Zaburi 40:11-13 “Nawe, Bwana, usinizuilie
rehema zako, Fadhili zako na kweli yako na zinihifadhi daima. Kwa maana mabaya
yasiyohesabika Yamenizunguka mimi. Maovu yangu yamenipata, Wala siwezi kuona. Yamezidi
kuliko nywele za kichwa changu, Na moyo wangu umeniacha. Ee Bwana, uwe radhi
kuniokoa, Ee Bwana, unisaidie hima.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kwamba kuna
nyakati katika maisha yetu ambapo mtu unaweza kujikuta katikati ya matatizo
mengi kwa wakati mmoja, Kibiblia hali hiyo sio ngeni na kama unakutana na hali
kama hiyo wewe sio wa kwanza, Mwandishi wa zaburi hii anaelezea naye hali
halisi ya mambo yaliyomkuta, akiwa katika mashinikizo ya changamoto zaidi ya
moja anazungukwa na mabaya yasiyohesabika na kutusaidia sisi kuelewa njia ya
kufuata na kufanya wakati tunapozungukwa na mabaya yasiyohesabika, usifikiri
wakati wowote kuwa labda una laana au una nuksi au Mungu anapatiliza makosa na
dhambi zako hapana, ziko nyakati tu katika maisha ya mwanadamu inaweza kutokea
ukapita katika hali kama hiyo na hayo ni mambo ya kawaida na wala hupaswi
kukata tamaa
2Wakorintho 4:8-10 “Pande zote twadhikika,
bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi;
twatupwa chini, bali hatuangamizwi; siku zote twachukua katika mwili kuuawa
kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu.”
Unaona mtume Paulo anaeleza
pamoja na kuwa mtu wa Mungu lakini walikuwa wakizungukwa na mabaya
yasiyohesabika yeye anaeleza kwa lugha nyingine kuwa twadhikika pande zote,
twaona shaka, twaudhiwa, twatupwa lakini hawakati tamaa, hawasongwi,
hawazidiwi, hawaangamizwi wala Mungu hawaachi, kuwa mtu wa Mungu au kuwa katika
agano na Mungu haimaanishi kuwa na maisha mepesi, iangalie Israel katika
ulimwengu wa kimwili ina picha halisi katika ulimwengu wa kiroho sawa na yale
unayoyapitia, wanashambuliwa na Hezibollah, (Washiha wenye siasa kali)
wanashambuliwa na Hamas (Wasuni wenye siasa kali), wanashambuliwa na Houthis
(Wa Ansar wenye siasa kali) wanashambuliwa na Palestinian Islamic Jihad hawa
wote wanafanya mauaji, wanateka watu, wanalipua mabomu, wanarusha maroketi na
makundi haya yote ya kigaidi yanafadhiliwa na taifa Fulani lenye uchumi mzuri, jambo linalowafanya wasiishi kwa amani ni
ukweli ulio wazi bila mkono wa Mungu Israel isingeliweza kusimama, halikadhalika
watu wa Mungu kila upande unashambuliwa na adui yetu shetani na hili ni swala
la kawaida katika maisha ya watu wa Mungu hupaswi kuogopa, kwa sababu
halitadumu, Leo basi tutachukua muda
kujifunza somo hili Kuzungukwa na mabaya yasiyohesabika! Kwa
kuzingatia vipengele muhimu vitatu vifuatavyo:-
·
Kuzungukwa na mabaya yasiyohesabika.
·
Mambo ya kufanya unapozungukwa na mabaya
yasiyohesabika.
·
Msaada wa Mungu wakati unazungukwa na mabaya
yasiyohesabika.
Kuzungukwa na mabaya yasiyohesabika
Neno mabaya yasiyohesabika katika lugha ya asili
ya Kiebrania yanasomeka “Ra’ot ein
mispar” katika muunganiko huo wa maneno au misamiati miwili ya Kiebrania
tunapata neno “Ra’ot” ambalo maana
yake kwa kiingereza “trouble” au “evils” kwa Kiswahili ni mabaya, maovu,
shinikizo, changamoto au matatizo na neno “Ein
Mispar” ambalo maana yake “countless”, au “without number” yasiyohesabika, yasiyo na idadi, kwa hiyo neno “Ra’ot ein mispar” linapounganishwa
pamoja kwa kiingereza unapata neno “countless
troubles” au “evil without numbers” maana yake ya kina ni kuwa mtu anayepitia
matatizo mengi mfululizo au matatizo mengi kwa wakati mmoja, au changamoto
zisizoweza kuhesabika au kujulikana zinaisha lini, mtu anayepitia mashinikizo
kutoka pande zote hali hii inapompata mwanadamu kimsingi unaweza kukata tamaa
na unazidiwa nguvu unajiuliza kimsingi
unawezaje kutoka katika hali hiyo kama ni magonjwa unajihisi mauti inakuzunguka
kila upande mtu unaweza kupitia changamoto nyingi mpaka ukajiuliza kichwani nimekanyaga
wapi, wakati Ayubu, Yeremia na Yona wanapitia
hali kama hii ya kuzungukwa na mabaya yasiyohesabika wao kwa nyakati tofauti tofauti walisema:-
Ayubu 19:8-10 “Yeye ameiziba njia yangu
nisipate kupita, Na kutia giza katika mapito yangu. Amenivua utukufu wangu, Na
kuiondoa taji kichwani mwangu. Amenibomoa pande zote, nami nimetoweka; Na
tumaini langu ameling'oa kama mti.”
Maombolezo 3:1-7 “Mimi ni mtu aliyeona
mateso Kwa fimbo ya ghadhabu yake. Ameniongoza na kuniendesha katika giza Wala
si katika nuru. Hakika juu yangu augeuza mkono wake Mara kwa mara mchana wote.
Amechakaza nyama yangu na ngozi yangu; Ameivunja mifupa yangu. Amejenga boma
juu yangu, Na kunizungusha uchungu na uchovu. Amenikalisha penye giza, Kama
watu waliokufa zamani. Amenizinga pande zote hata siwezi kutoka; Ameufanya
mnyororo wangu mzito.”
Yona 2:3-5 “Maana ulinitupa vilindini,
Ndani ya moyo wa bahari; Gharika ya maji ikanizunguka pande zote; Mawimbi yako
yote na gharika zako zote zimepita juu yangu. Nami nikasema, Nimetupwa mbali na
macho yako; Lakini nitatazama tena kukabili hekalu lako takatifu. Maji
yalinizunguka, hata nafsini mwangu; Vilindi vilinizunguka; Mwani ulikizinga
kichwa changu;”
Wenzetu hawa kwa nyakati tofauti
tofauti kama ilivyokuwa kwa Daudi mwandishi wa zaburi tunayoitafakari walipitia
katika nyakati za kuzungukwa na mabaya yasiyohesabika, kwa hiyo kuzungukwa na
mabaya sio jambo geni kwa watakatifu na watu wa Mungu ni hali ya kimaandiko na
tunajifunza hivyo kutoka katika maandiko kila mtu wa Mungu anaweza kupitia.
Mpendwa je wewe unazungukwa na mabaya yasiyohesabika pande zote? Watu wa Mungu katika maandiko walipitia, je
unapopita katika hali kama hiyo unafanyaje? Wenzetu walifanyaje? Yako mambo ya
kufanya
Mambo ya kufanya unapozungukwa na mabaya yasiyohesabika
Zaburi 40:11-13 “Nawe, Bwana, usinizuilie
rehema zako, Fadhili zako na kweli yako na zinihifadhi daima. Kwa maana mabaya
yasiyohesabika Yamenizunguka mimi. Maovu yangu yamenipata, Wala siwezi kuona.
Yamezidi kuliko nywele za kichwa changu, Na moyo wangu umeniacha. Ee Bwana, uwe
radhi kuniokoa, Ee Bwana, unisaidie hima.”
Tunajifunza kutoka katika andiko
la Msingi wakati wenzetu walipozungukwa na mabaya yasiyohesabika hawakulaumu
mtu wala hawakutafuta mchawi wala sababu au kufikiri kuwa wamerogwa na badala
yake WALIOMBA usinizuilie rehema
maana yake waliomba rehema, fadhili zako zinihifadhi daima walitafuta fadhili
za Bwana, walimueleza Mungu wazi wazi kuwa changamoto hizi zimewazidi,
walieleza moyo umekufa ganzi, na waliomba msaada wa Mungu, kilio cha mtu
anayezungukwa na mabaya humfanya Mungu aingilie kati sawasawa na ahadi zake
katika neno lake
Zaburi 50:15 “Ukaniite siku ya mateso;
Nitakuokoa, na wewe utanitukuza.” Kwa hiyo neno la Mungu linaonyesha
kuwa kila aliyezungukwa na mabaya
yasiyohesabika aliliitia jina la Bwana katika taabu yake na Bwana akasikia na
kuwaokoa, sisi nasi tukiliitia jina la Bwana Mungu atasikia na kujibu
Pamoja na maombi na kulia na
kumimina mioyo yao mbele za Mungu watakatifu waliotutangulia WALIMTUMAINI Bwana, hapo tunajifunza
kuwa walitambua kuwa hakuna mwingine anayeweza kuwasaidia isipokuwa Mungu, hii
ni kwa sababu ni kawaida kibinadamu kufikiria mtu wa kukusaidia unapopita
katika changamoto fulani fulani lakini lakini wanadamu wanaweza kutumiwa
kukuletea shinikizo kubwa zaidi wakati wa changamoto zako hivyo omba kisha weka
tumaini lako kwa Bwana
Mithali 3:3-6 “Rehema na kweli zisifarakane
nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako. Ndivyo
utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu.
Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.”
Zaburi 56:1-4 “Mungu, unirehemu, maana yuko
atakaye kunimeza, Mchana kutwa ananionea akileta vita. Adui zangu wanataka
kunimeza mchana kutwa, Maana waletao vita juu yangu kwa kiburi ni wengi. Siku
ya hofu yangu nitakutumaini Wewe; Kwa msaada wa MUNGU nitalisifu neno lake.
Nimemtumaini Mungu, sitaogopa; Mwenye mwili atanitenda nini?”
Msaada wa Mungu wakati unazungukwa na mabaya yasiyohesabika
Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu
huwa pamoja na wale wanaopitia au kuzungukwa na mabaya yasiyohesabika, na hatakuacha
uangamie Paulo anaeleza kuwa twazikika pande zote lakini hatuangamii kwa nini
Paulo anasema kuwa hatutaangamia hata tupitapo katika changamoto nzito?
2Wakorintho 4:8-10 “Pande zote twadhikika,
bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi;
twatupwa chini, bali hatuangamizwi; siku zote twachukua katika mwili kuuawa
kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu.”
1. Bwana huwa Karibu ili kuokoa na kuponya - Zaburi 34:19 “Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.”
2. Bwana atakuwa pamoja nawe na atakupa watu - Isaya 43:2-4 “Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza. Maana mimi ni Bwana, Mungu wako; Mtakatifu wa Israeli, mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa Kushi na Seba kwa ajili yako. Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako.”
3. Bwana atafanya mlango wa kutokea - 1Wakorintho 10:13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.”
4. Bwana atakusaidia Isaya 41:10-13 “usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi, Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia.”
5.
Bwana
atakupa hatima iliyo njema – Yakobo 5:10-11 “Ndugu,
watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya,
na wa uvumilivu. Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya
subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema,
mwenye huruma.”
Hitimisho
Ndugu zangu kaka zangu na dada
zangu kuzungukwa na mabaya yasiyohesabika sio mwisho wako ni hatua ya Mungu
kukupeleka katika kiwango kingine ni daraja tu ni mlango wa miujiza mikubwa
Bwana hatakuacha uzidiwe ataleta msaada wake haraka, hauna sababu ya kulia au
kulalamika au kukata tamaa najua wakati unapozungukwa na mabaya yasiyohesabika
ni wakati ambapo kila kitu kinakatisha tamaa ni wakati ambapo unaweza kupoteza
tumaini lakini neno la Mungu limetutia moyo ya kuwa Mungu hatatuacha atatuokoa
na kutuponya, atakuwa pamoja nawe na atatoa watu wakusaidie, atafanya mlango wa
kutokea, atakuwa pamoja nawe hakuna kitu kitakachoweza kusimama mbele yako, yeye
atakusaidia na kukupa mwisho ulio mwema jambo kubwa la msingi ni kusimama na
kuuona wokovu wa Bwana, Kama Mungu anavyowasaidia Israel na kuwalinda na
kuwatetea pamoja na kuzingirwa na wabaya wasiohesabika kila upande lakini Mungu
haogopi atakuandalia meza katikati ya watesi wako
Kutoka 14:13-14 “Musa akawaambia watu,
Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana
hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi,
nanyi mtanyamaza kimya.”
Wimbo: “Roho wa Bwana twakualika utawale, Karibu Roho, fanya mapenzi ya
Bwana”
Na. Rev. Innocent
Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi
mwenye Hekima

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni