Matendo 3:18-20 “Lakini mambo yale
aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba
Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo. Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu
zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate
kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani;”
Utangulizi:
Kwa kawaida mojawapo la hitaji
kubwa la kila mwanadamu duniani ni pamoja na kupata wakati wa kupumzika au
kuburudishwa, Mwanadamu anapopata pumziko na kuburudishwa anapata nafasi ya
kuwa na utulivu na kujijenga upya kimwili, kiakili, kihisia, kiroho na
kisaikolojia, hivyo kumwezesha kupata nafasi ya kujijenga na kujitia nguvu kwa upya,
Mwanadamu sio mashine au robot kwa sababu hiyo anaweza kuchoshwa na mambo mengi
na hivyo anahitaji kupumzika, wakati huo wa mapumziko mwanadamu anahitaji
kuburudishwa ili aweze kuwa vizuri kwaajili ya majukumu mengine mazuri zaidi,
Mungu anafahamu sana kuwa wanadamu wanahitaji mapumziko ili waweze kujijenga
upya.
Mathayo 11:28-29 “Njoni kwangu, ninyi nyote
msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu,
mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata
raha nafsini mwenu;”
Mapumziko ya mwanadamu yanaweza
kumsaidia mwanadamu kuwa na nguvu katika maeneo yote ya maisha, kuwa na uwezo
wa kustahimili migandamizo ya mawazo, kujenga mawazo mapya, kuwa na uwezo wa
kutafakari, kupunguza mawazo, kuabudu, kupumzisha akili, kupokea mtazamo mpya,
kuwa na mitazamo chanya, kusahau maumivu, na kuleta ufanisi unaomuondoa
mwanadamu katika kuishi maisha ya mambo yanayojirudia rudia tena na tena kwa
hiyo kuburudika ni hitaji kubwa la kiroho la Mwanadamu na ndio maana wanadamu
wana likizo, mapumziko na usingizi n.k. ili kujikarabati, hata hivyo leo
tutaangalia kwa undani na kwa kina namna ambayo Mungu huleta nyakati za
kuburudishwa kwa wanadamu hasa pale wanapotubu na kurejea na kupokea msamaha wa
Mungu kwa imani katika Kristo Yesu. Tutajifunza somo hili Nyakati za
kuburudishwa kwa kuzingatia maswala muhimu yafuatayo:-
·
Maana ya
nyakati za kuburudishwa.
·
Mwanadamu
na nyakati za kuburudishwa.
·
Jinsi ya
kuwa na nyakati za kuburudishwa.
Maana ya nyakati za kuburudishwa.
Matendo 3:18-20 “Lakini mambo yale
aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba
Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo. Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu
zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate
kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani;”
Tunaona katika kifungu hiki neno
la Mungu likizungumzia na kuwaita watu watubu na kurejesha uhusiano wao na
Mungu ili kwamba wapate nyakati za kuburudishwa kwa uwepo wa Bwana, ni muhimu
kwetu sasa kujiuliza kwamba neno kuburudishwa hasa lina maana gani?, Neno
kuburudishwa kimsingi linalotajwa hapo katika neno la asili la Kiyunani
linasomeka kama “Anapsuxis” au “Anapaύō” kwa kiingereza “refreshing” – Properly a recovery of
breath ambalo maana yake ni kupumzika, kuhuishwa, kutulia ili kupata nguvu
kwa upya, kujipa unafuu, kujituliza, kupunga upepo, kutuliza akili, kutuliza
roho mwili na nafsi, au kuvuta pumzi, kuburudika,
kujipa nafasi, raha, kupata pumzi mpya, kurejeshea nguvu zilizopotea,
kurudishia pumzi kwa usawia!.
Kutoka 23:12 “Siku sita utafanya kazi yako,
na siku ya saba utapumzika; ili kwamba ng'ombe wako na punda wako wapate
kupumzika, kisha mwana wa mjakazi wako na mgeni wapate kuburudika.”
2Samuel 16:13-14 “Basi wakaendelea njiani
Daudi na watu wake; Shimei naye akaaendelea juu ya ubavu wa kile kilima, kwa
kumkabili, huku akiendelea, akilaani, akimtupia mawe, na kurusha mavumbi. Naye
mfalme na watu wake wote waliokuwa pamoja naye wakafika, wamechoka sana; naye
akajiburudisha huko.”
1Wakorintho 16:17-18 “Nami nafurahi kwa
sababu ya kuja kwao Stefana na Fortunato na Akaiko; maana hawa wamenikirimia
kwa wingi yale niliyopungukiwa kwenu. Maana wameniburudisha roho yangu, na roho
zenu pia; basi wajueni sana watu kama hao.”
Warumi 15:30-32 “Ndugu zangu, nawasihi kwa
Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika
maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu; kwamba niokolewe na wale wasioamini
katika Uyahudi, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu;nipate
kufika kwenu kwa furaha, kama apendavyo Mungu, nikapate kupumzika pamoja nanyi.”
Kwa hiyo kimsingi kupumzika kwa
mwanadamu kuna uhusiano mkubwa sana na uwepo wa Mungu Roho Mtakatifu, Mwanadamu
anaweza kujipa raha au pumziko la kimwili tu lakini pumziko hilo sio pumziko la
uhakika likilinganishwa na pumziko analolitoa Bwana wetu Yesu Kristo endapo mtu
atampokea, tunafunuliwa katika andiko hilo kwamba, mwanadamu awapo dhambini
yuko katika wakati wa kutumikishwa, yuko matesoni, anafanyishwa kazi bila
hiyari yake, anatumikishwa na Shetani bila kupenda anateseka na kuelemewa na
mizigo na mateso ya aina mbalimbali na
kuwa Pumziko la kweli linapatikana kwa kukubali mwaliko wake Yesu Kristo pekee,
aidha mwanadamu anapokuwa katika magonjwa pia yuko vitani mwili wake unapigana
kupambana na magonjwa lakini anapopokea uponyaji wa mwili wake nafsi yake na
roho yake anapata nafasi ya kupumzika na Yesu Kristo anauwezo wa kutoa pumziko
hilo kuanzia nasfini mwetu anauwezo wa kutupumzisha.
Mathayo 11:28-29 “Njoni kwangu, ninyi nyote
msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu,
mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata
raha nafsini mwenu;”
Kwa hiyo tunajifunza hapo kuwa
nyakati za kuburudishwa ni wakati ambapo Mungu anampa mwanadamu pumzi mpya ya
uhai, na kuuhisha roho yake iliyochoka na kukata tamaa kwa sababu ya mapito ya
dunia baada ya kukubali toba na kumuamini Bwana Yesu kama Bwana na mwokozi.
Mwanadamu na nyakati za kuburudishwa.
Kila mwanadamu anahitaji nyakati
za kuburudishwa aliyeokoka na hata asiyeokoka wote wanahitaji burudiko la kweli
kwa sababu ya uchovu wa safari za duniani, Mwanadamu aliumbwa awe na nyakati za
kuburudika na kupumzika kila wakati na kila siku, Mungu alipomuweka mwanadamu
katika bustani ya Edeni alimuwekea mwanadamu mazingira ya mapumziko na wakati
wa kuwa na ushirika na yeye, anguko la mwanadamu limesababisha upungufu mkubwa
katika maisha ya mwanadamu, Mwanadamu ni kiumbe na ni kiumbe cha kibaiolojia,
chenye utashi na akili na hisia lakini zenye mipaka, baada ya anguko mwanadamu
amewekewa mazingira magumu ya kula kwa jasho, kushambuliwa na adui zake, uadui
wetu mapepo na na shetani, michongoma na miiba kutuzalia na kuzaa kwa uchungu
adhabu zote zile zilizotamkwa na Mungu zimemwekea mwanadamu mazingira ya
kuchoka kiroho, kimwili, kiakili, kisaokolojia na kibailojia, hivi vyote
vinamfanya mwanadamu kuwa mchovu katika safari ya maisha na kumfanya mwanadamu
awe mwenye kuhitaji mapumziko.
Mwanzo 3:9-19 “BWANA Mungu akamwita Adamu,
akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa
kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi?
Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo
mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.
BWANA Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema,
Nyoka alinidanganya, nikala. BWANA Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu
umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote
walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha
yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na
uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino. Akamwambia
mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa
watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala. Akamwambia Adamu,
Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza,
nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao
yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula
mboga za kondeni; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia
ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini
utarudi.”
Tangu baada ya anguko la
mwanadamu, hitaji la kupumzika limekuwa ni sehemu ya uhitaji mkubwa wa
mwanadamu, sio kimwili tu na hata kiroho na nafsi, hitaji la kupumzika na
kuburudika linaonyesha kuwa mwanadamu sio kiumbe mkamilifu na wala
hajitoshelezi bila Mungu, na kama mtu anaweza kushindana na hitaji la kuburudika
na kupumzika ni wazi kuwa anashindana na asili, kwani hata zaidi ya maisha ya
asili mwanadamu anahitaji kuburudika kiroho na hapo ndipo anapopata Amani,
kugundua kusudi la kuwepo kwake na kujikuta anakamilika kwa hiyo katika ulimwengu
wa anguko tunahitaji pumziko, Dhambi imeleta uhitaji mkubwa wa mapumziko,
wanadamu walianza kutafuta faraja kila wakati katika safari ya maisha mara baada
ya anguko ona
Mwanzo 4:20-22 “Ada akamzaa Yabali; huyo
ndiye baba yao wakaao katika hema na kufuga wanyama. Na jina la nduguye aliitwa
Yubali; huyo ndiye baba yao wapigao kinubi na filimbi. Sila naye akamzaa
Tubal-kaini, mfua kila chombo cha kukatia, cha shaba na cha chuma; na umbu lake
Tubal-kaini alikuwa Naama.”
Wanadamu walioanguka walijaribu
kufanya mambo mbalimbali ya kuwaletea burudani ikiwa ni pamoja na kugundua na
kutengeneza vyombo vya muziki kama kinubi na filimbi ili kujaribu kujituliza lakini
hata hivyo faraja hizo zote walizojibunia wanadamu hazikuweza kuwaletea amani ya kweli.
-
Utumwa wa
dhambi unachosha - Dhambi ilikuwa imemtenganisha mwanadamu na Mungu, maovu
yetu yaliuficha uso wake roho ya mwanadamu ikakumbwa na ukavu na kukosekana kwa
utoshelevu bila utoshelevu wa kiungu kwa kweli mwanadamu anakabiliwa na uchovu
na ukavu na hitaji la burudiko la mwili nafsi na roho
Isaya 59:1-2 “Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa
wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu
yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake
msiuone, hata hataki kusikia.”
Zaburi 32:3-4 “Niliponyamaza mifupa yangu ilichakaa Kwa kuugua kwangu
mchana kutwa. Kwa maana mchana na usiku Mkono wako ulinilemea. Jasho langu
likakauka hata nikawa Kama nchi kavu wakati wa kaskazi.”
Moyo wa mwanadamu ni kama ardhi kavu wakati wa joto au
kiangazi, uwepo wa Mungu ni kama maji, wakati roho zetu zinapokaukiwa tunahitaji
nyakati za kuburudishwa na burudiko hili na kiu hii inaweza kutimizwa na Mungu
peke yake na haiwezi kupozwa na mwanadamu wala katika mazingira ya kibinadamu.
-
Kila
mwanadamu anachoka – Ukiwa mwanadamu katika safari hii ya maisha kuna
kuchoka, watu wanachoka kimwili kiroho na Kisaikolojia, nafsini mwao na
wanaumia kwa hiyo kila mwanadamu anahitaji kutiwa nguvu kwa upya na anayeweza
kuwapa nguvu wanaochoka na kuzimia ni Bwana mwenyewe kupitia uwepo wake.
Isaya 40:29-31
“Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye
asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana
wataanguka;bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa
mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala
hawatazimia.”
-
Mateso
yanachosha sana – Kwa kuwa mwanadamu hakuumbiwa shida anapopita katika changamoto
na shida za aina mbalimbali hatimaye anachoka, unapokuwa mtumwa wa mazingira,
unapokosa uhuru wako mwenyewe, unapotumikishwa na kutumiwa unazidiwa na mateso
na kwa sababu hiyo unachoka na kujikuta unahitaji kupumzika
Maombolezo
5:1-5 “Ee Bwana, kumbuka yaliyotupata; Utazame na
kuiona aibu yetu. Urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni; Na nyumba zetu kuwa
mali ya makafiri. Tumekuwa yatima waliofiwa na baba; Mama zetu wamekuwa kama
wajane.Tumekunywa maji yetu kwa fedha; Kuni zetu twauziwa.Watufuatiao wa juu ya
shingo zetu; Tumechoka tusipate raha yo yote.”
-
Hata
kutenda mema kunachosha - Mwanadamu anapotenda mema na wakati mrefu ukapita
bila kuona matokeo pia anaweza kuchoka, unaomba, unatoa, unamlilia Mungu,
unafunga unakesha lakini huoni matokeo wakati mwingine pia unaweza kuzimia
moyo, unatendea mema watu wanakulipa maovu, unafadhili watu wanakuchukulia poa
au kukutumia kwa faida hii nayo inachosha kutokana na hali hii watu pia huweza
kuchoka kutenda mema.
Wagalatia 6:9-10 “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa
wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee
watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.”
Kutokana na changamoto za aina
mbalimbali anazokuwa amezipitia mwanadamu kila wakati changamoto hizo
zinakuchosha na hivyo unajikuta kuwa unahitaji wakati wa kuburudishwa, ukiishi
maisha ya utauwa utaudhiwa, ukiishi maisha ya anasa na dhambi utatumikishwa na
shetani kwa ujumla duniani tunayo dhiki hata hivyo habari njema ni kuwa ziko
nyakati za kuburudishwa hizi ni nyakati zinapatikana kwa toba na kufutiwa
dhambi na kupewa wakati wa kuburudishwa, yaani ubatizo wa Roho Mtakatifu, Petro
ndiye anatufunulia swala hili katika hutuba yake sikuya Pentekoste anaonyesha
kuwa katika Bwana kuna kuburudishwa kila mwanadamu anahitaji nyakati hizi
anahitaji burudiko la mwili wake, nasi yake na roho. Na burudiko hili linapatikana kwa kurejesha
uhusiano wetu na Mungu, baada ya toba Roho Mtakatifu anaposhuka ndani ya
mwamini anamwezesha kuishi maisha yenye burudiko
Matendo 3:18-20 “Lakini mambo yale
aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba
Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo. Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu
zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate
kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani;”
Jinsi ya kuwa na nyakati za kuburudishwa.
Mungu katika hekima yake
anafahamu kuwa wanadamu wanahitaji nyakati za kuburudhishwa na kwa sababu hiyo
neno lake limejaa ahadi za kuburudishwa.
Yeremia 31:23-25 “Bwana wa majeshi, Mungu
wa Israeli, asema hivi, Watatumia tena neno hili katika nchi ya Yuda, na katika
miji yake, nitakapowarudisha mateka yao; Bwana na akubariki, Ee kao la haki, Ee
mlima wa utakatifu. Na Yuda, na miji yake yote, watakaa humo pamoja; wakulima,
nao waendao huko na huko pamoja na makundi yao. Kwa maana nimeishibisha roho
yenye uchovu, nami nimeiridhisha kila roho yenye huzuni.”
Zaburi 68:8-10 “Nchi ilitetemeka Naam,
mbingu zilidondoka usoni pa Mungu; Hata Sinai usoni pa Mungu; Mungu wa
Israeli.Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema; Urithi wako ulipochoka uliutia
nguvu. Kabila yako ilifanya kao lake huko; Ee Mungu, kwa wema wako uliwaruzuku
walioonewa.”
Petro anaunganisha toba kama njia
ya kuleta amani na burudiko la kweli kwa mwanadamu, lakini zaidi sana
anazungumzia ile ahadi ya Roho Mtakatifu ndani ya mtu aliyeamini kwa kutubu
dhambi zake kwa kumaanisha kuziacha na kuzijutia, ni ukweli ulio wazi kwa kila
mtu kuwa ukijazwa Roho Mtakatifu unakuwa na wakati wa kuburudisha, Petro
alikuwa anamzungumzia Roho Mtakatifu ndani ya mwamini anakuwa ni kama maji ya
kunywa na kuoga wakati wa joto,
aliyeokoka anakuwa ni kama maji ya mito inayotiririka, Hakuna jambo linaleta
furaha na amani kama kumpokea Roho Mtakatifu muulize kila mtu ambaye amejazwa
Roho Mtakatifu atakuelezea jinsi ilivyo furaha kubwa sana hata unapopita katika
magumu yeye anakupa burudiko lisiloweza kuelezeka.
Matendo 4:24-31. “Hata walipofunguliwa,
wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu
wa makuhani na wazee. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo
mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na
bahari na vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha
babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila
wametafakari ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri
pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake. Maana ni kweli, Herode na Pontio
Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu
ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, ili wafanye yote ambayo
mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. Basi sasa, Bwana,
yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri
wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi
wako mtakatifu Yesu.Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale
walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la
Mungu kwa ujasiri.”
2Wakorintho 4:8-9 “Pande zote twadhikika,
bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi;
twatupwa chini, bali hatuangamizwi;”
Uwepo wa Roho Mtakatifu ndani ya
mtu aliyemwamini Yesu unayafanya maisha kuwa burudani kila wakati unamfanya mtu
aliyemwamini Bwana asitikiswe na lolote, awe na nguvu ya kustahimili kwa sababu
hata kama kwa nje anateseka kwa ndani kuna bubujiko la burudiko kubwa ndani
yake, Roho Mtakatifu anatoa nguvu ya kustahimili, anatoa msaada wa uungu ndani
yetu kushinda kila vikwazo vya kibinadamu na vya asili anatutia nguvu analihuisha
neno la Mungu ndani yetu na kulifanya liwe na uhai na kukuwezesha kustahimili
anakupa neema ya kuliona pendo la Mungu katika mateso na magumu na anakupa
kuwacheka na kuwahurumia wanaodhani wanaweza kukukwaza kwa sababu zozote zile
ndani yako maneno haya yanakuwa hai na halisi ndani ya mtu aliyeokoka.
Warumi 8:35-39 “Ni nani atakayetutenga na
upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari,
au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa,
Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote
tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha
kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye
mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu,
wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo
wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”
Waebrania 12:26-29 “ambaye sauti yake iliitetemesha
nchi wakati ule; lakini sasa ameahidi akisema, Mara moja tena nitatetemesha si
nchi tu, bali na mbingu pia. Lakini neno lile, Mara moja tena, ladhihirisha
kuhamishwa vile viwezavyo kutetemeshwa, kama vitu vilivyoumbwa, vitu
visivyoweza kutetemeshwa vikae. Basi kwa kuwa tunapokea ufalme usioweza
kutetemeshwa, na mwe na neema, ambayo kwa hiyo tumtolee Mungu ibada ya
kumpendeza, pamoja na unyenyekevu na kicho; maana Mungu wetu ni moto ulao.”
Uwepo wa Mungu ukitembea pamoja
nawe ni lazima utapoata raha, raha maana yake refreshment yaani kuburudishwa ni
katika uwepo wa Mungu kila mmoja wetu ataweza kubudurika hakuna namna nyingine
tunapouanza mwendo wa mwaka huu mpya wa 2026 kila mmoja wetu ajikite katika
kuutafuta uwepo wa Mungu, Kufanya kazi kwa bidii kutafuta fedha kwa njia za
halali bila kuacha kuutafuta uso wa Bwana kwa bidii ili atupe raha, Bwana Mungu
na atembee pamoja nawe katika mwaka huu na akupe nyakati za kuburudishwa katika
jina la Yesu Kristo aliye hai, ulivyotembea katika nyakati ngumu na za
majaribio imetosha sasa ni wakati wako wa kuburudishwa Mungu yuko tayari kutoa
raha, na burudiko kwa wanadamu wote waliookolewa n ahata wasiookolewa kila
mmoja wetu anahitaji kuburudishwa nami kama Petro alivyotangaza zikujie nyakati
za kuburudishwa nakutangazia kuwa tayari kwa kuburudishwa, Pokea uwepo wa Bwana
maishani mwako uwe na wakati wa kuburudishwa, mtii Mungu na itii sauti yake
zipate kuja nayakati za kuburudishwa kwako katika jina la Yesu Kristo aliye
hai.
Kutoka 33:14-17 “Akasema, Uso wangu
utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha. Naye akamwambia, Uso wako
usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa.Kwa maana itajulikanaje kuwa
nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja
nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi?
BWANA akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata
neema mbele zangu, nami nakujua jina lako.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
