Wafilipi 3:12-14 “Si kwamba nimekwisha
kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate
kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu,
sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu;
nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo,
niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.”
Utangulizi:
Mojawapo ya changamoto kubwa sana
katika ufanisi wa maendeleo ya mwanadamu kiroho na kimwili na kisaikolojia ni
pamoja na kutokusahau yaliyo nyuma,
“Living in the Past” kutokuyasahau yaliyo nyuma kumewafunga watu wengi sana
na kuwawekea mipaka ya kiimani, kuchelewesha ukuaji wao wa kiroho, kuzuia
maendeleo yao ya safari ya kiuchumi, kuwadumaza katika hali zote kuwanyima
maisha ya ushindi, kuathiri uwezo wa kufanya maamuzi, kupunguza nguvu zao kwa
mambo yajayo na kushindwa kuamini ahadi ya Mungu kuhusu mambo yajayo, hali hii
iliwasumbua sana wana wa Israel ambao hata walipookolewa kutoka Misri, hawakuliona
baadaye tendo lile kuwa ni kubwa sana na badala yake walinung’unika mara kwa
mara wakikumbuka kule Mungu alikowaokoa katika inchi ya utumwa, tena
wakikumbuka vitu vidogovidogo kama matango na mboga.
Hesabu 11:4-6 “Kisha mkutano wa wafuasi
waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena,
wakasema, N'nani atakayetupa nyama tule? Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri
bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu;
lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha
kutumaini isipokuwa hii mana tu.”
Kutokuyasahau yaliyo nyuma na kuamua
kuyachuchumilia yaliyo mbele kunaweza kukufanya usizione sababu za wito wa
Mungu na baraka alizokusudia kwako, kumbuka kila kitu duniani kina mchakato na
maisha yana mchakato wake na mwandishi wa mchakato huo ni Mungu, sasa basi
anapokuwa amekupitisha mahali na ukawa unalalamika unaweza kusababisha kupoteza
Baraka zilizokusudiwa kwako, kwa msingi huo basi leo tutachukua muda kujifunza
somo hili muhimu “Kuyachuchumilia yaliyo
mbele” kwa kuzingatia vipengele vikuu muhimu vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya
kuyachuchumilia yaliyo mbele
·
Umuhimu
wa Kuyachuchumilia yaliyo mbele!
·
Athari za
kutoyasahau yaliyo nyuma
Maana ya kuyachuchumilia yaliyo mbele
Wafilipi 3:13 “Ndugu, sijidhanii nafsi
yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo
nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele;”
Kabla hatujaingia ndani kuangalia
kile ambacho Mungu amekusudia kusema nasi leo ni muhimu kwetu kuyafanyia
uchunguzi maandiko au maneno yanayotumiwa na Paulo Mtume katika fungu hili la
maandiko yana maana gani, Waraka huu wa wafilipi uliandikwa kwa lugha ya
kiyunani (Koine Greek) ambayo ndiyo
ilikuwa lugha ya kisomi na kitaaluma ya nyakati za karne ya kwanza kwa hiyo
kitabu hiki kiliandikwa mnamo mwaka wa
62BK na maneno haya kuyachuchumilia
yaliyo mbele yanasomeka hivi katika kiyunani (Epekteinomenos tois emprosthen)
neno Epekteinomenos au epekteinomai kwa kiingereza linasomeka “stretching oneself forward“ ambalo
maana yake ni kujinyoosha kuelekea mbele kwa nguvu neno hili hasa lina asili ya mkao anaotakiwa
kujiweka mwanariadha anapokimbia mbio za Olympic ili aweze kushinda, kulingana na sheria
za Olympic umaliziaji wa mkimbiaji
wa riadha huamuliwa wakati kiwiliwili chake kinapovuka mstari wa kumalizia, kwa
hiyo katika mbio za riadha kutanguliza miguu au mikono hakuhesabiwi kama
umaliziaji wa mbio ulio halali, aidha mwanariadha anayetafuta ushindi huwaga
hana muda wa kuangalia nyuma wala pembeni nguvu zake zote fahamu zake zote huelekezwa katika kufikia
lengo na kwa sababu hiyo kila msuli na kila mfumo wa fahamu na neva hufanya
kazi kwa bidii kuelekea katika malengo yake, Kwa hiyo Paulo mtume anatumia
mfano wa wanariadha kwa sababu ilikuwa maarufu sana nyakati za kanisa la
kwanza, wakati wote Mungu anapotaka ushindi utokee katika maisha ya watu wake
huwaambia wasonge mbele
Isaya 43:18-19 “Msiyakumbuke mambo ya
kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani.Tazama, nitatenda neno jipya; sasa
litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji
nyikani.”
Kutoka 14:14-15. “BWANA atawapigania ninyi,
nanyi mtanyamaza kimya. BWANA akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie
wana wa Israeli waendelee mbele.”
Unaona! Katika fundisho lake
Paulo Mtume hataki Wafilipi wajidhanie kuwa wamekwisha kufika au wamekuwa
wakamilifu akitumia mfano wake anamtaka kila Mkristo kusonga mbele kwa nguvu
kwa imani na utii, kwa bidii, kwa nguvu kwa tumaini na kutokuangalia nyuma
mpaka kuhakikisha ya kuwa tunapata tuzo mbinguni na kuyafikia malengo yetu
yaliyo mbele, kwa hiyo kama mwanariadha uliye katika mbio za ushindani wa
kiroho angalia mbele tu!
Umuhimu wa Kuyachuchumilia yaliyo mbele!
Ni muhimu kujiuliza kwa nini
Paulo Mtume siku zote alikuwa akiyachuchumilia yaliyo mbele na akisahau yaliyo
nyuma, Kuangalia nyuma kungempa historia ya matukio yaliyopita ambayo kimsingi
yangemshika na kumpunguzia mwendo wake wa kusonga mbele katika imani aku kumpa
kuridhika sawa na mwanariadha anavyoweza kupoteza mwelekeo kama ataangalia
nyuma, Yeye alikuwa mtu mwenye bidii katika Torati kuliko mtu yeyote, aliishika
sheria kiasi ambacho kwa habari ya sheria hakuwa na dhambi, lakini alipompata
Yesu na kubaini ubora wa Yesu Kristo hata pamoja na mateso makali yaliyokuwa
yakimpata alidhamiria kuwa ataendelea kuwa na Yesu, hatamuacha Yesu
atashikamana na Yesu atashikamana na injili na hatarudi nyuma kwa sababu
yoyote, aliwaonya Wafilipi hivi na kujionyesha yeye mwenyewe kuwa mfano kwa
sababu ya watu waliofundisha mafundisho ya Sheria ya Musa na tohara ambao yeye
aliwaitwa umbwa au watu wajikatao akitaka kuwaonyesha Wafilipi faida ya
kumfuata Yesu na kuachana na mafundisho ya kale yasiyo na msingi, Paulo alikuwa
na mafanikio makubwa katika dini ya kiyahudi na heshima kubwa lakini alipuuzia
kwaajili ya Kristo. Alipompata Kirsto hakuangalia pembeni tena alikaza kwenda
mbele
Yeye aliliudhi Kanisa 1Wakorintho 15:9 “Maana
mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu naliliudhi
Kanisa la Mungu.”
Wagalatia 1:13-15 “Maana mmesikia habari za
mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba naliliudhi kanisa la
Mungu kupita kiasi, nikaliharibu. Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi
kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika
kuyashika mapokeo ya baba zangu. Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa
mama yangu, akaniita kwa neema yake,”
Wafilipi 3:2-7 “Jihadharini na mbwa,
jihadharini na watendao mabaya, jihadharini na wajikatao. Maana sisi tu tohara,
tumwabuduo Mungu kwa Roho, na kuona fahari juu ya Kristo Yesu, wala
hatuutumainii mwili.Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu ye yote
akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi. Nalitahiriwa siku
ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa
Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi,
mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na
hatia. Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa
ajili ya Kristo.”
Kila mtu aliyemuamini Bwana wetu
Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yake anapaswa kusahau yote
yaliyopita na kuweka akili zake zote na nguvu zake zote na moyo wake wote na
fahamu zake zote kuyachuchumilia yaliyo mbele, hii haimaanishi kuyafuta kabisa
lakini maana yake maisha yaliyopita kama yalikuwa ya raha au ya taabu yalikuwa
ya heshima ama kuvunjiwa heshima, yasiwe na machango wowote katika hali yako ya
sasa kwa kukufanya kuangalia nyuma na kumpuuzia Kristo na badala yake kujitoa
kwa nguvu zetu zote katika kumcha Mungu na kumtumikia bila hata kujali hali unayopitia
sasa, Neno la Mungu linaonyesha wazi kuwa Mungu havuitiwi kamwe na watu wasio
na maamuzi thabiti na badala yake anawataka watu wenye msimamo watakaosonga
mbele wazima wazima na sio nusu nusu, ushindi wetu utapatikana sio kwa
kuitanguliza mguu au mkono bali kiwiliwili chote
-Mke wa Lutu alitazama nyuma wakati Mungu alipowaokoa Lutu na familia
yake kutoka Sodoma, na matokeo yake hukumu ilimpitia ya kuwa nguzo ya chumvi,
yeye alikamatwa na maisha ya zamani, badala ya kuyasahau yaliyipita
alishikamana nayo na yakaharibu hatima yake, hatima yako inaweza kuathiriwa na
mambo ya nyuma
Mwanzo 19:16-26 “Akakawia-kawia; nao wale
watu wakamshika mkono, na mkono wa mkewe, na mkono wa binti zake wawili, kwa
jinsi BWANA alivyomhurumia, wakamtoa wakamweka nje ya mji. Ikawa walipomtoa
nje, mmoja alisema, Jiponye nafsi yako usitazame nyuma, wala usisimame katika hilo
bonde po pote; ujiponye mlimani, usije ukapotea. Lutu akawaambia, Sivyo, bwana
wangu! Tazama, mtumwa wako ameona kibali machoni pako, nawe umezidisha rehema
zako ulizonifanyia kwa kuponya nafsi yangu, nami siwezi kukimbilia mlimani
nisipatwe na yale mabaya, nikafa. Basi mji huu u karibu, niukimbilie, nao ni
mdogo, nijiponye sasa huko, sio mdogo huu? Na nafsi yangu itaishi. Akamwambia,
Tazama, nimekukubali hata kwa neno hili, kwamba sitauangamiza mji huo
uliounena. Hima, ujiponye huko, maana siwezi kufanya neno lo lote, hata
uingiapo humo. Kwa hiyo jina la mji ule likaitwa Soari. Jua lilikuwa
limechomoza juu ya nchi Lutu alipoingia Soari. Ndipo BWANA akanyesha juu ya
Sodoma na juu ya Gomora kiberiti na moto toka mbinguni kwa BWANA. Akaangusha
miji hiyo na Bonde lote, na wote waliokaa katika miji hiyo, na yote yaliyomea
katika nchi ile. Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi.”
Luka 9:62 “Yesu akamwambia, Mtu aliyetia
mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu.”
Siri ya maisha ya ushindi iko
katika kuyachuchumilia yaliyo mbele na kusahau yaliyo nyuma kama mtu anataka
kusonaga mbele ni lazima asahau kushindwa kwake, asahau maumivu yote ya nyuma,
asamehe endapo wako watu waliomuumiza, asahau majuto na aibu, asahau mafanikio
yanayokufanya ujivune na kupata kiburi, sahau
hata watu ambao walikuwa karibu nawe na makusudi ya kuwa karibu nao yameisha, na
umwangalie Yesu Kristo zaidi kwaajili ya mafanikio yako ya baadae ,
unapoyachuchumilia yaliyo mbele unafungua mlango mpya na mlango huo unakufanya ukimbie mbio zako na
kuufikia mwisho wenye ushindi na Mungu atakupa nguvu ya kukimbia hadi mwisho.
Athari za kutoyasahau yaliyo nyuma.
Wakati wowote watu wanapoangalia
nyuma wanakuwa watumwa wa yaliyopita, Kristo alitukomboa ili tuishi maisha
mapya yenye tumaini na uhuru yasiyo na hofu kwa hiyo kutokuyasahau yaliyo nyuma
kunaathiri maisha yako
1. Kunakufanya
usiendelee kiroho, kimwili na kisaikolojia kwa sababu unaweza kukwama na hatia
aibu au majuto, na ukajiona hustahili
Baraka mpya za Mungu, au ukabweteka na kile ulicho nacho!
2. Kunakufanya
uharibu furaha ya sasa – badala ya kumshukuru Mungu kwa yaliyopo na kukusaidia
kusonga mbele unabaki unalilia yaliyopita au unaridhika na kile unachiokiona!
3. Kutosahau
yaliyo nyuma kunakufanya usiweze kuyafikia malengo mfano Paulo alikuwa analenga
la kufika mbinguni na kupata thawabu na kukaa na bwana milele
4. Kutokuyasahu
yaliyo nyuma kunakufanya uwe mwoga wa hatua mpya – unashikwa na hofu ya
kushindwa au unajutia mafanikio yaliyopita
5. Kutoyasahau
yaliyo nyuma kunakufanya uishi wakati uliopita badala ya wakati wa sasa wa
kusudi la Mungu
Paulo alichagua neno moja tu
kuyasahau yaliyopita na kuyachuchumilia yaliyo mbele hii ndio siri ya ushindi
inayotoa ujasiri na kukufanya usiogope lolote, Neno la Mungu linatoa wito leo
kuwa ni lazima usahahu kushindwa kwako, usahahu mafanikio yako ya nyuma, sahahu
aibu, au kujilinganisha na wengine sahahu maumivu yako, usiishi katika majuto
angalia mbele na Mungu atakutokea, kama unahitaji mafanikio makubwa zaidi chuchumilia
yaliyo mbele!
Kumbukumbu 31:8 “Naye Bwana, yeye ndiye
atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope
wala usifadhaike.”
Mithali 4:25-27 “Macho yako yatazame mbele,
Na kope zako zitazame mbele yako sawasawa. Ulisawazishe pito la mguu wako, Na
njia zako zote zithibitike; Usigeuke kwa kuume wala kwa kushoto; Ondoa mguu
wako maovuni.”
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni