Jumatano, 28 Januari 2026

Hatimaye ndugu tuombeeni!


Warumi 15:30-32 “Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu; kwamba niokolewe na wale wasioamini katika Uyahudi, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu; nipate kufika kwenu kwa furaha, kama apendavyo Mungu, nikapate kupumzika pamoja nanyi.”




Utangulizi:

Ni muhimu kwetu kama kanisa kuwa na ufahamu, kuwa kuna changamoto kubwa katika kanisa la Mungu na changamoto mojawapo  kubwa ni hii ya kutokuwaombea watumishi wa Mungu, changamoto hii inaweza kuwa inachangiwa na ufahamu finyu wa neno la Mungu, au kutokutiliwa mkazo kwa fundisho hili muhimu na la msingi la kuwaombea watumishi wa Mungu, Mtume, Nabii, Mwinjilisti, Mchungaji na Mwalimu asiyekuwa na waombaji kwaajili yake hana tofauti na Askari aliyeingia vitani pake yake, akishambuliwa yeye hakuna tena msaada mwingine, Ni muhimu kuwa na maarifa na ufahamu ya kuwa kila huduma katika ufalme wa Mungu ina vita na mashambulizi mengi  ya upinzani wa ibilisi huelekezwa kwa watumishi wa Mungu, tunapowaombea tunawasaidia katika ulimwengu wa roho kuepushwa na mashambulizi makali na kuwawekea ulinzi dhidi ya utawala wa giza.

Mathayo 26:30-31 “Nao walipokwisha kuimba, wakatoka nje kwenda mlima wa Mizeituni. Ndipo Yesu akawaambia, Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika.”

Wakati Mungu amewatenga watumishi wake wawe kama chombo cha kuwakilisha kazi yake duniani, shetani naye anawalenga wawe silaha maalumu ya kuharibu kazi ya Mungu, au anaweza kutumia hila na mbinu mbalimbali kwa kusudi la kuwakwamisha ili kazi ya Mungu asiendelee mbele na ndio maana kwa kujua hali ilivyo katika ulimwengu wa Roho Paulo Mtume mara kwa mara aliwaomba watu wa makanisa mbalimbali wamuombee, tusipokuwa  na watu wa kutuombea katika huduma zetu tunajiweka katika hatari ya vita kali na kukabiliana na mashambulizi ya huduma peke yako, Jambo ambalo linaweza kusababisha ukadhoofika mapema na kuchoka.

2Wathesalonike 3:1-4 “Hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee, na kutukuzwa vile vile kama ilivyo kwenu; tukaokolewe na watu wasio haki, wabaya; maana si wote walio na imani. Lakini Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu. Nasi tumemtumaini Bwana kwa mambo yenu, kwamba mnayafanya tulivyowaagiza, tena kwamba mtayafanya.”

Tutajifunza somo hili muhimu Ndugu tuombeeni kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-

 

·         Umuhimu wa kuwaombea watumishi wa Mungu.

·         Hatimaye ndugu tuombeeni.

·         Mifano ya watumishi wa Mungu waliokuwa na timu za waombaji.

 

Umuhimu wa kuwaombea watumishi wa Mungu.

Ni muhimu kuwa na ufahamu na maarifa kuwa watumishi wa Mungu wa aina zote wanahitaji maombi, na sio tu kuombewa  na washirika pekee lakini ikiwa uko uwezekano pia wawe na timu yaani kikundi au watu maalumu ambao wanaifanya kazi hiyo kwa uaminifu, Swala la kuombewa kwa watumishi wa Mungu ni swala la kiroho kabisa, na ni la kibiblia, kuomba maombi kwa washirika wetu ni swala la kibiblia na ni swala la unyenyekevu unaoonyesha kuwa tunahitaji neema ya Mungu baadhi ya watumishi wa Mungu wanafikiri kuomba maombi kwa washirika na kuwa na timu maalumu ya kuwaombea ni kuonyesha udhaifu, Jambo hili sio sahihi Kwani neno la Mungu linaonyesha kuwa watumishi wa Mungu wanahitaji kuombewa, Nyakati za Kanisa la kwanza walipoteza viongozi Muhimu sana wenye uwezo mkubwa sana katika jamii ya Kikristo mpaka walipopata ufunuo wa kuhakikisha kuwa wanaomba kwa nguvu na juhudi kubwa kwaajili ya wachungaji wao.

Matendo 6:8-13 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye. Hata wakashawishi watu waliosema, Tumemsikia mtu huyu akinena maneno ya kumtukana Musa na Mungu. Wakawataharakisha watu na wazee na waandishi, wakamwendea, wakamkamata, wakampeleka mbele ya baraza. Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya torati;”

Matendo 7:57-60 “Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja, wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli. Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake.”

Matendo 12:1-5 “Panapo majira yale yale Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa. Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga. Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi akaendelea akamshika na Petro. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa. Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu.Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake.”

Tunaona jinsi nyakati za kanisa la kwanza shetani alivyowatumia watu waovu kupinga kazi ya Mungu hasa kwa kuwaua viongozi wa kanisa wale waliokuwa mstari wa mbele katika kuieneza kazi ya injili, aliuawa Stefano na pia Yakobo Mtume ndugu yake Yohana, na Petro akakamatwa, ni wazi kabisa huu ulikuwa ni mpango mkakati wa kishetani wa kutaka kulidhoofisha kanisa, kwa hiyo hata kama kanisa lilikuwa linaomba sasa waliongeza kasi ya kumuomba Mungu kwa juhudi kwaajili ya viongozi wengine, tunasoma kuwa hata Petro alikamatwa lakini kanisa lilipoomba kwa juhudi Mungu alimtuma malaika wake na Petro akawekwa huru, tangu wakati huu, viongozi na washirika walielewa kuwa wanapaswa kuwalinda watumishi wa Mungu kwa maombi na kuwaombea ili kazi ya kueneza neema hii iweze kusonga mbele, kazi ya Mungu ina upinzani mkubwa na viongozi ndio wanaowindwa zaidi kwa sababu hiyo ni muhimu sana kwa kanisa kuomba, kuwa na programu endelevu za maombi ya kimkakati kuwaombea watumishi wa Mungu, kazi ya Mungu iweze kuendelea, ishara na miujiza viweze kufanyika, Na neno la Mungu liendelee kuhubiriwa kwa ujasiri.

Matendo 4:21-31“Nao walipokwisha kuwatisha tena wakawafungua, wasione njia ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu; kwa kuwa watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa hayo yaliyotendeka; maana umri wake yule mtu aliyefanyiwa ishara hii ya kuponya ulipita miaka arobaini. Hata walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake. Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu. Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.”

Kwa hiyo kwa kuwaombea watumishi wa Mungu kanisa linashiriki kuwatia moyo kiroho kwaajili ya huduma zao, kutunza hisia zao, kuwaombea waweze kuwa na afya njema  na waweze kustahimili hasa wanapokutana na upinzani, waweze kubeba vema majukumu ya kikanisa na wawe na nguvu wakati wa kupambana na vita vya kiroho, kufanya hivyo pia ni njia ya kushiriki Baraka ya kazi wanayoifanya ya kuihubiri injili kwa usahihi na kuwalinda dhidi ya yule muovu, Mungu awape hekima ya maongozi, lakini zaidi ya yote ni njia ya kuonyesha upendo na ushirika pamoja nao.

Maandiko yanaonyesha pia shetani anaweza kuwazuia watumishi wa Mungu wasilifikie eneo Fulani kwa injili, Anga la Thesalonike lilikuwa gumu kwa Paulo mtume alipohubiri Thesalonike alikutana na upinzani mkali sana lakini sio hivyo tu hata alipotaka kurejea tena kwa kusudi la kuwaimarisha Shetani alimzuia na watumishi wengine, kwa hiyo shetani ni adui wa injili na ni adui wa wale wanaoipeleka injili anaweza kuwazuia wasifike eneo Fulani

1Wathesalonike 2:17-18 “Lakini sisi, ndugu, tukiwa tumefarakana nanyi kwa kitambo, kwa uso si kwa moyo, tulizidi kutamani kwa shauku nyingi kuwaona nyuso zenu.Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia.”

Kama shetani anaweza kumzuia Paulo Mtume na timu yake wasifike Thesalonike kuwaimarisha wakristo waliozaliwa katika hali ya dhiki nyingi tena sio mara moja jiulize anashindwaje kutuzuia wewe na mimi ambao hatuna mwombezi zaidi ya wake zetu, tena wakati mwingine anatugonganisha nao ili maombi yetu yazuiliwe, tunahitaji maombi ya watu waaminifu atakaotambua kile ambacho tumekibeba na kulia na kuomboleza na kufunga kwaajili yetu. 

Hatimaye ndugu tuombeeni

2Wathesalonike 3:1-4 “Hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee, na kutukuzwa vile vile kama ilivyo kwenu; tukaokolewe na watu wasio haki, wabaya; maana si wote walio na imani. Lakini Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu. Nasi tumemtumaini Bwana kwa mambo yenu, kwamba mnayafanya tulivyowaagiza, tena kwamba mtayafanya.”

Wote tunafahamu kuwa Paulo Mtume alikuwa ni moja ya viongozi hodari sana katika kuifanya kazi ya Mungu, Neno la Mungu linaonyesha ya kuwa Paulo mtume alitumiwa na Mungu kwa viwango vikubwa na vya juu sana katika kulijenga kanisa la Mungu, naweza kusema kuwa hakuna mtu anaweza kudai kuwa yeye ni wa kiroho kumzidi Paulo Mtume neno la Mungu linaonyesha ya kuwa alifanya kazi kuliko mitume wote, alipewa mafunuo makubwa kuliko mtu yeyote, lakini pia alitumiwa na Mungu kufanya miujiza ya kupita kawaida kwa mikono yake

1Wakorintho 15:9-10 “Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami.”

2Wakorintho 12:2-4 “Namjua mtu mmoja katika Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua). Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu. Nami namjua mtu huyo, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua); ya kuwa alinyakuliwa mpaka Peponi, akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haijuzu mwanadamu ayanene.”

Matendo 19:11-12 “Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.”

Hata pamoja na kutumiwa hivyo sana na Mungu, na kupewa mafunuo makubwa sana na kufanya kazi ya Mungu kwa neema kubwa kuliko mitume wote bado Paulo mtume kwa unyenyekevu mkubwa alionekana katika nyaraka nyingi akiomba kuombewa, mara kwa mara utaona akiomba maombi, ndugu tuombeeni, hatimaye ndugu tuombeeni, jitahidini pamoja nami katika maombi, hakuwa na kiburi wala hakufikiri kuwa anaweza peke yake na kumbuka kuwa yeye mwenyewe alikuwa mwombaji, watu wengi sana wa Mungu hawaijui siri hii wanadhani kuomba kuombewa na washirika ni kuonyesha  udhaifu, wanadhani ni sisi tu ndio wenye wajibu wa kuwaombea washirika  na ni kama washirika hawapaswi kutuombea  jambo hilo sio sahihi, au kuwa na timu ya watu wanaoomba kwaajili yako au hata wanaoomba pamoja nawe, huo sio udhaifu ni unyenyekevu na ni ukweli usiopingika kibiblia kuwa tunahitaji kuombewa, tunahitaji watu waaminifu, waliojitoa wanaojua nini wanakifanya kutuombea, tunahitaji maombi!

Warumi 15:30-32 “Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu; kwamba niokolewe na wale wasioamini katika Uyahudi, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu; nipate kufika kwenu kwa furaha, kama apendavyo Mungu, nikapate kupumzika pamoja nanyi.”

Waefeso 6:18-20 “kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote; pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili; ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo; hata nipate ujasiri katika huyo kunena jinsi inipasavyo kunena.”

Wakolosai 4:2-3 “Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani; mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake nimefungwa,”

2Wakorintho 1:9-11. “Naam, sisi wenyewe tulikuwa na hukumu ya mauti katika nafsi zetu ili tusijitumainie nafsi zetu, bali tumtumaini Mungu, awafufuaye wafu, aliyetuokoa sisi katika mauti kuu namna ile; tena atatuokoa; ambaye tumemtumaini kwamba atazidi kutuokoa; ninyi nanyi mkisaidiana nasi kwa ajili yetu katika kuomba, ili, kwa sababu ya ile karama tupewayo sisi kwa msaada wa watu wengi, watu wengi watoe shukrani kwa ajili yetu.”

Tunapowaombea watumishi wa Mungu wanapewa ujasiri, wanatumiwa na Mungu kwa miujiza, neno la Mungu linaenea kwa nguvu huku likishinda nguvu za upinzani, milango ya injili inafunguka, wananusuriwa na hatari za namna mbalimbali, huduma inaenea katika mataifa mengi kama wana kesi au wamefungwa minyororo inaachilia, lakini zaidi ya yote wanalindwa ili kwamba wasipepetwe katika imani wala imani zao zisitindike, Yesu alimuombea Petro awe imara,  Imani yake isitindike, ni maombi  yet utu ndio yatakayowadumisha watumishi wa Mungu na kuwafanya imara katika imani, mtumishi asiyeombewa hawezi kusimama, washirika wasio na akili husengenya na kuwashutumu watumishi wa Mungu wanapoingia majaribuni wakisahau kuwa hawajawahi hata siku moja kufanya wajibu wao wa kumlilia Mungu kwaajili yao ili wasimame imara na kushinda vikwazo vyote vinavyowakabili.

Luka 22:31-32. “Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.”

Mifano ya watumishi wa Mungu waliokuwa na timu za waombaji

Kwa kufahamu siri hii ya kuwa kila mtumishi wa Mungu anahitaji maombi, baadhi ya watumishi wa Mungu waligundua kuwa kama Paulo Mtume aliyekuwa wa kiroho sana bado kuna nyakati alihitaji maombi ni zaidi sana mimi na wewe tunahitaji maombi, ndugu unahitaji kuombewa ninahitaji sana maombi yako pia, Katika historia ya kanisa, wahubiri wengi waliotumiwa na Mungu na kuleta uamsho mkubwa hawakuwa wanategemea kipawa na upako wao peke yao,  wala maombi yao peke yao lakini vile vile walikuwa na timu maalumu za waombaji waliobeba huduma zao kwa maombi endelevu na ya kudumu!

John Wesley – alizaliwa june 28 1703 na kufariki 2March 1791 moja ya mwinjilisti mkubwa sana duniani na mwanatheolojia maarufu ambaye likuwa sababu ya uamsho mkubwa wa kanisa la Uingereza, alikuwa na vikundi vidogo vidogo vingi kama madarasa ya maombi, hakuruhusu kufanya huduma bila nidhamu ya kiroho, alisababisha uamsho mkubwa huko uingereza na kusababisha mabadiliko makubwa ya kijamii, maadili  katika kazi na familia  na kusababisha kanisa lililodumu hadi leo, tunajifunza kwake kuwa maombi ya pamoja huzalisha mabadiliko ya kitaifa

Charles Finney – Ni moja ya wahubiri waliotumiwa sana na Mungu kuleta uamsho mkubwa alizaliwa 29 August 1792 na kufariki mwaka 16 August 1875, alikuwa ni muhudumu wa kanisa la American Presbyterian alijulikana  sana kama kiongozi wa uamsho mkubwa wa Pili katika Marekani, alikuwa akisimama kabla hata ya kuhubiri watu walililia toba kabla ya mahubiri kuanza na kulikuwa na uamsho mkubwa sana nyakati zake lakini yeye alisema wazi “Mahubiri yangu yalibebwa na Maombi ya Nash” Daniel Nash maarufu kama (Father Nash) alikuwa mtu mmoja maalumu ambaye kazi yake ilikuwa ni kuomba bila kukoma kabla ya Finney kuhubiri, Daniel Nash alikuwa anaenda katika mji husika ambao Finney angehubiri kwa muda kuanzia wiki au miezi kabla, akifunga na kuomba, Mahubiri yenye matokeo makubwa sana hutanguliwa na maombi makubwa sana.

D. L Moody – Moja ya wainjilisti maarufu sana Duniani  alizaliwa February 5 1837 na kufariki December 1899 jina lake kwa urefu ni Dwight Lyman Moody maarufu kama D.L Moody mwinjilisti maarufu wa kimarekani alihubiri injili na kusababisha maelefu ya watu kuokoka huko ulaya na Marekani, aliendelea na huduma bila kuwa na Skendo injili ilienea kupitia yeye kizazi kwa kizazi  lakini yeye alikuwa na timu ya waombaji waliokuwa wakikaa nyuma ya pazia wakati yeye alipokuwa anahubiri alisema “Ni Afadhali nopate watu 10 wanaoomba kuliko 10,000 wanaonisikiliza” mafanikio yoyote ya jukwaani ni matokeo ya kazi katika chumba cha maombi

Reinhard Bonnke – Muhubiri mkubwa sana Duniani chini ya huduma ya Christ for All nations (CfaN) amehubriri watu zaidi ya milioni 79 waliookoka katika huduma yake, Mungu alimtumia kwa miujiza mikubwa wakati akihubiri Afrika, huduma yake ilimuwezesha kutembelea bara zima, Muhubiri huyu mwenye asili ya Ujerumani alikuwa na mtandao mkubwa sana wa kimataifa wa waombaji, ambao walifunga wiki kadhaa na saa kadhaa kila alipokuwa akifanya mkutano wa injili Bonke alikuwa na timu mahususi ya kuombea huduma yake kwa hiyo tunajifunza hapo kuwa Huduma kubwa huitaji Jeshi kubwa la siri la waombaji.

Billy Graham – Moja ya wahubiri wakubwa walioheshimika sana Marekani alizaliwa 7 November 1918 na kufariki 21 February 2018 alikuwa na timu ya maombi iliyoitwa “The prayer Partners” yeye hakuwahi kukubali mkutano wowote ufanyike bila maandalizi ya maombi ya muda mrefu, Mungu alimpa neema ya kuhubiria maraisi wa aina mbalimbali, mataifa mengi na mamilioni ya watu alikaa katika huduma kwa karibu miaka 60 bila kuharibiwa na maswala ya fedha, umaarufu kiburi au wanawake, tunajifunza kutoka kwake ya kuwa maombi hutunza sio huduma tu hata sifa nzuri za muhubiri anayeombewa.

David Yonggi Cho – Mwanzilishi wa Kanisa la Yoido Full Gosple Church alizaliwa 14 February 1936 na kufariki 14 september 2021 ni moja ya waanzilishi wa maswala ya mlima wa maombi (Prayer Mountain) alitenga wachungaji na waombaji kila wakati kwaajili ya kufunga na kuomba na kukemea au kupigana vita vya kiroho, matokeo yake akawa ndiye mchungaji mwenye kanisa kubwa zaidi kuliko watu wote duniani kwa nyakati zake, alichangia kwa kiasi kikubwa uamsho ulioko Korea ya kusini, na alifanikiwa kwa kuanzisha mfumo wa cell groups au makanisa ya nyumbani ambao nao ulibebwa na maombi, tunajifunza kutoka kwake kuwa kanisa linalotaka kukua kwa haraka lazima lijikite katika mzizi wa kuomba.

Zachary Kakobe – Ni mwanzilishi wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship nchini Tanzania, moja ya makanisa ya kipentekoste yenye asili yake nchini Tanzania na si kutoka nje, Muhubiri maarufu sana mwenye kanisa kubwa huko Mwenge jijini Dar es Salaam, Mchungaji Kakobe ana mfumo wa cell ziitwazo “Power House” ambapo washirika katika maeneo mbalimbali kila mtaa waliko washirika hukutana kila alhamisi kwa maombi mbalimbali  ya kikanisa ikiwa ni pamoja na kumuombea Mchungaji, aidha ana kikundi maalumu ya maombi kijulikanacho kwa jina la  Ana binti Fanuel ambao pamoja na mambo mengine humuombea Mchungaji sawasawa na maelekezo yake kikundi hiki kinaundwa na wajane maalumu ambao hutunzwa na kanisa, Matokeo yake Kanisa lake limeweza kuenea nchi nzima kwa muda mfupi, kuna uamsho mkubwa sana unaofukuta chini kwa chini, washirikia wake wamejengwa katika misingi ya kuomba kwa kuyataja maandiko, wanapenda mafundisho na wanaishi kwa nidhamu. Alizaliwa 6 June 1955 huko, Kakonko, Kigoma, uamsho katika kanisa lake unakua kwa kasi kupitia maombezi, semina na mikutano ya ndani kwa ndani, pamoja na yeye mwenyewe kuwa mwombaji, Kakobe mara kwa mara amesisitiza kuombewa, kama ilivyokuwa kwa Paulo mtume, Kumbe maombi yana nguvu ya kuwaleta maelefu kwa Yesu, kuwafanya wanafunzi hata bila kuathiri, shughuli na utendaji wa maisha ya kawaida ya watu na kujenga kanisa imara

 

Hitimisho!

Unapochunguza kwa makini mifano hii michache ya wahubiri ambao Mungu aliwatumia kwa uamsho mkubwa sehemu mbalimbali duniani utabaini kuwa maombi yanahusika kwa kiasi kikubwa, sitaki kusema kuwa kila uamsho unaletwa na maombi lakini nataka kusema kuwa, mahuburi na uamsho wa kina na endelevu unajengwa kwa maombi, watumishi wa Mungu tutake maombi kwa washirika wetu, hata pamoja na sisi wenyewe kuwa waombaji, lakini pia tuwe na timu za maombi watu wanaotuombea kwa kina, na sio vibaya kuwa na timu ya watu wanaoomba pamoja nawe au wanaokuombea, Yesu alimtaka Petro, Yakobo na Yohana, wakeshe au waombe pamoja naye, Licha ya kuwa alikuwa wa kiroho sana na ni mwana wa Mungu, nadhani ni afadhali mara elfu kuwa na waombaji  wanaokuombea kwa huduma yako kuliko kuwa na walinzi wanaokulinda “Body guards

Mathayo 26:36-38 “Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe. Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka.Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.”

Mtumishi wa Mungu mwombe Mungu akupe watu sahihi watakaokubebea mzigo katika maombi, omba Mungu akupe hekima kuchagua watu wasiri waliojaa maisha ya maombi wanyenyekevu, waaminifu, wenye upendo na mzigo au wajane wenye umri mkubwa wanaofanya kazi ya kuomboleza kwaajili yako, waelezee maono yako au mzigo unaotaka wakubebee, wafundishe masomo mbalimbali kuhusu kuomba, tengeneza mfumo au muda maalumu wa kuomba na siku maalumu za kuomba,  hata pamoja na kuwa na idara za maombi, amini sana katika watu wachache ambao maalumu au kipekee watakuwa wanakuombea, anza na watu wachache sana kikundi cha maombi kinatakiwa kuwa na watu 3-12 tengenezeni mawasiliano ya siri, wafundishwe kuishi maisha ya kujitoa na utakatifu, wenye matumizi mazuri ya kinywa wasio na mafarakano waandae kwa mafundisho maalumu ya waombaji kwaajili ya mtumishi wa Mungu kisha anzeni kuomba!

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: