1Timotheo 2:
12 “Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala
mwanamume, bali awe katika utulivu.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa Agano jipya liko wazi kabisa katika mafundisho
yake kuhusu nafasi ya mwanamke, kama ilivyo ya mwanamume katika utumishi wake
kwa Mungu, wanawake wamepewa Karama za rohoni kama ilivyo kwa wanaume 1Wakoritho
12:7-11, wote wanatumiwa na Mungu katika kuujenga mwili wa Kristo 1Petro
4:10, Huduma za wanawake ni muhimu katika kanisa kama na zina mchangoi
mkubwa katika ujenzi wa mwili wa Kristo na hilo halina shaka yoyote, 1.Wakoritho
12:12-26, Kuna mifano mingi sana katika Agano jipya jinsi Mungu
alivyowakirimia wanawake na kuwatumia katika kumtumikia Mungu.
Je lakini agano jipya limewakataza wanawake kuwa makasisi yaani kuwa
wachungaji? Hili linawezekana lakini litakuwa fundisho lenye utata mkubwa,
kutokana na mitazamo mbalimbali ya wanatheolojia, kwa mfano Makanisa makubwa ya
zamani, likiwemo kanisa la Orthodox wamekataa na kupinga wanawake kuwa
wachungaji kutokana na sababu ya tafasiri ya 1Timotheo 2:8-15, Katika
mistari hiyo Biblia inasema hivi;- “Basi, nataka
wanaume wasalishe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira
wala majadiliano. Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri,
pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu
na lulu, wala kwa nguo za thamani; bali
kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu. Mwanamke
na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna. Simpi mwanamke ruhusa ya
kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu. Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na
Hawa baadaye.Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa
akaingia katika hali ya kukosa. Walakini ataokolewa kwa uzazi wake, kama
wakidumu katika imani na upendo na utakaso, pamoja na moyo wa kiasi”.
Swala kubwa katika mabishano ya kitheolojia ni je Mwanamke anaweza kuwa
Mchungaji? Au Mwanamke anaweza kuwa Kuhani kwa wayahudi, au mwanamke aweza kuwa
Rabbi kwa wayahudi na je mwanamke aweza kuwa sheihk kwa waislam? Maswali hayo
yote yakijibiwa kwa ufasaha yanaweza kuleta jibu muafaka kama wanawake wanaweza
kuzishika nafasi hizo nyeti katika imani, licha ya kuwa Mungu anaweza
kuwakarimia karama zilezile ambazo wanaume wanaweza kuwa nazo bila upendeleo.
Swala la wanawake kuwa makuhani Priest ni lenye utata hata katika jamii
ya kiyahudi na ni swala la kihistoria ambalo ni vigumu kulitolea maamuzi
thabiti kwa sasa na katika mada fupi kama hii
Pichani mwanamke wa Kiyahudi anayefanya kazi za kikuhani, jambo hili
limewagawa Wayahudi kwamba wako wanaopinga na wako wanaokubaliana
Ujumbe:
1Timotheo 2:
12 “Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala
mwanamume, bali awe katika utulivu.
Tunaporejea katika ujumbe
wangu wa leo
Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume Mimi kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima nataka kuzungumzia mada tofauti
na ile ambayo nimeigusia katika utangulizi wangu, mimi nataka kutafasiri andiko
hilo hapo juu na kisha kuleta fundisho ambalo linaweza kuleta unafuu katika
ndoa zetu na kutupa amani
Simpi mwanamke ruhusa ya
kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu. Katima mstari
huu ukiacha mjadala wa mwanamke anaweza kuwa kasisi au la, kuna jambo la msingi
linalofunuliwa na andiko hili katika uhusiano wa wanandoa, mstari huu katika
lugha ya kiingereza unasomeka namna hii katika matoleo tofauti ya biblia mfano
KJV inasema “But I suffer not a woman to teach, nor
to usurp authority over the man, but to be in silence” NIV inasema “I do not Permit a woman to teach or to have
authority over a man; She must be silent. Maneno teach na neno Authority au Usurp yote yanabeba
maana moja katika biblia ya kiyunani neno linalotumika hapo ni kama to have
authority au to usurp ni neno “authentein”ambalo maana yake ni to take
position au to have a power without the right to do that au to have control au
Dominate.
Katika
lugha yetu ya Kiswahili neno “Kufundisha na kumtawala”katima maana ya kibiblia
hapo yana maana moja ambayo ni kutawala, au kushikisha adabu au kuwa na nafasi
ya juu kuliko mwanaume katika madaraka ya nyumba na kanisa, fundisho langu kuu
leo linalalia katika kutawala mume kwa maana ya madaraka au mamlaka katika ndoa.
Katika nyakati hizi za kidigital wanawakwe wengi na hata wanaume wamekuwa
wakisahau wajibu wao katika ndoa na hivyo kusababisha madhara makubwa na
mafarakano na hata kuweko kwa talaka, moja ya tatizo kubwa ambalo ndio
ningependa kulizungumzia leo ni wanawake kuwatawala waume zao, jambo hili
inawezekana umewahi kulishuhudia, au linakutokea au umewahi kuwasikia watu
wakisema na wakati mwingine hata wanawake wenyewe wakijisifu kuwa wamewaweka
kiganjani waume zao je jambo hili lina mustakabali gani kibiblia?
·
Kwa nini wanawake wanataka kuwatawala wanaume?
·
Kwanini baadhi ya wanawame tayari wanawatawala waume zao?
·
Kwanini kweli wako wanaume wanatawaliwa na wake zao na hawawezi kukohoa
au nkusema lolote mbele zao?
·
Kwa nini wanwake ndio wamekuwa mabwana na watawala wa waume zao?
Ni imani yangu kuwa utakuwa umelishuhudia hili katika ulimwengu huu tulio
nao duniani, utakuwa umeshuhudia kwa kiwango kikubwa kuwako kwa hamasa kubwa ya
wanawake kuwatawala wanaume na kuwaweka chini ya udhibiti wao, wanawake leo
wanafanya jitihada kubwa katika kuhakikisha wanawatawala waume zao, na kuwa
ndani ya nyumba hakuna anayekohoa isipokuwa mwanamke, leo nataka kutoa jibu au
majibu ya sanbabu hii ya changamoto kubwa inayojitokeza na kuharibu jamii.
Nataka kama mkuu wa wajenzi kujibu kwanini wanawake wanataka kuwatawala
wanaume?
1. Ni mpango wa shetani mwanamke
kumtawala mwanamume.
Ni
muhimu kwanza tukajenga msingi wa kiroho wa kuona kilichompelekea Paulo mtume
kuzungumza swala hili angalia 1Timotheo
2: 12-15 biblia inasema;-
“Simpi mwanamke
ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu. Kwa
maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye. Wala Adamu hakudanganywa,
ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa. Walakini
ataokolewa kwa uzazi wake, kama wakidumu katika imani na upendo na utakaso,
pamoja na moyo wa kiasi”.
Paulo
mtume anatoa sababu za katazo lale kwa nini hataki mwanamke kumtawala mwanamume
anaweka wazi sababu za kimaumbile kwanza akisisitiza kuwa Adamu ndiye
aliyeumbwa kwanza na Hawa baadaye, hii inamaanisha kimaumbile tu mwanamume ni
kiongozi, yeye ndiye aliyeumbwa kwanza na Hawa alifuata baadaye, katika bustani
ya Edeni aliyepokea maelekezo ya kwanza ya kutokula mti wa matunda
yaliyokatazwa alikuwa mwanaume, na mwanaume hakudanganywa kwanza maana yake
mwanaume alikuwa na msimamo, ndiye kiongozi ndiye mzaliwa wa kwanza kisha
mwanamke aliumbwa baadaye.
Pili
Paulo mtume anaeleza habari za utendaji wa kazi wa shetani, kwamba shetani
hakumfuata kwanza mwanamume, alimfuata mwanamke, shetani alijua udhaifu
aliokuwa nao mwanamke, aliutumia kumdanganya na kwa kuanza nayeye alileta
uharibifu kwa familia nzima na aina binadamu wote leo ulimwenguni, kwa mtindo
huo huo shetani ataendelea kuwatumia wanawake duniani kupitia udhaifu wao
kuleta maanagmizi katika familia na kanisa kwa ujumla.
Mungu
aliona katika mpango wake kuwa ili mwanamke awe salama anapaswa kuwa chini ya
mumewe anapaswa kujinyenyekesha chini ya mumewe angalia Mwanzo 3:16 “Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na
kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye
atakutawala.”
Katika
maandiko hayo Mungu alitangaza adhabu atakayokuwa nayo mwanamke kutokana na
anguko na moja ilikuwa ni kuzidishiwa kwa uchungu wake, na pili kwa utungu utazaa watoto na tatu tamaa
yako itakuwa kwa mumeo naye atakutawala.
Katika
mgogoro huu uliotangazwa na Mungu ni muhimu kukumbuka kuwa ni mgogoro wa milele
ambapo kila saa na kila wakati wanwake watajaribu kuwatawala wanaume moja kwa
moja au kwa namna nyingine kama tutakavyoona katika vipengele vingine.
KJV
inasema ;-
Unto the woman he said, I will
greatly multiply thy sorrow and thy conception; in sorrow thou shalt bring
forth children; and thy desire shall
be to thy husband, and he shall rule over thee
.
Kutokana
na mwanamke kudanganywa na ibilisi, biblia inaonyesha kuwa Mungu ataongeza
uchungu wa mwanamke, yaani huzuni, lakini vilevile uchungu wakati wa kuzaa na
zaidi tamaa yake itakuwa kwa mumewe na mumewe atamtawala
“Tamaa
yako itakuwa kwa mumeo na mumeo atakutawala” katika maneno haya Mungu yu
aonyesha kuwa wanawake watakuwa na tamaa ni tamaa gani hii sio tamaa ya ngono
ni tamaa ya kuwatawala wanaume lakini matokeo yake mumewe atamtawala Mungu
alitangaza mgogoro hapa kuwa mwanamke atashawishika kutaka kumtawala mwanaume
na matokeo yake yatakuwa mabaya kwa sababu Mungu ameandaa utawala kwa mwanaume,
kwa sabubu hiyo kiu nya wanawake kutaka kuwatawala wanaume inachochewa na
shetani kuiinua nia iliyoko ndani yao Mungu alikuwa anaonyesha njia ya amani
kwa mwanamke ni kunyenyekea na kukubali kutawaliwa na mumewe
Mara
zote chanzi kikubwa cha migogoro hutokea pale nyumba inapokuwa na mwanamke
mtawala, wanawake wengi hupigwa na hata kupewa talaka kwa sababu ya kutaka
kutawala waume zao, pale wanapojaribu tu kuwa juu ya waume zao, mgomgoro
unaibuka na kuanza, Mungu katika hekima yake alitaka kuwasaidia wanawake wapate
kutambua kuwa njia pekee ya wao kuwa na mafanikio katika ndoa zao ni kuwa
wanyenyekevu. 1Petro 3:1a “Kadhalika ninyi
wake, watiini waume zenu;” mwanamke awaye yote anayetaka kuheshimika
na kupendwa na kuthaminiwa katika ndoa yake ni muhimu akakubali muongozo huu wa
upenndo wa kiungu.
2. Ni kwa sababu ya malezi toka kwa
mama yake.
Nyani
hujifunza kuogopa nyoka pala wanapoona nyani wengine wakiogopa nyoka na
kutetemeka, wanadamu pia hujifunza kutoka kwa wanadamu wengine, kama mwanamke
amekulia katika mazingira ambayo mama ni mtawala wa mumewe hali kadhalika
binti yake au zake wanauwezo wa kukua
katika tabia na mwenedno huo huo Biblia inaonyesha hivyo wazi katika Ezekiel 16:44-45 “ Tazama, kila mtu atumiaye mithali atatumia
mithali hii kinyume chako, akisema, Kama mama ya mtu alivyo, ndivyo alivyo
binti yake. Wewe u binti ya mama yako,
amchukiaye mume wake na watoto wake; nawe u umbu la maumbu yako, waliowachukia
waume zao na watoto wao; mama yako alikuwa Mhiti, na baba yako Mwamori.”
Kama mama atakuwa mwanamke mtawala na
binti yake atakua akiwa na mtazamo huo na hapo ndipo mafanikio huweza kuwa
hatarini katika nyumba na familia za aina hii
3. Kutokana na kutokujiamini.
Hili
ni tatizo la kiroho na kisaikolojia kama mwanamke hajiamini huanza kuwadibiti
wengine yaani kuwatawala ili kwamba ajisikia yuko salama kitaalamu ningesema “when
someone feels insecure he might start to control others in order to feel in
control once again” Saikolojia sio kama 1+1=2, kwa hiyo hapa simaanshi kila
mwanamke mtawala anakuwa na tatizo la kutokujiamini HAPANA lakini mara nyingi wanawake wasiojiamini watajaribu
kujiweka huru na salama kwa kujaribu kudhibiti mazingira yanayomzunguka na
ikiwezekana atamjumuisha na mumewe.
4. Kujichukia au kuchukia jinsia yake.
Tatizo
hili ni tatizo la kisaikolojia na linatokea pale ambapo mwanamke najichukia
kuzaliwa manamke kwa kudhani kwamba kuwa mwanamke ni kuwa wa ngazi ya chini na
matokeo yake huanza kutumia nguvu za kiutawala kutawala watu na mumewe ili
kufidia au akifikiri kuwa yuko katika nafasi salama kama ya wanaume, Katika
saikolojia jambo hili huitwa Masculine protest ambayo maana yake kwa lugha ya
kigeni ni
Masculine protest is a tendency attributed especially
to the human female in the psychology of Alfred Adler to escape from the female
role by assuming a masculine
role and by dominating others; broadly: any tendency to compensate for feelings
of inferiority or inadequacy by exaggerated overt aggressive behavior.
5. Mwanamke
mtawala huchagua mwanamme dhaifu.
Kutokana na maswala ya
kisaikolojia na kiroho pia utaweza kuona ile tamaa ya kiutawala ndani ya
mwanamke itakuwa inatafuta mwanamume dhaifu ambaye anatawalika kwa njia rahisi
sana bila kutumia nguvu nyingi, hii maana yake mwanamke mwenye tamaa hii ya
kutawala haraka sana anavutiwa na mwanamume ambaye ni rahisi kutawalika, Endapo
atagundua kuwa hutawaliki wakati wa migogoro ya kiutawala atahitimisha kwa
kusema kuwa umekuwa na kiburi siku hizi, anaweza kusingizia uwezo ulio nao cheo
na hata fedha kuwa zimekubadilisha.
Njia
mbadala wanazotumia wanawake kuwatawala wanaume!
Katika
mgogoro huu uliotangazwa na Mungu ni muhimu kukumbuka kuwa ni mgogoro wa milele
ambapo kila saa na kila wakati wanwake watajaribu kuwatawala wanaume moja kwa
moja au kwa namna nyingine.
Ni
muhimu kufahamu kuwa huu ni mgogoro wa asili uliotokana na anguko la mwanadamu
hivyo ni muhimu kukumbuka kuwa wanawake watafanya hivyo kwa kusudi au hata bila
kukusudia ili mradi wajisikie salama kutawala, Hapo juu tumechambua njia ambazo
wanawake huzitumia kuwatawala wanaume moja kwa moja lakini sasa nataka kufunua
njia nyingine ambazo sio za moja kwa moja namna wanawake wanavyotafuta kutawala
ndoa zao au waume zao au nyumba zao, njia hizi huzitumia kutawala hata kama hawajawa au hawajafanikiwa
kushika madaraka hayo
1.
Kulitumia tendo la
ndoa kama njia ya kutawala.
Wanawake hutumia njia ya kunyima
tendo la ndoa kama njia ya kuwafanya waume zao watimize matakwa yao, mwanzoni
nilipokuwa nimeoa moja ya mgogoro mkubwa niliokutana nao ulikuwa ni huu wa
kunyimwa unyumba sikufahamu sana sababu zilikuwa ni nini lakini nilikonda na
kuwa mnyonge sana kwa sababu namcha Mungu na hakuna mahali pengine ningeweza
labda kupata tendo hilo, nilimuuliza Mchungaji wangu mmoja kuhusu hili na
alinijibu kwa ufupi tu “Ukiona mwanamke anakunyima unyumba ujue anataka
kukutawala” full stop mchungaji hakunifafanulia kwa undani jambo hili lilikuwa
lina maana gani, inawezekana ni kutokana na ufahamu wake aliokuwa nao wakati huo
na mimi sikuuliza maswali mengi pia kutokana na ufahamu wangu niliokuwa nao
wakati huo. Lakini sasa nafahamu kuwa hakuna jambo baya duniani kama kunyimana
unyumba na dawa ya jambo hili inaweza kuwa mbaya hata kuielezea hapa, Lakini
mjenzi mwenye hekima mwenzangu alisema tu shetani asije akapata nafasi
msinyimane.
1Wakoritho
7:2-5
“Lakini kwa
sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na
awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na
ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo
hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa
mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije
akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu”
Mwanamke mpumbavu huweza kuibomoa
nyumba yake kwa mikono yake miwili, kama mwanamke atalitumia tendo la ndoa kwa
matakwa yeke tu na kwa kusudi la kumtawala mumewe biblia iko wazi tu kwamba
shetani atafanikiwa kuwajaribu, na zinaa itatokea na anguko lilelile kama
lililomtokea Adamu na Hawa linaweza
kuwatokea na ninyi katika namna hii ambayo Mwanamke anatafuta utawala na ndio
maana hakuna jambo la msingi na maana sana duniani kama mwanamke kuwa
mnyenyekevu, wabarikiwe sana makabila yote ambayo wanawake wamefunzwa kuwapigia
goti wanaume mpaka chini na kuwaheshimu waume zao kama watawala na mabwana kwa
kufanya hivi hawapungukiwi na kitu lakini wataongeza kupendwa zaidi na waume
zao na kuaminiwa.
Malaki
2:16 “Maana
mimi nakuchukia kuachana, asema Bwana, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo
yake kwa udhalimu namchukia, asema Bwana wa majeshi; basi jihadharini roho zenu,
msije mkatenda kwa hiana.”
Pia kutokana na wanawake kufanya
hayo kuachana kunaweza kutokea jambo ambalo linamuudhi sana Mungu na sio hivyo
tu Mungu anachukizwa na “naye aifunikaye
nguo yake kwa udhalimu”kunaweza kuwa na tafasiri mbili tu katika kimstari
hicho yeye nafanyaye zinaa lakini zaidi sana yeye anayenyima unyumba, kufunika
nguo yako kwa udhalimu ni kukataa kuwa tayari kwa tendo la ndoa, wanawake wa
jinsi hii hupanda kitandani wakiwa na magwanda, hawatoi ushirikiano wa kutosha
katika tendo la ndoa, na tendo la ndoa hupewa mwanaume kama vile mtoto
anapohitaji kunyonya tu na sio kwaajili ya kuhakikisha nyumba inasimama
Kwa nini wanawake hunyima tendo
la ndoa makusudi wapate kutawala na tabia hii hufanywa zaidi na wanawake
waoajiita kuwa wacha Mungu, waliobarikiwa kuwa na Mume mmoja mcha Mungu na
mwaminifu na hatima ya jambo hili huwa mbaya
2. Hutumia
Machozi kama njia ya kutawala.
Baadhi ya wanawake huwatawala
wanaume kwa kutumia machozi, yaani hutumia njia ya kukimbilia kulia machozi
pale wanapokutana na vikwazo kuhusu jambo Fulani katika ndoa zao hii hutokea
endapo mwanamke ana mahitaji yake au madai yake ya aina Fulani, ama amefanya
jambo ambalo anajua kama mume utachukua hatua kali, kumdibiti hapo mwanamke
hukimbilia kulia kama kinga na njia yaw ewe kukubaliana naye au ushindwe
kuchukua hatua stahiki.
3. Hutumia
njia za kuaibisha au kusemelea.
Mwanamke anayetaka kutawala
hutumia njia ya kuaibisha yaani anaweza kutishiakuondoka akiwa amefungasha
mizigo yake yote, au baadhi ya nguo, hii itakuogopesha kwamba watu watajua kuwa
mmegombana na hivyo, utambembeleza, au kwamba unawaogopa wakwe zako na
unawaheshimu hivyo hutaki kuonekana mbaya na hivyo utanyenyekea mwanamke wako
na kutimiza matakwa yake aidha wanawake hao pia hukimbilia kwa watu
unaowaheshimu na kueleza mambo yenu ili kukuitisha vikao na kutafuta suluhu,
haya yote yatakufanya uogope kumfanya lolote ukijua kuwa utaaibika na hapo
ndipo wanapopata nafasi ya kutawala kama mwanaume hutakuwa na ufahamu wa
kukutosha kuhusu viumbe hao.
Ni
kwasababu nkama hizo na nyinginezo zisizoorodheshwa hapa shetani huzitumia
kupitia wanawake ili kuwatawala wanaume na ni kwaajili ya hayo Paulo mtume
anakataza kutoa nafasi hii kwa wanawake kuwatawala wanaume na kutokuheshimu
nafasi ya mwanamume katika ndoa na katika kanisa
Dawa
ya mwanamke mtawala.
Kama wewe ni mume au mwanaume
unayepitia mateso ya kuwa na mwanamke mtawala ujue una njia moja au mbili tu za
kusuluhisha tatizo lako moja kumsaidia kwa kumfundisha ili kwamba atambue
wajibu wake na mahitaji yake ya kisaikolojia na nafasi yake kiroho na
kimaandiko na njia ya pili ni kukubaliana naye kwa kumfanya ajione kama mtawala
na kutafuta namna unavyoweza kumtawala.
Njia ya kwanza sio rahisi kama
unavyodhani, mwanamke mtawala hawezi kukubali hilo na atahakikisha kuwa
anajisaidia vyovyote iwavyo ashike mpini, na hapo ndipo kosa linapotokea kwani
sasa mwanaume anaweza kujikuta akitumia nguvu na migogoro mingi hutokea
magomvi, vipigo, kunyimana unyumba, zinaa na talaka pia, hakuna mtu hasa
mwanaume anayeweza kukubali kukaa katika nyumba isiyo na amani.
Mfalme Sulemani alisema manen magumu
sana kuhusu kuwa na mwanamke mtawala Mitahli
21:9 Biblia inasema “Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika
nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi” pia Sulemani akarudia tena Mithali 21:19 “Ni afadhali kukaa katika nchi ya nyika; Kuliko
na mwanamke mgomvi, mchokozi.” Je wadhani Mfalme mwenye hekima
anazungumzia mwanamke mgomvi au mchokozi anamaanisha nini ni wanawake watawala.
Ugomzi utajitokeza na kama ukitumia
nguvu uhusiano utavunjika na kuachana kutatokea, ni muhimu kuwafunza wanawake
kutambua nafasi zao na kujinyenyekesha kwa waume zao, mfano mwema biblia
inamtaja Sarah alikuwa ni mwanamke wa kipekee sana aliyejali hisia za mumewe na
kumuheshimu sana kiasi ya kumuita BWANA 1Petro
3:1-6 “Kadhalika
ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe
kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno; wakiutazama mwenendo wenu safi, na
wa hofu. Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na
kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi; bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika
mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu
mbele za Mungu. Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa
zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao. Kama vile Sara alivyomtii
Ibrahimu, akamwita Bwana; nanyi ni watoto wake, mfanyapo mema, wala hamkutishwa
kwa hofu yo yote”
Unaona Sarah anatajwa kama mfano wa
wanawake watii waliowaheshimu waume zao Sara alimuheshimu sana Abraham, na kwa
sababu hiyo Abrahamu alimsikiliza sana Sarah kila mwanamke mcha Mungu anapaswa
kuiga mfano wa Sarah wa utii na unyenyekevu na heshima kwa mumewe kwa faida ya
nyumba yake na familia yake hutakuwa mjinga mwanamke ukijinyenyekeza lakini
utakuwa mpumbavu ukitafuta utawala.
Biblia inamtaka mwanamume kutumia
akili
1Petro
3:7 “Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa
akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi
pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.”
Biblia inamtaka mwanaume kuitumia
kili yake ipaswavyo katika kuishi naye mapambano yote ya mwanamke ya kutaka
kutawala yakiachiwa hivihivi ni hatari, mwanamke akifanikiwa kukutawala
atatawala kwa uangamivu wa nyumba yako yote nao wanapolenga kutawala wanalenga
kutawala Tendo la Ndoa, Fedha, kujaliwa na Muda wako kwa msingi huo ili
umtawale mwanamke ni lazima maswala hayo manne yawe yamakaa vema na uwe na
ujuzi nao na utaalamu nayo, Hakikisha una ujuzi wa kutosha katika Tendo la ndoa
na unampatia haki yake kana inavyopaswam hakikisha unaitunza familia yako na
kuipatia mahitaji yake yote na ukifanikiwa nay a ziada, hakikisha kuwa unamjali
kiasi ambacho anaweza kujifikiri kuwa yeye ndiye anayetawala na hakikisha
unampa muda wa kutosha, kama hutajali hayo utajikuta unaingia katika wakati
mgumu sana wanaume wengi hudharaulika kwa sababu ya kuwa dhaifu katika eneo
moja wapo kati ya hayo, mwanamke akiwa mpweke anaweza kufanya jambo lolote,
mwanamke akikosa tendo la ndoa anaweza kushiriki na yeyote hata mnayama,
mwanamke asipojaliwa anaweza kutoa muda wake hata kwa house boy, mwanamke kama
hana matuzo au yeye ndiye anakutunza unapoteza maana katika ndoa, aidha nitoe tahadhari
kwa watumishi wa Mungu wanaotoa muda mwingi sana katika kuomba bila ya wake
zao, hili ni kosa maombi yako hayatazuia mkeo kushughulikiwa na watu wa ajabu ajabu wanaweza kuwa wauza mchele tu, au madereva nk. kama hutampa mahitaji muhimu na kuishi
naye kwa akili, kla kitu kifanyika kwa kiasi, Mungu yu ajua kuwa tuko
ulimwenguni hivyo usihamie kwenye ulimwengu wa roho tu na kuacha ulimwengu wa akili ukitoa muda kwa mkeo na familia yako.
Ni matumaini yangu kuwa wanawake kwa
wanaume mmefaidika na mafundisho haya yenye Baraka, tafadhali kama somo hili
limekusaidia wewe Mwanamume na wewe mwanamke acha maoni yako hapa, ili
nimtukuze Mungu kwa somo hili au nitumie ujumbe au kunipigia kwa namba
zifuatazo.
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima
Rev. Innocent Kamote
0718 990 796 call any time
0784 394 550 call any time
0626 606 608 sms only
E mail ikamote @yahoo.com
Maoni 1 :
Bwana Mungu wetu aketiye mbinguni akubariki sana mtumishi wake hakika sijapoteza muda wangu kusoma makala haya yenye baraka.
0622759200
Chapisha Maoni