Isaya 53:2-5 “Maana alikua mbele zake kama
mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na
tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu
wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao,
Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu,
Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu,
na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu;
Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”
Utangulizi:
Leo ni siku ya Ijumaa kuu!
Wakristo wote Nchini wanaungana na wakristo wote duniani kukumbuka na
kuadhimisha kuteswa, kusulubiwa na kufa msalabani kwa Yesu Kristo wa Nazareth
kulikotokea huko nje ya Yerusalem Israel miaka zaidi ya 2000 iliyopita, Katika kujikumbusha tukio hilo kama
lilivyotabiriwa na Nabii Isaya zaidi ya miaka 700 kabla ya kuzaliwa kwake, Mateso yake haya yalifanyika dhidi
yake huku akiwa hakufanya kosa lolote, lakini maandiko yanaeleza kuwa yalimkuta
hayo kwaajili ya uponyaji wa wanadamu kwa sababu imeandika kwa kupigwa kwake
sisi tumepona
1Petro 2:22-24 “Yeye hakutenda dhambi, wala
hila haikuonekana kinywani mwake. Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano;
alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki. Yeye
mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa
mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa.”
Kwa msingi huo basi leo
tutachukua muda kutafakari na kujifunza kwa kina somo hili “HANA UMBO WALA UZURI HATA TUMTAMANI” kwa
kuzingatia vipengele vikuu vitatu muhimu vifuatavyo:-
·
Maana ya neno hana umbo wala uzuri hata
tumtamani
·
Yeye hana umbo wala uzuri hata tumtamani
·
Faida ya Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo
Maana ya neno hana umbo wala uzuri hata tumtamani.
Ni muhimu kufahamu kuwa nabii
Isaya alitabiri kuhusu mateso ya Yesu Kristo miaka 700 kabla ya Kristo kuzaliwa na hatimaye unabii wake ulikuja
kutimizwa, akimuona katika kioo cha kinabii Isaya anasema kuhusu Masihi katika
mateso yake “Yeye hana umbo wala uzuri;
Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani.” Maneno haya yana maana gani sasa
hebu tuyarejee tena.
Isaya 53:2 “Maana alikua mbele zake kama
mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na
tumwonapo hana uzuri hata tumtamani.”
Maneno haya hayamaanishi kamwe
kuwa Yesu hakuwa mzuri au hakuwa na mvuto wa kimwili hapana Yesu alikuwa mzuri
sana na kijana mwenye mvuto wa kupita kawaida, lakini Isaya anamuona katika
kipindi cha mateso yake Yesu akiwa ameharibiwa vibaya na kuchakazwa katika
sehemu zote muhimu za mwili wa kibinanadamu, Neno la Kiebrania linalotumika
kuelezea umbo ni “tô’ar” na uzuri ni “Hâdâr”
ambayo kwa kiingereza ni “appearance”
na “majesty” maana yake ni kuwa
mwili wake uliharibiwa vibaya sana “disfigured” na heshima yake au utukufu
wake ulidhalilishwa na kushushwa kupita maelezo “dishonoured” kwa hiyo Isaya
ni kama anaelezea kuwa wakati wa mateso yake Yesu Kristo hakuna mtu angeweza
kutamani kumuona, mateso yale yaliharibu kabisa muonekano wake na yalidhalilisha kabisa utu wake, hakuwa na
utukufu wa kifalme, wala huwezi kutamani kumuona na kwa sababu hiyo alidharauliwa sana, Mateso yake yalikuwa kama njia ya
kumvunjia heshima na kumdhalilisha kabisa na kuharibu heshima yake
waliomsulubisha sio tu walikuwa na uwepo wa kishetani lakini pia walimuonea
wivu kutokana na uzuri aliokuwa nao na wakakusudia kuuharibu kwa hiyo chuki za
waliomsulubisha pia na wivu ulihusika katika kuhakikisha kuwa wanamuharibu
kabisa sura yake na kumvunjia kabisa Heshima yake anaelezea mwandishi wa
historia wa kiyahudi wa Karne ya kwanza Flavours
Josephus walitaka kuhakikisha kuwa anakuwa na huzuni na nafasi ya kujisikitikia
Isaya 53:3-4 “Alidharauliwa na kukataliwa
na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu
humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika
ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa
amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.”
Yeye hana umbo wala uzuri hata tumtamani!
Kama tulivyoona maana ya kauli ya
hana umbo wala uzuri hata tumtamani ambayo ina maanisha ule uzuri aliokuwa nao
Yesu Kristo na utukufu wake uliweza kuharibiwa vibaya kiasi ambacho mtu
hangeweza kufikiri kuwa huyu ni mtu au ni mwanadamu yaani aliharibiwa katika
namna ambayo ni ngumu kujua kuwa huyu ni mtu yaani watesi walihakikisha
wanambomoa uso wake na mwili wake na nafsi yake na roho yake maandiko yanaeleza
kuwa aliharibiwa katika kiwango ambacho hakuna mwanadamu aliwahi kuharibiwa
hivyo
Isaya 52:14 “Kama vile wengi
walivyokustaajabia, (uso wake ulikuwa umeharibiwa sana zaidi ya mtu ye yote, na
umbo lake zaidi ya wanadamu),”
Isaya 53:5 “Bali alijeruhiwa kwa makosa
yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na
kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”
Watesi wa Yesu Kristo
walihakikisha kuwa Yesu anateseka kwa namna zote, anateseka kihisia, kimwili,
kijamii, kiroho na kisaikolojia, walimuharibu na kuuchakaza mwili wake kwa
mateso ambayo Biblia inaeleza hakuna mtu alichakazwa kwa mtindo na mfumo kama
aliofanyiwa Yesu, inawezekana filamu ya “Passion
of Christ” ikawa imeonyesha kwa kiwango Fulani uhalisia wa mateso yake, maandiko
yakisema aliharibiwa ujue aliharibiwa kweli!
Kihisia – Yesu alikataliwa na watu wake, alisalitiwa na Yuda
Iskariote, kisha wanafunzi wake walimkimbia na wakati wa mateso alibaki peke
yake, Petro alimkana mara tatu, mateso haya yakiongozwa na uwepo wa kishetani
yalikuwa ni kwaajili ya kusababisha manung’uniko katika moyo wa Yesu apate
maumivu ya kihisia na kudhalilika
Yohana 1:10-11 “Alikuwako ulimwenguni, hata
kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake,
wala walio wake hawakumpokea”
Mathayo 26:14-16 “Wakati huo mmoja wa wale
Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani, akasema, Ni
nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya
fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti.”
Mathayo 26:56 “Lakini haya yote yamekuwa,
ili maandiko ya manabii yatimizwe. Ndipo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.”
Luka 22:59-61 “Halafu, yapata saa moja, mtu
mwingine alikaza kusema, Hakika na huyu alikuwa pamoja naye, kwa kuwa yeye pia
ni Mgalilaya. Petro akasema, Ee mtu, sijui usemalo. Na papo hapo alipokuwa katika
kusema, jogoo aliwika. Bwana akageuka akamtazama Petro. Petro akalikumbuka lile
neno la Bwana jinsi alivyomwambia, Leo kabla hajawika jogoo utanikana mara tatu.”
Kimwili – Maandiko yanaonyesha kuwa mtumishi wa Mungu (Yesu Kristo)
angeteswa katika kiwango ambacho asingeliweza kutambulika, askari wa kirumi
walikuwa kama wenye mzuka au walipagawa lilipokuja swala la mateso ya Kristo,
walimpiga mijeledi mingi katika namna isiyoweza kuhesabika, walimvika taji ya
miiba, huku wakimpiga makofi na kumtemea mate, aliwambwa msalabani akisulubiwa
mikono na miguu, kimsingi hakuna mateso makali kama kusulubiwa msalabani,
lakini kabla ya hilo wanajeshi wa kirumi walishika mijeledi na kumfunga Yesu
kwenye kizimba ambapo unavuliwa nguo na kutandikwa mijeledi, Mijeledi ilikuwa
ni fimbo yenye nyuzi kumi na mbili na zile nyuzi zilikuwa na vipande vya vyuma
na mifupa ya wanyama wagumu, askari wawili wanaume wenye nguvu walitandika kwa
kushindana na wengi waliopitia adhabu hii walichanika tumbo na utumbo
ulimwagika nje, unabii wa Isaya na ule wa Daudi katika Zaburi unathibitisha
hali mbaya ya mateso ya Kristo namna alivyokuwa
Zaburi 22:14-18 “Nimemwagika kama maji,
Mifupa yangu yote imeteguka, Moyo wangu umekuwa kama nta, Na kuyeyuka ndani ya
mtima wangu. Nguvu zangu zimekauka kama gae, Ulimi wangu waambatana na taya
zangu; Unaniweka katika mavumbi ya mauti, Kwa maana mbwa wamenizunguka;
Kusanyiko la waovu wamenisonga; Wamenizua mikono na miguu. Naweza kuihesabu
mifupa yangu yote; Wao wananitazama na kunikodolea macho. Wanagawanya nguo
zangu, Na vazi langu wanalipigia kura.”
Yohana 19:1-3 “Basi ndipo Pilato alipomtwaa
Yesu, akampiga mijeledi. Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia
kichwani, wakamvika vazi la zambarau. Wakawa wakimwendea, wakisema, Salamu!
Mfalme wa Wayahudi! Wakampiga makofi.”
Mathayo 26:67-68 “Ndipo wakamtemea mate ya
uso, wakampiga makonde; wengine wakampiga makofi, wakisema, Ewe Kristo,
tufumbulie; ni nani aliyekupiga? ”
Mathayo 27:29-31 “Wakasokota taji ya miiba,
wakaiweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kuume; wakapiga
magoti mbele yake, wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Kisha
wakamtemea mate, wakautwaa ule mwanzi, wakampiga-piga kichwani. Walipokwisha
kumdhihaki, wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua
kumsulibisha.”
Kijamii - Yesu aliteswa kijamii. Alidhihakiwa hadharani dhidi ya
watu wale waliokuwa wakimuheshimu, alihesabiwa pamoja na wahalifu yeye akiwekwa
kati kati yao, lakini alivuliwa nguo hadharani tukio hili lilikuwa la
udhalilishaji na uaibishaji , jamii
hiyo hiyo wakati wa hukumu yake walipiga kelele wakisema asulubiwe asulubiwe!
Isaya 53:12 “Kwa hiyo nitamgawia sehemu
pamoja na wakuu, Naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari; Kwa sababu
alimwaga nafsi yake hata kufa, Akahesabiwa pamoja na hao wakosao. Walakini
alichukua dhambi za watu wengi, Na kuwaombea wakosaji.”
Yohana 19:23 “Nao askari walipomsulibisha
Yesu, waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu
lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia
tangu juu.”
Kiroho – kwa kuwa alikuwa amezibeba dhambi za ulimwengu mzima, kwa
wakati ule Mungu alikuwa amemuacha, kwa hiyo kwa wakati ule ilikuwa ni kama Mungu
amemuacha na kumtenga, Mungu hakumwangalia kama mwanae!
Isaya 59:1-2 “Tazama, mkono wa Bwana
haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze
kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu
zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.”
Mathayo 27:45-46 “Basi tangu saa sita
palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa. Na kama saa tisa, Yesu akapaza
sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu,
Mungu wangu, mbona umeniacha?”
Faida ya Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo.
Tunapoadhimisha mateso ya Bwana
wetu Yesu Kristo aliyeyatoa maisha yake kufa msalabani ni muhimu kwetu kufahamu
kuwa Yesu alikubali kufa Msalabani na kuharibiwa vibaya katika namna
tuliyojifunza kwa sababu ya makosa yetu na maovu yetu na kwaajili ya tukio hili
ziko faida nyingi zinazopatikana kwa kufa kwake Msalabani.
Isaya 53:4-5 “Hakika ameyachukua masikitiko
yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na
Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu
yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”
Kwa tendo la Yesu Kristo kufa
Msalabani, alizibeba dhambi zetu, na kuwapatanisha wanadamu kwa Mungu kwa
kuondoa kiambaza kilichokuwepo kati yetu na Mungu na sio hivyo tu bali
aliziharibu nguvu za shetani za kupata mashiko ya kutushitaki akituletea
uponyaji wa mwili nafsi na roho lakini kuu kuliko yote ni uzima wa milele
-
Tunapata
msamaha wa dhambi kwa sababu aliimwaga damu yake pale msalabani na pasipo
kumwagika damu hakuna ondoleo la dhambi
Waebrania 9:22
“Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa
damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo.”
-
Tunapata
uponyaji wa mwili nasfi na roho kwa sababu mateso yake yalibeba na
kusulubisha magonjwa yetu, maumivu yetu na udhaifu wetu
1Petro 2:24 “Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake
juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa
kupigwa kwake mliponywa.”
-
Tunapata
Amani ya ndani kabisa iliyopotea, Kila mtu aliyempokea Yesu hata pamoja na
kupitia changamoto za aina mbalimbali duniani utaweza kugundua kuwa anapewa
Amani ya ndani sana ambayo kimsingi gharama zake zililipwa pale msalabani
adhabu aliyopewa ilituletea sisi Amani ya kweli ya maisha ya ndani sana na
mwanadamu
Amani Isaya 53:4-5
“Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika
huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na
kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu
ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”
-
Tunaupata
ushindi dhidi ya shetani na nguvu zake zote za giza, tendo la kufa kwa Yesu
Kristio msalabani baada ya kusulubiwa kwake maaana yake alizivua enzi na
mamlaka yaani nguvu zake na utendaji wake shetani
Wakolosai
2:14-15 “akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya
kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena,
akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa
mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.”
-
Msalaba
ni njia ya uzima huu na uzima wa milele, Kifo cha Yesu kimetuletea uzima wa
mwili na uzima wa kiroho kwa hiyo katika
yeye tunao uzima wa milele
Yohana 10:10-11
“Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi
nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele. Mimi ndimi mchungaji mwema.
Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.“
1Yohana 5:12-13 “Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana
wa Mungu hana huo uzima. Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna
uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu.”
Hitimisho
Wokovu una gharama kubwa sana
umegharimu maisha ya mwana wa Mungu, hatuna budi kuujali na kutokuupuuzia ili
tuweze kupona, aliharibiwa namna ile ili sisi tutengenezwe na kufaa mbele za
Mungu, basi tuukubali wokovu.
Waebrania 2:2-4 “Kwa maana, ikiwa lile neno
lililonenwa na malaika lilikuwa imara, na kila kosa na uasi ulipata ujira wa
haki, sisi je! Tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao
kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia; Mungu
naye akishuhudu pamoja nao kwa ishara na ajabu na nguvu za namna nyingi, na kwa
magawanyo ya Roho Mtakatifu, kama alivyopenda mwenyewe.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni