Jumapili, 17 Agosti 2025

Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote!


Yohana 3:30-31 “Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua. Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.”




Utangulizi:

Moja ya watu waliokuwa na uwezo mkubwa sana wa kumuelezea vizuri Yesu Kristo na kumtambulisha kwa watu ni pamoja na Yohana Mbatizaji, huyu ni moja ya manabii waliopata neema ya ajabu sana ya sio tu kutabiri kuhusu ujio wa Maisihi, lakini kuonyesha moja kwa moja mubashara kuhusu Yesu Kristo, Mjadala kuhusu Yesu ulikuja baada  ya watu kumuhoji kuhusu habari za Yesu ambaye watu wengi walikuwa wameanza kumuendea, huku wengine wakiendelea kuonyesha heshima kubwa kwa Yohana Mbatizaji wakifikiri kwa kuwa alitokea nyikani na alikuwa kama Eliya kimtazamo na kimuonekano kwamba huenda ndiye angefaa kuwa masihi, Hata hivyo yeye aliendelea kuwasisitizia kuwa huyo anayefanya wanafunzi wengi ndiye masihi na yeye hana budi kupungua ili huyo aweze kuzidi

Yohana 3:26-31 “Wakamwendea Yohana, wakamwambia, Rabi, yeye aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Yordani, yeye uliyemshuhudia, tazama, huyo anabatiza na watu wote wanamwendea. Yohana akajibu, akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka mbinguni. Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya kwamba nalisema, Mimi siye Kristo, bali nimetumwa mbele yake. Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti yake bwana arusi. Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua. Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.”

Yohana anamuelezea Yesu kwa ufunuo mkubwa ambao sio rahisi mwanadamu wa kawaida kuwa nao, Yeye anamuelezea Yesu kama Yeye ajaye kutoka juu, ana anamfunua hivyo kwa umati mkubwa wa watu akimaanisha kuwa Yesu sio nabii wa kawaida wala Mwalimu wa kawaida wa duniani bali huyu ashuka kutoka mbinguni, Yohana alikuwa akiuthibitishia ulimwengu kuwa Yesu ana mamlaka kubwa sana kuliko hata yeye mwenyewe, Yesu ana asili ya uungu na sio ya kibinadamu tu, Kila Mwalimu wa kweli wa neno la Mungu ni lazima awe na uhakika wa Yesu ni nani na awe anajua kumuelezea vizuri, na kutokujaribu kuchukua nafasi yake na kumleta Yesu mzima mzima kwa jamii ili jamii imkubali na kupata masaada kutoka kwake, leo tutachukua muda kuijadili kauli hii ya Yohana Mbatizaji Yeye ajaye kutoka juu! kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Asili ya Yesu Kristo.

·         Yeye ajaye kutoka juu.

·         Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote!


Asiili ya Yesu Kristo!

Yohana ni moja ya manabii wa ajabu sana na wa tofauti mno, Kabla ya wanafunzi wa Yesu kutuelezea kwa kina kuwa Yesu Kristo ni nani Yohana mbatizaji ni mtu wa kwanza kutuelezea ukuu wa Yesu Kristo Yeye anamuelezea Yesu kama ambaye asili yake si ya dunia kama alivyo Yohana na manabii wengine na sisi, Yesu anaelezewa na Yohana Mbatizaji kama ambaye asili yake ni ya mbinguni yaani Yeye ajaye kutoka juu!

Yohana 3:31 “Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.”

Yohana anatufunulia hapa kwamba Yesu amekuja kutoka mbinguni na hivyo asili yake sio ya dunia, ukweli huu unakubalina na mafundisho ya kibiblia na maneno ya Bwana mwenyewe kwamba Yeye amekuwepo kabla hata ya Ibrahimu baba wa Imani ya kiyahudi hajakuwepo, Yeye Ibrahimu asijakuwako mimi niko (“Before Abraham was born I am!”) yaani kabla Ibrahimu hajazaliwa mimi niko alisema Yesu Kristo mwenyewe.

Yohana 8:56-58 “Ibrahimu, baba yenu, alishangilia kwa vile atakavyoiona siku yangu; naye akaiona, akafurahi. Basi Wayahudi wakamwambia, Wewe hujapata bado miaka hamsini, nawe umemwona Ibrahimu? Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko.”

Neno la Mungu vilevile linathibitisha ya kuwa Yesu Kristo kabla ya kuvaa mwili wa kibinadamu alikuweko tangu milele kama neno la Mungu na alihusika katika kuumba ulimwengu na hapa Duniani alijifunua kwetu kwa utukufu kama wa mwana pekee wa Mungu.

Yohana 1:1-3,1 4 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. 14 Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”

Kwa msingi huo neno la Mungu linabainisha wazi kuwa Yesu Kristo hakuwa mwanadamu wa kawaida, mamlaka yake na uwezo wake ulikuwa uko juu ya kawaida ya kibinadamu kama anavyoeleza Nabii Yohana mbatizaji, ufahamu huu kwa kweli sio ufahamu wa kawaida ni lazima uwe umefunuliwa na Roho Mtakatifu kumfahamu na kumtambua Yesu kuwa ni mtu wa namna gani, mapema kabla ya kuzaliwa kwake nabii Mika aliyeishi karibu wakati sawa na nabii Isaya alieleza mpaka mahali atakapozaliwa Masihi na kuutaja mji atakaozaliwa kuwa ni Bethelehemu, lakini kama haitoshi alieleza kuwa mtu huyu asiyekuwa wa kawaida asili yake imekuwepo tokea enzi na enzi.

Mika 5:2 “Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.”

Nabii Isaya akitabiri kuhusu kuja kwa masihi Yaani Bwana Yesu yeye naye alitabiri na kuonyesha kuwa Yesu atakuwa mfalme wa ajabu na baba wa milele, na Mungu mwenye nguvu, kwa ujumla maandiko yanamuelezea Yesu kwa namna pana zaidi kuliko watu wengine wanavyoweza kufikiri au kukosoa kwa kukosa maarifa Isaya anasema:-

Isaya 9:6-7 “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa Jina Lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda hayo.”

Kwa msingi huo sio kuwa wakristo wanamkuza tu Yesu Kristo na wengine wanadhani kuwa tunakufuru, lakini ni ukweli ulio wazi manabii walimfunua Yesu Kristo kwetu pamoja na mitume wake ambao kwaasili ni wayahudi wanatuwekea wazi kuwa Yesu Kristo asili yake ni Mbinguni na kuwa alikuwako huko toka milele na sio hivyo tu tunaelezwa kuwa alikuwa Mungu na kwa kuja kwake duniani ililikuwa swala la unyenyekevu mkubwa na kujidhili au kujishusha kwa namna isiyoweza kufananishwa au labda kuwa sawa na mtumwa ingawa yeye alijijua kuwa hakuwa mtu wa kawaida, Paulo mtume analiweka hilo sawa katika waraka wake kwa Wafilipi ona:-

Wafilipi 2:5-8 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.”

Kwa sababu hiyo Yohana alimtambua Yesu kuwa alikuwa mwanadamu wa viwango vingine, mwanadamu asiyekuwa wa kawaida alisema huyu ni mkuu mno akionyesha ukuu wa Yesu Kriso katika kiwango ambacho yeye mwenyewe alisema hastahili hata kulegeza gidamu za viatu vyake:-

Luka 3:16-17 “Yohana alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto; ambaye pepeo lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake, na kuikusanya ngano ghalani mwake, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.”  

Yohana anatusaidia wanazuoni kutokumchukulia Yesu Kristo kama mtu wa kawaida au kama manabii wengine, Yesu Kristo hafananishwi wala kulinganishwa na kitu chochote, kujishusha kwake na unyenyekevu wake wa kukubali kudhalilishwa msalabani kusiwanye wanadamu wawe na nafasi ya kumdhalilisha na kumkufuru badala yake wanapaswa kuogopa na kumchukulia kwa heshima kubwa kwani ni zawadi ya kipekee ambayo Mungu amewapa wanadamu ili tuweze kuokolewa Yesu yeye asili yake ni juu, yaani yeye ametokea Mbinguni ambako alikuweko tangu mwanzo, Yeye yuko juu y asana kuliko ufalme wowote, mamlaka yoyote, usultani wowote, enzi yoyote, na jina lolote litajwalo ulimwenguni humu na vitu vyote viliumbwa kwa njia yake na kwaajili yake

Waefeso 1:17-21 “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia;”             

Wakolosai 1:16-19 “Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae;”

Kwa msingi huu kwa uchunguzi wa kimaandiko utakubaliana nami kwamba Yesu, Yu Juu ya yote kama yanenavyo maandiko!

Yeye ajaye kutoka juu

Wako watu katika nyakati za leo hususani watu wanaoendesha mijadala ya kidini ambao humchukulia Yesu kwa mchezo mchezo na wala hawataki kumuelezea Yesu Katika namna ambayo maandiko humuelezea, mijadala ya aina hii, Nabii Yohana mbatizaji aliizima kabisa kwani wanazuoni wa wakati huo walitaka kumlinganisha Yeye (Yohana mbatizaji) au nabii (Yahaya bin Zekaria) na Masihi Bwana Yesu, wao walimtazama kwa mtazamo wa nje tu na kuona kama Nabii Yohana alionekana wa maana sana labda huenda hata kuliko Yesu, kwa sababu yeye alitokea Porini/Nyikani/jangwani na alivaa nguo za ngozi na singa za ngamia akila nzige na asali, akijiepusha na maisha ya kawaida ya mitaani akiishi nyikani, kujidhabihu kwake kulionekana kimtazamo kuwa alikuwa nabii kweli kweli na  maarufu sana labda huenda kuliko hata Masihi, Yesu alivyokuja na mtindo wake wa maisha pengine pia na kuonekana kwake kama kijana mdogo wa miaka 30 hivi, Yohana alitahadharisha kuwa Yesu sio wa kulinganishwa naye kumlinganisha yeye Yesu ni sawa tu na msimamizi wa harusi na Bwana harusi mwenyewe, aliwathibitishia kuwa maagizo yote anayoyatoa Yesu ni muhimu akasikilizwa kwa kuwa Yeye ni wa mbinguni na Yohana ni wa duniani, Yesu ni wa mbinguni anatoka juu na yuko juu ya manabii wengine wote ambao asili yao ni ya dunia na wananena mambo ya duniani Lakini sivyo ilivyo kwa Yesu Kristo ambaye asili yake ni juu na ananena maswala kutoka mbinguni!.

Yohana 3:25-31 “Basi palitokea mashindano ya wanafunzi wa Yohana na Myahudi mmoja juu ya utakaso.Wakamwendea Yohana, wakamwambia, Rabi, yeye aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Yordani, yeye uliyemshuhudia, tazama, huyo anabatiza na watu wote wanamwendea. Yohana akajibu, akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka mbinguni. Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya kwamba nalisema, Mimi siye Kristo, bali nimetumwa mbele yake. Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti yake bwana arusi. Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua. Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.”                 

Yohana alikuwa akiwahakikishia watu kuwa mamlaka ya Yesu sio ya kawaida  na kuwa iko juu kwa namna ambayo haiwezi kulinganishwa na mamlaka nyingine yoyote, alisema tena sifa za Yesu zinapaswa kuzidi na za kwake yaani Yohana mbatizaji zinapaswa kupungua, Yesu ni mwenye mamlaka na nguvu na hekina na akili na ujuzi na maarifa na ufahamu kuliko mtu mwingine yeyote, hakuna mamlaka, wala serikali,  wala usultani wala uongozi, wala bosi wala mwenye mamlaka wala mwenye serikali inayoweza kuzidi mamlaka aliyonayo Yesu Kristo, Yesu mwenyewe anathibitisha kuwa ameshuka kutoka mbinguni na anatakeleleza mapenzi ya baba yake wa mbinguni:-

Yohana 6:32-38 “Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima. Basi wakamwambia, Bwana, sikuzote utupe chakula hiki. Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe. Lakini naliwaambia ya kwamba mmeniona wala hamwamini. Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka.”

Yesu anadhihirisha wazi katika neno lake ya kuwa kama ile mana ilivyoshuka kutoka mbinguni na kuwapa uzima wa muda baba za wayahudi huko jangwani ambao kimsingi walikufa, yeye alikuwa anamaanisha kuwa ile mana ilikuwa ni ishara ya kuwa baba anawapa chakula kishukacho kutoka mbinguni na kuwa kama wakimuamini hawataona njaa tena na ya kuwa hawatakufa bali watakuwa na uzima wa milele wakati watu waliona kuwa yeye ni mwana wa seremala tu na wakidhani kuwa masihi atashuka moja kwa moja kwa jinsi ya kuonekana kimwili kama atakavyokuja mara ya pili duniani, Lakini masihi alikuja bila wao kuelewa. Ujio wa Yesu Kristo kutoka juu mbinguni una faida kubwa sana katika maisha ya wanadamu wote kama tutatambua kuwa Yesu yuko juu ya yote na kumuamini kuna faida lukuki ambazo tutafaidika kwa imani hii, Neno ajaye kutoka juu katika kiyunani linasomeka “Erchomai anōthen esti epanō ambapo maneno mawili “Anōthen na epanaō” yana maana “From the beginning he is over on” yaani mwenye mamlaka au mwenye cheo cha juu cha kijeshi tangu mwanzo, hii inazungumzia kuwa katika mamlaka za kijeshi Yesu ni jemadari tangu mwanzo na ni jemadari aliyeko juu ya mambo yote ya mbinguni na duniani, anaweza kukupigania vita ya aina yoyote ile, na anaweza kuagiza au kuamuru majeshi ya malaika kama amiri jeshi mkuu.         

Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote!

Yohana sio tu katika majibu yake anataka kuonyesha kuwa Yesu asili yake sio ya dunia na kuwa Yesu asili yake ni kutoka juu, lakini pia anakazia kuwa yuko juu ya yote, Yohana anapotuelezea kuwa Yesu yuko juu ya yote anafunua faida kubwa zenye maana pana sana kwa kila mwamini ulimwenguni, hii inaonyesha kuwa Yesu ana mamlaka yote mbinguni na duniani, ana heshima ya kipekee na nafasi ya kwanza katika kila jambo, Yesu kuwa juu ya yote ina maana gani na faida gani hasa

-          Ana mamlaka yote mbinguni na Duniani – Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.” maana yake Serikali yake iko juu ya serikali zote, dola yake iko juu ya dola zote, mamlaka ya  kimwili na kiroho iko na yeye, kama ni kukata rufaa unakata kwake, kama ni hospitali ya rufaa yeye ndio hospitali ya mwisho, kama umeonewa yeye ndiye yuko juu ya wale waliokuonea ana mamlaka yote kama kuna watu wanajitukuza na kujiiinua juu yako basi kumbuka ya kuwa Yeye ana mamlaka kubwa kuliko hiyo yu juu ya yote, chochote kinachojiinua dhidi yako kikumbushwe kuwa Yuko aliye juu zaidi yake

 

-          Jina lake lina nguvu kuliko majina yote – Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”

 

-          Hukumu yote ya wanadamu imewekwa chini yake – Matendo 17:31 “Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu.”

 

Yohana 5:22-23 “Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote; ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka.”   

 

-          Sisi tu warithi pamoja naye – Warumi 8:16-17 “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.”

 

-          Yeye ndiye anayehusika na ufufuo – Yoahan 11:25 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;”

 

-          Akifunga hakuna afunguaye, akifungua hakuna afungaye – Ufunuo 3:7-8 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye. Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.”

 

-          Yeye ndiye mwanzo na mwisho Alfa na Omega – Ufunuo 1:8 “Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.”

 

-          Ana mamlaka ya kusamehe dhambi – Marko 2:5-10 “Naye Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako. Na baadhi ya waandishi walikuwako huko, wameketi, wakifikiri mioyoni mwao, Mbona huyu anasema hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu? Mara Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri hivi mioyoni mwenu? Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza)        

 

-          Ana mamlaka dhidi ya shetani - Wakolosai 2:14-15 “akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.”

 

Yesu Kristo kuwa juu ya yote maana yake ana mamlaka ya kila kitu mbinguni na duniani na kuwa kila kitu kiko chini yake, yeye ni chanzo cha wokovu wetu wa mwili nafsi na roho, ni kiboko ya mahitaji yetu yote na ni mwenye nguvu dhidi ya adui zetu wote chochote kinachojiinua juu yako kikumbushe tu kuwa Yeye ajaye kutoka juu yu juu ya yote, mashetani, mapepo, wenye mamlaka wenye uwezo, wanajimu na wachawi, wasihiri, wapiga ramli, waganga wa kienyeji, waonevu,  magonjwa na mateso ya aina mbalimbali yakumbushwe tu kuwa Yeye ajaye kutoka juu  huyo yu juu ya yote, dhuruba yoyote ikikusumbua, mateso yoyote yakikusumbua, magonjwa yoyote yakikusumbua, majungu yoyote yakikusumbua, mtu yeyote akikusumbua, mwenye mamlaka yeyote akizingua, changamoto zozote zikikusumbua unapaswa kuzikumbusha tu kuwa AJAYE KUTOKA JUU HUYO YU JUU YA YOTE, Kristo Yesu sio wa kulinganishwa na nabii yeyote, wala mtume yeyote wa dini yeyote wala mwanafalsafa yeyoye, wala mwasiasa yeyote, wala msanii yeyote, wala kiongozi yeyote, watambulishe na kuwajulisha kuwa ajaye kutoka juu huyu yu juu ya yote, kama liko jambo linajitukuza juu yako, linaonekana kuwa gumu kwa sababu yoyote,  lina jina la kutisha, linakuogopesha, linakunyima usingizi, linakudhoofisha, iwe ni ndoa, watoto, kazini, biasharani, mdeni na kadhalika wote washitakie kwa Huyu mwamba aliye juu ya yote, aliye juu ya majeshi yote anayeweza kukushindia vita yoyote ambaye asili yake sio ya dunia huyu amekuja kutoka juu ana mamlaka yote kwa faida ya mahitaji yetu yu juu ya yote! Yesu kuwa juu ya yote maana yeke tunaweza kuliitia jina lake kwa changamoto zozote zile maana yeye yuko juu ya hizo, haupaswi kuogopa, haupaswi kulia, haupaswi kuhuzunika, haupaswi kusikitika tunaye aliye juu ya yote!

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!

0718990796

Jumapili, 10 Agosti 2025

Mlango wa Kutokea!


1Wakorintho 10:13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na MLANGO WA KUTOKEA, ili mweze kustahimili.”



Utangulizi:

Ni muhimu kuwa na ufahamu kuwa katika maisha ya wanadamu wote sio waliookoka peke yao wote kupitia katika majaribu mbalimbali ni jambo la kawaida na lisiloepukika, Maandiko yanatufundisha kuwa hakuna jaribu jipya kila majaribu au jaribu unalolipitia wewe duniani wako watu wamelipitia pia na wakati mwingine jaribu kubwa au analipitia kwa njia ngumu kuliko unayoipitia wewe, na kwa sababu hiyo hatupaswi kabisa kushangaa na kuona kuwa ni kitu kigeni au cha ajabu kitupatacho.

1Petro 4:12-13 “Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho. Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.”

Mitume walikuwa wanamaanisha Msiba/Majaribu au mambo ya kuhuzunisha na ya kuumiza yanayowapata watu wa Mungu ni ya kawaida kwa wanadamu wote ni mambo yanayowapata wanadamu wote wana wa Mungu na wanadamu wakawaida wasiomuamini Mungu, kwa vile tu tuko Duniani basi majaribu haya Mitihani hii/na Magumu yaani (test and trials or temptations) ni jambo la kawaida sio geni na sio ajabu na halikupati au halijawahi kukupata wewe peke yako, watu wengi sana wanapitia hayo kwa hiyo sio kitu kigeni, na habari njema zaidi  ambayo Roho Mtakatifu anaizungumza leo ni kuwa kwa kila jaribu Mungu atafanya na mlango wa kutokea, au atafanya njia mbadala ya kutokea!

Leo leo basi kwa uweza wa Roho Mtakatifu tutachukua muda basi kujifunza na kutafakari kwa undani kuhusiana na kifungu hiki muhimu cha maandiko kwa kukiangalia kwa kina na mapana na marefu ili tuweze kupata kile Mungu anataka kusema nasi kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Jaribu kawaida ya wanadamu;  

·         Mungu atafanya mlango wa kutokea:

·         Mlango wa kutokea

 

Jaribu kawaida ya wanadamu:

1Wakorintho 10:13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.”

Ni muhimu kwanza kufahamu kuwa Paulo mtume hapa anazungumzia kwamba majaribu/na mitihani ni kawaida ya wanadamu, Paulo hapa anawaelezea watu waliookoka wa Korintho kwamba majaribu ni kawaida ya wanadamu; maana yake majaribu ni ya kawaida kwa watu wote, na sio wailiookoka peke yao Katika Biblia ya kiyunani neno kawaida ya wanadamu linasomeka kama “Anthrōpinos” ambalo kwa kiingereza linasomeka kama “human common to man” kwamba majaribu huwapata wanadamu wote, aina binadamu wote, watoto wa Adamu wote, kila mtu, kila mwanadamu common to man, common to mankind, common to men after the manner of men kwa lugha nyingine It emphasize that no temptation/trials is unique to an individual in its nature  inakaziwa hapo kuwa hakuna jaribu au mtihani ambao unaweza kuwa wa kipekee kwa mtu fulani tu kwa asili na kwa sababu hii mitume wengi na manabii waliandika kuwa kamwe mwanadamu awaye yote hapaswi kuona kuwa ni ajabu, au ni kitu kigeni kimpatacho kwa hiyo tunapopitia changamoto mbalimbali zinazozalisha huzuni/msiba duniani hupaswi kudhani kuwa ni wewe tu unayepitia hayo, na hii inatusaidia tusilie  na kumlaumu Mungu Baba kwa nini mimi tu “WHY ME ALONE!” kwa hiyo maana yake swala la kujaribiwa, kuudhiwa, kupitia magumu, kuibiwa, kuonelewa, kudhulumiwa, kuachika, kutapeliwa, kufilisika, kukosa, kufukuzwa kazi, kushindwa kisiasa na kadhalika na mitihani mbalimbali mambo ya kuumiza hayakupati wewe pekee huwapata “WOTE” kwa sababu hiyo hauko peke yako na usione ajabu kwa hiyo tuwapo duniani/ulimwenguni dhiki ni kawaida, “KAWAIDA”

Yohana 16:33 “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.”

Yohana 16:1-4 “Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa. Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada. Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi. Lakini nimewaambia hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia. Sikuwaambia hayo tangu mwanzo, kwa sababu nalikuwapo pamoja nanyi.”      

1Petro 4:12-13 “Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho. Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.”

Kwa hiyo kwa mujibu wa neno la Mungu majaribu, vishawishi na dhiki na mateso na adha ni jambo la kawaida tuwapo Duniani, kila mwanadamu anapitia changamoto za aina mbalimbali kwa nyakati mbalimbali, unaweza ukapitia jambo zito na ukapiga kelele kumbe wako waliopita na wamekaa kimya hii ni hali ya kawaida na hatupaswi kuona ajabu wala hatupaswi kuona kuwa ni kitu kigeni. Jaribu haliwapata ninyi ISIPOKUWA LILILO KAWAIDA kwa hiyo mpenzi unayoyapitia ni ya KAWAIDA.

Mungu atafanya mlango wa kutokea:

1Wakorintho 10:13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.”

Katika namna ya kipekee sana Neno la Mungu linatutaarifu kuwa pamoja na kuweko kwa majaribu na mitihani ya aina mbalimbali Paulo anasema Mungu ni mwaminifu ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo yaani maana yake Mungu hataliacha jaribu likuumize au likuzamishe na au lilete uharibifu badala yake ataleta msaada maana yake ATAFANYA NA MLANGO WA KUTOKEA hapo liko jambo la kujifunza tena kuhusu tabia na mwenendo wa Mungu kwa watu wake Mungu atafanya mlango wa kutokea hii maana yake ni nini?

Katika Biblia ya kiyunani neno mlango wa kutokea linasomeka “Ekbasis” au “Exodos” ambalo kwa kiingereza ni “a way to escape” au “exit”, “way out”, “departure” au “release” kwa Kiswahili ni mlango wa kutokea, au njia ya kutoka au njia ya kutoka kwa uhuru, au kutolewa, Kimsingi anachokizungumzia Paulo mtume hapo ni Njia au mlango ambao mtu huweza kuutumia kuondoka wakati wa mazingira ya hatari au mazingira yenye shinikizo, Kwa hiyo Mungu katika Hekima yake kama walivyo wajenzi wa majengo mbalimbali duniani na vyombo mbalimbali vya moto huwa wanaweka mlango maalumu wa dharula linapokuwa limetokea tatizo ili watu waweze kuokoka na kuepuka madhara wakati wa matatizo, Mlango huo au njia hiyo huitwa mlango wa dharula, Milango hii huwa na alama maalumu za kuonyesha mahali pa kukimbilia na kutokea endapo kutatokea jambo la dharula na imeokoa wengi.

Mlango wa dharula kwa kawaida huweko katika majengo yote na vyombo vyote muhimu na ni mlango au njia inayotumika kwa makusudi ya usalama, Mlango wa kutokea EXIT hujengwa maalumu kwaajili ya matukio hatarishi kama moto au ajali  na hivyo hutoa njia iliyo wazi kwaajili ya kuwasaidia wahusika na kupunguza hatari na vifo kwa watu wa jengo au chombo husika badala ya kutumia mlango mmoja au mlango uliozoeleka jambo ambalo linaweza kusababisha maumivu makubwa sana, Mlango wa dharula wa kutokea hubuniwa na wajenzi kwa kusudi la kupunguza taharuki na kuwapa watu wepesi wa kuepuka madhara, ni mlango unaokufanya utoroke kwa haraka bila kuchanganyikiwa wala kubanana na watu, ni mlango unaosaidia watu kupata njia ya dhalula wakati wa mahitaji, ni mlango unaokueepusha na kifo, ni mlango wa wokovu, ni mlango wa kuzuia taharuki, ni mlango unaotoa urahisi na msaada wa haraka wakati wanadamu wanapokuwa wamechanganyikiwa kwa sababu ya vita, ni mlango wa kutorokea wakati umezingirwa na adui pande zote, ni mlango wa kukimbilia wakati wa tetemeko, ajali ya moto na changamoto nyinginezo, ni mlango ambao mafundi huutengeneza maalumu ukiwa na uhakika wa kutoa usalama kwa watumiaji wa majengo, magari, treni, ndege na uvamizi wa ikulu au majengo makubwa ya watu muhimu, na majengo ya serikalini, mlango huo huwekewa alama za mtu anayekimbia na maneno makubwa EXIT kunyesha eneo la kutokea kukiwa na dharula, wakaguzi wa majengo na wathibiti ubora wakikuta hakuna alama hizo au aina ya ujenzi unaotoa mlango wa kutokea wanaweza kugoma kutoa kibali cha usalama wa jengo au chombo husika, sasa basi ikiwa wajenzi hawa wa kawaida wanaweza kukumbuka kuweka mlango wa dharula katika majengo yao ya kawaida Paulo anatuambia kuwa Mungu naye katika hekima yake akiwa ni Mjenzi Mkuu Mwenye hekima na akili ya hali ya juu anajua kuwa bila kutuwekea njia ya dharula na njia ya kutokea wakati wa changamoto tunaweza tukaelemewa na changamoto hizo na zikatutoa katika mapenzi yake kwa hiyo ni ukweli ulio wazi kabisa kuwa kwa kila jaribu Mungu atafanya na mlango wa kutokea! Escaping way or door Haleluya!

Isaya 43:19-21 “Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani. Wanyama wa kondeni wataniheshimu, mbweha pia na mbuni; kwa sababu nimewapa maji jangwani, na mito nyikani, ili kuwanywesha watu wangu, wateule wangu; watu wale niliojiumbia nafsi yangu, ili wazitangaze sifa zangu.”

Mlango wa kutokea ni uweza wa Mungu wa kukufanya ushinde kikwazo chochote na kuleta suluhu wakati mazingira yanayokuzunguka yanaonyesha kuwa haiwezekani, Mungu wetu ni mwenye uwezo wa kufanya njia hata jangwani yaani mahali ambapo haiwezekani kufanya njia, Neno la Mungu linaposema atafanya njia jangwani kama unalifahamu jangwa vizuri huwa linakuwa na michanga na upepo mkali na kwa sababu hiyo sio rahisi kuona njia jangwani kwa hiyo Mungu wetu hufanya njia pasipo na njia, wakati mtu anapohitaji msaada wa karibu na ikaonekana kuwa ni ngumu msaada huo kupatikana yeye kwa uwezo wake analeta msaada huo na kwa sababu hiyo kwa kila jaribu Mungu hufanya njia, Mungu kamwe hawezi kufungwa na mipaka ya kibinadamu na ya kimazingira na ana uwezo mkubwa wa kuingilia kati kimuujiza na kukuwezesha kushinda mwamini yeye tu atafungua mlango huo kama alivyowafanyia wengine, kwa kila jaribu lako unalolipitia Mungu atafanya  mlango wa kutokea:-

-          Alifanya mlango wa kutokea kwaajili ya Ishamel na Hajiri walipokuwa wanakabiliwa na njaa na kiu alisababisha kisima cha maji kikatokea na Ishmael na Hajiri wakawa na uhai na maisha yao yakaendelea wakati ambapo Hajiri alikuwa akikitazamia kifo cha mtoto naye ye mwenyewe, Mungu alimtuma malaika wake na wakamfunulia jambo la kufanya!

 

Mwanzo 21:15-21 “Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde. Akakaa katika jangwa la Parani; mama yake akamtwalia mke katika nchi ya Misri.”

 

-          Alifanya mlango kwaajili ya wana wa Israel kwa kuifanya bahari ya Shamu kugawanyika kisha Israel wote wakapita kwa uweza mkubwa, ingawa walikuwa wako katika kufungwa utumwani na kuzingirwa na maadui na kuwa katika wakati Mgumu walipoogopa na kulia kwa kukosa matumaini yeye alifungua mlango ambao haujawahi kutarajiwa duniani!

 

Kutoka 14:8-18 “Na BWANA akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri. Wamisri wakafuata nyuma yao, farasi zote na magari yote ya Farao, na askari zake wenye kupanda farasi, na jeshi lake, nao wakawapata hali wamepanga pale karibu na bahari, karibu na Pi-hahirothi, kukabili Baal-sefoni. Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia BWANA. Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri? Neno hili silo tulilokuambia huko Misri, tukisema, Tuache tuwatumikie Wamisri? Maana ni afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani. Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya. BWANA akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele. Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu. Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa magari yake na kwa wapanda farasi wake. Na Wamisri watajua ya kuwa Mimi ndimi BWANA, nitakapokwisha kujipatia utukufu kwa Farao, na magari yake, na farasi zake.”               

 

-          Alifanya mlango wa kutokea kwa Samsoni ambaye alipokuwa anazimia kwaajili ya kiu na hakuwa na msaada Mungu akatokeza maji kutoka katika mwamba na roho yake ikaburudika, mtu ambaye alikuwa afe kwa kiu lakini alipomuomba Mungu alipewa ufumbuzi, Mungu aipasua mwamba na kumpa Samsoni maji a kunywa na roho yake ikaburudika

 

Waamuzi 15:18-20 “Kisha akaona kiu sana, akamwita Bwana akasema, Wewe umetupa wokovu huu kwa mkono wa mtumishi wako; na sasa nitakufa kwa kiu, na kuanguka katika mikono ya watu wasiotahiriwa. Lakini Mungu akapasua mahali penye shimo palipo katika Lehi, pakatoka maji; naye alipokwisha kunywa, roho yake ikamrudia, akaburudika; kwa hiyo jina la mahali pale likaitwa Enhakore, napo pa katika Lehi hata hivi leo.Naye akawa mwamuzi wa Israeli: katika siku za Wafilisti muda wa miaka ishirini.”

 

-          Alifungua Mlango kwaajili ya Petro aliyekuwa gerezani na akitarajiwa kuuawa na Herode kama tu alivyouawa mtume mwenzake siku zilizopita, Kanisa waliomba kwaajili yake Jaribu lilionekana kama halina suluhu lakini Mungu ni mwaminifu alifanya mlango wa kutokea

 

Matendo 12:1-11 “Panapo majira yale yale Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa. Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga. Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi akaendelea akamshika na Petro. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa. Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu. Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa analala katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza. Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi. Malaika akamwambia, Jifunge, kavae viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate. Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono. Na walipopita lindo la kwanza na la pili, wakaja hata mlango wa chuma wa kuingilia mjini, ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha. Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi.”

Kwa msingi huo bila kujali ni hali gani unaipitia, ni changamoto gani uliyo nayo, ni mtihani gani unatokea katika maisha yako, Kumbuka na kuelewa kuwa Mungu ni zaidi ya wajenzi na waundaji wa vitu mbalimbali; kama wanadamu wa kawaida tu wanaweza kukumbuka kuweka mlango wa ufumbuzi wa mambo basi kumbuka Mungu ni zaidi yao kwa hiyo kwa kila jaribu ameweka au ataweka na mlango wa kutokea, Bwana atakutoa katika majaribu yako, atakuokoa na changamoto zinazokukabili, atakuokoa na umasikini, atatokeza njia katika huzuni zako, atakutoa katika upweke wako, atafungua mlango wa ajira kwako, atatokeza mlango wa ndoa, ataokeza mlango wa uzazi Bwana ataweka mlango wa kutoka katika madeni, ataweka mlango wa kutoka katika maumivu yako kila jambo linalokusibu Bwana ana njia na ana mlango kwaajili ya hilo hatupaswi kuzitumainia akili zetu wenyewe bali tunapaswa kumtumainia Mungu kwani yeye atanyoosha mapito yetu yote maana yake atatutengenezea njia, kila linapokukuta jambo gumu usisite kuliitia jina la Mungu kwa msaada!

Mithali 3:5-6 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.”

Zaburi 34:17-19 “Walilia, naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.”

Mlango wa kutokea

Kimsingi Yesu Kristo anahusika moja kwa moja kama mlango wa kutokea, tunaweza kusema kuwa yeye ndiye MLANGO WA KUTOKEA kunapotokea changamoto za aina yeyote yeye ni mlango, yeye ni njia na yeye ndiye wa kutazamwa katika maisha yetu linapotokea jambo lolote lililo gumu, Mungu amemtoa Yesu Kristo kwetu kuwa mlango, kuwa njia na kuwa wa kutazamwa kama mlango wa kutokea, kila mtu na kila mwanadamu anapokabiliwa na lolote lile na changamoto yoyote ile tunaye Yesu Kristo ambaye ndiye  mlango wa kutokea.

Yohana 10:7-9 “Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. Wote walionitangulia ni wevi na wanyang'anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho.”

Yohana 14: 6 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.”

Yohana 3:14-16 “Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye. Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”

Mungu mwenye upendo mkubwa sana kwa wanadamu hajatuacha tu hivi hivi ili eti tuelemewe na majaribu ya aina mbalimbali mpaka tushindwe yeye ni mwaminifu kwetu na huliangalia neno lake apate kulitimiza, hangeweza na hataweza kutuacha bila ya msaada kwa sababu hiyo unapopita majaribuni kumbuka Mungu ameweka Mlango wa kutokea ni wajibu wetu sisi kuutumia mlango huo pale tunapochanganyikiwa na kujikuta wenyewe, kama tusio na msaada, au wenye kusongwa na mawazo na kufikiri kuwa tutafanyaje, kumbuka kuliitia jina la Bwana kwani kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa, Yesu ndiye Mlango wa kutokea, umebanwa kokote kule, una changamoto yoyote ile, unakabiliwa na mambo magumu yoyote yale changamka na kukumbuka kuwa uko Mlango wa kutokea kwaajili ya wokovu wako Mlango huo ni Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai!

1Wakorintho 10:13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.”

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote.

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumatatu, 4 Agosti 2025

Mungu anapoonekana kuwa mbali!


Zaburi 34:18-19 “Walilia, naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.”




Utangulizi:

Wengi wetu tunapokuwa tunapita katika nyakati ngumu za majaribu ya aina mbalimbali, huwa tunakumbwa na mawazo ya kufikiria kuwa huenda Mungu yuko mbali sana, na wako watu wengine duniani hufikiri kuwa haiwezekani kabisa kuwa na ukaribu na Mungu wala hatuwezi kamwe kuwa na ushirika na yeye, na kwa bahati mbaya hata unapokosea watu wengine hufikiri kuwa Mungu hawezi kuwa karibu na wewe na wanadhani Mungu atakuwa amekuacha, Kila mwanadamu aliyeumbwa na Mungu,Mungu huwa karibu naye lakini zaidi sana aaminiye na wale waliovunjika moyo! au wanaojinyenyekeza.


·         Mungu anapoonekana kuwa mbali!

·         Mungu si Mungu aliye mbali

·         Jinsi ya kuwa karibu na Mungu


Mungu anapoonekana kuwa mbali!

Hisia za kuhisi kuwa Mungu yuko mbali zinaweza kuchangiwa na sababu mbalimbali katika maisha ya mwanadamu, wakati mwingine kwa sababu ya mapungufu ya kibinadamu tuliyonayo, Upweke, na changamoto mbalimbali katika maisha zinapokuwa zimetusonga mioyo yetu na hisia zetu huhisi kuachwa na kufikiri kuwa Mungu yuko mbali na wakati mwingine kwa sababu ya kushuka kwa Imani zetu na tafasiri zetu za kimazingira, tunapolemewa na mawazo, mashaka, hofu na kukosa usalama tunaanza kufikiri kuwa Mungu yuko mbali nasi au ametuacha, na wakati mwingine kudhani kuwa wala hajibu maombi yetu pale anapochelewa kutoa msaada, ndani yetu kuna kilio mbona umeniacha

Zaburi 22:1-11 “Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu? Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu Na wakati wa usiku lakini sipati raha. Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli. Baba zetu walikutumaini Wewe, Walitumaini, na Wewe ukawaokoa. Walikulilia Wewe wakaokoka, Walikutumaini wasiaibike. Lakini mimi ni mdudu wala si mtu, Laumu ya wanadamu na mzaha wa watu. Wote wanionao hunicheka sana, Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao; Husema, Umtegemee Bwana; na amponye; Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye.Naam, Wewe ndiwe uliyenitoa tumboni, Ulinitumainisha matitini mwa mama yangu. Kwako nalitupwa tangu tumboni, Toka tumboni mwa mamangu ndiwe Mungu wangu. Usiwe mbali nami maana taabu i karibu, Kwa maana hakuna msaidizi.”

Zaburi 10:1-2 “Ee Bwana, kwa nini wasimama mbali? Kwani kujificha nyakati za shida? Kwa kiburi chake asiye haki mnyonge anafuatiwa kwa ukali; Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza.”

Mungu huonekana kuwa mbali tunapougua na akachelewa kuleta uponyaji, huonekana kuwa mbali tunapolia na akachelewa kuleta msaada, anaonekana kuwa mbali tunapopatwa na aibu ambayo yeye angeweza kuizuia, anaonekana kuwa mbali wakati adui zetu wanapofurahi na kutucheka ilihali yeye yupo, anaonekana kuwa mbali tunaposhutumiwa kwaajili ya uhusiano wetu na Yeye na Yeye haonyeshi nguvu zake upesi, anaonekana kuwa mbali wakati tuna shida na haonekani kufanya kitu au anapochelewa kufanya jambo kwa wakati wa moyo wa kibinadamu unapotamani kufanyiwa ni kawaida tu ya kibinadamu, kiroho na kisaikolojia kufikiria kuwa Mungu amemuacha kwa sababu wakati mwingine tunahitaji msaada wa haraka kisha yeye akaonekana kuwa amechelewa!

Yohana 11:1-6 “Basi mtu mmoja alikuwa hawezi, Lazaro wa Bethania, mwenyeji wa mji wa Mariamu na Martha, dada yake. Ndiye Mariamu yule aliyempaka Bwana marhamu, akamfuta miguu kwa nywele zake, ambaye Lazaro nduguye alikuwa hawezi. Basi wale maumbu wakatuma ujumbe kwake wakisema, Bwana, yeye umpendaye hawezi. Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo. Naye Yesu alimpenda Martha na umbu lake na Lazaro.Basi aliposikia ya kwamba hawezi, alikaa bado siku mbili pale pale alipokuwapo.”

Yesu alipewa taarifa mapema kwamba rafiki yako umpendaye hawezi yaani anaumwa sana Lakini hata hivyo Yesu hakufanya haraka kwenda maandiko yanaonyesha aliendelea kukaa siku mbili zaidi akiendelea na shughuli zake, hii iliwaletea fadhaa sana Martha na Mariamu, kwani walidhani kuwa kama Yesu angewahi hali isingelikuwa mbaya kiasi kile lakini Yesu alionekana kuchelewa, huwa unajisikiaje Mungu anapokawia kujibu maombi yako, unajisikiaje anapokawia kushughulika na yale yanayokusibu, au pale anapoonekana kana kwamba hashughulikii lolote huonekana kana kwamba alikuwa mbali hapo moyo wa mwanadamu husikitika na kuona kama kwamba Mungu yuko mbali!

Yohana 11:20-26 “Basi Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alikwenda kumlaki; na Mariamu alikuwa akikaa nyumbani. Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yo yote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa. Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka. Martha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho. Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?

Mungu alionekana kuwa mbali na familia ya Matha na Mariamu hata pamoja na kuwa ilikuwa ni familia ambayo Yesu alikuwa anawapenda sana, na ni ukweli ulio wazi kuwa kulikuwa na sauti ya lawama kutoka kwa Martha kuwa kama ungelikuwepo hapa ndugu yangu hangalikufa, yaani Yesu hakuwa karibu na kwa sababu alikuwa mbali amechelewa kujihusisha na taabu ya familia hii, huu ndio mtazamo wetu, wengi wetu pale Mungu anapoonekana kuchelewa kutoa mrejesho wa kile tunachokitarajia kutoka kwake, Mungu huonekana kuwa mbali. Lakini Mungu si Mungu aliye mbali!

Mungu si Mungu aliye mbali.

Neno la Mungu linazungumza kinyume na hisia zetu, lenyewe tofauti na mawazo yetu linakanusha kuwa yeye hayuko mbali na Mungu anajitambulisha katika neno lake kuwa ni Mungu aliye karibu:-

Yeremia 23:23-24 “Mimi ni Mungu aliye karibu, asema Bwana, mimi si Mungu aliye mbali. Je, mtu ye yote aweza kujificha mahali pa siri, nisimwone? Asema Bwana. Je! Mbingu na nchi hazikujawa nami? Asema Bwana.”          

Mungu anaweza kufikiwa na mtu yeyote na wakati wowote anaweza kuona hata yale tunayoyawaza kwa siri na kufikiri mioyoni mwetu yeye ni Mungu ambaye yuko mahali kote kwa wakati mmoja  na anaweza kuonekana na kupatikana kwa yeyote yule na anasikia, tunajua tu kuwa hatuwezi kumpangia kile tunachotaka hatuwezi kuingilia mapenzi yake lakini tunaweza kuliitia jina lake na akasikia na kujidhihirisha katika maisha yetu.

Zaburi 145:17-19 “Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote, Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote. Bwana yu karibu na wote wamwitao, Wote wamwitao kwa uaminifu. Atawafanyia wamchao matakwa yao, Naye atakisikia kilio chao na kuwaokoa.”

Mungu ameahidi katika neno lake katika torati ya kuwa hatatuacha atakuwa pamoja nasi na hatatuacha kamwe kwa sababu hiyo hatupaswi kuogopa lolote wala hatupaswi kuacha kumuamini

Kumbukumbu 31:6 “Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha.”

Mungu amehahidi katika neno lake kutoka kwa manabii ya kuwa tusigope yeye ni Mungu wetu na kuwa atatutia nguvu na kutusaidia na kutushika kwa mkono wake wa kuume, hivyo tusifadhaike katu

Isaya 41:10-13 “usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi, Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia.”

Mungu wakati wote anatamani kuingilia kati mfumo wa maisha yetu pale tunaposumbuliwa na yuko tayari kutoa msaada, faraja nguvu, muongozo, uponyaji na hata kuingilia kati kama kuna vita na kukulipia kisasi unachopaswa wewe ni kumkaribia yeye na kuwa na agano naye kupitia mwanaye Yesu Kristo!

Yakobo 4:7-10 “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za Bwana, naye atawakuza.”

Jinsi ya kuwa karibu na Mungu

Neno la Mungu sio tu linatujulisha na kutuhimiza kuwa Mungu ni Mungu aliye karibu lakini vile vile linatufundisha namna ya kumkaribia Bwana Mungu wetu kwa sababu hiyo pale tunapjisikia na kudhani kuwa Mungu ametuacha yako mambo ya kufanya ili tuweze kumkaribia naye yuko tayari kwaajili yetu!

-          Tubia maovu na kuachana na dhambi – Isaya 59:1-2 “Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.”

 

-          Mwamini Yesu aliye kuhani mkuu – Kazi ya kuhani mkuu ni kuomba kwaajili ya makosa ya watu wake kwa sababu hiyo kabla hata hujaanza kufanya lolote Yesu hutuombea kwa baba na kwa sababu hiyo tunayo haki kwa damu yake kumwendea baba kwa ujasiri

 

Waebrania 10:19-23 “Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake; na kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu; na tukaribie wenye moyo wa kweli, kwa utimilifu wa imani, hali tumenyunyiziwa mioyo tuache dhamiri mbaya, tumeoshwa miili kwa maji safi. Na mlishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu;”

 

1Yohana 2:1-2 “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.”

 

-          Mungu anataka tumrudie yeye – Ni maagizo ya neno la Mungu na wito wa Mungu mwenyewe kwamba tumrudie yeye, na tunapofanya hivyo yeye naye anaturudia sisi, hii ni sawa tu na kusema Mungunanataka tumkaribie Yeye na Yeye atatukaribia sisi na ameonyesha ni kwa namna gani tunaweza kumkaribia au kumrudia

 

Zekaria 1:3-4 “Basi, uwaambie, Bwana wa majeshi asema hivi, Nirudieni mimi, asema Bwana wa majeshi, nami nitawarudia ninyi, asema Bwana wa majeshi. Msiwe ninyi kama baba zenu, ambao manabii wa zamani waliwalilia, wakisema, Bwana wa majeshi asema hivi, Rudini sasa, na kuziacha njia zenu mbovu, na matendo yenu maovu; lakini hawakusikia, wala kunisikiliza, asema Bwana.”

 

Yoel 2:12-14 “Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya. N'nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa Bwana, Mungu wenu?                      

 

Kama ulikuwa na hisia ya kuwa Mungu yuko mbali, Neno la Mungu linakukumbusha kuwa Mungu ni Mungu aliye karibu na hayuko mbali na ni Mungu ambaye anajishughulisha sana na mambo yetu, sio tu kuwa Mungu yuko Karibu lakini kwa wale waliomwamini Yesu na kumkubali kuwa Bwana na mwokozi katika maisha yao wafahamu kuwa anaishi ndani yetu na neno la Mungu linasema kuwa ametupa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu kwa sababu hiyo kama yeye alivyo ndivyo na sisi tulivyo hapa ulimwenguni

1Yohana 3:1-3 “Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo. Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu.”

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Jumapili, 27 Julai 2025

Mungu anaposhika Kalamu!

 

Esta 3:8-11 “Basi Hamani akamwambia mfalme Ahasuero, Kuna taifa moja waliotawanyika na kukaa mahali mahali katikati ya mataifa walioko katika majimbo yote ya ufalme wako. Nao sheria zao zimefarakana na sheria za kila taifa; wala hawazishiki amri za mfalme; kwa hiyo haimpasi mfalme kuchukuliana nao. Basi, mfalme akiona vema, na iandikwe kwamba waangamizwe; nami nitalipa talanta kumi elfu za fedha mikononi mwao watakaosimamia shughuli hiyo, waziweke katika hazina ya mfalme. Ndipo mfalme alipoivua pete yake mkononi, akampa Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi. Kisha mfalme akamwambia Hamani, Hiyo fedha umepewa, na watu pia, fanya uonavyo vema.”

 


Utangulizi:

Mungu anaposhika kalamu ni usemi wa fumbo (Metaphor)  unaotumika kuelezea uwezo na utendaji wa Mungu katika kuamua mambo ya kitaifa, ulimwengu au mtu mmoja mmoja kuhusiana na mpango wake wa baadaye, Mungu ndiye mshika dau wa maisha ya kila mtu na anayeujua mwanzo na mwisho wa mtu au anayeamua kuwa hatima ya mtu itakuwaje, uweza wake huo hauwezi kuingiliwa wala kuathiriwa na mpango wowote wa kibinadamu wala Shetani, wakati wote yeye ndiye hubakia kuwa mwenye hatima ya mwisho wa kila mtu, familia, taifa na ulimwengu!, Hakuna mwanadamu, wala serikali wala ufalme wala mamlaka yenye uwezo wa kuamua hatima yako itakuwaje isipokuwa Mungu peke yake! Ni yeye peke yake ndiye anayetuwazia mema kwa sababu yeye ndiye aliye tuumba na kwa sababu hiyo anajua hatima yetu na sababu ya yeye kutuumba! Ameandika kila kitu kutuhusu hakuna wa kufuta.

Yeremia 29:11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.”

Kwa bahati mbaya wako watu duniani ambao hufiriki ya kuwa wao wanaweza kuamua hatima ya maisha yako au maisha yetu au kwamba hatima ya taifa letu iko mikononi mwao, na kwa sababu hiyo kwa kutumia nafasi waliyo nayo wakati mwingine wameweza kuingilia na kujaribu kuzuia au kuwakwamisha watu wengine katika mpango wa Mungu wakidhani kwa mawazo mafupi kuwa wao wanaweza kufanya hivyo, Lakini hatimaye Mungu huingilia kati na kubadilisha mambo ni mpango wake peke yake unaoweza kuhitimisha mambo kinyume na matarajio na mipango ya wanadamu ni wazo lake na shauri lake na kusudi lake pekee linaloweza kusimama.

Zaburi 33:8-11 “Nchi yote na imwogope Bwana, Wote wakaao duniani na wamche. Maana Yeye alisema, ikawa; Na Yeye aliamuru, ikasimama. Bwana huyabatilisha mashauri ya mataifa, Huyatangua makusudi ya watu. Shauri la Bwana lasimama milele, Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi.”

Leo basi tutachukua muda mfupi, kujifunza kwa kina na mapana ujumbe huu wa muhimu “Mungu anaposhika kalamu”na tutajifunza ujumbe huu kwa kuzingatia vipengele viwili muhimu vifuatavyo:-

·         Njama za kuharibiwa kwa hatima yako.

·         Mungu anaposhika kalamu.


Njama za kuharibiwa kwa hatima yako

Katika dunia hii iliyojaa iliyojawa na watu wenye chuki, uadui, uchawi, wivu, hasira, faraka uzushi, husuda, ulafi, tamaa mbaya, chuki zisizo hata na sababu majungu na fitina, kuharibiana na kuchafuana, kuwindana na kutafutana watu wanaweza kwa sababu au hata bila sababu kukutafutia namna ya kukutengenezea hatima mbaya, adui zako watatamani wakati wote wasikie unaharibikiwa na mambo yako hayaendi na wakati mwingine watakusudia uwe na hatima mbaya hata kinyume na mapenzi ya Mungu, watatamani kuona ndoto zako, maono yako na matamanio yako uliyopewa na Mungu hayatimii kwa mbinu na hila za kibinadamu, kwa hiyo unaweza kuwekewa mpango mkakati na watu ili wahakikishe ya kuwa mambo yako yanakwama, kama haya yanakukuta hilo sio jambo geni kwako wala kwetu, maandiko yanatutia moyo kuwa tusione kuwa ni ajabu tunapopatwa na changamoto za aina mbalimbali

1Petro 4:12-13 “Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho. Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.”

Nyakati za Biblia walikuweko watu kama wewe na wanadamu kama wewe waliokutana na changamoto kama zako watu wakiwakusudia kuwakwamisha kwaajili ya maslahi yao au kwa sababu ya husuda ya kitu cha kiungu ambacho Mungu amekiweka ndani yako:-

1.       Yusufu – Mungu alimpa ndoto kubwa za maisha yake ya baadae,  na ya nduguze lakini sio hivyo tu alipata kibali kwa Mungu na kwa baba yake, Mungu alimpenda Yusufu na alikuwa pamoja naye, lakini pia baba yake alimpenda sana na Mungu alimpa Yusufu ndoto kuhusu hatima yake lakini hata hivyo nduguze walichukizwa na ndoto hizo na kuanza kula njama ya kutaka kumuangamiza.

 

Mwanzo 37:2-11 “Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye alikuwa kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akamletea baba yao habari zao mbaya. Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani. Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi? Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili.”

 

Ni jambo la kushangaza kwamba Yusufu alichukiwa na ndugu zake na sio kumchukia tu walimuhusudu walikuwa na wivu wenye uchungu mkubwa dhidi yake na kwa sababu ya ndoto zake walihakikisha wanaweka mkakati wa kummaliza ili waone ndoto zake zitatimiaje yaani walitaka kumuua!

 

Mwanzo 37:13-20 “Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao. Akamwambia, Mimi hapa. Akamwambia, Enenda, basi, ukaone kama ndugu zako hawajambo, na kundi nalo li salama, ukaniletee habari. Basi akampeleka kutoka bonde la Hebroni, akafika Shekemu. Mtu mmoja akamkuta, naye alikuwa anazunguka-zunguka katika nyika; yule mtu akamwuliza, akisema, Unatafuta nini? Akasema, Nawatafuta ndugu zangu; tafadhali uniambie mahali wanakochunga. Yule mtu akasema, Wametoka hapa, maana niliwasikia wakisema, Twendeni Dothani. Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani. Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake.”

 

Wanadamu bila kufahamu kuwa Mungu alikwisha kumuandikia mtumishi wake Yusufu kuwa atakuwa mkuu, wao walikuwa wakijaribu kuandika kinyume na kile ambacho Mungu alikuwa amekikusudia kwa Yusufu, ndugu yangu hayo unayoyapitia ni kuwa wanadamu wanataka kujaribu kuandika hitoria yako kinyume na kile ambacho Mungu amekikusudia katika maisha yako!

 

2.       Daniel – Alifanyiwa njama na Mawaziri wenzake  baada ya kuwa ameinuliwa sana na Mungu na kupata kibali kwa mfalme ambaye aliamua kumuweka juu sana katika madaraka ya nchi ya uhamishoni, Mawaziri wa kikaldayo walikuwa na mpango wa kuharibu hatima ya Daniel na kwa kuwa alikuwa na uadilifu walikosa sababu, wakaona watumie njama ya kuzuia maombi kwa Mungu aliye hai, jambo ambalo lingesababisha Daniel ashindwe na kupata sababu ya kumhukumu kwa hiyo mawaziri waliandika mswada na kuupitisha

 

Daniel 6:1-16 “Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote; na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara. Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote. Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake. Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake. Basi wale mawaziri na maamiri wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia hivi, Mfalme Dario, uishi milele. Mawaziri wote wa ufalme, na manaibu, na maamiri, na madiwani, na maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga marufuku, ya kwamba mtu ye yote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba. Sasa, Ee mfalme, piga marufuku, ukatie sahihi maandiko haya, yasibadilike, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza kubadilika. Basi mfalme Dario akayatia sahihi maandiko yale, na ile marufuku. Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo. Basi watu hao wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake. Ndipo wakakaribia, wakasema mbele ya mfalme katika habari ya ile marufuku ya mfalme; Je! Hukuitia sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba? Mfalme akajibu, akasema, Neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza kubadilika. Basi wakajibu, wakasema mbele ya mfalme, Yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku. Basi mfalme aliposikia maneno haya alikasirika sana, akakaza moyo wake ili kumponya Danieli; akajitaabisha kumwokoa hata jua likachwa. Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia mfalme, Ee mfalme, ujue ya kuwa ni sheria ya Wamedi na Waajemi, lisibadilike neno lo lote lililo marufuku, wala amri yo yote iliyowekwa na mfalme. Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya.”

 

3.       Wayahudi waliokuwa uhamishoni – Mungu alikuwa amewabarikia sana wayahudi waliokuwa utumwani, wao walikuwa na moyo ule ule wa kumcha Mungu wakiwa wamejifunza kwamba kupitia kuabudu miungu mingine wao walihukumiwa kwenda utumwani kwa hiyo wayahudi waliokuwa uhamishoni hawakutaka kuabudu sanamu wala mtu waliipeleka heshima yote kwa Mungu, Kwa sababu hiyo Hamani ambaye alikuwa amemchukia Modrekai kwa sababu alikuwa hainami mbele zake aliamua kupitisha mswada bungeni ili kwamba ipitishwe sheria ya kuwaangamiza wayahudi wote na hivyo waliandika mswada wa maangamizi

 

Esta 3:8-11 “Basi Hamani akamwambia mfalme Ahasuero, Kuna taifa moja waliotawanyika na kukaa mahali mahali katikati ya mataifa walioko katika majimbo yote ya ufalme wako. Nao sheria zao zimefarakana na sheria za kila taifa; wala hawazishiki amri za mfalme; kwa hiyo haimpasi mfalme kuchukuliana nao. Basi, mfalme akiona vema, na iandikwe kwamba waangamizwe; nami nitalipa talanta kumi elfu za fedha mikononi mwao watakaosimamia shughuli hiyo, waziweke katika hazina ya mfalme. Ndipo mfalme alipoivua pete yake mkononi, akampa Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi. Kisha mfalme akamwambia Hamani, Hiyo fedha umepewa, na watu pia, fanya uonavyo vema.”

 

Hata hivyo katika namna isiyoweze kuelezeka sheraia za waamedi na waajemi zilikuwa zikipitishwa haikuwa kitu rahisi kubatilisha isipokuwa tu kama Mungu ataingilia kati kwani sharia zao zikipita zimepita

 

Esta 8:8 “Basi waandikieni Wayahudi pia vyo vyote mpendavyo, kwa jina la mfalme, mkatie muhuri kwa pete ya mfalme; kwa kuwa andiko lililoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa muhuri kwa pete ya mfalme hakuna awezaye kulitangua.”

 

4.       Yesu Kristo – Ambaye alishitakiwa kwa husuda na wakuu wa makuhani ili tu kumsambaratisha na wakidhani kwa kufanya hizo njama watakuwa wamemmaliza kabisa, aliandikiwa hati ya hukumu ya kufa msalabani

 

Mathayo 27:17-20 “Basi walipokutanika, Pilato akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo? Kwa maana alijua ya kuwa wamemtoa kwa husuda. Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto kwa ajili yake. Nao wakuu wa makuhani na wazee wakawashawishi makutano ili wamtake Baraba, na kumwangamiza Yesu.”

 

Wakati mwingine adui zako watafanya njama na kukushambulia kwa hila na njia mbalimbali ilimradi tu wahakikishe kuwa wanakupoteza au wanaharibu hatima yako kama tunavyoona katika mifano hiyo hapo juu katika maandiko, ndugu msomaji wangu na msikilizaji wangu inawezekana kuwa mara kadhaa na wewe unaweza kuwa umekutana na changamoto za aina mbalimbali ambazo zote zinalenga kumaliza au kuharibu hatima yako au hata kukuua kwa makusudi yale yale ya kuua kitu cha kiungu ambacho kimewekwa ndani yako! Lakini hata hivyo uzoefu wa kimaandiko unaonyesha ya kuwa Mungu huingilia kati na kubadilisha mambo pale anaposhika kalamu yake. Mungu huwaacha wanadamu waandike miswada yao kisha yeye kama mfalme wa wafalme huitangua, Mungu anaposhika kalamu historia yote na matarajio yote ya adui hubatilika

Mungu anaposhika kalamu.

Mungu anaposhika kalamu maana yake Mungu anauwezo wa kubadili historia ya mambo, wanadamu na shetani wanapokusudia kuharibu na kusitisha kile kitu ambacho Mungu amekiweka ndani yako au kuharibu hatima yako na kukupakazia ubaya au kukukusudia ubaya Mungu anauwezo wa kubadili historia ya mambo mabaya na kuigeuza kujwa njema, au uwezo wa kubadili maji machungu kuwa matamu, anauwezo wa kuandika upya hatima yako ya familia yako na taifa lako na hata ulimwengu kwa ujumla, Mungu anauwezo wa kurejesha heshima ambayo imeharibiwa, ana uwezo wa kuharibu mipango mibaya ya adui na kuifanya kuwa myema au kupitia mpango huo mbaya akatokeza jambo jema kwa uwezo wake mkuu na kwa mkono wake wa nguvu ulionyooshwa

Warumi 8:28-30 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.”

Yusufu aliyefanyiwa njama na kaka zake ili kwamba ndoto zake zisitimie Mungu aliitumia njia iiliyoonekana kuwa ya uchungu na ya kuumiza kuleta wokovu kwa taifa zima, Mungu alibadili hatima mbaya iliyokusudiwa na wanadamu kutimiza hatima yeke iliyokusudiwa na yeye Mungu anaposhika kalamu mambo hubadilika.  

Mwanzo 50:15-20 “Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; naye atatulipa maovu yetu tuliyomtenda.  Wakapeleka watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema, Mwambieni Yusufu hivi, Naomba uwaachilie ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utuachilie kosa la watumwa wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia waliposema naye. Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumwa wako. Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu? Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo.”

Mungu aliingilia kati maswala ya Daniel ambaye alishitakiwa kwa hila na Mungu aliona wazi kuwa hakuwa na hatia na mfalme akabadili mawazo kwa kumtoa Daniel katika tundu la simba na kuwaingiza washitaki wake na familia zao Ni kitu gani kilitokea Mungu alposhika kalamu makanwa ya simba hayakumuweza Daniel na badala yake adui zake walishughulikiwa!

Daniel 6:21-27. “Ndipo Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele. Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno. Basi mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danieli katika lile tundu. Ndipo Danieli akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake, kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake. Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danieli, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu. Ndipo mfalme Dario akawaandikia watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, waliokaa juu ya uso wa dunia; Amani na iongezeke kwenu. Mimi naweka amri, ya kwamba katika mamlaka yote ya ufalme wangu watu watetemeke na kuogopa mbele za Mungu wa Danieli; maana yeye ndiye Mungu aliye hai, adumuye milele, na ufalme wake ni ufalme usioharibika, na mamlaka yake itadumu hata mwisho. Yeye huponya na kuokoa, hutenda ishara na maajabu mbinguni na duniani, ndiye aliyemponya Danieli na nguvu za simba.”

Mungu alishika kalamu na kuondoa mashitaka dhidi ya wayahudi waliokuwa uhamishoni na wakapewa mamlaka ya kujilinda na kuwafanyia lolote adui zao, ingawa tunaona kuwa Hamani alikuwa na mpango mbaya lakini Mungu alibadili mpango huo na hata msalaba ambao Hamani alikuwa amemuandalia Mordekai ukweli ni kuwa alisulubiwa yeye

Esta 8:7-11 “Mfalme Ahasuero akawaambia malkia Esta na Mordekai, Myahudi, kusema, Tazama, nimekwisha kumpa Esta nyumba yake Hamani, naye mwenyewe wamekwisha kumtundika juu ya mti, kwa sababu aliwatia mikono Wayahudi. Basi waandikieni Wayahudi pia vyo vyote mpendavyo, kwa jina la mfalme, mkatie muhuri kwa pete ya mfalme; kwa kuwa andiko lililoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa muhuri kwa pete ya mfalme hakuna awezaye kulitangua. Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa pale pale, siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa tatu, ndio mwezi wa Siwani; na kama vile Mordekai alivyoamuru, Wayahudi wakaandikiwa, pamoja na maakida na maliwali, na wakuu wa majimbo toka Bara Hindi mpaka Kushi, majimbo mia na ishirini na saba, kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; na Wayahudi kwa mwandiko wao na kwa lugha yao. Akaandika kwa jina la mfalme Ahasuero, na kutia muhuri kwa pete ya mfalme, akazipeleka barua kwa matarishi, wamepanda farasi, wamepanda wanyama wepesi sana waliotumika kwa huduma ya mfalme, ndio waliozalishwa katika zizi la mfalme. Katika barua hizo mfalme aliwaruhusu Wayahudi wakusanyike katika kila mji na kuzisimamia maisha zao, kuangamiza, na kuua, na kulifisha jeshi lote la watu na la jimbo watakaowaondokea, wao na wadogo wao na wanawake; na kuyachukua mali yao kuwa nyara;”

Mungu alimfufua Yesu Kristo ambaye wazee walimshulubisha wakidhani ya kuwa wamemaliza hatima yake, walipomuua waliomba kwamba kaburi lake lilindwe na likawekwa na muhuri kuwa lisibadilike neno lolote katika kile ambacho kimeagizwa na askari waliwekwa kulinda lakini Yesu alifufuka siku ya tatu!

Matendo 3:14-18 “Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake. Na kwa imani katika Jina Lake, jina lake limemtia nguvu mtu huyu mnayemwona na kumjua; na imani ile iliyo kwake yeye imempatia huyu uzima huu mkamilifu mbele yenu ninyi nyote. Basi sasa, ndugu, najua ya kuwa mliyatenda haya kwa kutokujua kwenu, kama na wakuu wenu walivyotenda. Lakini mambo yale aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo.”

Mungu yule yule ambaye alibadilisha historia za watau wake hapo juu anauwezo wa kubadilisha historia yako, Mungu anaposhika kalamu anafungua ukurasa mpya katika maisha yako  na kusababisha kitu kipya katika maisha yako kitokee, haijalishi unapitia katika mapito gani, Wanadamu wote walikuwa wameandikiwa kifo na laana ya dhambi lakini kupitia kazi iliyofanywa na Bwana wetu Yesu Kristo pale msalabani Yesu amekuandikia habari mpya , ameifuta ile hati iliyoandikwa ya sheria iliyokuwa na shuhuda zetu na kesi iliyokuwa inatukabili ameigongomelea msalabani isiwepo tena ile hati ya kutuhukumu imefutwa, Mungu anaweza kukufanya kuwa kiumbe kipya leo kama uliandikiwa hukumu hati ya hukumu imefutwa, kama uliandikwa katika kitabu cha hukumu mambo yako ya kale yamepita na yamekuwa mapya leo, haijalishi wanadamu wamekusudia nini leo katika maisha yako nakuletea Yesu Kristo mzima mzima ambaye atayabadilisha maisha yako na kuyafanya upya, wale waliokuzomea na kukuandalia kaburi, wale waliokushitaki na kukuandikia hukumu, Yesu anabadilisha maisha yako anabadili hatima yako, hakuna mwanadamu mwenye hati miliki ya Mungu, Mungu ni wa wote ni Mungu wa wote wenye mwili, na Mungu akiishika kalamu na hubadili maisha yako kabisa na kukupa muelekeo mpya, Mungu anaposhika kalamu ndugu yangu kila kitu kitakuwa kipya tofauti na matarajio yako, Mungu anaposhika kalamu hakuna historia mbovu isiyoweza kubadilishwa, hakuna aliyechelewa sana asiyeweza kusawazishiwa, hakuna aliye na doa kubwa lisiloweza kufutika, hakuna aliyekatwa asiyeweza kuchipuliwa, hakuna aliyeachwa asiyeweza kurejezwa, Muda usingeliweza kutosha kukupa shuhuda za Ayubu ambaye shetani alifilisi kila kitu lakini Mungu aliposhika kalamu, Ayubu akawa tajiri mara mbili zaidi, Muda usingeliweza kutosha kuleta habari za Petro na Paulo na Sila ambao walitiwa gerezani na maadui zao wakitarajia kuwa watakuwa wamewaweza au kuwaweka kizuizini ili yamkini wawaangamize baadaye lakini Mungu aliposhika kalamu hali ilibadilika na mambo yakawa tofauti itakuwa hivyo pia kwako leo, katika maisha yako, katika  ndoa yako,  katika huduma yako, kwaajili ya watoto wako, kabila lako, jamii yako, taifa lako, ukoo wako, biashara zako, masomo yako, tumbo lako la uzazi na kadhalika, Ni swala la Muda tu Mungu anaposhika kalamu kila kitu huwa tofauti, waliosema hutoboi Mungu nanaposhika kalamu wataisoma namba, hakuna jambo lililogumu lisilowezekana kwa Mungu, Hatima yako iko mikononi mwa Mungu, hakuna mchawi, wala mganga wala mzimu, wale pepop, wala shetani. Wala jinni wala mtu yeyote yule anayeweza kukuandikia kinyume na kile Mungu amekiandika leo ni siku yako ya kuwekwa huru, ni siku ambayo Mungu ataweka sawa pale palipoyumba katika maisha yako Haleluyaaaa!

Dua!   

Ee Bwana mtumwa wako ninaomba! Katika jina la Yesu Kristo; nakusihi ushike kalamu sasa na kubadilisha maisha ya kila mmoja wetu na kuandika hatima mpya, andika hatima mpya ya ndugu yangu huyu, andika hatima mpya ya dada yangu huyu, andika hatima mpya ya familia zetu, andika hatima mpya ya huduma zetu, andika hatima mpya ya vizazi vyetu, andika hatima mpya ya taifa letu, andika ee Bwana tofauti na wanadamu walivyoandika, andika ee Bwana kwaajili ya jina lako tafakatifu, andika ee Bwana kupitia neema yako na upendo wako mkubhwa sana na wingi wa rehema zako tafadhali Bwana mwandikie kila mmoja wetu ukurasa mpya wenye kufaa kama ulivyokusudia toka mwanzo  namwombea kila mmoja anayesoma ujumbe huu katika jina la Mwanao Mpendwa Yesu Kristo ameeen!

Na Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!