Mwanzo 20:3-7 “Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku,
akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni
mkewe mtu. Basi Abimeleki alikuwa hakumkaribia, akasema, Ee BWANA, Je! Utaua
hata taifa lenye haki? Je! Hakuniambia mwenyewe, Huyu ni ndugu yangu? Na
mwanamke mwenyewe naye alisema, Huyu ni ndugu yangu. Kwa ukamilifu wa moyo
wangu, na kwa kuwa safi mikono yangu, nimefanya hivi. Mungu akamwambia katika
ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo
nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse. Basi sasa
umrudishe mwanamke kwa mtu huyo, maana yeye ni nabii, naye atakuombea, upate
kuishi. Bali usipomrudisha, fahamu ya kwamba kwa hakika utakufa wewe na watu
wote ulio nao.”
Utangulizi:
Leo tutachukua muda kujifunza kwa kina
na mapana na marefu swala zima linalohusiana na Malipizo ya ndoa, Somo kuhusu malipizo
ya ndoa ni mojawapo ya somo gumu ambalo, liko katika fungu la masomo yaitwayo
chakula kigumu, na kwa sababu hiyo sio rahisi sana kupokelewa vema na hata
kutendewa kazi linapokuwa limefundishwa au kuhubiriwa makanisani, hata hivyo
hatuwezi kuacha kuisema kweli yote ya Mungu vilevile kama Neno la Mungu
linavyoagiza, sisi tunahubiri agizo lote la Mungu (All Gospel)
Waebrania 5:11-14 “Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na
ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia. Kwa maana, iwapasapo
kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu
mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si
CHAKULA KIGUMU. Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa
kuwa ni mtoto mchanga. Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili
zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya.”
Somo kuhusu malipizo ya ndoa
linazungumzia katika ujumla wake swala zima la kumrejesha mume au mke ambaye
kwa asili sio wa kwako, yaani kama unaishi na mke au mume ambaye sio wa kwako
wewe ni dhalimu na unasababisha laana au madhara makubwa sana katika familia
yako na mbele za Mungu na ni wazi kuwa ni vigumu sana kwako kuurithi ufalme wa
Mungu na pia unaweza kufa! Au kupata majanga.
Yohana 4:16-18 “Yesu akamwambia, Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa. Yule
mwanamke akajibu, akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume;
kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo
umesema kweli.”
Kwa msingi huo basi tutajifunza somo
hili MALIPIZO YA NDOA kwa kuzingatia
vipengele vitatu viuatavyo:-
·
Maana ya Malipizo
·
Kwa nini Malipizo ya Ndoa?
·
Faida za kufanya Malipizo
ya Ndoa.
Maana ya Malipizo
Neno malipizo Katika lugha ya kiyunani linatajwa kama neno “Epistrofi” au “apodidōmoi” ambalo kwa kiingereza
tunapata neno Restitution au restoration au compensation au reparation
ambalo kwa kiswahili ni kurejesha, kurudisha au kulipa au kufidia, Katika Lugha
ya Kiebrania linatumika neno “shuv”
ambalo maana yake ni kurudisha “to
return” Neno hili katika mafundisho kuhusu wokovu linaenda sambamba na kazi
ya toba au matokeo ya kutubu na kusudi kubwa
la jambo hili ni kutafuta amani au suluhu na ustawi wa kweli miongoni mwa
jamii, malipizi au malipizo yanaweza kufanywa kwa sababu ya kurekebisha makosa
ya zamani ikiwemo kama ulidhulumu, au ulikosea au ulimtakili mwenzi wako na
mambo mengine, Malipizo ni sehemu ya mafundisho ya wokovu ambao msingi wake unaanzia
katika torati na unakaziwa katika injili pia, tunaokolewa kwa imani na kwa
neema baada ya kuamini na kutubu, hata hivyo malipizi ni sehemu muhimu ya kuonyesha
toba yetu kivitendo kuelekea wengine!,
Luka 19:8-10 “Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu
ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila
namrudishia mara nne. Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa
sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta
na kuokoa kile kilichopotea.”
Kwa msingi huo tunapata picha na
kujifunza kuwa Malipizo ni matunda yatokanayo na toba, yaani kabla ya kukutana
na Yesu, au kabla ya kuokoka au hata ndani ya wokovu kama ulimdhulumu mtu na
baadaye ukatubu, toba yako itaambatana na kurejesha vile vitu ulivyodhulumu,
kivitendo, kurejesha vitu vya watu ni tunda la kuonyesha jamii na Mungu
badiliko kubwa ulilonalo la uamuzi wako wa kurejea kwa Mungu sawa tu na waganga
na wachawi wanavyochoma vifaa vya kichawi na uganga! Baada ya kuokolewa kwao.
1Samuel 12:3-5 “Nami nipo hapa; basi, mnishuhudie mbele za Bwana, na
mbele ya masihi wake,nalitwaa ng`ombe wa nani? au nalitwaa punda wa nani? au ni
nani niliye mdhulumu? Ni nani niliyemwonea? Au kwa mkono wa nani nimepokea
rushwa inipofushe macho? NAMI NITAWARUDISHIA NINYI. Nao wakasema,
hukutudhulumu, wala hukutuonea, wala hukupokea kitu kwa mkono wa mtu awaye
yote. Akawaambia, Bwana ni shahidi juu
yenu, na masihi”
Walawi 6:2-5 “Mtu awaye yote akifanya dhambi, na kuasi juu ya BWANA,
akamdanganya mwenziwe katika jambo la amana, au la mapatano, au la
kunyang'anya, au kumwonea mwenziwe; au kuzumbua kitu kilichopotea na kutenda la
uongo juu yake, na kuapa kwa uongo; katika mambo hayo yote mojawapo
atakalolitenda mtu, na kufanya dhambi kwalo; ndipo itakapokuwa, akiwa amefanya
dhambi, na kupata hatia, atarudisha hicho alichokipata kwa kunyang'anya, au
kitu kile alichokipata kwa kuonea, au ile amana aliyowekewa, au kitu kile
kilichopotea alichokizumbua yeye, au kitu cho chote ambacho amekiapia uongo; ATAKIRUDISHA
HATA KWA UTIMILIFU WAKE, kisha ataongeza na sehemu ya tano zaidi juu yake; naye
atampa huyo mwenyewe, siku hiyo ambayo atakapohukumiwa kuwa mwenye hatia.”
Kutoka 22:10-13 “Mtu akimpa mwenziwe punda, au ng'ombe, au kondoo, au
mnyama ye yote, ili amtunzie; yule mnyama akafa, au akaumia, au akachukuliwa
mtu asione; patakuwa na kiapo cha BWANA katikati ya watu hao wawili, kwamba
alipeleka mkono wake kutwaa mali ya mwenziwe, na mwenyewe atakubali hayo, wala
hatalipa. Lakini kwamba aliibiwa mnyama huyo, SHARTI AMLIPE YULE MWENYEWE.
Kwamba aliraruliwa na mnyama mkali, na amlete uwe ushahidi; hatalipa kwa ajili
ya mnyama aliyeraruliwa.”
2Samuel 12:1-6 “Ndipo Bwana akamtuma Nathani aende kwa Daudi. Naye
akamwendea, akamwambia, Palikuwa na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao
alikuwa tajiri, wa pili maskini. Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng'ombe wengi
sana; bali yule maskini hakuwa na kitu, ila mwana kondoo mmoja, mdogo, ambaye
amemnunua na kumlea; naye akakua pamoja naye, na pamoja na wanawe; hula sehemu
ya posho lake, na kukinywea kikombe chake, na kulala kifuani mwake, akawa kwake
kama binti. Hata msafiri mmoja akamfikilia yule tajiri, naye akaacha kutwaa
mmoja wa kondoo zake mwenyewe au mmoja wa ng'ombe zake mwenyewe, ili
kumwandalia yule msafiri aliyemfikilia, bali alimnyang'anya yule maskini
mwana-kondoo wake, akamwandalia yule mtu aliyemfikilia. Ndipo hasira ya Daudi
ikawaka sana juu ya mtu yule; akamwambia Nathani, Aishivyo Bwana, mtu huyo
aliyetenda jambo hili, HAKIKA YAKE ASTAHILI KUFA; NAYE ATAMRUDISHIA YULE
MWANA-KONDOO MARA NNE, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na
huruma.”
Filemoni 1:10-19 “Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika
vifungo vyangu, yaani, Onesimo; ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa
sana, wewe na mimi pia; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu
hasa; ambaye mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo
vya Injili. Lakini sikutaka kutenda neno lo lote isipokuwa kwa shauri lako, ili
kwamba wema wako usiwe kama kwa lazima, bali kwa hiari. Maana, labda ndiyo
sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele; tokea sasa, si kama
mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe
zaidi sana, katika mwili na katika Bwana. Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika
nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe. NA KAMA AMEKUDHULUMU, AU UNAMWIA KITU,
UKIANDIKE HICHO JUU YANGU. MIMI PAULO NIMEANDIKA KWA MKONO WANGU MWENYEWE, MIMI
NITALIPA. Sikuambii kwamba nakuwia hata nafsi yako.”
Kwa hiyo tunajifunza hapa kwamba watu
waliompokea Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yao aidha kabla au hata baada
kama umedhulumu kitu chochote cha mtu basi baada ya toba unapaswa kukirudisha
kitu hicho, au kukilipa au vitu hivyo kwa kufanya hivyo unaonyesha kuzaa
matunda ya toba, rejesha vitu vyovote ambavyo ulidhulumu, kabidhi bunduki
ulizokuwa ukizitumia kwa ujambazi polisi,vitabu ulivyoiba shuleni au Maktaba au
ukiharibu kitu cha mtu, au kupoteza mali ya mtu ilipie kwa kufanya hivyo
unaonyesha matunda ya toba na huko ndio kunaitwa kufanya malipizo au malipizi.
Mathayo 3:7-8 “Hata alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo
wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya
ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi
zaeni matunda yapasayo toba;”
Ni katika hali kama hiyo kama umechukua
na kukaa na mke wa mtu au unaishi na mume wa mtu ambaye aliolewa kihalali
katika ndoa yake au kuoa kwa halali katika ndoa yake na kisha akaachana na
mumewe au mkewe na ukawa unaishi naye wewe na mume huyo au mke huyo bado yu hai
basi mwanamke huyo au mwanaume huyo umemchukua kwa dhuluma na kwa sababu hiyo
unapaswa kufanya malipizo au marejesho ya ndoa, rudisha mwanamke huyo kwa
mumewe, au rudisha mwanaume huyo kwa mkewe mwachie aende, toba ya kweli
inahusisha kuacha dhuluma, na Mungu hafurahii udhalimu achia mke au mume wa mtu
haraka! Hali kadhalika kwa fedha, mali, ardhi na vitu ulivyodhulumu virejeshwe
haraka
Mwanzo 20:3-7 “Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku,
akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, MAANA NI
MKEWE MTU. Basi Abimeleki alikuwa hakumkaribia, akasema, Ee BWANA, Je! Utaua
hata taifa lenye haki? Je! Hakuniambia mwenyewe, Huyu ni ndugu yangu? Na
mwanamke mwenyewe naye alisema, Huyu ni ndugu yangu. Kwa ukamilifu wa moyo
wangu, na kwa kuwa safi mikono yangu, nimefanya hivi. Mungu akamwambia katika
ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo
nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse. BASI SASA
UMRUDISHE MWANAMKE KWA MTU HUYO, maana yeye ni nabii, naye atakuombea, upate
kuishi. BALI USIPOMRUDISHA, FAHAMU YA KWAMBA KWA HAKIKA UTAKUFA WEWE NA WATU
WOTE ULIO NAO.”
Kwa hiyo neno la Mungu katika kanuni
zake linatuelekeza kufanya malipizo ya kitu chochote ambacho tunakaa nacho
pasipo haki, Lengo kuu la kufanya malipizo ni kutafuta kwa bidi kuwa na amani
na watu wote, kutenda haki, na kuonyesha badiliko la kweli lililofanywa na
Mungu ndani ya mioyo yetu, kwa hiyo ni vema kurudisha chochote ulichoiba,
ulichodhulumu, lipa madeni ya kila unachodaiwa, fanya marekebisho makubwa ya
kitabia, malipizo ni sehemu ya toba na sehemu muhimu ya wokovu wetu, tunafanya
hayo ili tusilaumiwe katika mioyo yetu na rehema za Mungu ziwe juu yetu na
tuweze kusamehewa, na kusamehe, lakini
kubwa zaidi tusiwe kwazo la namna yoyote wala watu wa kulaumiwa!
“2Wakorintho 6:3-4 “Tusiwe kwazo la namna yo yote katika jambo lo lote, ili
utumishi wetu usilaumiwe; bali katika kila neno tujipatie sifa njema, kama
watumishi wa Mungu; katika saburi nyingi, katika dhiki, katika misiba, katika
shida;”
Kwa nini Malipizo ya Ndoa?
Unaweza kujiuliza ni kwa nini Malipizo
ya ndoa?, Ni muhimu kufahamu kwa kina na mapana na marefu ni kwanini Maandiko
yazungumzia swala zima la Malipizo na pia kwa nini tuzungumzie malipizo ya
ndoa? Kwaajili ya kujibu swala hilo ni lazima kwanza kupata ufafanuzi wa jinsi
na namna Mungu ambaye ndiye mwanzilishi wa ndoa anavyoichukulia ndoa.
Ndoa ni taasisi iliyoasisiwa na Mungu katika
bustani ya Edeni ambapo Mungu alimuumba mtu mke na mtu mume na kuwabariki kuwa wakazae
na wakaongezeke, Kwa sababu hiyo ndoa ni utaratibu uliowekwa na Mungu kwaajili
ya upatikanaji wa familia, taifa na jamii, ndoa imekusudiwa kuwa taasisi ya
kudumu mpaka kifo na ndoa ni ya jinsia mbili tofauti ya kike na ya kiume na
imethibitishwa na Yesu Kristo. Miaka ya zamani hakukuwa na vyeti vya ndoa au
ndoa zilikuwa hazisajiliwi, lakini kijamii zilikuweko ndoa za kimila na zote
Mungu aliziheshimu, kwa sababu hiyo Mungu katika mtazamo wake huziona ndoa zote
kuwa ni halali endapo zimefuata utaratibu wowote uwe wa kimila, kikabila,
kidini, kiislamu, kikristo, kibudha, kihindu, kienyeji, kiserikali na
kadhalika, jambo kubwa la msingi la kujiuliza ni kama unataka kuoa au kuolewa
je yule unayemuoa au anayekuoa hajawahi kuwa na ndoa nyingine? Jiulize alioa
kwanza? Aliolewa kwanza? Je mumewe au mkewe yu hai? Kwa sababu wale wanaooana
wanaingia kwenye kifungo cha maisha na kuwako kwa cheti hakuifanyi ndoa hiyo
kuwa halali kama mambo ya msingi ya kujua kama mwanaume huyo au mwanamke huyo
hana kifungo kingine cha ndoa, au kama alikuwa na mtu mwanzoni.
Mathayo 19:4-10 “Akajibu,
akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na
mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana
na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena,
bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.
Wakamwambia, Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha?
Akawaambia, Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha
wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi. Nami nawaambia ninyi, Kila mtu
atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine,
azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini. Wanafunzi wake wakamwambia, Mambo ya
mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa.”
1Wakorintho 7:10-11 “Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si
mimi, ila Bwana; mke asiachane na mumewe; lakini, ikiwa ameachana naye, na akae
asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe.”
Ndoa ilikusudiwa na Mungu iwe taasisi
ya kudumu na uwezekano wa kuwa huru unaweza kutokea ikiwa tu kifo kimejitokeza
na sio vinginevyo, kwa hiyo mwanaume au mwanamke atakuwa huru kuoa au kuolewa
na mwingine endapo mwenzi wake atafariki dunia, kwa hiyo ndoa iwapo duniani ni
ya kudumu na Mungu hatambui kuvunjika kwa ndoa duniani
1Wakorintho 7:39 “Mwanamke hufungwa maadamu mumewe yu hai, lakini ikiwa
mumewe amefariki, yu huru kuolewa na mtu ye yote amtakaye; katika Bwana tu.”
Warumi 7:2-3 “Kwa maana mwanamke aliye na mume amefungwa na sheria kwa
yule mume wakati anapokuwa yu hai; bali akifa yule mume, amefunguliwa ile
sheria ya mume. Basi wakati awapo hai mumewe, kama akiwa na mume mwingine
huitwa mzinzi. Ila mumewe akifa, amekuwa huru, hafungwi na sheria hiyo, hata
yeye si mzinzi, ajapoolewa na mume mwingine.”
Unaweza kuona kama mwanamke aliolewa na
mumewe akiwa hai, na mwanamke huyo akaolewa na mwanaume mwingine mwanamke huyo
huitwa mzinzi, kwa hiyo Mungu katika mpango wake anatambua kuwa kifo peke yake
ndicho kinachoweza kumuweka huru mtu mbali na ndoa yake kwa hiyo uhakikisho wa
kuwa mtu huyo yuko huru ni lazima ufanyike kabla watu hawajaingia katika agano
la ndoa, na ili mtu asiishi na mke wa mtu au mume wa mtu iko haja ya kupata
kibali cha wazazi hasa wa mwanamke hata kama ni ndoa ya kimila wazazi wa
mwanamke wakithibitisha kuwa mwanamke huyu yuko huru kuolewa anaweza kuolewa.
Mwanzo 24:54-57 “Wakala wakanywa, yeye na watu waliokuwa pamoja naye, nao
wakakaa usiku. Wakaondoka asubuhi, naye akasema, Nipeni ruhusa niende kwa bwana
wangu. Ndugu yake na mama yake wakasema, Msichana na akae kwetu kama siku kumi,
zisipungue, baadaye aende. Naye akawaambia, Msinikawilishe, mradi BWANA
amefanikisha njia yangu; nipeni ruhusa niende kwa bwana wangu. Wakasema, Na
tumwite huyo msichana, tumwulize mwenyewe. Wakamwita Rebeka wakamwuliza, Je!
Utakwenda na mtu huyu? Akasema, Nitakwenda. Ndipo wakampeleka Rebeka ndugu yao,
na yaya wake, na mtumishi wa Ibrahimu, na watu wake.”
Katika mtazamo wa Mungu ndoa
ilikusudiwa na Mungu iwe ya milele, kwa hiyo Mungu hakubaliani na swala la
talaka, swala la talaka linaweza kufanywa kimahakama na hakimu au na kadhi,
lakini swala la kuachana halina uhusiano na viongozi wa kidini na kiimani, kwa
sababu maandiko yanakataza kuachana, Mungu anachukia kuachana, Kimsingi Mungu
hamtegemei mtu aliyemuamini yeye kuwa na ndoa itakayovunjika, wala ndoa ya
kikristo haijawahi kukusudiwa kuwa ya watu wengi, kuachana na kutalikiana
kunaonyesha uchanga wa kiroho, upofu wa kiimani, ukosefu wa ukomavu, hitaji la
kimsaada, kushindwa kumtii Mungu na kuchukuliana na wanadamu wengine wenye
udhaifu, au kushindwa kuvumilia, au kukosekana kwa upendo, kuachana ni hiyana,
kuachana ni kushindwa kusamehe, kuachana ni kushindwa kupatana ni kushindwa
kuwa na amani na watu wote, ni uwezo mdogo wa kutatua migogoro, ni changamoto
ya kiadilifu.
Mwanzo 2:22-24 “na ule ubavu alioutwaa katika Adamu BWANA Mungu akaufanya
mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa
yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa
katika mwanamume. Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye
ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.”
Mathayo 19:4-10 “Akajibu,
akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na
mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana
na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena,
bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.
Wakamwambia, Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha?
Akawaambia, Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha
wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi. Nami nawaambia ninyi, Kila mtu
atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine,
azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini. Wanafunzi wake wakamwambia, Mambo ya
mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa.”
Malaki 2:13-16 “Tena mnatenda haya nayo; mnaifunikiza madhabahu ya Bwana
kwa machozi, kwa kulia na kwa kuugua, hata asiiangalie tena hiyo dhabihu, wala
kuitakabali mikononi mwenu na kuiridhia. Lakini ninyi mwasema, Ni kwa sababu
gani? Ni kwa sababu Bwana amekuwa shahidi kati ya wewe na mke wa ujana wako,
uliyemtenda mambo ya hiana, angawa yeye ni mwenzako, na mke wa agano lako.
Hakuna mtu mmoja aliyetenda hivi, ambaye alikuwa na ufahamu kidogo. Au je! Kuna
mtu mmoja atafutaye mzao mwenye kumcha Mungu? Kwa hiyo jihadharini roho zenu;
mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana. Maana mimi
nakuchukia kuachana, asema Bwana, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake
kwa udhalimu namchukia, asema Bwana wa majeshi; basi jihadharini roho zenu,
msije mkatenda kwa hiana.”
Neno la Mungu linatufundisha ya kuwa
kinachoweza kuvunjwa ni uchumba tu, uchumba unaweza kuvunjwa na kumuacha kila
mmoja huru kwa sababu tu ya uasherati, yaani mfano kama umeposa mtu mke au
umemchumbia na kabla ya ndoa ikabainika kuwa mke huyo sio muaminifu kwa maswala
ya ngono mke huyo (Mchumba) unaweza kumuacha, Biblia ya Kiebrania inatumia neno
mke kuanzia katika hatua ya awali ya uchumba, kwa mfano Yusufu na Mariamu
waliokuwa wamechumbiana, Yusufu alipoona mkewe au mchumba wake ana mimba yeye
aliamua kumuacha kwa siri kwa hiyvo maandiko hayatumii neno mchumba kwa sababu
neno mchumba katika kiebrania haliko bali yanatumia neno mke kwa hiyo kama mke
au mchumba au mwanamwali “arusa” akionekana
amefanya uasherati basi uchumba au uhusiano huo ungevunjika, lakini swala la
kuachana haliwezi kufanyika baada ya kuoana ambako kimsingi ni agano.
Mathayo 1:18-20 “Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama
yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba
kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa
haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri
hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana
wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho
Mtakatifu.”
Kumbukumbu 22:22-25 “Akifumaniwa mtu mume amelala na mwanamke aliyeolewa na
mume, na wafe wote wawili, mtu mume aliyelala na mwanamke, na yule mwanamke
naye; ndivyo utakavyoondoa uovu katika Israeli. Pakiwa na kijana aliye
mwanamwali ameposwa na mume, na mwanamume akimkuta mjini, akalala naye; watoeni
nje katika lango la mji ule, mkawapige kwa mawe hata wafe; yule kijana, kwa
kuwa hakupiga ukelele, naye yu ndani ya mji; na yule mume, kwa kuwa amemtweza
mke wa mwenzake; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako. Lakini yule mtu mume
kama akimkuta kondeni kijana aliyeposwa, naye mume akamtenza nguvu, akalala
naye; yule mtu mume aliyelala naye na afe pekee;”
Kwa kuwa ni mpango wa Mungu ndoa
kutokuvunjika ni muhimu kufahamu kuwa hata mtu anapookoka mmoja na mwingine
ikawa bado hiyo sio sababu ya muhimu kuachana Mungu ametuita katika Amani,
wengi wa wale wanaoachwa kwa sababu ya wokovu wanaachwa kwa sababu ya kukosa
hekima, unakaa sana kanisani na kupuuzia usimamizi wa nyumba yako, unakosa
kiasi, unaonyesha heshima kubwa kwa mchungaji wako kuliko mume wako na ujinga
ujinga mwingine, lakini hata nyumbani unaangalia sana program za tv za wahubiri
fulani bila kuweka uwiano wa kuwaachia na wengine waangalie mambo yao, aina
hizi za wokovu wa kipumbavu wa kutokutumia akili au kukosa hekima kumesababisha
migogoro mikubwa baada ya watu kuokoka, viongozi wa kiroho weka ratiba, tunza
muda waachie watu waende majumbani kwao kwa waume zao na watoto wao, ukichagua
viongozi basi zingatia sana mahusiano yake nyumbani kama mumewe hataki mwachie
huru mtu wa watu! Ili wewe usiwe sababu ya migogoro hiyo!
Maandiko yamekataza talaka katika agano
jipya, Mungu anachukia kuachana na kwa sababu hizo endapo watu wataachana neno
la Mungu linawataka wakae hivyo hivyo au wapatane warudiane lakini wasiachane,
hii maana yake kwa kuwepo kwetu duniani, inaweza kutokea watu wakahitilafiana
kiasi cha kutengana na kujitafuta kwa muda na kujitafakari na baada ya mioyo
kupoa basi watu hao na wapatane na warudiane.
1Wakorintho 7:10-11 “Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si
mimi, ila Bwana; mke asiachane na mumewe; lakini, ikiwa ameachana naye, na akae
asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe.”
1Wakorintho 7:12-16 “Lakini watu wengine nawaambia mimi, wala si Bwana, ya
kwamba iwapo ndugu mmoja ana mke asiyeamini, na mke huyo anakubali kukaa naye
asimwache. Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali
kukaa naye, asimwache mumewe. Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika
mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe; kama isingekuwa hivyo,
watoto wenu wangekuwa si safi; bali sasa ni watakatifu. Lakini yule asiyeamini
akiondoka, na aondoke. Hapo huyo ndugu mume au ndugu mke hafungiki. LAKINI
MUNGU AMETUITA KATIKA AMANI. Kwa maana wajuaje, wewe mwanamke, kama utamwokoa
mumeo? Au wajuaje, wewe mwanamume, kama utamwokoa mkeo?”
Kwa msingi huo sasa Malipizo ya ndoa
yanatupa nafasi ya kujitafakari Kama tunaishi na mume wa mtu au mke wa mtu?
Wokovu wetu unaweza kulaumiwa na uadilifu wetu kutiliwa mashaka endapo umeokoka
lakini mke au mume unayeishi naye sio wa kwako na zaidi ya yote unaishi katika
zinaa na hauwezi kamwe kuurithi ufalme wa Mungu kutokana na kuishi kwako katika
zinaa na mume au mke asiyekuwa halali kwako
1Wakorintho 6:8-10 “Bali kinyume cha hayo ninyi wenyewe mwadhulumu watu na
kunyang'anya mali zao; naam, hata za ndugu zenu. Au hamjui ya kuwa wadhalimu
hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa
Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala
wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi.”
Mungu ametuita katika Amani, maana yake
sio mpango wake aokoe mmoja alafu itokee Muachane kwa sababu ya wokovu, kwa
msingi huo bado Mpango wa Mungu uko vile vile katika swala la kutikuachana kwa
sababu Paulo alitioa maoni yake na sio agizo la Bwana
Faida za kufanya Malipizo
ya Ndoa.
Malipizo ya ndoa yana faida gani? Yanasaidia nini? Malipizo ya ndoa ni sehemu
muhimu ya theolojia ya uadilifu (Moral
theology) tunapoifanyia kazi inaonyesha kujutia kwetu kwa dhati na maamuzi
yetu ya kubadilika kiimani na kimaadili, malipizo ni kama tiba inayofanyika au
tunayoifanya kwa watu ambao tumewajeruhi,
hatuwezi tu kupuuzia na kudai kuwa tunampenda Mungu huku kuna watu
wanaumia na kukumbuka kuwa umemchukulia mumewe au umemchukulia mkewe na uko
naye na unaendelea naye huku unadai umeokoka, kwa hiyo ni kama unaamua
kumuabudu tu Mungu huku kuna mtu una shida naye au ana shida na wewe!,
unawezaje kabisa kujikausha katika wokovu huku unamiliki mume au mke asiyekuwa
wako? Hapo unaendeleza zinaa bila kujali ni baraza gani limepitisha swala lako.
Malipizo ni sehemu muhimu sana ya
mafundisho ya wokovu ambayo makanisa mengi wanaikaushia na kuwaacha watu waende
motoni kwa kutokuwakumbusha watu hao kutenda haki, kutenda kwetu haki ni pamoja
na kuwaomba radhi wale tuliowakosea, kurejesha vitu vyao tulivyodhulumu na
kuwarejeshea wake zao au waume zao ambao tumewachukua kibabe au kwa tamaa zetu
au hata kwa kuhalalisha talaka kimahakama. Unamuona baba yule au mama yule
anajifanya kaokoka lakini anaishi na mke wa mtu au mume wa mtu! Ushuhuda wa
aina hii unaifanya injili kukutana na wakati Mgumu, kila anayeoa ni lazima ajue
wazi na mapema kuwa ndoa sio swala la kuchukulia mzaha!
Unapoendelea kukaa na mume wa mtu au
mke wa mtu unakiuka agizo la Mungu na katazo lake kwani ndoa huunganishwa na Yeye
mwenyewe na wewe unafanya ukaidi na kusimama mahali ambapo utahukumiwa, andiko
limesema alichokiunganisha Mungu mwanadamu asikitenganishe wewe ndiye huyo
mwanadamu sasa uliyetenganisha ndoa ya watu, tarajia hukumu ya kutisha kutoka
kwa Mungu aliye hai asiyedhihakiwa! Endapo unaishi na mke wa mtu au unaishi na
mume umetenganisha kile Mungu alichokiunganisha.
Marko 10:6-9. “Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume
na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe;
na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili
mmoja. Basi ALICHOKIUNGANISHA MUNGU, MWANADAMU ASIKITENGANISHE.”
Malipizo ni tunda la toba ya kweli,
Zakayo alipopokea wokovu moja kwa moja aliyajua mapenzi ya Mungu na kuamua
kurejesha vile alivyodhulumu na Yesu alithibitisha kuwa huu ndio wokovu wa
kweli, unaokokaje huku umeacha mkeo? Umeacha mumeo? Unakaa na mali ya watu au
unaona sawa sawa hapo ni mene mene tekeli na peresi
Luka 19:8-10. “Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu
ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila
namrudishia mara nne. Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa
sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu.Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta
na kuokoa kile kilichopotea.”
Malipizo ni maonyo kwa watu wasiokaa
kwa utaratibu, Mungu wetu ni Mungu wa utaratibu, kama kanisa litatoa mpenyo na
njia rahisi ya watu kuachana na kuoa tena kama watakavyo, au kuachwa na kuolewa
tena kama watakavyo tutatoa mpenyo kwa watu kuishi bila utaratibu, na
kujifanyia kama watakavyo na hata kufikia hatua ya kushika ngazi za juu za
kimaongozi katika kanisa huku wakiwa na historia mbaya ya ndoa zao, ni lazima
kanisa lichukue hatua barabara na kusimama kama Yesu mwenyewe alivyoweka
msimamo mkali katika swala zima la ndoa. Ni lazima watu waishi kwa utaratibu.
1Wathesalonike 5:14-15 “Ndugu, twawasihi, waonyeni wale wasiokaa kwa utaratibu;
watieni moyo walio dhaifu; watieni nguvu wanyonge; vumilieni na watu wote.
Angalieni mtu awaye yote asimlipe mwenziwe mabaya kwa mabaya; bali siku zote
lifuateni lililo jema, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote.”
Malipizo ni ishara ya kuwa sasa unataka
Amani na unaitafuta Amani kwa bidii, neno la Mungu limetuagiza kutafuta Amani
kwa bidii, kutafuta Amani sio swala jepesi na wala haliji kwa maombi linakuja
kwa sisi kuachukua hatua madhubuti na wakati mwingine kuingia gharama kubwa
sana kuitafuta Amani.
Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo
utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”
Warumi 12:17-18. “Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni
pa watu wote. Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote.”
Malipizo ni utii wa amri ya pili
iliyokuu kivitendo isemayo Mpende jirani yako kama nafsi yako, na ile sheria ya
dhahabu inayosema watendeeni wengine yale mnayotaka nanyi mtendewe, ama siwatendee
wengine mambo ambayo hungependa nawe utendewe!
Mathayo 22:37-39 “Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote,
na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena
ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama
nafsi yako.”
Luka 6:31 “Na kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni
vivyo hivyo.”
Malipizo yanatukumbusha gharama ya
dhambi na kutuhakikishia kuwa hatuna mpango tena wa kuishi katika dhambi na
hatia na hatuko tayari tena kuyarudia matapishi, kwamba ulifanya upumbavu na
hutaki kufanya upumbavu tena, Malipizo ni kujitia nidhamu ni kujiadhibu na
kujiwekea msingi kuwa haitakuja urudie tema makosa kama yale
Mithali 26:11 “Kama vile mbwa arudiavyo matapiko yake; Kadhalika
mpumbavu afanya upumbavu tena.”
Malipizo ni kufanya masahihisho ya makosa
tuliyoyafanya kwa Mungu na kwa wahusika tuliowakosea zamani ili tuweze kuwa na
dhamiri njema isiyo na hatia mbele za Mungu na wanadamu na watu wote
wanaotuzunguka ili tusilaumiwe kwa habari ya karama hii tunayoitumikia yaani
wokovu, kama sisi ni watumishi wa Mungu au watu tuliookolewa na tunaishi na mke
au mume asiyekuwa wakwako, jamii inapata kigugumizi na inashindwa kukuelewa
kuwa wewe ni mtu wa namna gani na uhusiano wako na Mungu ukoje ikiwa utakuwa na
madai ya kumcha Mungu huku una mume au mke wa mtu!
Matendo 24:16 “Nami ninajizoeza katika neno hili niwe na dhamiri isiyo
na hatia mbele za Mungu na mbele ya watu siku zote.”
Matendo 26:20 “bali kwanza niliwahubiri
wale wa Dameski na Yerusalemu, na katika nchi yote ya Uyahudi, na watu wa
Mataifa, kwamba watubu na kumwelekea Mungu, WAKIYATENDA MATENDO YANAYOPATANA NA
KUTUBU KWAO.”
2Wakorintho 8:20-21 “Tukijiepusha na neno hili, mtu asije akatulaumu kwa
habari ya karama hii tunayoitumikia; tukitangulia kufikiri yaliyo mema, si
mbele za Bwana tu, ila na mbele ya wanadamu.
Malipizo hutusaidia kusonga mbele, yanasababisha
ujisamehe mwenyewe na kukupa fursa ya kuwa huru kwa Mungu na kuyafanya maombi yako
yasizuiliwe, Malipizo hudhihirisha upendo wa kweli, na kinyume chake ni
kudhihirisha kuwa hatuna upendo kufanya huduma, kuhubiri, kuomba sana kuwa na vyeo
vikubwa katika madhehebu yetu kote kunaweza kuhesabika kuwa hakuna maana Mbele
za Mungu na wanadamu kama kuna watu tumewajeruhi na kuwaumiza na kujikausha
huku tukijifanya tunaendelea mbele na Mungu wetu, Mungu hadhiakiwi iko siku
utavuna kile ulichokipanda, dua zako na maombi yako na kila ulifanyalo ni bure
kama huna upendo, kama hujali kuwa kuna watu wanaugua na kupata shida kwaajili
yako, manabii wengi, na mitume wengi na waimbaji wengi wa injili wengi wameacha
wake zao wa awali na wameoa wengine, huku wakiendelea kutumiwa na Mungu na
kusifiwa huku na kule lakini wake zao wanalia na watoto wao wanalia, wengine
wana watoto hawawajali wala hawawatunzi na ili hali wao wana mafanikio makubwa
sana somo hili linakuja kwako kukutaka uwe mkristo wa kweli na usimame katika
kweli vinginevyo njia ya jehamnamu ni nyeupe sana haijalishi unafanya nini.
1Wakorintho 13:1-8 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina
upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na
kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza
kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote
kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo,
hainifaidii kitu. Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo
hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni
uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;
huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo
haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha,
zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.”
Hitimisho:
Baada ya kuwa tumefahamu hayo hatuna
budi kutambua kua mtu anayekua kwenye uzinzi hawezi kurithi ufalme wa Mungu.
Kwa msingi huo kama unajitambua kuwa una malipizi ya ndoa basi ni muhimu kwako kuyafanyia
kazi maneno haya, hata hivyo hekima ya kiungu inahitajika sana katika kuchukua
maamuzi haya, lakini usipochukua unahesabika miongoni mwa wadhalimu na
hautaurithi ufalme wa mbinguni.
1Wakoritho 6:9-10 “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu?
Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu,
wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala
walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi.”
kwa msingi huo itatupasa kuhesabu gharama
kabla na kujenga mnara na kujipima na kujiangalia ili tuchague kuingia mbinguni
au la, Zaidi ya yote omba sana Amani ya Mungu itamalaki na kukuwezesha kutii
maagizo haya magumu ambayo ni mifupa katika mafundisho ya wokovu, ni
mafundi9sho magumu kwa sababu yanagusa hisia na mwingiliano wa kisaokolojia
lakini hatuna budi kumtii Mungu kuliko nafsi zetu.
Yohana 14:27 “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi
sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.”
Watumishi wa Mungu tuisimamie kweli,
Mungu hapokeii uso wa mwanadamu, tuache kujifanya kuwa sisi ni miungu na kuwa
tunaweza kutangua neno la Mungu au kulibadilisha kwa kuwaachia watu waishi
watakavyo, tunaweza kupoteza watu wengi na kuwacha waende jehanamu au kufa
wakiwa wameacha utata duniani ikiwa haijulikani kama wako mbinguni au motoni,
lililotukuka kwa wanadamu ni chukizo kwa Mungu hebu tuisimamie kweli na
kuwaonya watu vinginevyo damu zao na roho zao zitadaiwa mikononi mwetu,
tujifunze kujua taarifa za watu kwa usahihi iwe ni washirika au wachungaji ili
tusifanye makosa ya kupoteza roho za watu kwa kuwapaka mafuta ili hali
tungewaeleza ukweli wangeweza kupona na kwenda Mbinguni, awezae kulipokea neno
hili na alipokee lakini Mungu atatudai damu ya watu ambao amewaleta karibu yetu
na tukashindwa kuwaambia ukweli kwa kuogopa kuwakwaza. Mimi nimenawa!
Ezekiel 33:7-9. “Basi wewe, mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi kwa nyumba
ya Israeli; basi ulisikie neno hili kinywani mwangu, ukawape maonyo yangu.
Nimwambiapo mtu mbaya, Ewe mtu mbaya, hakika utakufa, nawe husemi neno la
kumwonya mtu huyo, aiache njia yake, mtu mbaya huyo atakufa katika uovu wake,
lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. Walakini ukimwonya mtu mbaya kwa sababu
ya njia yake, kusudi aiache; wala yeye asiiache; atakufa huyo katika uovu wake,
lakini wewe umejiokoa roho yako.”
Na. Rev Innocent Samuel
Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye
hekima!