Jumapili, 1 Februari 2026

Nyota za Abrahamu!


Mwanzo 15:1-5. “Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana. Abramu akasema, Ee Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski? Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu. Nalo neno la BWANA likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi. Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.”




Utangulizi:

Katika aya tulizosoma hapo juu, tunataarifiwa kuwa Mungu alimtembelea Abrahamu katika njozi na kumpa maneno ya kutia moyo, wakati huu Abrahamu alikuwa hana mtoto bado na umri wake ulikuwa umeenda sana na mke wake pia alikuwa mzee, na sasa anawaza kuacha urithi wake kwa Eliezeri mtumishi wake, kimsingi Abrahamu alikuwa amekata tamaa, na Mungu alikuja kumpasha habari za muhimu sana ambazo zilikuwa zinapita uwezo wa kufikiri kwake, wakati Abrahamu alikuwa anafikiri juu ya mtoto mmoja tu, Mungu alikuwa anafikiri uzao mwingi sana kama nyota za angani, Yeye alimleta Abrahamu nje na kumpa kazi ya kuzihesabu nyota na kisha alimhakikishia kuwa ndivyo utakavyokuwa uzao wake! Ahadi hii ya kipekee inazungumzia kuzidishwa kusikoweza kuhesabika, wema na kibali kikubwa sana cha Mungu kwa Abrahamu, na urithi wa kiroho usio na mipaka na hivyo kama wewe ni mtoto wa Abraham kwa ahadi na kwa imani maono haya yanaashiria kuwa wewe sio wa kawaida kama unavyoweza kudhani na Baraka za Mungu kwako hazina mipaka na kuwa hauko duniani kwa hasara, una ushawishi mkubwa na uwepo wako unachangia kitu Fulani duniani, wewe ni nuru inayong’aa gizani, umeinuliwa juu sana wewe si wa kawaida, maono haya hayaleti ujumbe wa uzao tu kwa Abrahamu bali pia yanaleta ujumbe kwetu kuwa sisi ni watoto wa namna gani katika uhusiano wetu na Mungu ona  

1Petro 2:9-10 “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.”

Wafilipi 2:14-15. “Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano, mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu,”

Leo basi tutachukua muda wetu kujifunza kile Mungu anazungumza na Abrahamu kutuhusu sisi pamoja na wana wa Abrahamu wengineo na kile ambacho Mungu alikuwa anamaanisha katika ujumbe wake kwa Abrahamu na kwetu tutajifuza somo hili “Nyota za Abrahamu” kwa kuzingatia vipengele muhimu vitatu vifuatavyo:-


·         Maana ya Nyota za Abrahamu

·         Nyota za Abrahamu

·         Jinsi ya kuwa nyota za Abrahamu

 

Maana ya Nyota za Abrahamu.

Mwanzo 15:1-5. “Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana. Abramu akasema, Ee Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski? Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu. Nalo neno la BWANA likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi. Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.”

Ni muhimu kufahamu kuwa asili ya ndoto hii ambayo Mungu alisema na Abrahamu ina uhusiano mkubwa na watoto wa Abrahamu wa kiroho zaidi kuliko watoto wa Abrahamu wa kimwili, kumbuka kuwa hii ilikuwa ni mara nyingine tena zaidi Mungu akizungumza na Abrahamu kuhusu uzao, hasa kwa sababu ya hali yake ya kutokuwa na watoto, Mungu alizungumza kwa namna mbili tofauti na ni lazima namna zote mbili tuzielewe vema, anapozungumza na Abrahamu kuhusu uzao mwingi na uzao wa kimwili au kibaiolojia Mungu anamwambia Abrahamu kuwa uzao wako utakuwa mwingi kama Mchanga au kama mavumbi ya nchi!

Mwanzo 13:14-18 “BWANA akamwambia Abramu, alipokwisha kutengana na Lutu, Inua sasa macho yako, ukatazame kutoka hapo ulipo, upande wa kaskazini, na wa kusini na wa mashariki na wa magharibi;maana nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele.Na uzao wako nitaufanya uwe kama mavumbi ya nchi; hata mtu akiweza kuyahesabu mavumbi ya nchi, uzao wako nao utahesabika. Ondoka, ukatembee katika nchi hii katika mapana yake, na marefu yake, maana nitakupa wewe nchi hiyo. Basi Abramu akajongeza hema yake, akaja akakaa kwenye mialoni ya Mamre, nayo ni miti iliyoko Hebroni, akamjengea BWANA madhabahu huko.”

Hesabu 23:8-10 “Nimlaanije, yeye ambaye Mungu hakumlaani? Nimshutumuje, yeye ambaye Bwana hakumshutumu? Kutoka kilele cha majabali namwona; Na kutoka milimani namtazama; Angalia, ni watu wakaao peke yao, Wala hawatahesabiwa pamoja na mataifa. Ni nani awezaye kufanya idadi ya mavumbi ya Yakobo, Au kuhesabu robo ya Israeli? Na nife kifo chake mwenye haki, Na mwisho wangu uwe mfano wa mwisho wake.”     

Mwanzo 32:10-12 “mimi sistahili hata kidogo hizo rehema zote na kweli yote uliyomfanyia mtumwa wako; maana nalivuka mto huo wa Yordani na fimbo yangu tu, na sasa nimekuwa matuo mawili.Uniokoe sasa na mkono wa ndugu yangu, mkono wa Esau, maana mimi namwogopa, asije akanipiga, na mama pamoja na wana. Nawe ulisema, Hakika nitakutendea mema, nami nitafanya uzao wako uwe kama mchanga wa bahari, usiohesabika kwa kuwa mwingi.”           

Mungu anazungumza na Abrahamu katika fungu hili akumuahidi watoto wa mwilini, wale watakaoirithi nchi pale mashariki ya kati, watoto hawa wanawakilishwa na mavumbi ya nchi, mchanga au mchanga wa bahari, na hapo katika lugha za kinabii wanazungumziwa watoto wa Abrahamu wa kimwili wa kidunia  wanaweza kuwa Wayahudi na Waarabu wa kawaida wasiookoka, kwa hiyo tunafunuliwa hapa katika maandiko kuwa Abrahamu ana watoto wa aina mbili wa mwilini na watoto wa kiroho, au waliozaliwa kwa mwili na wale waliozaliwa kwa Ahadi, tunafahamu kuwa baada ya kifo cha Sara Abraham alikuwa na watoto wengine kupitia Ketura ambao ni Zimran. Yokshan, Medani, Midiani Ishbaki na Shua ambao wengi wanaunda falme za kiarabu mashariki ya kati hata hivyo Ishamel na Isaka ndio wanaotumika zaidi kitheolojia kutufunza watoto hao wa aina mbili wa Abrahamu, yaani mmoja wa mwilini na mwingine wa ahadi, mmoja wa mjakazi na mwingine wa Muungwana, sasa hawa wanawakilishwa na mavumbi na nyota, mavumbi ni wale wa mwilini na Nyota ni wale wa Rohoni, au wa ahadi.

Wagalatia 4:22-23 “Kwa maana imeandikwa ya kuwa, Ibrahimu alikuwa na wana wawili mmoja kwa mjakazi, na mmoja kwa mwungwana. Lakini yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, yule wa mwungwana kwa ahadi.”

Kwa hiyo maana ya maono ya nyota za Abrahamu hapo, wanazungumziwa watoto wa kiroho wa Abrahamu wana wa ahadi, wale wanaomwamini Mungu kama Abrahamu alivyomwamini Mungu akahesabiwa kuwa na haki, hawa ni wale waliookoka waliomwamini Yesu kama Bwana na mwokozi kutoka kila mahali duniani wawe ni Wayahudi au Wayunani vyovyote kama wamemuamini Bwana Yesu kwa imani hao ni wana wa Ibrahimu wanaotajwa kama nyota

Wagalatia 3:6-9 “Kama vile Ibrahimu alivyomwamini Mungu akahesabiwa haki.Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu.Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa. Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani.”

Kwa hiyo Mungu anapozungumza na Abrahamu kwa habari ya watoto wa Mwilini anamuahidi uzao kama mavumbi ya nchi na anapozungumza naye kuhusu watoto wa kiroho anazungumza na Abrahamu kwa ahadi ya kuhesabia nyota, kwa hiyo nyota za Abrahamu ni watoto wake wa kiroho yaani wewe na mimi tuliookoka tulio mwamini Yesu na kuhesabiwa haki kwa imani sisi ndio “Nyota za Abrahamu” kwa hiyo katika ahadi ya uzao kwa Ibrahimu kumbuka kuna uzao kama nyota za angani na uzao kama mchanga wa bahari au mavumbi ya nchi hii inatofautisha watoto wa mwilini na watoto wa rohoni  wa Ibrahimu mwenye kusikia na asikie! Mungu anaahidi kuwabariki watoto hao wote

Mwanzo 22:16-18. “akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako KAMA NYOTA ZA MBINGUNI, na KAMA MCHANGA ULIOKO PWANI; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.”

Nyota za Abrahamu.

Mwanzo 15:1-5. “Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana. Abramu akasema, Ee Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski? Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu. Nalo neno la BWANA likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi. Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.”

Kimsingi katika maono haya Mungu alikuwa anafanya agano na Abrahamu kuwa atakuwa na watoto wa agano au watoto wa ahadi, au watoto wa imani ambao watakuwa na uwezo mkubwa sana na wenye Baraka za kudumu, watakuwa ni watoto ambao hawawezi kueleweka kwa hesabu za kibinadamu, watakuwa na ushawishi mkubwa duniani, watatoa muelekeo, wataipa dunia nuru, watatofautishwa na giza, wao hawatakuwa wa kawaida, wasioweza kuwekewa mipaka, wasiohesabika, watoto hao ni sisi na uweza wao unaelezewa katika maandiko kwa njia ya kipeke

1.       Ni watoto wa Imani – Abrahamu alikuwa katika mashaka makubwa sana , umri unaenda mkewe amezeeka na anawasiwasi kuhusu warithi wake, Lakini kwa Mungu hiyo haikuwa shida alikuwa amekusudia kumpa Abrahamu watoto wa aina zote watoto wa mwilini na watoto wa rohoni na wote wangekuwa wengi sana wa mwilini kama mchanga wa bahari na wa kiroho au wa Imani kama nyota  za mbinguni ona:-

 

Mwanzo 22:16-18. “akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako KAMA NYOTA ZA MBINGUNI, na KAMA MCHANGA ULIOKO PWANI; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.”

 

Watoto wanaofananishwa na Nyota za mbinguni ni watoto wa kiroho ni watoto wa Imani, hawa sio wale wanaozaliwa kwa damu na nyama bali ni wale wanaozaliwa kwa imani wale waliomwamini Mungu kama Ibrahimu aliyomwamini Mungu na kuhesabiwa kuwa haki.

 

Wagalatia 3:6-9 “Kama vile Ibrahimu alivyomwamini Mungu akahesabiwa haki.Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu.Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa.Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani.”

 

2.       Ni watoto wasio na mipaka - Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako, Mungu alimtoa Abrahamu nje, ilikuwa nje ya hema yake, ilikuwa nje ya kuta za nyumba, ilikuwa nje ya dunia,  ilikuwa nje ya mipaka ya kimazingira, ilikuwa nje ya fikra finyu, inayoishia kwenye anga la dunia, akamwangalisha juu, alimtazamisha mbinguni akamuamuru ahesabie nyota kama ataweza akamwambia ndivyo utakavyokuwa uzao wako, Mungu alikuwa anasema na Abrahamu kuwa wazao wake Nyota za Abrahamu hawatakuwa na mipaka, wala hawawezi kuhesabiwa kwa hesabu za kidunia wala za kibinadamu, mtu yeyote anayetaka kuangalia mambo kwa upana haangalii mambo ya duniani pekee, anaangalia yaliyo juu, watoto wa Abrahamu au nyota za Abrahamu huangalia mambo kwa upana, wanaona mbali, hawaangalii vya muda wanaaangalia vya milele, hawafikri yaliyo katika nchi pekee wanafikiri yaliyo juu, huwezi kuwawekea mipaka watu wenye mtazamo unaozidi mtazamo wa kidunia, nyota hazikai katika anga hili nyota zinakaa mbali ziko juu sana na ni kubwa mno

 

Wakolosai 3:1-2 “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi.”

 

2Wakorintho 4:16-18. “Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana; tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.

 

3.       Ni watoto wenye wito wa mbinguni – Nyota za Abrahamu ni watoto wa Imani wa Ibrahimu ambao wameitwa na Mungu kwaajili ya wito mkuu wa Mungu wa maisha yasiyokuwa ya kawaida kusudi lao si la kidunia kusudi lao ni la kimbingu, ni watu ambao wenyeji wao uko mbinguni wao wako ulimwenguni lakini sio wa ulimwengu huu,  

 

Waebrania 3:1-2. “Kwa hiyo, ndugu watakatifu, wenye kuushiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini sana Mtume na Kuhani Mkuu wa maungamo yetu, Yesu, aliyekuwa mwaminifu kwake yeye aliyemweka, kama Musa naye alivyokuwa, katika nyumba yote ya Mungu.”

 

Wafilipi 3:20-21 “Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo; atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake.”

 

Yohana 15:18-19. “Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia.”

 

4.       Ni watoto wenye hekima isiyo ya dunia hii – Watoto wa Abrahamu au nyota za Abrahamu ni wenye kutoa muongozo. Wanatoa nuru na wako tofauti na wana wa giza, tofauti na wana siasa na watawala wa dunia hii hekima waliyonayo wanaitumia kuwavuta wengi na kuwaongoza katika kuishi maisha ya haki, Nyota zinaashiria ushawishi wenye manufaa, zinaashiria uwezo wa juu wa kimtazamo, mawazo  mapana na hekima ya hali ya juu, hekima isiyokuwa ya kawaida, isiyo ya duania hii, hekima iliyohifadhiwa kwaajili yetu tu

 

Daniel 12:3 “Na walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele.”

 

1Wakorintho 2:6-7 “Walakini iko hekima tusemayo kati ya wakamilifu; ila si hekima ya dunia hii, wala ya hao wanaoitawala dunia hii, wanaobatilika; bali twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wetu;

 

Yakobo 3:15-17 “Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani. Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya. Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki.”

 

5.       Ni watoto wa Nuru – Nyota zina sifa maalumu na sifa mojawapo ni kung’aa gizani, na hivyo kuziwezesha kung’aa usiku zadi wakati dunia ikiwa giza, dunia inapokuwa imeharibiwa na giza la dhambi, giza la kutokuyajua mapenzi ya Mungu, giza la kutokuona mbele, giza la kutokumfahamu Mungu watoto wa Abrahamu ambao ni nyota huiangaza Dunia hawa ni wana wa Nuru na kamwe sio wana wa giza, kazi yao ni kuleta ufumbuzi, ni kuiangazia dunia isiwe na ukiwa, isiwe na giza, isipoteze ladha  na isiwe yenye kutisha

 

Mathayo 5:14-16 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.”

 

1Wathesalonike 5:4-5 “Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza.”

       

6.       Ni watoto wenye uwezo wa kutangaza fadhili/utukufu wa Mungu – Nyota za Abrahamu maisha yao ni ya ushindi na ushuhuda, tabia zao na matendo yao humtukuza Mungu, na shuhuda zao zinatangaza fadhili za Mungu, Kama jinsi maandiko yasemavyo kuwa moja ya kazi za anga au mbingu ni kuhubiri utukufu wa Mungu hivyo ndivyo uzao wa Abrahamu yaani nyota za Abrahamu hutangaza fadhili na utukufu wa Mungu

 

Zaburi 19:1-4 “Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake. Mchana husemezana na mchana, Usiku hutolea usiku maarifa.Hakuna lugha wala maneno, Sauti yao haisikilikani. Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. Katika hizo ameliwekea jua hema,”

 

1Petro 2:9-10 “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.”

 

7.       Ni watoto wasioweza kurogeka wala kulaanika – Nyota za Abrahamu ni watoto waliobarikiwa ambao nguvu za giza, uchawi na waganga hauwawezi, wao wanalindwa na nguvu za Mungu awaye yote atakayejaribu kufanya lolote la kichawi au la kiganga kwa lengo la kuwadhuru watoto wa Abrahamu wa Imani atashughulikiwa na Mungu mwenyewe. Watoto wa duniani wanaweza kurogwa kwa kuchukua Mchanga wa mbinguni utachukua nini huwezo kuchota nyao za watoto wa mbinguni, huwezi kufukia kitu kwao ukatoboa hawarogeki!

 

Hesabu 23:7-9 “Akatunga mithali yake, akasema, Balaki amenileta kutoka Aramu, Mfalme wa Moabu kutoka milima ya mashariki, Njoo! Unilaanie Yakobo, Njoo! Unishutumie Israeli. Nimlaanije, yeye ambaye Mungu hakumlaani? Nimshutumuje, yeye ambaye Bwana hakumshutumu? Kutoka kilele cha majabali namwona; Na kutoka milimani namtazama; Angalia, ni watu wakaao peke yao, Wala hawatahesabiwa pamoja na mataifa.”

 

Hesabu 23:18-24 “Naye akatunga mithali yake, akasema, Ondoka Balaki, ukasikilize; Nisikilize, Ee mwana wa Sipori; Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza? Tazama, nimepewa amri kubariki, Yeye amebariki, nami siwezi kulitangua. Hakutazama uovu katika Yakobo, Wala hakuona ukaidi katika Israeli. Bwana, Mungu wake, yu pamoja naye, Na sauti kuu ya mfalme i katikati yao. Mungu amewaleta kutoka Misri, Naye ana nguvu kama nguvu za nyati. Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu! Tazama, watu hawa wanaondoka kama simba mke, Na kama simba anajiinua nafsi yake, Hatalala hata atakapokula mawindo, Na kunywa damu yao waliouawa.”

 

8.       Watawashinda adui zao – Hakuna adui atakayeweza kusimama kinyume na Nyota za Abrahamu, Neno la Mungu la kinabii limeahidi ushindi dhidi ya adui wote wanaowazunguka watoto wa Abrahamu, watakata pembe za adui zao, watawavunja vunja wana wote wa ghasia, Uzao huu utamiliki mlango wa adui zao

 

Hesabu 24:16-19 “Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Na kuyajua maarifa yake Aliye Juu. Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho, Namwona, lakini si sasa; Namtazama, lakini si karibu; Nyota itatokea katika Yakobo Na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli; Nayo itazipiga-piga pembe za Moabu, Na kuwavunja-vunja wana wote wa ghasia. Na Edomu itakuwa milki Seiri pia itakuwa milki, waliokuwa adui zake; Israeli watakapotenda kwa ushujaa.Mwenye kutawala atakuja toka Yakobo, Atawaangamiza watakaobaki mjini.”

Mwanzo 22:16-18. “akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako KAMA NYOTA ZA MBINGUNI, na KAMA MCHANGA ULIOKO PWANI; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.”

                                 

Jinsi ya kuwa nyota za Abrahamu

Ni muhimu kuwa na uelewa na ufahamu kuwa Nyota za Abrahamu sio swala la ndoto na maono ya kawaida Nyota za Abrahamu leo ni mimi na wewe, Nyota za Abrahamu ni wana wa angani ni wana wa ahadi, Abrahamu ana wana wa aina mbili Nyota na Vumbi, wewe mwenyewe unaweza kuchagua kuwa mwana wa Abrahamu kwa maisha yako unaishije? Unaangaza au umefichwa, umefufuka au umezikwa, ni wa chini au ni wa juu wewe ni wa ulimwengu huu au wewe sio wa ulimwengu huu, wewe ni mwana wa Nuru au u mwana wa giza  unaishi kwa Imani au kwa kuona? una mchango duniani kwa kuangaza au huangazi, kama wewe ni mwana wa Abrahamu Nyota za Abrahamu utaenenda kwa Imani na sio kwa kuona, pale ambapo dunia inasema haiwezekani watu wa Mungu wanasema inawezekana, wana wa Abrahamu ni watoto wenye Imani, wanaishi wakimpendeza Mungu kwa Imani, hakuna jambo lenye mipaka Mbinguni, wakiroga mavumbi ya ardhi sisi haturogeki mpaka upande mbinguni, ukituweka kwenye giza tunang’aa,. Sisi ni wana wa ahadi ahatukuzaliwa kwa mwili, sisi ni wa maono ya kimbinguni na sio ya kidunia huwezi kumuwekea mipaka kwa uhuru tulio nao angani, unataka kuwa mwana wa Abrahamu ambaye ni Nyota hapa duniani uokoke leo, unataka kuwa Mwana wa Abrahamu mavumbi usiokoke ukanywagwe duniani.

2Wakorintho 5:7-9 “(Maana twaenenda kwa imani, si kwa kuona.) Lakini tuna moyo mkuu; nasi tunaona ni afadhali kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana. Kwa hiyo, tena, ikiwa tupo hapa, au ikiwa hatupo hapa, twajitahidi kumpendeza yeye

Luka 19:8-10 “Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”

Zakayo alikuwa Myahudi, lakini alikuwa uzao wa Abrahamu upande wa mavumbi, lakini alipookolewa Yesu alisema huyu naye ni mwana wa Ibrahimu, ukimkubali Yesu kuanzia leo unakuwa mwana wa Ibrahimu, ukiendelea kung’ang’ania dini kama mafarisayo unapoteza sifa ya kuwa mwana wa Ibrahimu, Wayahudi wengi waligeuka kuwa wana wa Ibilisi na wana wa mavumbi na kamwe hawakuwa nyota ya Abrahamu kwa sababu dini iliwageuza wakawa na roho mbaya na wauaji, wenye kujihesabia haki na wala hawakutenda mapenzi ya Mungu unataka kuwa Nyota za Abrahamu toka gizani leo uje nuruni, Mwombe Mungu uokolewe! Ukiokoka na kumwamini Yesu wewe ni nyota!

Yohana 8:39-44 “Wakajibu, wakamwambia, Baba yetu ndiye Ibrahimu! Yesu akawaambia, Kama mngekuwa watoto wa Ibrahimu, mngezitenda kazi zake Ibrahimu.Lakini sasa mnatafuta kuniua mimi, mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli, niliyoisikia kwa Mungu. Ibrahimu hakufanya hivyo. Ninyi mnazitenda kazi za baba yenu. Ndipo walipomwambia, Sisi hatukuzaliwa kwa zinaa; sisi tunaye Baba mmoja, yaani, Mungu. Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma. Mbona hamyafahamu hayo niyasemayo? Ni kwa sababu ninyi hamwezi kulisikia neno langu. Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.”

Wafilipi 2:14-15. “Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano, mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu,”

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!     

Hakuna maoni: