Ayubu 14:13-14 “Laiti ungenificha kuzimuni, Ukanilinda kwa siri, hata
ghadhabu zako zitakapopita, Na kuniandikia muda ulioamriwa, na kunikumbuka! Mtu
akifa, je! Atakuwa hai tena? Mimi ningengoja siku zote za vita vyangu, Hata
kufunguliwa kwangu kunifikilie.”
Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye
hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele
Leo hii wakristo wote nchini
wanaungana na wakristo wengine duniani kote pamoja na wayahudi kuadhimisha
sikukuu ya Pasaka, kukumbuka tukio la kusulubiwa, kufa na kufufuka kwa Yesu
Kristo kulikotokea miaka zaidi ya 2000 iliyopita, huku Wayahudi wakiadhimisha
miaka zaidi ya 3000 Tangu walipoadhimisha Pasaka ya kwanza katika siku ya 15 ya
mwezi wa Nisan kwa mujibu wa Kalenda ya kiyahudi Hapo walipookolewa kutoka Misri.
Miaka mingi sana kabla ya
kufufuka kwa Yesu, mtumishi wa Mungu Ayubu aliwahi kuuliza swali la msingi sana
katika maisha ya mwanadamu, swali hili ni moja ya miongoni mwa maswali ya
kifalsafa, swali hili liliulizwa kutokana na hoja zilizotolewa na watu wenye
hekima mbali mbali waliokuja kumtia moyo ayubu na kujiuliza swali kwanini
wanadamu wanateseka, swali kuhusu mateso hata leo limekuwa ni swali kubwa sana
lenye mjadala mkubwa sana katika imani mbalimbali
·
Wahindu
wanaamini mateso yanatokana na KARMA yaani kuishi kwa kutenda Mema wanaamini
kama ukiishi vibaya utazaliwa kitu kibaya na utapata shida, na hivyo katika
mzunguko wa maisha Mungu atakupa mabaya na utachelewa kufika NIRVANA yaani
mbinguni kukaa na Mungu
·
Wabudha
wanaamini kuwa mateso yanatokana na tamaa, yaani kama mwanadamu ataishi mbali
na tamaa atakuwa ameingia NIRVANA hata kama bado yuko Duniani, hivyo wao
hujifunza kuridhika na kujikana na kuitesa miili yao
·
Waislam
wanaamini kuwa mateso ni matokeo ya Kudra za mwenyezi Mungu, yaani ni mapenzi
ya Mungu kwa kadiri ya majaliwa yake
·
Wayahudi
waliamini kuwa mtu anaweza kupata mateso kama matokeo ya dhambi zake au za
wazazi wake kutokana na Mungu alivyoahidi kushuhulika na kizazi hata ta tatu na
nne cha wampendao au wanaomchukiza
·
Wakristo
swala kuhusu Mateso ni swala pana sana na linaweza kuwa na ufafanuzi mpana sana
wa kwanini wanadamu wanateseka, hata hivyo Kiongozi mkuu wa wokovu wetu yaani
Yesu alikamilishwa kwa njia ya mateso
Katika kitabu cha Ayubu ni wazi
kuwa Ayubu pamoja na rafiki zake walikuwa wakijadili kuhusu Mateso na sio
mateso ya kawaida bali mateso ya mtu aliyeishi kwa haki, Ayubu ambaye
inasemekana kuwa aliihi maisha ya hali alikuwa anateseka sana na hakuwa amepata
tiba, licha ya mali yake kuwa imetekekea, licha ya kuwa amepoteza watoto wake
wote, pia alikuwa na majipu mabaya yaliyokuwa yakifumba na kufumbuka mwili
mzima kutoka kichwani hata unyayoni, Ayubu na wenzake walikuwa wamejadili na
kutafuta suluhu bila kupata ufumbuzi na hivyo Aybu alikuwa anatazamia kufa
aliamini kuwa sasa hakuna tumaini lingine lililosalia zaidi ya kifo tu, ndipo Ayubu akauliza katika hali yakukata
tamaa
Kwamba mbona miti ikikatwa shina
lake huchipuka? Na maji ya bahari hupwa na kujaa ni kama inaonekana kuwa viumbe
hivyo vina matumaini lakini sivyo ilivyo kwa mwanadamu, inaonekama kama mtu
akifa ni mwisho wa kila kitu na hakuna matumaini ya kurejea tena, Ayubu
anamwambia Mungu kwa kuwa siku za mwanadamu za kuishi ni chache na zimejaa taabu,
ni afadhali angewaacha tu bila kupata mateso maana hawatakuwako tena, Hata
hivyo Ayubu alikuwa na imani kuwa iko namna atamuona Mungu tu hata kama mwili
wake utaharibiwa alikuwa na imani kuwa macho yake yatamuona tu
Ayubu
19: 25-27 “Lakini
mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya
nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa
hivi, Lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu; Nami nitamwona mimi
nafsi yangu, Na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine. Mtima wangu unazimia
ndani yangu.”
Swali
lililoulizwa na Ayubu Mungu aliwahi kumuuliza mtumishi wake Ezekiel katika
namna nyingine,
Ezekiel 37:1-3 “.Mkono wa Bwana
ulikuwa juu yangu, naye akanichukua nje katika roho ya Bwana, akaniweka chini,
katikati ya bonde; nalo limejaa mifupa; akanipitisha karibu nayo pande zote; na
tazama, palikuwa na mifupa mingi katika ule uwanda! Nayo, tazama, ilikuwa
mikavu sana. Akaniambia, Mwanadamu, je!
Mifupa hii yaweza kuishi? Nami nikajibu, Ee Bwana MUNGU, wajua wewe”.
Wakati huu taifa la Yuda lilikuwa limechukuliwa utumwani Babel na kila kitu
iimeaharibiwa na kufa hakukuwa na matumaini ya uhai tena ndio maana swali hili
lilikuwa Gumu kwa Ezekiel yeye alijibu tu kuwa Bwana unajua wewe! Mtu awaye
yote anapopitia katika mateso na huzuni na kukata tamaa huwa anafikiri kuhusu
kurejeshwa tena katika hali aliyokuwa nayo mwanzoni your Golden Age!
Mtume Yohana ndiye mtume
aliyeteseka sana kuliko mitume wote, inasemekana aliwahi kuviringishwa katika
yasi na kuwashwa moto lakini alitoka akiwa safi, aliwahi kuchemshwa katika
pipala mafuta ya lami lakini alitoka akiwa hai, alishuhudia wenzake na wakrito
wengine wakifa na kuawa kwa kuliwa na simba kuchomwa moto na kadhalika yeye
kutokana na kushindikana kufa waliamua kumpeleka katika kisiwa cha Patmo ili
akateseke huko maisha yalikuwa ni yenye kuhuzunisha na kukatisha tamaa, Yesu
alimuona Yohana akiwa amekata tamaa na alimpa ujumbe mkubwa wa kutia moyo
Yohana 1:17-18 “Nami
nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa
kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye
hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami
ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.”
Swali la muhimu la kujiuliza ni
kwanini Yesu alijitambulisha kuwa yu hai yaani amefufuka? Ni muhimu kufahamu
kuwa ujumbe muhimu kwa mtu ANAYETESEKA,
ALIYEKATA TAMAA, na ALIYE KATIKA
HALI YA KUFA ni UJUMBE WA UFUFUO Yesu alifahamu kuwa
huu ndio ujumbe pekee unaoweza kumpa mtu tumaini Jipya!
Habari njema kwa ndoa iliyokufa
sio kuolewa tena ni kurejea tena kwa furaha iliyotoweka na upendo uliotoweka
katika ndoa yake.
Tunapoisheherekea pasaka na
kukumbuka kufufuka kwa Bwana wetu Yesu ni ujumbe wa matumaini kwamba Bwana Yesu alikufa na akafufuka na kuwa
mauti haimuwezi na kuwa ni yeye ndiye mwenye funguo za mauti na kuzimu, ki
msingi Yesu anajibu la swali la Ayubu kuwa mtu akifa atakuwa hai tena Yesu
anajibu swali hili kuwa ndio mtu akifa anaweza kuwa hai tena na anatutangazia
wazi kuwa yeye anazofunguo za mauti na kuzimu na hivyo anauwezo wa kufufua
matumaini yaliyotoweka kwako, anauwezo wa kufufua huduma yako, anauwezo wa
kurejesha watoto wako, ana uwezo wa kurejesha kila kilicho haribiwa na kuuawa
na ibilisi, ana uwezo wa kurejesha na kufufua taifa linalomtumaini yeye, Pasaka
hii mimi sihitaji habari nyingine yoyote nahitaji kusikia habari za matumaini
ya kuwa Yesu Kristo yuko hai na ndiye mwenye Mamlaka ya kifo na uzima na ana uwezo wa kufufua ndoto zetu,
maisha yetu, matumaini yetu, uzima wetu,
mimi sihitaji waraka wa maaskaofu nahitaji kumuona mteteaji wangu akisimama
kiunitetea dhidi ya kila aina ya unyonge na utumwa Pasaka ina uhusiano na
ukombozi nahitaji kumuoja Yesu akinikomboa mimi na familia yangu na watu wangu
na taifa langu hii ndio habari njema ya ujasiri kuwa mauti haina nguvu katika
maisha yetu, imepoteza mamlaka ni yesu pekee mwenye mamlaka hiyo yeye atafufuka
pamoja na mashaka yangu yeye atahuisha nafsi yangu!
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni