Jumapili, 6 Septemba 2026

Nafsi yangu imeokoka kama ndege!


Zaburi 124:6-8 “Na ahimidiwe Bwana; Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao. Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka. Msaada wetu u katika jina la Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.”




Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa na hekima na maarifa yatakayokusaidia kujua namna inavyokupasa kuenenda katika ulimwengu huu wenye hila nyingi, ili uweze kujihami na kuwa salama, Katika maisha haya yenye maadui wengi!

Wakati mwingine katika maisha watakuwepo watu wenye hila, ambao kimsingi, watataka kukudhibiti, au kukuwekea mipaka katika maisha, huduma, biashara, masomo na kazi na hata kutaka kukupotezea muda kukutawala na kukukandamiza ili uwatumikie au kile kitu ambacho Mungu amekiweka ndani yako kisiweze kufanya kazi katika mazingira makuu  ya uhuru yaliyokusudiwa na Mungu au ili wewe usitoke kimaisha na ikiwezekana uendelee kuwa mtumwa wa kazi wajibu na fikra za mtawala mjanja ambaye anaweza kukunyima njia ya kujichagulia, kukunyima uhuru wa kujitegemea kuwa na maamuzi yako mwenyewe na kujiendeleza kwa sababu ya hofu yake, wivu wake au mawazo machafu hila na wao ndio wawe na maamuzi juu ya maisha yako siku zote angalia:-

Kutoka 1:8-11 “Basi akainuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu. Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi. Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii. Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi

Hali kama hii ndio ilikuwa sababu kubwa ya mtawala mpya katika Misri kuwaogopa Israel na kuanza kuweka mitego ya kuwadhoofisha ili ikiwezekana waweze kumezwa na wamisri na kufutika juu ya uso wa Dunia, kama sio mkono wa Mungu ulioonyooshwa na kuwatetea isingelikuwa rahisi Israel kutoka Misri, Hali hii sio stori ya Israel tu ni stori ya kila mtu amwaminiye Mungu duniani katika mikono ya adui yetu mkuu shetani na maajenti wake ambaye ndiye anataka kuitawala nafsi yako!.

Daudi na watu wake wanamshukuru Mungu kwa ukombozi wake na kwa mkono wake ulionyooshwa hata kuwapa Israel ushindi, inaonekana wazi kabisa ujanja wa adui ulikuwa wa kimkakati na wenye ulaghai mwingi sana, adui alikuwa amejipanga kuwatumikisha watu wa Mungu na  kuwabana kiasi ambacho wasingeliweza kupata msaada; mwenyewe anaona mpango wa adui ulikuwa ni kuwameza wakiwa hai, Kumezwa ukiwa hai ni kuchukuliwa mateka na kunyimwa uhuru wako huku ukiteswa nafsi yako  na kutumikishwa  ukiwa umefungwa kabisa kiasi ambacho ni mpaka usaidiwe na mtu wa nje hivi ndivyo adui alivyokuwa amemkusudia Daudi na jamii yake iliyokuwa ikimzunguka. Ona:-

Zaburi 124:1-5 “Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi, Israeli na aseme sasa, Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi, Wanadamu walipotushambulia. Papo hapo wangalitumeza hai, Hasira yao ilipowaka juu yetu Papo hapo maji yangalitugharikisha, Mto ungalipita juu ya roho zetu; Papo hapo yangalipita juu ya nafsi zetu Maji yafurikayo

Daudi anaizungumzia hali iliyoikuta nafsi yake na jamii yake sawa na ndege aliyetegewa mtego kisha akakamatika na kuwekwa tunduni, ndege huyu angekosa uhuru wake na maamuzi yake na angetawaliwa maisha yake yangekuwa chini ya amri ya aliyemkamata na kumwekea mtego tu, kama ndege asiyekuwa na nguvu katika mikono ya utawala wa watega mitego isingekuwa rahisi kupata ukombozi mpaka mtu mwenye nguvu zaidi aje akukomboe, Kwa hiyo Daudi na wenzake wanauona wokovu walioupata kuwa sio swala la kubahatisha  bali ni tendo la Mungu mwenye nguvu kuingilia kati na kuivunja mitego ya adui na ndipo nafsi zao zikaokoka na ndio maana katika Zaburi hii anamhimidi Bwana ambaye alizuia kwa namna zote wao kuwa mawindo ya adui na kuwaokoa:-

Wakolosai 1:13-14 “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;”

Leo katika mpango wa Mungu tutachukua muda kujifunza somo hili “Nafsi yangu imeokoka kama ndege” kwa kuzingatia vipengele vitatu muhimu vifuatavyo:-

 

·         Ndege katika mtego wa wawindaji.

·         Nafsi katika mitego ya wawindaji.

·         Nafsi yangu imeokoka kama ndege.

 

Ndege katika mtego wa wawindaji.

Zaburi 124:6-8 “Na ahimidiwe Bwana; Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao. Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka.  Msaada wetu u katika jina la Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.”

Ni muhimu kufahamu kuwa kama kuna viumbe wameumbwa wakiwa na uhuru wa asili, basi Ndege ni kiumbe aliyeumbwa akiwa na uhuru huo wa asili, wana uhuru wa asili na mpana sana waliopewa na Mungu, lakini sio hivyo tu ni viumbe ambao Mungu anawajali kiasi kwamba hawana hofu ya maisha, Mungu mwenyewe anawalisha na kuwatunza kwa kiwango cha ajabu sana, Ndege wana ulinzi wa ajabu sana kwa mujibu wa Biblia hakuna ndege anayeanguka bila mbingu kuwa na taarifa, kwa hiyo ndege ni kiumbe chenye ulinzi wa ajabu kutoka kwa Mungu.

Mwanzo 1:20-22 “Mungu akasema, Maji na yajawe kwa wingi na kitu kiendacho chenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu. Mungu akaumba nyangumi wakubwa, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho, ambavyo maji yalijawa navyo kwa wingi kwa jinsi zao, na kila ndege arukaye, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akavibarikia, akisema, Zaeni, mkaongezeke, mkayajaze maji ya baharini, ndege na wazidi katika nchi.”

Mathayo 6:25-26 “Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao?

Mathayo 10:28-31 “Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum. Je! Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu; lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi; bora ninyi kuliko mashomoro wengi.”

Unaona Mungu amewaumba ndege wawe na uhuru mpana wa asili, waitamalaki dunia vyovyote wapendavyo, Ndege wanatunzwa na Mungu, hawaangaiki kulima wala kuweka ghalani, lakini Mungu anawalisha, wana furaha wana amani, lakini zaidi ya yote Mungu anawajali kiasi ambacho hawaanguki chini bila mbingu kuwa na taarifa, Lakini changamoto kubwa ya ndege ni wawindaji, Mwanadamu ni kiumbe wa maana zaidi kuliko ndege, Mungu anamjali mwanadamu katika namna isiyoweza kuelezeka Mwandishi mmoja mpka akamuhoji Mungu, Mtu ni kitu gani hata umwangalie

Hata hivyo adui mkubwa wa mwanadamu ni mwanadamu, Mwanadamu ambaye wakati wewe ukiwa huna madhara kwa mtu wala huwazii mabaya juu ya mtu, wawindaji wanakuwazia mabaya na wanataka kuitega nafsi yako, Ndege ni kiumbe dhaifu sana na kuna watu wanataka kumkamata ili wamweke katika tundu, hapo wanataka ndege awe na uhuru finyu, na walimshe wao badala ya Mungu, huu ndio mkakati wa shetani, yeye anataka kuikamata nafsi yako, aifunge akutumikishe usifurahie ule uhuru na maisha uliyopewa na Mungu, leo hata kama nasfi yako imekamatika ninakutangazia kuwa ni siku ya kwenda kuzifungulia nasfi zilizofungwa na kuwekewa mipaka katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai.

Wawindaji sio watu wazuri hata kidogo, wao mpango wao ni kuikamata nafsi yako, na hili ndilo jangwa kubwa sana la kiroho hapa duniani  yaani pale nafsi yako inapokuwa imekamatika, Maandiko yanaonyesha kuwa mtu akifanikiwa kuiteka nafsi yako hususani kama ni adui anaweza kukuweka katika hali ya hatari kubwa sana na kusababisha uharibifu mkubwa wa kiroho na kuitishia usalama wako na kukukosesha amani katika maisha, Waandishi wa Zaburi mara kwa mara wameonyesha kuwa adui anaziwinda nafsi zetu na ili uweze kupata msaada kama umekamatika au unawindwa basi ni Mungu peke yake  ndiye anayeweza kukusaidia na kukuokoa na kuirejesha nafsi yako katika uhuru wake ona:-

Zaburi 7:1-2 “Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe, Uniokoe na wote wanaonifuatia, uniponye. Asije akaipapura nafsi yangu kama simba, Akiivunja-vunja pasipokuwa na wa kuponya.”

Zaburi 59:1-3 “Ee Mungu wangu, uniponye na adui zangu, Uniinue juu yao wanaoshindana nami. Uniponye nao wafanyao maovu, Uniokoe na watu wa damu. Kwa maana wanaiotea nafsi yangu; Wenye nguvu wamenikusanyikia; Ee Bwana, si kwa kosa langu, Wala si kwa hatia yangu.”

Mwandishi wa Zaburi hii Daudi anazungumza kwa lugha ya fumbo au lugha ya kimashairi akilinganisha maisha yake au nafsi yake kama maisha ya ndege, Ndege ni viumbe dhaifu sana na hawana nguvu ya kujitetea  na wala wengi hawajui kama wanawindwa au wana maadui, moyo wa ndege wengi ni moyo mwororo na mnyoofu ndege hawana neno na mtu wao wanapoamka asubuhi hawafikiri kufanya uadui na mtu, wao huamka na kumtukuza Mungu kisha kuendelea na majukumu yao ya kila siku, hawajui kama kuna mtu ataamka na kuwawekea mtego, wala hawajui kuwa kuna mtu ataamka na kuwageuza wao kuwa mfugo au kitoweo au kuwafungua katika tundu hawajui kama kuna wawindaji, ni muhimu ukaishi maisha yako lakini uwe makini na wawindaji, wawindaji wako kila mahali!

Lugha hii anayoitumia mwandishi wa Zaburi inawahusu watu wanaomcha Mungu, wengi wanawindwa nafsi zao lakini hawajui, wengi huamini kila mtu na wakati mwingine hawajui kama kuna mtu anaweza kuwa adui na kuziwinda nafsi zao, Ndege anawakilisha udhaifu wa mwanadamu, Hakuna mwanadamu mwenye nguvu ya kuvunja mitego ya adui Shetani na hata kujiokoa katika mikono yake, Shetani hutumia njia mbalimbali katika kuhakikisha kuwa unaingia kwenye mitego yake ikiwa ni pamoja na kuitumia hofu, magonjwa, dhambi, mauti,  na mashambulizi makali kutoka kwa majeshi yake ya pepo wabaya na watumishi wake wanadamu yaani maajenti wake, waganga, wachawi,  wanga, wenye hila na wenye wivu,Tunapoishi duniani fahamu na kuelewa kuwa wewe ni dhaifu kama ndege na bila masaada wa Mungu ni vigumu kwako kuwa huru kama Mungu mwenye nguvu hatakulinda na kukuepusha na mitego ya wawindaji, kila kitu duniani ulicho nacho kinawindwa, wewe hujui, ndoa yako inawindwa, kazi yako inawindwa, cheo chako kinawindwa, mali zako zinawindwa, biashara yako inawindwa, familia yako inawindwa, masomoni, unawindwa, huduma yako inawindwa, wawindaji ni watu wenye uchungu, ni wenye wivu, ni wenye nia mbaya, ni wenye hila na wamejaa kila mahali duniani, hata kwenye genge lako la nyanya pale sokoni, unawindwa, kama ndege katika mtego wa wawindaji, Bwana akupe neema kuigundua mitego yote unayotegewa na akuokoe na mitego ya wawaindaji katika jina la Yesu Kristo sema ameeeen!

Nafsi katika mitego ya wawindaji

Tumeona kuwa maisha ya mwanadamu ni kama maisha ya ndege katika mitego ya adui, na kinachowindwa katika maisha yetu mara tu baada ya kuzaliwa kwetu ni Nafsi, Neno nafsi katila lugha ya kiebrania ni “Nephesh” ambalo linamaanisha uhai, nafsi au mtu wa ndani, mwanadamu ana sehemu kuu tatu Mwili, Nafsi na Roho, vita vyetu vyote vya kiroho na kimaamuzi vinafanyika katika nafsi, nafsi inaponaswa katika mtego ambao unajulikana kama “Pach” Kiebrania ikimaanisha “tanzi”, au mbinu za kunasia, na wawindaji wanaitwa “Yagosh” Kiebrania yaani  watu wenye hila au wanasao kwa hila, wenye wivu, wenye uchungu, wasiopenda maendeleo yako, sasa nafsi inapokamatwa unaingizwa katika utumwa wa mwindaji na huwezi kuachiwa mpaka Mungu aingilie kati, mtu anapokuendea kwa mganga kukuroga maana yake anaitafuta nafsi yako aikamate na kuielekeza kule anakotaka yeye, nafsi yako ikikamatwa unaingia utumwani unamezwa ukiwa hai unapoteza uhuru uliokusudiwa na Mungu katika maisha yako!, unaona maisha yako ni kama yako gizani nafsi yako imekalishwa mahali penye giza, watu wamekufunga, umekuwa kama ndege katika tundu unafugwa badala ya kuwa na uhuru wako mpana wa asili uliokusudiwa na Mungu!

Zaburi 143:3-4 “Maana adui ameifuatia nafsi yangu, Ameutupa chini uzima wangu. Amenikalisha mahali penye giza, Kama watu waliokufa zamani. Na roho yangu imezimia ndani yangu, Moyo wangu ndani yangu umesituka.”

Adui wanapoipata nafsi yako kila kitu ndani yako na mali yako kinachukuliwa mateka na nafsi yako ndiyo inayoteseka, na maisha yako yanaharibiwa unatupwa chini, unawekwa kwenye giza na unakuwepo duniani lakini ni kama mtu aliyekufa, wawindaji wakiishika nafsi yako wanajivunia majivumo makubwa wanatamba kuwa wamekuweza na huwezi kufurukuta tena, wamekuweka kwenye kiganja, wokovu wako au ukombozi wako ni mpaka Bwana pekee aingilie kati, nafsi ikishikwa unakuwa mtumwa huwezi kufanya unalotaka wala huwezi kufanya mapenzi ya Mungu bali utafanya kile nafsi yako inakokukokota na adui zako wanakokupeleka, utasikia yule sisi tumemuweka kwenye kiganja ujue wameishika nafsi yako, Utasikia Bosi mimi haniambii kitu nimemuweka hapa! ahaa nafsi imeshikwa, Makahaba wanaoiba waume za watu huwa wanatafuta kuwashika nafsi, wakishawashika, mumeo harudi kwako kwa watai, fedha anapeleka huko, anapewa raha za ajabu na kupikiwa vizuri ili wewe usahau familia yako na umtese mkeo wako kwa nini changamoto nafsi ikishatekwa umetekwa maisha yako yote, ukitaka kumtumikisha mtu mshike nafsi yake, watu wengi wameshikwa na wanatumika wakati mwingine bila kupenda!

Farao alipowakamata Israel na kuwaweka kwenye tundu la utumwa nani angeweza kuwafungulia? Ni mpaka mwenye nguvu alipoingilia kati na kushughulika na adui ndipo Bwana alipowaweka huru! Ona  

Kutoka 15:6-13 “BWANA, mkono wako wa kuume umepata fahari ya uwezo, BWANA, mkono wako wa kuume wawaseta-seta adui. Kwa wingi wa ukuu wako wawaangusha chini wanaokuondokea, Wapeleka hasira yako, nayo huwateketeza kama mabua makavu. Kwa upepo wa mianzi ya pua yako maji yalipandishwa, Mawimbi yakasimama juu wima mfano wa chungu, Vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari. Adui akasema, Nitafuatia, nitapata, nitagawanya nyara, Nafsi yangu itashibishwa na wao; Nitaufuta upanga wangu, mkono wangu utawaangamiza. Ulivuma kwa upepo wako, bahari ikawafunikiza; Wakazama kama risasi ndani ya maji makuu. Ee BWANA, katika miungu ni nani aliye kama wewe? Ni nani aliye kama wewe, mtukufu katika utakatifu, Mwenye kuogopwa katika sifa zako, mfanya maajabu? Ulinyosha mkono wako wa kuume, Nchi ikawameza. Wewe kwa rehema zako umewaongoza watu uliowakomboa, Kwa uweza wako uliwaelekeza hata makao yako matakatifu

Unaona Israel waliposhikwa ni Bwana ndiye aliyekuja kuwatoa, leo ni siku ambayo kila ambaye ameshikilia nafsi yako anaiachia kwa mkono wa Bwana ulio hodari ulioonyooshwa katika jina la Yesu!

Nafsi yangu imeokoka kama ndege

Zaburi 124:6-8 “Na ahimidiwe Bwana; Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao. Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka.  Msaada wetu u katika jina la Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.”

Mwandishi anaijua historia na mbinu ya adui kuwa anachikotafuta ni nafsi na anaelewa wazi kuwa nafsi inawindwa kama ndege na kuwa wenye hila huweka mitego yao ili kutunasa kama ndege na wokovu wako unaweza kuja kwa namna mbili aidha Mungu akuokoe usiwe mawindo, ASIYETUTOA KUWA MAWINDO KWA MENO YAO au kama umekamatika AUVUNJE MTEGO, Daudi anaonyesha kuwa kutokuingia katika mtego sio kwa sababu ya ujanja wetu bali kwa sababu ya ulinzi wa Mungu na kama umeingia katika mtego kutoka sio kwa uwezo wako bali mtego umevunjika na mtego huo hauvunjiki wenyewe ni kwa msaada wa Bwana, hii maana yake ni nini mwenye uwezo wa kuvunja nguvu za adui zetu ni Mungu aliyeziumba mbingu na nchi, Ni Mungu pake yake anayeweza kukuokoa na mauti, Ni Mungu peke yake anayeweza kukuokoa na dhambi, na ni Mungu pake yake anayeweza kumshinda Shetani kwa niaba yetu na ni yeye anayeweza kuwa msaada kwa nafsi zetu, na ndege akitoka mtegoni huwa harudi tena, mtegoni, Amani ya kweli inamkalia, furaha ya moyo inarudi mzigo wa utumwa unakuwa mwepesi kwa wokovu wake, ndege hawana mikono wanahitaji mkono wa Mungu, wanapowekwa tunduni hawawezi kutoka wenyewe mpaka mwenye huruma awafungulie, leo mwenye huruma ataifungua nasfi yako, mwenye huruma atakuepusha na mtego, wengine wamekamatwa na dini, wengine ulevi, wengine uraibu wa madawa ya kukevya na ukahaba lakini yuko anayeweza kukuweka huru, popote pale ambapo nafsi yako imeshikwa Yesu yuko tayari kukufungua.

Yohana 8:31-36 “Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru. Wakamjibu, Sisi tu uzao wake Ibrahimu, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wo wote; nawe wasemaje, Mtawekwa huru? Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Wala mtumwa hakai nyumbani sikuzote; mwana hukaa sikuzote. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.

Mathayo 11:28-30 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”

Mwandishi wa zaburi hii anaiona kazi ya kuingilia kati na kuisaidia nafsi ya mwanadamu ni ya Mungu na ni yeye anayestahili kuhimidiwa na kutukuzwa hakuna mwanadamu mwenye mchango wowote katika kazi ya ukombozi wa mwanadamu zaidi ya kuokolewa kwa neema, mwanadamu ni dhaifu sana bila Mungu, hila za shetani ziko kuishambilia nafsi ya kila mmoja wetu ili aimeze lakini Mungu kwa rehema zake ndiye anayeweza kuuvunja mtego wa adui zetu au kutufungulia na tukaruka zetu angani tukiwa huru kama ndege, kila mtu aliyeokolewa anapaswa kujua wazi kuwa ni kwa neema tu na ni kwa msaada wa Mungu tunaokolewa, Mungu amekusudia tuwe na uwanda mpana wa kuufurahia uwepo wake na sio kufungiwa kwenye tundu kama ndege asiye na uhuru, Shetani anatumia mitego iliyojificha kuliko mashambulizi ya wazi na ni Mungu peke yake anayeweza kukusaidia kwanza usiingie katika mtego wa adui na kuwa mawindo, pili kama umenaswa kuuvunja mtego ili uweze kuwa huru, Ndege hana nguvu yoyote ya kwake ya kumsaidia kujifungulia mtego, Lakini yuko anayeweza kututunza tusiingie mtegoni na kama umeingia anaweza kutufungulia!, Mpenzi je wewe uko katika hali ya namna gani Umenaswa? Au unataka kunaswa? Bwana akupe neema na kukuhurumia asikuache kuwa mawindo kwa meno yao nafsi yako iokoke kama ndege katika mtego wa wawindaji na mtego uliokukamata uvunjike katika jina la Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai haleluyaaaaaaaaaaa

Zaburi 124:6-8 “Na ahimidiwe Bwana; Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao. Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka.  Msaada wetu u katika jina la Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.”

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wawajenzi mwenye Hekima