Andiko: 2Wakoritho 1: 3-7
“3. Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu
Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote”
Utangulizi:
Neno Mungu wa faraja yote
linalojitokeza hapa na sehemu nyingine katika agano jipya limetokana na neno la
asili la kiyunani “Paraklesis”
ambalo maana yake ni wakili au mtetezi au mtu anayesimama karibu na mtuhumiwa
ili kumtetea na kumsaidia,Neno hili limetumiwa mara nyingi sana na Paulo mtume
katika nyaraka zake, na Mwandishi Luka na baadhi ya waandishi n wengine wa
nyaraka na katika waraka wa Waebrania, ambapo neno hilo hujitokeza Mara 12 au kwa maneno yanayofanana na hilo
mara 28
Neno hili ni la muhimu sana kwa
wakristo wanaopitia magumu na mapito ya aina mbalimbali lakini zaidi sana
mapito a taabu zinazotokana na kazi ya injili, ni muhimu sana kufahamu kuwa
maisha ya ukristo yanajumuisha pamoja na kuteseka kwaajili ya Kristo biblia
inasema tumeitwa si kumwamini tu bali kuteseka pamoja na Kristo, lakini hata
pamoja na mateso hayo wakati huu Mungu hujihusisha kwa namna ya kipekee katika
kufariji na hiki ndicho Paulo anakikazia katika kifungu hiki tunachojifunza
leo.
Tutajifunza somo hili kwa
kuzingatia maswala ya msingi yafuatayo:-
·
Ahimidiwe Mungu. Mstari 3
·
Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo Mstari 3
·
Baba wa Rehema Mstari wa 3
·
Mungu wa Faraja yote Mstari wa 3
Ahimidiwe Mungu.
Neno Ahimidiwe Mungu katika
Biblia ya kiingereza ya NIV linasomeka “Praise be to the God” na Biblia ya kiingereza ya
KJV ambaoyo ndiyo iliyotumika kutafasiri Biblia ya Kiswahili ya Union Version
linasomeka katika lugha hiyohiyo ambayo Kiswahili chake kingesomeka “Abarikiwe
Mungu” Hata hivyo Biblia ya kilatili Vulgate inatumia neno “Benedictus” ambalo
kiingereza chake lingesomeka “Heartfelt thanks be to the God” ambalo lingesomeka
kwa Kiswahili rahisi Atukukuzwe au Ashukuriwe
sana Mungu, unaweza kuona vema katika Waefeso 1:3 “Atukuzwe Mungu”
Salamu hizi kwa ujumla zinafunua
moyo wa Paulo mtume ambaye alikuwa amejawa na wingi wa shukurani, na hivyo
anaonyesha kufurahi na kushukuru kwa kiwango cha juu sana kwa Mungu, kwa nini
Paulo anajawa na wingi wa shukurani kiasi hiki kwa Mungu? Paulo alikuwa ni mtu
mwenye mzigo na kazi ya Mungu, alikuwa ni mtume mwenye moyo wa kichungaji,
alikuwa na mambo mengi sana ya kuwaonya na kuwafundisha wakoritho hasa baada ya
kanisa kumuandikia na kumsimulia yale waliokuwa wakiyapitia wakati akiwa
hayupo, na aliwajibu kwa kuandika waraka wa Wakoritho ule wa kwanza sasa
anapata taarifa kuwa Kanisa la Koritho sasa linaendelea vizuri, Paulo mtume
alikuwa amekemea mambo mengi katika waraka wake wa kwanza ambao ulileta huzuni
na toba kwa kanisa la Koritho na waliweza kufanya marekebisho mengi, sasa Paulo
amesikia taarifa kuwa Kanisa linaendelea vema na sasa anafarijika na kufurahi
sana kutokana na maendeleo mazuri ya Kanisa la Koritho, habari za maendeleo
mazuri Paulo alizipata kutoka kwa Tito aliyekuwa akisimamia makanisa ya Akaya
au Macedonia 2Wakoritho 7:8-10,12-16,
Ni kwasababu hii Paulo mtume anamtukuza Mungu, anafurahi anamhimidi Mungu, ni
kama mtu uliyekuwa na mgonjwa kisha ukapewa taarifa kuwa mgojwa huyo sasa
anaendelea vema, au ameruhusiwa, kila mchungaji mwenye mapenzi ya kweli na
kanisa hawezi kufurahi kanisa linapoharibika, hafurahii watu wakienenda katika
njia isiyopasa, lakini watu wanapoendelea vizuri kunakuwa na furaha kubwa sana
hali kadhalika walimu watafurahi kusikia wanafunzi wao wanaendelea vizuri
wanafanya vizuri, madaktari na manesi hawafurahii kuona wagonjwa wakipoteza
maisha wanapenda kuona wagonjwa wanapona
Huu ndio ulikuwa moyo wa Paulo
Mtume anafurahi, anamtukuza Mungu anamhimidi bwana Mungu anamsifu anaonyesha
moyo wa kufurahi, mambo yanapokwenda vema, kila mmoja anapaswa kufurahia
mabadiliko mema ya kila mmoja wetu katika kumpenda Mungu, hatutarajii watu
watasababisha huzuni, kila mmoja ataonyesha ukomavu, maendeleo katika kila Nyanja
ni jambo hilo linaleta faraja kubwa sana, hakuna mama anayefurahia kuwa na
mtoto asiyekua, lakini kila mtoto anapopiga hatua kina mama hushangilia sana
anakaa, anatambaa, anaota meno, anasimama, anatembea anazungumza na hatua
nyinginezo zote huleta faraja kubwa sana kwa kina mama wanaofanya malezi ya
watoto.
Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo Mstari 3
Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo –
Mahali hapa Paulo anamtaja Mungu lakini anaunganisha Mungu Baba wa Bwana wetu
Yesu Kristo, kwa nini ? sababu kubwa ni kuwa hakuna mtu anaweza kuunganishwa na
rehema za Mungu baba pasipokuweko kwa Yesu Kristo, Ni muhimu kufahamu kuwa watu
wengi sana duniani hata wapagani wanafahamu sana Mungu kama Baba wa rehema lakini
tatizo kubwa ni kuwa hawa wanataka kwa vinywa vyao tu hawajui kuwa rehema hizi
za Mungu zimepitia kwa Yesu Kristo, ni kwa mateso ya yesu Kristo tu, ni kwa
kusulubiwa kwake tu ni kwa kuiamini kazi aliyoifanya Yesu Kristo tu ndipo watu
wanaweza kufaidika na rehema za Mungu baba
na upendo wake hakuna njia nyingine, Upendo wa Mungu umeunganishwa kwa
mwana wake wa pekee Yesu Kristo na hakuna namna nyingine, kama tunapitia mateso
katka imani yetu ni kupitiamateso ya Kristo 2Wakoritho 1:5 kama tunafarijika faraja hiyo ni kwaajili ya Yesu
Kristo tu, Pasipo Kristo hatuwezi kufanya neno lolote. Shukurani anazozitoa
Mtume Paulo kwa Mungu baba pia zinaunganishwa na Yesu Kristo yeye pekee ndio
kipatanisho cha kweli kati ya Mungu na wanadamu
Baba wa Rehema Mstari wa 3
Baba wa Rehema – Ni muhimu
kufahamu kuwa Paulo mtume alikuwa Mwebrania na ingawa aliandika waraka huu
kiyunani, ni wazi kuwa alikuwa anawaza kiebrania, katika tamaduni za Kiibrania
neno Baba lilitumika pia kumaanisha MWANZILISHI au chanzo kwa msingi huo
linapotumika hapa linamaanisha Rehema zinatoka kwa Mungu, asili yake ni kutoa
Rehema na ndiye mwenye kuitunza rehema,
Rehema ni sifa kuu ya Mungu,
Ndani ya rehema kuna huruma, neema uvumilivu usioelezeka tunaita Mungu wa
Rehema na neema , mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli Zaburi 86: 15 na ni
kupitia sifa hizo ndio Mungu husaidia na kufariji, Vitabu vya tamaduni za
kiyahudi Talmud vinaeleza kuwa ndiye yeye huanza kwa rehema na kumaliza kwa
rehema, kila sura ya Quran isipokuwa moja tu zinaanza kwa kusema Mungu ni
mwingi wa Rehema, hii ilikuwa ni salamu ya kawaida kwa waru wa mashariki ya
kati kuhusu tabia ya Mungu kwa kiibrania “RACHAMIM”
likimaanisha huruma au rehema Warumi 12:1 ni kutokana na tamaduni hizi na sifa
hii ya kweli ya Mungu ilikuwa ni utaratibu wa kawaida kwa nyakati za kanisa la
kwanza kumtaja Mungu kama Baba wa rehema
Mungu wa Faraja yote Mstari wa 3
Neno hili Mungu wa faraja yote
ndio nenola Muhumu sana key word dhidi ya maneno yote katika kifungu hiki ni
wazi kuwa kutoka mstari wa 3-7 neno faraja limetajwa mara kumi likiunganishwa
na neno Mateso mara nne hivi au dhiki
Mahali hapa panatupa matumaini
yalkiyo wazi kuwa katika dhiki ya aina yoyote na mateso ya aina yoyote kamwe
Mungu hawezi kutuacha wala kujitenga na upendo wake, Paulo ameona katika uzoefu
wake kuwa wakati wote walipopita katika magumu Mungu alikuwa ni faraja , kwa
msingi huo Mungu anafaraja yote, Mungu anaweza kuruhusu sisi kupita katika
mateso na dhiki ili tuweze kuwafunza wenzetu jinsi Mungu alivyo mwema tuwe na
ujasiri wa kuwashuhudia wengine upendo na neema ya Mungu,
Mungu singeliweka faraja zake
tungelikata tamaa, Dunia ni ngumu lakini kwaajili ya faraja zake tumejifunza
kuvumilia kwa kuwa na tumaini Mungu anatufariji kwa Roho wake Mtakatifu, Paulo
anaiona faraja nyingine kuwa ni kuendelea mbele na kukua wa kanisa la Koritho
ambalo alilitaabikia, likaingiliwa na waalimu wa uongo, likaonyesha dalili
mbaya akakemea ingawa alitumia waraka wake wa kwanza sasa wanaendelea vizuri,
wanakua kiroho kwa kasi, kwa Paulo mtume hii ni aina ya faraja, Mungu
anatufariji kwa viwango vikubwa anajua kutufariji katika kila aina ya dhiki na
mateso, kila aina ya pito lisilo jema unalolipitia kumbuka kuwa Yuko Mungu wa
faraka yote
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa Wajenzi.
Maoni 1 :
TEMBEA NA YESU
Chapisha Maoni