Ayubu 1:7-9 “Bwana akamwuliza Shetani,
Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika
kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha Bwana
akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana
mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu
na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu
yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba
yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali
yake imeongezeka katika nchi.”
Utangulizi:
Leo tunalenga kujifunza au
kujikumbusha juu ya ulinzi wa Mungu usioonekana kwa watu wanaomwamini Mungu,
katika kifungu cha maandiko ya msingi tunafunuliwa moja ya jambo la msingi
lililoko katika ulimwengu wa roho ambalo macho yetu hayawezi kuona na huu ni ulinzi
wa Mungu kupitia Malaika, Ukuta wa moto, Ukuta wa shaba, na wigo au ukigo
usioonekana ambao kimsingi unawekwa na Mungu mwenyewe kwa watu wake, siri hii
ya ukigo wa ulinzi uliowekwa na Mungu inafunuliwa na Shetani mwenyewe ambaye
anakiri kuwa alikuwa hawezi kumshambulia Ayubu kwa sababu Mungu alikuwa
amemuwekea ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo,
ulinzi huu wa Mungu ni ulinzi usioonekana, ni ulinzi wa kiroho unaotokana na
uhusiano wetu na Mungu na ni ulinzi unaowekwa na Mungu mwenyewe katika
ulimwenguwa roho.
Zekaria 2:5 “Kwa maana mimi, asema Bwana,
nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka pande zote, nami nitakuwa huo utukufu ndani
yake.”
Yeremia 15:20-21 “Nami nitakufanya kuwa
kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana nawe; lakini
hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na kukuponya, asema
Bwana. Nami nitakuokoa na mkono wa watu wabaya, nami nitakukomboa katika mkono
wao wenye kutisha.”
Kwa msingi huo leo, tutachukua
muda kujifunza somo hili Kuzingirwa kwa ukigo usioonekana kwa kuzingatia
vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya
ukigo usioonekana.
·
Kuzingirwa
kwa ukigo usioonekana.
·
Jinsi ya
kuzingirwa na ukigo usioonekana.
Maana ya ukigo usioonekana.
Siri ya kwamba watu wanaomcha
Mungu wanazingirwa na ukigo pande zote inawekwa wazi kwa mara ya kwanza na
Shetani mwenyewe wakati wa mazungumzo yake na Mungu katika ulimwengu wa roho
kuhusu Mtumishi wa Mungu Ayubu aliyekuwako huku Duniani, Shetani katika mazungumzo
yake na Mungu anaonekana kumjua vema Ayubu, kwa sababu hakuuliza ni Ayubu yupi?
Na tena inaonekana wazi alikuwa anafahamu Ayubu anaishi wapi? Alikuwa
anamfahamu Ayubu vizuri nje ndani na bila shaka alikuwa anafahamu kuwa Ayubu ni
Mtumishi wa Mungu ambaye alikuwa mwaminifu kama maandiko yasemavyo, habari hii
inatufunulia kwa kina kuwa kuna uwezekano wasaidizi wa shetani yaani mapepo na
wenye mamlaka na wakuu wa giza kwa namna Fulani wamewahi kuwa na mpango mkakati
wa kumshambulia Ayubu na huenda walishindwa, na walitoa taarifa kwa bwana wao
kuwa Yule Bwana hawezekani analindwa na nguvu za Mungu, na inawezekana hatimaye
hata Shetani mwenyewe alijaribu kumtembelea Ayubu na kujaribu kutaka
kusababisha uharibifu lakini mbinu zilishindikana, ilibainika wazi kuwa Ayubu
anazingirwa na ulinzi maalumu wa Mungu, na kila anachikifanya Mungu
amekibariki.
Ayubu 1:7-9 “Bwana akamwuliza Shetani,
Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika
kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha Bwana
akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana
mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu
na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu
yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba
yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali
yake imeongezeka katika nchi.”
Tunafunuliwa hapo kuwa ulinzi huu
wa Mungu ambao hapo unatajwa kama UKIGO
sio ulinzi unaoweza kuonekana kwa macho ya nyama, ni ulinzi maalumu unaotokana
na uhusiano bora kati ya Ayubu na Mungu, inawezekana Ayubu hakuwa anaujua, wala
hakuna mtu aliyeweza kuuona kwa macho lakini Shetani katika ulimwengu wa roho
alifahamu kuwa Ayubu anazingirwa na ukigo pande zote, ulinzi huu wa Mungu
hautokani na juhudi zetu wala haki yetu kwa hiyo sio sisi tunaoweza kuuweka
ulinzi huo bali Bwana mwenyewe anawalinda watu wake, hii ni zawadi ya kila
aaminiye.
1Petro 1:3-5 “Ahimidiwe Mungu, Baba wa
Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili
tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate
na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili
yenu. Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu
ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.”
Sasa ulinzi huo maalumu wa Mungu
au nguvu za Mungu zinatotulinda kwa mujibu wa Shetani ameziita ukigo, UKIGO hasa ni nini? Neno ukigo
linalotumika katika maandiko hapo katika Lugha ya Kiebrania linasomeka neno “sûk”
au neno “ώuk”
ambalo linatamkwa sook kwa
Kiingereza “Hedge” ambalo maana yake
ni Ukuta au Ukingo maalumu unaomzingira mtu kwa kusudi la kuweka mipaka ili
asizuriwe, it’s a way of protecting
oneself against quality loss of financial, circumstances, health garden,
properties, flocks etc. ni njia ya kulinda ubora wa mtu, uchumi, mazingira,
afya, bustani, mali, na mifugo ili isipatwe madhara hii ni maana ya kawaida ya UKIGO lakini Ukigo aliouona Shetani
katika maisha ya Ayubu ulikuwa ni ukigo wa kiroho, yaani ukigo usioonekana “An unseen hedge” huu sasa ukigo
usiionekana ni ukigo wa kiroho unaowekwa na Mungu kwa mtu aliyeokoka
kumuwezesha mtu huyo kuwa na ulinzi wa Mungu kwa habari ya maisha yake na mali
zake, uchumi wake, afya yake, watoto wake, mifugo yake mashamba yake na
kadhalika, An unseen hedge is a
spiritual barrier of divine protection placed by God around belivers and their
possessions. Kwa hiyo mtu anayemcha Mungu analindwa na Mungu katika
ulimwengu wa roho kiasi ambacho shetani analalamika kuwa hawezi kusababisha
uharibifu katika jambo lolote kwa sababu Mungu anakulinda.
Kuzingirwa kwa ukigo usioonekana.
Kwa hiyo sasa tunapata ufahamu ya
kuwa kila mtu aliyeokoka, kila amwaminiye Mungu, kila aliyeamini, analindwa na
Mungu katika ulimwengu wa roho bila yeye mwenyewe kutambua na unaweza
kulitambua hilo endapo utaruhusiwa kuona kwa macho ya rohoni, Neno la Mungu
linatufunulia hivyo kwamba kila mtu aliyeokoka anazingirwa na UKIGO usioonekana, ulinzi huu
hauonekani kwa macho lakini ni halisi, ni ulinzi wa kiroho na hauwezi kuonekana
kwa macho ya nyama, ni ulinzi unaowekwa na Mungu mwenyewe na sio kwa jitihada
za kibinadamu, ulinzi huu unazunguka Maisha yako, uhai wako, afya yako, familia
yako, mali zako, watu wako, mazingira yako, Tunaweza kujifunza kutokana na
Nabii Elisha nyakati za agano la kale namna na jinsi alivyokuwa na utambuzi ya
kuwa uko ulinzi katika ulimwengu usioonekana kwa macho ambao unawazingira watu
wa Mungu pande zote ona
2Wafalme 6:15-17 “Hata asubuhi na mapema
mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi
la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia,
Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje? Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi
ni wengi kuliko wale walio pamoja nao. Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana,
nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule
mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari
ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote.”
Unaona hapo tunaona kuwa Elisha alikuwa
na ufahamu kuwa analindwa na jeshi kubwa sana la malaika wasioonekana kwa macho
ya nyama lakini alipomuombea mtumishi wake naye alipewa uwezo wa kuona na kugundua
kuwa kulikuwa na magari ya farasi ya moto yaliyowazunguka pande zote, huu
ulikuwa ukigo wa kiroho unaowazingira watumishi wa Mungu pande zote, mtu mmoja
alisema ikiwa Elisha wa agano la kale alilindwa kiasi hiki ni wazi kuwa waamini
katika Kristo nyakati hizi za agano jipya wanalindwa zaidi na nguvu za Mungu na
ukigo usioonekana katika ulimwengu wa
roho, kuliko Elisha ambaye Yesu alikuwa hajamfia Msalabani, ikieleza namna watu
wa Mungu wanavyolindwa Biblia iko wazi kwamba kila aliyemwamini Yesu analindwa
iwe anajua au hajui
Marko 16:15-18 “Akawaambia, Enendeni
ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa
ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio;
kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata
wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya
wagonjwa, nao watapata afya.”
Awaye yote ambaye anamtegemea
Mungu na kumcha yeye na kuendelea kukaa katika uwepo wa Mungu kimsingi
anajiweka katika ulinzi wa Mungu, kwa sababu hiyo kimsingi kila mtu
anayemtumainia Mungu anajiweka katika kuzingirwa kwa ukigo usioonekana, inaweza
kuwa malaika, ama ukuta wa moto au ukuta wa shaba na kadhalika na ni Mungu
ndiye anayetulinda kupiria serikali yake ya mbinguni, ile mamlaka ya kiungu
inahusika na ulinzi wetu
Zaburi 91:1-11 “Aketiye mahali pa siri pake
Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi. Nitasema, Bwana ndiye kimbilio
langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini. Maana Yeye atakuokoa na
mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo. Kwa manyoya yake atakufunika,
Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao. Hutaogopa
hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana, Wala tauni ipitayo gizani, Wala uele
uharibuo adhuhuri, Ijapo watu elfu waanguka ubavuni pako. Naam, kumi elfu mkono
wako wa kuume! Hata hivyo hautakukaribia wewe. Ila kwa macho yako utatazama, Na
kuyaona malipo ya wasio haki. Kwa kuwa Wewe Bwana ndiwe kimbilio langu; Umemfanya
Aliye juu kuwa makao yako. Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia
hema yako. Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote.”
Daniel 6:18-22 “Kisha mfalme akaenda
nyumbani kwake, akakesha usiku kucha, akafunga; na vinanda havikuletwa mbele
yake; na usingizi wake ukampaa. Asubuhi mfalme akaondoka mapema, akaenda kwa
haraka mpaka penye lile tundu la simba. Naye alipolikaribia lile tundu,
akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danieli, Ee
Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako, unayemtumikia daima,
aweza kukuponya na simba hawa? Ndipo Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme,
uishi milele. Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya
simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia;
tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno.”
Kwa msingi huo kupitia maandiko
haya na ufunuo wa neno la Mungu tunajifunza hapa kuwa mtu anayemtegemea na
kumtumainia Mungu anazingirwa kwa ukigo usioonekana katika ulimwengu wa roho ni
pale tu unapokuwa na macho ya rohoni na unapolielewa neno la Mungu ndipo
unapoweza kuelewa ya kuwa katika ulimwengu wa roho tunao ukigo usioonekana yaani
tunao ulinzi usioonekana kwa macho.
Jinsi ya kuzingirwa na ukigo usioonekana.
Tunahakikishiwa kuwa ukigo
usioonekana ni Dhahiri kwa watu wa Mungu, na ni wa muhimu, lakini swali kubwa
ni kuwa tunawezaje kuzingirwa na ukigo huu usiioonekana je tunaweza kuomba
ulinzi wa Mungu? Maandiko yanaonyesha wazi kuwa sio dhambi kuomba ulinzi wa
Mungu, japokuwa Mungu mwenyewe huwa anawalinda watu wake kwa hiyari yake na
mapenzi yake, Shetani alipolaumu kuhusu ulinzi wa Ayubu alisema wewe
umemzingira kwa ukigo pande zote maana yake ilikuwa ni Mungu kwa hiyari yake na
kwa mapenzi yake alimlinda Ayubu
Ayubu 1:7-10 “Bwana akamwuliza Shetani,
Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika
kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha Bwana
akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana
mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu
na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu
yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba
yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali
yake imeongezeka katika nchi.”
Hata hivyo ingawa ulinzi wa Mungu
ni tukio la hiyari linalofanywa na Mungu mwenyewe maandiko hayakatazi kuomba
ulinzi wa Mungu, viko viashiria kadhaa wa kadha vya kimaandiko vinavyotuthibitishia
kuwa tunaweza kuomba ulinzi wa Mungu na huu ni ukweli usioweza kupingika, mfano
katika sala ya Bwana iliyofundishwa na Bwana Yesu kuna sehemu ya kujiombea
ulinzi, lakini sio hivyo tu Yesu katika maombi yake yeye mwenyewe alituombea
ulinzi
Mathayo 6:13 “Na usitutie majaribuni,
lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu,
hata milele. Amina.]”
Yohana 17:14-16 “Mimi nimewapa neno lako;
na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa
ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule
mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.”
Ezra 8:21-23 “Ndipo nikaamuru kufunga, hapo
penye mto Ahava, ili tupate kujinyenyekeza mbele za Mungu, na kutafuta kwake
njia iliyonyoka, kwa ajili yetu sisi wenyewe, na kwa ajili ya watoto wetu, na
kwa mali yetu yote. Maana naliona haya kumwomba mfalme kikosi cha askari na
wapanda farasi, ili kutusaidia juu ya adui njiani; kwa maana tulikuwa tumesema
na mfalme, tukinena, Mkono wa Mungu u juu ya watu wote wamtafutao, kuwatendea
mema; bali uweza wake na ghadhabu yake ni kinyume cha wote wamwachao. Basi
tukafunga, tukamsihi Mungu wetu kwa ajili ya hayo; naye akatutakabali.”
Kwa hiyo tunajifunza ya kwamba
mojawapo ya njia ya kuzingirwa na ukigo usioonekana ni pamoja na kuomba ulinzi
wa Mungu kwaajili yetu japo kuwa swala la kulindwa na Mungu liko katika mikono
yake, na sisi tu mali yake
Njia nyingine ya kukaribisha
ulinzi wa Mungu au kuzingirwa na ukigo usioonekana katika maisha yetu ni kuwa
na Maisha ya kumcha Mungu, Neno la Mungu linathuthibitishia ya kuwa Mungu
huwazingira kwa ngao wale wanaotembea katika haki yaani wale wanaomcha Mungu.
Zaburi 5:11-12 “Nao wote wanaokukimbilia
watafurahi; Watapiga daima kelele za furaha. Kwa kuwa Wewe unawahifadhi, Walipendao
jina lako watakufurahia. Kwa maana Wewe utambariki mwenye haki; Bwana,
utamzungushia radhi kama ngao.”
Zaburi 34:7-9 “Malaika wa Bwana hufanya
kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa. Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema;
Heri mtu yule anayemtumaini. Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao
hawahitaji kitu.”
Ulinzi wa Mungu unathibitika wazi
kwa wale wanaomcha Mungu, ni muhimu kufahamu kuwa ahadi za Mungu zinategemea (Conditional) pande zote mbili, Mungu
anatoa ahadi ya kutupigania na kutulinda lakini ni wajibu wetu kumtii, kama
utaharibu ukigo wako wewe mwenyewe utauharibu kwa kutokuwa mwaminifu kwa Mungu
na hapo ni lazima utakula mkong’oto, hapa nisikupake mafuta kwa mgongo wa chupa
niweke wazi kuwa kama ukimkosea Mungu huna budi kutubu na kurekebisha kwa
haraka usitegemee ulinzi wa Mungu wakati wa kuasi kinyume na mapenzi yake ndio
maana siku hizi hata walokole wanarogwa! Wanarogwaje kwa sababu wanaishi maisha
ya kawaida na kuendelea katika dhambi huku wakidhani Mungu anatendelea kuwa
mlinzi kwao tuambiane ukweli usimpe ibilisi nafasi, Mungu alimuhakikishia
Joshua ushindi yaani maana yake pamoja na ulinzi lakini sharti ilikuwa lazima
atende sawasawa na yote yaliyoandika
katika kitabu cha torati ya Musa vinginevyo unapigwa ona:-
Yoshua 1:5-7 “Hapatakuwa mtu ye yote
atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa
pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala
sitakuacha.Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu
hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na
ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa
mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate
kufanikiwa sana kila uendako.”
Yoshua 7:1-12 “Lakini wana wa Israeli
walifanya dhambi katika kitu kilichowekwa wakfu; maana Akani, mwana wa Karmi,
mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila ya Yuda, alitwaa baadhi ya vitu
vilivyowekwa wakfu; hasira ya Bwana ikawaka juu ya wana wa Israeli. Kisha
Yoshua akatuma watu kutoka Yeriko mpaka mji wa Ai, ulio karibu na Bethaveni,
upande wa mashariki wa Betheli, akawaambia, akisema, Pandeni juu mkaipeleleze
nchi, basi wakapanda juu wakaupeleleza Ai. Wakarejea kwa Yoshua wakamwambia,
Wasiende watu wote, ila waende watu kama elfu mbili, tatu, wakaupige Ai;
usiwataabishe watu wote kwa kuwaendesha huko; maana watu hao ni wachache tu.
Basi watu wakaenda huko wapata elfu tatu tu; nao wakakimbia mbele ya watu wa
Ai. Watu wa Ai wakawapiga watu kama thelathini na sita; wakawafuatia kutoka
mbele ya mlango mpaka Shebarimu, wakawapiga huko kwenye matelemko; mioyo ya
watu ikayeyuka, ikawa kama maji. Yoshua akararua mavazi yake, akaanguka
kifudifudi mbele ya sanduku la Bwana hata jioni, yeye na wazee wa Israeli;
wakatia mavumbi vichwani mwao. Yoshua akasema, Ee Bwana MUNGU, kwa nini
umewavusha watu hawa mto wa Yordani, ili kututia katika mikono ya Waamori, na
kutuangamiza? Laiti tungelikuwa radhi kukaa ng'ambo ya Yordani Ee Bwana, niseme
nini baada ya Israeli kuwapa visogo adui zao? Maana Wakanaani na wenyeji wote
wa nchi hii watasikia habari hii, nao watatuzingira, na kulifuta jina letu
katika nchi. Nawe utafanya nini kwa ajili ya jina lako kuu? Bwana akamwambia
Yoshua, Haya! Inuka, mbona umeanguka kifudifudi hivi? Israeli wamefanya dhambi,
naam, wamelivunja agano langu nililowaagiza; naam, wametwaa baadhi ya vitu
vilivyowekwa wakfu; tena wameiba, tena wameficha na kuvitia pamoja na vitu vyao
wenyewe. Ndiposa wana wa Israeli hawawezi kusimama mbele ya adui zao; wakawapa
visogo adui zao, kwa sababu wamelaaniwa; mimi sitakuwa pamoja nanyi tena,
msipokiharibu kitu kile mlicho nacho kilichowekwa wakfu.”
Kumbukumbu 1:41-45 “Ndipo mkanijibu,
mkaniambia, Sisi tumefanya dhambi juu ya Bwana, tutakwea kupigana kwa mfano wa
yote tuliyoamriwa na Bwana. Mkajifunga kila mtu silaha zake za vita, mkafanya
wepesi kukwea mlimani. Bwana akaniambia, Uwaambie, Msiende, wala msipigane;
kwani mimi si kati yenu; msije mkapigwa mbele ya adui zenu. Basi niliwaambia,
msinisikize, bali mliasi amri ya Bwana, mkajikinai, na kukwea mlimani. Na
Waamori waliokuwa wakikaa katika mlima huo, waliwatokea juu yenu, wakawafukuza,
kama wafukuzwao na nyuki, wakawapomoshea Seiri mpaka Horma. Mkarudi mkalia
mbele za Bwana; Bwana asiisikize sauti yenu, wala hakuelekeza masikio yake
kwenu.”
Neno la Mungu linatufundisha wazi
hapo kuwa ulinzi wa Mungu ni Dhahiri kwa wale wamchao, lakini kama tukimuasi
tunakuwa tumeharibu ukigo unaotuzingira na kwa sababu hiyo ni rahisi kushindwa
na kushambuliwa na inaweza kuwa aibu kwetu, kama watu wanamtaka Mungu basi
wamtake jumla jumla na sio nusu nusu, Neno la Mungu linasema yeye abomoaye boma
nyoka watamuuma
Muhubiri 10:8-9 “Mwenye kuchimba shimo
atatumbukia ndani yake; Na yeye abomoaye boma, nyoka atamwuma. Mwenye kuchonga
mawe ataumizwa kwayo; Naye apasuaye miti huona hatari katika hiyo.”
Kama hujaokoka na unahitaji
ulinzi wa Mungu basi ni vema ukampokea Yesu,awe bwana na mwokozi wa maisha
yako, Damu ya Yesu ni ulinzi na usalama wa maisha yako na Yule muharibifu
anapoona alama ya damu yeye atapita juu yako na hataleta madhara katika nyumba
yako kwa sababu umeiamini ile kazi iliyofanywa naye pale Msalabani.
Kutoka 12:12-13 “Maana nitapita kati ya
nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya
Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya
Misri; Mimi ndimi BWANA. Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba
mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo
lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri.”
Kuzingirwa na ukigo usioonekana
ni swala la uhakika kwa wana wa Mungu, Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu,
ukweli tunaweza tusione kwa macho kile kinachoendelea katika ulimwengu wa roho
lakini neno la Mungu linatuhibitishia kuwa tunalindwa, malaika wapo, ukuta wa
moto uko unatuzunguka na mbingu zinatambua uwepo wetu na mahitaji yetu na wema
wake utatuzunguka
Zakarika 2:5 “Kwa maana mimi, asema Bwana,
nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka pande zote, nami nitakuwa huo utukufu ndani
yake.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
.jpg)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni