Isaya 49:14-16 “Bali Sayuni alisema, YEHOVA
ameniacha, Bwana amenisahau. Je!
Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo
lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama,
nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.”
Utangulizi:
Upendo wa Mungu kwa watu wake ni
mkubwa sana na wa kudumu, hata kuliko upendo wa mama anayenyonyesha, Mungu
anajenga hoja kwa watu wake ambao walikuwa utumwani huko Babeli na walikuwa
wanadhani ya kuwa kwa vile wanapita katika hali ngumu sana na wameonewa na adui
zao kwa kiwango cha kusikitisha sana waliona kama Mungu amewaacha na pia kama
vile amewasahau, akijibu hoja zao Mungu anaanza kwa kujibu manung’uniko yao kwa
kuuliza swali Je mama aweza kumsahau
mtoto anayenyonya? Asimuhurumie mwana watumbo lake? Kisha anasema hawa
wanaweza, Lakini Mimi sitakusahau wewe! Mungu anatuonyesha kuwa yeye ana upendo
na huruma ya kweli isiyotikisika kama ilivyo ya mama anyonyeshaye yeye ni
zaidi! Yeye akionyesha jinsi wewe ulivyo wa muhimu kwake anasema amekuchora
katika vitanga vya mikono yake.
Isaya 49:16-19 “Tazama, nimekuchora katika
vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.Watoto wako wafanya
haraka, hao wakuharibuo, nao waliokufanya ukiwa, watatoka kwako. Inua macho yako, ukatazame pande zote; hao
wote wanajikusanya na kukujia. Kama niishivyo, asema Bwana, hakika utajivika na
hao wote, kama kwa uzuri, nawe utajifungia hao, kama bibi arusi. Maana katika
habari za mahali pako palipokuwa ukiwa, pasipokaliwa na watu, na nchi yako
iliyoharibika hakika sasa utakuwa mwembamba usiwatoshe wenyeji wako, nao
waliokumeza watakuwa mbali.”
Mungu anajizungumzia mwenyewe
kuwa ni Mungu mwenye kujali, anajielezea kuwa huruma zake kwa watu wake sio za
kawaida, upendo wake kwa watu wake hauwezi kufananishwa na lolote, yeye ana
huruma na upendo na ni mwenye kujali kuliko mama anayenyonyesha, yaani kama
mama anavyomuhurumia mwana wa tumbo lake, yeye ni zaidi, hakuna unachoweza
kulinganisha naye namna anavyojali na kujihusisha na maisha ya watu wake,
hakuna unachoweza kulinganisha nacho duniani, wote tunafahamu jinsi wakina mama
wanavyowajali watoto wachanga lakini maelezo ya Mungu yanaonyesha kuwa kujali
kwao huko hakuwezi kamwe kufananishwa na kujali kwa Mungu
Neno ameniacha katika lugha ya Kiebrania linasomeka kama “âzab”
kwa kiingereza fosake ambalo
limetumiwa mara 129 na katika
Kiyunani limetumika neno “aniēmi” kwa kiingereza leave au abandoned ambalo maana zake
“turn away from entirely” sawa na
neno kutelekeza katika Kiswahili au
kuacha bila msaada au kukuacha kabisa katika ufafanuzi wa kutelekeza maana yake
ni unyanyasaji wa kumuacha mtu anayehitaji msaada wako bila malezi au kumpa
mahitaji yanayohitajika kwa kutokumjali, Mwanadamu anaweza kutelekeza na kuacha
hata kitoto kichanga kinachonyonya lakini Mungu hawezi kukuacha wewe! Tutajifunza
somo hili Je mama aweza kumsahau mtoto anayenyonya kwa kuzingatia vipengele
vitatu vifuatavyo:-
·
Yehova ameniacha,
Bwana amenisahau.
·
Je mama
aweza kumsahau mtoto anayenyonya.
·
Mimi
sitakusahau wewe.
Yehova ameniacha, Bwana amenisahau
Isaya 49:14 “Bali Sayuni alisema, YEHOVA
ameniacha, Bwana amenisahau.” Kulikuwa na manung’uniko miongoni mwa watu wa Mungu kutokana na hali ngumu
walizokuwa wanazipitia wakaona ni kama Mungu amewaacha, na ni kama Mungu
hawajali, Sayuni inawakilisha watu wa Mungu hapo, Sayuni ni mji wa Yerusalem na
hapo unasimama kama uwakilishi wa watu wa Mungu, Mungu ameahidi mara nyingi
katika neno lake ya kuwa atawasaidia watu wake na kuwaokoa, lakini wao walipokuwa
wakiyatazama mazingira ya nje na hisia zao za ndani waliona kama wametelekezwa
kama wameachwa, watu wa Mungu walichukuliwa utumwani na mfalme katili, mnyama
sana, ambaye aliitiisha Dunia kwa hofu, akiiongoza dunia kwa mkono wa chuma
yaani dikteta, alikuwa na nafsi ngumu sana katili mno, aliipiga Yerusalem yaani
Sayuni, akaliharibu hekalu lao na kulitia moto, mji wote uliharibiwa, alikuwa
tajiri sana kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufanya biashara, alikuwa na nguvu
kiasi cha kusahau kuwa kuna Mungu na kutaka hata kuabudiwa yeye, aliwaonea watu
wa Mungu na kuwafanyia unyama, Wayahudi walipelekwa utumwani kilomita 1448 sawa na miles 900 kwa miguu moja kwa moja bila
kupumzika wala kupewa nafasi ya kuomba au kusali njiani, waliishi maisha ya
huzuni Babeli na walilia sana walipokumbuka Sayuni nyumbani kwao.
Zaburi 137:1-4 “Kando ya mito ya Babeli
ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati
yake Tulivitundika vinubi vyetu. Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka
tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za
Sayuni. Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika nchi ya ugeni?”
Kutokana na changamoto lukuki
walizokuwa wamekutana nazo, waliona kuwa ni Dhahiri kuwa Mungu amewaacha na sio
tu kuwa amewaacha lakini pia ni kama amewasahau, Mungu alikuwa amewaahidi kuwa
atawaletea mwokozi, lakini hawakuona matumaini yoyote na badala yake hali yao ilizidi
kuwa mbaya, Ndivyo wote tunavyofikiri kila wakati na kujiona wakati hali inapokuwa mbaya,
tunadhani ya kuwa maombi yetu hayasikiwi, hakuna mguso, hakuna uponyaji, hakuna
nuru ni giza kila mahali, nasfi inasagika sagika tunanung’unika, tunalia
tunadhani na kufikiri kuwa Mungu ametuacha, hivi ndivyo walivyokuwa wakifikiri
Wayahudi wakati walipokuwa katika hali ngumu utumwani.
Je mama aweza kumsahau mtoto anayenyonya.
Kabla Mungu hajajibu hoja yao,
aliwataka kwanza wafikiri kuhusu mfano wa mama anayenyonyesha, Mungu aliutumia
mfano huu kwa sababu ulikuwa ni mfano uliokaribu na unaoleweka vema na wanadamu
wote wenye akili timamu, mfano wa mama anayenyonyesha unajenga uzito mkubwa wa
kisaokolojia, kihisia, na kiroho, kwa sababu
1.
Mama
anayenyonyesha ana ukaribu wa hali ya juu sana na mwanaye – Ni vigumu sana
Mama kuwa mbali na mtoto anayenyonya, na ndio maana utaweza kuona sio rahisi
kumuacha hata kama mama ana safari mtoto anayenyonya yuko karibu sana na moyo
wa mama yake na akili ya mama yake kwa hiyo kuna uhusiano wa karibu mno, mama
anayenyonyesha akimtelekeza mtoto katika hali ya kawaida, kama hatafikiriwa
kuwa ni katili basi huenda akafikiriwa kuwa hana akili, uhusiano wa mama na
mtoto anyonyaye ni uhusiano wa asili uliokomaa na usioweza kutenganishwa katika
mazingira yoyote kwa hiyo Mungu anatuthibitishia kuwa yeye anawahurumia watoto
wake kuliko mama anayenyonyesha.
Zaburi 103:13-14 “Kama
vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao. Kwa
maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.”
2.
Mama anayenyonyesha anaijua hali ya mtoto kwa
ukaribu zaidi – Mama anayenyonyesha anaijua hali ya mtoto kwa ukaribu zaidi
kuliko watu wengine nyumbani, anaweza kujua kama ana joto, njaa na hali
nyingine yoyote anayoipitia, Mungu anaonyesha kupitia mfano wa mama
anyonyeshaye ya kuwa yeye anatujua vema zaidi kuliko mtu awaye yote anatujua
kukaa kwetu, kuamka kwetu na mawazo yetu na maneno yetu hata kabla hatujayasema
na zaidi ya yote hata nywele zetu za kichwani yeye Mungu peke yake anajua idadi
yake
Zaburi 139:1-4 “Ee
Bwana, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu;
Umelifahamu wazo langu tokea mbali. Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote. Maana hamna neno ulimini mwangu Usilolijua kabisa,
Bwana.”
Luka 12:6-7 “Je!
Mashomoro watano hawauzwi kwa senti mbili? Wala hasahauliwi hata mmojawapo
mbele za Mungu. Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope
basi, bora ninyi kuliko mashomoro wengi.”
3.
Mama
anayenyonyesha ni mwangalizi na mlinzi wa mtoto – Kitendo cha kunyonyesha
humfanya mama awe mwangalizi wa karibu na wa muda wote wa mtoto na mlinzi, kwa hiyo
mfano wa mama anayejali unatufundisha ya
kuwa Mungu ni mlinzi na mwangalizi wa karibu anayetuangalia usiku na mchana na
hatuwezi kupotea katika macho yake, Mama mlezi hata wakati wa usiku halali wala
hasinzii kwaajili ya kuhakikisha usalama wa mtoto
Zaburi 121:3-8 “Asiuache
mguu wako usogezwe; Asisinzie akulindaye; Naam, hatasinzia wala hatalala
usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli. Bwana ndiye mlinzi wako; Bwana ni uvuli
mkono wako wa kuume. Jua halitakupiga mchana, Wala mwezi wakati wa usiku. Bwana
atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako. Bwana atakulinda utokapo na
uingiapo, Tangu sasa na hata milele.”
Isaya 46:3-4 “Nisikilizeni,
enyi wa nyumba ya Yakobo, ninyi mlio mabaki ya nyumba ya Israeli, mliochukuliwa
nami tangu tumboni, mlioinuliwa tangu mimbani; na hata uzee wenu mimi ndiye, na
hata wakati wenu wa mvi nitawachukueni; nimefanya, nami nitachukua; naam, nitachukua
na kuokoa.”
4.
Mama
anayenyonyesha hawezi kusahau mtoto wake – haijawahi kutokea mama
anayenyonyesha akasahau kuwa ana mtoto wake anayemtegemea yeye, Mungu
anaonyesha kwa mfano huu kuwa hawezi kutusahau kamwe, na kulithibitisha hilo
anasema wazi kuwa amatuchora katika vitanga vya mikono yake, wakati ambapo baba yako na mama yako wanaweza kukuacha yeye bwana
anakupokea na kamwe hawezi kukuacha
Isaya 49:15-16 “Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto
wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza
kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya
mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.”
Zaburi 27:9-10 “Usinifiche
uso wako, Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu,
usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. Baba yangu na mama yangu
wameniacha, Bali Bwana atanikaribisha kwake.”
Kwa hiyo neno la Mungu
linatuthibitishia kuwa ziko nyakati ambapo hata mama wa kawaida wa kibinadamu
anaweza kumsahau mtoto anayenyonya, Lakini sivyo kwa Mungu, ninakumbuka kuna
wakati ambapo, kulitokea ajali ya jahazi kwenye bahari huko Pemba kuja Pangani,
wakati wa ajali hiyo maji yalianza kuingia kwenye jahazi, na matokeo yake
baadhi ya kina mama kwa hofu ya kifo waliwatupa watoto wao baharini, upendo huu
wa asili wa akina mama kuna wakati unagoma lakini upendo na huruma ya Mungu
wetu haina wakati wa kugoma, Je mama aweza kumsahau mtoto wake anayenyonya?
Huyo anaweza lakini sio Mungu wetu tunayemtegemea na kumuabudu.
Mimi sitakusahau wewe.
Isaya 49:14-16 “Bali Sayuni alisema, YEHOVA
ameniacha, Bwana amenisahau. Je!
Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo
lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora
katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.”
Wakati jamii ilipokuwa inapitia
changamoto za aina mbalimbali wao walidhani na kufikiri ya kuwa Mungu amewaacha
na kuwasahau, Hata hivyo tunaona Mungu nanatumia mfano huo wenye mguso wa
kupita kawaida kujijengea hoja madhubuti ili wanadamu waweze kufahamu jinsi
Mungu wetu anavyojali, mama anapokuwa amemsahau mtoto kwa kawaida kibinadamu
linakuwa ni jambo lenye kushangaza sana
wao wana upendo wa asili unaoumiza, Mungu anaonyesha kuwa yeye anaumia
zaidi kuliko mwandamu wa kawaida na anaonyesha ya kuwa upendo wa mama unaweza
kuharibika lakini sio wake, kwa hiyo hakuna makosa yanatokea katika maisha yako
ukadhani Mungu amekosea au haoni, kila mwanadamu anapopita katika changamoto
mbalimbli za maisha hufikiri kuwa Mungu amemuacha, Yesu pale Msalabani alilia
Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha lakini Mungu alikuwa na mpango wa
kumfufua mwanae na kumpaisha juu Mbinguni na kuweka adui zake wote chini ya
miguu yake, yeye anathibitisha ya kuwa hata kama upendo wa mama unaweza kufikia
ukingoni wake hauwezi, Mungu anakujua, Mungu anakufikiria, Mungu anakujali,
Mungu anakulinda, Mungu anakulisha, Mungu anakutunza, Mungu anatupenda kupita upendo wa kibinadamu
na upendo wake ni wa milele kwa hiyo haupaswi kuogopa unayoyapitia
Yeremia 31:3 “Bwana alinitokea zamani,
akisema, Naam nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa
fadhili zangu.”
Ziko nyakati katika maisha yetu
unaweza kufikri kuwa umeachwa na Mungu, leo nataka tujikumbushe kuwa mawazo
hayo ni batili, na hasi na sivyo ilivyo kwa Mungu wetu kutokana na maneno yake
ya uzima, Kila mtu anaweza kukuacha lakini sio Mungu wetu ahadi zake ni ndio na
kweli na kamwe hawezi kukusahau wewe, Yeye ni mwaminifu kama alivyoahidi
atatenda.
“Je mama aweza kumsahau
mtoto anayenyonya? Huyo aweza, lakini Mungu hatakusahau wewe”
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni