Mwanzo 45:21-24 “Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli. Yusufu akawapa magari kama Farao alivyoamuru, akawapa na chakula cha njiani. Akawapa kila mtu nguo za kubadili; lakini Benyamini, alimpa fedha mia tatu na mavazi matano ya kubadili. Na babaye akampelekea kama hivi, punda kumi waliochukua mema ya Misri, na punda wake kumi waliochukua nafaka, na mikate, na chakula kwa babaye njiani. Akaagana na ndugu zake, wakaenda zao; naye akawaambia, Msigombane njiani.”
Utangulizi:
Mojawapo ya agizo la msingi na la
muhimu sana lililotolewa na Yusufu kwa ndugu zake ni pamoja na agizo hili, la “Msigombane njiani”, Agizo hili lilikuwa
ni la muhimu na lenye kujenga umoja na amani ya kitaifa na kifamilia, hasa
baada ya mafarakano, toba na msamaha na mapatano baada ya wana wa Israel
kumuuza ndugu yao Yusufu utumwani ambako kwa neema ya Mungu alipata madaraka
makubwa na akajitambulisha kwao, Yusufu anatoa maagizo haya ili kuilinda jamii
yake wasiwe na mafarakano katika wakati wa mpito, kuelekea kwenye kuishi pamoja
kwa furaha na amani kupitia mwaliko wake kwa familia nzima waje kuishi katika
inchi ya Misri, wana wa Israel wangeliweza kuanza kushutumiana na kulaumiana
kwaajili ya mambo yaliyopita wakati Yusufu amekwisha kutoa msamaha, maneno ya
Yusufu kwao yanasimama kama onyo lenye kuweka msingi wa kuepusha migogoro njiani.
Neno la Mungu linaonya vikali
kwamba katika vitu ambavyo ni chukizo kubwa kwa Mungu ni pamoja na kupanda
mbegu ya fitina kati ya ndugu, yaani kugombanisha watu, Yusufu hakutaka kutoa
ruhusa kwa ndugu zake ambao kimsingi aliwapima na kujua kuwa wamebadilika sana
mioyoni mwao kwa hiyo asingelitoa nafasi ya wao kufarakana na kuumizana kwa
sababu ya fitina na ugomvi kama wa mwanzo uliowafarakanisha wao na yeye kwa ndugu
zake.
Mithali 6:16-19 “Kuna vitu sita
anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi,
ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia;Moyo uwazao mawazo
mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu; Shahidi wa uongo asemaye uongo;
Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.”
Yusufu alikuwa amefahamu mpango
wa Mungu, kwamba watu wanaweza kufarakana na kufitiniana lakini Mungu akawa
amekusudia jambo jema katika fitina hizo na kutimiza mpango wake, kwa sababu
hiyo sasa ulikuwa ni wakati wa kuhakikisha kuwa familia inakuwa na umoja, na
inalinda mpango wa Mungu wa kuwa na amani, na kwa sababu hiyo agizo lake sio
adhabu, bali ni somo la kiroho kwa jamii yake, taifa lake na ndugu zake kwamba
wasigombane tena kwa sababu Mungu amekwisha kutimiza mpango wake kwao!
Tutajifunza somo hili Msigombane njiani kwa kuzingatia vipengele muhimu vitatu
vifuatavyo:-
·
Maana ya
kugombana njiani
·
Msigombane
njiani
·
Athari za
kugombana njiani
Maana ya kugombana njiani
Mwanzo 45:21-24 “Ndivyo walivyofanya wana
wa Israeli. Yusufu akawapa magari kama Farao alivyoamuru, akawapa na chakula
cha njiani. Akawapa kila mtu nguo za kubadili; lakini Benyamini, alimpa fedha
mia tatu na mavazi matano ya kubadili. Na babaye akampelekea kama hivi, punda
kumi waliochukua mema ya Misri, na punda wake kumi waliochukua nafaka, na
mikate, na chakula kwa babaye njiani. Akaagana na ndugu zake, wakaenda zao;
naye akawaambia, Msigombane njiani.”
Moja ya jambo ambalo linavuruga
sana umoja wa kifamilia, kitaifa na kijamii ni pamoja na ugomvi, kugombana kuna
athari kubwa sana yaani athari hasi katika maisha ya mtu mmoja mmoja, wanandoa,
jamii na taifa, watu wanaogombana wanaharibiana na kuleteana athari kubwa sana
kimaisha, kihisia na mahusiano na kuacha majeraha ya uchungu, hasira, kisasi,
chuki na mgawanyiko, kwa ujumla ninaweza kusema hakuna sumu mbaya katika
mahusiano kama ugomvi, watu wanapoanza kugombana, kuchukiana na kuchochea
hasira na migawanyiko, mwelekeo wake unakuwa ni kutengeneza matatizo makubwa
zaidi yanayoharibu maisha hususani ya wale wanaohusika katika ugomvi huo,
akilijua hili Yusufu katika hekima yake na akili yake aliwaonya ndugu zake kuwa
wasigombane njiani!, kama kuna jambo huwa linasikitisha sana katika jamii ni
kuishi katika jamii inayogombana!
Kugombana njiani hasa maana yake
ni nini? Katika lugha ya asili ya Kiebrania neno kugombana linasomeka kama neno “ragaz” au “tirgәzῡ” kwa Kiyunani “orgizethe”, au “orgē” maana
zake kwa kiingereza ni “fall not out”, “quarrel”, “argue”, “become
troubled”, “disagree in words”, kwa Kiswahili tunaweza kusema “Msikosoane”,
au “msikoseane”, “Msigombane” au
“msibishane”, Msisumbuane”, au msileteane taabu, msisumbuane kwa meneno, au msikose kufikia muafaka, na neno njia kwa kiyunani ni “hodō” ambalo maana yake ni safari ya maisha, kwa hiyo sio tu njia
ya kawaida lakini katika maisha, kwa msingi huo neno la Mungu linamtaka kila
mmoja katika jamii, wanandoa, kanisa, ndugu, jamaa, marafiki na taifa lolote
kwamba wasigombane njiani, yaani wasiwe na mafarakano katika safari ya maisha,
watu waache kuwa na uchungu, waache hasira, wasiwe watu wasiofikia muafaka,
kimsingi mafarakano yoyote humzimisha Roho Mtakatifu na kuondoa maarifa, hekima
na busara katika mioyo ya watu.
Yusufu alikuwa na ufahamu kuwa mambo mabaya
yanaweza kutokea pale watu, ndugu, wanandoa au jamii na taifa kwa ujumla
wakiruhusu magomvi, wanafungua ufunguo wa shina la uchungu, kupoteza umoja, kuruhusu
mafarakano, migawanyiko na hata mauaji lakini sio hivyo tu watu wanaogombana
wanafanya upumbavu na kumuhuzunisha Roho Mtakatifu, na kuthibitisha kuwa wao
bado hawana ukomavu wa kiroho, kiakili na kifikra na wanaharibu uhusiano wao na
Mungu na kutengeneza kizuizi kwa maombi na baraka za Mungu zilizokusudiwa katika
maisha yao. Ugomvi huwaweka watu katika vifungo vya kiroho na kuweka ukwazo wa
wao kufunguliwa na kuwahuru
Mithali 20:3 “Mtu kujitenga na ugomvi ni
heshima kwake; Bali kila mpumbavu ataka kugombana”.
Mathayo 5:22-26.“Bali mimi nawaambieni,
Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake,
itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto. Basi ukileta
sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu
yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu
yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. Patana na mshitaki wako upesi, wakati
uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi
akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani. Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe
hata uishe kulipa senti ya mwisho.”
Msigombane njiani.
Mwanzo 45:24 “Akaagana na ndugu zake,
wakaenda zao; naye akawaambia, Msigombane njiani.” Kimsingi Yusufu alitoa agizo Msigombane
njiani akiwa na uzoefu wa kutosha na mpana sana wa kutaka kuilinda jamii yake,
kama kila Taifa, Kanisa, wanandoa na
jamii wanataka kujilinda ana aibu na kujilinda na kumpa shetani nafasi hawana
budi kujilinda na mafarakakano, na ugomvi usio na tija, mtu mmoja Mwalimu wa
zamani sana wa chuo cha Biblia Dodoma (AGBC)
kwa sasa (CBC) Mwalimu Ndosi mwaka 2000 alisema hivi nanukuu “Watu wanapopendana huwa hatuulizi kwanini wamependana na wala hatuwaingilii,
lakini watu wanapogombana tunaingilia na kuuliza ni kwanini wanagombana”
mwisho wa kunukuu, Mwalimu Ndosi alikuwa anamaanisha kuwa watu wanapopendana
huwa hakuna kelele kwa hiyo hakuna mtu anayesikia na kujua kuwa nini
kinaendelea lakini watu wanapogombana kunakuwa na makelele na hivyo watu
wengine huja kuingilia na kuuliza kwa nini mnagombana, ugomvi huleta aibu, na
kumfanya kila mtu hata majirani kujiuliza kwanini hawa wanagombana, mnapopendana
hakuna vikao, mnapogombana vikao vinaanza, mnapopendana mnafukuza maadui
mnapogombana maadui wenu huanza kupata mwanya wa kuwaingilia na kuwavuruga
zaidi hii ni kuanzia ngazi ya familia hadi ngazi ya kitaifa, hususani katika
nyakati za leo ambako kuna uwazi mkubwa wa vyombo vya habari na mitandao ya
kijamii hamuwezi kujificha, Kaini na Habili walipoanza kuwa na mzozo kwa sababu
ya wivu wa Kaini kwa nduguye, Mungu aliingilia kati na kuanza kuuliza, lakini
walipoishi kwa umoja, amani na upendo hata Mungu hakuuliza maswali, kwani hali
ilikuwa shwari.
Mwanzo 4:3-11 “Ikawa hatimaye Kaini akaleta
mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa
wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na
sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika
sana, uso wake ukakunjamana. BWANA akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na
kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema, hutapata kibali?
Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe,
walakini yapasa uishinde. Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende
uwandani]Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua.
BWANA akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni
mlinzi wa ndugu yangu? Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako
inanililia kutoka katika ardhi. Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua
kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako;”
Kaini hakutenda haki, hakufanya
vizuri, lakini Habili alitenda haki na alifanya vizuri, waliishi kwa utulivu
lakini walipoanza kugombana Mungu alisikia ugomvi wao, Mungu aliingilia kati na
Mungu alielekeza njia ya kufanya, Mungu amekusudia kumpa kibali kila mmoja, na
amekusudi kumbariki kila mmoja jambo la msingi ni kila mtu kusimama katika
wajibu wake na kutenda haki, UKITENDA VEMA HUTAPATA KIBALI? agizo la
kutokugombana njiani lilikuwa linamtaka kila mmoja kutokuwa sababu ya ugomvi na
sababu ya malumbano katika jamii, kama viko vyama vya siasa vyama hivyo vina
wajibu wa kuwatumikia wananchi na kuwatendea haki na kuwaletea maendeleo, tuko
katika safari ya kuelekea kwenye kilele cha maendeleo na hakuna sababu ya
kugombana njiani, kama mtu anahisi kupoteza kibali, njia sahihi ni kufanya
vizuri na kutokugombana, kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu kwa maslahi mapana
ya jamii na sio kwa manufaa ya watu wachache na ubinafsi, Yusufu aliwaasa ndugu
zake kutokugombana sio kwa maslahi yao tu bali na masalahi ya familia nzima,
alitaka kumlinda na Yakobo Baba yake, alifahamu kuwa ugomvi wa ndugu hawa njiani
pia ungemuathiri Baba yao, ambaye alikuwa amedanganywa kuwa Yusufu amekufa na
wakachukua kanzu yake na kuichana chana na kuitia damu na kumwambia Baba yao
kuwa Yusufu amekufa!, Ugomvi wao ungemuhuzunisha mzee kule nyumbani na hasa
kama sasa angejua ukweli kuwa sasa Yusufu yuko hai!.
Mwanzo 37:31-34 “Wakaitwaa kanzu ya Yusufu,
wakachinja mwana-mbuzi, na kuichovya kanzu katika damu. Wakaenda nayo ile kanzu
ndefu, wakamletea baba yao, wakasema, Tumeona hii; basi, utambue kama kanzu hii
ni ya mwanao, ama siyo. Akaitambua, akasema, Ndiyo kanzu ya mwanangu, mnyama
mkali amemla; bila shaka Yusufu ameraruliwa. Yakobo akararua mavazi yake,
akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi.”
Yusufu alikuwa anajua kuwa ugomvi
wa kifamilia, kitaifa na kijamii unawahuzunisha sana wazee, alifahamu kuwa
mgogoro wao unaweza kuwafikia wazazi na kuwafanya walie na kuhuzunika, wazee
wetu ambao wametulea kwa shida na taabu mpaka tumekua wametuoza, wametusomesha
na kuhakikisha ya kuwa tuna maisha haya tuliyo nayo wamestaafu na kutulia
nyumbani, wamelitumikia taifa hili na kulipigania, wamepambana tangu kuipatia
uhuru nchi yetu hatuwezi kuwalipa upumbavu, hatuwezi kuwapelekea maiti wala
kanzu zilizojaa damu, mgogoro wa Kaini na Habili ulimuhuzunisha Adamu, migogoro
yetu na ugomvi unahuzunisha watu wasio na hatia na kuwafanya wahuzunike na
kujisikia vibaya, Mzozo na ugomvi ni aibu kubwa sana kwa familia, jamii na
taifa msigombane njiani.
Wazee wetu wanahitaji habari
njema, wanahitaji mavazi, chakula utulivu, Amani na kula mema ya nchi
waliyoyataabikia na hawahitaji tena kusikia magomvi, wanahitaji kucheza na
wajuu zao na sio kupelekewa kanzu zilizojaa damu, wala kupelekewa kazi ya
kutatua migogoro ya ndoa zenu, wala kusikia habari mbaya wanahitaji habari
njema iliyokamilika, mioyo yao ichangamke, Yakobo alipopokea habari njema roho
yake ilifufuka ndani yake
Mwanzo 45:21-24 “Ndivyo walivyofanya wana
wa Israeli. Yusufu akawapa magari kama Farao alivyoamuru, akawapa na chakula
cha njiani. Akawapa kila mtu nguo za kubadili; lakini Benyamini, alimpa fedha
mia tatu na mavazi matano ya kubadili. Na babaye akampelekea kama hivi, punda
kumi waliochukua mema ya Misri, na punda wake kumi waliochukua nafaka, na
mikate, na chakula kwa babaye njiani. Akaagana na ndugu zake, wakaenda zao;
naye akawaambia, Msigombane njiani.”
Mwanzo 45:26-28 “Wakampasha habari,
wakisema, Yusufu angali hai; naye ndiye mtawala katika nchi yote ya Misri. Moyo
wake ukazimia, kwa sababu hakuwasadiki. Wakamwambia maneno yote ya Yusufu,
aliyowaambia; na alipoona magari aliyoyapeleka Yusufu, ili kumchukua, roho ya
Yakobo baba yao ikafufuka.Israeli akasema, Yatosha! Yusufu mwanangu angali hai;
nitakwenda, nionane naye kabla sijafa.”
Israel/Yakobo alipopewa habari
njema roho yake ikafufuka alisema neno moja tu YATOSHA hakutaka kusikia habari nyingine alijawa na furaha, aliona
na magari aliyoletewa na mwanae; Je ugomvi wetu una manufaa gani kwa jamii,
unamanufaa gani kwa watoto wetu, una manufaa gani kwa wanawake una manufaa gani
hata kwetu wenyewe, ROHO YAKE IKAFUFUKA katika
Kiebrania linatumika neno “Châyâh”
kwa kiingereza “recovered” au
“repaired” Yakobo alipokea uponyaji wa roho yake kwa sababu alipokea habari
njema na akasema “Yatosha” ameridhishwa
na habari njema na taarifa njema hiki ndio familia inataka kusikia, hiki ndicho
jamii inataka kusikia, hiki ndio taifa na watu wa Mungu yaani kanisa tunataka
kusikia, habari za ugomvi na mafarakano katika jamii huongeza migandamizo ya
mawazo, hurudisha watu nyuma, huleta majeraha na vidonda vya moyo na kuufisha
moyo tuache kugombana!
Yusufu aliweka katazo lenye
kuleta Baraka na kujenga umoja wa kijamii,kifamilia na kitaifa ambao kimsingi
unaruhusu uwepo wa Mungu na kusababisha baraka kubwa sana, safari ya kutoka
Misri mpaka Kanaani kwa kutembea pamoja na punda na ngamia ingeweza kuchukua
kati ya siku 10 -14 muda huu kama
usingelikuwa na onyo kama hili la msigombane njiani wangefika wakiwa wamevurugana
vya kutosha lakini pia ilikuwa aibu kwa wageni waliombatana nao kwa magari
maalumu yaliyokuwa yanaenda kumpelekea Yakobo zawadi na kumchukua kuja Misri
Zaburi 133:1-3 “Tazama, jinsi ilivyo vema,
na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja. Ni kama mafuta mazuri kichwani,
Yashukayo ndevuni, ndevu za Haruni, Yashukayo mpaka upindo wa mavazi yake. Kama
umande wa Hermoni ushukao milimani pa Sayuni. Maana ndiko Bwana alikoamuru
baraka, Naam, uzima hata milele.”
Athari za kugombana njiani.
Neno la Mungu linatupa uwanja
mpana wa kuelewa kuwa ugomvi una athari hasi, na zenye kuharibu, mahusiano ya
kijamii na maisha ya kiroho, watu wanaoanzisha magomvi wanafananishwa na watu
au mtu anayetoboa mtumbwi ukiwa kwenye maji, na mafuriko yanaweza kuuzamisha na
safari ikakwama.
Mithali 17:12-14 “Afadhali mtu akutwe na
dubu aliyenyang'anywa watoto wake, Kuliko na mpumbavu katika upumbavu wake.
Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya hayataondoka nyumbani mwake.
Mwanzo wa ugomvi ni kama kutoboa penye maji; Basi acheni ugomvi kabla
haujafurika.”
Kwa hiyo tunajifunza kwamba kuna madhara
au athari kubwa sana ya kimwili na kiroho na hata kisaikolojia inayosababishwa
na ugomvi, na huenda Yusufu mwana wa Yakobo alikuwa na ufahamu huo na alitaka kuilinda
na kuitunza familia yake kiroho na kimwili ili wawe na uhusiano mzuri na Mungu
na pia wawe na uhusiano mzuri wao kwa wao hapa ziko athari kadhaa zitokanazo na
kugombana njiani:-
Ø Kutokugombana njiani kunatujengea uhusiano
mwema na Mungu, wakati migogoro na ugomvi unaweza kuharibu mawasiliano yetu
na Mungu na kuzuia maombi na ibada, kutokugombana kuna athari chanya kwani
kunatujengea uhusiano mwema na Mungu.
Wanandoa wanaogombana sio tu kuwa wanaiweka ndoa yao rehani, lakini pia
wajue ibada zao, maombi yao na dua zao haziwezi kukubalika kwa Mungu kama kuna
mtu hujamalizana naye, hujapatana naye na kuweka mambo vizuri, ibada yako na
sadaka yako hazikubaliwi
1Petro 3:7-9 “Kadhalika
ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo
kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu
kusizuiliwe. Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye
kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya,
au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili
mrithi baraka.”
Mathayo 523-24 “Basi
ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno
juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na
ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako.”
Ø Ugomvi ni dalili ya kutokukomaa kiroho na
kifikra – Paulo mtume anawaona watu wenye mafarakano kama watu waliokosa
ukomavu, watu walio wachanga na wenye kuonyesha udunia kama ni Wakristo basi
wanaitwa Wakristo wa mwilini. Lakini jamii yoyote ile isiyokuwa na ukomavu na
subira hishia katika ugomvi
1Wakorintho 3:1-3 “Lakini,
ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni,
bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika
Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza.
Naam, hata sasa hamkiwezi,kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya
mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya
mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?”
Ø Ugomvi humuuzunisha Roho Mtakatifu – watu
wa Mungu wanapojihusisha na ugomvi, hasira, ghadhabu, uchungu, kelele na
matukano ambayo kimsingi ni matunda au matokeo ya ugomvi humuuzunisha Roho
Mtakatifu na kuanza kumfifisha katika kanisa la Mungu na jamii na taifa.
Waefeso 4:29-31 “Neno
lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye
kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia. Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu
wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi.Uchungu wote na
ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna
ya ubaya;”
Ø Ugomvi unaweza kuwakosesha watu ufalme wa
Mungu – Ugomvi ni moja ya matunda ya mwili au kazi za mwili, na wote
wanaohusika na ugomvi kamwe hawawezi kuurithi ufalme wa Mungu.
Wagalatia 5:19-21 “Basi
matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya
sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda,
ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama
nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo
hawataurithi ufalme wa Mungu.”
Ø Ugomvi ni hekima ya Shetani – Ugomvi ni
chanzo na sababu ya dhambi nyingine, Shetani katika hekima yake anajua namna na
jinsi ya kuondoa Amani miongoni mwa wanajamii na taifa kwa sababu hiyo ugomvi
ni hekima ya shetani anajua kabisa katika magomvi atazalisha kiburi, mafarakano
na kusababisha uharibifu mkubwa utakaozaa dhambi nyingine ikiwezekana hata
mauaji, sio hivyo tu ataondoa Amani kwa
mfano hata wanandoa hawawezi kufurahia ndoa kama ugomvi unakuwa ni moja ya mtindo
wa maisha kwa hiyo upendo huathiriwa, Yakobo anaonyesha kuwa hii ni hekima ya
kishetani kwani yeye ndiye sababu ya
machafuko!
Yakobo 3:15-17 “Hekima
hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na
Shetani. Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo
baya. Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole,
tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina,
haina unafiki.”
Hitimisho:
Neno la Mungu linatuagiza kwamba
tutafute kwa bidii kuwa na amani na watu wote, nyakati za Biblia wazee wetu
walihakikisha kuwa wanatafuta Amani kwa bidii, kwa kuwa tuko duniani hitilafu zinaweza
kutokea lakini hitimisho lililobora kwa watu wa Mungu na watu wenye busara ni
kuhakikisha kuwa wanazika tofauti zao na kuitafuta Amani kwa bidii na huo ndio
moyo wa kiungu ambao wazee wetu wa imani walikuwa nao.
Warumi 12:18-20 “Kama yamkini, kwa upande
wenu, mkae katika amani na watu wote. Wapenzi, msijilipize kisasi, bali
ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi
nitalipa, anena Bwana. Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu,
mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake.”
Waebrania 12:14-15 “Tafuteni kwa bidii kuwa
na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana
asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la
uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa
hilo.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni