Yeremia 8:21-22 “Kwa sababu ya maumivu ya binti ya watu wangu nimeumia mimi; nimevaa kaniki; ushangao umenishika. Je! Hapana zeri katika Gileadi? Huko hakuna tabibu? Mbona, basi, haijarejea afya ya binti ya watu wangu?”
Utangulizi:
Tuwapo duniani kama wanadamu
wakati mwingine yako majeraha na maumivu ya mambo tunayokutana nayo katika
maisha ambayo ni magumu kupona hususani majeraha ya moyoni, wako watu ambao
wanaishi kwa mashaka, wamevunjika moyo, wamekosa amani, wamekata tamaa, wana
misiba ya aina mbalimbali katika maisha na wengine wameumizwa na mioyo yao
imejaa uchungu hakuna utulivu katika maisha yao, wamelia machozi mpaka
wamechoka, hawawezi kutibiwa katika hali ya kawaida, hawawezi kusaidiwa na
wanasaikolojia wala washauri nasaha, wanateseka, wana maumivu endelevu wana makovu,
mashaka na mgandamizo wa mawazo wameshindwa kupata tiba ya kibinadamu inayoweza
kuwasaidia, hakuna dawa, leo nawajulisha kuwa iko Dawa isiyoshindwa!
Nyakati za Biblia ilikuwepo dawa
inayojulikana kama “Dawa isiyoshindwa”
ambayo ilikuwa na uwezo wa kutuliza maumivu na kurejesha afya ya mtu
aliyeumizwa dawa hii ilijulikana kama Zeri ya Gileadi, dawa hii Zeri ilikuwa
inapatikana katika sehemu ya kaskazini Mashariki ya Israel katika bonde la mto
Jordan, dawa hii ilikuwa inatumika kutibu na kufariji watu waliopatwa na
maumivu na majeraha ya aina mbalimbali sugu, Dawa hii ilijipatia umaarufu
mkubwa na ilikuwa ni moja ya bidhaa adimu sana.
Kwa hiyo ilikuwa kama mtu
amejeruhiwa na kuumizwa, na kisha ikaonekana kana kwamba Jeraha lake haliponi
na akahangaika kutumia dawa nyingi sana na zikigonga ukuta basi dawa ya mwisho
ilipendekezwa kuwa Zeri kwa sababu, Zeri ilikuwa ni dawa isiyoshindwa kwa
jitihada za kibinadamu.
Yeremia 46:11-12 “Panda uende Gileadi,
ukatwae zeri, Ee binti, bikira wa Misri; unatumia dawa nyingi bure tu; hupati
kupona kamwe. Mataifa wamesikia habari za aibu yako, nayo dunia imejaa kilio
chako; maana shujaa amejikwaa juu ya shujaa mwenzake, wameanguka wote wawili
pamoja.”
Leo basi tutachukua muda kuzungumzia kwa ufupi kuhusiana ana dawa hii isiyoshindwa iliyotumika kutibu majeraha sugu unhealed wounds or chronic wound iliyoitwa Zeri ya Gileadi kwa kuzingatia vipengele vya msingi vitatu vifuatavyo:-
·
Ufahamu
kuhusu Zeri ya Gilead
·
Matumizi
ya Zeri nyakati za Biblia
· Dawa isiyoshindwa
Ufahamu kuhusu Zeri ya Gilead
Ni muhimu kufahamu kuwa Zeri
nyakati za Biblia ulikuwa ni mmea ambao ulitumika kutengenezea viungo na mafuta
yenye harufu nzuri ambayo yalitumika kutibu majeraha na vidonda sugu pamoja na
maradhi mbalimbali yaliyoshindikana, Dawa hii ilipatikana katika eneo maarufu
huko Jordani kaskazini mashariki mwa Israel katika bonde la mto Jordani ambako
kulikuwa na misitu mizito yenye mimea ya dawa zenye thamani kubwa ukiwepo mmea
huu uitwao Zeri ambao kwa Kiebrania unaitwa
“Tsoriy” na kwa kiingereza “Balm of Gilead” Sifa mojawapo ya Zeri ilikuwa ni kutibu
kwa haraka, kuleta faraja na urejesho wa uponyaji wa jeraha lililoshindikana,
Kama mtu alikuwa anakuheshimu sana mojawapo ya zawadi ambayo angeweza kukuletea
pamoja na viungo mbalimbali basi angeweza kukupatia na zeri katika zawadi zake,
lakini moja ya biashara kubwa sana nyakati za agano la kale pamoja na mambo
mengine ilikuwa ni Zeri ambayo kimsingi
inapatikana Gilead tu!
Mwanzo 37:23-25 “Ikawa Yusufu alipofika kwa
ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa
wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji. Nao wakakaa
kitako kula chakula; wakainua macho yao, wakaona, msafara wa Waishmaeli
wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane,
wakisafiri kuvichukua mpaka Misri.”
Mwanzo 43:11-13 “Israeli, baba yao,
akawaambia, Kama ndivyo, fanyeni hivi; twaeni tunu za nchi katika vyombo vyenu,
mkamchukulie mtu huyo zawadi, zeri kidogo, na asali kidogo, ubani, na manemane,
na jozi, na lozi. Mkatwae fedha maradufu mikononi mwenu, na fedha zile zilizorudishwa
kinywani mwa magunia yenu zirudisheni mikononi mwenu; labda zilisahauliwa. Mtwaeni
na ndugu yenu, mwondoke na kurudi kwa mtu yule.”
Matumizi ya Zeri nyakati za Biblia
Nyakati za Biblia ilikuwa kama
mtu amepata majeraha na kuumia na kutibiwa kwa tiba za aina nyingine na tiba
hizo zikashindikana kisha jeraha likachukua wiki zaidi ya nne mpaka sita bila
kupona kwa matabibu wa kila aina basi shauri la mwisho kwa mgonjwa angeshauriwa
apande kwenda Gilead kwani huko angeweza kupata tiba ya zeri dawa isiyoshindwa ambayo ilijulikana
kama zeri ya Gilead
Yeremia 8:21-22 “Kwa sababu ya maumivu ya
binti ya watu wangu nimeumia mimi; nimevaa kaniki; ushangao umenishika. Je!
Hapana zeri katika Gileadi? Huko hakuna tabibu? Mbona, basi, haijarejea afya ya
binti ya watu wangu?”
Yeremia 46:11-12 “Panda uende Gileadi,
ukatwae zeri, Ee binti, bikira wa Misri; unatumia dawa nyingi bure tu; hupati
kupona kamwe. Mataifa wamesikia habari za aibu yako, nayo dunia imejaa kilio
chako; maana shujaa amejikwaa juu ya shujaa mwenzake, wameanguka wote wawili
pamoja.”
Yeremia 51:6-8 “Kimbieni kutoka kati ya
Babeli, kila mtu na ajiokoe nafsi yake; msikatiliwe mbali katika uovu wake;
maana ni wakati wa kisasi cha Bwana, atamlipa malipo. Babeli umekuwa kikombe
cha dhahabu mkononi mwa Bwana; kilicholevya dunia yote; mataifa wamekunywa
mvinyo wake; kwa sababu hiyo mataifa wameingiwa na wazimu. Babeli umeanguka na
kuangamia ghafula; mpigieni yowe; twaeni zeri kwa maumivu yake; ili labda apate
kuponywa.”
Unaona nyakati za Biblia mtu alipokuwa anaugua na mauti ikaonekana inanyemelea maisha ya mgonjwa na kuiondolea familia faraja suluhu kubwa ilikuwa ni kwenda Gilead au kutafuita tabibu mwenye ujuzi wa kutibu kwa kutumia Zeri ili yamkini kuweza kurejesha afya ya muathirika, hii ilikuwa ni dawa isiyoshindwa ilikuwa ni suluhu na mwisho wa changamoto ya mtu, wagonjwa waliposikia Zeri imepatikana walirudisha matumaini wakijua ya kuwa uponyaji wao umepatikana kwani Zeri iliponya maumivu yao kwa haraka na kuwarejeshea matumaini, na kuwaondolea msongo wa mawazo na mashaka ya wauguzaji na kilio cha waliokata tamaa kingefikia ukingoni, zeri ilirudisha mzunguko wa uhai wa damu, ingedhoofisha maambukizi, na kurejesha mfumo wa kinga kwa haraka! Na kuziponya seli zilizoanza kufa na kusababisha uponyaji ulikuwa ni mmea wa ajabu na wa faida.
Dawa isiyoshindwa
Kimsingi maandiko ya agano la
kale yalikuwa yanatoa picha ya kinabii (metaphor) iliyokuwa ikimuonyesha Yesu
Kristo kama dawa ya kweli isiyoshindwa, Yesu Kristo ndiye zeri ya Gilead, yeye
ndiye mwenye uwezo wa kutibu, majeraha ya moyo na kuleta faraja kwa watu
waliokosa tiba katika mazingira mengine ya kawaida, Zeri ya Gilead ilikuwa ikitoa
unabii kivuli wa dawa halisi isiyoshindwa na ni dawa ya milele yenyewe inauwezo
wa kuponya kila kilichoshindikana katika mazingira ya kawaida ya kibinadamu,
Uponyaji uliotolewa na zeri ulikuwa ni uponyaji wa muda tu lakini uponyaji
unaotolewa na Yesu Kristo ni uponyaji wa milele, Yesu sio tu anauwezo wa kuponya
majeraha lakini pia ana uwezo wa kuponya mioyo iliyojerushiwa kwa dhambi na
changamoto mbalimbali za maisha
Yesu Kristo ni tabibu wa roho
zote zilizojeruhiwa, kama zeri iliponya mwili na maumivu yake Yeye Yesu Kristo
ana uwezo wa kuponya mwili nafsi na roho na kufutilia mbali majeraha yote ya
moyoni na uchungu wa aina mbalimbali, sio hivyo tu kila ugonjwa na changamoto
zilizowakumba watu ambazo zilishindikana kwa matabibu wote zilipoletwa kwa Yesu
Kristo ilikuwa ni kama mtu amepanda kwenda Gileaed kwani angepokea uponyaji wake wa uzina huu
bna ule ujao wa milele!
Luka 4:17-19 “Akapewa chuo cha nabii Isaya,
akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu,
Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma
kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha
huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”
Marko 5:25-29 “Na mwanamke mmoja mwenye
kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya
matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo,
bali hali yake ilizidi kuwa mbaya aliposikia habari za Yesu, alipita katika
mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake
tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini
mwake kwamba amepona msiba ule.”
1Petro 2:23-25 “Yeye alipotukanwa,
hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye
kwa haki. Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti,
tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa
kwake mliponywa. Kwa maana mlikuwa mnapotea kama kondoo; lakini sasa mmemrudia
Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu.”
Je hapana zeri katika Gilead? Je
hakuna tabibu huko? Mbona watu wanaumia mbona watu hawaponi? Ni kwa sababu watu
hawataki wenyewe kuja kwa Yesu, kama watu wa Mungu watajinyenyekesha na
kutubu na kuacha njia zao mbaya uponyaji
upo na unawasubiria watu wa Mungu, tunatoa wito kwa watu wote waliojeruhiwa na
wenye maumivu waje kwa Yesu kwa uponyaji yeye ni dawa ya kweli yeye ni dawa
isiyoshindwa!
2Nyakati 7:13-15 “Nikizifunga mbingu isiwe
mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa
watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na
kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na
kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na
masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.”
Ni tabibu wa karibu, tabibu wa
ajabu! Tenzi Na:7
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni