Andiko: 1Nyakati 4: 9-10 Biblia inasema hivi:-
“ Naye Yabesi alikuwa mwenye
heshima kuliko nduguze; na mamaye akamwita jina lake Yabesi akisema; Ni kwa
sababu nalimzaa kwa huzuni, Huyo Yebesi akamlingana Mungu wa Israel, akisema,
Lau kwamba ungenibarikia kwelikweli na kunizidishia hozi yangu na mkono wako
ungekuwa pamoja nami, nawe ungenilinda na uovu ili usiwe kwa huzuni yangu, Naye
Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba.”
Utangulizi:
Kitabu cha Mambo ya nyakati
kinaanza kwa kutupa Historia ya ukoo wa Kabila la Yuda na Simeon, hasa katika
sura ya 4:1-43, Hata hivyo katika namna ya kushangaza sana mwandishi anaonyesha
kuwa katika ukoo huo kulikuwa na mtu anaitwa Yabesi na inaelezwa kuwa alikuwa
ni mtu mwenye heshima kubwa sana kuliko ndugu zake wote, ni katika aya mbili tu
yaani ya 9-10 tunapata maelezo yote kuhusu Yabesi, na inaonekana kabla ya kuwa
mtu mwenye kuheshimiwa sana miongoni mwa ndugu zake, inaonekana alikuwa mwenye
kudharauliwa na mwenue huzuni kubwa sana, Biblia inaonyesha kuwa mama yake
alimpa jina hilo YABESI akimaanisha juu ya huzuni, kwa sababu alimzaa kwa
huzuni. Hatufahamu kwa undani sana ninikilitokea katika nyakati zake, ni shida
gani iliipata familia yake lakini ni wazi kuwa alikuwa na mfumo wa maisha ya
huzuni na alizaliwa katika mfumo huo na alipewa jina la jinsi hiyo, Habari njema
ni kuwa hata hivyo Yabesi alifanikiwa kubadili mfumo wa Maisha yake na hatimaye
kuwa mtu mwenye heshima sana, na mwenye utajiri mkubwa na mwenye kutegemewa na
ndugu zake na kuheshimika sana
Jinsi ya kubadili mfumo wa maisha
Yabesi anatufundisha jinsi
alivyofanikiwa kubadili mfumo wa Maisha na kufanikiwa kutoka katika huzuni kuwa
mwenye furaha, kutoka katika maisha yasiyo na heshima kwenda kwenye
kuheshimika, kutoka katika maisha yaliyojaa umasikini kuelekea kwenye utajiri wa
kweli ni namna gani Yabesi alibadili mfumo wa maisha yake kanuni alizozitumia
Yabesi zinauwezo mkubwa sana wa kubadili mfumo wa maisha yetu pia
1.
Yabes
akamlingana Bwana Mungu wa Israel.
Kumlingana Mungu
wa Israel maana yake ni kumtafuta Mungu kwa njia ya maombi na kukubali kufuata
sheria zake, kwa ufupi ni kuhakikisha kuwa anauhusiano wa kweli na Mungu wa
kweli aliye hai, Mtu yeyote yule atakayekubali kuwa na uhusiano thabiti na
Mungu aliye hai, atafanikiwa, Yabesi aliona namna pekee ya kuondoka katika hali
ngumu aliyokuwa nayo kwanza ni kutembea na Mungu, ni kuwa na Mungu wa kweli, ni
kutembea na Mungu aliye hai ni kushikamana naye awaye yote atakayedumisha
uhusiano na Mungu atafanikiwa
2.
Yabesi
aliomba kwaaajili ya hali yake aliyokuwa nayo.
Ni muhimu kufahamu
kuwa jambo lingine lililomletea Yabesi Heshima alikuwa muombaji, alikuwa
akimuomba Mungu na tunaelezwa kuwa “Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba” mtu
awaye yote akidumisha uhusiano wake na Mungu atakuwa na maombi yenye matokeo,
maombi yenye kujibiwa, Yabesi aliomba Mungu ambadilishie hali ngumu alizokuwa
nazo,ni ukweli usiopingika kuwa Yesu alituambia kuwa ninyi mkikaa katika neno
langu, na maneno yangu yakikaa nadi yenu ombeni mtakalolote nayi mtatendewa.
3.
Yabesi
aliomba kwamba Mungu apate kumbariki.
Ni muhimu
kufahamu kuwa hakuna Baraka za muhimu zilizo kuu kama Baraka za kiroho, huo
ndio msingi wa mambo mengine ya kimwili, Baraka za Mungu ni halisi na ndizo
zinageuka kuwa vitu halisi, unaweza kuwa na kila kitu lakini bila mkono wa Mungu
ukakosa amani, Yabesi hakutaka mchezo na Mungu aliomba kwa kudhamiria Lau
Kwamba Ungenibariki kweli kweli Biblia ya KJV “Oh that You would bless me
indeed” NIV “Oh, that you would bless me” hapa napenda Tafasiri ya Mfalme James
KJV kwamba ungenibariki kweli kweli, unibariki hasa
4.
Yabesi
aliomba kwamba Mungu apanue HOZI yake.
Neno hozi
linazungumzia umiliki, mipaka, mtaji, mali heshima, uthamani, Thamani yake
ilikuwa chini na sasa anamuomba Mungu azidishe uthamani wake kama alikuwa
anazaraulika katika jamii mungu aongeze heshima,kama alikuwa anamiliki kidogo
amiliki zaidi, NIV-expand my territory!, NASB-enlarge my border, KJV-enlarge my
border, hapa pia napendezwa na tafasiri ya KJV kukuza uthamani, ili kubadilisha
mfumo wa maisha ni muhimu tukamuomba Mungu akuze uthamani, awaye yote
asilidharau Taifa letu, shule yetu, familia yetu, jamii yetu, lugha yetu,
tamaduni zetu na maisha yetu Mungu ayaongeze thamani, tunaweza kudharaulika kwa
sababu ya umasikini tulio nao, elimu tulizo nazo lakini Mungu anaweza
kubadilisha mfumo wa maisha yako kwa kumsihi azidisha Hozi yako.
5.
Yabesi
aliomba kwamba Mkono wa Mungu uwe pamoja naye.
Ndugu yangu
hakuna jambo baya sana duniani kama mkono wa Mungu ukiondoka juu yako, Naomi alielewa
vizuri kuwa mkono wa Bwana ukitoka juu yako hakuna mafanikio mikozi na balaa
vinaweza kukuandama , kila unalolifanya halifanikiwi Ruthu 1:11-14, mkono wa Bwana ukiondoka juu ya mtu, kinachofuata ni
uchungu kilio na maombolezo na hasara, hakuna utakachokifanya kinaweza
kufanikiwa, Yabesi alielewa kuwa mkono wa Bwana ukiwa juu yako kila kitu
kitafanikiwa na ndio maana Yabesi alifahamu umuhimu wa mkono wa Mungu kuwa
pamoja naye Mkono wa Bwana ukiwa juu ya mtu, maana yake Bwana atakuongoza,
atakulinda, atakupa kibali,utapata fadhili na kufanikiwa katika mambo yote.
6.
Yabesi
aliomba kwamba Mungu amlinde na Uovu.
Kulindwa na uovu
kunakotajwa hapa kumekuwa na tafasiri mbali mbali, uovu unaotajwa hapa unaweza
kumaanisha pia dhambi, lakini hapa Biblia nyingi katika tafasiri zake zimetumia
maneno kama matatu ya kiingereza “Evil,
Pain, Harm, Stresses” ikimaanisha uovu wenye kuleta Huzuni, ni wazi kuwa dhambi
inasababisha huzuni katika maisha yetu na ni vema kumuomba Mungu akatulinda na
kutuweka mbali nayo, lakini Biblia inazungumzia zaidi, uovu unaoleta huzuni
yaani hasara na kulindwa na maadui au uonevu, kimsingi tunaweza kumuomba Mungu
atulinde na Uovu wa dhambi, Uovu wa taabu na huzuni, uovu wa maadui na kuonewa
uovu wenye kuharibu mafanikio yetu Mithali 10:22 “Baraka za Bwana hutajirisha wala hachanganyi huzuni nayo”
Mungu alijibu Maombi ya Yabesi na
kubadilisha mfumo wa Maisha yake, awaye yote ambaye anataka kubadili mfumo wa
maisha yake kutoka katika hali yoyote ile isiyokupendeza unaweza kumuomba Mungu
kama Yabesi na Mungu atakusikia na kukujalia uliyoyaomba. Bwana ampe neema kila
mmoja wetu kubadili mfumo wa maisha yake katika Jina la Yesu Kristo mwana wa
Mungu aliye hai amen!
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!