Jumatatu, 13 Februari 2017

Mshitaki wa Ndugu zetu!



Andiko la Msingi: Ufunuo 12:10Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini MSHITAKI wa ndugu zetu, yeye AWASHITAKIYE mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.”


Marko 15:3Nao wakuu wa Makuhani walikuwa WAKIMSHITAKI mambo mengi



Ni muhimu kufahamu kuwa shetani ndiye adui mkuu wa kila mwanadamu na kwa watu wa Mungu, Naye hufanya kazi kwa mbinu mbalimbali katika kuwashambulia wanadamu na watu wa Mungu moja ya mbinu kuu anayoitumia katika kufanya mashambulizi kwetu ni kutushitaki, au kutushutumu au kutulaumu, Leo tutachukua muda kutafakari kwa kina moja ya mbinu hii anayoitumia shetani kutushambulia ili asipate kutushinda kwa kukosa kuzijua Fikra zake au mbinu zake katika Jina la Yesu. 2Wakoritho 2:11Shetani asije akapata kutushinda kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.” Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Maana ya neno Mshitaki.
·         Makusudi makuu ya mshitaki wetu.
·         Jinsi ya kumshinda Mshitaki wetu.

Maana ya neno Mshitaki.
Neno mshitaki kwa asili linatokana na neno la Kiyunani “Kategoros” au “Kategor” ambalo kwa kiingereza ni “An accuiser” which means one who blames another, or charges another with crime ambalo maana yake ni “Yeye mwenye kutafuta na kuinua lawama kwa Mwingine” au yeye mwenye kushitaki mwingine kwa uhalifu, Unaweza kuona ni katika namna ya kushangaza sana shetani mwenyewe au kupitia maajenti wake huitumia mbinu hii katika kuhakikisha anabomoa kazi ya injili, au sifa za mtu, au kanisa, ili lisiweze kukubalika kwa wasioamini au kuwafanya walioamini kupungukiwa na imani. Neno hili limetajwa mara kadhaa katika biblia likionyesha kusudi la Ibilisi au maajenti wake wakilifanya kwa kusudi la kuharibu mpango wa Mungu!. Mfano:-

Yohana 8:10 Biblia inasema hivi “Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia Mwanamke, wako wapi wale WASHITAKI wako? Je Hakuna aliyekuhukumu kuwa na Hatia? Akamwambia  Hakuna Bwana Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako wala usitende dhambi tena” 

Katika kifungu hicho hapo juu mwanamke huyu alikamatwa katika kosa la zinaa na kwa mujibu wa Torati wazinzi walipaswa kupigwa mawe hata kufa, hata hivyo katika nyakati hizi serikali ya Warumi ndio ilikuwa inatawala Dunia na Israel pia, wao walikuwa wamepiga marufuku mtu yeyote kuendesha hukumu ya kifo isipokuwa serikali ya Rumi, katika kisa hicho hapo juu shetani aliitumia dhambi ya mwanamke huyu na washitaki wake ili kumtega Yesu aingie katika mtego wa kuruhusu hukumu ya kifo na hatimaye Yesu apate kushitakiwa unaona? Kisa kinaonekana kumlenga mtu mwingine lakini ndani yake kinamlenga Yesu Kristo ili ashitakiwe yeye, Mungu alimpa Hekima namna ya kuwasaidia wote akiwemo mwanamke huyo, shetani ndiye mshitaki wetu mkuu kumbuka, swala la kumtega Yesu ili aingie hatiani lilikuwa ni swala la kila siku la shetani na maajenti wake ili wapate kisa cha kumshitaki

Mathayo 12:10Na tazama yumo mtu mwenye mkono umepooza: wakamwuliza, wakisema Ni halali kuponya  watu siku ya Sabato? Wapate KUMSHITAKI.”

Marko3:2Wakamvizia ili kuona kama atamponya siku ya sabato wapate KUMSHITAKI

Marko 12:13-15Wakatuma baadhi ya Mafarisayo na Maherodi, ili wamnase kwa maneno, Kumnasa kwa maneno maana yake wapate namna ya KUMSHITAKI

Marko 15:3Nao wakuu wa Makuhani walikuwa WAKIMSHITAKI mambo mengi
Muda usingeliweza kutosha kuweza kuangalia maandiko mengi zaidi yanayoonyesha neno hilo Mshitaki linavyotumiwa katika Biblia katika maeneo mengoi sana kote huko shetani akitafuta hatia dhidi ya watu wa Mungu.

Makusudi makuu ya Mshitaki wetu!
Shetani kuitwa mshitaki wetu sio jambo geni katika agano jipya tangu zamani hizi zimekuwa sifa zake kubwa na tabia yake kuu mno, shetani ameonekana katika maandiko mengi ya kale akifanya kazi ya kuwashitaki wenye haki mfano katika :-

Ayubu 1:6-11 Bilia inasema hivi “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao. Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.  
       
Ayubu 2:1-5 Biblia inasema hivi “Tena kulikuwa na siku hao wana wa Mungu walipokwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao, ili kujihudhurisha mbele za Bwana. Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi? Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu; naye hata sasa anashikamana na utimilifu wake, ujapokuwa ulinichochea juu yake, ili nimwangamize pasipokuwa na sababu. Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Ngozi kwa ngozi, naam, yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai wake. Lakini sasa nyosha mkono wako, uuguse mfupa wake na nyama yake, naye atakukufuru mbele za uso wako. Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yeye yumo mkononi mwako; lakini tunza tu uhai wake

Zekaria 3:1-5Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye. Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni? Basi, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu sana, naye alikuwa akisimama mbele ya malaika. Naye huyo akajibu, akawaambia wale waliosimama mbele yake, akisema, Mvueni nguo hizi zenye uchafu. Kisha akamwambia yeye, Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi. Nikasema, Na wampige kilemba kizuri kichwani pake. Basi, wakampiga kilemba kizuri kichwani pake, wakamvika mavazi; naye malaika wa Bwana akasimama karibu”.
1Nyakati 21:1Tena shetani akasimama juu ya Israeli, akamshawishi Daudi kuwahesabu Israeli.”

Unaweza kuona kazi za shetani katika vifungu vyote vya maandiko hapo juu kwa nini shetani hutumia lawama, mashitaka, na masingizio kwa wanadamu na kwa jamii ya wenye haki ambao maandiko yanawaita Ndugu zetu yaani waamini? Kusudi kubwa ni kuharibu sifa na kuvunjilia mbali ushawishi walionao waamini katika jamii ili Mungu azomewe na kazi zake za ukombozi zionekane kuwa bure, Hii ndio imekuwa sifa ya Shetani na maajenti wake siku zake zote Kazi hii Maandiko yanaonyesha kuwa shetani huifanya Usiku na Mchana

Kwa kutumia maandiko hayo utaweza kuliona wazi kusudi la shetani kuwashitaki wateule
Ø  Anamshitaki Daudi ili Israel wapigwe wakataliwe na Mungu, Mungu awakasirikie watu wake na wapate hasara na shetani kufurahia angamizo la watu wa Mungu
Ø  Anamshitaki Zakaria ili asihesabiwe haki, aonekane hana sifa kwa Mungu aliyemchagua
Ø  Anamshitaki Ayubu kuonyesha kuwa mungu haabudiwi tupu, kwamba watu wake wanamuabudu kwa sababu Mungu amewapa Maisha mema, ili ionekanane kwamba binadamu akikosa kitu hawezi kumuweka Mungu mbele.
Ø  Kushitaki pia huja kwa kusudi la kutuletea Mateso katika jamii, akipata kitu cha kutusingizia na tukauhumiwa tutateseka sana kwaajili ya Kristo.
Ø  Anataka kuharibu mioyo yetu na kutujengea mazingira ya kuwa wenye hatia na usijione kuwa unastahili. Kisha upoteze Haki zako. Na kuleta aibu kubwa
Ø  Jumla ya yote ni ili karama tunayoitumikia iweze kulaumiwa yaani watu waone kuwa hakuna wokovu

Jinsi ya kumshinda Mshitaki wetu.

1.      Biblia inaonya kwamba tuwe na kiasi na wenye kukesha! 1Petro 5:8Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa MSHITAKI wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.” Njia pekee ya Kumshinda ni kuishi maisha ya kiasi, Mungu alituokoa ili tupate kuishi kwa kiasi, tusizidiwe na mambo ya ulimwengu huu kiasi ya kwamba yatatutoa katika mapenzi yake na adui akapata sababu ya kulaumu, Tito 2:11-12 Biblia inasema hivi “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;” Unaweza kuona Mungu anatutaka tuishi kwa kiasi na kwa haki adi Yetu shetani asipate la kutushitaki Mungu anapokuwa ametuokoa anatupa nguvu dhidi ya mamlaka na utawala wa shetani na shetani hawezi kufurahia kuanguka kwetu au kupatikana kwetu katika lawama ni njia yake ya kututamani ili kwamba turejee katika utawala wake, njia pekee ni kujitia nidhamu ni kuishi kwa kiasi.

2.      Biblia inatukumbusha namna nyingine ya kumshinda mshitaki wetu ni kuendelea kumwangalia Yesu Kristo ambaye kwa upendo wake mkubwa alitufia msalabani na zaidi ya yote ndiye anayetuombea, lazima tujue kuwa ni vigumu kutenganishwa na upendo huu Warumi 8:33- 39Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu”.     Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu, Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki, iko wazi kuwa haki tuliyonayo sio haki yetu wenyewe ni haki inayotokana na Kristo, ni muhimu kwetu kuendelea kuwa kuishi kwa imani na kuendelea kuaminikatika upendo wake nayeye mwenyewe atamkemea Shetani, kama ilivyokuwa kwa kuhani mkuu Zekaria, Shetani alipomshitaki Malaika alimtetea na kumtaka bwana amkemee, lazima tuendelee kumwangalia Yesu kama mtetezi wetu aliye hai.

3.       Damu ya Yesu ni jibu lingine la kumshinda mshitaki wetu, Yohana 12:10-11Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku. Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. Kama tukiwa na hisia za hatia tusiogope hatia sio jambo baya kusudi lake ni kutuleta katika toba, na toba hii inatupa wepesi wa kusamehewa na kuitumia damu ya Yesu kwa imani iliyomwagika msalabani tu narudi katika kuhesabiwa haki na shetani anapoteza nafasi ya kutushitaki.
4.      Yesu Kristo ni mpatanishi wetu Ni lazima tuelewe kuwa tunaye mpatanishi anayestahili yeye ndiye anayeweza kusimama mahali palipobomoka kati yetu na Mungu na kutupatanisha hatupaswi kuogopa turudi kwa mung mara tunapogundua kuwa tumemkosea na Kristo kama wakili wetu anatuombea kwa baba na kutupatanisha na Mungu kabla ibilisi hajapata la kutushitaki 1Yohana 2:1-2Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki,  naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.” 

        Hatupaswi kuogopa na kufikiri kuwa kila kitu kimeisha eti kwa sababu tulikosea jambo la msingi ni kurudi kwa Mungu na pia kuelewa kuwa tunaye mpatanishi na atafanyia upatanisho na Mungu.

5.      Usishitaki watu wa Mungu bali uwaombee, watu wengi wa Mungu hasa wana tabia ya kushutumu sana wanapoona makosa ya wengine badala ya kuwaombea Mungu kamwe hafurahii tabia ya aina hiyo, Mungu anaweza kukuhukumu wewe kwa vile unageuka na kusimama katika nafasi ya shetani kosa kama hili liliwahi kufanywa na Nabii Eliya Warumi 11: 2-4Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa na maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu, Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho yangu. Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali”. Wakristo ni lazima wajifunze kuombeana na kusamehe kwa haraka kutokusamehe kwa haraka ni kumpa ibilisi nafasi Efeso 4:26-27 inasema “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala msimpe Ibilisi nafasi.” Shetani anapataje nafasi ni kwa watu kutokusameheana nah ii inaweza kumpa yeye wakati wa kutushitaki kwa kulijua hili Paulo mtume aliagiza msamaha kwa ndugu aliyefanya dhambi na kupokea maonyo, alilisihi kanisa kumsamehe mtu huyo, kwani kama wasingelifanya hilo shetani angeweza kuwashinda angalia 2Wakoritho 2:10-11Lakini kama mkimsamehe mtu neno lo lote, nami nimemsamehe; kwa maana mimi nami, ikiwa nimemsamehe mtu neno lo lote, nimemsamehe kwa ajili yenu mbele za Kristo, Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.” Unaweza kuona kumbe kutokusamehe kunaweza kumpa ushindi mshitaki wetu ni lazima tuwe wenye kusamehe na kutokuwashutumu na kuwalaumu wengine, na badala yake kuwaombea vinginevyo shetani atapata nafasi kwetu pia.
Itaendelea na Rev. Innocent Kamote Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: