Zaburi 118:10-14. “Mataifa yote walinizunguka; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali. Walinizunguka, naam, walinizunguka; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali. Walinizunguka kama nyuki, Walizimika kama moto wa miibani; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali. Ulinisukuma sana ili nianguke; Lakini Bwana akanisaidia. Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu, Naye amekuwa wokovu wangu.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa katika
maisha yetu wakati mwingine tunaweza kujikuta tumezungukwa na shinikizo la
vitisho kutoka kila upande wa maisha yetu, unaweza kuzingirwa na mazingira
hatarishi ya vita kutoka kila pembe ya maisha yako, unaweza kuzingirwa na
shinikizo la upweke, shinikizo la kukosa afya, shinikizo la afya ya akili,
shinikizo la kifedha na kiuchumi, shinikizo la hofu ya changamoto za kazini,
shinikizo la matukio ya kutisha na kuumiza moyo, shinikizo la mabadiliko katika
maisha, malezi, ndoa, na kadhalika hizi zote zinaweza kuwa hali zinazokusukuma
ili ukate tamaa na kuvunjika moyo, na kuzungukwa na hofu za kifo, lakini Neno
la Mungu leo linatukumbusha kuwa Bwana atakusaidia, yeye ni nguvu na wokovu,
atakuwa msaada mkubwa kwetu tutakapoliitia jina lake atatusikia na atatuitikia
kwa wingi wa neema na rehema zake.
Zaburi 116:1-5 “Haleluya. Nampenda Bwana
kwa kuwa anaisikiliza Sauti yangu na dua zangu. Kwa maana amenitegea sikio
lake, Kwa hiyo nitamwita siku zangu zote. Kamba za mauti zilinizunguka, Shida
za kuzimu zilinipata. Naliona taabu na huzuni; Nikaliitia jina la Bwana. Ee
Bwana, nakuomba sana, Uniokoe nafsi yangu. Bwana ni mwenye neema na haki, Naam,
Mungu wetu ni mwenye rehema.”
Mungu atakuwa msaada wako wewe na
mimi tunapokuwa katika mashinikizo ya maisha haya, iwe shinikizo la kimwili au
la kiroho Mungu atakusaidia nawe utaufurahia uweza wa Bwana katika kututetea na
kutupigania katika hali yoyote ile unayoipitia usilie wala usikate tamaa
utasaidiwa naye
·
Maana ya
kusukumwa sana.
·
Walinisukuma
sana ili nianguke.
·
Nguvu za
Mungu wakati wa kusukumwa.
Maana ya kusukumwa sana.
Zaburi 118:12-13 “Walinizunguka kama nyuki,
Walizimika kama moto wa miibani; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.
Ulinisukuma sana ili nianguke; Lakini Bwana akanisaidia.”
Kimsingi kifungu hiki cha
maandiko kinaonyesha kuwa Mwandishi alikuwa amezingirwa na majeshi ya mataifa
mbalimbali na kumuwekea shinikizo kubwa kutoka kila upande ili waweze kumshinda
lakini aliwakatilia mbali kwa jina la Bwana na kuwashinda, Kimsingi maadui
walimsonga sana ili ikiwezekana ashindwe na kumalizwa lakini Bwana alimsaidia.
Kwa asili maneno Ulinisukuma sana
ili nianguke; lakini Bwana akanisaidia yanapaswa kusomeka hivi Walinisukuma sana
ili nianguke Lakini Bwana akanisaidia, hii ni kwa sababu maadui waliokuwa
wakimsonga walikuwa ni wengi na sio mmoja na ukweli huo unaweza kuthibitishwa
na matoleo mengine ya Biblia kwa mfano Biblia za kiingereza zifuatazo
zinaonyesha kuwa neno hili lilipaswa kuwa katika wingi “Walinisukuma” na sio katika umoja “Ulinisukuma” angalia kwa makini English
Christian Standard Bible inasema hivi “They pushed me hard to make me fail but
the Lord helped me”
Contemporary English Version inasema hivi “Their attacks were so fierce that I
nearly fell, but the Lord helped me”
New International Version inasema hivi “I was pushed back and about to fall, but
the Lord helped me”
God’s word translation inasema hivi “They pushed hard to make me fall, but the
Lord helped me”
Unapoangalia asili ya kifungu kizima
utaweza kugundua kuwa mwandishi alikuwa akizungumzia kwa wingi, wingi wa
maadui, wingi wa mataifa, wingi wa mashinikizo ya changamoto na majaribu ya kufutiliwa mbali na maadui na
kwa msaada wa Mungu aliwakatilia mbali maadui zake kumbuka walikuwa wengi kama
nyuki lakini aliwateketeza kama moto wa miiba, sasa hebu tuangalie maana ya
kusukumwa, Neno kusukumwa katika lugha ya Kiebrania linasomeka kama “dâchâh dâchach”
linalosomeka kwa sauti “daw-khaw” ambalo
kwa kiingereza linasomeka kama
“outcast” ambapo maelezo yake ni someone who is rejected or cast out, as
from home or society or some way excluded, looked down upon or ignored kwa
tafasiri ya Kiswahili ni mtu
aliyekataliwa na jamii, aliyefukuzwa nje ya nyumbani au katika jamii, mtu aliyeonekana
kuwa hana maana wa kudharaulika, asiyefaa kwa lolote asiye na mchango wowote, kwa
hiyo mwandishi alikuwa ni mtu aliyekataliwa, aliyefukuzwa na anayewindwa na
maadui kila upande auawe huku akiwa katika mashinikizo mbalimbali yanayomkabili
kila upande kiroho na kimwili kiakili na kisaikolojia kwa ujumla alikuwa kama
anazidiwa kiasi cha kukaribia kuzimia au kushindwa, maadui hawakutaka awe na
utulivu kila wakati walimchokoza na kumsumbua na walitaka kuhakikisha
anatokomea huko huko shimoni, hata hivyo mwandishi aliwashinda adui zake wote
na hatimaye alirudi katika jamii na kuwa mtu mkubwa sana, Jambo ambalo
liliwashangaza watu wote, Mateso haya yalimpata Daudi kimsingi
Zaburi 118:22-23 “Jiwe walilolikataa waashi
Limekuwa jiwe kuu la pembeni. Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu
machoni petu.”
Walinisukuma sana ili nianguke.
Kimsingi zaburi hii iliandikwa na
Daudi kutokana na maisha aliyoyapitia, lakini kwa vile mtu huyu alikuwa nabii
alikuwa pia anazungumza kwa niaba ya Israel, Yesu Kristo pamoja na wewe na mimi,
Israel ni Taifa ambalo linaonelewa na kuchukiwa na jamii ya kimataifa sana, ni
taifa ambalo adui zake wanatamani walifute lisiwepo, linazingirwa na watu
wanaolichukia kutoka kila upande, hata sasa tunapozungumza Israel iko katika
vita na baadhi ya nchi za kiarabu na vikundi vya kigaidi wote wakipeleka
shinikizo ili ikiwezekana waweze kuwafuta, Israel inachukiwa na Hamas (Harakat
al-Muqawama al-Islamiya au Islamic Resistance Movement) hiki ni chama cha siasa
nan a Jeshi la waislamu wa Sunni walioko Palestina Eneo la Ukanda wa Gaza, Lengo
lao likiwa ni kufutilia mbali wayahudi kokote duniani, Inachukiwa na Hezbollah
(Hezb Jeshi au chama Allah- Mungu) Chama cha Mungu au Jeshi la Mungu hawa
walioko Lebanon wakisaidiwa na Iran neno Hezbollah maana yake chama cha Allah
lengo lao kuu ni kuiangamiza Israel hili ni kundi la kigaidi la Washiha, Israel
inachukiwa na Iran ambao wanaiona Israel kama kansa ambayo inatakiwa kufutwa,
wanapambana na mamlaka ya Palestina huko ukanda wa Magharibi, inashambuliwa na
kundi la wa Houthis hawa wanaitwa Ansar Allah ni tawi la Madhehebu ya Shiha
(Shiite) ambao wako Yemen wanaoungwa mkono na Iran, kila mahali kuna shinikizo
na yote yanalenga kuwamaliza watu wa Mungu, Daudi kama nabii anaiona Israel
kuwa watasaidiwa na Mungu na pamoja na mashinikizo yanayowakabili kama yeye
alivyozingirwa na maadui Mungu ataandaa meza machoni pa watesi wetu.
Zaburi 23:4-5. “Naam, nijapopita kati ya
bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa
watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika.”
Aidha unabii huu pia unamhusu
Yesu Kristo, ambaye naye alikataliwa na jamii na kukatiliwa mbali na watu wake
na kuteswa vibaya walimsukumia mbali hata katika shimo la mauti lakini Mungu
alimfufua kutoka kwa wafu, Yesu huyu atakuja tena na kuwa mtawala wa ulimwengu
wakati wa utukufu pale Israel litakapokuwa taifa kubwa litakaloitawala Dunia
mfalme wake atakuwa ni Yesu
Isaya 53:3-5 “Alidharauliwa na kukataliwa
na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu
humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua
masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa,
Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa
kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake
sisi tumepona.”
Unabii huu pia unakuhusu wewe na
mimi, Shetani anatuchukia bure anafanya mashambulizi kupitia watu na mapepo
anatushinikiza kila sehemu na kila mahali kwaajili ya kumpenda Mungu tumekuwa
na maadui kila mahali, kwaajili ya kumtumikia Mungu tunachukiwa lakini
tunakumbushwa na zaburi hii ya kuwa Mungu hatatuacha hivi hivi hatimaye atakuja
kutusaidia nasi tutatawala pamoja na Bwana wetu Yesu Kristo katika ufalme wake!
Mwandishi anatumia lugha picha
kuonyesha bidii na juhudi za maadui dhidi yetu wanasukuma sana wanajitahidi
wana hasira, lakini hata hivyo kwa msaada wa Mungu maadui walishughulikiwa
mmoja baada ya mwingine kwa kukatiliwa mbali kwa jina la Bwana tunaweza kuwa na
maadui wa kimwili, maadui wa kiroho na maadui wa maisha yaani masumbufu ya
maisha haya na yanaweza kutuletea shinikizo za namna mbalimbali lakini kwa
mujibu wa mwandishi ni kuwa Bwana atatusaidia.
Tunaweza kusukumwa na watu
kupitia chuki zao, wivu, kejeli au vitendo vya kutukatisha tamaa, mambo haya
yanaweza kufanywa na wenzetu, majirani na hata wanafamilia wanaweza kutusukuma
kwa maneno au kwa vitendo, Yusufu alitupwa shimoni alitendwa vibaya lakini
Mungu alimsaidia.
Mwanzo 49:22-25 “Yusufu ni mti mchanga
wenye kuzaa, Mti mchanga wenye kuzaa karibu na chemchemi, Matawi yake yametanda
ukutani. Wapiga mishale walimtenda machungu, Wakamtupia, wakamwudhi, Lakini
upinde wake ukakaa imara, Mikono yake ikapata nguvu, Kwa mikono ya Mwenye Enzi
wa Yakobo; Kwa jina la mchungaji, yeye jiwe la Israeli, Naam, kwa Mungu wa baba
yako atakayekusaidia; Kwa mibaraka ya mbinguni juu. Mibaraka ya vilindi vilivyo
chini, Mibaraka ya maziwa, na ya mimba.”
Tunaweza kusukumwa wakati
mwingine na hali mbaya ya maisha, ugumu wa maisha kutokumudu hali ngumu ya
maisha umasikini, magonjwa makali, kushindwa au hasara za kifedha, zote
zionaweza kutumika kama misukumo inayokugandamiza ili uanguke, unaweza
kusukumwa na upinzani wa nguvu za giza, nguvu za mashetani kusukumwa na hofu,
woga na mashaka au majaribio ya kuachana na imani, mifumo ya dunia ya uchumi na siasa yote yanaweza kukufanya
ukawa katika shinikizo ambalo linalenga kukuangusha vyote hivi vinalenga
kukusukuma ili uanguke lakini Mungu ndiye msaada wetu, Mungu wetu yuko pamoja
nasi, Mungu wetu atatusaidia hatakuacha uaibike!
Zaburi 124:1-8 “Kama si Bwana aliyekuwa
pamoja nasi, Israeli na aseme sasa, Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi,
Wanadamu walipotushambulia. Papo hapo wangalitumeza hai, Hasira yao ilipowaka
juu yetu. Papo hapo maji yangalitugharikisha, Mto ungalipita juu ya roho zetu;
Papo hapo yangalipita juu ya nafsi zetu Maji yafurikayo. Na ahimidiwe Bwana;
Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao. Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika
mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka. Msaada wetu u katika jina
la Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.”
Nguvu za Mungu wakati wa kusukumwa.
Neno la Mungu linaonyesha wazi
kuwa wakati watu, maisha na shatani anapoifanya kazi ya kutusukuma ili
tushindwe kumbe Mungu ananyoosha mkono wake kutusaidia hiki ndicho anachokishuhudia
mwandishi wa zaburi, na kutukumbusha kuwa msaada wetu uko kwa Mungu yeye ndiye
anayetusaidia hataacha tuanguke, wala hataacha tuzimie hasinzii wala halali
atafanya kitu tu
Zaburi 118:10-14. “Mataifa yote
walinizunguka; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali. Walinizunguka, naam,
walinizunguka; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali. Walinizunguka kama nyuki,
Walizimika kama moto wa miibani; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.
Ulinisukuma sana ili nianguke; Lakini Bwana akanisaidia. Bwana ni nguvu zangu
na wimbo wangu, Naye amekuwa wokovu wangu.”
Isaya 41:10-13 “usiogope, kwa maana mimi ni
pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam,
nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote
walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe
watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe;
watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu
yako. Kwa maana mimi, Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume,
nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia.”
Yeremia 1:18-19 “Maana, tazama, nimekufanya
leo kuwa mji wenye boma, na nguzo ya chuma, na kuta za shaba, juu ya nchi yote;
juu ya wafalme wa Yuda, na juu ya wakuu wake, na juu ya makuhani wake, na juu
ya watu wa nchi hii. Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi
nipo pamoja nawe, asema Bwana, ili nikuokoe.”
Haijalishi kuwa maisha yako
yanazingirwa na mashinikizo ya namna gani lakini kila mahali Mungu yuko na
atakusaidia, watu wanaweza kuinuka kinyume nawe, hali inaweza kuinuka kinyume
nawe, mazingira yanaweza kuwa kinyume nawe, wakuu wa dini wanaweza kuwa kinyume
nawe, lakini Mungu atakuwa msaada mkubwa kwako yeye atakufanya wewe kuwa mji
wenye boma, na nguzo ya chuma na ukuta wa shaba maana yake Mungu
anakuhakikishia kuwa huwezi kuvamiwa pamoja na mashinikizo ya upinzani na
vitisho vya kila aina wewe katika yeye ni Mshindi na zaidi ya kushinda,
haijalishi nani wanakusukuma ili uangamie, nani anakuusukuma ili uanguke kwa
jina la Bwana watakatiliwa mbali katika jina la Yesu Kristo Mwana wa Mungu
aliye hai
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni