Jumapili, 8 Februari 2026

Kanuni za kuwekea/kuwekewa Mikono:


Matendo 13:1-3Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.”




Utangulizi.

Leo nataka kuzungumzia mojawapo ya ibada ya muhimu na ya msingi na ya zamani sana, katika utamaduni wa kanisa na kimaandiko na hii ni ibada ya kuwekea mikono au kuwekewa mikono, Ibada hii ni ya muhimu kwa sababu ni ya kimaandiko na inaendelea kutenda kazi hata katika siku zetu, ingawa kuna umuhimu wa kujikumbusha ili tuweze kuwa na uelewa wa kina na mapana na marefu kuhusu kuwekea au kuwekewa mikono, kuwekea au kuwekewa mikono kuna uwezo wa kuruhusu neema ya Mungu juu ya maisha ya huduma na utumishi wa mtu, aidha pia mikono inahusika katika kupitisha Baraka, neema na uponyaji wa mwili nafsi na roho kwa hiyo uko umuhimu wa Kanisa kuwa na uelewa.

Kumbukumbu 34:9 “Na Yoshua, mwana wa Nuni, alikuwa amejaa roho ya hekima; maana Musa alikuwa amemwekea mikono yake juu yake; wana wa Israeli wakamsikiliza, wakafanya kama Bwana alivyomwamuru Musa.”

2Timotheo 1:6-7 “Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.”

Kwa msingi huu leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu kuhusu swala zima la kuwekea au kuwekewa mikono, ambalo kimsingi ni lazima liambatane na maombi kama ilivyo kwenye swala la kufunga, au kupaka mafuta vilevile kuweka mikono huendana na kuomba au kusema maneno yanayoambatana na kusudi la kuwekea mikono huko, ili kulitungua kusudi hilo kutoka katika ulimwengu wa roho na mkao wa Moyo kwa kusudi la kutimiza mapenzi ya Mungu, tutajifunza somo hili Kanuni za kuwekea au kuweka Mikono kwa kuzingatia vipengele vifuatavyo:-


·         Asili ya kuwekea au kuwekewa mikono.

·         Makusudi ya ibada ya kuwekea au kuwekewa mikono

·         Kanuni za kuwekea au kuwekewa mikono


Asili ya kuwekea au kuwekewa mikono.

Kuwekea mikono au kuwekewa mikono “laying on of hands” ni tendo la ibada la kimwili ambapo mtu au watu au kikundi cha watu huweka mikono inayoambatana na maombi juu ya wengine kama ishara ya kiroho yenye lengo la kubariki, kuhamisha mamlaka, kuweka wakfu viongozi, kuwatenga watu kwaajili ya huduma, kufanya maombezi ya uponyaji, kuchochea karama, kurithisha Baraka na kutambulisha na ubatizo wa Roho Mtakatifu, Tendo hili ingawa linafanyika katika mwili kiibada linaunganisha mamlaka ya Mungu ndani ya Mwanadamu anayepokea kusudi hilo. Ni ishara inayoonekana ya neema ya Mungu isiyoonekana na uweza wa Roho Mtakatifu.

Tendo la kuwekea mikono kwa asili linaonekana katika maandiko ya Kiebrania likitajwa kwa kiebrania kwa neno “Semikhah” kwa kiingereza “succession” kwa kiwahili ni kurithisha kwa mfululizo, mfano kutoka katika uongozi wa mtu mmoja kwenda katika uongozi wa mtu mwingine kwa kurithishana kwa Amani au kwa lengo la kuendeleza au kusaidia au kupitisha mfano Musa alipozidiwa na majukumu ya kichungaji katika kanisa lililokuwako Jangwani alichagua wazee sabini “70” kwa maelekezo ya Mungu na kuwawekea mikono na kwa tendo hilo sehemu ya utendaji wa Musa  iliwapata wazee wale sabini ili waweze kumsaidia majukumu yake.

Hesabu 11:24-29 “Musa akatoka, akawaambia watu maneno ya Bwana; akawakutanisha watu sabini miongoni mwa wazee wa watu, akawaweka kuizunguka Hema. Ndipo Bwana akashuka ndani ya wingu, akanena naye, akatwaa sehemu ya roho iliyokuwa juu ya Musa, akaitia juu ya wale wazee sabini; ikawa, roho hiyo ilipowashukia, wakatabiri, lakini hawakufanya hivyo tena. Lakini watu wawili walisalia kambini, jina la mmoja aliitwa Eldadi, na jina la wa pili aliitwa Medadi; na roho ile ikawashukia; nao walikuwa miongoni mwao walioandikwa, lakini walikuwa hawakutoka kwenda hemani; nao wakatabiri kambini. Mtu mmoja kijana akapiga mbio, akaenda akamwambia Musa, akasema, Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini. Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee bwana wangu Musa, uwakataze. Musa akamwambia, Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa Bwana wangekuwa manabii na kama Bwana angewatia roho yake.”

Hesabu 27:16-20 “Bwana, Mungu wa roho za wenye mwili wote, na aweke mtu juu ya mkutano, atakayetoka mbele yao, na kuingia mbele yao; atakayewaongoza watokapo, na kuwaleta ndani; ili mkutano wa Bwana wasiwe kama kondoo wasio na mchungaji. Bwana akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu mwenye roho ndani yake, ukamwekee mkono wako; kisha ukamweke mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote; ukampe mausia mbele ya macho yao. Nawe utaweka juu yake sehemu ya heshima yako, ili mkutano wote wa wana wa Israeli wapate kutii.”

Asili nyingine ya kuwekea mikono ilifanywa na makuhani kwa kuweka mikono yao juu ya mnyama kwaajili ya sadaka ya kuteteketezwa ya dhambi, Kuhani angeweka mikono yake juu ya mnyama kama ishara ya kusafirisha dhambi ya hatia kutoka kwa mwanadamu anayeombewa au kufanyiwa upatanishi kuelekea kwa mnyama huyo kisha angechinjwa na kuteketezwa kama ishara ya msamaha wa dhambi kutoka kwa muathirika, aidha tukio kama hili lilifanywa na kuhani mkuu kwaajili ya dhambi za taifa kwa mwanambuzi wa hazazeli mbuzi wa kafara ambaye angechukua uovu wa watu na kupotelea nao jangwani.

Walawi 1:2-5 “Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtu wa kwenu atakapomtolea BWANA matoleo, mtatoa matoleo yenu katika wanyama wa mifugo, katika ng'ombe na katika kondoo. Matoleo yake kwamba ni sadaka ya kuteketezwa ya ng'ombe, atatoa ng'ombe mume mkamilifu; ataleta mlangoni pa hema ya kukutania, ili akubaliwe mbele ya BWANA. Kisha ataweka mkono wake juu ya kichwa cha hiyo sadaka ya kuteketezwa; nayo itakubaliwa kwa ajili yake, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake. Naye atamchinja huyo ng'ombe mbele ya BWANA; kisha wana wa Haruni, hao makuhani, wataileta karibu hiyo damu, na kuinyunyiza damu yake kando-kando katika madhabahu iliyo hapo mlangoni pa hema ya kukutania.”

Walawi 16:21-22 “Na Haruni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha yule mbuzi aliye hai, na kuungama juu yake uovu wote wa wana wa Israeli, na makosa yao, naam, dhambi zao zote; naye ataziweka juu ya kichwa chake yule mbuzi, kisha atampeleka aende jangwani kwa mkono wa mtu aliye tayari.Na yule mbuzi atachukua juu yake uovu wao wote, mpaka nchi isiyo watu; naye atamwacha mbuzi jangwani.”

Asili nyingine ya tendo la kuwekea mikono ni kwaajili ya urithi au kuhamisha Baraka, ambapo tunaona Yakobo akiwarithi watoto wa Yusufu na kuwa wa kwake, huku akiweka mkono wa kuume juu ya mdogo na mkono wa kushoto juu ya mkubwa ili kumuinua Efraimu na kumshusha Manase katika mbaraka wake.

Mwanzo 48:13-16 “Yusufu akawaweka wote wawili, Efraimu katika mkono wake wa kuume, kuelekea mkono wa kushoto wa Israeli; na Manase katika mkono wake wa kushoto, kuelekea mkono wa kuume wa Israeli, akawasogeza karibu naye. Israeli akanyosha mkono wake wa kuume akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, aliyekuwa mdogo, na mkono wake wa kushoto akauweka juu ya kichwa cha Manase, huku akijua atiavyo mikono; maana Manase ndiye aliyezaliwa kwanza. Akambariki Yusufu, akasema, Mungu ambaye baba zangu, Ibrahimu na Isaka, walienenda mbele zake, yeye Mungu aliyenilisha, maisha yangu yote, hata siku hii ya leo, naye Malaika aliyeniokoa na maovu yote, na awabariki vijana hawa; jina langu na litajwe juu yao, na jina la baba zangu, Ibrahimu na Isaka; na wawe wingi wa watu kati ya nchi.”

Ibada ya kuwekea mikono imekuwa na matumizi makubwa sana katika nyakati za agano jipya katika mazingira mbalimbali, Mwandishi wa kitabu cha Waebrania anayataja mafundisho ya msingi katika Kristo na mojawapo ya mafundisho haya ni pamoja na ibada za kuwekea mikono

Waebrania 6:1-3 “Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa Mungu, na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele. Na hayo tutafanya Mungu akitujalia.”

Makusudi ya ibada ya kuwekea au kuwekewa mikono.

Kwa ujumla unapolichunguza neno la Mungu kuhusu swala zima la kuwekea mikono utaweza kugundua kuwa ibada ya kuweka mikono au kuwekea mikono inafanyika kwa makusudi ya aina mbalimbali kama ifuatavyo:-

1.       Kwa kusudi la kubariki – Kimsingi moja ya sababu ya kuwekea mikono au kuwekewa mikono ni kwaajili ya Baraka za Mungu kwa yule anayewekewa mikono, Baraka za Mungu humfanya mtu awe na kibali na awe na mafanikio katika jambo analolifanya au analowekwa kulifanya kwaajili ya ufalme wa Mungu au kwa makusudi mengine, Mfano tunaona Yakobo akiweka mikono juu ya wajukuu zake ili kuwatakia Baraka za kinabii katika maisha yao, Lakini sio hivyo tu tunamuona bwana Yesu akiweka mikono juu ya watoto kwa kusudi la kuwabariki, aidha katika tamaduni za kikanisa pia watu wamekuwa wakiwawekea mikono wana ndoa wakati wa kuwatakia maisha mema katika ibada ya ndoa hili linaingia katika kundi hili la kuwekea mikono ili kuwabariki.

 

Mwanzo 48:20 “Akawabariki siku ile akasema, Katika ninyi Waisraeli watabariki, wakisema, Mungu na akufanye kama Efraimu na Manase. Akamweka Efraimu mbele ya Manase.”

 

Mathayo 19:13-15 “Ndipo akaletewa watoto wadogo ili aweke mikono yake juu yao na kuwaombea; wanafunzi wake wakawakemea. Lakini Yesu akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao. Akaweka mikono yake juu yao, akatoka huko.”

 

Na kwa mujibu wa maelekezo ya kibiblia kama mtu atafanya ibada ya kubariki anayebariki anapaswa kuwa mkubwa kwa sababu Baraka hutoka kwa mkubwa kwenda kwa mdogo, kwa maana mtu huyo awe kuhani kwa maana ya mtumishi wa Mungu ambaye ni mkubwa kwa mamlaka aliyopewa na Mungu ya kubariki, lakini pia awe mkubwa kiumri, kwa hiyo ile mila ya kuwekewa mkono na mtoto mdogo kwa kuamini kuwa atakubariki ni kinyume na maelekezo ya kibiblia

 

Waebrania 7:1-7 “Kwa maana Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki; ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani; hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele. Basi, angalieni jinsi mtu huyo alivyokuwa mkuu, ambaye Ibrahimu, baba yetu mkuu, alimpa sehemu ya kumi ya nyara. Na katika wana wa Lawi nao, wale waupatao ukuhani, wana amri kutwaa sehemu ya kumi kwa watu wao, yaani, ndugu zao, kwa agizo la sheria, ijapokuwa wametoka katika viuno vya Ibrahimu. Bali yeye, ambaye uzazi wake haukuhesabiwa kuwa umetoka kwa hao, alitwaa sehemu ya kumi kwa Ibrahimu, akambariki yeye aliye na ile ahadi. Wala haikanushiki kabisa kwamba mdogo hubarikiwa na mkubwa.”

 

2.       Kwa kusudi la kurithisha Uongozi – sababu nyingine ya ibada ya kuwekea mikono ni kwaajili ya kurithisha uongozi, “Semikhah” kwa kiingereza “succession hii hufanyika kwa kusudi la kumrithisha kiongozi kutoka kwa uongozi wa zamani kuja kwa uongozi mpya, wakati huu sehemu kama ile ya heshima au Roho yule yule aliyetenda kazi na kiongozi aliyepita hufanya kazi na kiongozi ajaye hata kama ni katika mtindo na mfumo wa aina nyingine na tabia nyingine lakini Roho ni yeye yule, Jambo hili linapofanyika sehemu ya heshima au mamlaka iliyokuweko juu ya kiongozi wa awali huamia kwa uongozi mpya na kumpa neema ya kutumika sawa na kiongozi wa awali au zaidi katika namna nyingine apendavyo Roho yeye yule.

 

Hesabu 27:16-20 “Bwana, Mungu wa roho za wenye mwili wote, na aweke mtu juu ya mkutano, atakayetoka mbele yao, na kuingia mbele yao; atakayewaongoza watokapo, na kuwaleta ndani; ili mkutano wa Bwana wasiwe kama kondoo wasio na mchungaji. Bwana akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu mwenye roho ndani yake, ukamwekee mkono wako; kisha ukamweke mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote; ukampe mausia mbele ya macho yao. Nawe utaweka juu yake sehemu ya heshima yako, ili mkutano wote wa wana wa Israeli wapate kutii.”

 

3.       Kwa kusudi la kuombea uponyaji na kufanya miujiza – Neno la Mungu linaonyesha kuwa ibada ya kuweka mikono pia inaweza kufanywa kwa nia ya kufanya maombezi na kuwaponya watu au kutumiwa na Mungu kwa njia ya miujiza, kwa hiyo utaweza kuona Yesu, na mitume kadhaa akiwemo Petro na Paulo na kadhalika ambao waliweza kuwaombea watu kwa kuwawekea mikono na wakapokea uponyaji, hata Yesu Kristo mwenyewe aliahidi ya kuwa wale wamuaminio watatumiwa kwa ishara mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuweka mikono juu ya wagonjwa nao kupokea afya

 

Marko 6:4-5 “Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake. Wala hakuweza kufanya mwujiza wo wote huko, isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache, akawaponya.”

 

Matendo 9:11-12 “Bwana akamwambia, Simama, enenda zako katika njia iitwayo Nyofu, ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu aitwaye Sauli, wa Tarso; maana, angalia, anaomba; naye amemwona mtu, jina lake Anania, akiingia, na kumwekea mikono juu yake, apate kuona tena.”

 

Matendo 28:7-8 “Karibu na mahali pale palikuwa na mashamba ya mkuu wa kisiwa, jina lake Publio; mtu huyu akatukaribisha kwa moyo wa urafiki, akatufanya wageni wake kwa muda wa siku tatu. Ikawa babaake Publio alikuwa hawezi homa na kuhara damu. Paulo akaingia kwake, akaomba, akaweka mikono yake juu yake, na kumpoza.”

 

Marko 16:17-18 “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”

 

4.       Kwa kusudi la kumpokea Roho Mtakatifu – Uko ushahidi wa kimaandiko unaoshiria kuwa pamoja na kuweko kwa njia nyingi sana za watu kubatizwa kwa Roho Mtakatifu, inaonekana pia kuwa watu huweza kupokea Ubatizo wa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono  mfano

 

Matendo 8:14-19 “Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana; ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu. Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema, Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu.”

 

Matendo 19:1-6 “Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko; akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana. Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.”

 

5.       Kwa kusudi la kuchochewa kwa karama – Wakati mwingine watu wa Mungu huwa na karama za Roho Mtakatifu ndani yao na vipawa mbalimbali lakini wakati mwingine karama zina tabia ya kujificha na hivyo mtu anaweza kuwekewa mikono na karama zikachochewa, tunapoendelea kumtumikia Mungu kama ilivyokuwa kwa Timotheo kwa muda Fulani wakati mwingine kuna uwezekano wa moto kupungua kutokana na changamoto mbalimbali Paulo alimtaka Timotheo ili kumuwekea mikono yake ili karama ziendelee kuwaka na kufanyakazi kwa kiwango cha juu Zaidi, karama pia huweza kuambukizwa ndani ya Mtu kwa kuwekewa mikono.

 

2Timotheo 1:6-7 “Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.”

 

1Timotheo 4:13-14 “Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha. Usiache kuitumia karama ile iliyomo ndani yako, uliyopewa kwa unabii na kwa kuwekewa mikono ya wazee.”

 

6.       Kwa kusudi la kusimika au kuweka wakfu viongozi wa kanisa na wale walioitwa katika wito maalumu – Viongozi wote makanisani wanapokuwa wameteuliwa au kuchaguliwa kwaajili ya kutimiza majukumu yao kadhaa waliyoitiwa na Roho Mtakatifu katika kanisa wanapaswa kuwekewa mikono ili wapokee neema ya kuwawezesha kubeba majukumu yao ya kikanisa au ya kitumishi kwa hiyo nyakati za kanisa la Kwanza kila walipoweka viongozi waliwawekea mikono.

 

Matendo 6:5-6 “Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia; ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao.”

 

Matendo 13:1-3 “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.”

 

7.       Huwezi kupokea roho chafu kwa kuwekewa mikono – Kumekuwepo na hofu kubwa sana kutoka kwa washirika na hata  baadhi ya watumishi wa Mungu mbali mbali wakionya kuwa uko uwezekano wa kupokea roho chafu kutokana na kuwekewa mikono, ni muhimu kufahamu kuwa Mkrito aliyeokoka vizuri na aliye muaminifu hawezi kamwe kupokea roho chafu kwa kuwekewa mikono  na mhudumu asiye mwaminifu, Mkristo aliyeokoka vema na kujazwa Roho Mtakatifu yeye ni Hekalu la Roho Mtakatifu na Roho wa Mungu anakaa ndani yake  

 

1Wakorintho 6:19 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe;”

 

Roho wa Mungu aliye ndani ya waamini au watu waliookoka ni mkuu kuliko yeye aliyeko katika ulimwengu huu kwa hiyo utabarikiwa na kufanikiwa kwa sababu ya tendo la kiungu na ibada inayofanyika ndani yako na sio kwa sababu ya hali ya mtumishi anayekuwekea mikono

 

1Yohana 4:4 “Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.”  

 

Yesu anaonyesha katika maandiko na mafundisho yake kuwa Mwamini hupewa kile anachokiomba na Mungu sio dhalimu kwamba akupe nyoka wakati umeomba samaki, au nge wakati umeomba yai na jiwe wakati umeomba Mkate Mungu huangalia moyo na atakupa sawasawa na uhitaji wa moyo wako na sio kwa sababu ya hali ya muhubiri au kiongozi anayekuwekea mikono

 

Luka 11:9-13 “Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka? Au akimwomba yai, atampa nge? Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?

 

Hana alipata mtoto katika wakati ambao watoto wa Eli yule kuhani walikuwa wameharibika na neno la Bwana lilikuwa adimu lakini kupitia maneno ya Eli na uhitaji wa mwanamke yule moyoni Mungu alijibu maombi nyake sawasawa na uhitaji wake kiyume kabisa na hali ya kuhani nyumbani mwa Bwana kwa hiyo hali ya kuhani sio changamoto ya kumfanya mtu asipokee kitu halisi anachikitamani na kukihitaji kutoka kwa Mungu.                        

 

Kanuni za kuwekea au kuwekewa mikono

Kama utakuwa umefuatilia vema somo hili utagundua kuwa kuweka mikono ni swala la kiroho na la Muhimu na kwa sababu hiyo lina kanuni zake, haliwezi kufanyika hovyo hovyo ama bila kufuata utaratibu na maelekezo ya kibiblia, kuwekea watu mikono ni njia ya kuruhusu neema ya Mungu kutoka kwa Roho Mtakatifu kupitia mikono yetu na kutimiza kusudi lake kwa mtu anayewekewa Mikono kwa hiyo tukio hili kama ilivyo kwa tukio la kupaka mafuta ni lazima lifanyike pamoja na maombi. Lakini pia kwa kuzingatia kanuni, kila anayeweka mikono ni lazima awe anajua anachokifanya na kujiuliza kwa nini anafanya na kusudi la kufanya hivyo, hivyo jambo hili lisifanyike ilimradi tu kwani ni ibada kamili.

Anayeweka mikono ni lazima awe anajua anachokifanya – Mtu anayeweka mikono anatakiwa awe anajua ni kwa nini anafanya hivyo, hili ni swala la kiroho na ni swala la maisha ni swala la kuinua mtu na kushusha mtu kwa hiyo anayeweka mikono anatakiwa kuwa na ujuzi na kile anachikifanya kwanza akiwa na ufahamu wa kawaida lakini pia kama ameongozwa na Mungu au roho ya kinabii kufanya hivyo ni lazima aelewe kusudi  linalomuongoza katika kuwekea mikono, Kwa mfano wakati Yakobo anamuwekea mkono wa kuume Efraimu na mkono wa kushoto Manase wakati Manase ndiye mkubwa na Efraimu ndiye mdogo, Yusufu alikuwa akielewa na kufikiri kuwa babaye anakosea lakini Yakobo alisisitiza kuwa anajua anachokifanya ona kumbe muwekewa mikono anapaswa kujua anachokifanya

Mwanzo 48:13-19 “Yusufu akawaweka wote wawili, Efraimu katika mkono wake wa kuume, kuelekea mkono wa kushoto wa Israeli; na Manase katika mkono wake wa kushoto, kuelekea mkono wa kuume wa Israeli, akawasogeza karibu naye. Israeli akanyosha mkono wake wa kuume akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, aliyekuwa mdogo, na mkono wake wa kushoto akauweka juu ya kichwa cha Manase, HUKU AKIJUA ATIAVYO MIKONO; maana Manase ndiye aliyezaliwa kwanza. Akambariki Yusufu, akasema, Mungu ambaye baba zangu, Ibrahimu na Isaka, walienenda mbele zake, yeye Mungu aliyenilisha, maisha yangu yote, hata siku hii ya leo, naye Malaika aliyeniokoa na maovu yote, na awabariki vijana hawa; jina langu na litajwe juu yao, na jina la baba zangu, Ibrahimu na Isaka; na wawe wingi wa watu kati ya nchi. Yusufu alipoona kwamba babaye anaweka mkono wake wa kuume juu ya kichwa cha Efraimu, ikawa vibaya machoni pake. Akauinua mkono wa babaye auondoe katika kichwa cha Efraimu, ili auweke juu ya kichwa cha Manase. Yusufu akamwambia babaye, Sivyo, babangu, maana huyu ni mzaliwa wa kwanza; weka mkono wako wa kuume kichwani pake. Babaye akakataa, akasema, NAJUA, MWANANGU NAJUA, yeye naye atakuwa taifa, yeye naye atakuwa mkuu; lakini ndugu yake mdogo atakuwa mkubwa kuliko yeye, na uzao wake watakuwa wingi wa mataifa.”

Unaona utagundua katika kifungu hiki kuwa Yusufu na Yakobo walikuwa wanajua kuwa anayewekewa mikono wakati wa Baraka ikiwa atawezewa mkono wa kuume huyu ndiye atakuwa mkubwa na anayewekewa mkono wa kushoto atakuwa mdogo, hii ni kanuni ya kibiblia ambayo watumishi wengi wa Mungu huikosea hasa wakati wa kubariki maharusi kwa mfano unakuta wanaweka mikono hovyo na wakati mwingine mke anawekewa mkono wa kuume na mume anawekewa mkono wa kushoto hili ni kosa kubwa la kiufundi na kosa katika kanuni ya kuwekea mikono muweka mikono ni lazima awe anajua anachikifanya NAJUA MWANANGU NAJUA, HUKU AKIJUA ATIAVYO MIKONO je unajua jinsi ya kuweka mikono au unaweka tu? Sio hivyo tu jua kuwa sasa naweka mikono kwaajili ya uponyaji, au naweka mikono kwaajili ya kuchochea karama, au naweka mikono kwaajili ya kuweka kiongozi na kadhalika na wakati wote lile kusudi la kuweka mikono litatamkwa kwa maombi (kunuizia), unapoweka mikono kusimika kiongozi muwekee mkono wa kuume sio wa kushoto, shikiwa maiki na mtu kisha tumia mikono yako yute miwili muwekee mikono kiongozi mkuu, unakuta mtu ameshima maiki kwa mkono wa kulia anaweka wakfu kiongozi akitumia mkono wa kushoto na watu wote wanakodoa macho na kuona tukio hilo kama tukio la kawaida inaumiza sana watu kukosea kanuni za kuwekewa watu mikono!, Yusufu aliumia alipoona Manase anawekewa mkono wa kushoto kwa nini kwa sababu alitambua kimsingi kanuni hii

Kuweka au kuwekea mikono ni urithi wa kiroho – Katika ulimwengu wa roho tendo la kumuwekea mtu mikono ni tendo la kurithi, au kurithisha tunajifunza kuwa wakati Yakobo anaweka mikono juu ya Manase na Efraimu hawa walikuwa wajukuu wake lakini kitendo cha kuwawekea mikono kilibadilisha mfumo wa maisha ya Manase na Efraimu kutoka kuwa wajukuu zake na kuwa watoto wake sawa kabisa na Simeoni na Reuben  ona

Mwanzo 48:3-6 “Yakobo akamwambia Yusufu, Mungu Mwenyezi alinitokea huko Luzu, katika nchi ya Kanaani, akanibariki, akaniambia, Mimi hapa, nitakuongezea uzao wako, na kukuzidisha, nami nitakufanya uwe kundi la mataifa; kisha nitawapa wazao wako nchi hii baada yako, iwe milki ya milele. Basi sasa wanao wawili uliozaliwa katika nchi ya Misri kabla sijaja kwako Misri ni watoto wangu, yaani, Efraimu na Manase watakuwa wangu, kama Reubeni na Simeoni. Na wazao wako utakaozaa baada ya hawa watakuwa wako; kwa jina la ndugu zao wataitwa katika urithi wao.”

Hii maana yake ni nini anayeweka mikono anawarithi anaowawekea mikono kuwa wanaye na wanaowekewa mikono wanamrithi anayewawekea mikono kuwa baba yao nadhani ni katika dhana kama hii kumekuwa na hofu kwa watu wengi kuogopa kuwekewa mikono na kila mtu kwa kuhofia kuwa baba wa mtu ambaye humjui vema au kuwarithi watoto usiowafahamu vema kwa kuwa katika ulimwengu wa roho mnabadilishana DNA za kimamlaka na uongozi

Kuwekea mtu mikono ni kumuidhinisha au kumtambulisha – Tendo la kuwekea mtu mikono ni tendo la kumuidhinisha au kumtambulisha mtu kihuduma au kumuweka katika mamlaka ya uongozi, unamuweka mtu wakfu kwaajili ua huduma aliyoteuliwa au kuchaguliwa kuifanya kama ushemasi, umisheni na kadhalika kwa hiyo kitendo cha kumuwekea mikono ni utambuzi wa hadharani kuhusu aina ya wito aliyoitiwa anayewekea mikono au kuchochea karama au kuhamishia karama na mamlaka kumuwezesha mtu huyo kutumikia vema kusudi alilowekewa  na ndio maana bado Biblia inatoa tahadhari kuwa na umakini na unayemuwekea mikono ili kama ni mwovu kumuwekea mikono maana yake ni kushiriki kazi zake mbovu au kushiriki uovu kwa hiyo lazima unayemuwekea mikono uwe umemthibitisha kuwa hatakuaibisha

1Timotheo 5:21-22 “Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, na mbele za malaika wateule, uyatende hayo pasipo kuhukumu kwa haraka; usifanye neno lo lote kwa upendeleo. Usimwekee mtu mikono kwa haraka, wala usizishiriki dhambi za watu wengine. Ujilinde nafsi yako uwe safi.”      

Unapomuwekea mtu mikono kwaajili ya huduma maana yake unagonga muhuri wako na kumuidhinisha mtu huyo katika huduma ile aliyoitiwa sasa endapo mtu huyu hayuko sawa maana yake kushindwa kwake kunawakilisha kushindwa kwako, wekea mikono mtu anayekuwakilisha vema, ambaye umemfunza vema  

Kuwekea mikono ni njia ya kupitisha neema ya Mungu.- tendo la kuwekea mikono kama ilivyo tendo la kupaka mafuta yote ni matendo ya kuipitisha neema ya Mungu kupitia mikono yetu kwenda kwa wengine kwa hiyo ni lazima tendo hili litumike pamoja na Maombi, kama ni kwaajili ya mgonjwa kutakuwa na dua maalumu kwajili ya mgonjwa kama ni kwaajili ya kuweka wakfu kiongozi dua itatamkwa ya kuweka wakfu kwa viongozi wanaohisika na waliokidhi vigezo

Yakobo 5:14-15 “Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa.”

Matendo 15:40-41 “Lakini Paulo akamchagua Sila, akaondoka, akiombewa na wale ndugu apewe neema ya Bwana. Akapita katika Shamu na Kilikia akiyathibitisha makanisa.”

Kwa hiyo ibada zote za kuwekea mikono iwe ni kwaajili ya uponyaji, kubariki ndoa kuweka viongozi zote maana yake ni kuruhusu neema ya Mungu ipite juu ya wahusika na kuwawezesha katika wajibu unaohusika kwa hiyo ni lazima maombi yahusike kwa sababu hiyo kuwekea mikono sio uchawi ni njia ya kupitisha neema ya Mungu kwa hiyo kuwekea mikono ni njia inayoonekana ya kupitisha mambo yasiyoonekana ya kiungu kwenda kwa watu husika, kwa umaalumu wake kwa kanisa na ulimwengu lakini mwenye kutoa Baraka hizo ni Mungu mwenyewe, wakati wa kubariki watoto tunaweza kuwawekea mikono, wakati wa kubatiza tunaweza kumuwekea mtu mikono na kumuombea neema ya maisha ya uchaji wa Mungu na utumishi, wakati wa kuombea wagonjwa tunaweza kuwaombea wagonjwa neema ya kupokea uponyaji, wakati wa kubariki maharusi tunaweza kuwaombea maharusi neema na wakati wa kuweka wakfu viongozi mashemasi, makasisi, maaskofu na kadhalika na hata wakati wa kusimika askofu na viongozi mbalimbali ni vema wakawekewa mikono kuwaombea neema ya Mungu kisha Mungu mwenyewe atafanya kazi yake pamoja na watu wake kwa makusudi yaliyokusudiwa, kumbuka wakati wa kuwekea maharusi mikono ya Baraka weka mkono wa kuume kwa mume na mkono wa kushoto kwa mke kufanya kinyume na hayo ni kutengeneza migogoro ya kiroho na kimaongozi kwani Mungu hadhihakiwi waweka mikono lazima wajue nini wanachokifanya wakati wanaweka mikono. Ikiwa kanisa linaweka mikono kwa askofu mkuu, na askofu mkuu aliyekuwepo madarakani hayuko, askofu mkuu mteule atawekewa mikono na mtu mwenye mamlaka ya askofu mkuu aliyetsaafu au wa kanisa lingine, ama kutoka kwa wamishionari waanzilishi wa kanisa husika au mtu mwenye mamlaka ya huduma ya kitume.

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: