanyima watoto wa
kike urithi hususani wa Ardhi imeleta mafarakano katika jamii nyingi duniani,
ni Sheria, Mila na Desturi ambayo
imeleta ubaguzi wa kijinsia, lakini hiki ambacho Mungu alikifanya baada ya
mabinti wa Selofehadi kimeleta
mtazamo mpya wa kijamii na usawa wa kijinsia, hivyo sio tu swala la ardhi
lakini watoto wasomeshwe na wasiozwe katika hali ya utoto, lakini wajaliwe na
kutunzwa na kuhudumiwa kama watoto wengine, Katika sheria za kislamu watoto wa
kike hupewa urithi japo ni nusu ya kile wanapewa wanaume, Lakini wale wenye
mila mbovu zinazo-mbagua mtoto wa kike wafahamu tu kuwa Mungu anawathamini nao
vilevile kama anavyothamini watoto wa kiume hivyo ni wakati sasa kwa jamii
kubadilika ni wakati wa mabunge kutunga sheria zenye kuzingatia uaswa wa
kijinsia na kuondoa mila potofu na kandamizi katika jamii na kuachia zile zenye
manufaa
Rev. Innocent Samuel Kamote
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni