Jumapili, 11 Januari 2026

Mwanzi uliopondeka hatauvunja!


Isaya 42:1-4 “Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu. Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli. Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sheria yake.”



Utangulizi:

Kaka zangu na dada zangu katika Bwana, Leo tutachukua muda kujifunza mojawapo ya unabii wa muhimu sana katika huduma ya Masihi ambao kimsingi ulikuja kutimizwa katika agano jipya, Wakati wa huduma ya Masihi hapa duniani, Unabii huu ambao kimsingi unatufundisha kusudi kubwa la huduma na moyo wa Masihi Yesu Kristo hapa ulimwenguni, jinsi alivyojawa na huduma iliyojaa rehema na upendo unaopitiliza mipaka ya kawaida ya huduma za kibinadamu na kidini.

Mathayo 12:15-21 “Naye Yesu hali akiyafahamu hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote, akawakataza wasimdhihirishe; ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; Mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; Nitatia roho yangu juu yake, Naye atawatangazia Mataifa hukumu. Hatateta wala hatapaza sauti yake; Wala mtu hatasikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hata ailetapo hukumu ikashinda. Na jina lake Mataifa watalitumainia.”

Kwa ujumla unabii wa Isaya na kutimia kwake kunatukumbusha jambo muhimu sana na lenye kutia moyo ya kuwa Ufalme wa Mungu unatenda kazi katika msingi wa rehema, urejesho na huruma zisizotikisika! “Mwanzi uliopondeka hatauvunja na utambi utokao moshi hatauzima” vinawakilisha nini hasa katika ujumbe huu? Bila shaka Mungu Roho Mtakatifu atatupa kuelewa; Tutajifunza somo hili Mwanzi uliopondeka hatauvunja kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-

·         Ufahamu kuhusu mwanzi uliopondeka na utambi utokao moshi

·         Huduma ya kimasihi mwanzi uliopondeka na utambi utokao moshi

·         Mwanzi uliopondeka na utambi utokao moshi


Ufahamu kuhusu mwanzi uliopondeka na utambi utokao moshi.

Ni muhimu kufahamu kuwa usemi wa “mwanzi uliopondeka na utambi utoka moshi” ni usemi wenye maana gani kinabii kabla ya kuunganisha na kuangalia huduma ya kimasihi itakavyokuwa, Neno mwanzi linalotumika katika maandiko ya kiingereza linatumika neno “REEDS” ambalo kwa Kiswahili maana yake ni nyasi, Hata hivyo nyasi ziko za aina mbalimbali, kwa hiyo nyasi hizi katika

lugha ya Kiebrania zinaitwa kwa kutumia neno Kāneh kwa lugha ya Kilatini na Kiyunani linatumika neno Canna kwa kiingereza Cane  mmea huu kwa kawaida ulistawi sana pembeni mwa mto Jordan katika taifa la Israel kwa Kiswahili unaitwa MWANZI, majani ya Mwanzi au Cane kwa Kiyunani yanajulikana kama kálamos au Calamus, kwa Kiswahili Kalamu. Nyakati za agano la kale kabla ya kuwepo kwa teknolojia ya uandishi tuliyo nayo sasa Manabii na waandishi walitumia majani ya muanzi kama kalamu ya kuandikia, waliyatumia majani haya na kuchovya kwenye wino na kuyatumia kuandikia katika karatasi maalumu za nyakati hizo (Papyrus) au Magombo ya chuo ya ngozi, walichovya katika bakuli la wino kwa kutumia majani hayo yaliyoitwa kalamu na kisha kuyatumia kuandikia endapo kalamu ingechoka au kupondeka waliitupa na kuchomoa jani lingine la muanzi yaani kalamu na kutoka kwenye kitita cha majani hayo na kulitumia kuandika, waandishi wangeifanya kazi hiyo ngumu kutwa nzima na usiku, huku usiku wakitumia taa ya kibatali iliyotumia mafuta na utambi, manabii na waandishi walifanya kazi ya kuandika mpaka mafuta yangewaishia na taa ikazimika na utambi ungebaki unafuka moshi hapo wangezima kabisa na kulala wakiwa wamechoka sana kitendo cha kuvunjika kwa Kalamu au kuisha kwa utambi kulikwamisha kwa kiwango kikubwa kazi nzima ya uandishi, wakati huu nabii Isaya alipokea ujumbe wa kinabii kwamba kazi hiyo ya kuchosha itakuwa nyepesi, wakati wa Masihi, na wakati wa Masihi kalamu haitavunjika wala utambi hautaisha na kufuka moshi, uwepo wake utasababisha uzima katika mazingira yote.

Isaya 42:1-3 “Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu. Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli.”

Huduma ya kimasihi mwanzi uliopondeka na utambi utokao moshi

Kimsingi Mwanzi uliopondeka na utambi unaofuka moshi ulikuwa ni usemi uliotumika kuelezea pia kitu ambacho kimepoteza maana, hakifai tena kwa matumizi, kitu kinachokwamisha kazi ya uandishi kusonga mbele, lakini sio hivyo tu usemi huu ulitumika pia kuwaita mataifa mengine wasio wayahudi yaani mataifa, hao waliitwa pia mwanzi uliopondeka, na utambi utokao moshi ulimaanisha watu wa Mungu ambao wamepoteza thamani yao, yaani walikuwa Nuru na sasa wamezimika hawafai tena kwa matumizi, Mwanzi mataifa wasiofaa, Utambi wayahudi waliopoa.

Mwanzi uliopondeka – Uliwakilisha mataifa au watu wenye dhambi lakini pia, walemavu au wagonjwa, watu wasio na matumaini, waliokandamizwa ambao kila kitu kwao kimepoteza maana wamepoteza maana katika jamii, hawafai, wamevunjika, hawana matumizi tena, ni wa kutupwa, wanyonge, waliochoka nafsi zao, sababu ya changamoto, wenye laana, wenye mikosi wasioofaa kitu, wasio na uhakika wa wokovu, wanaohesabika kuwa sio kitu wanaosubiria kuchomwa moto.

Utambi utokao moshi – Uliwakilisha watu wa Mungu Israel wenyewe waliokuwa nuru lakini wamepoteza thamani wamepoa wamerudi nyuma, hawana thamani tena ni watenda dhambi wamepoa, wote wanaosubiria hukumu yao tu hawana kitu cha ziada zaidi ya kukwamisha kazi.

Isaya anaona kuwa wanasubiri maamuzi ya hakimu ambaye ni Masihi, yeye anajua atawahukumuje hiki ndicho Isaya alichokuwa anakiona katika unabii wake lakini anaona kama Masihi atakapokuja huenda mambo yatakuwa tofauti, kwani hukumu zake ni tofauti na uweza wake ni tofauti yeye Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima kwa kuwa yeye ana Roho wa Mungu, anapendezwa na Mungu anajua atayatimiza vipi mapenzi ya Mungu, Kwa Masihi hakutakuwa na mtu asiye na faida, hakutakuwa na mtu wa kutupwa, au kuzimwa ni wakati wa uamsho mkubwa sana Masihi atatenda kwa namna ya tofauti sana na mitazamo ya dini ya Kiyahudi

Huyu mataifa wanamtumainia, Kimsingi Isaya aliyatabiri maswala hayo katika unabii wake na Kristo Yesu alipokuja Duniani aliyatimiza haya na ndio Mathayo alipoyaona alikumbuka kile alichokuwa amekitabiri nabii Isaya akaandika sawa na unabii wa Isaya

Mathayo 12:15-21 “Naye Yesu hali akiyafahamu hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote, akawakataza wasimdhihirishe; ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; Mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; Nitatia roho yangu juu yake, Naye atawatangazia Mataifa hukumu. Hatateta wala hatapaza sauti yake; Wala mtu hatasikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hata ailetapo hukumu ikashinda. Na jina lake Mataifa watalitumainia.”

Masihi alipokuja alihukumu kwa haki kwani kwanza aliwaona wote kuwa ni wenye dhambi, Mataifa na Wayahudi pia na hakukuwa na aliye bora kuliko mwingine wote wanahitaji msaada wake, Wayahudi na Mataifa mengine wote ni wenye dhambi wote wanamuhitaji Masihi hakuna mwenye haki hata mmoja wala hakuna anayemtafuta Mungu wala hakuna anayetenda mema hata mmoja wala hakuna anayemcha Mungu, hakuna aliye bora kuliko mwingine hakuna mwenye nafuu wote wanahitaji rehema za Mungu na Masihi amekuja kwaajili hiyo hakuja kuhukumu amaekuja kutangaza rehema za Mungu, amekuja kutangaza msamaha wa dhambi, fadhili za Mungu na kuponya mwili na roho

Warumi 3:9-18 “Ni nini basi? Tu bora kuliko wengine? La! Hata kidogo. Kwa maana tumekwisha kuwashitaki Wayahudi na Wayunani ya kwamba pia wamekuwa chini ya dhambi; kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja. Koo lao ni kaburi wazi, Kwa ndimi zao wametumia hila. Sumu ya fira i chini ya midomo yao. Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu. Miguu yao ina mbio kumwaga damu. Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao. Wala njia ya amani hawakuijua. Kumcha Mungu hakupo machoni pao.”

Huduma ya Masihi inatoa rehema kwa wote waliovunjika na waliopoa wanaofuka moshi tu lakini moto umezimika wote wanamuhitaji Yesu, achochee utambi uwake na aponye waliovunjika,  uvumilivu na upole na upendo wa Bwana wetu Yesu Kristo ndio unaowavumilia watu leo na kuwapa nafasi ili waponywe na moto uwake tena, lakini sio hivyo tu Yesu yuko tayari kushughulika na wote walioumizwa, wanaohitaji rehema na upendo wake yeye yuko tayari kuwahudumia na kuwaponya watu wote wanapaswa kumuendea na watu wote wanapaswa kulitegemea jina lake, Yeye hazimii wala hakati tamaa na mtu, watu wote watamtumainia na kuliitia jina lake yeye yuko tayari kusaidia.

Matendo 4:10-12 “jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”                 

Mwanzi uliopondeka na utambi utokao moshi.

Mathayo 12:15-21 “Naye Yesu hali akiyafahamu hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote, akawakataza wasimdhihirishe; ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; Mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; Nitatia roho yangu juu yake, Naye atawatangazia Mataifa hukumu. Hatateta wala hatapaza sauti yake; Wala mtu hatasikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hata ailetapo hukumu ikashinda. Na jina lake Mataifa watalitumainia.”

Mathayo alipokuwa anawaona watu mbalimbali matajiri kwa masikini, wenye nguvu na wasio na nguvu wakimiminika kwa kutafuta msaada kwa Yesu alikumbuka kutimia kwa unabii wa Isaya na anaunukuu.

Huduma ya Masihi ilikazia ukweli kuwa Yesu hakuja kwaajili ya wenye nguvu, wala wenye kujitosheleza, wanaojifikiria kuwa wao ni wakamilifu amekuja kwaajlii ya waliovunjika wasio na faida waliozimika, Yesu alitakasa wenye ukoma, aliwagusa wakoma waliokuwa wamekataliwa, alisamehe wenye dhambi, aliwarejesha hata wale waliomkana mara tatu kama Petro, alishughulika na wale ambao wangestahili kubadilishwa na kutupwa, Mwanzi uliovunjika haukufaa tenza kwa waandishi zaidi ya kuchomwa moto na kutumia mwingine na utambi uliofuka moshi ulisubiri kubadilishwa, Lakini Masihi yeye angehuisha vile vinavyoonekana kutokufaa viweze kufaa kwa utukufu wa Mungu

Luka 5:30-32 “Ikawa Mafarisayo na waandishi wao kuwanung'unikia wanafunzi wake, wakisema, Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Yesu akajibu akawaambia, Wenye afya hawana haja na tabibu, isipokuwa walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.”

Marko 16:6-7 “Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka. Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia.”             

Yohana 21:15-17 “Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam ,Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.”

Huduma ya kimasihi ni huduma ya uponyaji wa mwili nafsi na roho, ni huduma ya uvumilivu ni huduma ya huruma na upendo ni huduma ya kuchukuliana  na ni huduma ambayo haioni mkamilifu inaona kuwa kila mtu anahitaji huduma yake isipokuwa wale wenye kiburi tu na wale wanaojihesabia haki, kila mtu na kila mmoja anamuhitaji Bwana Yesu na ukarabati wa watu wa Mungu wa aina zote unatakiwa kupatikana kanisani, kanisani sio mahali pa watakatifu tu ni mahali pa watu wote wenye nguvu na dhaifu atakayekuja kuchuja ni Yesu mwenyewe, wajibu wetu sisi ni kuhubiri injili, na kuwafundisha watu na Neno la Mungu lenyewe litawabadilisha, Yesu mwenyewe atawaokoa na kuwasamehe watu wake yeye ndiye anayeweza kuwafinyanga watu wake wakawa kama yeye alivyo, hukumu halali itatolewa siku ya mwisho na mwenyewe sio sisi

Mathayo 13:47-50 “Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna; hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa. Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.”

Uko uwezekano kuwa unaona ujumbe huu huku ukiwa umevunjika moyo, una ndoa iliyovunjika, una uchumba uliovunjika una mahusiano yaliyopondeka, una nuru iliyozimika una hasara katika biashara na hujui utainukaje, una madeni, au utambi wako wa rohoni umezimika, matumaini ya maisha yako na ndoto zako zimekwama mahali.  Giza limetanda na kila kitu kinaonekana kukwama katika maisha yako, uwezo wako wa kusimama tena umepotea, muda wako umepotea, unajiuliza itakuwaje tena katika maisha yangu? Itakuwaje katika roho yangu? Je naweza kusimama tena hata baada ya kuharibu namna hii? Lakini kwa uwezo wa Bwana wetu Yesu Kristo, yeye anakuganga na kukuponya na kukuinua tena nakuhakikishia moto uliozimika utawaka na moyo uliovunjika utainuka hii ndio kazi ya Masihi amka leo acha kulia katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai, Yesu alikuja kwaajili ya watu kama wewe watu ambao wanatarajiwa kutupwa, na wanaoonekana kutokufaa katika jamii wenye matumaini yaliyofifia yeye haogopi hayo na anatoa mwaliko kuwa watu wote wenye changamoto zozote zile waje kwake

Mathayo 11:28-29 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;”

“Maombi yangu yafike kwako Moyo, uliopondeka hutadharau, Kiu yangu na haja yangu, nifanane nawe nifanane nawe, nifanane nawe, Nifanye kama wewe, unifinyange, nifinyange, wakinitazama wakuone wewe unifinyange, nifinyange”

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: