Jumamosi, 13 Julai 2019

Kwa mfano wetu na kwa sura yetu!


Mwanzo 1:26 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.




Utangulizi:


Ni muhimu kufahamu kuwa moja ya siri ya mafanikio makubwa sana ya mwanadamu, ni pamoja na kuwa katika mfano  na sura ya Mungu, (Image and likeness). Mwanadamu wa kwanza kabisa katika bustani ya Edeni hakuwa mtu wa kawaida alikuwa mkamilifu na mtakatifu, alikuwa ameumbwa tayari kwa kuutawala ulimwengu na kila kilichomo ndani yake, hakuwa amekusudiwa afe, augue au akose kitu au apoteze uhusiano wake na Mungu hakukusudiwa akose amani na furaha au akose utoshelevu, Chini ya uwepo wa Mungu mwanadamu aliumbwa afanikiwe katika kila jambo, Afanikiwe katika mambo yote, aweke mambo yote chini ya miguu yake, atawale atiishe,awe na mamlaka na uweza chini ya uwepo wa Mungu, Hata hivyo Biblia inaonyesha Katika mwanzo 3 kuwa kila kitu kiliharibika mara baada ya anguko, mwanadamu alipoteza sura na mfano wa Mungu, alipungukiwa na utukufu wa Mungu,


Warumi 3:10-12,23 “10. kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. 11. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. 12. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja. 23. kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;


Matokeo yake ni kuwa mwanadamu alitawaliwa na Mazingira yake, alipoteza hekima ya kuyatawala mazingira yake, alipoteza ukamilifu, uwezo wa kuutawala ulimwengu ulipungua, na mwanadamu amepoteza tumaini na Mfano na sura ya Mungu iliharibiwa, Ili mwanadamu aweze kuwa na mafanikio makubwa na kuwa na nguvu kama ile iliyokusudiwa kwa Adamu, ni muhimu sana akarejea katika Mfano na sura ya Mungu.


Kwa mfano wetu na kwa sura yetu.


Katika moja ya mistari ya Msingi na ya Muhimu sana katika kitabu cha mwanzo Mstari wa Mwanzo 1: 26, Mstari huu una nguvu kubwa sana, Uelewa wa kutosha katika mstari huu utatufanya tuweze kuona ubora wa mwanadamu na kumtukuza Mungu hata kwa jinsi alivyotuumba na kisha kuendelea kumtegemea Mungu kwa asilimia 100 na kuacha kujivuna.


Kwa mfano wetu na kwa sura yetu. (in our image, in our Likeness)
Kwa sura wetuin our image – A representation of the external form of a person- Muonekano wa nje
Kwa mfano wetuin our likeness – The fact or quality of being alike, similarity -  mfanano wa kitabia na uadilifu.


Kwa msingi huo ni wazi kuwa mwanadamu aliumbwa akiwa anafanana na Mungu kimaumbile, kitabiana kimaadili. Hivyo basi mafundisho yoyote au theory yoyote inayoshusha thamani ya mwanadamu, au tabia au mwenendo wowote unaoshusha thamani ya mwanadamu kimaandiko unamkosea sana Mungu na kumdhalilisha Mungu na ubora wa uumbaji wake, katika mstari huu tunajifunza sasa kwamba;-


1.       Unaonyesha wazi kabisa kuwa Mwanadamu aliumbwa na Mungu na kuwa hakutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi, “Evolution theory” Mwanzo 1;27, Mathayo 19:4, Marko 10:6 Mwanzo 1:27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.”  Mathayo 19:4 “Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke,” Marko 10:6 “Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke.” 


     Mistari hii ya Musa na maneno ya Yesu inatuthibitishia wazi kuwa mwanadamu anatokana na kuweko kwa kusudi la Mungu, Mwanadamu sio kiumbe cha kawaida, Mungu amemtukuza mwanadamu na kumtawaza juu ya kazi zake zote, na kamwe mwanadamu sio matokeo ya bahati mbaya wala mabadiliko ya tabia ya nchi, mwanadamu ni kiumbe cha juu zaidi katika kazi na utendaji wa Mungu, sio kiumbe cha kudharauliwa wala kuvunjiwa heshima, sio kiumbe kilichoumbwa kuwa mtumwa wa mtu au mazingira, sio bidhaa inayoweza kuuzwa kama ng’ombe kila mtu anapaswa kuelewa kuwa anaposhughulika na mwanadamu anashughulika na kiumbe ambacho Mungu amekitukuza mno, uhai wake haupaswi kutolewa kijinga na kirahisi, maisha ya kiumbe hiki hayapaswi kupuuziwa na kuachwa yapotee kirahisi, Mwanadamu ni wa thamani, ametoka katika wazo na mpango kamili wa Mungu.


2.       Mwanadamu ndio kiumbe pekee kilichoumbwa kuwa na ushirika wa karibu zaidi sana na Mungu, hata kama viumbe vyote vimeumbwa kwaajili ya utukufu wa Mungu ili vipate kumuabudu Mungu, Mwanadamu ndie kiumbe bora zaidi ambaye Mungu anapendezwa naye, anafurahia kuabudiwa naye, Mungu alikusudia kuwa na ushirika wa karibu na mshikamanifu sana na Mwanadamu kuliko kiumbe kingine chochote Waebrania 2:6Mwanadamu ni nini hata umkumbuke, Ama mwana wa binadamu, hata umwangalie?” linapokuja swala kuhusu Mwanadamu Mungu huwezi kumwambia kitu, yuko tayari kumkumbuka yuko tayari kumwangalia, Historia ya mwanadamu inaonekana hapa kwamba alikuwa na ushirika “mgumu” “Athletic fellowship na Mungu, walikuwa na uadilifu wa hali ya juu, walikuwa wakamilifu, hawakuwa na dhambi, walikuwa watakatifu, wenye hekima, moyo wa ujasiri, waliokuwa na upendo kamili, ukarimu na wasiokuwa na ubinafsi wala choyo, na uamuzi uliweza kutumika kufanya maamuzi yaliyo sahihi, Mungu alikusudia nawe na ushirika wa karibu zaidi na mwanadamu unaozidi undugu na kwamba mwanadamu amtegemee yeye.


3.       Walipewa neema ya kuwa mfano na sura ya Mungu, Hili nalo ni moja ya jambo muhimu sana ambalo wasomi wengi wa kimaandiko hawaelewi uzito wa andiko hili, Swali kubwa la kujiuliza linalozaliwa na Mwanzo 1:26 ni kuwa sisi tuliumbwa kwa mfano na sura yake Mungu, hii ina maana gani? Andiko hili lina maana kubwa sana kinabii kwamba Mungu mwenyewe aliwapa wanadamu Mwili (Sura, Umbile Muonekano) ambao yeye mwenyewe angeweza kuja kujitokeza na kuonekana kwao, na kuwa wenzake 


     Mwanzo 18:1-141.BWANA akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari. 2. Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi, 3. akasema, BWANA wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako. 4. Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu. 5. Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema. 6. Basi Ibrahimu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate. 7. Ibrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng'ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa. 8. Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala. 9. Wakamwambia, Yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo hemani. 10. Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. 11. Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. 12. Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee? 13. BWANA akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? 14. Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda BWANA? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume” Unaweza kuona Mungu aliweza kujitokeza kwa Abrahhamu na kufanya mazungumzo naye katika namna ya kawaida kabisa kwa mwili ule ambao Mungu alikuwa nao; Zaidi ya yote Mungu alikuwa anamaanisha kuwa kinabii angekuja na kujitokeza kwa wanadamu akiwa na mwili sawa na ule wanaoutumia wanadamu ili awaonyeshe njia mwili ambao Yesu alikuwa nao Luka 1:35 “Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.” Kimsingi Mungu alipokuwa akimuumba mwanadamu alikuwa na wazo la Yesu, au wazo lake yeye mwenyewe, kwa hiyo basi mwanadamu kuwa na mfano na sura ya Mungu maana yake ni kuwa kama Yesu, ambaye ni Mungu na alikuja duniani kwa nia ya kuutwaa mwili Yohana 1;1,14Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa MunguNaye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli. Mungu amekusudia wote tuwe kama Yesu tangu mwanzo, tofauti yetu ni kuwa sisi na baba yetu Adamu alipoteza hali ya kuwa na mfano na sura ya Mungu (Likeness) tunapokuwa tumeokolewa na kumuamini Yesu Mungu anaturatajia turejee na kuwa wakamilifu kama yeye mwenyewe kwa kuufuata mfano wa Yesu Kristo “Kwa mfano wetu na kwa sura yetu” tunapomuamini Yesu kwa imani tunakuwa kama Yesu Mungu anatukubali kwa neema na kututazama kama yeye mwenyewe na kuwa na ushirika nasi kama atakavyo yeye, inahitajikia neema ya Mungu kulielewa hili. Na Mungu akupe neema hiyo katika jina la Yesu.


4.       Mstari huu Mwanzo 1;26 unatukumhbusha sisi asili yetu Kimaadili, kwamba tulikuwa wakamilifu kama Mungu, lakini tumepoteza ile hali yabuadilifu ya kuwa kama Mungu, sio hilo tu tumepoteza hali ya kuwa na ushirika na Mungu, kuja kwa Yesu Duniani kulikuwa na kusudi la kutujenga tena katika ule uadilifu, na hivyo Yesu ametuachia kielelezo tukifuate Yohana 13:15 Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo.”


Madhara ya kupoteza sura na mfano wa Mungu.


Ni muhimu kufahamu kuwa ili tuweze kuwa na ushirika wa karibu na Mungu ni lazima tushughulikie sana swala la kufanana na Mungu “likeness” ambalo mwanadamu amelipoteza, hili ndio jambo la msingi, tunapokuwa na watumishi wa Mungu walioitwa kwa makusudi mbalimbali ya kuujenga mwili wa Kristo lazima ikumbukwe kuwa kusudi letu kuu ni kuwa kama Kristo, Adamu wa kwanza alikuwa kama Kristo lakini alipoteza, na kuathiri jamii nzima ya iana binadamu, sasa basi ni lazima tulenge kuwa kama Kristo Waefeso 4:11-13 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa KristoHili ndio Jambo la msingi na la muhimu mno Yesu amekuwa kielelezo chetu tunapaswa kumfuata tunapaswa kumuigiza tunapaswa kuwa kama yeye, kila mmoja wetu anapaswa kujiuliza kama anafanana na Yesu, Ushirika wa karibu na wenye nguvu na Mungu utategemea namna na jinsi tunavyomtegemea yeye, kwa nguvu zetu hatuwezi lakini chini ya neema yake tunaweza kujitegemeza kwake na sura na mfano wa Mungu ukawepo ndani yetu. Hili ni jambo la Muhimu


Mwaka 1972 wakati wa uchaguzi wa Rais Huko Marekani, wagombea wawili maarufu sana waipambana kuwania kiti cha urais, 1 aliitwa Richard Nixon, aliyetokea California akiwakilisha chama cha the republican na Mpinzani wake aliitwa George McGovern, aliyetokea jimbo la South Dakota akiwakilisha chama cha Democratic Katika uchjaguzi huo George McGovern alishindwa vibaya, Kura za turufu za Marekani Electoral vote Nixon alipata 520 na George alipata 17, Inaelezwa moja ya sababu kubwa ya kushindwa kwa George ni kuwa wakati walipofanya kampeni zao kwa njia ya Radio kila mtu alivutiwa sana na George Sauti yake ilikuwa yenye mvuto mkubwa sana na yenye ushawishi ukilinganisha na Nixon hata hivyo mara walipokuja kuonekana kwa njia ya Television Muonekano wao ulikuwa tofauti sana George alikuwa ametoka kuugua, na hivyo alikuja studia akiwa amejifunika koti na sweta, alionekana kuchoka sana na muonekanao wa afya yake pia haukuwa mzuri, alikataa kufanyiwa make –up na kupakwa poda na kufanyiwa maandalizi ya kurushwa katika televisheni huku Nixon alionekana mwenye afya njema na aliyekuwa amefanyiwa make up ili muonekano wake uwe Mzuri, kumhbuka hii ilikuwa debate ya mwisho, watu walikata tamaa sana walipoona muonekano wa George na hivyo Nixon ambaye hakuwa mnenaji Mzuri alichaguliwa kura rais wa marekani.


 

 








 
George McGovern  Kushoto – Democratic  na Richard Nixon Kulia- Republican


Nini kilimpa Nixon ushindi mkubwa ilikuwa ni Sura yake, muonekano wake, nini kitatupa ushindi katika maisha yetu, ni kitu gani kitatufanya tukubaliwe na Mungu na wanadamu, nini kitatufanya tuwe na mvuto na ushirika wa karibu sana na Mungu ni Sura na mfano wa Mungu, Mwanadamu atakuwa kiumbe chenye utukufu mkubwa anapokuwa anazishika njia za Mungu, atakuwa na ukaribu naMungu akijitahidi kuwa kama Yesu, Ni lazima kila mmoja wetu akubali kumwamini Yesu na kujifunza kuwa kama Yeye ili tuweze kupata kibali kwa Mungu, Shetani atakosa la kutushitaki ikiwa tutamfanania Mungu, Bwana na ampe neema kila mmoja wetu kuwa na sura na mfano wa Mungu ili tuweze kupata kibali mbele za Mungu. Lazima tujitahidi kujionyesha kuwa tumekubaliwa na Mungu 2Timotheo 2;15

Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!

Endapo umebarikiwa na Masomo yangu tafadhali usisite kunijulisha namna na jinsi ulivyobarikiwa kama wafanyavyo wengine sms au whatsapp me kwa +255 718 990 796

Jumatano, 10 Julai 2019

Ee Bwana unijie Hima!


Zaburi 141:1-2Ee Bwana, nimekuita, unijie hima, Uisikie sauti yangu nikuitapo. Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba, Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni.”

Muhamiaji aliyeingia Nchini Ufaransa na kugeuka Mwokozi wa haraka Mamouddou Gassama .

Utangulizi:
Tarehe 28 May 2018 Dunia ilipata habari za mshangao na mara moja jina la raia wa Mali ajulikanaye kama Mamoudou Gassama lilipata umaarufu mkubwa, Mara baada ya kijana huyo kufanya tukio la kishujaa la kumuokoa mtoto mdogo aliyekuwa ananing’inia Katika ghorofa na aliyekua anaonekana anakaribia kuachia na kupoteza maisha

Tukio hili la haraka la kuokoa maisha ya mtoto, ghafla liliweza kubadilisha jina la kijana huyuwa Mali, aliyekuwa ni mzamiaji tu katika nchi ya Ufaransa, kijana huyu alijulikana kama shujaa na watu wengi walimuita “SPIDERMAN” Gassama kutokana na ushujaa wake alialikwa na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ikulu na kupata naye chai kisha kumpongeza kwa tendo lake la ushujaa, alifutiwa halia ya kuwa mzamiaji na kupangiwa kupewa kazi na mafunzo kupitia kikosi cha uokoaji  na zimamoto cha ufaransa BRAVO alisema rais Macron akimsifia Gassama kwa kazi njema, lakini pia alimzawadia medali ya Ujasiri na kujitoa, Gassama alipanda kwa haraka baraza kwa baraza mpaga ghorofa ya tano alikokuiwako mtoto huyo wa mika minne na kufanikiwa kuyaokowa maisha yake.

Gassama anasema walikuwa wakiangalia mpira na ghafla alisikia sauti ya watu wakipiga kelele za mayowe ya kukata tamaa na alipotoka na kuona ni mtoto anasema alimuhurumia na kwa kuwa anapenda watoto hakujiuliza maswali alijikuta anapanda na kuokoa maisha ya mtoto huyo kwa haraka.

Ee Bwana nimekuita unijie hima!

Ni muhimu kufahamu kuwa katika maisha yetu yako majaribu na changamoto za aina mbalimbali na kwa kawaida changamoto na majaribu huwa hayapigi hodi wakati yanapokuja , unaweza ghafla tu ukajikuta umevunjika moyo na umekata tamaa, ama unaweza kuwa kwenye wakati wa furaha kubwa , au ukajikuta umejeruhiwa na kushindwa bila maandalizi, wala hodi, wala kibali, majanga yanakuja tu yanakukabili kama kimbunga na wakati wote majaribu yanakuja kwa kusudi la kukupeleka chini na kukukatisha tamaa

Majaribu yanaweza kukuweka au kukuacha ukiwa unabembea kama mtoto yule na huu ndio wakati ambapo uatamtaka mwokozi ajitokeze kwa haraka aje akusaidie na hiki ndicho kilichomkuta mwandishi wa Zaburi 141: 1Ee Bwana, nimekuita, unijie hima, Uisikie sauti yangu nikuitapo. Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba, Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioniMwandishi alikuwa anahitaji msaada wa haraka Biblia ya kiingereza ya NIV inasomeka hivi “O lord, I call to you; come quickly to me , hear my voice when I call to you”wataalamu wa maandiko wanasema Zaburi hii ni ya Daudi na ni wazi kuwa ilisemwa wakati wa tukio linalotajwa katika 1Samuel 24:1-22 hususani kwa kitendo cha Sauli aliyekuwa akimtafuta Daudi kwa hasira na kutaka kumuua, wakati huu Sauli aliingia katika pango ambalo kwa bahati Nzuri Daudi alikuwa amejificha na watu wake, Daudi angeliweza kumdhuru Sauli kwa kumkata na panga huko ENGEDI lakini Daudi aliweza kujizuia asiyadhuru maisha yake, aliweza kukata upindo nwa vazi lake, na akiwa kimyaaa baadaye Sauli alitoka katika Pango lile na Daudi alitoka katika pango lile nankisha akakaa ng’ambo na kumueleza kuwa angeweza kumuua lakini aliheshimu kuwa yeye ni mpakwa mafuta japokuwa yeye alitoka kutafuta kumuua na timu yake yote lakini yeye Daudi hakumuua

Ni Katika wakati ule wa hatari sana Daudi aliomba maombi haya wakati Adui yake akiwa karibu kabisa kumuangamiza na endapo tu angeshindwa hata kuzuia kinywa chake Sauli angegundua kuwa daudi nyuko karibu na angemuangamiza

Lilikuwa ni jaribu zito na la ghafla katika maisha ya Daudi Lakini Mungu alimetetea, tunajua kuwa wakati wa Mungu ni mzuri zaidi, na kuwa hatuwezi kumlazimisha Mungu kujibu maombi yetu, Lakini iwe ni kwa haraka au taratibu ni lazima tumuonyeshe Mungu kuwa hatuna kingine tunachikitegemea isipokuwa yeye tu

Kwa vile bado tungalimo duniani, jambo lolote laweza kutokea je wakati huo unakimbilia nini? Ni jambo gani unaweza kulitumaini kwa haraka, ni jina gani unaweza kuliita kwa haraka unapokuwa umevamiwa na changamoto, lazima tujikite katika kuonyesha kuwa tunahitaji rehema za Mungu, kila wakati katika maisha yetu, tuendelee kuliiitia jina la Mungu

Pale jijini Paris watu wengi walikuwa wamemuona mtoto yule aliyekuwa anabembea, na wote walianza kulia na kupiga kelele, mtoto alikuwa hatarini alikuwa kwenye uhitaji wa msaada wa haraka wakati huu Mungu alimtumia mkimbizi, muhamiaji, mzamiaji kutoka mali, mweusi kumuokoa mtoto huyu, Hakuwa ndugu yake wala wa jamaa yake alimuonea huruma akafanya haraka

Uko wakati katika maisha yetu tunamuhitaji Mungu kwa haraka aafnye hima atusaidie, hatujui atatumia njia gani, lakini tukimtegemea yeye yeye ni msaada ulio karibu, Yeye si Mungu aliyembali

Zaburi 46:1-3
Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.”

Namsihi sana Mungu awe Msaada ulio karibu katika maisha yako wakati yanapokujia maswala mazito ya ghafla

Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima.

Endapo umebarikiwa na mafundisho haya tafadhali moyo wangu ungependa kujua sms kwa namba 0718990796 pia kwa whatsApp Ubarikiwe sana

Walioalikwa Harusini wawezaje kuomboleza



Mathayo 9:14-15Wakati ule wanafunzi wake Yohana wakamwendea, wakasema, Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi? Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga.

  

Utangulizi:

Wanafunzi wa Yohana Mbatizaji walikuwa miongoni mwa watu waliopendezwa sana na kuvutiwa na utendaji  na mafundisho ya Yesu Kristo, Licha ya Yohana Mbatizaji kuwa nabii mwenye nguvu na kuheshimika sana,ambaye kazi yake kubwa ilikuwa ni kuandaa njia kwaajili ya Masihi, wanafunzi wake vile vile walivutiwa kumsikiliza Yesu, huenda nao pia walitaka kulinganisha kweli kadhaa kuhusu mafundisho ya Yesu na yale ya mwalimu wao wa kwanza Yohana Mbatizaji.

Yohana mbatizaji alikuwa amewafundisha watu wake kufunga, hili ni moja ya somo muhimu sana la wakati wote tuwapo Duniani, Yesu hajawahi kulikataaa somo kuhusu kufunga hata na yeye alisisitiza sana watu wafunge, Yesu mwenyewe kabla ya huduma alifunga siku 40, kufunga ni muhimu sana, Katika hutuba yake ya Mlimani Yesu alikazia sana juu ya kufunga na tena alitaka kufunga kwa wanafunzi wake kuwe ni zaidi ya kufunga kwa Mafarisayo akithibitisha kuwa baba anaona sirini na kujalia kile ambacho mfungaji amekikusudia, Mungu atatupa thawabu tufungapo sawa na maelekezo ya Yesu


Mathayo 6:16-18
Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi” Swali kubwa la wanafunzi wa Yohana Mbatizaji ilikuwa mbona sisi na Mafarisayo tunafunza lakini wanafunzi wako hawafungi? Jibu la Yesu ndilo linalotupa somo kuu katika siku ya leo;-

Yesu alijibu walioalikwa Harusini wawezaje Kuomboleza?

Kwa mujibu wa tamaduni za kiyahudi mtu alipooa, waliooana walitakiwa kukaa nyumbani kwa mapumziko, walitakiwa kuwa kama Mfalme na Malkia, walihudumiwa na watu maalumu, waliokuwa na majina maalumu, walioitwa wana wa chumba cha harusi, walihudumia watu kwa furaha wiki nzima watu wakifurahi na kula na kunywa vyakula vya aina mbalimbali, ulikuwa ni wakati wa furaha kwa tamaduni za Israel.

Katika desturi za kinabii manabii wengi walitabiri kuja kwa Masihi, ujio wake ulifananishwa na ujiio wa bwana harusi kila mmoja alijua kuwa siku za faraja na furaha zinakuja na Masihi mkuu atakapokuja

Isaya 54:4-6
Usiogope; maana hutatahayarika; wala usifadhaike; maana hutaaibishwa; kwa kuwa utaisahau aibu ya ujana wako, pia mashutumu ya ujane wako hutayakumbuka tena. Kwa sababu Muumba wako ni mume wako; Bwana wa majeshi ndilo jina lake; na Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako; Yeye ataitwa Mungu wa dunia yote. Maana Bwana amekuita kama mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni, kama mke wakati wa ujana, atupwapo, asema Mungu wako”. Unaweza pia kuona katika

Isaya 62:4-5Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefsiba; na nchi yako Beula;kwa kuwa Bwana anakufurahia ,na nchi yako itaolewa.Maana kama vile kijana amwoavyo mwanamwali, ndivyo wana wako watakavyokuoa wewe; na kama vile bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe”.

       
Kwa hiyo wataalamu wa maandiko wa Kiyahudi walikuwa wanajua wazi kuwa Bwana harusi anayetajwa na kutabiriwa katika maandiko hayo ni Masihi, hivyo walikuwa wakimsubiri, Majibu ya Yesu kwa wanafunzi wa Yohana Mbatizaji yalitaka mioyo yao ifunguliwe waelewe kuwa Yeye ndio Masihi, na kwa sababu hiyo anapokuwepo Masihi yaani kwanini watu wasifurahi, kimsingi Yesu hakukataza watu wasifunge, Lakini funga yetu haiwezi kuwa funga ya maombolezo kama watu wasio na matumaini, haipaswi kuwa ya kujivika magunia na kujipaka Majivu, na kulia kama watu waliokata tamaa, hii ilikuwa funga yenye mtazamo wa agano la kale, sisi kwetu kufunga ni ibada

Matendo 13:1-21
. “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia

Yesu anataka watu wake wamfanyie ibada sii maombolezo unafunga huku uko smart unatabasamu, unaoga unajipaka mafuta na kupendeza na kwa siri wala si kwa namna ya mafarisayo walikuwa wanafanya, Kimsingi Yesu ni ukamilifu wa Furaha.

Alipo Yesu maana yake Mungu yupo, ukiwa naye maana yake uwepo wa Mungu upo, Yaani inakuwaje mtu awe katika uwepo wa Mungu kisha awe anaomboleza? Popote Yesu alipo haiwezekani kuwe na matanga, Haiwezekani mtu aalikwe Harusini au aje kwenye Karamu amefunga uwepo wa Mungu katika maisha yetu ni wa muhimu sana, Hakuna jambo tamu duniani akama kukaa katika uwepo wa Mungu, Ni furaha kuwa katika uwepo wa Mungu, Kufunga katika agano la kale kulimaanisha kupoteza matumaini, kukumbwa na huzuni, kuomboleza, kuwa na huzuni kwa sababu ya dhambi na kuharibika kwa dunia, kwa sababu ya kutengwa mbali na Mungu, kwa sababu ya majanga, kwa sababu ya kupoteza matumaini hivyo waliofunga katika agano la kale walikuwa katika mtazamo wa kuhuzunika wakihitaji msaada wa Munhgu aweze kuingilia kati, kuwa na Yesu kuwa na uwepo wa Mungu kutakufanya usiwe na huzuni, Alipo Yesu ni Harusi na sio matanga.

Mahali alipo Bwana Yesu ni furaha na amani, Hakuna huzuni ambayo Yesu anashindwa kushughulika nayo, naweza kusema kuwa tafuteni kwa bidii kuwa na uwepo wa Mungu na mengine yote yatashughulikiwa, Masihi alitarajiwa katika Israel kama Bwana harusi ambaye angeondoa huzuni za watu waliokata tamaa, angeweza kujibu kila aina ya changamoto ambazo watu wangekutana nazo, kama kuna jambo kubwa tunapaswa kulifurahia ni kuwa na huyu Bwana mkubwa na kutunza uwepo wake, Yeye ni tabibu kwa wasio na afya,ni mfariji kwa wenye huzuni, ni kicheko kwa wanaolia, ni majibu kwa wenye maswali, ni furaha kwa wenye huzuni, ni harusi kwa wanaoomboleza, anaweza kubadili msiba kuwa harusi, anaweza kubadili matarajio ya ya adui zako wanaofikiri umekwisha wanashangaa unainuliwa.

Watu wa ulimwengu wakikusumbua usihuzunike wewe umealikwa harusini wawezaje kuomboleza? Tembea kifua mbele, acha unyonge ni wakati wa kuinjoy, ni wakati wa kufurahia; furahi pamoja na bwana harusi, achana na mambo yaliyokwisha kupita alika na wengine harusini , watu wale na kunywa. Wewe unaye Yesu unaye Bwana harusi maombolezo ni ya nini, yeye ana majibu yote ya misiba yako, jiving nguo za harusi, ukiwa na Yesu acha kulia changamka, ahaaa haiwezekani uomboleze ili hali umealikwa harusini, haiwezekani ujipake majivu, haiwezekani uvae nguo za maombolezo ili hali mwana wa seremala anaoa, na wewe ni mgeni wa Bwana harusi, Nasema hivi changamka huzuni yako lazima ibadilike kuwa furaha , msiba wako lazima ugeuke kuwa harusi, huzuni yako lazima igeuke kuwa kicheko kwa sababu Mwana wa seremala amenituma nikukumbushe kuwa uwepo wake ni wa thamani kubwa sana kaa uweponi mwake hapa ndipo penye kilele cha furaha, ukiondoka uweponi mwake umerejea kwenye maombolezo, ndio maana mimi nimekusudia nitaandamana na Yesu, nitamfuata Yesu, nitamshika Yesu, nitamuhubiri Yesu, sitajali watru wananena nini juu yangu, ama wanahistoria gani kunihusu mimi najua neno moja tu niko uweponi mwake wala sitaondoshwa, nina kadi nimealikwa rasmi na Bwana Yesu nikionyesha kadi yangu hakuna wa kunizuia mlangoni nina kibali chake naungana naye kusheherekea, ni wakati wa kufurahi huwezi kunichinganisha na Bwana harusi,best mana wake ni Yihana mbatizaji ahaaaaaa Yeye alithibitisha wazi kuwa Yesu ndiye Bwana harusi mwenyewe

Yohana 3:27-30 “Yohana akajibu, akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka mbinguni. Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya kwamba nalisema, Mimi siye Kristo, bali nimetumwa mbele yake. Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti yake bwana arusi. Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua

Alipo Yesu ni Harusi na sio Matanga!
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.

Endapo umebarikiwa na Ujumbe huu tafadhali uisiste kunijulisha kwa ujumbe au Kwa whatsApp kwa namba 0718990796

Jumanne, 11 Juni 2019

Bwana atamwuza Sisera katika mkono wa mwanamke!


Waamuzi 4:1-9Hata alipokufa Ehudi, wana wa Israeli wakafanya yaliyo maovu tena mbele za macho ya Bwana. Bwana akawauza na kuwatia katika mkono wa Yabini, mfalme wa Kanaani, aliyetawala huko Hazori; na Sisera, aliyekaa katika Haroshethi wa Mataifa, alikuwa amiri wa jeshi lake. Wana wa Israeli wakamlilia Bwana; kwa kuwa Sisera alikuwa na magari ya chuma mia kenda; naye akawaonea wana wa Israeli kwa nguvu muda wa miaka ishirini. Basi Debora, nabii mke, mkewe Lapidothi, ndiye aliyekuwa mwamuzi wa Israeli wakati ule. Naye alikaa chini ya mtende wa Debora, kati ya Rama na Betheli, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu; wana wa Israeli wakakwea kwake, awaamue. Huyo akatuma mtu akamwita Baraka wa Abinoamu toka Kedesh-Naftali, akamwambia, Je! Bwana, Mungu wa Israeli, hakutoa amri, akisema, Enenda, ukawavute kwako, huko katika mlima wa Tabori, watu elfu kumi wa wana wa Naftali, na wa wana wa Zabuloni? Nami nitakuvutia Sisera, amiri wa jeshi lake Yabini, hata mto wa Kishoni, pamoja na magari yake, na wingi wa watu wake; nami nitamtia mkononi mwako. Baraka akamwambia, Kama utakwenda pamoja nami ndipo nitakwenda; bali kama huendi pamoja nami, mimi siendi. Basi akasema, Hakika nitakwenda pamoja nawe, lakini safari utakayoiendea haitakupatia heshima wewe; maana Bwana atamwuza Sisera katika mkono wa mwanamke. Debora akainuka, akaenda pamoja na Baraka mpaka Kedeshi.



Utangulizi:-

Ni muhimu kufahamu kuwa katika kanuni za Mungu, Mungu hufanya kazi kwa njia tofauti na njia za wanadamu, na kwa mawazo tofauti na mawazo ya wanadamu, na hata kwa uzoefu tofauti na uzoefu wa wanadamu, Biblia inaonyesha hekima hii ya Mungu na namna yake katika utendaji nwake wa kazi ona:-

1Wakoritho 1:26-29Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu

Katika kitabu cha waamuzi Yaeli ni mojawapo ya mfano wa watu dhaifu ambao MUngu aliweza kuwatumia kuleta ushindi mkubwa kwa wana wa Israel waliokuwa wakionewa na wakanaani chini ya Mfalme Yabin kwa zaidi ya miaka 20, wanawake kumbuka katika jamii ya kiyahudi walikuwa hawapewi umuhimu mkubwa sana waoa hata kuhesabiwa walikuwa hawahesabiki, lakini tunaona Mungu akiwatumia baadhi yao kwa utukufu wake.

Yaeli alikuwa moja ya wanawake ambao Biblia haijawahi kuzungumza habari zao kwa undani, tunajua tu kuwa alikuwa miongoni mwa ma bedui walioishi jangwani na aliyeolewa katika Familia ya Heber mkenizi au mkeni. Mwanamke huyu ndiye aliyetumiwa kukamilisha ushindi wakati wa waamuzi Debora na Baraka.

Israel katika Shida na dhiki.

Ushindi dhidi ya wakanaani ulikuja wakati wana wa Israel wamechoswa na mateso yaliyokuwa yakiwakabili kutoka kwa mfalme wa kanaani Yabin mfalme huyu alikuwa anatawala kanaani na Biblia inasema kuwa alikuwa na Mkuu wa majeshi (Amiri wa majeshi) aliyejulikana kama Sisera, hawa walikuwa na jeshi kali sana Biblia inaeleza kuwa alikuwa na Magari ya chuma mia tisa,  na aliweza kuwaonea sana Israel tena biblia inasema aliwaonea kwa nguvu muda wa miaka 20, halki hii ilikuwa ngumu, Mungu alikuwa kama amewauza yaani ameruhusu wateseke kutokana na kumsahau yeye ingawa yeye hangeliweza kulisahahu Agano lake, hali hii ilipelekea wana wa Israel kulia na kuuugua kwa sababu ya msiba ule wa mateso.

Israel walipolia kwaajili ya mateso yale Maandiko yanaeleza kuwa alikuwepo nabii mke jina lake Deborah aliyekuwa akiwaamua Israel, yeye alijaa Roho na kuambiwa na Bwana amuite mtu anaitwa Baraka ambaye Mungu alimchagua aweze kuyakabili majeshi ya Yabin na kamanda wake Sisera, aliyekuwa Hodari na katili sana na aliyewatesa sana wana wa Israel

Hata hivyo katika namna ya kushangaza Baraka alisisitiza kuwa hawezi kwenda bila Deborah kumbuka Debora alikuwa mwanamke Waamuzi 4:6-9Huyo akatuma mtu akamwita Baraka wa Abinoamu toka Kedesh-Naftali, akamwambia, Je! Bwana, Mungu wa Israeli, hakutoa amri, akisema, Enenda, ukawavute kwako, huko katika mlima wa Tabori, watu elfu kumi wa wana wa Naftali, na wa wana wa Zabuloni? Nami nitakuvutia Sisera, amiri wa jeshi lake Yabini, hata mto wa Kishoni, pamoja na magari yake, na wingi wa watu wake; nami nitamtia mkononi mwako. Baraka akamwambia, Kama utakwenda pamoja nami ndipo nitakwenda; bali kama huendi pamoja nami, mimi siendi. Basi akasema, Hakika nitakwenda pamoja nawe, lakini safari utakayoiendea haitakupatia heshima wewe; maana Bwana atamwuza Sisera katika mkono wa mwanamke. Debora akainuka, akaenda pamoja na Baraka mpaka Kedeshi”.


Bwana atamwuza Sisera katika mkono wa mwanamke!

Debora alikubali ombi la Baraka lakini alimueleza wazi kuwa kutokana na ktaka kwenda vitani na mwanamke ili halinyeye ni mwanaume basi Sisera atauawa na mwanmke  na mwanamke huyo ndiye Yael, Majeshi ya Baraka yalijipanga huku Debora nabii akiwa pamoja naye na bwana alianza kuyafadhaisha majeshi ya Sisera na kuanza kuwapiga vibaya jambo lililopelekea Sisera kukimbia ili kuayasalimisha maisha yake, alikimbilia kwa Yael ambaye nyumba yake iliuwa na mani nay eye hivyo alifikiri kuwa atasalimika alifunikwa na nguo nzito ili kujipumzisha na alipoomba maji ya kunywa alipewa maziwa, maziwa huwa yana tabia ya kuleta usingizi mzito sana na yael alipoona Sisera amelala alichukua mambo na nyundo na kuipigilia kichwani mpaka ardhini na kumuua.

Waamuzi 4:21-24Ndipo Yaeli, mkewe Heberi, akatwaa kigingi cha hema, akashika nyundo mkononi mwake, akamwendea polepole, akamtia kile kigingi katika kipaji chake, nacho kikapenya, hata kuingia mchangani; kwa maana usingizi mzito ulikuwa umemshika; basi akazimia, akafa.  Na tazama, Baraka alipokuwa akimfuatia Sisera; Yaeli akatoka ili kumlaki, akamwambia, Njoo, nami nitakuonyesha yule mtu unayemtafuta. Basi akamwendea, na tazama, Sisera amelala humo, amekufa, na hicho kigingi kilikuwa kipajini mwake.  Basi hivyo Mungu akamshinda Yabini, mfalme wa Kanaani mbele ya wana wa Israeli siku hiyo. Mkono wa wana wa Israeli ukazidi kupata nguvu juu ya Yabini, mfalme wa Kanaani, hata walipokuwa wamemwangamiza Yabini, mfalme wa Kanaani.”

Njia za Mungu sio njia zetu, ni muhimu kufahamu kuwa Nabii katika Biblia anasimama kwa niaba ya watu wa Mungu na Mwanamke anasimama kwa niaba ya kanisa, Kanisa likiomba ni lazima ifahamike kuwa kuna nguvu kubwa sana ya ajabu iliyofichika katika kanisa lake kila mtu anaweza kujipatia ushindi mkubwa kupitia Yesu Kristo, yeye hataweza kulisahahu agano lake alilolifanya nasi pale msalabani atatupa ushindi kwa dhahiri,

·         Ushindi wako hautakuja katika njia ya kawaida unayoidhani Mungu anakwenda kufanya jambo jipya litakalokushangaza

·         Mungu atatumia ulicho nacho katika mkono wako kukupa ushindi nalitumia nyundo na mambo tu kumaliza tatizo kubwa lililodumu kwa miaka 20

·         Haijalishi kuwa tatizo lako lilikuwa baya au ni baya kiasi gani na limekugharimu miaka mingapi leo kwa neno la kinabii kama la Debora ninatamka muujiza na uponyaji kwaajili yako katika jina la Yesu

·         Haijalishi adui yako ana nguvu kiasi gani Sisera alikuwa na magari ya chuma mia tisa lakini alikimbia mbele ya upanga wa Baraka nataka nikuambie na nkukutamkia kinabii leo kuwa kwa jina la Yesu Kristo aliye hai tatizo lako lazima likimbie mbele yako bila kujali kuwa lina nguvu kiasi gani
·         Haijalishi kuwa hujajibiwa mamombi kwa muda gani lakini leo natabiri kwako katika jina la Yesu Kristo Israel waliteseka kwa miaka 20 lakini ka neno la Nabii Debora na na upanga wa Baraka siku moja tu ilileta ushindi mkubwa katika maisha ya Israel na kuwafanya salama leo ninatangaza usalama wako natangaza kwa neno la kinabii na uweza wa jina la Yesu kuwa utajibiwa maombi yako

·         Mungu anakwenda kuzigeuza fadhaa zako kuwa furaha, adui zako kuwa watumwa wako, watesi wako kuwa wakimbizi, waoneziwako kuwa waonewa, waliokutisha kuwa waoga, natangaza mapinduzi ya kijeshi dhidi ya nguvu za giza, dhidi ya majeshi yanpopi wabaya katika ulimwengu wa Roho kwa jina laYesu Kristo na kwa njia ya imani natanmka ushindi dhidi ya msomaji wangu namsikilizaji wangu awekwe huru na amani idumu kwake


·         Hajalishi kuwa kesi yako imesumbua kwa miaka mingapi, wanaokudai hawajarudisha madeni, waliokudhulumu na kukuonea Nasimamisha mwamuzi leo, tunaye muamuzi leo,. Muamuzi wetu leo sio Baraka wala sio Debora wala sio Yael Yuko muamuzi  mwenye haki aliyetupa ushindi kwa njia ya Msalaba huyu ni mwanaume anaitwa Yesu, na akuweke huru leo na akutetee na akutegemeze na akukomboe na akupe furaha na akufungue na akukumbuke na akutazame na akusikie na akufariji na akuinue dhidi ya udhalimu wa kila aina katika masiha yako!

·         Yail hakutumia nguvu hakuwa na uzoefu wa vita hakwenda hata vitani hajui hata kupigana lakini ndiye aliyeu Shujaa aliyesumbua Israel kwa miaka 20, Ndugu zangu neema ya Mungu ikiwa juu yako hakuna kitakachoweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako!

Ramakarashat! Rimasakarutarama! sakatarino, trembeshederengendebe! rimosakarapati yetereseka yatoroseka yakarakata yatoromoskomoli, yenderebisakuramato rimamama sakarenderebe katabash karabakat yerekerebeshe masokolipatei birikuromoto sakarambat.

Nakuombea neema ya Mungu kila amwaminieye hatatahayarika  atakupa kushinda, na kukutetea na kukufungua uwe mtu wa kipekee mtu wa tofauti mtu wa kushangaza na kwa njia laini bwana ana atende na kukutetea dhidi ya uonevu wa kila namna katika jina la Yesu amen. Adui yako na auzwe kwenye mkono wa mwanamke tu. Na aaaibike kwa namna ya ajabu katika Jina la Yesu, amen. Mungu bhatafanya kwa sababu ya ujuzi wetu, uzoefu wetu, elimu yetu bali atafanya kwa sababu ya neema siri ya ushindi wa kanisa ni neema sio mazoezi, sio nguvu, sio uwezo ni neema yake neema yake na iwe juu yako kama ilivyokuwa kwa Yael

Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima.