Jumapili, 28 Juni 2026

Mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana!


Wakolosai 1:9-11 “Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni; MWENENDE KAMA ULIVYO WAJIBU WENU KWA BWANA, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu; mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha; mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru.”

 



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa mara baada ya kuwa tumeokolewa kwa neema ya Mungu, kwa njia ya imani, tunapaswa sana kuzingatia mwenendo wetu, Mtu aliyeokoka hataishi maisha anayojitakia tu kwa sababu ameokolewa, Lakini maandiko yanatoa maelekezo ya jinsi tunavyopaswa kuishi, yaani uko wajibu wetu tunaopaswa kutembea katika huo ili tuweze kuwa mfano wa kuigwa kama wana wa Mungu tuwapo hapa ulimwenguni, mwenendo huo ni wa lazima na wala sio wa hiyari, tunapaswa kuendenda kama vile Yesu Kristo mwenyewe alivyoenenda hapa duniani.

 

1Yohana 2:4-6 “Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake. Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake. Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa KUENENDA mwenyewe vile vile kama yeye ALIVYOENENDA.”

 

Katika maandiko yetu ya Msingi Paulo mtume anawaandikia Wakolosai aina ya maombi anayowaombea na kuwalekeza watu hao wajazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni ili kwamba waenende kama ulivyo wajibu wao kwa Bwana wakimpendeza yeye Kabisa!, Kumbe tunagundua ya kuwa kuna namna basi Wakristo tunapaswa kuenenda na swala hili liko wazi kabisa katika neno la Mungu. Kuna namna ya kutembea katika ulimwengu huu

 

Wafilipi 2:14-15 “Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano, mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu,”

 

Tito 2:11-12 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;

 

Wakolosai 2:4-6 “Nasema neno hili, mtu asije akawadanganya kwa maneno ya kuwashawishi. Maana nijapokuwa sipo kwa mwili, lakini nipo pamoja nanyi kwa roho, nikifurahi na kuuona utaratibu wenu na uthabiti wa imani yenu katika Kristo. Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, ENENDENI vivyo hivyo katika yeye;”

 

Kwa msingi huo utaweza kuona kuwa maandiko matakatifu yana namna ambayo kwamba Roho Mtakatifu ametukusudia sisi kuenenda sawasawa na maelekezo yanayotolewa katika maandiko lakini ili tuweze kuendelea kuelewa vizuri hatuna budi kufahamu maswala kadhaa ikiwa ni pamoja na maana ya neno mwenendo, tutajifunza somo hili Mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana! Kwa kuzingatia vipengele muhimu vitatu vifuatavyo;-

 

·         Maana ya neno mwenendo.

·         Jinsi inavyotupasa kuenenda.

·         Mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana!

 

Maana ya neno mwenendo.

 

Neno mwenendo ambalo limejitokeza zaidi ya mara 13 katika maandiko ya Kiyunani linasomeka kama “AnastrophÄ“” ambalo katika Biblia ya kiingereza linasomeka kama “conversation”, au “Behavior” au “Conducts” Katika Biblia ya Kiswahili limetumika neno mawazo, au mtazamo, tabia au mwenendo  kwa mfano kabla ya kuokoka mtu anaweza kuwa na tabia au mwenendo  ua mawazo yanayomuongoza kuwa na tabia hiyo, kwa hiyo mwenendo ni jumla ya mtazamo wa mtu na mazingira yanayopelekea awe na tabia hiyo aliyo nayo, Paulo mtume kabla ya kuokoka alikuwa na mtazamo kuwa Ukristo sio imani ya kweli na kwa sababu hiyo aliwatesa sana Wakristo na kanisa la kwanza kwa sababu mtazamo wake ulipelekea kuwa na mwenendo au tabia aliyokuwa nayo kabla ya kukutana na Bwana Yesu.

 

Wagalatia 1:13Maana mmesikia habari za MWENENDO wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba naliliudhi kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu. Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu. Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake,”

 

Kwa hiyo mtu aliyeokoka anapaswa kuwa na mabadiliko ya mwenendo wake wa kwanza au ule wa zamani na anapaswa kuvaa mwenendo mpya unaotembea katika hali ya uchaji wa Mungu kwa kuzingatia kweli, haki na utakatifu, kwa sababu hiyo mtu aliyemwamini Bwana anatarajiwa awe na mwenendo tofauti na ule aliokuwa akiuendea zamani, haya ni mabadiliko yanayoanzia kwemye mtazamo, fundisho na kuonekana katika tabia na mtazamo mpya unaompa Mungu utukufu baada ya kumpokea Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yetu!

 

Waefeso 4:20-24 “Bali ninyi, sivyo mlivyojifunza Kristo; ikiwa mlimsikia mkafundishwa katika yeye, kama kweli ilivyo katika Yesu, mvue kwa habari ya MWENENDO wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.”

 

Jinsi inavyotupasa kuenenda.

 

Tumejifunza sasa maana ya mwenendo na tumeona jinsi maandiko yanavyotuelezea kuwa uko mwenendo ambao tuliuendea zamani kabla ya kuokolewa na sasa baada ya kuwa tumeokolewa kuna aina ya mwenendo ambao tunapaswa kuuenenda na bila kufundishwa wakati mwingine inaweza kuwa ngumu kwetu kujua ni mwenendo gani tunapaswa kuufuata? Kwa hiyo yako mambo kadhaa ambayo Biblia inatuasa kuyafuata au kuyajifunza ili yaweze kuwa dira na njia ya kuujenga mwenendo wetu na huo ndio wajibu wetu ambao umesisitizwa katika maandiko ya msingi kwamba Mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana ni wajibu upi huo hapa yako mambo kadhaa ya kuyaangalia

 

1.       Ni wajibu wetu kuenenda kwa utakatifu – Utakatifu ni moja ya mwenendo ambao watu waliookoka wanapaswa kuwa nao, ni muhimu kuelewa kuwa ni vigumu kumuona Mungu bila ya kuwa na mwenendo wa utakatifu, utakatifu ni nini hasa? Biblia ya Kiyunani inatumia neno “Hagio” ambalo ni sawa na neno la Kiingereza “Pure morally” au “Blameless  maana yake kuendenda kwa uadilifu, au kutembea bila lawama, wakati wote katika maisha yetu isitokee tumelaumiwa kama watu wabaya au kwa kutenda mambo yasiyo ya uadilifu

 

1Petro 1:14-16. “Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika MWENENDO wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”

 

2.       Ni wajibu wetu kuendenda kwa imani – watu wa Mungu wanapaswa kuenenda kwa Imani, pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, kwa hiyo yote tuyatendayo tunapaswa kuyafanya kwa imani, Mungu aliwaangamiza wana wa Israel wengi jangwani kwa sababu ya kutokuamini kwao, tukiendenda kwa imani ni rahisi kumpendeza Mungu, watu wa Mungu wanapaswa kuliamini neno la Mungu na kulitii kwa imani na sio kwa kutegemea yale tuyaonayo kwa macho ya kibinadamu au mazingira yanayokuzunguka

 

2Wakorintho 5:6-8 “Basi siku zote tuna moyo mkuu; tena twajua ya kuwa, wakati tuwapo hapa katika mwili, tunakaa mbali na Bwana. (Maana TWAENENDA kwa imani, si kwa kuona.) Lakini tuna moyo mkuu; nasi tunaona ni afadhali kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana.”

 

3.       Ni wajibu wetu kuenenda kwa Upendo – Kuenenda kwa upendo ni mojawapo ya agizo la watu wa Mungu, kuishi kwa upendo, kutembea kwa upendo kujawa na upendo maisha yetu ni lazima yaonyeshe upendo wa kujitoa kama vile Kristo alivyojitoa kwetu na kwa ulimwengu ili kila amuaminiye aokolewe, chuki, husuda na wivu, magombano, visasi na majungu kamwe sio mwenendo wanaopaswa kuwa nao watu ambao Kristo amewafia Msalabani kwa kujitoa kuliko kukuu hata tulipokuwa wenye dhambi

 

Waefeso 5:1-2 “Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa; MKAENENDE katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato.”

 

4.       Ni wajibu wetu kuenenda nuruni – Kuenenda nuruni kwa ufupi maana yake ni kutembea kwa kuweka kipaumbele maswala na maagizo ya Mungu, Mungu ni Nuru, Yesu Kristo mwenyewe pia alisema yeye ni Nuru ya ulimwengu, kwa sababu hiyo tunapoweka kipaumbele maswala Yote ambayo Yesu Kristo ametufundisha na kumfuata, maana yake tunaendenda Nuruni, kwenda kinyume na maagizo ya neno la Mungu ni kuenenda gizani

 

1Yohana 1:5-7 “Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba Mungu ni nuru, wala giza lo lote hamna ndani yake.Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli; bali TUKIENENDA NURUNI, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.”

 

5.       Ni wajibu wetu kuenenda katika upya wa maisha – kutembea katika upya wa maisha kunamaanisha ni lazima maisha yetu yabadilike tuwe na mwenendo mpya na sio ule wa zamani, kabala ya kuokolewa, hatupaswi tena kuitumikia dhambi ambayo tuliiendea zamani kabla ya kukutana na Yesu, sasa kwa kuwa tumekutana na Yesu hatuna budi kuenenda katika upya huu wa maisha na kutembea na Mungu, uongo, ulevi, tamaa mbaya, uchafu, kiburi, masengenyo, ubinafsi na kujihesabia haki pamoja na maovu ya kila namna hayapaswi kuonekana tena kwa mtu anayewajibika kuenenda katika upya wa maisha

 

Warumi 6:4-6 “Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi TUENENDE KATIKA UPYA WA UZIMA. Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake; mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena;”

 

6.       Ni wajibu wetu kuenenda kwa Roho – kuenenda kwa Roho maana yake ni nini? Ni maisha ambayo Roho Mtakatifu ndiye anayetawala, kila mtu aliyeokolewa ni muhimu na lazima atoe nafasi na kumruhusu Roho Mtakatifu kuyaongoza na kuyatawala maisha yake katika kila nyanja ya maisha na kumruhusu yeye kutusaidia kukomaa kiroho na kuzaa matunda ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu, maisha yako unayaongoza wewe mwenyewe au unamuachia Roho akuongoze? Kuenenda kwa roho ni kumuachia yeye atuongoze maisha yetu.

 

Wagalatia 5:16-23 “Basi nasema, ENENDENI kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka. Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.”

 

7.       Ni wajibu wetu kuenenda kama unavyostahili wito wetu – Kila mtu aliyeokolewa kuna namna Mungu amemuita amtumikie katika mazingira mbalimbali na huo ndio wito wako, hapa wito haimaanishi ule wito wa kumtumikia Mungu pekee, wito maalumu, unaweza kuwa Mwalimu, Polisi, Daktrari, Mtoza ushuru, Mwanasiasa na kadhalika Mungu anataka uwe na mwenendo mwema katika kila aina ya wito ulioitiwa au kokote kule unakokuweko hata kama wewe ni fundi cherehani, iko miiko ya utumishi katika kile eneo la wito wa maisha basi huko enenda kama unavyoustahili wito wako, zaidi sana katika nyumba ya Mungu  huku tukitunza amani.

 

Waefeso 4:1-3 Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, MWENENDE kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.”

 

8.       Ni wajibu wetu kuenenda kwa Hekima – Ni kama maandiko yanatuambaia wazi kuwa muda wetu duniani sio wa kwetu ni muda wa Mungu, Ni muda ambao tumepewa kwa kusudi la kumtumikia Mungu na kutimiza kusudi lake au mapenzi yake kwa hiyo Muda ni wa maana sana kwa watu waliookoka na haupaswi kupotezwa bure, watu wanaopoteza muda wanaitwa wasio na hekima au wajinga, ni lazima tujiangalie tunautumiaje Muda hasa sisi waafrika, tunaweza kutumia muda mwingi sana kupiga soga ua kusengenya muda ambao tungeweza kuutumia kwaajili ya Mungu, kwa kuyajua mapenzi yake na kuyafanya

 

Waefeso 5:15-17 “Basi angalieni sana jinsi MNAVYOENENDA; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana.”

 

9.       Ni wajibu wetu kuenenda vilevile kama tulivyompokea Kristo – Kuenenda vile vile kama tulivyompokea Kristo hakumaanishi ubaki vilevile baada ya kuokoka, lakini maana yake kila siku tunapaswa kuishi vile vile sawasawa na mafundisho tunayoyapokea kwa Bwana wetu Yesu Kristo kupitia Mwalimu wa Kweli Roho Mtakatifu, huku ni kuendelea kudumisha uhusiano wetu na Mungu kwa kutii na kujileta katika neema yake kukua katika upendo, unyenyekevu na hekima na kuhakikisha kuwa haturudi nyuma tangu tulipoanza uhusiano wetu na yeye.

 

Wakolosai 2:6-7 “Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, ENENDENI vivyo hivyo katika yeye; wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani.

 

10.   Ni wajibu wetu kuenenda kwa kuikulia neema – Tumeokolewa kwa neema sisi kama wana wa Mungu ni wana wa neema kwa msingi huo hatuna budi kukua kwa kuikulia neema ya Mungu ni neema ya Mungu ndiyo inayotusaidia katika, kuukulia wokovu na kukomaa kiroho kwa hiyo hatuna budi kujitoa sisi wenyewe na kuenenda kwa kuikulia neema kwa kuendelea kutenda mema

 

Waefeso 2:8-10 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili TUENENDE NAYO.”

 

Mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana!

 

Wokovu ni Msaada wa Mungu kwetu, hata hivyo tabia na mwenendo ni wajibu wetu na ndio maana neno la Mungu linasema mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, ni wajibu wetu kujitoa kwa Mungu na kukubali neema ya Mungu ituendeshe katika maisha haya kama watoto wake uili tuweze kuwa na mvuto hapa ulimwenguni, mwenendo wetu una nafasi kubwa mbili, kuimarisha uhusiano wetu wa ndani na Mungu, na pili kuwavutia wengine au kuwafundisha kivitendo jinsi Mungu alivyo mwadilifu, kuenenda kama ulivyo wajibu wetu kwa Bwana kumpa Mungu heshima inayoonyesha kuwa Mungu anabadilisha  maisha ya watu wake, tunaweza kuitangaza injili hata bila kusema neno kupitia tu mwenendo mwema, aina binadamu wote duniani wanajua kiwango cha uadilifu ambao watu wa Mungu wanapaswa kuenenda na ndio maana ukifanya mambo ya ajabu wanajua, kutokana na umuhimu wa jambo hili Paulo mtume aliwaombea sana wakolosai wajazwe maarifa, na hekima na ufahamu wa rohoni ili waenende kama ulivyo wajibu wao kwa Bwana wakimpendeza kabisa sio hivyo tu wakiwavutia watu wengine wasioamini waweze kuokolewa ili hayo yatimie hatuna budi kujitoa na kuhakikisha vile vile tunajileta wenyewe kanisani katika ibada za mafundisho ili tukutane na neno la Mungu litakalotupoa hekima na maarifa ili tujue nemna inavyotupasa kuenenda

 

Wakolosai 1:9-11 “Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni; MWENENDE KAMA ULIVYO WAJIBU WENU KWA BWANA, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu; mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha; mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru.”

 

1Petro 3:1-2 “Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa MWENENDO wa wake zao, pasipo lile Neno; wakiutazama MWENENDO wenu safi, na wa hofu.”

 

Mwenendo ni msingi muhimu sana katika maisha ya Ukristo, ni lazima kila Mkristo awe na mwenendo unaomuakisi Yesu Kristo na hii ni kanuni Muhimu sana katika maisha ya ukristo na mwenendo wa kibiblia, mwenendo mwema mbele ya watu wasiomjua Mungu huwavutia watu wengine wapate kuokolewa, na sio hivyo tu ni mwenendo ndio unaotusaidia kupata viongozi wa kanisa ambao mfano wao unaweza kuigizwa na wengine mwenendo unatajwa kama hekima na tabia nzuri, unatajwa kama utetezi tunaposingiziwa, unaonyesha kielelelzo kama viongozi katika nyumba ya Mungu kwa hivyo tukiwajibika vizuri kwa Bwana tutawavutia watu kukubali ukweli ya kuwa Mungu anaokoa na anabadilisha watu wake kwa sababu watu wataona mabadiliko makubwa ya mwenendo wetu.

 

Yakobo 3:11-13. “Je! Chemchemi katika jicho moja hutoa maji matamu na maji machungu? Ndugu zangu, Je! Mtini waweza kuzaa zeituni, au mzabibu kuzaa tini? Kadhalika chemchemi haiwezi kutoa maji ya chumvi na maji matamu. N'nani aliye na hekima na ufahamu kwenu? Na aonyeshe kazi zake kwa MWENENDO wake mzuri, katika upole wa hekima.”

 

1Timotheo 4:12 “Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na MWENENDO, na katika upendo na imani na usafi.”

 

1Petro 2:12 “Mwe na MWENENDO mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa.”

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: