Jumapili, 28 Septemba 2025

Kuishi zaidi ya maneno!


Zaburi 109:1-3. “Ee Mungu wa sifa zangu, usinyamaze, Kwa maana wamenifumbulia kinywa; Kinywa cha mtu asiye haki, cha hila, Wamesema nami kwa ulimi wa uongo.  Naam, Kwa maneno ya chuki wamenizunguka, Wamepigana nami bure.”




Utangulizi:

Wote tutakuwa tunafahamu nguvu kubwa iliyoko katika maneno, maneno yana nguvu!, yana nguvu kubwa kiasi cha kuweza kujenga, yana nguvu kubwa kiasi cha kuweza kubomoa, yana uwezo wa kuponya, yana uwezo wa kujeruhi, yana uwezo wa kutia moyo, yana uwezo wa kuvunja moyo, Neno la Mungu linasema kuwa maneno yana uwezo wa kuleta mauti au kuleta uzima unaona!

Mithali 18:20-21 “Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake. Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.”

Leo nataka tuzungumzie kile ambacho Roho Mtakatifu anataka nikizungumzie kwaajili ya watu wake anaotaka kuwasaidia na hii ni kuishi zaidi ya maneno hasi, Ujumbe huu ulinijia kwa lugha ya kiingereza “Beyond the negative words” lakini mimi nahudumia watu wanaozungumza Kiswahili, kwa hiyo nimeUita ujumbe huu Kuishi zaidi ya maneno!, Kila mtu aliyemwamini Mungu anapaswa kuishi zaidi ya maneno, hususani maneno hasi yaani yale yanayokuja kwetu kupitia Shetani na mawakala wake ambao wanatutupia maneno ili tuishi kwa mipaka, ili tukate tamaa, ili tuvunjike moyo, ili tushindwe, ili tuogope, ili tusiendelee, ili tutawalike, ili kutuonea na kutujeruhi, ili kuondoa ujasiri wetu, ili ususie na kadhalika, Roho Mtakatifu amenituma nikutie moyo kwamba unaweza kuishi zaidi ya maneno, na kuwa wako watakatifu waliotutangulia ambao kimsingi walishi zaidi ya maneno na wakapata ushindi na kusonga mbele katika maisha yao ya kawaida na ya kiroho Ishi zaidi ya maneno, Tutajifunza somo hili kuishi zaidi ya maneno kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Maneno ya kuvunja moyo.

·         Wanadamu na maneno ya kuvunja moyo.

·         Kuishi zaidi ya maneno


Maneno ya kuvunja moyo.

Mojawapo ya namna na jinsi Shetani anavyowashambulia watu wa Mungu ni pamoja na kuwashambulia kwa maneno, hususani maneno ya kuvunja moyo, Shetani anaweza kuwatumia watu yaani mawakala wake, na wanaweza kuwa na sura yoyote ile, wanaweza kuwa ni waamini wenzako, waimbaji wenzako katika kwaya, watumishi wenzako, wakristo wenzako ndugu au watu wa karibu na wakati mwingine watu wa ulimwengu huu watakurushia maneno ya kukuvunja moyo, ili ujihoji kama unastahili, uwe na mashaka, uwe na wasiwasi hata kuhusu ahadi za Mungu, watakuhukumu, watakujaza woga na hofu, watashambulia imani yako, watakuvunja moyo, wataiba furaha yako. Shetani anaweza kutumia marafiki, maadui na jamii na wakati mwingine hata moyoni mwako unaweza ukajihukumu! Kwamba labda wewe sio bora sana, wewe sio mwema sana, labda wewe huwezi kufanikiwa, hutoboi, au Mungu amekuacha, maneno haya yatakushambulia kama mshale yakitafuta kukuvunja moyo na kukukatisha tamaa na unaweza hata kudhani kuwa labda wokovu kwako hauna maana au Mungu hana msaada kwako, Kristo Yesu alishambuliwa kwa maneno wakati akiwa msalabani katika hali ya mateso.

Luka 23:35-37 “Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake. Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki, huku wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe.”

Luka 23:38-39 “Na juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI. Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.”

Mathayo 27:39-43 “Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisa-tikisa vichwa vyao, wakisema, Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani. Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe. Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu.”

Neno la Mungu linaonya na kukemea, likitaka wanadamu wawe na matumizi mazuri ya ulimi yaani maneno kwani yanaweza kusababisha madhara makubwa sana, uharibifu wa aina nyingi sana duniani na hata vita kubwa duniani zilianza na ulimi tu, talaka, majungu makazini, kufukuzwa watu kazi, kuharibia wengine maisha kumesababishwa kwa kiwango kikubwa na ulimi, yaani maneno maneno yameumiza wengi, yameua wengi, yamefarakanisha wengi, yamechongea wengi na kuleta uharibifu katika maisha ya wengi kiroho, kiakili, kiuchumi, kisaikolojia na kadhalika.

Yakobo 3:5-6 “Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana. Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum.”             

Wanadamu na maneno ya kuvunja moyo

Hebu tuwe wakweli tu maneno ya kuvunja moyo ni sehemu ya maisha ya Mwanadamu, tunaishi katika ulimwengu uliooza na kuharibikwa kwa dhambi, kwa sababu hiyo aidha watu kwa kupenda au hata kwa kutokupenda, kwa kudhamiria au hata kwa kutokudhamiria, watapiga domo, watapiga umbeya, wanadamu ni wambeya wanadamu ni waongo wanadamu wana maneno yaliyojaa sumu, wanadamu wana maneno, wanadamu ni wazushi, watu wana maneno watu wanazungumza bhana maneno ya kuumiza, maneno ya kubomoa, maneno ya kukosesha watu wanasengenya, ukiwa mwema utasengenywa, ukiwa mbaya utasengenywa, vyovyote uwavyo kila mwanadamu anasemwa mahali fulani na wakati mwingine wanazungumza maneno yanayoumiza sana, wanazungumza maneno ya kuharibu, wanazungumza vitu vya kuharibu usalama wako, wanakuweka uchi, wanakuwekea mipaka, wanaharibu maisha, na wakati mwingine wanatumiwa wazi wazi na adui Shetani kuumiza na kukatisha tamaa wengine na hata waliookoka huingia katika mtego huu na hata sisi wenyewe tunaweza kujifikiri vibaya kama hatutaacha kujitazama katika mtazamo wa Mungu, kwa ujumla ndimi za wanadamu zimejaa sumu, yaani watu wana maneno yenye madhara na wanaweza kuzungumza bila kujifikiri, hawafikiri madhara, hawafikiri mauti wanatumiwa tu na yule shetani, ukitenda mema watasema, ukitenda mabaya watasema ni mawakala wa Shetani.

Zaburi 140:1-3. “Ee Bwana, uniokoe na mtu mbaya, Unihifadhi na mtu wa jeuri. Waliowaza mabaya mioyoni mwao, Kila siku huondokesha vita. Wamenoa ndimi zao kama nyoka, Sumu ya fira i chini ya midomo yao.”

Kwa hiyo utakubaliana nami kuwa maneno ya kukatisha tamaa ni sehemu ya maisha ya kila siku na ya kawaida katika ulimwengu huu wa watu wasio wakamilifu, Mwandishi wa Zaburi amewahi kulalamika kuwa wakati mwingine hata rafiki zetu wa karibu wanaweza kutunenea mabaya, watu tunaosali nao pamoja, marafiki na hata ndugu, yaani yeyote anaweza kutumiwa! Haijalishi ni nani!

Zaburi 55:12-14 “Kwa maana aliyetukana si adui; Kama ndivyo, ningevumilia. Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye; Kama ndivyo, ningejificha asinione. Bali ni wewe, mtu mwenzangu, Rafiki yangu, niliyejuana nawe sana. Tulipeana shauri tamu; na kutembea Nyumbani mwa Mungu pamoja na mkutano.”

Warumi 3:10-14 “kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja. Koo lao ni kaburi wazi, Kwa ndimi zao wametumia hila. Sumu ya fira i chini ya midomo yao.Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.”

Endapo hutajifunza na kuelewa kwa kina na mapana na marefu Neno la Mungu unaweza kusumbuka sana, lakini ukielewa kuwa tuko Duniani na Dunia imejaa wazushi na waongo na waharibifu na wasema vibaya na waumizaji hutaweza kuishi zaidi ya maneno “Beyond the negative words” Lakini ashukuriwe Mungu atupaye kushinda Roho Mtakatifu atatuwezesha kuishi zaidi ya maneno, Maneno ni aina ya vita, ambayo Shetani anaitumia, kama ilivyo katika ulimwengu wa kawaida mabondia na wapiganaji kabla ya kupigana huanza na tambo za maneno au propaganda hii ni vita ambayo watakatifu waliotutangulia waliifahamu na kujua namna na jinsi ya kuipigana, kwa nini Shetani hutumia vita vya maneno kuwashambulia watu wa Mungu hii ni kwa sababu:-

-          Unashambuliwa ili ujisahau kuwa wewe ni nani – anataka usahahu kuwa wewe ni chagua la Mungu na Mungu amekuumba kwa jinsi ya ajabu, amekuumba kwa kusudi na kwa ushindi na kukuita kwenye kusudi lake kwa sababu hiyo ni lazima Shetani akushambulie, akushitaki.

 

Zaburi 139:13-14Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu, Uliniunga tumboni mwa mama yangu, Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana,”

 

1Petro 2:9-10 “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.”

 

-          Unashambuliwa ili utoke katika kusudi la Mungu – Maneno yanaweza kukutia mashaka na kukufadhaisha ili ikiwezekana yakutoe katika mpango na mapenzi ya Mungu au kusudi ambalo kwalo Mungu amekuitia

 

Nehemia 4:1-3 “Lakini ikawa, Sanbalati aliposikia ya kwamba tulikuwa tukiujenga ukuta, akaghadhibika, akaingiwa na uchungu sana, akawadhihaki Wayahudi. Akanena mbele ya nduguze na mbele ya jeshi la Samaria, akisema, Wayahudi hawa wanyonge wanafanyaje? Je! Watajifanyizia boma? Watatoa dhabihu? Au watamaliza katika siku moja? Je! Watayafufua mawe katika chungu hizi za kifusi, nayo yameteketezwa kwa moto? Basi Tobia, Mwamoni, alikuwa karibu naye, akasema, Hata hiki wanachokijenga, angepanda mbweha, angeubomoa ukuta wao wa mawe.”              

 

-          Unashambuliwa kwaajili ya kuidhoofisha Imani – Maneno yanaweza kutumika kama njia ya kukuvunja moyo, ili ushindwe kulitimiza kusudi la Mungu kwa Imani na kurudi katika mashaka Israel walipokuwa wanakaribia kuingia katika inchi ya Kanaani wapelelezi kumi walitumiwa na shetani wakwavunja moyo watu kwa maneno yao na watu wakakubali kuvunjika moyo.

 

Hesabu 13:31-33Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi. Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno. Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.”

 

Hesabu 14:1-3 “Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule. Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri?”                           

Kuishi zaidi ya maneno;

Ili kila mtu duniani awe na amani ya kweli na ushindi dhidi ya maneno ya kukatisha tamaa na kuumiza moyo tunayokuta nayo duniani basi inatulazimu kuishi zaidi ya maneno hasi, na ili uweze kuishi zaidi ya maneno unapaswa kuishi kwa kuliangalia Neno la Mungu linasema nini juu yako na sio kile watu wanachokisema, wewe na mimi sio matokeo ya kile watu wanasema wewe na mimi ni matokeo ya kile Mungu anachokisema Neno la Mungu lina nguvu kuliko nyundo ivunjayo mawe vipande vipande, Neno la Mungu ni moto mkali wenye nguvu ya kuumba!

Yeremia 23:28-29 “Nabii aliye na ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu. Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema Bwana. Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?”

Watakatifu waliopata ushindi katika kila vita waliyokutana nayo ya maneno walijikita katika Neno la Mungu na ujuzi wao kuhusu Mungu, ukawafanya wawe washindi, wale walioogopa maneno walinywea lakini wale walioliangalia neno la Mungu na kile Mungu ameahidi hawakuogopa

a.       Daudi na Gloiath – Walipigana vita vya maneno kwanza kabla ya kuingia katika vita halisi, Goliathi aliogopewa sana sio tu kwa sababu ya ukubwa wake lakini pia kwa sababu ya maneno yake hasi ambayo yalitisha sana na watu wote wakaogopa na pia walimkimbia ilikuwa ni aibu kubwa sana. Lakini Daudi alifahamu namna ya kushughulika naye. Daudi alikutana na maneno mengi ya kukatisha tamaa lakini yeye aliishi zaidi ya maneno! Ona:-

 

1Samuel 17: 1-11 “Wakati huo Wafilisti walikusanya majeshi yao kwa vita, nao wakakusanyika huko Soko, ulio mji wa Yuda, wakatua kati ya Soko na Azeka, katika Efes-damimu. Naye Sauli na watu wa Israeli wakakusanyika, wakatua katika bonde la Ela, nao wakapanga vita juu ya hao Wafilisti.Wafilisti wakasimama juu ya mlima upande huu, na Waisraeli wakasimama juu ya mlima upande huu, napo palikuwa na hilo bonde katikati. Ndipo akatoka shujaa katika kambi ya Wafilisti, aliyeitwa Goliathi, wa Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita na shibiri moja. Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani, tena amevaa darii ya shaba; na uzani wake ile darii ya shaba ulikuwa shekeli elfu tano za shaba. Tena amevaa mabamba ya shaba miguuni mwake, naye alikuwa na mkuki wa shaba kati ya mabega; yake. Na mti wa fumo lake ulikuwa kama mti wa mfumaji; na kichwa cha mkuki wake kilikuwa shekeli mia sita za chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia ngao yake akamtangulia. Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. Kama akiweza kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane. Basi Sauli na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.”

 

1Samuel 17:24-28 “Na watu wote wa Israeli walipomwona yule mtu wakakimbia, wakaogopa sana. Watu wa Israeli wakasema, Je! Mmemwona mtu huyu aliyepanda huko? Hakika ametokea ili awatukane Israeli; basi, itakuwa, mtu yule atakayemwua, mfalme atamtajirisha kwa utajiri mwingi, naye atamwoza binti yake, na kuifanya mbari ya baba yake kuwa huru katika Israeli. Daudi akaongea na watu waliosimama karibu, akisema, Je! Atafanyiwaje yeye atakayemwua Mfilisti huyo, na kuwaondolea Israeli aibu hii? Maana Mfilisti huyu asiyetahiriwa ni nani hata awatukane majeshi ya Mungu aliye hai? Nao watu wakamjibu vivyo hivyo, wakisema, Ndivyo atakavyofanyiwa mtu yule atakayemwua. Naye Eliabu, mkubwa wake, alisikia hapo alipoongea na watu; na hasira yake Eliabu ikawaka juu ya Daudi, akasema, Mbona wewe umeshuka hapa? Na kondoo wale wachache umemwachia nani kule nyikani? Mimi nakujua kiburi chako, na ubaya wa moyo wako; maana umeshuka ili upate kuvitazama vita.”

 

1Samuel 17:32-33 “Daudi akamwambia Sauli, Asizimie moyo mtu ye yote kwa ajili ya huyu; mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana na Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake.”

 

1Samuel 17:37 “Daudi akasema, Bwana aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na Bwana atakuwa pamoja nawe.”

 

1Samuel 17:42-46Hata Mfilisti alipotazama huku na huku, akamwona Daudi akamdharau; kwa kuwa ni kijana tu mwekundu, tena ana sura nzuri. Mfilisti akamwambia Daudi, Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake. Mfilisti akamwambia Daudi, Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni. Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli.”

 

Daudi ni mfano wa watu ambao hawakukubali kuishi kwa maneno ya kukatisha tamaa kama angeyasikiliza aibu kubwa ingelipata taifa zima la Israel, lakini aliishi zaidi ya maneno alimkiri Mungu mwenye nguvu aliyeweza kumuokoa yeye na wanyama wakali wakiwepo simba na dubu akitambua ya kuwa Mungu huyu na neno lake ana nguvu kuliko maneno na umbile la adui

 

b.      Hanna na Penina – Hana alipata maneno ya kuumiza na kukatisha tamaa kutoka kwa Penina kwa sababu Hana hakuwa na watoto, alichokozwa na kusemwa vibaya kwa maneno hasi Penina alifanya hivyo mwaka kwa mwaka mpaka Hana aliacha kula na kusikitishwa sana naye

 

1Samuel 1:6-7 “Ila mwenzake humchokoza sana, hata kumsikitisha, kwa sababu Bwana alikuwa amemfunga tumbo. Tena mumewe akafanya hivyo mwaka kwa mwaka, hapo yule mwanamke alipokwea kwenda nyumbani kwa Bwana, ndivyo yule alivyomchokoza; basi, kwa hiyo, yeye akalia, asile chakula.”

 

Hata pamoja na maneno ya kuumiza na kukatisha tamaa Hana alifamya uamuzi wa kuishi zaidi ya maneno yeye aliongeza kasi kwenye maombi na kumlilia Mungu na Mungu hakumuangusha kwani alimjibu na kumpa mtoto Samuel na watoto wengine, kinywa cha Hana kilizungumza lugha nyingine kwa furaha

 

1Samuel 2:1-10 “Naye Hana akaomba, akasema, Moyo wangu wamshangilia Bwana, Pembe yangu imetukuka katika Bwana, Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu; Kwa kuwa naufurahia wokovu wako; Hakuna aliye mtakatifu kama Bwana; Kwa maana hakuna ye yote ila wewe, Wala hakuna mwamba kama Mungu wetu. Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa maarifa, Na matendo hupimwa na yeye kwa mizani. Pinde zao mashujaa zimevunjika, Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu. Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula, Na hao waliokuwa na njaa wamepata raha. Naam, huyo aliyekua tasa amezaa watoto saba, Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika. Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu. Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka ulimwengu juu yake. Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake; Bali waovu watanyamazishwa gizani, Maana kwa nguvu hakuna atakayeshinda; Washindanao na Bwana watapondwa kabisa; Toka mbinguni yeye atawapigia radi; Bwana ataihukumu miisho ya dunia; Naye atampa mfalme wake nguvu, Na kuitukuza pembe ya masihi wake.”

 

Kaka zangu na dada zangu Mungu anatutaka tuishi zaidi maneno, hatuishi kwa sababu ya maneno ya watu tunaishi kwa sababu ya neno la Mungu, ushindi wa maisha yetu umefungwa katika neno la Mungu na sio katika maneno ya wanadamu sisi ni washindi na zaidi ya kushinda. Hakikisha katika maisha yako unajaa neno la Mungu ili kila neno utakaloshambuliwa uwe unajibu lake katika neno la Mungu Ni neno la Mungu tu litakaloulinda moyo wako na mashambulizi ya shetani, litaiweka sawa akili yako litakulinda na kukuhifadhi  maneno ya kukatisha tamaa hayatakuwa na nguvu kwa mtu aliyejaa neno la Mungu ushindi wako utakuwa kama Daudi dhidi ya Goliati na Hana dhidi ya Penina, au Nehemia na akina Sanbalati, jifiche katika neno la Mungu imba ahadi zake kumbuka hakuna silaha itakayofanyika juu yako ambayo itafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka dhidi yako katika kuhukumu utauhukumu kuwa mkosa na huu ndio urithi wa watumishi wa Mungu!

 

Isaya 54:17 “Utathibitika katika haki; utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa; na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia.Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako. Tazama, nimemwumba mhunzi avukutaye moto wa makaa, akatoa silaha kwa kazi yake; nami nimemwumba mharibu ili aharibu. Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.”

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: