Ijumaa, 2 Machi 2018

Kuingia kwa mfalme Kinyume cha Sheria!


Andiko la msingi: Esta 4:15-16Basi Esta akawatuma ili wamjibu Mordekai, Uende ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani, mkafunge kwa ajili yangu; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala mchana, nami na wajakazi wangu tutafunga vile vile; kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie.”



Utangulizi:

Wiki hii ni wiki ya sikukuu ya PURIM kule Israel wayahudia huandimisha sikukuu ya Purim kwa mujibu wa kalenda ya kiyahudi sikukuu hii ya Purim huazimishwa kila ifikapo February 28 na 29 ya kila mwaka  ambayo ni sawa na siku ya 13, 14  na 15 ya mwezi wa Adar na Nissan yaani sawa na katikati ya mwezi Februari na March ya kalenda ya kawaida, Wayahudi huadhimisha sikukuu hii kutokana na amri ya Mordekai pamoja na malkia Esta kuwa ni lazima siku hii ikumbukwe. Esta 9: 29-32Ndipo malkia Esta, binti Abihaili, pamoja na Mordekai Myahudi, alipoandika kwa mamlaka yote kuithibitisha barua hii ya pili ya Purimu. Akapeleka barua kwa Wayahudi wote katika majimbo yote mia na ishirini na saba ya ufalme wake Ahasuero, maneno ya amani na kweli, ili kuzithibitisha siku hizo za Purimu kwa majira yake, kama Mordekai Myahudi na malkia Esta walivyoamuru, na kama walivyojiagizia juu yao wenyewe, na juu ya wazao wao, kwa habari ya kufunga na kilio.  Amri yake Esta ikayathibitisha mambo hayo ya Purimu; ikaandikwa katika kitabu” Ni kutokana na agizo hilo ndio mpaka leo Wayahudi huadhimisha sikukuu iitwayo PURIM au PURI wakimaanisha siku waliyopigiwa KURA au Kupitishiwa MSWAADA wa kuuawa Lakini kwa neema ya Mungu wakaokolewa. Siku ya Purim ni siku ya furaha sana kwa Wayahudi, wao hushangilia na kufurahi na kuruka ruka na kucheza ngoma na kunywa divai, Lakini katika masinagogi na ibada huwa ni wakati wa kusomwa kwa kitabu cha Esta.
Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia mambo muhimu yafuatayo:-

·         Sababu na Mpango wa kuangamizwa kwa Wayahudi.
·         Utaratibu wa Sheria na tamaduni za kiamedi na kiajemi.
·         Kuingia kwa mfalme Kinyume cha sheria.

Sababu na Mpango wa kuangamizwa kwa Wayahudi.

Ni muhimu kufahamu kuwa Kitabu cha Esta ni mojawapo ya kitabu ambacho kiliandikwa kuonyesha Msimamo wa kiimani wa wayahudi waliokuwa Uhamishoni, wakati huu wayahudi waliokuwa uhamishoni huko Babeli maisha yao na imani yao kwa Mungu wa kweli ilikuwa imani kali sana na hawakutaka kuleta mchezo na msimamo wao wa kiimani katika Mungu wa kweli wa Israel, walikuwa wamejifunza madhara makubwa ya kumuacha Mungu hata kwa sekunde moja, hivyo walishikamana na Mungu wao kwa uthabiti hata pamoja na kuwa mbali na Israel, Kisa na sababu ya kutaka kuangamizwa kwao kinaashiria wazi kuwa ulikuwa ni mpango wa Ibilisi, ili kufuta Historia ya kuwepo kwa Mungu, kisa au sababu inaanzia kwa mtu mmoja aliyeitwa Hamani ambaye alipandishwa Cheo na Mfalme kuamuru watu wote walio chini yake wamsujudie Esta 3:1-4Baada ya hayo mfalme Ahasuero alimwongezea cheo Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, akampandisha, akamwekea kiti chake juu ya maakida wote waliokuwapo pamoja naye. Nao watumishi wote wa mfalme, walioketi mlangoni pa mfalme, wakainama na kumsujudia Hamani, maana ndivyo alivyoamuru mfalme kwa habari zake. Bali Mordekai hakuinama, wala kumsujudia. Basi watumishi wa mfalme walioketi mlangoni pa mfalme wakamwambia Mordekai, Mbona wewe waihalifu amri ya mfalme? Ikawa, waliposema naye kila siku asiwasikilize, wakamwarifu Hamani, ili kuona kama mambo yake Mordekai yatasimama; maana alikuwa amewaambia ya kuwa yeye ni Myahudi.”  Unaweza kuona maandiko yanaonyesha sababu ya kisa cha wayahudi kuchukiwa ilikuwa ni tamaa na ubinafsi wa mtu mmoja tu kutaka Heshima na kuabudiwa, wakati mwingine migogoro mikuwa ya kitaifa au taasisi inaweza kuanza kwa chuki ya mtu mmoja tu, kwa maslahi yake na tamaa zake akaingiza wengine katika mgogoro mkubwa, ni Chuki ya hamani dhidi ya Mordekai ndio iliyopelekea Hamani kutaka kuwaangamiza Wayahudi wote, Esta 3:5-15Hata Hamani alipoona ya kwamba Mordekai hainami wala kumsujudia, alighadhibika sana.  Akaona si shani kumtia mikono Mordekai peke yake; maana wamemjulisha kabila yake Mordekai; kwa hiyo Hamani alitaka kuwaangamiza Wayahudi wote waliokuwa wakikaa katika ufalme wote mzima wa Ahasuero, yaani, watu wake Mordekai. Basi mwezi wa kwanza, ndio mwezi wa Nisani, mwaka wa kumi na mbili wa mfalme Ahasuero, wakapiga Puri, yaani kura, mbele yake Hamani; siku kwa siku, na mwezi kwa mwezi, hata mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari. Basi Hamani akamwambia mfalme Ahasuero, Kuna taifa moja waliotawanyika na kukaa mahali mahali katikati ya mataifa walioko katika majimbo yote ya ufalme wako. Nao sheria zao zimefarakana na sheria za kila taifa; wala hawazishiki amri za mfalme; kwa hiyo haimpasi mfalme kuchukuliana nao. Basi, mfalme akiona vema, na iandikwe kwamba waangamizwe; nami nitalipa talanta kumi elfu za fedha mikononi mwao watakaosimamia shughuli hiyo, waziweke katika hazina ya mfalme. Ndipo mfalme alipoivua pete yake mkononi, akampa Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi. Kisha mfalme akamwambia Hamani, Hiyo fedha umepewa, na watu pia, fanya uonavyo vema. Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza; na barua zikaandikwa, kama vile Hamani alivyoagiza vyote, kwa maakida wa mfalme, na maliwali waliokuwa juu ya kila jimbo, na wakuu wa kila taifa; kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; zikaandikwa kwa jinsi la mfalme Ahasuero, na kutiwa muhuri kwa pete yake. Barua zikapelekwa kwa mikono ya matarishi mpaka majimbo yote ya mfalme kuwaangamiza Wayahudi wote, na kuwaua, na kuwafisha, vijana kwa wazee, watoto wachanga na wanawake pia, siku moja, yaani, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili ndio mwezi wa Adari; na kuyachukua mali yao kuwa nyara.  Nakili ya andiko, ya kupigwa mbiu katika kila jimbo, ilitangazwa kwa mataifa yote wawe tayari siku ile ile.Matarishi wakaondoka wakaenda haraka kwa amri ya mfalme; kukapigwa mbiu huko Shushani ngomeni. Mfalme na Hamani wakaketi ili kunywa divai; bali mji wa Shushani ukafadhaika” Mpango huu ulikuwa ni mpango mbaya sana haukuwa na tofauti na kile alichokifanya “Adolf Hittler” ambaye yeye alifanikiwa kuwaua wayahudi wengi sana Duniani, ni jambo lenye kushangaza kuwa wakati mwingne shetani anaweza kukuza na kutekeleza chuki kubwa isiyokuwa na sababu maalum kwa watu wa Mungu, wanatheolojia wanaiita chuki hii kuwa ndio chuki ya ajabu iliyomkuta Yesu Kristo aliyeuawa na watu aliowatendea Mema, Mfalme alikuwa amesahau na wala hajui kuwa Mordekai alikuwa ni afisa usalama wa ngazi ya juu kabisa aliyefanikiwa kuokoa Maisha yake alipotaka kuuawa na sasa bila kuelewa amekubaliana na hamani na kupitisha sheria mbaya zaidi isiyoweza kutanguliwa ili kuwaangamiza wayahudi bila kufikiri Esta 2:21-23Ikawa siku zile, Mordekai alipokuwa akiketi mlangoni pa mfalme, wawili katika wasimamizi wake mfalme, Bigthana na Tereshi, wangoje mlango, walighadhibika, wakataka kumpelekea mikono mfalme Ahasuero. Basi Mordekai akapata kulijua jambo hilo, naye akamjulisha Esta, malkia; naye Esta akamwambia mfalme habari hiyo kwa jina la Mordekai. Na jambo hilo lilipochunguzwa, na hakika ikapatikana, hao wote wawili wakatundikwa juu ya mti. Hayo pia yakaandikwa katika kitabu cha taarifa mbele ya mfalme.”

Pamoja na wema huu na ulioweza kuwekwa katika taarifa Mfalme hakuona kuwa Mordekai na jamii yake ya Wayahudi kama watu waliokuwa na maana na alikubali waangamizwe ni muhimu kufahamu kuwa hapa ilikuwa imebaki siku ya kupigwa kura tu kuwa ni lini wayahudi watauawa lakini mswada ulikuwa umekwisha kupitishwa na kwa mujibu wa sheria za kiamedi na kiajemi jambo hili lisingeliweza kutanguliwa kwa namna yoyote, ili tuweze kufahamu vema hebu tuangalie desturi zao zilikuwaje katika kipengele kifuatacho.

Utaratibu wa Sheria na tamaduni za kiamedi na kiajemi.

Kwa mujibu wa Historia ya kibiblia Sheria za Uamedi na uajemi katika desturi yao zilikuwa zikipitishwa au zikiamriwa hakukuwa na kurudi nyuma kwa namna yoyote na ni vigumu hata mfalme mwenyewe kuweza kuitangua sheria na desturi iliyopitishwa naye msimamo wa aina hii ulithibitika wazi na lilikuwa ni jambo la fedhea na aibu kubwa sana kwa mfalme kugeuka nyuma ilionekana kama mfalme huyu sio mwenye moyo thabiti na imara na ni mfalme kigeugeu kutengua sheria kungeweza kumfanya mfalme asiaminike na watu wagepoteza imani naye japokuwa bado mfalme alikuwa ndio mwenye mamlaka ya mwisho na mwenye uwezo hata wa kutangua lolote kwa manufaa yake na taifa lake, Jambo hili liliwafunza Israel kuwa thabiti katika kutunza uadilifu wao kwa Mungu, hata ingawa walikutwa na hatari za kuishi katika mazingira magumu na yenye maamuzi kama hayo ya kushangaza.

-          Daniel 6: 12Ndipo wakakaribia, wakasema mbele ya mfalme katika habari ya ile marufuku ya mfalme; Je! Hukuitia sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba? Mfalme akajibu, akasema, Neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza KUBADILIKA.”

-          Esta 1:19Basi mfalme akiona vema, na itoke kwake amri ya kifalme, nayo iandikwe katika sheria za Waajemi na Wamedi ISITANGUKE, ya kwamba Vashti asifike tena mbele ya mfalme Ahasuero; na umalkia wake mfalme ampe mwingine aliye mwema kuliko yeye.”

Unaweza kuona kuwa sheria zao zilikuwa kali na za kidikteta zisizoweza kutanguaka au kubadilishwa, hata hivyo kutokana na chuki na wivu kwa wayahudi wakati mwingine sheria za aina hii zilipitishwa ili kushindana na watu wa Mungu kama Daniel, pia Shadrak, Meshak na Abdednego, pia katika kitabu cha esta yanamkuta Mordekai na jamii nzima ya kiyahudi, ambao sasa wamepitihwa kuwa wauawe katika muswada huu wa sheria za watu hawa ambazo ni ngumu mno kuiztanbgua au kzibadilisha.

Ni muhimu kufahamu kuwa katika ulimwengu wa Kiroho, hali kadhalika ni vigumu kubadilisha jambo ambalo Mungu ameliamuru lipite au lisipitishwe, na sio hivyo tu lakini hata upande wa shetani ni vigumu kwake kuwa kigeugeu, yeye anapodhamiria kuleta uharibifu kwako huwa hatanii, anapokusudia kukushuhsia hukumu huwa hana muda wa kupoteza, mtu mwenye chuki anapokuendea kwa mganga na wachawi ili kukuharibu ni vigumu kwa Mchawi kurudi nyuma na kugeuka, ikiwa shetani amekukusudia kukuharibia, kukuaibisha,anahakikisha kuwa anakubana katika kiwango ambacho huwezi kuchomoka mpaka akubamize, atakufuatilia bila kurudi nyuma bila kubadilika bila kuitangua dhamira yake, jambo hili lilitambulika vema kwa wayahudi pia kuhusu makusudio mabaya ya Waamedi na waajemi dhidi yao. Maandiko wakati wote yanatuonyesha kuwa ni Mungu pakee anayeweza kuubadili Moyo wa mfalme kama apendavyo  Mithali 21:1Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa Bwana; Kama mifereji ya maji huugeuza po pote apendapo.”  Unaona Biblia inatuthibitishia kuwa ni Mungu peke yake ndiye anayeweza kuugeuza moyo wa mfalme kokote apendapo yaani atakapo Mungu, lakini sio hivyo tu ni kwake yeye ndiko tunakoweza kukata rufaa ya sheria za kipuuzi zilizopitsihwa kwa misingi ya uonevu wa Ibilisi ni kwanamna gani tunaweza kufanya hilo ni kwa kuingia kwa mfalme kinyume cha sheria.

Kuingia kwa Mfalme kinyume cha sheria.

Kwa vile Esta na Mordekai walikuwa wanazifahamu sheria za waamedi na waajemi pamoja na desturi zao kwamba halikuwa jambo rahisi kuweza kuwaponya wayahudi na kujikoa wao wenyewe na mauti iliyokuwa imekusudiwa kuwakumba, Esta na Mordekai walikuwa wamekwisha kuwa na ujuzi kuwa wakati wowote unapokutana na jambo gumu ni maombi na pamoja na kufunga na kuomba tu ndio ilikuwa njia pekee ya kuweza kutangua sheria za kubahatisha za wanadamu, Esta aliamini katika nguvu ya kufunga na kuomba, watu wengi na dini nyingi zinaamini katika nguvu ya kufunga na kuomba hata na mimi ninaamini kuna nguvu katika kufunga na kuomba Yesu pia aliamini katika nguvu ya kufunga na kuomba yeye mwenyewe Yesu akasema kuna na mambo mengine hayawezekani isipokuwa kwa kufunga na kuomba Mathayo 17 :21[Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]Yesu alikuwa akimaanisha  kuwa kuna nguvu kubwa katika maombi yenye kujitoa kwa jambo lolote lile kama maombi ni hafifu matokeo yake yanakuwa hafifu na kama maombi ni yenye bidii matokeo yake yanakuwa makubwa sana, Esta alikuwa sio anakabiliwa na sheria na Muswada uliokuwa umepitishwa tu lakini kama malikia ambaye angeweza kuingia kwa mfalme kuwaombea wayahudi rehema yeye mwenyewe alikuwa anakabiliwa na desturi isiyotanguliwa ambayo nayo ingemgharimu kifo, kulikuwa na sesturi nyingne ya kiajemi ya kuwa malikia kama hujaitwa kwa mfalme na kisha ukaingia kwa mfalme bila kibali chake ungehukumiwa kufa, isipokuwa tu kama utapata neema na kunyooshewa fimbo ya dhahabu, kupitia nguvu ya maombi haya Esta alipata kibali kwa mfalme na kunyooshewa fimbo ya dhahabu na kupata neema ya kuwaombea wayahudi na kuitangua sheria iliyokuwa imewekwa Esta 4:15-16Basi Esta akawatuma ili wamjibu Mordekai, Uende ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani, mkafunge kwa ajili yangu; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala mchana, nami na wajakazi wangu tutafunga vile vile; kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie.” Ni baada ya tukio hili ndipo Mungu alipoleta wokovu kwa  wayahudi na Mordekai na matendo yake mema mema Mordekai yaliyokuwa yamekaliwa yalikumbukwa na msalaba aliokuwa ameandaliwa kutundikwa ulitundikwa Hamani adui yake na adui wa Wayahudi  Esta 9:1-21 . “Hata ulipofika mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, siku yake ya kumi na tatu, amri ya mfalme na mbiu yake ilipowadia kutekelezwa; ambayo siku ile adui za Wayahudi walitumaini kuwatawala, bali kumebadilika kinyume, hata Wayahudi waliwatawala wale waliowachukia; siku ile ile Wayahudi wakakusanyika mijini mwao katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero ili kuwatia mikono wale watu waliowatakia hasara; wala asiweze mtu kuwazuia, kwa kuwa hofu yao imewaangukia watu wote. Nao maakida wa majimbo, na majumbe, na maliwali, na wale waliofanya shughuli ya mfalme, waliwasaidia Wayahudi; kwa sababu hofu ya Mordekai imewaangukia. Maana Mordekai alikuwa mkuu nyumbani mwa mfalme, na sifa yake imevuma katika majimbo yote, kwa kuwa huyo Mordekai amezidi kukuzwa. Basi Wayahudi wakawapiga adui zao wote mapigo ya upanga, na machinjo, na maangamizo, wakawatenda kama wapendavyo wale waliowachukia. Hata huko Shushani ngomeni Wayahudi wakawaua watu mia tano, na kuwaangamiza.  Wakawaua na Parshandatha, na Dalfoni, na Aspatha, na Poratha, na Adalia, na Aridatha, na Parmashta, na Arisai, na Aridai, na Waizatha, wana kumi wa Hamani bin Hamedatha, adui ya Wayahudi; walakini juu ya nyara hawakuweka mikono. Siku ile mfalme akaletewa hesabu ya hao waliouawa huko Shushani ngomeni. Mfalme akamwambia malkia Esta, Wayahudi wamewaua watu mia tano hapa Shushani ngomeni na kuwaangamiza, pamoja na wana kumi wa Hamani, je! Wamefanyaje basi katika majimbo ya mfalme yaliyosalia! Basi, una nini uombalo? Nawe utapewa; ama unayo haja gani tena? Nayo itatimizwa. Ndipo Esta aliposema, Mfalme akiona vema, Wayahudi walioko Shushani na wapewe ruhusa kufanya tena kesho sawasawa na mbiu ya leo, na hao wana kumi wa Hamani watundikwe juu ya mti ule. Mfalme akaamuru vifanyike vivyo hivyo, mbiu ikapigwa huko Shushani, wakawatundika wale wana kumi wa Hamani. Basi Wayahudi wa Shushani wakakusanyika tena siku ya kumi na nne pia ya mwezi wa Adari, wakawaua watu mia tatu huko Shushani; walakini juu ya nyara hawakuweka mikono. Nao Wayahudi wengine waliokaa katika majimbo ya mfalme walikusanyika, wakazishindania maisha zao, wakajipatia raha mbele ya adui zao, wakawaua waliowachukia, watu sabini na tano elfu; walakini juu ya nyara hawakuweka mikono. Hii ndiyo siku ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari; na siku ya kumi na nne ya mwezi huo wakapumzika, wakaifanya kuwa siku ya karamu na furaha. Lakini Wayahudi wa Shushani walikusanyika siku ya kumi na tatu ya mwezi huo, na siku ya kumi na nne pia; na siku ya kumi na tano ya mwezi uo huo wakapumzika, wakaifanya kuwa siku ya karamu na furaha. Kwa sababu hii Wayahudi wa vijijini, wakaao katika miji isiyo na boma, huishika siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, kuwa siku ya furaha na karamu, sikukuu ya kupelekeana zawadi. Basi Mordekai aliyaandika mambo hayo; naye akapeleka barua kwa Wayahudi wote waliokaa katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero, waliokuwa karibu na waliokuwa mbali, kuwaonya wazishike siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, na siku ya kumi na tano yake, mwaka kwa mwaka,” Unaona kilio cha wayahudi kilibadilika kuwa furaha adui za wayahudi waliuawa wao, msalamba walikuwa wameutundika hamani kwaahiji ya Mordekai alitundikwa yeye mwenyewe, Heshima aliyokuwa akiitafuta Hamani ilipotea na Heshima ile alipewa Mordekai Esta 5:14, 6:1-2, Mfalme hatimaye aliongeza wema wake kwa wayahudi Esta 7. Mungu na kuongezee wema ikiwa utakubali kujitia chini yake na kuutafuta uso wake kwa kufunga.

Ndugu yangu mpendwa muamini Mungu yaamini maandiko huitaji kuhangaika dhidi ya adui zako ndani yako uko uwezo, unaozidi nguvu ya wadhalimu, unaozidi nguvu ya wachonganishi unaozoidi nguvu ya ibilisi, unaozidi nguvu za wanafiki, unaozidi nguvu za waganga na wachawi, unaozidi nguvu za maadui zako iko furaha uliyoandaliwa unayo ya kuingia kwa mfalme kinyume cha sheria na kukata rufaa, pale nguvu zetu zoinapopungua, pale kanisa linap[olemewa pale ibilisi na adui anapotukalia langoni iko dawa moja tu kwa kufunga na kuomba tutaweza kumsambaratisha adui na kupata kibali kwa mfalme na kutangua sheria yoyote inayotenda kazi kinyume na maisha yako; ni kwa kufunga na kuomba ni kwa kufunga na kuomba ni kwa kufunga na kuomba tunaweza kulete furaha ya kweli katima maisha yetu asomaye na afahamu.

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni: