Ijumaa, 18 Septemba 2026

Kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka!


Kutoka 1:8-12. “Basi akainuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu. Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi. Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii. Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi. Lakini kwa kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka na kuzidi kuenea. Nao walichukiwa kwa sababu ya wana wa Israeli.”


Utangulizi:

Ni muhimu ikafahamika tena na tena kwa wanadamu wote Duniani kuwa kusudi la Mungu kwa mtu yeyote duniani haliwezi kubatilishwa na mtu awaye yote hata kama mtu huyo ana nguvu kuliko tunavyofikiri, Stori ya wana wa Israeli Kutoka Misri inaanza kwa kuinuka kwa mfalme mpya ambaye kwa ujeuri tu alijifanya hafahamu Historia  na mchango wa Yusufu katika nchi ya Misri, Kwa hofu yake dhidi ya Waisraeli anapanga njama na kukusudia kuwatesa na kuwakandamiza Israel ili ikiwezekana waangamie na kupotelea mbali, Lakini jambo la kushangaza ni kuwa “Kadiri walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka”, Kanuni ya Mungu hapa inatenda kazi ya kuwa huwezi kumlaani Mtu ambaye Mungu amembariki, na huwezi kumshusha mtu ambaye Mungu amemuinua.

Hesabu 23:5-8 “Bwana akatia neno katika kinywa chake Balaamu, akasema, Umrudie Balaki; ukaseme maneno haya. Akarudi kwake, na tazama, amesimama karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, yeye na wakuu wote wa Moabu pamoja naye. Akatunga mithali yake, akasema, Balaki amenileta kutoka Aramu, Mfalme wa Moabu kutoka milima ya mashariki, Njoo! Unilaanie Yakobo, Njoo! Unishutumie Israeli. Nimlaanije, yeye ambaye Mungu hakumlaani? Nimshutumuje, yeye ambaye Bwana hakumshutumu?

Mamlaka ya Mungu ni kubwa kuliko mamlaka za kibinadamu, uweza wa Mungu ni mkuu kuliko uweza wa wenye kuonea, Rehema za Mungu ni kubwa kuliko matendo ya wenye dhuluma, Njama za kibinadamu haziwezi kushindana na mpango kazi na mpango mkakati wa Mungu, Hofu ya mfalme wa Misri ilikuwa kubwa kwa sababu Mungu alikuwa amewabariki Israel na wakawa wengi na wenye nguvu kuliko Wamisri, si kuwa watu hao walikuwa waovu bali walikuwa wanastawi na ustawi wao ukawa ni tishio kubwa kwa wamisri na mfalme wao, lakini katika namna ya kushangaza sana Kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka!, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele muhimu vitatu vifuatavyo:-


·         Jinsi Baraka za Mungu zinavyokufanya uwe tishio.

·         Kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka!.

·         Kusudi la Mungu haliwezi kufutwa na wivu wa wanadamu.


Jinsi Baraka za Mungu zinavyokufanya uwe tishio.

Ni muhimu kufahamu kuwa Israel kushuka kule Misri halikuwa tukio la bahati mbaya bali ulikuwa ni mpango wa Mungu, Mungu alimweleza wazi rafiki yake Abrahamu kuwa uzao wake utashuka Misri na kukaa huko kwa muda mrefu na kisha baadae angeliwapandisha katika inchi ya Kanaani nchi ambayo Bwana alikuwa amemwapia Ibrahimu ya kuwa atampa yeye na uzao wake.

Mwanzo 15:13-16 “BWANA akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali mengi. Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema. Na kizazi cha nne kitarudi hapa, maana haujatimia uovu wa Waamori bado.”

Kwa hiyo aliyopitia Israeli ulikuwa ni mpango na makusudi ya Mungu, Mungu alikuwa amefanya agano na Ibrahimu na Isaka na Yakobo kuhusu wao na uzao wao, kwa sababu hiyo isingelikuwa rahisi agano hilo kuvunjika kwa sababu yoyote ile, Mungu aliwabariki sana  na kuwapa mafanikio makubwa, Kimsingi Israel hawakuwa watu waovu walikuwa wema na watu wa Mungu hata hivyo walichukiwa kwa sababu Mungu alikuwa amewabariki, na Mungu aliwapa ustawi mkubwa, hata leo hii Mkono wa Mungu unapokuwa juu yako kwa sababu zozote zile mafanikio yako yatazaa wivu, chuki na upinzani na wakati mwingine majaribio ya kipumbavu ya watu kutaka kukuangamiza hili ni jambo la kawaida kwa mujibu wa mafundisho ya kibiblia Baraka zako zitakufanya uogopwe na kuwavutia maadui wenye wivu

Kutoka 1:7-10 “Na wana wa Israeli walikuwa na uzazi sana, na kuongezeka mno, na kuzidi kuwa wengi, nao wakaendelea na kuongezeka nguvu; na ile nchi ilikuwa imejawa na wao. Basi akainuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu. Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi. Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii.”

Unaona! Mungu anapokupenda na kuwekeza kitu cha ziada ndani yako watu hawapendi na hawawezi kufurahi na kwa sababu hiyo watatumia mamlaka zao na nguvu zao na hila zao na ubinadamu wao kukuletea upinzani au kujaribu kuharibu mpango wa Mungu ulioko ndani yako lakini jambo la ajabu ni kuwa kila wakati watakapojaribu kufanya hivyo wewe utaongezeka na hutazoofika lakini wao kwa upande wao watadhoofika na kupata hofu kubwa zaidi, kanuni hii imejitokeza mara kadhaa katika maisha ya watu wa Mungu na kwako sio jambo la ajabu ona;-

Mwanzo 26:12-16 “Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, BWANA akambariki. Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu. Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi. Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi.”

1Samuel 18:6-9 “Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.”

Daniel 6:1-5 “Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote; na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara. Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote. Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake. Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake.”

Unaona mkono wa Mungu unapokuwa juu yako, watu wanaweza kukuogopa, wanaweza kukufukuza, wanaweza kukuonea wivu na wanaweza kutengeneza majungu dhidi yako, kama uko au unazungukwa na watu wa mwilini hata mnaosali pamoja kanisani na wengine wanaweza kuwa na cheo kikubwa kabisa kuliko wewe na lakini ukuu wa Mungu ulioko ndani yako unawogopesha, unaonekana kama unaweza kuwa na madhara kwao hata kama huna lengo wala nia ya kuwadhuru, wataogopa sana wakiona mioyo ya watu inaambatana nawe, watajaribu kukufukia na kukukandamiza na hata kukusema ili uonekane kuwa wewe sio kitu lakini kama mkono wa Mungu uko juu yako na wewe ni uzao wa agano lake hawatakuweza na kadiri wanavyokutesa ndivyo unavyozidi kuongezeka  na kuwa tishio               

Kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka!

Biblia inatuonyesha kanuni ambayo iko kinyume na mtazamo wa kibinadamu, kadiri Mfalme wa Misri alivyokuwa akifanya mpango wa kuwaangamiza Israel ndivyo Israel walivyozidi kuongezeka na kustawi sana, ingetegemewa kuwa mbinu ya chuki na njama za Farao zingeliweza kuwa na mafanikio makubwa na kuwafanya Israel kuwa dhaifu lakini hata hivyo Mungu alifanya kinyume na matazamio yake, Mungu hugeuza laana kuwa baraka, Waliwatesa ili wasiongezeke lakini Israel waliongezeka, waliwaumiza ili wasiwe na nguvu lakini wakawa na nguvu zaidi, waliwadhalilisha lakini Mungu aliwaheshimisha, walitaka kuwaua watoto wao lakini wanawake walizaa kwa uhodari, waliwakandamiza lakini Mungu aliwainua Mungu alisimamia kusudi lake na Agamo lake alilofanya na Ibrahimu.

Mwanzo 12:1-3 “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”

Mpango wa Mungu kwa maisha yetu uko Dhahiri kiimani na kihistoria na kivitendo, Mungu anapokuwa amekusudia kukubariki hakuna mtu anaweza kuufuta mpango huo, wakati watu wanataka kukushusha Mungu atakupandisha kwa nguvu, hakuna mbinu, njama wala silaha au hila itakayoweza kufanikiwa dhidi yako, Mungu atakubariki kupitiliza na utatoboa kimaisha utafanikiwa na utapanda juu sana na adui zako watakuogopa kila watakapojaribu kukushambulia watashambuliwa vikali na nguvu iletayo wokovu juu yako na kimsingi utaongezeka, mfano huu ni Dhahiri katika maisha yetu na katika taifa la Kiyahudi kwa sababu ya agano lake alilofanya na  baba yetu Ibrahimu

Mwaka 1967 mwezi June kuanzia Tarehe 5 mpaka Tarehe 10 pale mashariki ya kati palitokea vita kali sana kati ya Muungano wa mataifa ya kiarabu ikiwemo Misri, Jordani, na Syria na baadaye Iraq dhidi ya Israel, mataifa haya yalikuwa na mpango kabambe wa siri wa kuishambulia Israel na kuifuta katika ramani ya dunia kila taifa lilijiandaa thabiti kuhakikisha kuwa watu wakiamka asubuhi hakuna Israel, Katika namna ya kushangaza Israel iliwapiga vikali sana jirani zake na kupata ushindi wa ajabu ulioifanya Israel kuongezeka kiramani mara dufu zaidi, Israel iliendesha oeperesheni iliyoitwa kwa kiingereza “Operation Focus”  na kuipiga vibaya Misri na kuiteka ghuba ya Sinai, Jodran ilipigwa vibaya na kuachilia ukanda wa Gaza, huku Syria ikipoteza Milima ya Golan pamoja na hayo Misri ilipoteza ndege vita zaidi ya 338 masaa ya mwanzo tu ya vita, Sryria ikipoteza ndege vita 73 na Jordani ndege 29 Iraq ambao nao walijiunga baadae kwa kusudi la kujihami walipoteza ndege 29 Israel ikaibuka mshindi wa vita ile huku ikiwa imeongeza mipaka yake yote ikiwa na udhibiti kamili wa maeneo hayo waliposhambuliwa zaidi walijiongeza! Unaona

Kwa nini nimetoa mfano huo mtu wa Mungu usiogope kadiri adui zako wanavyojaribu kukusumbua na kukuundia zengwe wewe utazidi kuongezeka na hofu kubwa itawakalia wao, wewe utaendelea kustawi kama Israel inavyostawi leo, hakuna mtu atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako, wanadamu wanaweza kupinga kusudi la Mungu lilioko ndani yako lakini kamwe hawawezi kuufikia mpango wa Mungu ulioko juu yako kwa sababu wewe umebarikiwa! Kadiri wanavyopigana na wewe ndivyo na wewe unavooongezeaka!

Isaya 54:14-17 “Utathibitika katika haki; utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa; na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia. Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako. Tazama, nimemwumba mhunzi avukutaye moto wa makaa, akatoa silaha kwa kazi yake; nami nimemwumba mharibu ili aharibu. Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.”

Ayubu 42:1-2 “Ndipo Ayubu akamjibu Bwana, na kusema. Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.”     

Adui zako watakapojaribu kukushambulia na hatimaye watagundua kuwa hauwezekaniki na kuwa mkono wa Bwana uko juu yako watakuogopa kwa sababu watabaini ya kuwa Bwana Mungu wako yuko pamoja nawe

1Samuel 18:12-16 “Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli. Kwa ajili ya hayo Sauli akamwondosha kwake, akamfanya awe akida wake juu ya askari elfu; naye akatoka na kuingia mbele ya watu. Naye Daudi akatenda kwa busara katika njia zake zote naye Bwana alikuwa pamoja naye. Sauli alipoona ya kwamba alitenda kwa busara sana, yeye alimwogopa. Lakini Israeli wote na Yuda wakampenda Daudi; kwa kuwa alitoka na kuingia mbele yao.”

Kusudi la Mungu haliwezi kufutwa na wivu wa wanadamu

Ni muhimu kufahamu kuwa kusudi la Mungu ndani yako haliwezi kufutwa na wivu wa wanadamu, Farao alipanga njama za kila aina kujaribu kuwaangamiza Israel lakini kila alichokikusudia kilikuwa kinyume na hakikuweza kufanikiwa hii ni kwa sababu Mungu alikuwa pamoja nao, Mungu akiwa upande wako hakuna mtawala mwenye nguvu, wala mwenye mamlaka wala mwenye kijicheo chochote cha Dunia hii atakayeweza kuuzuia mpango Mungu dhidi yako, walimuuza Yusufu na bado akawa mtawala, walimfukuza Daudi na bado akawa mfalme, walimtupa Daniel shimoni lakini akatukuzwa, walimuua Yesu lakini alifufuka siku ya tatu na kaburi halikuweza kumshika wewe kama mwana wa Mungu na Mungu ana kusudi na wewe usiogope kwa sababu Mungu yuko na yu aweza kukusaidia

Kutoka 1:8-12. “Basi akainuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu. Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi.Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii. Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi. Lakini kwa kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka na kuzidi kuenea. Nao walichukiwa kwa sababu ya wana wa Israeli.”

Kila mtu aliyeko katika nafasi yoyote hapa duniani anapaswa kukumbuka kuwa Mungu ndiye anayetawala hatupaswi kuwa na kiburi na majivuno au kutumia nafasi tulizo nazo kwaajili ya kuwakandamiza wengine, Farao alijifikiri kuwa yeye ndiye mwenye mamlaka na kwa sababu hiyo aliyatumia vibaya dhidi ya Israel, Mungu alikuja kumfutilia mbali katika bahari ya Shamu na historia yake imeandikwa lakini yeye na majeshi yake walifutika, Mungu hataaachilia watu wake waonelewe kamwe na kama mtu anatafuta kupotea aendelee kucheza na watu wanaomtegemea Bwana!

Zaburi 105:14-15 “Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao. Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.”

Kama unamtegemea Mungu na umemfanya Mungu kuwa kimbilio lako, umemfanya bwana kuwa ngao yako, Basi elewa na kukumbuka ya kuwa, hakuna uchawi, wala fitina, wala chuki, wala mateso, wala njama zinazoweza kumuangamiza mtu wa Mungu, au mtu ambaye Mungu ameweka mkono wake, changamoto na mateso tunayoyapitia hayamaanishi kuwa Mungu amewatupa watu wake, Neno la Mungu linaonyesha wazi kuwa Israel walikuwa katika mapenzi ya Mungu lakini walionelewa tu na Mungu alikuja kuingilia kati kwaajili ya utukufu wake, usiwagope wanaokunyanyasa kwa sababu historia yao itafutika upesi, changamoto unazozipitia haziwezi kamwe kufuta mpango wa Mungu, na kwa bahati mbaya sasa kadiri wanavyokutesa ndivyo unavyozidi kuongezeka ila wao hawajui, Farao alipopanga kuwapunguza Mungu alipanga kuwaongeza, Farao alipokusudia kuwadhoofisha Mungu alikusudia kuwatia nguvu, Farao alipodhani kuwa atawamaliza Mungu alikuwa anakusudia kuutimiza mpango wake kwa msingi huo kama unapitia dhiki yoyote ile leo usiogope ni njia ya Mungu ya kukuongeza katika ulimwengu wa roho, kupigana na mtu ambaye Mungu ameweka mkono wake au kumtesa au kumzushia, au kufanya hila  na njama zozote hakuwezi kumfanya Mungu mwenye haki asimtokee Kadiri walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka!

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima


Hakuna maoni: