Yoahana 12:23-25 “Naye Yesu akawajibu,
akasema, Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu. Amin, amin, nawaambia, Chembe ya
ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali
ikifa, hutoa mazao mengi. Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye
aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele.”
Utangulizi:
Leo tunachukua muda kiasi
kutafakari maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo aliyoyasema karibu na mwishoni
kabisa mwa huduma yake Duniani, Yesu alikuwa ametembelewa na kundi kubwa la
jamii ya watu wasiokuwa wayahudi, yaani Wayunani ambao kimsingi nao walikuwa na
kiu na hamu na shauku ya kupata huduma ya Bwana wetu Yesu Kristo, Yesu anaiona
shauku yao kama hitaji kubwa sana la kiroho kwa jamii ya watu wote duniani kama
watu wanaomuhitaji Mungu na Mwokozi katika maisha yao, Hata hivyo kuhudumia
jamii ya watu wote duniani kwa vyovyote vile kungemlazimu kutimiza mapenzi ya
Mungu ya kufa msalabani ili aweze kuwa fidia ya wengi kama yanenavyo maandiko:-
Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu
aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye
asipotee, bali awe na uzima wa milele.”
Luka 2:34-35 “Simeoni akawabariki,
akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka
wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga
utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.”
Akifafanua juu ya mauti yake huku
akiunganisha na mafundisho yahusuyo kujikana nafsi, Yesu anatumia mfano wa
wakulima wa ngano ili kufafanua kanuni ya kiroho ya kuleta mafanikio na kuzaa
matunda mengi inavyogharimu maisha ya waanzilishi ili kuleta uzima kwa wengi au
kwa ulimwengu na ndipo anapotumia mfano wa Chembe ya ngano (Yaani mbegu ya ngano) kwamba ili iweze
kutoa mazao mengi ni lazima ife na kuzikwa na inapoota yaani kufufuka
inasababisha mazao mengi sana.
Tutajifunza ujumbe huu Chembe ya ngano isipoanguka kwa
kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo;-
·
Maana ya
kuanguka kwa chembe ya ngano.
·
Chembe ya
ngano isipoanguka!.
·
Faida za
kuanguka kwa chembe ya ngano.
Maana ya kuanguka kwa chembe ya ngano.
Ni muhimu kufahamu kuwa Pamoja na
ukulima wa zabibu, ufugaji wa wanyama wa aina mbalimbali,kama kondoo, mbuzi na ng’ombe,
watu wa mashariki ya kati hususani Israel na baadhi ya waarabu ni watumiaji
wazuri sana wa ngano kwaajili ya chakula na hasa mikate, sasa ili Yesu aweze
kueleweka vizuri katika jamii yake alitumia mifano ya vitu vya karibu na
vilivyozoeleka katika jamii yake ili aweze kuwasilisha ujumbe wa kiroho wenye
maana inayoeleweka kwa watu wake, Yesu hapa anatumia mfano wa chembe ya ngano (yaani
mbegu ya ngano) ambayo ili iweze kuzaa matunda mengi zaidi hutupwa au kuzikwa
shambani na kisha inakufa katika udongo au ardhini na inapofufuka/kuota kama
mmea na kuzaa inazalisha matunda au mbegu nyingine bora zaidi hii ndio kanuni
ya kilimo.
Yohana 12:24 “Amin, amin, nawaambia, Chembe
ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali
ikifa, hutoa mazao mengi.”
·
Chembe ya
ngano kwa kiyunani (Greek) inaitwa “ho
kokkos tou sitou” kwa kiingereza “a grainof
wheat” ikimaanisha mbegu ya ngano
·
Kuanguka kwa kiyunani (Greek) linatumika neno
Piptō linalomaanisha kuanguka chini kwa hiyari, au kuangushwa
kwa kusudi au kupanda
·
Kufa kwa kiyunani (Greek) linatumika neno apothnēskō
linalomaanisha
kufa kimwili au kufa kwa hiyari yaani kwa kiingereza “Self- denial” “Self-sacrificial” kujitoa dhabihu, kujikana au
kujikataa au kujitoa sadaka.
Waebrania katika mtazamo wao
kuhusu mbegu siku zote waliamini ndani ya mbegu kua kuna UZIMA, URITHI, na KIZAZI, walikuwa wanatambua kuwa uhai hauwezi
kuendelea bila ya kuwako kwa mbegu, lakini ili mbegu iweze kuendeleza uhai na
uzima na urithi na kizazi ni lazima mbegu hiyo itolewe kutoka kwenye
kuhifadhiwa na itupwe katika moyo wa ardhi, kisha ife na izikwe na kuchipuka
ndipo iweze kuendeleza kizazi kwa hiyo mbegu katika mukthadha wa wayahudi
inaitwa ZERA ikimaanisha UZAO
Mwanzo 22:12-18 “Malaika wa BWANA akamwita
Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema
BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,
katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama
nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango
wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa
sababu umetii sauti yangu.”
Yesu alikuwa anatambua kwamba ni
lazima ajidhabihu yeye mwenyewe kwaajili ya kuufikia ulimwengu, alifahamu wazi
kuwa yeye hakuja kwaajili ya wayahudi pekee, bali alikuja kwaajili ya ulimwengu
mzima, alifahamu kuwa anahitajika sio na wayunani pekee bali na ulimwengu mzima
na kwa sababu hiyo, kujidhabihu kwaajili ya ulimwengu mzima kungerahisisha
ukombozi utakaozaa matunda kwa Mungu wetu yaliyo mengi, Lakini wakati huo huo
Yesu aliwataka wanafunzi wake wote ikiwa ni pamoja na wewe na mimi kuwa na
ufahamu ya kuwa maisha ya uanzilishi wa kitu chchote yanahusisha kujitoa na
kujidhabihu na matunda yake yangelikuja kuonekana mbeleni!, Yeye kama Uzao wa
Ibrahimu ilikuwa ni lazima ajitoe sadaka yeye mwenyewe kwa hiyari ili mataifa
yote waweze kubarikiwa
Tito 2:11-14 “Maana neema ya Mungu
iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa
za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu
wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo
Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu,
ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe,
wale walio na juhudi katika matendo mema.”
Waefeso 5:1-2 “Hivyo mfuateni Mungu, kama
watoto wanaopendwa; mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda
ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya
manukato.”
Maandiko hayo yanadhihirisha wazi
kuwa kusulubiwa kwa Yesu Kristo halikuwa tukio la kupangwa na wazee na wakuu wa
makuhani, lakini lilikuwa ni tukio la Yesu Kristo mwenyewe kujidhabihu na
kukubali kufa na kufufuka kutoka kwa wafu ili atukomboe wanadamu, Yeye
alikuwa ni chembe ya ngano ambayo
ilikuwa lazima ianguke ili kusababisha mazao mengi sana duniani.
Chembe ya ngano isipoanguka!.
Yoahana 12:23-25 “Naye Yesu akawajibu,
akasema, Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu. Amin, amin, nawaambia, Chembe ya
ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali
ikifa, hutoa mazao mengi. Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye
aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele.”
Yesu anatumia msemo huu wa chembe yaani mbegu ya ngano kama mfano (Metaphor) kuonyesha kuwa mbegu ili iweze kuleta mavuno
mengi sana ni lazima ianguke, izikwe ardhini kisha inapochipuka yaani kuota na
kustawi inaleta mavuno makubwa sana, kanuni hii ni kanuni ya kilimo lakini ni
kanuni ya kiroho na kanuni ya kawaida katika maisha.
Yesu anaonyesha kuwa wakati mwingine
ili mtu aweze kuzaa matunda, hakuna budi watu wajikane nafsi na kujidhabihu kama
yeye, lakini sio hivyo tu kuishi maisha ya kumfuata Yesu na kumpendeza vile
vile kunahitaji kujikana nafsi, Ni lazima ujikane ili uweze kuishi maisha
matakatifu nay a mfano, bila kujikana ni ngumu kuona mazao
Luka 9:22-25 “akisema, Imempasa Mwana wa
Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na
waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka. Akawaambia wote, Mtu ye yote
akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku,
anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu
atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa
yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza
mwenyewe?”
Chembe ya ngano isipoanguka
hakuna lolote linaloweza kutokea, watu wasipojidhabihu na kujioa hakuwezi
kutokea mabadiliko yoyote chanya katika jamii, mambo mengi tunayoyaona duniani
na kuyafurahia wakati mwingine yamegharimu maisha ya watu wengine lakini wengi
wanafaidika leo kutokana na kuumia kwa watu wengine, hususani waanzilishi wa
mambo, Imani, mataifa, ustawi, uanzishwaji wa taasisi yoyote ile, upatikanaji
wa Amani na kadhalika, huwa haviwezi kupata usitawi bila watu kujikana, kujiyoa
na kujidhabihu, maisha ya kujitoa kwaajili ya jamii yanaweza kuumiza wachache
lakini yakanufaisha wengi, Leo hii tunaushangilia wokovu na kujivunia lakini
yaligharimu maisha ya Mwana wa Mungu, Yesu Kristo aligharimika pale msalabani
na kwa kupigwa kwake tumepona
Marie Curie ambaye ni mgunduzi wa
tiba ya kutumia mionzi (Radiation in
Medicine) alifariki dunia tarehe 04
Julai 1934 huko ufaransa akiwa na miaka 66, Mwanamke huyu aliyekuwa mwanasayansi alihatarisha maisha yake
hata kufa baada ya kuathiriwa na mionzi hiyo alipokuwa anafanya kazi za
kitafiti na matumizi ya tiba ya mionzi ya (radium
and Plonium) ambayo leo imekuwa msaada mkubwa sana katika tiba ya
kiuchunguzi ya mionzi kama X-Rays
Katika maisha wakati mwingine
mambo hayawezi kutokea mpaka watu wengine wamesimama kidete na kuhatarisha
maisha yao au hata kufa kwaajili ya kusababisha mabadiliko yatokee, Mahatma Gandhi alijitoa maisha yake
kusababisha nchi ya India kupata uhuru wake
kutoka kwa waingereza akianzisha harakati za kuandamana bila kufanya
ghasia, akivumilia vifungo mbalimbali na hata wakati mwingine aliacha kula
yaani akifunga na kujinyima ili haki za kibinadamu zipatikane katika India inayofurahia matunda ya uhuru
huo leo.
Wakristo, na watumishi wa Mungu
katika mazingira mbalimbali, tunapaswa kuelewa Yesu alikuwa anamaanisha kwamba
bila wengine kujitoa muhanga, maisha yao, fedha zao, starehe zao, mifungo yao,
kesha zao, maisha ya familia zao, haki, na injili haiwezi kuwafikia watu wa
Mungu, umasikini hauwezi kuondoka, unyonge hauwezi kuisha, ukandamizwaji
hauwezi kukomeshwa, udhalimu hauwezi kutokomea, maovu yataendelea kuongezeka,
amani haiwezi kupatikana, ubaguzi hauwezi kuisha, upendeleo hauwezi kuisha,
haki haiwezi kupatikana, na uhuru wa kweli hauwezi kupatikana bila baadhi ya
watu kujitoa dhabihu yaani Chembe ya
ngano isipoanguka! Inabakia ile ile!
Faida za kuanguka kwa chembe ya ngano.
Kuanguka kwa chembe ya ngano ni
kujitoa au kujidhabihu kwaajili ya Mungu, Neno la Mungu linatueleza kuwa
kujitoa ndio dhabihu iliyo hai, takatifu na ya kupendeza, kama mtu anataka
kumpendeza Mungu basi ni lazima akubali kujitoa, au kujidhabihu, Kwa nini Mungu
alipendezwa na Yesu Kristo hata kujivunia kuwa huyu ndiye mwanangu mpendwa
ninayependezwa naye? Sababu kubwa ni kuwa Yesu alijitoa yeye mwenyewe
Warumi 12:1 “Basi, ndugu zangu, nawasihi,
kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya
kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.”
Wafilipi 2:6-11 “ambaye yeye mwanzo alikuwa
yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha
kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa,
akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu,
alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena
Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa
jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya
chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa
Mungu Baba.”
Mwanafunzi wa kweli wa Yesu
Kristo ni yule anayejitoa, unapodai kuwa unamfuata Yesu lakini hujitoi maana
yake ni sawa na kuwa hauufuati mfano wake, Yeye mwenyewe anamkana kila mtu
anayedai kuwa anamfuata yeye lakini hataki kuteseka kwaajili ya Kristo!
Kimsingi huwezi kuwa mwanafunzi wa Yesu kama hutaki kugharimika na kumfuata
Luka 14:27 “Mtu ye yote asiyeuchukua
msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.”
Kila anayejikana kwaajili ya Yesu
Kristo na jamii nafsi yake haitapotea kwani atalipwa uzima wa milele,
tunapojitoa na kujidhabihu hata kufa kwaajili ya wengine/kifo au mauti yako
inayotokana na kujidhabihu haiwi mwisho badala yake unakuwa mwanzo wa uzima na
maisha mapya yenye Baraka nyingi na yenye kukuzalia matunda
Isaya 53:5-11 “Bali alijeruhiwa kwa makosa
yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na
kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja
wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi
sote. Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama
mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao
manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa
aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na
nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Wakamfanyia
kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa
hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake. Lakini Bwana aliridhika
kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi,
Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi, Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi
mwake; Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake
mtumishi wangu mwenye haki Atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua
maovu yao.”
Yoahana 12:25-26 “Yeye aipendaye nafsi yake
ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha
hata uzima wa milele. Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na
mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.”
Hitimisho.
Kuishi maisha matakatifu
kunahitaji kujikana, kuishi kwaajili ya Kristo kunahitaji kujikana, kuwatumikia
watu kunahitaji kujikana, kuanzisha kazi mpya kunahitaji kujikana, kufanya
umisheni kunahitaji kujikana, kumtumikia Mungu kunahitaji kujikana, kufanya
uinjilisti kunahitaji kujikana, kuimba kwaya kunahitaji kujikana, kuomba
kunahitaji kujikana, kukesha kunahitaji kujikana, kila kitu duniani na
mafanikio yoyote yale duniani hayawezi kuja kama hatuna kujikana, kuleta
maendeleo kunahitaji kujikana, bila kujikana katika jambo lolote lile hakuwezi
kuwako na matunda yanayokusudiwa, mwanafunzi ili afaulu mitihani yake anahitaji
kujikana, kusoma kunahitaji kujikana, biashara inahitaji kujikana, kilimo
kinahitaji kujikana maendeleo yoyote yake yanahitaji kujikana hali kadhalika
maisha ya kiroho yanahitaji kujikana hii ndio kanuni ya mafanikio, ni lazima
chembe ya ngano ianguke, isipoanguka inabakia ile ile, lakini ikifa ikizikwa
inatoa mazao mengi sana hii ni kanuni ya wokovu, ni kanuni ya kiroho na ni
kanuni ya maisha, na ni kanuni ya kuleta
mafanikio makubwa duniani chembe ya ngano isipoanguka ikafa, hukaa
hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi, Ni dua yangu na maombi
yangu wasomaji wangu na wasilikizaji wangu tujitoe kwaajili ya kazi ya Mungu
kabla ya kuangalia faida zetu binafsi.
1Wakorintho 15:36-38 “Ewe mpumbavu!
Uipandayo haihuiki, isipokufa; nayo uipandayo, huupandi mwili ule utakaokuwa,
ila chembe tupu, ikiwa ni ya ngano au nyingineyo; lakini Mungu huipa mwili kama
apendavyo, na kila mbegu mwili wake.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima.
+255718990796
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni