Zaburi 40:1-3 “Nalimngoja Bwana kwa saburi,
Akaniinamia akakisikia kilio changu. Akanipandisha toka shimo la uharibifu,
Toka udongo wa utelezi; Akaisimamisha miguu yangu mwambani, Akaziimarisha hatua
zangu. Akatia wimbo mpya kinywani mwangu, Ndio sifa zake Mungu wetu. Wengi
wataona na kuogopa, Nao watamtumaini Bwana”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kwamba tuwapo
duniani ziko nyakati ambazo tunaweza kupita katika mazingira ya hatari sana,
mazingira ya kutisha ambayo kimsingi yanaweza kukuweka katika hali ya kukosa
msaada wala hata kusikilizwa kwa sauti yako na ukakosa msaada ni nyakati ambazo
unaweza kuchagua kifo kuliko uhai, wakati ambao unaweza kuchagua kukata tamaa
kuliko kujipa moyo, nyakati ambazo umezama katika giza na huoni hata dalili ya
nuru unachokiona mbele yako ni dalili za uharibifu yaani mauti, hali hiyo
inaweza kuwa misiba, inaweza kuwa upotevu wa mali, inaweza kuwa kutapeliwa
fedha nyingi, inaweza kuwa changamoto za kiafya inaweza kuwa mashambulizi
kutoka kwa maadui, watu wanaokuchukia, inaweza kuwa magonjwa makubwa yasiyo na
tiba na kadhalika hayo yanapokushambulia katika lugha ya kibiblia linaitwa
shimo la uharibifu, katika nyakati hizo hata Mungu huonekana kuwa kimya unaweza
ukamuita na ukasubiri na bado akakunyamazia, kipindi hicho huwa ni kipindi
kigumu sana kwa mwanadamu na waandishi wa mashairi ya kibiblia wamekiita shimo
la uharibifu! Je umewahi kupita au je unapita katika shimo la uharibifu? wako
watu walipita
Zaburi 40:1-3 “Nalimngoja Bwana kwa saburi,
Akaniinamia akakisikia kilio changu. Akanipandisha toka shimo la uharibifu,
Toka udongo wa utelezi; Akaisimamisha miguu yangu mwambani, Akaziimarisha hatua
zangu. Akatia wimbo mpya kinywani mwangu, Ndio sifa zake Mungu wetu. Wengi
wataona na kuogopa, Nao watamtumaini Bwana”
Katika maandiko yetu ya msingi,
tunajifunza ushudua wa Daudi mwandishi wa zaburi hii akimshukuru Mungu baada ya
kumuokoa na kumtoa katika shimo la uharibifu, lenye matope na uterezi,
kuimarisha hatua zake na kutia wimbo mpya kinywani mwake, Pamoja na kuwa zaburi
hii ilimuhusu Daudi, inamuhusu vile vile Yesu Kristo ambaye aliteswa akafa na
kuzikwa na kufufuka siku ya tatu akitolewa katika shimo la uharibifu (kaburi),
sio hivyo tu zaburi hii inamuhakikishia kila mmoja wetu kuwa Mungu atakutoa
katika shimo la uharibifu unalolipitia, tutajifunza somo hili Akanipandisha toka shimo la uharibifu! kwa kuzingatia vipengele vikuu muhimu vitatu
vifuatavyo;-
·
Maana ya
shimo la uharibifu
·
Kupandishwa
toka shimo la uharibifu
·
Mamlaka
ya kupandishwa toka shimoni
Maana ya shimo la uharibifu.
Shimo la uharibifu katika lugha
ya Kiebrania linaitwa “Shâ’ôn bôr” kwa kiingereza ni “Horrible pit” au “Destruction bore”, au “tumult Pit” au “Sheol”
kuzimu au kaburi au hatari ya kifo, ambalo maana yake ni shimo lenye
kutisha, au shimo la uharibifu, au shimo la mateso, lenye kelele, lenye
kuchanganya, Mwandishi anajaribu kusimulia hali ngumu ambayo Mungu anaweza
kuiacha mtu wake akaipitia ambayo kimsingi, ni hali ya shinikizo kubwa sana la
mateso ambayo kibinadamu ni vigumu kuyaepuka ni shimo ambalo unanasa na huwezi
kujiokoa shimo la utelezi, shimo hili ni kama kuingizwa kaburini ukiwa umekufa
ambako sio rahisi kutoka kwa nguvu zako na akili zako za kibinadamu mpaka kwa
msaada wa Mungu, Ni Mungu peke yake ndiye anayeweza kukutoa huko!
Zaburi
28:1-2 “Ee Bwana, nitakuita Wewe, mwamba wangu,
Usiwe kwangu kama kiziwi. Nisije nikafanana nao washukao SHIMONI, Ikiwa
umeninyamalia. Uisikie sauti ya dua yangu nikuombapo, Nikipainulia patakatifu
pako mikono yangu.”
Zaburi
88:3-6 “Maana nafsi yangu imeshiba taabu, Na uhai
wangu umekaribia kuzimu. Nimehesabiwa pamoja nao washukao SHIMONI; Nimekuwa
kama mtu asiye na msaada. Miongoni mwao waliokufa nimetupwa, Kama waliouawa
walalao makaburini. Hao ambao Wewe huwakumbuki tena, Wametengwa mbali na mkono
wako. Mimi umenilaza katika shimo la chini, Katika mahali penye giza vilindini.”
Zaburi 30:1-3 “Ee Bwana, nitakutukuza kwa
maana umeniinua, Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu. Ee Bwana, Mungu
wangu, Nalikulilia ukaniponya. Umeniinua nafsi yangu, Ee Bwana, kutoka KUZIMU.
Umenihuisha na kunitoa Miongoni mwao washukao SHIMONI.”
Isaya 38:17-18 “Tazama; nalikuwa na uchungu
mwingi kwa ajili ya amani yangu; Lakini kwa kunipenda umeniokoa na SHIMO LA
UHARIBIFU; Kwa maana umezitupa dhambi zangu zote nyuma yako. Kwa kuwa KUZIMU
hakuwezi kukusifu; mauti haiwezi kukuadhimisha; Wale washukao SHIMONI hawawezi
kuitarajia kweli yako.”
Unaona neno shimo katika maandiko
au shimo la uharibifu linazungumzia hali ya hatari, hali ya mateso makali,
kukata tamaa, hali ya kushindwa na kukandamizwa ni shida na taabu ambazo
zinaelekea kelele za mauti na wakati huohuo huwezi kujiokoa au kujitoa katika
shimo hilo kwa kuwa ni shimo la matope, hali hii inaweza kufanana kabisa na
hali ya mateso aliyoyapitia Bwana wetu Yesu Kristo na kufa kwake msalabani
ambapo hakupata msaada wowote wakati wa mateso, kwa hiyo wakati mwingine
tunapitia hali kama hiyo ambayo kimsingi tunaweza kufikia kukata tamaa, shimo
hili linaweza kuwa shimo la madeni, linaweza kuwa shimo la umasikini, linaweza
kuwa shimo la magonjwa, linaweza kuwa shimo la msongo wa mawazo, linaweza kuwa
shimo la dhambi, linaweza kuwa shimo la mauti, linaweza kuwa shimo la kushindwa
kiroho, linaweza kuwa la matatizo
Kupandishwa toka shimo la uharibifu.
Tunapoadhimisha msimu huu wa
pasaka na kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo kutoka kwa wafu, tunajikumbusha
vile vile kazi ya Mungu ya kuwatoa wanadamu kutoka katika mashimo ya uharibifu
mashimo ambayo huwezi kujitoa bila nguvu ya ufufuo, kukutoa katika shimo lako,
Yesu alipokufa aliwekwa shimoni na adui zake walililinda na kaburi ili
kuhakikisha ya kuwa hatoki humo, Yesu aliingia katika shimo la mateso, alikataliwa
na watu jamii nzima ilizomewa jamii ikisema asulubiwe asulubiwe, alipigwa
mijeledi, na kuwambwa msalabani akiwa uchi na kufa msalabani na kuzikwa mahali
pa giza nene, kaburi lake na mateso yake yalikuwa ni alama ya aibu, kifo, na
kushindwa katika macho ya wanadamu, wanadamu wakikuchukia ni kawaida yao
kukuweka shimoni
-
Walimuweka Yusufu katika shimo la matope Mwanzo 37:18-24 “Wakamwona
toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue.
Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende,
tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla;
kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake. Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono
yao, akasema, Tusimwue. Reubeni akawaambia, Msimwage damu; mtupeni katika
birika hii iliyopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika mikono
yao, akamrudishe kwa baba yake. Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua
Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa katika
birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji.”
-
Walimuweka Yeremia katika shimo la matope Yeremia 38:6-9 “Basi
wakamtwaa Yeremia, wakamtupa katika shimo la Malkiya, mwana wa mfalme, lililo
katika uwanda wa walinzi; wakamshusha kwa kamba. Na mle shimoni hamkuwa na
maji, ila matope tu; naye Yeremia akazama katika matope hayo. Basi, Ebedmeleki,
Mkushi, towashi, aliyekuwa katika nyumba ya mfalme, aliposikia kama wamemtia
Yeremia shimoni; na wakati huo mfalme alikuwa amekaa katika lango la Benyamini;
Ebedmeleki akatoka nyumbani mwa mfalme, akamwambia mfalme, akisema,Ee bwana
wangu, mfalme, watu hawa wametenda mabaya katika mambo yote waliyomtenda
Yeremia, nabii, ambaye wamemtupa shimoni; naye hakosi atakufa pale alipo, kwa
sababu ya njaa; kwa kuwa hapana mkate kabisa katika mji.”
-
Walimtupa Daniel katika shimo lenye simba wakali Daniel 6:16-17 “Basi
mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa katika tundu la simba.
Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya.
Likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu; naye mfalme akalitia muhuri
kwa muhuri yake mwenyewe, na kwa muhuri ya wakuu wake, lisibadilike neno lo
lote katika habari za Danieli.”
Wote waliowekwa shimoni hapo juu
walichukiwa, walikataliwa walifanyiwa hila na njama ili ikiwezekana waweze
kumalizwa na wasitoke lakini Mungu alikuwa pamoja nao, Daudi pia aliishi
mashimoni yaani katika mapango akitafutwa
kuuawa, Yesu Kristo aliwekwa kwenye shimo yaani kaburi, na liliwekwa Muhuri
kama la Daniel wote walikuwa wanakabiliwa na mauti, walikandamizwa, walionewa,
waliteswa Neno la Mungu linaonyesha ya kuwa ni Mungu mwenyewe ndiye aliyewatoa
kutoka katika shimo la uharibifu kama mwandishi wa Zaburi anavyosema
Zaburi 40:1-3 “Nalimngoja Bwana kwa saburi,
Akaniinamia akakisikia kilio changu. Akanipandisha toka shimo la uharibifu,
Toka udongo wa utelezi; Akaisimamisha miguu yangu mwambani, Akaziimarisha hatua
zangu. Akatia wimbo mpya kinywani mwangu, Ndio sifa zake Mungu wetu. Wengi
wataona na kuogopa, Nao watamtumaini Bwana”
Wakati wa shida yako unapopita
katika shimo la uharibifu unaweza kuliitia jina la Bwana naye atakuokoa kutoka
shimoni uwezo huo na mamlaka hiyo ya kumtoa mtu kutoka shimoni iko mikononi mwa
Mungu, Mwandishi wa zaburi alikuwa katika wakati mgumu aliliitia jina la Bwana
na Mungu akikuwa kimya kwa Muda lakini baadae alimchungulia na kisha akamtoa
akaimarisha hatua zake, akamuweka juu ya mwamba na kisha akatia wimbo mpya, ni
maombi yangu pasaka hii iwe ushuhuda
Ayubu 33:23-24 “Kwamba akiwapo malaika
pamoja naye, Mkalimani, mmoja katika elfu, Ili kumwonyesha binadamu hayo
yampasayo; Ndipo amwoneapo rehema, na kusema, Mwokoe asishuke SHIMONI; Mimi
nimeuona ukombozi.”
Ayubu 33:28-30 “Yeye ameikomboa nafsi yangu
isiende SHIMONI, Na uhai wangu utautazama mwanga. Tazama, hayo yote ni Mungu
anayeyafanya, Mara mbili, naam, hata mara tatu, kwa mtu, Ili kurudisha roho
yake itoke SHIMONI, Ili atiwe mwanga kwa mwanga wa walio hai.”
Yona 2:5-6 “Maji yalinizunguka, hata
nafsini mwangu; Vilindi vilinizunguka; Mwani ulikizinga kichwa changu;
Nalishuka hata pande za chini za milima; Hiyo nchi na mapingo yake yalinifunga
hata milele; Lakini umeipandisha nafsi yangu kutoka SHIMONI, Ee Bwana, Mungu
wangu,”
Zaburi 103:3-4 “Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako na KABURI, Akutia taji ya
fadhili na rehema,”
Mamlaka ya kupandishwa toka shimoni
Zaburi 40:1-3 “Nalimngoja Bwana kwa saburi,
Akaniinamia akakisikia kilio changu. Akanipandisha toka shimo la uharibifu,
Toka udongo wa utelezi; Akaisimamisha miguu yangu mwambani, Akaziimarisha hatua
zangu. Akatia wimbo mpya kinywani mwangu, Ndio sifa zake Mungu wetu. Wengi
wataona na kuogopa, Nao watamtumaini Bwana”
Mwandishi wa Zaburi hii yaani
Daudi anaonyesha ya kuwa hakuna mwingine anayeweza kumtoa mtu katika shimo la
uharibifu isipokuwa Bwana mwenyewe kwa hiyo anasema alimgoja Bwana kwa
uvumilivu yaani kwa Saburi, ukombozi wetu unaanza pale tunapoliitia jina la
Bwana na kuvumilia yeye ndiye mwenye mamlaka ya kukuchomoa kutoka katika shimo
lenye matope, lenye utelezi, yeye anayo mamlaka ya kukutoa katika minyororo, na
mazingira yoyote magumu na kubadilisha yale yasiyowezekana na yakawezekana,
Hakuna shimo lolote ambalo linaweza kuwa refu kuliko mkono wa Mungu, Mungu anapokutoa
hukuweka juu ya mwamba na kuimarisha hatua zako na kukupa ushuhuda mpya wimbo
mpya na kila mtu atajifunza kutoka kwako na watu watamtumaini na kumtegemea
Mungu, shimo lolote la kushindwa, shimo la dhambi, shimo la mauti, shimo la
kukata tamaa, shimo mateso, shimo la madeni, shimo la uharibifu, shimo la aibu,
na changamoto.
Katika jina la Yesu Kristo,
mwenye mamlaka ya mauti na uzima, mwenye ufunguo wa Daudi naamuru kila mmoja
aliyewekwa katika shimo la uharibifu shimo hilo likuachie haraka, shimo la
mapepo, shimo la uchawi, shimo la madeni, shimo la kukataliwa, shimo la
kusalitiwa, shimo la kuonewa, shimo la
mafarakano, shimo la talaka, shimo na uharibifu katika ndoa, shimo la uharibifu
katika familia, shimo la utumwa
wadhambi, shimo la magonjwa sugu, shimo la uonevu naamuru katika jina la Yesu
Kristo aliyefufuka kutoka kwa wafu, kila shimo lililokumeza likutapike
likuachie katika jina la Yesu Kristo wa Nazareth aliye hai, Bwana akuchomoe
katika shimo la matope kama Mchungaji anavyomchomoa Kondoo wake katika jina la
Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai Amen!
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni