Ijumaa, 5 Februari 2016

Vijana na Stadi za Maisha



UTANGULIZI.
       Moja ya makundi muhimu katika jamii na ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na jamii pamoja na kanisa ni vijana. Si vema kuwapuuzia, vijana ni kundi muhimu ambalo shetani analitamani sana ili aweze kulitumia Lakini Mungu pia anapenda kuwatumia vijana, kumbuka Bwana Yesu Mwenyewe aliishi maisha ya ujana tu, alisulubiwa akiwa na miaka kama 33.5 Lakini kwa kuwa alipata malezi Mazuri ya kiroho aliweza kusaidia jamii iliyomzunguka na jamii iliyoko leo na hata jamii ijayo kwa mambo muhimu aliyoyafanya, wewe je unautumiaje ujana wako?

      Ni kitu gani unataka jamii ijifunze kutoka kwako haya yoote yatakuwa na umuhimu endapo utafanya kazi ya ziada ya kuutunza ujana wako. Kumbuka kuwa ni wewe mwenyewe mwenye jukumu la kujitunza utu wako na ujana wako. Katika somo hili la Ngome ya vijana Mchungaji Innocent Mkombozi Kamote atakuwa akishughulikia Maswala muhimu ya vijana kimwili na kiroho ili waweze kuukulia wokovu huku wakiwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali katika Maisha Bila kufikia viwango vya kuharibika katika dunia hii yenye changamoto nyingi.

     Mchungaji Kamote ni kijana lakini ameweza kuutumia ujana wake katika kumtumikia Mungu na hivyo amekuwa mlezi mwema wa vijana, kati ya mambo anayoyapenda ni kuielimisha jamii katika yale anayodhani yanaweza kuwasaidia watu Kamote ni Mwandishi wa kitabu Jinsi waislamu wanavyoweza kujibiwa ambacho ni maarufu sana, pia ni mwandishi wa kitabu Jinsi ya kuwa na Amani ya kweli katika ndoa na kitabu cha uchambuzi wa waraka wa waebrania ambacho kinafanyiwa marekebisho kabla ya kutoka!. hiki ni kitabu cha Nne katika uandishi wake na vyote ni vizuri na vina mvuto mkubwa sana Fuatilia Mafundisho haya ya muhimu kwa vijana ambayo pia naamini yaweza kuwa Msaada Mkubwa si kwa vijana tu bali na kila mtu anayependa Kujifunza au kufundisha maswala kuhusu vijana, kitabu hiki kitakuwa ngao au ilinzi kwa vijana kuhusiana na maisha yao ndio maana niliamua kukiita Ngao ya vijana.

    Mchungaji Kamote pia amekuwa mnnenaji hodari katika semina mbalimbali za vijana hususani katika makongamano ya Pasaka ya Casfeta kwa miaka mingi amefundisha masomo kuhusu ujazo wa Roho mtakatifu,Karama za Roho,Maswala ya vijana na  huku akijibu Maswali ambayo vijana huuliza, na jinsi ya kukabiliana na changamoto za kiislamu fuatilia somo hili naamini litakuwa baraka kwako kama ilivyokuwa kwa Masomo yale mengine.Kwa hakika kitabu hiki ni ngome kwa vijana unataka usiharibikiwe soma kitabu hiki Ngome ya vijana. Hamasisha na wengine kukisoma na fundisha yale unayojifunza katika kitabu hiki Neema na amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi.  


Somo la Kwanza;
Vijana na Stadi za Maisha.
       Stadi za maisha ni moja ya masomo muhimu sana kwa vijana kwani huwapa mbinu mbalimbali namna wanavyoweza kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha ili kutunza uhai na uthamani wa maisha, hususani ya vijana; Somo hili hufundishwa pia huko duniani katika Elimu nyingine za kawaida Hapa mchungaji Kamote analifundisha katika Mtazamo wa kibiblia.Stadi za maisha hujumuisha mbinu, maarifa na akili zinazotusaidia katika maisha yetu, Mungu husikitishwa tunapoangamia kwa kukosa maarifa (Hosea 4;6) Katika somo hili tutachambua maarifa ambayo kijana au mtu yeyote anapaswa kuwa nayo ili aishi kwa amani na watu wote na kujiepusha na mambo ya hatari, pia kujibu kweli kadhaa kuhusu maisha.

    Kujitambua;-
      Kila mwanadamu mwenye akili timamu anapaswa kujitambua, Kuna umuhimu mkubwa sana katika kujitambua, Kujitambua ni hali ya kuelewa uthamani ulionao, wewe ni wa thamani kuliko unavyojifikiri lakini kama hujitambui huwezi kulinda uthamani huo ulionao, ili mtu ajue uthamani alionao ni muhimu ujaribu kuwaza kama wewe ungekuwa bidhaa fulani Je thamani yako ingekuwa ni shilingi ngapi? Na ungependelea uwe bidhaa gani? Maswali hayo yatakufanya ujitambue, Paulo mtume alitamani Timotheo aliyekuwa kijana ajitambue uthamani alionao (1Timoth 4;12)
 Ni muhimu kujihoji maswali haya
·         Je?  wewe ni nani?
·         Ndoto zako ni nini katika maisha?
·         Una umuhimu gani kwa Baba yako, mama yako, wadogo zako, nduguzo, Taifa lako, kijiji chako, kabila yako n.k?
·         Wajibu wako katika jamii ni upi?
·         Matarajio na malengo yako katika jamii ni yapi?
·         Jamii yako Inatarajia nini kutoka kwako?
·         Kwa nini ulizaliwa?
·         Je Ni mambo gani yanadumisha ukamilifu wako kimwili, kijamii, kisaikolojia, kiuchumi, na kiroho?
Unapokuwa na majibu ya Maswali hayo hapo juu ndipo unapoweza kutambua uthamani ulio nao na utakua umejitambua. Mtu anapokuwa amejitambua hawezi kuyafanya maisha yake kuwa kitu cha kuchezea atayaheshimu maisha, watu wengi hushindwa kujiheshimu kwa sababu Hajajitambua kuwa yeye ni nani? Na anathamani gani katika dunia hii hajatambua yeye ni wa Muhimu kiasi gani Kwa Mungu na wanadamu; Mungu atupe neema kutambua uthamani wetu Kama yeye anavyotutambua akatuumba tofauti Na mtu yeyote duniani, si unajua kuwa hatufanani kila mmoja ni wa pekee wewe ni wa thamani. Lolote tulifanyalo tutalifanya kwa ujasiri tukijitambua kuwa sisi ni nani. Nehemia alijitambua kuwa yeye ni nani na yuko kwa ajili ya nani hii ilimsaidia kuzikabili changamoto alizokutana nazo katika jamii yake soma. (Nehemia 6; 10-13). Kadiri mtu anavyojitambua na kujua uthamani alionao au umuhimu alio nao katika jamii ndivyo maisha yanavyokuwa na thamani kwake, Kwa bahati mbaya watu wengi wakiwemo vijana hawatambui uthamani walionao na hivyo hujidhulumu nafsi zao au kusababisha hasara kwa wengine jaribu kuwaza juu ya mfano wa dada huyu ambaye hakutambua uthamani wake wala kujifikiri kuwa yeye ni nani.
   Dada mmoja aliyeitwa jina Sophia (Jina zuri la kiyunani ambalo maana yake ni Hekima),Sophia alikuwa ni mtoto wa kwanza wa mkulima mmoja wa matunda wilayani Lushoto,Sophia alilelewa katika maadili mazuri na wazazi wake na kwa msingi huo alikuwa ni mtoto aliyejitunza yaani Bikira jambo ambalo ni nadra sana katika jamii ya nyakati za leo kukuta msichana amejitunza yaani ni bikira asiyejua mume, Binti huyu alisoma masomo yake ya shule ya msingi wilayani Lushoto na alifanikiwa kufaulu na kuendelea na masomo ya sekondari na hatimaye alifanikiwa kufaulu na kuendelea na masomo ya sekondari ya juu A-level kwa bahati nzuri Sophia alifanikiwa kusoma shule ambazo zilikuwa ni za mchanganyiko yaani zenye wavulana na wasichana,Sophia alikuwa ni mwenye mvuto mkubwa kwa kweli alikuwa mzuri na hivyo wavulana wengi walijigonga kwake hata hivyo waliambulia patupu kwani Sophia aliendelea na msimamo wake wa Elimu kwanza mapenzi baadae moja ya vijana waliomsumbua sana aliitwa Kelvin kijana huyu naye alikuwa ameumbika hivyo alikuwa Handsome na kwa kuwa alikuwa mchangamfu alifanikiwa kuwanasa mabinti wengi lakini aligonga ukuta kwa Sophia jambo hili lilimsumbua sana kwani kila Lugha aliyoitumia haikuweza kubadili msimamo wa Binti yule wa kisambaa.Jambo hili lilipelekea wenzake pamoja na Kelvin kutumia njia za maudhi ikiwa ni pamoja na kumuita Sophia Mshamba! Jambo ambalo lilimuudhi sana Sophia hata hivyo aliendelea kuwa mgumu.
    Siku moja kabla kidogo ya kufanya mtihani wa kidato cha sita ambapo siku hizi sherehe za mahafali hufanyika mapema kabla ya Mtihani, katika siku hii wanafunzi walipongezwa kwa tabia mbalimbali zikiwemo usafi, uwezo wao darasani, nidhamu, ushirikiano n.k Sophia alikuwa moja ya watu waliopongezwa kwa nidhamu hata hivyo kama ilivyo ada ya siku ya mahafali siku ile disco lilipigwa usiku kucha na wasichana waliamua kujirusha kwa furaha huku wakiwa na rafiki zao wa kiume au wa kike yaani washikaji, kujirusha kulinoga na alikuwa ni Sophia tu aliyeonekana kuwa mpweke kwani kila mtu alikuwa na wake, moyoni alijihoji kuwa yamkini mimi kweli ni mshamba! yaani hata siku ya leo ya kuhitimisha masomo wenzangu wanaenjoy mimi nikoniko tu aah! Alijiuliza moyoni mwake.Kana kwamba Kelvin alijua nini kinaendelea katika ubongo wa Sophia aliamua kujisogeza karibu naye na kujaribu kumsemesha na kumnunulia kinywaji kwa mbali sana Sophi alijihisi kuwa naye ni mtu hivi na kuanza kujisikia vizuri, “Dada Sophie eeh! Hata leo siku yako ya kuhitimisha masomo bado uko mnyonge njoo basi tucheze japo kidogo masomo si yamekwisha njoo tujirushe dada umeumbwaje wewe kuinyima raha hata nafsi yako njoo basi mpendwa eeh” hayo yalikuwa ni baadhi ya maneno kati ya mengi aliyokuwa akiyarusha Kelvin kwa Sophia maneno yanayoonekana kuwa yaliumba kitu Fulani katika Moyo wa Soph, Kwa kweli Sophie uzalendo ulimshinda aliamua kujitosa katika mziki nakupata kilaji kwani alijipa moyo kuwa ni siku yake baada ya kazi ngumu ya masomo kwanini asijipongeze? Kelvin aliitumia nafasi ya kucheza mziki kumpapasa Sophie ambaye alikuwa hajui lolote wakati wote huu katika taa za giza wanafunzi wengine waliendelea na disco huku wakibusiana na kunyonyana ndimi zao yaani Denda na wengine walionekana kumtia moyo Sophie kwa kuamua kukamua muziki siku ile akiwa kama mtu aliyechangamka na anayeibuka kutoka kwenye ulimbukeni kama ilivyo kwa wengine ambao walikuwa wakitoka nje kwa starehe nyingine zaidi Kelvin aliamua Kumshawishi Sophie ambaye bila tarshishi alikubali aah! Si ilikuwa siku yake kwa nini aonekane mshamba nao waliamua kutoka nje ambako wengi walikuwa wakifanya mapenzi katika kona mbalimbali za ukumbi wa disco gizani huko nje Sophie aliyekuwa bikira naye siku ile kwa mara ya kwanza alijiruhusu kuingiliwa na Kelvin, Kwa kweli alipoteza ubikira wake, hata hivyo alijipa moyo kuwa hatarudia tena tabia hiyo na kwakuwa watu wengi hawajui angejikausha tu bila watu kujua amefanya nini.
    Siku za mitihani ziliwadia na wanafunzi wote walifanya mitihani yao na kumaliza shule, Hata majibu yalipotoka miongoni mwa watu waliochaguliwa kwenda chuo kikuu Sopjie alikuwa mmoja wao alifaulu tofauti na wengine yeye alikwenda chuo kikuu sehemu ya Muhimbili kwa ajili ya kusomea fani ya Udaktari wa maswala ya binadamu huko nako alifaulu na kuanza kazi katika moja ya hospitali zetu hapa nchini Sophie alibahatika kuolewa na daktari mwenzake kijana ambaye naye alikuwa na sifa ya kujitunza kama ilivyokuwa kwa Sophie, Sophie na mumewe huyo walifanikiwa kuishi katika ndoa kwa muda kama wa mwaka moja hivi wakiwa ni wenye kutumainiwa na wazazi wao kwa pande zote mbili ndugu zao, kanisani na serikalini na taifa na jamii kwa ujumla kwani walikuwa ni wenye damu mbichi yaani ni vijana, ndani ya mwaka ule moja wa ndoa Sophie alifanikiwa kupata ujauzito na kujifungua mtoto wa kiume ambaye katika hali ya kusikitisha aliugua magonjwa ya ajabu na kufariki, kadhlika hali ya Sophie na mumewe kiafya haikuwa nzuri tangu wakati ule na kwakuwa wenyewe walikuwa ni wataalamu wa afya iligundulika kuwa walikuwa wameathirika kwa virusi na hatimaye ugonjwa wa ukimwi ambao ulipoteza maisha yao wote wawili, Hii ni habari ya kusikitisha sana kwani wazazi wa kila upande waligharimika kuwasomesha vijana wao ambao sasa walikuwa wamefikia katika kilele cha maisha ambapo labda wangejenga familia yao na kuwasaidia wazazi wao au hata ndugu zao kumbuka pia walikuwa msaada mkubwa kwa jamii kwani wote walikuwa wataalamu!. Je umejifunza nini?Je unapoitwa mshamba inakupunguzia utu wako? Je unadhani Sophia alijitambua? Je kutokujitambua kwa Sophie kulileta madhara gani katika jamii je Sophia alitambua uthamani alio nao katika jamii? Usijiue, usikate tamaa, usikubali kuyumbishwa katika msimamo wako wewe ni wa thamani kuliko unavyojifikiri ni kwa sababu tu hujajua Mungu amekusudia nini au uwe nani katika maisha yako lakini ukiyajua hayo Hutakubali kuyachezea maisha, vijana wengi hawajitambui na ndio maana huamua Hata kujiua au kunywa sumu eti kwa sababu tu Mchumba amekuacha! Kwani kuachwa na mchumba ndio mwisho wa dunia? Mimi nakuasa kama Mtumishi wa Mungu usiharibu maisha yako kwa namna yoyote wala kwa kuvuta sigara au bangi au kufanya mapenzi holela au kujihusisha na madawa ya kulevya kwani kuna kitu cha ziada katika maisha yako Mungu amekiweka ni cha kipekee sana kitunze kwani kinategemea kuishi kwako kwa Muda mrefu ili kijitokeze na dunia ipate kufaidika na kile kilichomo ndani yako wewe ni wa thamani!.  
      Katika Maisha yako usikubali chochote kikutoe katika kusudi ambalo kwalo Mungu amekuumbia, usijali ni hali gani unazipitia au taifa letu linapitia au familia yako inapitia nani ajuaye labda wewe ndie mkombozi wa taifa hili au wa familia yako, Kristo alikuja kuwa msaada kwa Dunia alipofikisha umri wa miaka thelathini hivi unaonaje kama angekata tamaa mapema? Na alizaliwa katika hali duni na ya kukatisha tamaa baba yake akiwa ni seremala kama waliokuwa wamefulia hivi lakini hakukata tamaa, Usikate tamaa tunza ujana wako tambua uthamani wako katika nyanja zote fanya kazi zako kwa bidii au soma kwa bidii kila ulifanyalo lifanye kwa bidii na Mungu wa mbinguni atakubarikia.

   Mahusiano;-
      Kila mtu anapaswa kujihoji kuwa anahusiana vipi na wenzake katika jamii, Mtu yeyote aliye bora ni yule ambaye ana mahusiano mazuri na jamii ya watu wanao mzunguka tunao wafahamu na hata tusio wafahamu.Je una uhusiano mwema na kila mtu? Je wenzako wanakuonaje katika mahusiano? Jiulize je nyumbani, kanisani, shuleni, barabarani na majirani zako, bosi wako au watumishi wako wakazi, wafanyakazi wenzio, wanafunzi wenzio, wapangaji, wanakwaya na wanajamii katika ujumla wake je una amani nao? Biblia inatufundisha kuwa tutafute kwa bidii kuwa na amani na watu woote soma (Waebrania 12;14),hii maana yake hata tunapokuwa tumekosewa ni muhimu kwetu kutafuta amani na wale tuliowakosea au waliotukosea,Huku wewe ukiwa wa kwanza kutafuta amani hiyo hata kama wewe ndiwe uliyekosewa hii ndio ishara ya mtu aliye bora! Huwezi kusema unampenda Mungu huku unamchukia mwenzako unaye muona kwa macho (1Yohana 4;20-21).Je ni lugha gani unayoitumia?Je unaheshimu watu kiasi gani? Uhusiano wako kwa wakubwa na wadogo ukoje? Wazazi wetu ni marafiki zetu? Wachungaji na viongozi wako wa dini  kwako ni nani?Ndugu zako wa kike au wa kiume katika bwana na hata nje ya hapo ni nani kwako? Je unatafasiri vipi uhusiano? Je Kila mwanamume au mwanamke yaani watu wa jinsia tofauti na wewe ni lazima uwe na uhusiano nao kimapenzi? Je ngono ni kigezo cha uhusiano kwako? Mahusiano kwako ninini na yanakuongoza vipi? Je unatarajia watu wakufanyie nini je wewe unafanya Yale unayotaka watu wakufanyie? Yesu alisema nini angalia (Mathayo 7;12). “Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii.” Je wewe unawatendea watu Nini? Angalia Mfano huu;-
Dada mmoja aliyekuwa mtanashati hivi, siku moja alipanda kwenye daladala, Dada huyu aliyekuwa na maringo aliingia moja kwamoja na kuelekea kukaa kwenye moja ya siti aliyokuwa ameketi kaka mmoja hivi aliyeonekana wa kawaida tu, Kwa kuwa dada yule mtanashati hivi alikuwa na maringo na majivuno vijana waleo wanasema ananata! Aliona hakuwa hata na sababu ya kumsalimia kaka aliyekuwa amemkuta na kukaa naye katika siti moja, Kwa kweli dada alijiona Sana! na alijiona kuwa yuko salama na safari ikaendelea;,katikati ya safari kondakta alianza kutoza nauli kama ilivyo ada na mara ndipo ilipofika zamu ya dada yule,kama unavyojua makondakta wetu hapa nchini wako kikazi zaidi na hawataki uzuri zaidi ya nauli na unapomletea mzaha anaweza kukukoromea hata bila kujali nani wanakuzunguka katika gari yeye anajali nini Bwana ahaa si unajua jioni ndo hesabu anataka fedha tu na ukiweka adabu nyuma yeye alikwisha imwaga miaka tangu alipokuwa mpiga debe,Dada yule alifungua pochi yake kwa madaha sana na kumbe kwa bahati mbaya alikuwa amesahau nauli nyumbani hivyo pochi yake haikuwa na kitu lo! Aibu iliyoje kwani konda hakuwa anaelewa somo zaidi ya kudai nauli bila adabu huku akinyesha mvua ya matusi “Si tuko kazini bwana unazani tumekuja kununua sura hapa Nataka nauli alisisitiza Konda huyu huku akishusha matusi kedekede abiria wakiwa kimya, Mungu si athumani yule kaka aliyekuwa karibu na dada yule ambaye alipoingia hata kumsalimu aliona ni kujipotezea muda aliamua kumpa dada yule nauli ili kumtuliza konda kisha kaka yule alimuuliza unayo naya kurudia? Dada yule alijivunga kupokea kwa madai kuwa angepitia benk hivyo swala la nauli ya kurudia halitasumbua, gari lilipofika kituoni dada huyu ambaye tayari mazingira yalimfundisha adabu alimshukuru yule kaka na kutokomea mtaani.
   Mfano huu unatufundisha nini Je unaweza kumdharau kila mtu tu? Tunahusiana vipi na wengine Hakuna mtu wa kumpuuzia kila mtu anastahili heshima bila kuangalia sura heshima haiuzwi ni kitu cha Bure,Yeyote unaemtendea ubaya leo aweza kuwa msaada wa baadae kwako, Ndio maana Yesu akasema “Lakini mimi Nawaambia,Wapendeni adui zenu ,Waoombeeni wanaowaudhi”. (Mathayo 5;44)

Mawasiliano;-
   (1koritho 14;26-27). Katika mistari hii kwa ufupi tunaweza kusema kuwa Paulo mtume hapo alikuwa anashighulikia swala la Mawasiliano,kwa maana nyingine ili watu waweze kuwasiliana  na kuelewana ni lazima kuwepo na utaratibu,Je umeshawahi kupeleka ujumbe Fulani muhimu na baadae ukagundua kuwa haukueleweka?Je ulijiuliza ni kwa sababu gani?
  Kuwasiliana kunakuwa na maana kama pande zote mbili zinazohusika zinaelewana,Hivyo ili ueleweke jitahidi kujifunza mbinu za mawasiliano (Communications skills),Jaribu kutumia mwili wako,Ishara na vitendo unapowasilisha ujumbe (non- Verbally)Vitendo husaidia kupeleka ujumbe kuliko Maneno Mkao wako na mvao wako pia unawasilisha ujumbe kuwa wewe ni mtu wa namna gani.Jaribu kuwaza kuwa unapovaa viguo vya nusu uchi unapeleka ujumbe wa namna gani?unapozungumza huku unalembua macho au kubana pua kidogo au kama unaeng’ata kidole unapeleka ujumbe wa namna gani?Unapopeleka ujumbe huku mwili wako uko tofauti na ujumbe kuna uwezekano ujumbe wako usipokelewe.Angalia kielelezo kifuatacho; 

    
     Nimetoka kwenye uwepo wa Mungu sasa hivi nina ujumbe Muhimu kwa ajili yako leo na kwa mafanikio yako (Picha na maelezo kwa hisani ya maktaba ya Mchungaji Innocent Kamote)

       Angalia Muhubiri huyo hapo juu ana ujumbe muhimu wa mafanikio yako! Je maneno yake na muonekano wake unaweza kuufanya ujumbe wake wa mafanikio kupokelewa? Ni muhimu kujiangalia kila wakati na kujitokeza mbele ya hadhira tukiwa na muonekano unaoendana na kile tunachokikifanya, kukisema kukiamini au kukitetea ili Muonekano wetu uweze kuhusika katika kupeleka ujumbe. Manabii wengi wakati wa agano la kale iliwapasa kufanya mambo mengi sana yaliyochangia kufikisha ujumbe ule waliokuwa wameukusudia kuufikisha kwa jamii husika na wakaeleweka.

Namna ya kutatua Matatizo ;( 1Falme 3;16-27)
  Kutatua matatizo ni mojawapo ya jambo gumu na linalosumbua watu wengi sana hususani vijana mtu anayejitambua anapaswa kuwa makini wakati anapojishughulisha na kutatua matatizo ni muhimu hapa kujiuliza kwanza Tatizo lako ni nini? Au tatizo uliloletewa ni lipi? Na ni muhimu ukapata muda wa kutafakari na kisha kufikiri ni njia gani utazitumia baada ya kutafakari njia mbalimbali za kuweza kutatua tatizo hilo,na kwa kila njia pima kuwa unapoichagua njia hiyo inaleta matokeo gani (mazuri au mabaya).Baada ya hayo unaweza kuchagua njia ambayo inaleta matokeo mazuri wakati wote huo ni muhimu kuzingatia maswala yafuatayo tunapotatua matatizo 1.Angalia kwanza tatizo lenyewe, 2.chagua njia za kutatua tatizo hususani zisizo na madhara 3. pima matokeo ya namna unavyotatua matatizo kwa mfano kama u mchungaji si kila wakati kumtenga mshirika kunatatua tatizo lazima ieleweke kuwa lengo la kumtenga mtu ni kumrejesha awe hai kiroho na sio kumvunjia heshima kama wafanyavyo watu wengine (Wagalatia 6;1).

Namna ya Kufanya Maamuzi (Ruthu1;1-22,Mwanzo13;1-13).
     (1Falme 12;4-11).Kufanya uamuzi ni moja ya mambo ya maana sana katika maisha yetu.Ni muhimu kufahamu kuwa uamuzi tunaoufanya leo ndio utakaoamua maisha yetu ya mbeleni au baadae.wakati wakufanya uamuzi ndio wakati wakuonyesha upeo na ukomavu alionao mtu.katika ulimwengu wakiroho Mungu au Shetani huangalia kwa makini sana mtu anapofanya maamuzi ili kila upande uweze kutekeleza matakwa yake kulingana na uamuzi husika hivyo utaona kuwa kufanya uamuzi ni jambo la muhimu sana.
 Hebu jaribu kuwaza mfano huu “Umeagana na mpenzi wako kuwa akupitie ili mkatese mjini; anafika na gari yake akiwa amelewa au amezitwika ze laga kichwani kiasi cha kutosha hivi! Na anataka akuendeshe kwenye gari yake je utahairisha safari? Au utaenda hapo pana hitaji kufanya uamuzi na ni mahali pa kufikiri kipi ni cha muhimu woote tunakubali kuwa Uhai ni mtamu sana utachagua nini? Mtu anayejitambua atajiuliza maswala ya muhimu yafuatayo;-
  1. Je unamfahamu vizuri huyo mpenzi wako?
    • Akiwa amelewa ana stamina ya kuendesha gari?
    • Ikitokea hatari atakuwa na nguvu ya kukutetea?
    • Je akilewa hufanya fujo au la?
  2. Je wewe utaelewekaje?
    • Watu wanaokufahamu wakikuona umeongozana na mpenzi anayenesanesa kwa ulevi watakuelewaje?
    • Akikuona mtu anayekuheshimu na kukuamini ataathirika vipi?
    • Je hali hiyo inakubalika katika jamii yako au kwenu?
  3. Je wewe unajichukuliaje?
    • Jew ewe ni wakuendeshwa na mlevi?
    • Je kama unakwenda kutesa utatesa kweli?
    • Je kuna kitu unahisi unajihofia?
    • Jew ewe unawajibika vipi kwa usalama wako?
  4. Je kuna njia nyingine yoyote ya kutayua tatizo?
    • Je kuna uwezekano wa kuhairisha safari?
    • Je ukihairisha safari kutatokea nini?
    • Je ni lipi lililo bora kwako
  5. Je ni lipi La muhimu kwako?
    • Je ni maisha?Mpenzi?au Kutesa? lipi la muhimu kwako ukuisha kujiuliza maswali hayo ndipo sa unapoweza kufanya uamuzi je wewe ungechagua nini ?

Namna ya kuhimili Mihemko; (Mwanzo 39;6-9.2samuel 13;10-15).
   Mihemko au mhemko nihisia zote zinazopanda na kushuka katika maumbile ya mwanadamu,mfano hasira,jazba,huzuni,aibu,furaha,Nyege, n.k. vijana ndio ambao husumbuliwa zaidi na tatizo la mihemko kwa sababu ya vichocheo (homonies) zao zinakuwa zimevurugika wanapokuwa katika hali ya kukuwa na hivyo vichocheo vinakuwa haviko sawa yaani havija Balance.” Maladjustiment of homonies”kwa msingi huo iko haja ya kujifunza mapema namna ya kuhimlili mihemko kwa wale waliokoka Roho mtakatifu hutusaidia kuhimili mihemko,kuhimili mihemko kwa kupiga punyeto au kujichua hakuwezi kuwa na faida sana kwani kunaweza kuchochea kufanya vitendo halisi swala hili nitalijadili huko mbeleni, lakini ni muhimu kujihadhari na hali zozote zinazochangia katika kuchochea mihemko tuliyo nayo ikiwa ni pamoja na kujihadhari na watu wenye maudhi au wagomvi ili wasiamshe hasira zako au kujihadhari na vijarida au picha zenye kuchochea maswala ya ngono.Biblia inasema kila mmoja wenu ajuwe kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima mwili una nguvu sana unavuta katika maswala matamu ya dunia hii ambayo ndani yake kuna mauti nani aweza kutusaidia ni Roho wa Mungu pekee (1Thesalonike 4;3-5.7-8soma pia Rumi 7;14-25, 8;5-11).
Namna ya kuhimili Msongo (mgandamizo wa mawazo).
     Watu wengi sana hupatwa na msongo,hii ni hali ya kuwa na  kusongwa na mambo mengi.Mambo mengi yanayosababisha msongo(Depression) ni pamoja na kutotimizwa kwa ndoto mbalimbali katika maisha,kubakia yatima,kulaumiwa,ujane,kufiwa na wazazi,kusakamwa au kunyanyaswa kazini,nyumbani na wakati mwingine hata kanisani au popote,matarajio yasiyofikiwa,kufukuzwa kazi,kupatwa na kashfa nk mara nyingi mambo kama haya husababisha watu kushuka moyo,kutokuona umuhimu wa kuishi,kukata tama,kuwa na huzuni na kusongwa na mawazo wengi wanaopatwa na haya huamua kujiua,huchanganyikiwa na kusikika wakizungumza wenyewe barabarani,kutokuweza kufanya lolote au kujiingiza kwenye ulevi wa kupindukia,wengine kunywa sumu,kujinyonga n.k. mtu anayejitambua atajifunza namna ya kuhimili msongo hebu angalia mfano huu;-
       Chukulia wewe ni mtu mwaminifu na unayemcha Mungu sana na katika kumtumikia kwako Mungu unakamatwa na kutiwa gerezani kwa ajili ya injili kanisa lako linapata taarifa;wanaamua kutuma mtu mwaminifu sana aje akutie moyo na kukuhudumia ukiwa gerezani,kasha anapofika huko naye anaugua mahututi sana,kwakuwa wewe ni muhubiri mwenye upako na umekuwa ukiombea wagonjwa wengi sana unamuombea,baada ya maombi ugonjwa unazidi kiasi cha kufa na anakua mahututi sana hali inakuwa mbaya je ungekuwa wewe ungefanya nini? Je unaweza kufikiri kuwa Mungu amekukataa? Au utafikiri kuwa umefanya dhambi? Je hali hii inaweza kuwapata watu wa Mungu ?je utaamua kuacha wokovu? Soma (Wafilipi 2;25-30),Hali hii ilimpata Paulo mtume alipokuwa amefungwa na kanisa la Filipi likamtuma Epafrodito kwa ajili ya kumtia moyo naye aliugua sana,Lakini Paulo mtume alikuwa amejifunza katika Mungu kuhimili msongo,Wengi wanaokufa kwa presha au shinikizo la damu ni wale ambao hawajaweza kuhimili mikikimikiki ya kupokea matatizo mengi kwa wakati mmoja hali hii ilimpata kuhani Eli katika (1Samuel 30;1-10).tofauti na Ayubu ambaye aliweza kuhimili msongo alipopatwa na mabaya mengi kwa wakati mmoja (Ayubu 1-2) jifunze kuhimili misongo wala usizimie moyo wakati wa taabu na umwangalie Mungu (Mithali 24;10).

Namna ya kuwa na Fikira Bunifu.
     Kuwa na fikira bunifu ni kitendo cha kuwa na uwezo wa kutatua tatizo kwa haraka, Unatumia akili nili kupambana na tatizo la ghafla lililotokea bila wewe kutegemea, Mungu ametuumba tofauti wako watu ambao wamejaliwa uwezo wa kutatua tatizo kwa haraka, lakini walio wengi wanaposhitukizwa jambo Fulani linalowahitaji kuchukua uamuzi wa haraka huishiwa nguvu kabisa na kupoteza uwezo wa kufikiri halafu baadae ndipo hupata majibu lakini mengi huwa ni yenye majuto Ningejua! Biblia inatufundisha jinsi Daniel,Shedrak na Meshak na Aberdnego walikuwa na fikira bunifu kujiokoa na kujitia unajisi (Daniel 1;6-16),pia tunapata taarifa za Raheli ambaye aliiba miungu ya babaye na babaye kuamua kufanya utafutaji wa miungu yake haraka kwa ubunifu alijifanya yuko katika siku zake na kujiokoa (Mwanzo 31;19,30-35) aidha wanawake hawataweza kumsahau mwanamke mwenye akili Abigaili ambaye  alikuwa na fikira bunifu  na kutatua tatizo la kutaka kuuawa kwa mumewe na familia yake (1Samuel 25;4-35)Je unapopatwa na hali zinazo hitaji ubunifu Fulani wa haarkaharaka wewe unafanyaje? Jaribu kuwaza mfano huu;-
             Chukulia kua wewe ni msichana na umealikwa kwenye pati na rafiki yako inayofanyika mbali na nyumbani kwenu,wewe humfahamu mtu yeyote yule zaidi ya rafiki yako mnapofika kwenye pati watu woote uliowakuta wanaonyesha ukarimu na uchangamfu kwako na urafiki,chakula na vinywaji vinapatikana na mziki mzuri karibu na mwisho wa part usiku mwingi unagundua kuwa rafiki yako hayupo na unapoulizia unaambiwa kuwa alipatwa na dharula ya kumpeleka mgeni nyumbani na huenda hatarudi,Kaka wa rafiki yako ambaye hajaokoka na alikuwa ameshalewa anakuondoa wasiwasi kwamba kwakua ana gari atakusindikiza nyumbani,kaka huyu ambaye alishaanza kukuzoeazoea tangu mwanzoni mwa pati,na kwa kuwa saa zile hakuna  daladala wala huwezi kupata hata tax ya kukodi na mfukoni huna fedha je utafanya nini? Hapo ndipomunapohitaji fikira bunifu.

Namna ya kuwa na fikira Adilifu.
  Biblia inasema katika ( Mathayo 5;8) “Heri wenye moyo safi maana hao watamuona Mungu” tunapozungumzia fikira adilifu tunazungumzia ile hali ya moyono kifikira kama je unafikiri kwa usahihi,hisia zako ni safi? Je unafikiri kwa nia njema,wako watu amabao wanashida katika kufikiri na wengi wakundi hili ni wale wanaoitwa wameokoka ni muhimu kufahamu kuwa kama u mtu sahihi utafikiri kwa usahihi si unajua kuwa Mungu atakapohukumu wanadamu hatahukumu matendo yao tu bali atahukumu na nia ile iliyopelekea wao kutenda,hivyo kuna faida za muhimu kifikira kama tutafikiri kiadilifu na kwa moyo safi angalia mfano huu;-
    Kijana mmoja mzuri alikuwa amemaliza masomo yake katika moja ya vyuo vya ustawi wa jamii huko Arusha,baada ya masomo yake alirudi Daresalaam ambako alikwenda kubangaiza ajira kama unavyojua kuwa siku hizi ajira ni za shida katika nchi yetu,hasa ukichukulia kuwa mfumo wetu wa elimu tangu mwanzo ulikuwa umebuniwa kwa namna ya kusoma ili uje uajiriwe na si kujiajiri,hivyo kaka huyoalifanikiwa kupata ajira katika moja ya vituo vya kulea watoto yatima kilichoko sinza Daresalaam,Siku ambayo yule kaka alikwenda kutafuta kazi,mama mmoja mtanashati na mwenye mvuto, alionekana kumtetea sana yule kijana ili apewe kazi si unajua unaweza kuingia katika ofisi Fulani kasha ikatokea mtu amekuchunuku tu na kukupenda hata bila ya sababu hili ndilo lililomtokea kijana huyu mama huyu mweupe wastani aliyekuwa na mwanya na aliyekuwa mcheshi alifaniukiwa kumshawishi bosi wake kumuajiri kijana hutu,hata hivyo bosi huyu alisema kijana huyu atakuwachini ya majaribio kwa miezi miwili hivi (Under probation).kijana alianza kazi na kila mtu alimuonyesha ushirikiano na kwakuwa mama yule alikuwa mcheshi pale kazini na alionyesha kumchangamkia kijana yule tangu siku ya kwanza na kwa kadiri walivyozoeana pia walikuwa wakitaniana katikamaeneo mbalimbali hata hivyo kumbuka kuwa mama yule alikuwa na mumewe yaani ni mrs. Wakiwa ndani ya miezi miwili ya kuangaliwa siku moja kama ilivyo ada kijana yule aliyependa kwenda ofisini kwa mama pindi kazi zinapokuwa zimepungua na kuamua kumtania siku hiyo aliamua kwenda na kumtania mama yule amabaye pia alikuwa si mwepesi wa kukasirika hata utani unapopita mipaka siku hiyo kijana aliamua kumpasukia mama yale yaliyokuwa yakimsibu moyoni kijana alisema “Mama mi leo uvumilivu umenishinda nimeona nipasue jipu linalonisibu moyoni nimechoka kuugua leo nahitaji dawa yaani kwa ufupi mama mi nimekuzimia” Mama yule aliangua kicheko na kumuuliza kijana yule “acha utani wako bwana yaani huko mtaani umekosa dawa kijana mzuri kama wewe uje utafute dawa ofisini tusidanganyane bwana!”alijibu mama yule Hata hivyo kijana yule siku ile alikuwa amemaanisha yaani yuko Sirius ,alizidi kujimwaga kwa maeneno ya kimahaba na kuamua kumsogelea mama yule na kuanza kumpapasapapasa kuanzia kifuani na maeneo mengine wakati woote hu yule mama alikuwa ametulia tuli akishangaa jinsi ambavyo utani ule unapitiliza mipaka na kuwa ukicheka na mbwa basi utaingia naye msikitini!,mwisho mama yule aliamua kuchomoka na kwenda moja kwa moja katika ofisi ya meneja wa utawala (Admnistrative manager and human resourses) na kumweleza kilicho msibu meneja aliwaita watuwoote ofisini na mwishoni alimwagiza askari kumleta kijana yule ambaye punde alipoona watu wakiwa wamebadilika sura alielewa kuwa leo iko kasheshe kufupisha habari kijana aliachishwa kazi kwani kumbuka alikuwa katika kipindi cha uangalizi.aibu ilimpata kijana huyu nini kilimponza? Mara nyingi tunapoona mtu wa jinsia tofauti akituchangamkia wakati woote huwa himaanishi kuwa anakutaka kimapenzi wako watu ambao wameumbwa wakiwa wachangamfu tu na mioyoni mwao hawana nia mbaya je wewe una moyo safi? Unajisikiaje unapoona mtu wajinsia tofauti wameketi wakiongea mambo yao unadhani kuwa wakati woote wako kwa ajili ya uzinzi? Si kweli si kila wakati watu wanaweza kuwa na nia hiyo lakini tunawezaje kuepuka kuwafikiria watu vibaya ni kwa kuwa na mawazo adilifu tusipende kuwawazia watu kwa upumbavu mtu aweza asiwe karibu na mwanamke na akawa mzinzi wa kutupwa tu biblia inatufundisha mambo ya kutafakari Hatimaye ndugu zangu,mambo yoyote yaliyo ya kweli yoyote yaliyo ya staha,yoyote yaliyo ya haki,yoyote yaliyo safi,yoyote yenye kupendeza yoyote yenye sifa njema ukiwapo wema wowote,ikiwapo sifa nzuri yoyote yatafakarini hayo.(Wafilipi 4;8), Je wewe umekuwa ukitafakari mambogani je unahukumu wengine je unafikira adilifu? Mungu atupe neema kuwa watu wenye fikira adilifu na kuwa watu safi tunaofikiri sawasawa.

Namna ya kuwa na fikira Yakinifu (Kusimama katika kweli).
     Fikira yakinifu ni hali ya kusimama katika kweli ni uwezo wa kuisimamia kweli hata kama jambo hilo limeamuliwa na mtu mkubwa au unaye mwamini,mzazi au mtu yeyote,ni uwezo wa kuamua ukwelina kuuusimamia na wala sikwa mazoea tu, Ni lazima tujifunze kupinga jambo lolote lisilo sahihi au lisilo la kweli,hakuna jambo linalopendeza kama kuwa mkweli Shadrak, meshak na Abdednergo waliweza kuisimamia kweli pale mfalme alipowaamuru mkwa vitisho kuabudu miungu,Daniel hakuacha kuomba pamoja na sheria iliyopitishwa ili kumtishia asiombe Mungu,Mitume waliendelea kuhubiri pamoja na amri kutoka kwa viongozi wa dini ya kiyahudi waliowakataza kuhubiri katika jina la Yesui (Matendo 5;29,4;19). Tunapojifunza kuwa wakweli tangu ujuana tunajiandaa kupata taifa lenye watu waadilifu na wakweli si wakati woote ni rahisi kuwa wakweli lakini kumbuka kuwa unaposhindwa kujifunza kuwa mkweli au kusismama katika kweli unaweza kujikuta unaingia katika madhara Fulani angalia mfano huu;-
 “Fikiria kuwa wewe ni dada uliyeokoka na unapokaribia au kuingia katika siku zako tumbo huwa linakuuma sana, hatimaye unaamua kwenda hospital na unapoingia katika chumba cha daktari ambaye unaamini atakusaidia, wakati huu hujaolewa bado, daktari anakuambia kuwa dawa ya tumbo lako ni kwa sababu hujakutana na mwanaume na ukipata mwanaume tumbo lako litaacha kasha anaonyesha nia ya kutaka kukusaidia yaani kwa yeye kumaliza shida yako hiyo kama njia ya matibabu je wewe utafanyaje?”

Vijana wengi wamedanganywa na kujikuta wakifanywa ngono kwa sababu ya kutokuisimamia kweli kwani maumivu hayo wakati mwingine hayawezi kuisha kwa kufanya ngono kuwa na mume au kuzaa kwa wanawake wengine hali hii huendelea,na wengine huacha yenyewe. 

     
  Martin Luther King alikuwa na fikira yakinifu, alisimama katika kweli na kupinga ubaguzi wa rangi waliotendewa weusi huko Marekani na ingawa aliuawa lakini ndoto zake sasa zinaheshimika,ni vijana wangapi wanaweza kuisimamia kweli hata kama itagharimu mauti? (Picha na maelezo kwa hisani ya maktaba ya Mchungaji Innocent Mkombozi kamote).

Namna ya kuwa mwenye Ushirikeli (Namna unavyoliona tatizo la mwingine).
 Ushirikeli ni hali ya kuwa na huruma ni hali ya kuona tatizo la mwenzi wako kama vile ni la kwako,ushirikeli pia ni hali ya kuwajali wengine,namna tunavyowaelewa kikamilifu,na namna tunavyowatendea haki na namna tunavyo tunavyothamini mawazo na mitazamo yao.Ni katika njia hii tunaweza kuwatambua wenzetu vilivyo na kuwajali,Yesu nalikuwa na huruma sana wakati woote aliwahurumia watu alichukua matatizo ya watu kama matatizo yake na kutafuta utatuzi,mtu bora ni yule ambaye pia hujali wengine,hali hii huboresha uhusiano na wengine katika somo lijalo tutazungumzia juu ya mahusiano.


                         
 Mama Teresa wa Culcuta India (1910-1997) anaheshimika sana duniani kwa kuwahurumia wengine,alipewa nishani ya Nobel 1979,alianza akiwa masikini lakini alianzisha vituo vya ukarimu kwa ajili ya kuwasaidia yatima na wajane,wasiojiweza na wenye njaa,leo hii kuna matajiri wengi sana wasio na huruma kwa wengine wanaongoza kwa dhuluma na ufisadi wewe utalifanyia nini taifa ushirikeli unaweza kukusaidia kuhisi maumivu ya wengine (Maelezo na picha Kwa hisani ya makatba ya Mchungaji Innocent  Mkombozi Kamote)

Fikira achilifu (Mathayo 5;7).
     Hii ni hali ya kuwa na moyo wenye kusamehe,kuachilia kusamehe jambo lolote lile  ambalo ni gumu kuachilika (Mwanzo 45;4-5).hili ni jambo gumu sana lakini tunapaswa kujifunza kusamehe wako watu ambao huwakwaza wenziwao kiasi ambacho inakuwa ngumu kuwasamehe hali hii isipodhibitiwa huweza kusababisha watu kuuana kama ilivyo katika inchi nyingine zilizoendelea vijana huuana sana kwa sababu ya visa na mikasa ambayo watu hufanyiana kwa kushindwa kusameheana na kuachilia.

 
   Kabla ya kuwa rais wa kwanza mwafrika inchini Afrika ya kusini 1994 Nelson Mandela aliteseka gerezani kwa miaka 27 hivi,akipinga sera za kibaguzi za makaburu,aliposhika madaraka haukuwa wakati kwake kulipiza kisasi na kubagua wazungu bali alisamehe na kuchilia je wewe ungekuwa Mandela ungefanya nini?(picha na maelezo kwa hisani ya maktaba ya Mchungaji Innocent Mkombozi Kamote).

Namna ya kuwa na hali toshelevu.
     Hali toshelevu ni hali ya kuridhika,je unajua kuridhika sio jambo rahisi kama tunavyofikiri,lakini ni muhimu kujifunza kuridhika.kwa kawaida katika maisha kuna matokeo makuu ya aina mbili kuna kupanda na kushuka, kwa msingi huo ni muhimu kuwalea vijana kuzijua hali zote mbili mtuma Paulo alifundishwa na mungu kuhimili hali hizo zote mbili (Wafilipi 4;11-12) hivyo haya ni maamuzi ambayo mwanadamu aweza kujifunza,Hebu jiulize jinsi ambavyo watu wanabahatika kupata vyeo vikubwa serikalini na hata katika makanisa lakini pamoja na mishahara mikubwa wanayoipata angalia rushwa na ufisadi wa kutisha kumbuka ile kashfa ya Richmond ambayo shirika hili lilikuwa linalipwa milioni 152 hivi kwa siku,watanzania wako kama million 40 hivi hii ni sawa na kusema kila mtanzania angeweza kupata milioni tatu na ushee hivi kila siku?kama mabo ndivyo yalivyo ni wachache tena wenywe vyeo na mishahara mikubwa waliofanya haya,kama hayo hayatoshi wengi wanapoachishwa kazi huchanganyikiwa kwanini kwa sababu hawako radhi na aina nyingine za maisha ni muhimu kwetu kuwa tayari na aina zote za maisha,Yesu aliishi maisha ya kuridhika,mitume na wengi lakini hata mwalimu Nyerere kiongozi wa kwanza wa Tanzania alikuwa mwenye kuridhika hakuwa na tabia ya kujilimbiklizia mali ili tusiishi maisha yenye maumivu tujifunze kuridhika
  
                      
     Julius Nyerere hakuwa na makuu hakujilimbikizia mashamba makubwa wala makampuni makubwa aliishi maisha ya kuridhika,hakusomesha watoto wake ulaya, walikwenda shule kwa miguu kama watanzania wengine alilinda rasilimali za taifa hili kwa faida ya vizai vijavyo leo hii maliasili,wanyama,madini na hata gesi ni dili za wachache na wanainchi hawafaidiki na lolote kila siku ugumu wa maisha ya kugawana umasikini unaendelea ni vema mungu akijipatia watu waadilifu,watakaokubali kuridhika na kuhakikisha kuwa na wengine wanafaidi matunda ya uhuru (Picha na maelezo ni kwa hisani ya Mchungaji Innocent Kamote).

    Mali tunazojilimbikizia hatutaweza kuondoka nazo duniani biblia inasema hivi “Usiogope mtu atakapopata utajiri na fahari ya nyumba yake itakapozidi,maana atakapo kufa hatachukua chochote utukufu wake hautashuka ukimfuata” (Zaburi 49;16-17). Jiponye na roho ya tamaa ya mali vijanawengi wamepoteza maisha kwa kutokuridhika mimi sitaki wewe uwe hivyo somo hili staid za maisha litakusaidia ukilitendea kazi ubarikiwe.

Alhamisi, 4 Februari 2016

Umuhimu wa Kuhudhuria Ibada!



Mstari wa msingi Matendo 2; 46 “Na sikuzote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya Hekalu…….”
Somo la umuhimu wa kuhudhuria ibada zote ni moja ya masomo muhimu sana , ufahamu kuhusu somo hili kunamfanya mtu aliyeokoka kupiga hatua kubwa sana katika kukua kiroho  na hatimaye yeye naye kuwa mwalimu wa wengine kwa upesi zaidi,Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo;-
Kanisa Mjini Dubai wakristo wanaruhusiwa kuabudu na kujenga makanisa bila kuweka alama ya msalaba juu ya Majengo yao


·         Umuhimu wa kuhudhuria ibada zote
·         Kwanini inatupasa kuhudhuria ibada zote
·         Tuhudhurie ibada katika kanisa lipi?

Umuhimu wa kuhudhuria ibada zote
Moja ya ishara ya muhimu inayoonyesha kuwa mtu ameokoka ni kuwa na shauku ya kumtafuta Mungu kilka siku Isaya 58;2 mtu aliyeokoka atapenda kujisomea Biblia  na kufanya maombi binafsi nyumbani  kila mara anapopata nafasi  atakuwa akitafakari na kujifunza neno la Mungu lakini pia atakuwa akihudhuria ibada 

Kuhudhuria Ibada ni amri ya Mungu kwa kila mtu aliyeokoka Biblia inasema katika Kumbukumbu 12;5 “Lakini mahali atakapopachagua Bwana Mungu  wenu …..Apaweke jina lake maana ni makao yake, elekezeni nyuso zenu hapo nawe wende huko” Maneno nawe wende huko katika Biblia ya kiingereza ya New International Version yanasomeka “To that place you must go” kwa msingi huo kwa tafasiri rahisi tunaweza kusema mahali hapo ni lazima uende unaona kwa hiyo kuhudhuria ibada ni swala la lazima Mungu anasema lazima uende kanisani Biblia inaagiza kutokuacha kukusanyika Waebrania 10;25. 

Yesu kristo mwenyewe alionyesha wazi jinsi ilivyo lazima kuwako nyumbani mwa Mungu Luka 2;49 Akawaambia kwani kunitafuta ? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo nyumbani mwa baba yangu? Yaani imenilazimu  Kama kwa Yesu ilikuwa ni lazima basi sisi ni zaidi sana  Biblia inasema Yeye asemaye ya kuwa anakaandani yake imempasa kuenenda vilevile kama Yeye alivyoenenda  1Yohana 2;6, Watakatifu waliotutangulia kwao ilikuwa ni furaha walipoambiwa kwenda nyumbani mwa Bwana  na waliona siku moja ya kuwamo nyumbani mwa Bwana ni bora kuliko siku elfu za shughuli za dunia soma Zaburi 122;1,84;1-2,10, ilikuwa ni kawaida kwa manabii na mitume kutunza muda wa kwenda kusali soma Luka 2;36-37,24;53 Matendo 3;1 sisi nasi kama tunataka kutumiwa sana na Mungu inatupasa kuiga mfano wao
Watu waliookoka nyakati za kanisa la kwanza siku zote walidumu kwa moyo mmoja ndani ya hekalu Matendo 2;46 hii ndio siri kubwa ya mafanikio yao  tusikubali kamwe kwa namna yoyote ile masumbufu ya dunia hii kutunyima muda wa kwenda kuabudu.

Kwanini inatupasa kuhudhuria ibada zote
Tukiisha kujifunza kuwa neno la Mungu ni nini na sisi tuliookolewa ni akina nani ufahamu huu utatupa kuelewa vizuri umuhimu wa kuhudhuria ibada zote
1.       Neno la Mungu ni chakula cha kiroho Yeremia 15;16, Mathayo 4;4, Yohana 6;48-49,57-58, Kumbukumbu 8;3  Ili mtu apige hatua kubwa ya kiroho katika wokovu inampasa kulipenda Neno la Mungu kuliko hata chakula cha kimwili  Ayubu 23;12 watu wanaokula mara tatu kwa siku pamoja na mapochopocho mengine kwa wiki wana kula zaidi ya mara 21 kuulisha mwili maana yake na sisi ni muhimu kuhakikisha kuwa tunazilisha roho zetu kwa kuhudhuria ibada na kuomba na kuabudu na kujisomea neno n.k.
2.       Sisi ni wanafunzi wa Yesu Baada ya kuwa tumeokolewa tunageuka kuwa wanafunzi wa Bwana Yesu Mathayo 27;57, Yesu Kristo anakuwa ni mwalimu wetu  Yohana 13;13, Naye amelipa kanisa wasaidizi wa kutusaidia kufundisha neno la Mungu Waefeso 4;11-12 , Mathayo 28;19-20 kwa msingi huo waliookolewa ni wanafunzi wa Yesu na ili mwanafunzi aweze kufanikiwa anapaswa kuhudhuria darasani vipindi vyote bila kukosa  kama tutalizingatia hili ndipo tutakapokuwa miongoni mwa hao washindao Ufunuo 2;11.
3.       Tuhudhurie ibada katika kanisa lipi?
Baada ya kuokolewa Biblia inatupa muongozo wa dhahiri juu ya mahali sahii pa kuabudu Biblia inasema hatupaswi tena kuyarudia mafundisho yaliyo manyonge Wagalatia 4;9 sasa tunawezaje kujua kuwa mahali hapa ni penye mafundisho manyonge? Tutachunguza alama zifuatazo na ukigundua moja kati ya hizo basi mahali hapo hapafai kwa kuabudu

§  Mahali ambapo pana viongozi vipofu Luka 6;39, Mathayo 15;14 yaani mahali ambapo kuna wachungaji au wainjilisti au wazee wa kanisa wa dhehebu lolote ambao ulevi, zinaa na uasherati na kila aina ya dhambi inawatawala hao hawawezi kuwa msaada wa mtu wa kiroho kwa sababu mtu aliyeokoka amepewa kuona Yohana 9;39-41 hivyo hupaswi kuongozwa na kipofu
§  Mahali ambapo matendo ya giza hayakemewi Waefeso 5;11
§  Mahali ambapo sanamu zinashirikishwa katika Ibada  Isaya 31;7,1Wakoritho 10;14, 1Yohana 5;21
§  Mahali ambapo wanafuata maneno yaliyotungwa na wanadamu na sio neno la Mungu 2Petro 2;1-3
§  Mahali ambapo hawaamini kuwa Yesu ni mwana wa Mungu 1Yohana 4;15,5;10-12,Yohana 3;36 .
§  Mahali ambapo Neno la Mungu halihubiriwi bali zina hubiriwa hadithi  tu na hakuna kukaripiwa kukemewa wala kuonywa Neno siku zote linakuwa ni kufariji tu 2Timotheo 4;1-2,Ayubu 16;1-2,Waebrania 12;5-8.
§  Mahali ambapo kila mtu hata mtoto mchanga anapewa zamu ya kutoa neno badala ya kukaa chini  na kujifunza neno kwanza kwa kukaa chini ya waalimu 1Koritho 12;28-29 Waebrania 5;11-12
§  Mahali ambapo watu wanafundishwa kushika sheria ya Musa kwa kutokula aina Fulani ya vyakula kushika sabato n.k. Wakolosai 2;16-17,1wakoritho 10;25-27
§  Mahali ambapo hakuna changamoto bali unakaa tu na hakuna jipya unaingia ukiwa na kiu ya kujifunza na unatoka ukiwa hajapata kitu Yohana 7;46
§  Mahali ambapo wanakwepa kuwafundisha watu maneno magumu ya uzima wa milele Yohana 6;60-61,66-68

Baada ya kuokoka kama utakaa mahali pa namna hii kwenye mafundisho manyonge ni muhimu kufahamu kuwa wewe nawe utakuwa mnyonge na hutaweza kuingia mbinguni kwani hakuna kinyonge kitakachoingia huko Ufunuo 21;27 wala usikubali vyeo au namna yoyote ya kuwapendeza wanadamu na kukubali kukaa katika unyonge kwa sababu hizo Yeremia 45;5,Wagalatia 1;10, baada ya kuchagua kanisa lisilo na mafundisho manyonge  sasa kaa hapo na uabudu na kumtumikia Mungu. Mungu akubariki sana