Jumapili, 18 Januari 2026

Walinichukia bure!


Zaburi 69:4 “Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao kunikatilia mbali wamekuwa hodari, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua.”

Yohana 15:24-25 “Kama nisingalitenda kwao kazi asizozitenda mtu mwingine, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa wametuona mimi na Baba yangu, na kutuchukia. Lakini litimie lile neno lililoandikwa katika torati yao, Walinichukia bure.”



Utangulizi:

Je umewahi kupitia hali katika maisha ambapo umekumbana na watu katika mazingira fulani kisha wakakuchukia tu bila ya sababu?  Au wakakupinga tu au wakakukataa, au ukakaliwa vikao, au kuitwa kwenye mabaraza ya watu waliojaa chuki na wivu wewe ukawa ndio agenda na kisha yakatolewa maamuzi ya kukuhukumu wewe hata bila ya sababu yenye mashiko? “Walinichukia bure bila ya sababu” ni moja ya usemi wenye nguvu sana wa kibiblia  ambao kivuli chake ni Zaburi 69:4 na Asili yake ni Yohana 15:24-25 ambapo Daudi pamoja na Yesu Kristo wanaelezea namna na jinsi walivyochukiwa na watu au maadui zao bila ya sababu, wakiwashambulia na kuwachukia  na kuwahukumu, na kuwapinga, na kuwafukuza bila sababu za haki, au kwa sababu ya chuki, wivu na kutokueleweka!, hata ingawa kuchukiwa, kukataliwa, kutokueleweka, na kuhukumiwa isivyo haki kunaweza kuwa na maumivu fulani kisaikolojia au kimwili, lakini kimaandiko jambo hili sio jipya kwani Biblia inatufundisha namna ya kuonyesha jinsi kupokea na kuonyesha mwitikio kwa mambo madogo kama haya kiroho  na sababu kwa nini unachukiwa bure bila sababu za maana, tutajifunza somo hili zuri Walinichukia bure! kwa kuzingatia vipengele vikuu muhimu vitatu vifuatavyo;-

·         Maana ya kuchukiwa bure!

·         Sababu za kuchukiwa bure

·         Jinsi ya kupokea na kuitikia chuki zao za bure


Maana ya kuchukiwa bure!

Yohana 15:24-25 “Kama nisingalitenda kwao kazi asizozitenda mtu mwingine, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa wametuona mimi na Baba yangu, na kutuchukia. Lakini litimie lile neno lililoandikwa katika torati yao, Walinichukia bure.”

Ni muhimu kufahamu kuwa neno kuchukiwa katika lugha ya Kiebrania linatumika neno śānē  ambalo maana yake kwa kiingereza ni to detest, oppose or treat as an enemy  kwa Kiyunani (Greek) ni miseō ambalo kwa kiingereza ni to detest, reject, persecute or love less intentionally  katika msamiati wa kisaikolojia linatumika neno “antipathy” ambalo kiingereza ni a strong feeling of dislike kwa hiyo kuchukiwa katika lugha ya Kiswahili kwa maana hizo hapo juu tunaweza kutafasiri kama Hisia kali za kutokukubali, hisia za kukukataa, hisia za kukupinga, hisia za kukuona kama adui, hisia za kutokukupenda, hisia za kutamani wakutese au upatwe na mabaya au usiwepo, au kuhisi kukuchukia tu bila sababu za maana za makusudi au za kutokukusudia chuki hii inasukumwa na wivu wa kiroho moyoni mwa watu kwa sababu ya kibali cha kiungu ndani yako, kwa hiyo chuki hii wakati mwingine inaweza kutoka kwa watu waliokuzidi kila kitu,  wana cheo, wana mali, wana elimu, wakati mwingine hata umri mkubwa kuliko wako lakini wakikuona tu wanakuchukia bila sababu na unaweza kujiuliza mbona mimi sina lolote kama wao lakini wanakuchukia tu, Daudi anasema walionichukia ni hodari  wanaotamani kumkatilia mbali wana nguvu lakini hata hivyo walimchukia bure tu, hii ni chuki ambayo asili yake ni mambo ya rohoni na wivu wenye uchungu!

Zaburi 69:4 “Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao kunikatilia mbali wamekuwa hodari, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua.”

Hapo tumeona maana ya neno chuki lakini vile vile neno “bure” katika biblia ya kiebrania linasomeka kama “hinnām” ambalo kwa kiingereza ni “unjustly” na katika biblia ya kiyunani linasomeka kama “dōrean” ambalo maana yake “undeservedly”  katika Kiswahili cha kimahakama kuchukiwa huku kulikuwa kusikokuwa na sababu za haki, kwa dhuluma, bila makosa ya kimahakama, bila kukutwa na hatia, isivyohalali, kwa hiyo watu wanaweza kukuchukia wewe kwa sababu isiyoweza kuthibitishwa kimahakama, kwamba mtuhumiwa ana makosa gani, kwa mfano Daudi alilipishwa kwa nguvu vitu ambavyo hakuvichukua, au Yesu alihukumiwa mahakamani huku hakimu akigundua kuwa ilikuwa ni wivu tu, walimtoa kwa husuda, hakuwa amewakosea wao, wala mtu yeyote.

Mathayo 27:17-18 “Basi walipokutanika, Pilato akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo? Kwa maana alijua ya kuwa wamemtoa kwa husuda.”

Unaona ndugu yangu unaweza kuchukiwa bure katika maisha haya ya kutembea na Yesu unaweza kupigwa vita, unaweza kuchukiwa bila ya sababu, unaweza kuchukiwa kwa sababu zisizo za kweli wala za haki, unaweza kuchukiwa hata na watu uliowahi kuwaomba msamaha hata pamoja na kuwa wamekukosea wao, chuki hii ni chuki ya husuda na haina mashiko, yanapokutokea haya katika maisha ya wokovu na wakati mwingine kutoka kwa watu waliookoka tena wenye nguvu kuliko wewe fahamu umebeba kusudi kubwa na maalumu, fahamu wewe ni mwanafunzi wa Yesu kweli kweli wala usifadhaike, Neno la Mungu linatufunulia siri hizo muhimu zinazopelekea wewe uchukiwe

Sababu za kuchukiwa bure.

Ni muhimu kufahamu kuwa chuki za bure kwako zinafunua maana pana sana za kiwango cha kiroho ulichokifikia, wakristo wengi leo wanaishi maisha ya kinafiki na sio wakweli kwa Mungu wala kwa wanadamu, wengi wanaishi maisha ya kuigiza, wanaonekana kama watu maarufu kwa nje, wakiwa na elimu kubwa, na vyeo vikubwa na wenye pesa na nguvu lakini hawana nguvu za kiroho walishakufa zamani na wamepoteza kabisa kujiamini, na kiroho wamefilisika, unapokuwa mwanafunzi wa kweli wa Yesu na mfuasi wa kweli wa Bwana Yesu katika karne hizi, watakupendea nini? Wakupende kwa lipi? Kama wewe ni mwana wa Mungu tu hawakupendi, kama hujawahi kuwafanya lolote tu wanakuchukia bure je wataweza kuwapenda adui wa kweli ambao Yesu amesema wapendeni adui zenu? Waombeeni wanaowaudhi?, huoni kuwa agizo hilo ni la juu zaidi? Wewe maisha yako yanawapa tabu, kama Yesu alivyowapa taabu mafarisayo na masadukayo, kwa hiyo unapoona wanakuchukia bure ziko sababu nyingi na hapa na ainanisha chache:-

1.       Kwa sababu wewe ni nuru – Mtu wa Mungu ni hivi unapoishi maisha ya nuruni, hapa maana yake wewe ni mkweli kwa Mungu, unapokosea unatubu, na unasonga mbele na huna kinyongo na mtu na Mungu yuko upande wako na anakutetea na kukupigania basi elewa hivi maisha yako ya nuruni yanalifanya giza lidhalilike, hata kama husemi lolote lakini kuishi kwako kwa haki hata bila ya maneno kunawafunua wenye dhambi, kwa hiyo watu wanaweza kukuchukia sio kwa sababu ya kitu umefanya bali kwa sababu kuna kitu unakiwakilisha

 

Yohana 3:19-21 “Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu.”

 

1Yohana 2:9-11 “Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa. Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo. Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.”          

 

2.       Kwa sababu wewe si wa ulimwengu huu – Mtu wa Mungu kama wewe ni wa Yesu Kristo hivi unadhani ulimwengu utakupenda? Ukupende wewe nani? Ukupende wewe umeutendea nini? Ukupende wakati unafunua siri za Mungu? Ukupende wakati hata Yesu Mwenyewe walimchukia bure wewe kama u mwanafunzi wa Yesu utachukiwa tu, Yesu alisema kama mimi mwenyewe walinickukia mwanafunzi hampiti Mwalimu wake yaani kila mwanafunzi wa kweli wa Yesu atachukiwa tu, mpendwa chuki hiyo ni ushahidi wa wazi kwamba unamlingania Yesu Kristo, kuchukiwa kwako sio ushahidi wa kushindwa kwako bali ni ushahidi ya kuwa unamuishia Yesu Kristo  na sio hivyo tu hata mafundisho yetu yatakataliwa kama yalivyokataliwa ya Yesu

 

Yohana 15:18-20 “Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu.”

 

3.       Kwa sababu wewe ni wa rohoni na wao ni wa mwilini – Mtu wa Mungu ninataka nikuambie ya kwamba ulimwengu tulio nao una makundi makuu mawili tu, haijalishi kundi hilo liko kanisani au nje lakini kokote kwenye watu kuna aina mbili za watu watu wa rohoni na watu wa mwilini, wale wa mwilini huwaudhi wale wa rohoni hii ni kanuni ya kibiblia iliyokuwako zamani na inatenda kazi hata sasa, kama wewe ni mzaliwa wa kiroho utaudhiwa na yule wa mwilini tu ona  

 

Wagalatia 4:29 “Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa.”

 

4.       Kwa sababu ya kibali cha Mungu juu yako – Ndugu yangu mpendwa kama Mungu amekupa kibali, Mungu amekupaka mafuta, Mungu ana matumizi na wewe Mungu ana kusudi na wewe kibali cha Mungu juu yako kinawanyanyasa kisaikolojia wale wasio na kibali hicho sasa wakuchekee? Wakutie moyo, wakukubali wakati wanatamani kusikia umeharibikiwa, wanatamani hata ufe leo, Daudi anasema wanaomchukia ni wengi kuliko nywele za kichwa chake, kaangalie mashariki ya kati Israel inapendwa? Wanatamani waifutilie mbali wanatamani waikatilie mbali ndivyo ulivyo na wewe mtu wa Mungu, kibali chako kinawasumbua haijalishi hali ya nje kuwa wao wana nguvu lakini upako wako unawanyanyasa ndio maana wanakuchukia bure

 

1Samuel 29:6-8 “Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme?

 

Mwanzo 37:3-11 “Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani. Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi? Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili.”

 

5.       Kwa sababu ya wivu wenye uchungu – Mpendwa wakati mwingine wewe unachukiwa bure kwa sababu ya wivu, ni wivu tu, kuna kitu wakijilinganisha na wewe au na ninyi  wanakuona kabisa unakwenda mbele, wanakuona kabisa uko tofauti hata kama kwa sasa huna kitu wanakuona na wanajua uweza wa Mungu juu yako na kile ambacho Mungu amewekeza ndani yako wakupende kwa lipi wakati wamejaa wivu, wamejaa wivu huu ni wivu wenye uchungu wivu wa kujilinganisha na wao na wakijilinganisha na wewe wanaona kuna kitu cha ziada kwako wivu huu wa kujilinganisha unaitwa “phthonos” kwa kiingereza “is hatred rooted in comparison”  Yesu alichukiwa kwa sababu alikuwa na kitu cha ziada kuliko mafarisayo na masadukayo, kwa hiyo walikuwa na wivu uliojaa chuki aina hii ya wivu wakati mwingine huwazungumzia watu vibaya  na mambo mabaya ili wao waonekane wema yule mwema aonekane mbaya.

 

Mathayo 27:17-18 “Basi walipokutanika, Pilato akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo? Kwa maana alijua ya kuwa wamemtoa kwa husuda.”

 

Matendo 5:16-20 “Nayo makutano ya watu wa miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu wakakutanika, wakileta wagonjwa, nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa. Akaondoka Kuhani Mkuu na wote waliokuwa pamoja naye, (hao ndio walio wa madhehebu ya Masadukayo), wamejaa wivu, wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza; lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema, Enendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu.”

 

Waebrania 12:14-15. “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.”    

 

6.       Kwa sababu ya vita vya kiroho – Wakati mwingine ile chuki inatokana na mapepo, kwa kadiri shetani alivyo adui yetu na anavyotuchukia sisi ndivyo anavyowatumia mapepo na maajenti wake au wakristo dhaifu kutumiwa na mapepo kutushambulia kwa hio wakati mwingine hii chuki kubwa unayoiona dhidi yako mtu wa Mungu ni ya shetani akiwatumia watu wake au vyombo vyake ili kupingana na kile ambacho Mungu amewekeza ndani yako

 

Waefeso 6:12 “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.”

 

7.       Kwa sababu ya kuishi maisha ya utauwa -  kila unapokusudia na kuthubutu kuishi maisha ya tofauti na wengine maisha ya utakatifu na kuimarisha uhusiano wako wa siri na Mungu watu wabaya  na wadanganyaji wanaendelea kuteseka  na watakucukia, wewe jaribu kuishi na kuigiza kila alichikifanya bwana Yesu, jitoe kama yeye fuata mfano wake uone kama dunia itakupongeza hata kidogo!  Utachukiwa, utateswa, utadhihakiwa, utakataliwa, utaonekana huna faida, kwa sababu maisha ya kujitoa kwa Mungu yanapingana nay a dunia hii, viwango vya kuishi kama Kristo vinawaudhi wahuni,  vinawapa changamoto na kuwafanya wote walio vufuvugu na wasiookoka  wakose Amani, kwa hiyo kuchukiwa ni sehemu ya gharama za uaminifu wako kwa Mungu au kumfuata Yesu kwa uaminifu

 

2Timotheo 3:12-15 “Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa. lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika. Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu.”   

 

Jinsi ya kupokea na kuitikia chuki zao za bure

Ni jambo la kumshukuru Mungu kwamba Mungu ametupa akili na ufahamu katika neno lake namna na jinsi ya kushughulika na watu wanaotuchukia na njia hizo ni njia za kiroho, ambazo kimsingi zitakufanya wewe kuzidi bali adui zako kupungua, njia hizi ukizitumia zitakamilisha uwezo wako wa kiroho na kukunoa na kukufanya wewe uendelee kukua kiroho zaidi na kumfanania baba wa mbinguni

1.       Kunyamaza kimya – Moja ya njia ya kiroho ambayo Yesu Kristo aliitumia pale waliokuwa wakimchukia walipokuwa wakimsingizia mambo ya uongo ambayo hayana ukweli wowote bali kwa lengo la kumchafua na kuharibu tu wito wake yeye alikaa kimya, alipoonewa aikaa kimya alipoteswa na kutukanwa alikaa kimya, Neno kukaa kimya katika kiyunani ni “loidoreō kwa kiingereza ni “revile” ambalo maana yake ni “to insult verbally” hakutumia lugha chafu kujibu alinyamaza kimya badala ya kujibu “silence over revenge”  na alijikabidhi kwa Mungu ahukumuye kwa haki, Mpendwa mwachie Mungu atajibu kwa haki, Mungu huwapigania watu wakimya

 

1Petro 2:21-23 “Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake.Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake. Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki.”

 

Isaya 53:7 “Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake.”

 

Hesabu 12:1-9 “Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi. Wakasema, Je! Ni kweli Bwana amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? Bwana akasikia maneno yao. Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi. Bwana akanena ghafula na Musa, na Haruni na Miriamu, na kuwaambia, Tokeni nje ninyi watatu, mwende hemani mwa kukutania. Basi hao watatu wakatoka nje. Bwana akashuka katika nguzo ya wingu akasimama pale mlangoni pa Hema, akawaita Haruni na Miriamu, nao wakatoka nje wote wawili. Kisha akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, Bwana, nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto. Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la Bwana yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa? Hasira za Bwana zikawaka juu yao; naye akaenda zake.”

 

2.       Waombee wanao kuudhi – Maandiko yanatufundisha kutoka mafundisho na maendo ya Bwana wetu Yesu na watakatifu walioyutangulia kuwa kuna haja ya kuwaombea wale wanaotuchukia, tuwaonee huruma na tuwapende kwa sababu wao ni dhaifu

 

Mathayo 5:43-45 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.”

 

Luka 23:33-34 “Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto. Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura.”

 

3.       Endelea kutenda mema -  Lengo kubwa la shetani wakati mwingine kukushambulia kupitia watu ni ili wewe uwe mtu mbaya, uone kuwa kila unapotenda mema unalipwa mabaya kwa hiyo unaamua kufunga milango yako ya wema na kuwa mbinafsi lakini neno la Mungu linatutaka tuendelee kuwa washindi kwa kutenda mema, kadiri unavyoendelea kuwa mwema na kutenda haki wema wako utawanyamazisha maadui zako na kila ubaya wanaokuzushia

 

Warumi 12:19 “Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana.Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake. Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.”

 

4.       Endelea kupiga kazi, endelea kumtumikia Mungu – Wakati maadui zako wanapokushambulia wewe ongezea viwango vya kumtumikia Mungu na kufanya kazi kwa bidii, kadiri unavyoendelea kumtumikia Mungu kwa bidii Mungu ataendelea kukubariki na kazi unazozifanya zitatangaza kile kitu Mungu ameweka ndani yako,  na kuudhihirishia ulimwengu kuwa yeye yuko na wewe, unapoendelea kumtumikia Mungu kwa nguvu Baraka zako zinaendelea kuongezeka na adui zako wanaendelea kuwekwa uchi neno la Mungu linasema adui zako watakuonyesha maungo yao, yaani uchi zao zitafunuliwa, aibu zao zitawekwa wazi, utupu wao utahukumiwa na kazi unazozifanya wataaibika na kazi yako itasema si biblia imesema kwa matunda yao mtawatambua, je mti mbaya unaweza kuzaa matunda mema?

 

Kutoka 23:25-27 “Nanyi mtamtumikia BWANA, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza.Nitatuma utisho wangu utangulie mbele yako, nami nitawafadhaisha watu wote utakaowafikilia, nami nitawafanya hao adui zako wote wakuonyeshe maungo yao.”   

 

Yohana 10:37-38 “Kama sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini; lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba.”

 

Chuki kutoka kwa wapendwa na watumishi wenzako haimaanishi kuwa Mungu amekuacha bali inakufundisha kuelewa maswala ya kiroho, sio kuwa wakati wote watu watakuchukia kwa sababu wewe ni muovu hapana bali kwa sababu wao ni dhaifu kiroho, Mungu anakufundisha uwezo wa kuvumilia kabla ya kukuinua kukubariki na kukutumia, Mungu anakufundisha kuwa kama Yeye, wewe hujasahaulika, wewe hujashindwa wewe uko sawa na Daudi, uko sawa na Yusufu unafafanana na Yesu  na  ndio maana unachukiwa bila ya sababu za halali, wewe utakuwa kiroho vizuri zaidi, ukiyamudu hayo machungu yote ujue wazi kuwa thawabu yako ni kubwa sana mbinguni


Mathayo 5:11-12 “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.”              

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote


Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni: