Mwanzo 29:20-26 “Yakobo akatumika miaka
saba kwa kumpata Raheli. Ikawa machoni pake kama siku chache tu kwa vile
alivyompenda. Yakobo akamwambia Labani, Nipe mke wangu, maana siku zangu
zimetimia; niingie kwake. Labani akakusanya watu wote wa mahali pale, akafanya
karamu. Ikawa wakati wa jioni akamtwaa Lea, binti yake, akamletea Yakobo, naye akaingia
kwake. Labani akampa Lea mjakazi wake Zilpa, awe mjakazi wake. Ikawa,
kulipokuwa asubuhi, kumbe! Ni Lea. Akamwambia Labani, Nini hii uliyonitenda?
Sikukutumikia kwa Raheli? Mbona umenidanganya? Labani akasema, Havitendeki hivi
kwetu, kumtoa mdogo kabla ya mkubwa;”
Utangulizi:
Hakuna linalotokea kwa bahati
mbaya Duniani, wakati mwingine Mungu anaweza kuruhusu, ufanye kazi, au
biashara, au huduma au usomee fani ambayo kimsingi inaweza ikawa sio chaguo
lako, na hali kadhalika unaweza kuwa katika mahusiano na mtu ambaye moyo wako
unaweza usiwe umemridhia moja kwa moja isipokuwa ni kwa sababu ya mazingira
fulani, katika maisha yangu nimekuwa karibu na wanafunzi na walimu na watu wa
kada mbalimbali za kitaaluma, na nimesikia kwa masikio yangu wengine wakisema
nilitaka kuchukua masomo ya Sayansi, lakini walimu walinishauri nichukue masomo
ya Sanaa, nilitaka kuchukua masomo ya Sanaa lakini wazazi wangu walinishauri
nichukue Sayansi, nilitaka kuwa daktari lakini serikali ilinipangia ualimu,
nilitaka kuwa mwanasheria lakini nililazimika kuwa mwanahabari, nilikuwa na
mipango yangu kadhaa lakini nimejikuta nimekuwa Mwalimu, Mungu katika hekima
yake wakati mwingine anaweza kuruhusu ubebe mzigo ambao moyo wako hungependelea
kuubeba kwa kusudi la kutimiza mpango wake usioweza kuuona kwa wakati huo au
kwa macho yako na sio hivyo tu wakati mwingine Mungu anaruhusu hivyo kwaajili
ya ukuaji wa kiroho, kukufundisha kuacha mapenzi yako na kusikiliza ya kwake,
kukufundisha uvumilivu, kupenda kisichoweza kupendeka na kukunyima kutimiza
mapenzi yako uli uweze kujisalimisha kwenye mapenzi yake, hali kama hiyo ndiyo
iliyomtokea Yakobo wakati anataka kuoa, alijiandaa na kufanya kazi kwa bidii
kwaajili ya Raheli lakini akaozwa Lea bila kutaka!, Kumbe ni Lea badala ya
Raheli.
Mwanzo 29:16-20 “Labani alikuwa na binti
wawili, jina la mkubwa ni Lea, na jina la mdogo ni Raheli. Naye Lea macho yake
yalikuwa dhaifu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo, na mzuri uso. Yakobo
akampenda Raheli akasema, Nitakutumikia miaka saba kwa kumpata Raheli, binti
yako mdogo. Labani akasema, Afadhali nikupe wewe kuliko mtu mwingine; kaa
kwangu. Yakobo akatumika miaka saba kwa kumpata Raheli. Ikawa machoni pake kama
siku chache tu kwa vile alivyompenda.”
Kuna maumivu kiasi fulani ambayo
wengine wanaweza wasiyaseme kwa maneno lakini yakaishia moyoni, maumivu ya
kupata ua kufanya jambo ambalo kimsingi hujalipenda toka moyoni, hujalitamani,
hujalitaka wala hujaliomba, au hujalisomea, unaweza kabisa katika maisha
ukasomea ujuzi fulani kisha ukapangiwa mwingine, unaweza kuomba kazi fulani na
ukapewa nyingine unaweza kutarajia kuwa ungeoa mke wa aina fulani au ukaolewa
na mume wa aina fulani, lakini ukaishia kuolewa na mwingine, ungetaka idadi fulani
ya watoto au watoto wa jinsia fulan unashangaa umepewa wa aina fulanii, au
ulikuwa na ndoto ya maisha fulani na ukajikuta unaishi maisha tofauti, haya
ndiyo yaliyo mtokea Yakobo, alipoenda kwa mjomba wake kuoa alikuwa na nia ya
kumpata Raheli na kimsingi alimpenda Raheli aliwekeza nguvu zake na akili zake
na hisia zake kwa Raheli, na akatumika miaka saba ili ampate kipenzi wake
Raheli lakini siku ya harusi yake anaamka asubuhi kumbe ni Lea! Hali hii
inawakuta watu wengi, katika maisha kujikuta
kuwa wana kile walichokua hawajakitaka, ujumbe huu ni kwa watu wanaopitia hali
kama hiyo na Mungu ana makusudi na wewe na anataka kusema nawe, tutajifunza
ujumbe huu KUMBE NI LEA BADALA YA RAHELI
kwa kuzingatia vipengele muhimu vitatu vifuatavyo:-
·
Inapokuwa
Lea badala ya Raheli
·
Kumbe ni
Lea badala ya Raheli
·
Kusudi la
Mungu kupitia Lea
Inapokuwa Lea badala ya Raheli
Wote tutakuwa tunakumbuka kuwa
baada ya Yakobo kuchukua mbaraka wa Esau na mgogoro kujitokeza katika familia
Rebeka alimshauri Isaka kuwa kijana wao na aende kwa kaka yake Rebeka yaani Labani
ili ajipatie mke huko badala ya kujitwalia mke katikati ya Wakanaani ambao roho
yake Rebeka haikuwaridhia, Yakobo alisafiri kuelekea Haran kwa mjomba wake
Labani ili ajipatie mke huko na alipofika huko kimsingi Yakobo alimpenda sana
Raheli kwa sababu ndiye aliyekuwa anamvutia kimwili na kiumbo na kwa uzuri,
walipatana na mjomba wake kuwa mahari itakuwa ni kumtumikia kwa miaka 7
kwaajili ya Raheli, kwa hiyo Yakobo alifanya kazi kwa bidii sana kwaajili ya
kile alichokuwa amekiona, amekitamani na kukipenda, mke wa ndoto yake, stori
nzima iko hapa:-
Mwanzo 29:16-30 “Labani alikuwa na binti
wawili, jina la mkubwa ni Lea, na jina la mdogo ni Raheli. Naye Lea macho yake
yalikuwa dhaifu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo, na mzuri uso. Yakobo
akampenda Raheli akasema, Nitakutumikia miaka saba kwa kumpata Raheli, binti
yako mdogo. Labani akasema, Afadhali nikupe wewe kuliko mtu mwingine; kaa
kwangu.Yakobo akatumika miaka saba kwa kumpata Raheli. Ikawa machoni pake kama
siku chache tu kwa vile alivyompenda. Yakobo akamwambia Labani, Nipe mke wangu,
maana siku zangu zimetimia; niingie kwake. Labani akakusanya watu wote wa
mahali pale, akafanya karamu.Ikawa wakati wa jioni akamtwaa Lea, binti yake,
akamletea Yakobo, naye akaingia kwake. Labani akampa Lea mjakazi wake Zilpa,
awe mjakazi wake. Ikawa, kulipokuwa asubuhi, kumbe! Ni Lea. Akamwambia Labani,
Nini hii uliyonitenda? Sikukutumikia kwa Raheli? Mbona umenidanganya? Labani
akasema, Havitendeki hivi kwetu, kumtoa mdogo kabla ya mkubwa; timiza siku zake
saba, nasi tutakupa huyu naye kwa utumishi utakaonitumikia, miaka saba mingine.
Yakobo akafanya hivi, akatimiza siku zake saba. Naye akampa Raheli binti yake
kuwa mkewe. Labani akampa binti yake Raheli mjakazi wake Bilha, awe mjakazi
wake. Akaingia kwa Raheli naye, akampenda Raheli kuliko Lea, akatumika kwa
ajili yake miaka saba mingine.”
Unaweza kuona mtu anafanya kazi
kwa bidii na kwa kujituma kweli kweli akiwa na ndoto ya kumpata Raheli lakini
hatimaye anakuja kupewa Lea, hili linaweza kuwa jambo lenye kuumiza sana kwamba
unafanya kazi, unasoma au unajituma kwaajili ya malengo fulani alafu unakuja
kujikuta ni kama ulimwengu unataka ufanye jambo lingine, jambo hili linaumiza,
unatoa juhudi zako zote, unatoa muda wako wote, unawekeza moyo wako wote lakini
matokeo yanakuwa sio yale uliyoyatarajia, hali hii iko hivyo duniani, kuna watu
wamewapenda sana wachumba zao, wakawafulia, wakawapikia, wakawa wakiwajulia
hali lakini na kuwapa kila kitu, lakini yule bwana akaja akaoa mwanamke
mwingine, kuna watu wamejitoa kwaajili ya wachumba wao wakawasomesha wakawahudumia
na kuwafadhili, hata wakafunga na kuomba kwaajili yao kwa kulia, lakini wakaja
kuolewa na mwanaume mwingine, kuna watu walikuwa na ndoto ya kuendesha ndege
lakini leo ni Askari polisi, kuna watu walitaka kuwa madaktari lakini leo ni
walimu, Moyo wako unaweza kuchoka na kuumia na kuumizwa na matarajio
yaliyovunjika na unaweza kujiuliza Mungu kwa nini hali hii inakuwa hivi? Unasomea
fani Fulani kisha unakuja kupata kazi flani tofauti na ile uliyoisomea na
iliyoko moyoni mwako! Wala sicho ulichokitarajia, unahisi kuchanganyikiwa,
unahisi kuumia na unaanza kumuhoji Mungu! Imekuwaje? Ndoto yangu ilikuwa hii
mbona nafanya jambo hili?
Mithali 13:12 “Kilichotarajiwa kikikawia kuja,
moyo huugua. Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima.”
Tunao watu wengi sana leo hii
katika jamii ambao mioyo yao imejeruhiwa kwa kuwa na matokeo wasiyoyatarajia,
mtu amesoma kwa bidii na kufanya mtihani wake kwa umakini anakuja kupata Division
three ambayo hakuitegemea, unaweza kuolewa na mume ambaye hata hukuwa na hata hisia naye, unaweza kuwa
na mke ambaye huna hata hisia naye lakini mnajikuta ndio mnaishi, yako maisha
ambayo unaweza kuwa ndani yake lakini moyo wako ukawa haupo humo, haki hii ndiyo
ilityomtokea Yakobo anampenda Raheli na ameganya kqzi miaka saba kwaajili yake,
lakini amepewa Lea, kwa hiyo katika maisha yetu inapokuwa Lea badala ya Raheli
watu hukosa amani na furaha na kuona kama maisha yameshakataa na wakati
mwingine unaweza kuwaza na kufikiri umekosea wapi katika kaninu za maisha,
unaweza kujikuta hufurahii maisha, hufurahii kazi, unakosa furaha kwa kile
ulichonacho na ukijilinganisha na wengine ndio unachoka unaweza kudhani wewe
una balaa, lakini nataka nikugusie kuwa Mungu ana mpango!, Hakuna jambo lolote
linalotokeaau kukupata nje ya mpango wa Mungu, hapa duniani hatujaja kutimiza
mpango wetu, tumekuja duniani kutimiza mpango na mapenzi ya Mungu, hivyo sio
jambo la ajabu yakakupata yaliyo mageni
Kumbe ni Lea badala ya Raheli
Neno la Mungu linaonyesha ya kuwa
njia za Mungu ziko juu sana kuliko njia za mwanadamu na wala mawazo yetu si
kama mawazo yake, njia za Mungu ziko juu sana, mpango wa Mungu ni mkuu kuliko
matakwa ya mwanadamu, Mungu hafanyi kazi kwa kusikiliza hisia zeu, ana mpango
mkubwa sana kuliko hisia zako, Hapa duniani ulizaliwa kwa kusudi la Mungu na
kwa sababu hiyo mwenye mji wake ni Mungu na mwenye mpango wake ni yeye kwa hiyo
wewe unaweza kumtaka Raheli lakini Mungu akakupa Lea, unaweza kudhani kuwa
dunia imekulazimisha Lea na we ulitaka Raheli lakini, Lea ndio mpango kamili wa
Mungu. Raheli unaweza kuwa sio mpango wa kudumu wala wa milele lakini Lea
unaweza kuwa mpango wa Mungu wa kudumu na wa milele, na wenye faida unajua
nini watoto wote maalumu ambao Mungu alikuwa
na kusudi lake la kudumu walipita kwa Lea na sio Raheli
Mwanzo 29:31-35 “BWANA akaona ya kwamba Lea
hakupendwa, naye akafungua tumbo lake; bali Raheli alikuwa hazai. Lea akapata
mimba akazaa mwana, akampa jina lake, Reubeni, maana alisema, Kwa kuwa BWANA
ameona teso langu; sasa mume wangu atanipenda. Akapata mimba tena akazaa mwana,
akasema, Kwa kuwa BWANA amesikia ya kwamba mimi sikupendwa, amenipa na huyu;
akamwita jina lake Simeoni. Akapata mimba tena, akazaa mwana, akasema, Basi
wakati huu mume wangu ataungana nami, kwa sababu nimemzalia wana watatu. Kwa
hiyo akamwita jina lake Lawi. Akapata mimba tena, akazaa mwana. Akasema, Mara
hii nitamsifu BWANA; kwa hiyo akamwita jina lake Yuda; akaacha kuzaa.”
Mungu aliwatumia Walawi, kutoka
kwa Lea kuwa makuhani kwaajili ya utumishi wa Mungu katika nyumba yake na Mungu
na Mungu alimtumia Yuda kutoka kwa Lea kuleta viongozi mashuhuri na wacha Mungu
kama Daudi na kupitia Lea na Yuda alimleta Yesu Kristo
Mathayo 1:1-2.“Kitabu cha ukoo wa Yesu
Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu. Ibrahimu alimzaa Isaka; Isaka
akamzaa Yakobo; Yakobo akamzaa Yuda na ndugu zake;”
Mungu aliruhusu Lea kuwepo katika
maisha ya Yakobo kwa sababu Lea ndio ulikuwa mpango wa Mungu, Lea alikuwa ni
darasa la unyenyekevu, Lea alikuwa ni chuo cha uvumilivu, Lea alikuwa ni shule
ya haki ya Mungu, Lea ilikuwa ni shule ya kujifunza kupenda kile ambacho Mungu
amekupangia, Mungu anatufundisha kumfuata yeye na sio hisia zetu, Lazima ufike
wakati katika maisha yetu tuamue kufuata hisia zetu au kutimiza mpango wa
Mungu, Lea alilazimika kutaka kumpendeza Yakobo lakini hata pamoja na kumzalia
watoto wengi wa kume mfuluzizo bado Yakobo hakuona nguvu za Mungu, Lea aliamua
kumuita mtoto wake Yuda akisema
NITAMSIFU BWANA Furaha ya kweli haipatikani kwa wanadamu bali inapatikana
kwa Mungu, Mungu aliona kitu ndani ya Lea ambacho kimsingi hakikuweko ndani ya Raheli
Mungu anaona kile ambacho wanadamu hawakioni, Lea hakuwa mzuri wa uso lakini
alikuwa mzuri moyoni, Yule aliyeyependwa na aliyekuwa mzuri wa uso moyoni
hakuwa ameshikamana na Mungu na aliibeba kwa kuiiba miungu ya baba yake na alikufa
baaadae kwa neno la Yakobo ona:-
Mwanzo 31:19-35 “Basi Labani alikuwa
amekwenda kuwakata manyoya kondoo zake, na Raheli akaviiba vinyago vya babaye.
Yakobo akamhadaa Labani, Mshami, kwa kuwa hakumwambia ya kwamba anakimbia. Basi
akakimbia yeye na yote aliyokuwa nayo; akaondoka akauvuka mto, akaelekeza uso
wake kwenda mlima wa Gileadi. Hata siku ya tatu Labani akaambiwa ya kwamba
Yakobo amekimbia, akatwaa ndugu zake pamoja naye, akamfuata mwendo wa siku
saba. Akampata katika mlima wa Gileadi. Mungu akamjia Labani, Mshami, katika
ndoto ya usiku, akamwambia, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la
shari. Labani akamfikia Yakobo, na Yakobo alikuwa amepiga hema zake katika
mlima, na Labani na ndugu zake wakapiga hema zao katika mlima wa Gileadi.
Labani akamwambia Yakobo, Umefanya nini? Umenihadaa, ukawachukua binti zangu
kama mateka waliotwaliwa kwa upanga. Mbona umekimbia kwa siri ukanihadaa, wala
hukuniambia, nipate kuagana nawe uende zako kwa furaha, na nyimbo, na ngoma, na
kinubi? Wala hukuniacha niwabusu wanangu, na binti zangu; basi umetenda upumbavu.
Ninao uwezo mkononi mwangu wa kukufanyia madhara; lakini Mungu wa baba yako
usiku huu ameniambia, akisema, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala
la shari. Basi sasa, umetoka kwa sababu umetamani sana nyumba ya baba yako.
Mbona basi umeiiba miungu yangu? Yakobo akajibu, akamwambia Labani, Kwa sababu
naliogopa, nikasema, Usije ukaninyang'anya binti zako kwa nguvu. Awaye yote
utakayemwona kuwa nayo miungu yako, yeye asiishi. Mbele ya ndugu zetu ukitambue
kilicho chako kwangu, ukakichukue. Maana Yakobo hakujua ya kwamba Raheli
ameiiba. Labani akaingia katika hema ya Yakobo, na hema ya Lea, na hema ya
vijakazi wawili, wala hakuiona. Akatoka katika hema ya Lea, akaingia katika
hema ya Raheli. Basi Raheli alikuwa amevitwaa vile vinyago ameviweka katika
matandiko ya ngamia, na kuvikalia. Labani akapapasa hema yote wala hakuviona.
Naye Raheli akamwambia babaye, Bwana wangu asikasirike kwa sababu siwezi
kuinuka mbele yako, maana nimeshikwa na mambo ya kike. Akatafuta, wala
hakuviona vile vinyago.”
Raheli alikuwa muabudu miungu,
aliiba miungu ya baba yake Neno vinyago linalotajwa hapo katika Kiebrania
linatajwa kama “Teraphim” ambao ni
miungu midogo midogo yenye sura kama ya mwanadamu ambayo ilichongwa na
kuabudiwa zamani hasa huko mashariki ya mbali na ambayo ilitumika kwa uganga na
uchawi na kupigia ramli, miungu hii ilichongwa kwa mfano wa wanadamu na iliyorithiwa
toka mababu na mababu na ilirithishwa kwa viongozi wa familia kwa hiyo kuwa na
miungu hiyo kulimaanisha kutaka kuwa kiongozi wa familia na Labani alipokuja kuulizia miungu hiyo
Raheli aliificha, Yakobo bila kuelewa alimwambia Labani yeye atakayekutwa na miungu yako na
asiishi, tukio hili lilipelekea kifo cha mapema cha Raheli, Kumbe Lea
alimuabudu Mungu wa kweli lakini Raheli miungu!
Mwanzo 35:16-18 “Wakasafiri kutoka Betheli,
hata ukabaki mwendo wa kitambo tu kufika Efrathi, Raheli akashikwa na utungu wa
kuzaa, na utungu wake ulikuwa mzito. Ikawa alipokuwa anashikwa sana na utungu,
mzalisha akamwambia, Usiogope, maana sasa utamzaa mwanamume mwingine. Ikawa
hapo katika kutoa roho yake, maana alikufa, akamwita jina lake Benoni, lakini
babaye alimwita Benyamini.”
Je bado una huzuni ya kumkosa
Raheli? Mungu alikuwa na mpango, sio kila Raheli ni Baraka na sio kila Lea ni
Laana wakati mwingine Raheli ni tamaa yako na Lea ni mapenzi ya Mungu kwako,
Mpango wa Mungu haujafichwa ndani ya kile unachikipenda bali uko ndani ya kile
alichokupa, acha kutokukubaliana na Lea katika maisha yako, Lea sasa anahitaji
upendo wako, ni muhimu sasa ukakubaliana na kile ambacho Mungu amekiruhusu
katika maisha yako, ni lazima ukubali mapenzi ya Mungu na kutafuta kusudi la
ndani la hali uliyo nayo, badala ya kujutia kile ulichonyimwa furahia kile ulichopewa
na Mungu na kipokee kwa shukurani maana katika hilo uko mpango wa Mungu, Yesu
anatoka kwa Lea na sio kwa Raheli, kile usichokipenda kinaweza kubeba hatima
yako! Na kusudi la Mungu katika mpango wake, yako mambo tunaweza kuchagua na
yako mambo Mungu mwenyewe anakuchagulia, furahia kile Mungu amekuchagulia,
hakuna bahati mbaya katika kile Mungu amekupangia, oooo kumbe ni Lea badala ya
Raheli.
Kusudi la Mungu kupitia Lea
Mungu anataka kutufunza hapa kuwa
wakati mwingine katika hekima yake atafanya mambo kinyume na yale
tunayoyatarajia ambayo kimsingi ni shauku na tamaa zetu au hisia zetu, Mungu
anataka kuivunja ile hali ya kujitegemea katika maamuzi yetu anataka ukomavu
anataka kurekebisha tabia zetu anataka kutuumbia moyo wa kuwa na uhusiano wa
karibu sana na yeye ili tumtegemee yeye, hali hizo zote zinaruhusiwa kwaajili
ya ukamilifu wetu kwa hiyo wale wote ambao wako katika hali kama ile
aliyoipitia Yakobo wanapaswa kuelewa kuwa ni mchakao wa Mungu utimize mapenzi
yake na sio ya kwako kwa hiyo fanya kwa upendo na uaminifu kile ambacho Mungu amekuchagulia.
Warumi 8:28-29 “Nasi twajua ya kuwa katika
mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema,
yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili,
aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe
mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.”
Mungu anataka tuache kujitegemea
na kujitumainia na badala yake tuishi kwa kumtegemea yeye, Mungu ataupiga chini
mpango wetu wa ubinafsi na atabadilisha mambo ili tumtegemee yeye
2Wakorintho 12:7-9. “Na makusudi nisipate
kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili,
mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya
kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke.Naye akaniambia, Neema
yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia
udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.”
Mungu anataka utii hata katika
mazingira magumu, kwa msingi huo badala ya kujiuliza kwanini mimi ninayapitia
haya wewe jiulize Mungu atatukuzwaje kwenye jambo hili, Je kwa kuwa tumepewa
uhuru wa kuchagua wadhani ya kuwa Mungu hana nafasi ya kuonyesha ubwana wake
katika maisha yetu? Ubinafsi wetu na starehe zetu lazima zife linapokuja swala
la kutimiza mpango wa Mungu, Kumbe ni Lea badala ya Raheli.
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni