Jumapili, 15 Februari 2026

Sauti ya kijana huko jangwani!


Mwanzo 21:14-20 “Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde.”




Utangulizi:

Kama kuna mojawapo ya matukio magumu sana duniani ni pamoja na tukio la kukataliwa na baba yako aliyekuzaa, maumivu ya kukataliwa na baba yanaweza kusababisha jeraha lisiloweza kukoma, hofu, kukosa kujiamini na kutelekezwa, jambo ambalo linaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa uwezo wa kuwaamini watu, lakini pia linaweza kusababisha msongo wa mawazo, kushindwa kujitambua na kutokujitosheleza, inahitajika nguvu ya ziada sana kuweza kuwa kawaida na kuishinda hali ya kukataliwa, Lazima uwe na kitu cha ziada kuweza kujijenga kuwa unastahili na kujikomboa kutoka katika maumivu hayo ya kihisia kwani hali hii inazalisha hali ya kutaka  kujithibitisha.

Haya ndiyo yaliyomkuta Ishmael baada ya kufukuzwa nyumbani kwa baba yake ambaye kimsingi alikuwa tajiri sana wa mifugo fedha na dhahabu, lakini inaelezwa kuwa Ishamel na mama yake walitolewa mikono mitupu, wakipewa maji na mkate tu na hawakuwa hata na mtu wa kuwasindikiza, wala hawakuwa na chakula hata cha akiba, bali tupu.

Mwanzo 13:21-3 “Abramu akapanda kutoka Misri, yeye, na mkewe, na kila alichokuwa nacho, na Lutu pamoja naye, mpaka kusini. Naye Abramu alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu. Akaendelea kusafiri kutoka kusini mpaka Betheli, mahali pale palipokuwapo hema yake kwanza kati ya Betheli na Ai;”

Abrahamu alikuwa ni mtu aliyefanikiwa sana, alikuwa na makundi makubwa ya mifugo, wasimamizi, wafanyakazi, utajiri mkubwa wa fedha na dhahabu, lakini alikuwa ni mtu mwenye jeshi kali lililoweza kupigana vita na wafalme wakubwa katika vita, na moja ya vita maarufu aliyopigana na kuteka nyara ni vita iitwayo “opereshini Lutu”, ambapo alikwenda kupigana kumuokoa Lutu, Jeshi hilo lilikuwa na makomandoo 318 ambao walikuwa wamefunzwa vizuri  

Mwanzo 14:5-16 “Na mwaka wa kumi na nne akaja Kedorlaoma na wafalme waliokuwa pamoja naye, wakawapiga Warefai katika Ashteroth-karnaimu, na Wazuzi katika Hamu, na Waemi katika Shawe-kiryathaimu,na Wahori katika mlima wao Seiri, mpaka Elparani iliyo karibu na jangwa. Kisha wakarudi wakaja mpaka Enmisfati, ndio Kadeshi, wakapiga nchi yote ya Waamaleki, na Waamori waliokaa Hasason-tamari. Mfalme wa Sodoma, na mfalme wa Gomora, na mfalme wa Adma, na mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari, wakatoka wakapanga vita panapo bonde la Sidimu; wapigane na Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu, na Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, wafalme wanne juu ya wale watano. Na bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami. Nao wafalme wa Sodoma na Gomora wakakimbia, wakaanguka huko, nao waliosalia wakakimbia milimani. Wakachukua mali zote za Sodoma na Gomora na vyakula vyao vyote, wakaenda zao. Wakamtwaa Lutu, mwana wa nduguye Abramu, aliyekaa huko Sodoma, na mali yake, wakaenda zao. Mtu mmoja aliyeponyoka akaenda, akampasha habari Abramu Mwebrania; naye amekaa panapo mialoni ya Mamre, yule Mwamori, ndugu ya Eshkoli, na ndugu ya Aneri, na hao walikuwa wamepatana na Abramu. Abramu aliposikia ya kwamba nduguye ametekwa mateka, akawapa silaha vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani. Akajipanga apigane nao usiku, yeye na watumwa wake, akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba, ulioko upande wa kushoto wa Dameski. Naye akarudisha mali zote, akamrudisha na Lutu nduguye na mali zake, na wanawake pia, na watu.”

Kwa hiyo unapata picha jinsi Abrahamu alivyokuwa mtu mkubwa sana mwenye uwezo mwingi na utajiri na mtu mwenye kumiliki Jeshi lake binafsi, na alipigana na wafalme zaidi ya watano na kuwashinda na kumrejesha Lutu na familia yake nyumbani na mifugo na mali zake sasa anamfukuza mtoto wa kumzaa mwenyewe tena mikono mitupu! Kwa mujibu wa  vitabu vya mafafanuzi ya kiyahudi na tamaduni zake viitwavyo “Talmudi” na “Midrashi” vinaeleza hivi kwa lugha ya kiingereza kuhusu Ishamel “Ishmael’s experience upon being sent away by Abraham was one of severe trauma, desperation and existential abandonment” kwa tafasiri yangu isiyo rasmi wanasema swala la kufukuzwa kwa Ishmael na Abrahimu lilikuwa ni mojawapo ya tukio baya, la kusikitisha, na kutelekezwa kikatili, kusikokuwa kwa kawaida” mtu tajiri mwenye uwezo mkubwa usiokuwa wa kawaida anamtoa mtoto wake wa kumzaa mikono mitupu bila kujali hali yake ya baadaye itakuwaje hata kama alizaliwa na mjakazi!

Mgogoro ulianza wakati Sara alipomshuhudia Ishmael akimdhihaki Isaka siku ile alipofanyiwa ibada ya shukurani kwaajili ya muujiza ule mkubwa wa kuzaliwa kwake Isaka na kuachishwa kunyonya

Mwanzo 21:6-10 “Sara akasema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atacheka pamoja nami. Akasema, N'nani angemwambia Ibrahimu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake. Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka.”

Jambo hili halikumfurahisha Abraham, hata hivyo Mungu alimwambia Abrahamu afanye kile ambacho Sara ameagiza

Mwanzo 21:11.-12 “Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa.”

Jambo hili linamuweka Ishmael na mama yake katika wakati mbaya sana sasa wanapitia hali ngumu na ya uchungu sana, tutaliangalia somo hizi Sauti ya kijana Jangwani kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Maumivu ya kukataliwa

·         Sauti ya kijana huko jangwani

·         Mungu anamkumbuka kijana huko jangwani

Maumivu ya kukataliwa

Tunawaona Ishmael na mama yake wakiwa jangwani maji yanawaishia na mkate unamalizika hali ya mauti sasa ndiyo inayomzunguka mtoto, akiwa ni kijana wa miaka 16 tu ambaye alilelewa maisha ya kudekezwa kama mtoto pekee nyumbani ghafla maisha yanabadilika na anatupwa jangwani, moyoni ana maumivu makali ya kutupwa na kukataliwa anajiona kama mtu asiye na bahati na ambaye amesalitiwa na baba yake na sio hivyo tu ametelekezwa, Ishmael na mama yake wanachanganyikiwa wamefukuzwa nyumbani nani kama wanatakiwa kuja kufia jangwani.

Mwanzo 21:14-16 “Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia.”  

Maji yamekwisha chakula pia kimeisha ni jambo la kushangaza kuwa wanatupwa hata bila ya chakula cha akiba na wanapotelea katika jangwa anakabiliwa na kiu anachoka na wamekuwa dhaifu, mama yake anamuweka katika kichaka cha nyikani anakimbia mbali ili asimuone mtoto wake anapokata roho ana wasiwasi na hofu ya kuona mauti ikimmaliza mwanae

Kijana anajutia kumdhihaki Isaka anatambua kosa lake ambalo sasa linamletea mateso, anakuwa imara na anapokea mabadiliko toba yake inaonekana kwa ushahidi kuwa alimalizana vizuri na baba yake kwani alielewa upumbavu wake na sasa alimuheshimu Isaka kwa mujibu wa masimulizi ya marabi wa kiyahudi “Rabbinic tradition” (Genesis Rabbah) adhabu hii ilileta toba na mabadiliko makubwa kwani alikuja kumzika baba yake kwa heshima akiwa na Isaka ona:-

Mwanzo 25:8-10. “Ibrahimu akafariki, naye akafa katika uzee mwema, mzee sana, ameshiba siku, akakusanyika kwa watu wake. Isaka na Ishmaeli wanawe wakamzika katika pango ya Makpela, katika shamba la Efroni bin Sohari Mhiti, lielekealo Mamre. Katika lile shamba alilolinunua Ibrahimu kwa wazawa Hethi, huko ndiko alikozikwa Ibrahimu na Sara mkewe.”

Ndugu yangu kutelekezwa hakumaanishi kuwa umefika mwisho wa maisha, kutelekezwa hakumaanishi kuwa Mungu amemalizana na wewe watu wanaweza kukukataa na kukutelekeza lakini Mungu kamwe hawezi kufanya hivyo, Mikono yake bado iko wazi na anaweza kukupokea, Jangwa ndilo linalomfanya mtu kuwa imara na kuacha upumbavu wake, Jangwa lilikuwa eneo la somo kwa Ishmael, alijifunza kusamehe hakumuwekea kinyongo baba yake  Mungu aliisikiliza sauti yake kule jangwani  na alikuwa amemuandalia kisima kizuri cha maji ambayo yangeokoa uhai wake na kumfanya kuwa kijana shujaa,

Zaburi 34:6-9 “Maskini huyu aliita, Bwana akasikia, Akamwokoa na taabu zake zote.Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa. Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini. Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao hawahitaji kitu.”

Sauti ya kijana huko jangwani

Mwanzo 21:17-21 “Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde. Akakaa katika jangwa la Parani; mama yake akamtwalia mke katika nchi ya Misri.”

Jina Ishmael maana yake Mungu amesikia kilio changu, Mungu alisikia kilio cha mtoto, Mungu sio dhalimu hata pale inapoonekana kuwa ndoto zako zimezikwa na unabii kukuhusu umefukiwa katika mchanga, Mungu ataendelea kuwa mwaminifu kwa watu wake na neno lake mbingu ziliitikia sauti jangwani, kijana kweli alikuwa amefukuzwa nyumbani lakini hakuwa amefukuzwa kutoka kwenye uwepo wa Mungu, Mungu alimwambia Hajiri usiogope, na Mungu aliyafunua macho yake na akaona kisima chenye maji, kisima ambacho kimsingi kilikuwapo pale  tayari, watu wengi sio kuwa Mungu amewaacha bali watu wengi wamefungwa macho wasione fursa na ndio maana wanalia, Ni kazi ya Roho wa Mungu kukufunulia fursa, hauna sababu ya kulia lakini unapaswa kuinua macho yako uone.

Unaweza kukataliwa, kuteswa na kufukuzwa na hata kuwekwa nje ya mtandao “Systems” unaweza kutupwa na baba yako wa kiroho kabisa na unaweza usijaliwe na wale waliotakiwa kukujali lakini hili ndio tunalojifunza kuwa kama Mungu nanaweza kusikia kilio jangwani taabu yako haiwezi kunyamaziwa mbinguni, inaweza kunyamaziwa na wanadamu lakini Mungu hawezi kunyamaza, unaweza kufukuzwa, unaweza kuwa na kiu na unaweza hata kusahaulika , lakini Mungu hawezi kuacha kukusikia, utembeleo wa malaika hauzuiliki na hali, na uhakika wa maisha yako ya baadae uko mikononi mwa Mungu, maji yanaweza kuisha, mkate unaweza kumalizika, milango inaweza kufunga na watu wanaweza kukaa kimya lakini Mungu anayemsikiliza Ishmael yuko hata leo yeye hatakuacha ufie jangwani atakufunulia macho yako na atakuelekeza nini cha kufanya, Mungu alikuwa pamoja na Ishamel Mungu hana upendeleo haijalishi wewe ni wa mwanamke muungwana au wa mjakazi.

Mungu anamkumbuka kijana huko jangwani

Mungu alikumbuka agano lake alilolifanya na mama yake kuhusu kijana aliahidi kuwa angemfanya taifa kubwa na kwa sababu hiyo kufa jangwani haukuwa mpango wa Mungu, Mungu alikumbuka mpango wake na Mungu alisikia kilio cha Ishmael Mungu akamkumbuka kijana huko jangwani!

Mwanzo 16:6-11 “Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. Malaika wa BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai. Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono yake. Malaika wa BWANA akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi. Malaika wa BWANA akamwambia, Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Ishmaeli, maana BWANA amesikia kilio cha mateso yako.”

Mungu alizungumza na Hajiri wakati wa changamoto, Mungu huleta ufumbuzi wakati wa changamoto, Mungu alimwambia asiogope, na Mungu alimfunulia macho kuona kisima cha maji, Mungu alikuwa ameahidi kumfanya Ishamel kuwa taifa kubwa na Ishamel akawa mkuu mno na wafalme 12 walitokea katika viuno vyake

Mwanzo 25:12-17 “Hivi ndivyo vizazi vya Ishmaeli, mwana wa Ibrahimu, ambaye Hajiri, Mmisri, mjakazi wa Sara, alimzalia Ibrahimu. Na haya ndiyo majina ya wana wa Ishmaeli, kwa majina yao, na kwa vizazi vyao. Mzaliwa wa kwanza wa Ishmaeli, ni Nebayothi, na Kedari, na Abdeeli, na Mibsamu, na Mishma, na Duma, na Masa, na Hadadi, na Tema, na Yeturi, na Nafishi, na Kedema. Hao ndio wana wa Ishmaeli, na hayo ni majina yao, katika miji yao, na katika vituo vyao, maseyidi kumi na wawili kwa kufuata jamaa zao. Na hii ndiyo miaka ya maisha ya Ishmaeli, miaka mia na thelathini na saba. Akakata roho, akafa, akakusanyika kwa watu wake.”

Mungu ndiye anayeshikilia maisha yako, mipango yako iko katika mikono yake tangu kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu, hakuna bahati mbaya yeye ni muumba mwenye upendo, kila mtu duniani yuko katika mpango wake na ni yeye ndiye anayeziongoza njia zako, na makusudi yake kwako atayatimiza mwenyewe katika mpango wake haijalishi ni vikwazo gani utakutana navyo au ni giza gani liko mbele yako hiyo haimaanishi kuwa Mungu amekuacha ni swala la kufumba na kufumbua tu amini mchakato wa Mungu “trust the process” yeye atakulinda, atakuongoza atakuweka katika njia iliyo sahihi, hakuna anayeweza kuuzuia mpango wake wala makusudi yake, Mungu anaweza kuwainua watu kwaajili yako na wakakutendea mema watakusaidia kulifikia kusudi lako haijalishi watu wamekuchezea kiasi gani lakini Mungu ni mwenye nguvu kuliko wao, Je uko kwenye jangwa gani? Mungu anaisikia sauti yako, hutafia jangwani yeye bado hajamalizana na wewe, Mungu ana ahadi na wewe na ni lazima aitimize!

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima 

Hakuna maoni: