Maombolezo 5:19-21. “Wewe, Bwana, unadumu milele; Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi. Mbona watusahau sikuzote; Na kutuacha muda huu mwingi? Ee Bwana, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.”
.jpg)
Utangulizi:
Je? umewahi kufikiri kuwa siku
kadhaa au miaka kadhaa huko nyuma ilikuwa bora katika maisha yako kuliko ilivyo
sasa? Siku ambazo furaha yako ilikuwa timilifu, siku ambazo afya yako ilikuwa
njema, siku ambazo uhusiano wako na Mungu ulikuwa mzuri sana, siku ambazo
ulikuwa mwombaji sana, siku ambazo ulikuwa hukosi mikesha, huachi kufunga, siku
ambazo hata upitie taabu gani hukuona shida, siku ambazo ni kama zilikuwa siku
za ushindi wako, siku ambazo familia ziliishi kijamaa, tuliwatembelea Babu na
Bibi zetu vijijini, tulikutana na ndugu wengi, ulikuwa na marafiki wengi, watu
walikaa pamoja kwa umoja na upendo ulikuwa ni kama umefikia kilele cha hali ya
juu cha furaha ya maisha, unazikumbuka siku zile na unatamani kama zingerudia
tena upya! Hali kama hii ndiyo iliyomkuta nabii Yeremia alikumbuka siku za
utukufu mkubwa wa Mungu katika Uyahudi, wakati Hekalu la Yerusalem lililojengwa
na Suleimani bado halijatiwa moto na kubomolewa zilikuwa siku njema, lakini
Mungu alikuwa ameziondoa na sasa anaona uharibifu na mambo hayako kama siku
zile, anaona ni kama Mungu amewaacha na kuwasahau kwa muda mrefu na kwa siku
nyingi sana.
Maombolezo 5:19-21. “Wewe, Bwana, unadumu
milele; Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi. Mbona watusahau
sikuzote; Na kutuacha muda huu mwingi? Ee Bwana, utugeuze kwako, nasi
tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.”
Hali hii ni hali ya kuhuzunisha
sana ni hali yenye mchanganyiko wa majonzi na kukata tamaa ni wakati ambapo
maisha ya mwanadamu yanakuwa yamezidiwa na kumbukumbu ya mambo mabaya
yaliyotokea na yanayoendelea katika wakati ulioko, huku ukikumbuka siku zile za
utukufu ambazo sasa unatamani ungezirudisha siku nyuma, uweze kuzifurahia na
kupata Amani, Kisaikolojia hili tukio linaitwa “Nostalgia”. Nostalgia is a state
of being sick emotional for the past period or homesick, university days etc. Hali
ya kuumwa kihisia kwaajili ya kukumbuka mambo mazuri ya zamani au kukumbuka
nyumbani au siku zako za chuoni na kadhalika, Yeremia sasa anaumwa ugonjwa huu
na anamuomba Mungu kwamba asikawie anamuomba Mungu awageuze nao watageuka na
azifanye mpya siku zao kama siku za zamani!, ilikuwa ni sauti ya kuomboleza iliyojaa
uchungu hasa baada ya Hekalu la Yerusalem kutiwa moto na kubomolewa na mfalme
wa Babeli mwaka 586 KK Yeye alikuwa
ameshuhudia siku nzuri za utukufu wa Hekalu hilo na siku mbaya za uharibifu mkubwa
Hekalu likiwa limebomolewa, watu wamechukuliwa kwenda uhamishoni, taifa
limepoteza fahari yake, na Mungu anaonekana kuwa kimya kwa hiyo moyo wake
umejaa ombi lenye huzuni, toba na matumaini. Wewe je unapitia hali ya namna
gani hapo ulipo? Familia yako je? Umri wako je? Ndoa yako Je? Hali yako ya
kiuchumi, hali yako ya kiroho? Uhusiano wako je? Kanisa lako je kuna uamsho?
Watu wanampenda Mungu kama zamani? Uzuri wako? kazini kwako je zipi siku bora
katika maisha yako? Leo tutachukua muda kujifunza kwa undani somo hili muhimu
lenye kichwa Zifanye mpya siku zetu kama
siku za kale! Na tutajifunza somo hili litakalo kurejeshea matumaini kwa
kuzingatia vipengele vitatu muhimu vufuatavyo;-
·
Kilio cha
kukumbuka siku za kale
·
Sababu za
kukumbuka siku za kale
·
Zifanye
mpya siku zetu kama siku za kale!
Kilio cha kukumbuka siku za kale
Maombolezo 5:19-21. “Wewe, Bwana, unadumu
milele; Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi. Mbona watusahau
sikuzote; Na kutuacha muda huu mwingi? Ee Bwana, utugeuze kwako, nasi
tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.”
Kimsingi kifungu hiki yalikuwa ni
maombolezo au kilio ya Nabii Yeremia ambaye alikuwa akiomboleza baada ya
mashambulizi mazito na hali mbaya ambayo watu wake na yeye mwenyewe walikuwa
wameishuhudia, uharibifu mkubwa uliofanywa na majeshi ya Wakaldayo chini ya
utawala wa Nebukadreza mfalme wa Babeli, Yeremia alikuwa anaona uchungu na sasa
anaomboleza juu ya mateso ya taifa huku akiona kana kwamba Mungu amewasahau na
kuwaacha kwa hiyo Yeremia alikuwa akimlilia Mungu na kumtaka awarejeze katika
hali yao waliyokuwa nayo mwanzo.
Kisaikolojia hisia hizi zinaitwa
“Nostalgic feelings” yaani hii ni
tabia ya mwanadamu kukumbuka siku nzuri za utukufu za zamani zilizokuwa za
furaha kwaajili ya kufidia hali ngumu anayokutana nayo katika wakati ulioko,
akili haitaki kuona mambo mabaya inataka mambo mazuri, akili haitaki nyakati
ngumu inataka amani raha na utulivu tu kwa hiyo kwa mfano umri unapokuwa
unaenda mtu anaanza kukumbuka enzi za ujana wake, anakumbuka siku za zamani
shuleni, chuoni na kadhalika, katika mahusiano anaanza kukumbuka siku nzuri
ambazo alikuwa na soko, anapendwa na kila mtu, unapokuwa mpweke unakumbuka
zamani familia zilipokuwa zinakaa pamoja na kula na pamoja na sikukuu
tulizokuwa tunaenda kwa Babu na Bibi na kujumuika pamoja, unapokuwa na afya
mbaya unakumbuka siku zako ulizokuwa na uzima ukiwa na nguvu, ulipokuwa na
uwezo wa kula nyama na mahindi ya kuchoma na sasa meno hayana uwezo huo tena,
unakumbuka siku za kale mlivyokuwa mkihubiri injili, unakumbuka wahubiri
wakubwa wa zamani, miujiza mikubwa iliyokuwa ikifanyika, unakumbuka nyakati
ambazo ulikuwa maarufu, na wakati wa mafanikio, unakumbuka nyimbo za zamani,
wachezaji wazuri wa timu yako uliyoipenda ilipokuwa ikitwaa ubingwa, unakumbuka
vipindi maalumu ambavyo sasa ni kama vimepita na haviwezi kurudi tena,
unakumbuka kipindi chako kiitwacho “the
golden age” hii ni hali ya kawaida wakati mwanadamu anapopitia magumu,
Israel walikumbuka chakula walichokuwa wanakula Misri japo walikuwa utumwani na
waliteswa
Hesabu 11:4-6 “Kisha mkutano wa wafuasi
waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena,
wakasema, N'nani atakayetupa nyama tule? Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri
bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu;
lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha
kutumaini isipokuwa hii mana tu.”
Hali kama hii inamkuta nabii
Yeremia anakumbuka jinsi Wayahudi walivyokuwa na amani katika taifa lao,
walivyokuwa wakipanda kwenda Hekaluni, anakumbuka Mungu alivyokuwa mtetezi wao
na jinsi Mungu aliyokuwa akisema nao na kuwapa wafalme na mahitaji yao, sasa
kila kitu kimebakia historia mambo yameharibika, watu wamechukuliwa uhamishoni
Babeli, Taifa limepoteza matumaini hakuna uhai tena, watu wako utumwani Mungu
yuko kimya amegeuza uso wake Yeremia anamlilia Mungu anamuomba kwa unyenyekevu,
anamuuliza mbona umetuacha, umetuacha muda mwingi, yaani unakawia, utugeuze
kwako nasi tutageuka, lakini zaidi ya yote zifanye mpya siku zetu kama siku za
kale.
Yeremia 5:20-21 “Mbona watusahau sikuzote;
Na kutuacha muda huu mwingi? Ee Bwana, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye
mpya siku zetu kama siku za kale.”
Sababu za kukumbuka siku za kale.
Maombolezo 5:19-21. “Wewe, Bwana, unadumu
milele; Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi. Mbona watusahau
sikuzote; Na kutuacha muda huu mwingi? Ee Bwana, utugeuze kwako, nasi
tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.”
Kwa nini Yeremia anakumbuka siku
za kale? Kwa nini wewe na mimi tunazikumbuka siku zile? Siku za kale ulikuwa ni
wakati wa utukufu, ulikuwa ni wakati watu wamejitoa kwa uaminifu, ulikuwa
wakati wa uhusiano mzuri na Mungu, ulikuwa ni wakati watu waliabudu na kutembea
na uwepo wa Mungu na miujiza mingi ilifanyika, ulikuwa ni wakati wa uhusiano
mzuri, urafiki mwema wakati wa kuoneana shauku, wakati ambapo kila unaloliomba
linajibiwa ulikuwa ni wakati wa Baraka, akitokea adui watu walijaa Roho
Mtakatifu na maadui walikimbizwa, taifa lilikuwa na heshima, watu walikuja
kutafuta Hekima na kumuabudu Mungu wa Yakobo, watu walivyotoa sadaka kwa
unyoofu wa moyo, katika mahusiano watu walipendana, sasa nyakati hizo haziko
tena, majumba yamekuwa magofu, upako haupo, miujiza imepotea, watu hawana
mikesha tena, hekalu limechomwa moto Yeremia analia anaomboleza anamwambia
Mungu zifanye upya siku zetu kama siku za kale, msikilizaji wangu na msomaji
wangu wewe u hali gani sasa? Uko wapi, familia yako iko wapi, ndoa yako iko
wapi, malezi yako yako wapi, furaha yako iko wapi, utukufu wako uko wapi, u hali
gani, kanisa lako li hali gani na wewe mwenyewe hali yako ya kiroho ikoje? Je unaugua kama Yeremia? Asante Mungu
kwaajili ya nabii Yeremia alimfahamu Mungu alijua ya kuwa Mungu anauwezo wa
kuzifanya upya ziku zetu na kuzirejeza zikawa kama siku za kale, leo ni siku
yako ambayo Bwana atazifanya upya siku zako Mungu wetu anauwezo wa kurejesha,
neno la Mungu linatueleza hivyo ana uwezo wa kututia nguvu
Zaburi 103:1-5 “Ee nafsi yangu, umhimidi
Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu. Ee nafsi
yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako
yote, Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya
fadhili na rehema, Aushibisha mema uzee wako, Ujana wako ukarejezwa kama tai;”
Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale!
Mungu anawezaje kuzifanya upya
siku zetu kama siku za kale? Yeremia alikuwa amegundua siri mojawapo muhimu
katika dua yake ambayo inatufunulia maswala muhimu sana yanayoweza kutuasaidia
na sisi katika Maisha yetu ili tusiweze kumezwa na huzuni kutokana na hali
unayoipitia!
Maombolezo 5:21 “Ee Bwana, utugeuze kwako,
nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.”
Katika lugha ya Kiebrania kifungu
hiki muhimu kinasomeka hivi “Hashivenoo ADONAI elecha venashuvah,
chadash yamenu ke’kedem” Kwa kiingereza maneno hayo yanasomeka hivi “turn us back Adonai and we will come back, renew our days, as they
were in the past”
Hashivenoo (shuv) - Uturudishe
nyuma, utugeuze, uturejeshe, tugeuze, tubadilishe, ni neno linalotumika katika
lugha ya Kiebrania mara nyingi likimaanisha kutubu, kubadilika moyo, kutoka
dhambini, kumrudia Mungu, Yeremia hasemi tunageuka anasema utugeuze,
akimaanisha Mungu ndiye chanzo cha toba ya kweli, hii inamaanisha toba ya kweli
sio matokeo ya hisia zetu na matakwa
yetu wanadamu tu bali ni neema ya Mungu inayoufanya moyo wa mwanadamu ulainike
na kumgeukia Mungu na kuamua kufuata njia za Mungu, kwa hiyo Yeremia anajua ya
kuwa siku njema kama za zamani haziwezi kurejea hivi hivi bila ya msaada wa
Mungu, ni lazima Mungu atuamshe tena na kuwasha upya moto ndani yetu
utakaotusaidia kurudi kwake na sio maamuzi ya kibinadamu.
Warumi 9:15-16 “Maana amwambia Musa,
Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye. Basi, kama ni
hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule
arehemuye, yaani, Mungu.”
Venashuvah – Tutageuka, tutaitikia,
tutakubali, yaani tutakubali mabadiliko tutatii, Yeremia anatambua kuwa ili
siku njema ziweze kurejeshwa ni lazima Mungu mwenyewe awashe moto wa
mawasiliano na kugeuza mioyo yetu na kuturehemu na sisi nasi tuitikie kwa kutii
kwa hiyo hapa tunajifunza kwamba uamsho ni ushirikiano kati ya Mungu na
Mwanadamu, Mungu anapoanza kwa rehema zake sisi ni wajibu wetu kuitikia kwa
toba na utii kwa uaminifu na moto ule utawaka.
Chadash (Chadesh) – Kufanywa upya kurejesha, kuhuhisha kujenga hari
mpya, neno Chadash linatokana na
neno Chodesh ambalo maana yake ni
mwezi mpya mwenzi mchanga, mwezi unaochomoza kwa upya kutoka gizani, Yeremia
anamsihi Mungu aanzishe jambo jipya katika mioyo yetu alete uhai katika mambo
yote yalitopotea atupe mwanzo mpya arejeshe hali ya kiroho, kiuchumi na
kimaisha aturejeshee furaha, atupe nuru hii pia ni kazi ya Mungu ndani yetu
kutuhuisha
Zaburi 51:10-12 “Ee Mungu, uniumbie moyo
safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu Usinitenge na uso wako, Wala
roho yako Mtakatifu usiniondolee. Unirudishie furaha ya wokovu wako;
Unitegemeze kwa roho ya wepesi.”
Maombi ya Yeremia yalikuwa
yamejaa ujuzi na hekima ya kuwa ni Mungu mwenyewe peke yake na mwitikio wetu
kwa rehema zake unaoweza kusababisha mabadiliko na kurejeswa kwa siku zetu kama
siku za kale, Kama watu wa Mungu wanataka kurejeshewa siku za furaha na amani
basi ni lazima tumsihi Mungu kama Yeremia alivyoomba kwamba Mungu aturejeshe na
sisi tukubali kurejea tukatae kupoa kiroho, tukatae ubaridi katika uhusiano wetu
na Mungu ambaye ndiye chanzo cha Baraka, tumsihi Mungu afufue mambo yote yaliyokufa
ndani yetu, aiponye mioyo iliyovunjika atupe uwezo wa kusamehe, atupe nguvu ya
kuomba, atupe kuliheshimu neno lake, atupe ile hali ya kumuhofu, atupe
kuihubiri injili ya kweli na Mungu ataturudishia siku zetu zilizopotea hii haimaanishi
kuwa ataturudisha tulikotoka au kwenye miaka ile ya zamani, lakini maana yake
zitakuja nyakati za kuburudishwa ambazo roho zetu zitafurahi tena na tutasahu
maumivu yetu, Mungu yuko tayari kuzifanya upya siku zetu yuko tayari
kuziburudisha siku zetu na kuyafutilia mbali machozi yetu yote badala ya
kukumbuka mambo ya zamani yeye ameahidi kufanya mambo mapya katika maisha yetu.
Matendo 3:19-21 “Tubuni basi, mrejee, ili
dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake
Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani; ambaye ilimpasa
kupokewa mbinguni hata zije zamani za kufanywa upya vitu vyote, zilizonenwa na
Mungu kwa kinywa cha manabii wake watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu.”
Isaya 43:18-19 “Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya
zamani. Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa?
Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni