Jumatatu, 5 Machi 2018

Njia za kurahisisha Maisha yako!


Andiko la Msingi: Mathayo 6:25 -27Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao?  Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja?”



Na maisha ya nini kuyasumbukia!

Nyakati hizi tulizonazo ni nyakati ambazo ni ngumu sana kimaisha, watu wengi sana wanaishi maisha ya huzuni yasiyo na furaha na yaliyojawa na wingi wa migandamizo ya maisha, siku inaweza kupita na ukajikuta hakuna ulichokamilisha kila wakati unafikiri labda utapata siku nzuri ambayo unaweza kukamilisha maswala yako yote muhimu unayotaka kuyakamilisha,  lakini mambo sivyo yalivyo, watu wengi wa kizazi hiki wamekuwa busy na maisha lakini ni wachache wanaofurahia kuwa busy kwao, kwa mtindo huu utaweza kugundua kuwa Maisha yanakuwa magumu na muda unakuwa hautoshi, Hakuna wa kulaumiwa muda wako unapokuwa hautoshi, unapokuwa umekusudia kufanya mambo mengi lakini mwisho wa siku unajikuta hakuna hata moja ulilolikamilisha, unaweza hata kumlaumu Mungu unaweza kufikiri kuwa muda hautoshi kumbuka  hivyo sivyo maisha yanavyopaswa kuwa; Yesu alikusudia watu wake waishi maisha mepesi yasiyo na mizigo mizito wala hofu wala kongwa la utumwa! 

Ni muhimu kufahamu kuwa Yesu alikusudia watu waishi maisha yaliyojaa pumziko na raha nafsini mwao na ili mtu aweze kufurahia maisha hana budi kuzingatia maswala muhimu ya kibiblia na mafundisho ya Yesu juu ya kuishi kwa raha bila usumbufu wa aina yoyote Mathayo 11:28-29Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;”

Kama mungu alikusudia watu wawe na furaha wasiwe na Mizigo, wasielemewe wasisumbuke kwanini watu wengi wanasumbuka leo na kuishi maisha ya kujichosha? Yesu alihoji ni nani kwenu ambaye kwa kujisumbua aweza kuongeza kimo chake hata mkono mmoja? Mungu anatufundisha katika neno lake jnsi na namna ya kuishi kwa furaha? Yafuatayo yatatusaidia kuishi maisha rahisi na kujikuta tunafurahi bila kuelemewa na lolote

1.       Fanya jambo moja tu kwa wakati.

Mathayo 6: 24 “Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.Ingawa mstari huu unaweza kuwa na maana pana nyingi lakini moja ya maana rahisi anayotaka kuikazia Yesu Kristo ni kuwa kuna mafanikio ya kufanya jambo moja kwa wakati mmoja kuliko kutamani kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, watu wengi wanaojichosha katika maisha na kujikuta muda hautoshi na wanaamka wakiwa wamechoka ni wale wanaotaka kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, akili yetu inapokuwa katika jambo lingina na mikono yetu ikitenda kitu kingine maisha yatakuwa magumu na tunaweza kumaliza siku hakuna ulichokamilisha!

Wataalamu wa mapishi wanasema kuwa unaweza kutenganisha kiini cheupe cha yai na kiini cha manjano cha yai na ukavitumia kwa matumizi fulani ya mapishi yaliyo mazuri, lakini hata hivyo utapoteza muda na ni vigumu kuliko kama utavuruga yai lote na kulila moja kwa moja.

Mwanafunzi amabaye anakusudia kufanya au kujisomea masomo mengi kwa wakati mmoja wa maandalizi hawezi kuwa na ufanisi kama yule anayefanya moja baada ya jingine, mwanafunzi ambaye atakuwa na simu ya mkononi, yenye kila kitu huku anasoma atapoteza mwelekeo hata kama ni mzuri kiasi gani, mwanafunzi anayeshiriki Mapenzi huku anasoma, atapoteza mwelekeo, kwa kanuni ya Yesu huwezi kutumikia mabwana wawili, fanya jambo moja kwanza Mungu hataki ujisumbue Wafilipi 4:6 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.” Jaribu kufanya jambo moja tu kwa wakati mmoja na utaweza kuona unafanikiwa na kuyafurahia maisha, na kisha pumzika. Hutachanganyikiwa wala hutalala na stresses.

Mungu aliifurahia kazi yake ya uumbaji aliyokuwa akiifanya na kuikamilisha kwa siku ile ile, kila siku alitimiza wajibu wa uumbaji fulani na alipokamilisha alifurahi na kupumzika Mwanzo 1:3-4, Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru. Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema;” Mungu akatenga nuru na giza. kila kitu alikuwa akikikamilisha na kujipongeza siku moja baada ya nyingine hivyo kwa siku sita ulimwengu uliumbwa

2.       Usiogope kuhusu kesho?.

Mathayo 6:34 “Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.” Mungu anatutarajia tumuamini katika kiwango ambacho hatutaogopa kuhusu kesho itakuwaje, aliwafundisha wana wa Israel kutokuogopa maisha yao kwamba itakuwaje kesho kwani kila siku alikuwa amewaandalia riziki yao, hii haimaanishi kuwa tusiweke akiba, hii haimaanishi kuwa tutumie vibaya kile tulicho nacho, hapana hapa Mungu anatufundisha kwamba tusiogope kesho itakuwaje, watu wanaoogopa kesho itakuwaje wanaishi maisha ya taabu sana  nay a kujitesa na hivyo wanaweza kukosa raha, Mungu aliwafundisha Israel Jangwani kwamba mtu hataishi kwa mkate tu, bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu, Kutoka 16: 15-21Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao BWANA amewapa ninyi, mle. Neno hili ndilo aliloagiza BWANA, Okoteni ninyi kitu hicho kila mtu kama ulaji wake ulivyo; kichwa pishi, kama hesabu ya watu wenu ilivyo; ndivyo mtakavyotwaa, kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani mwake.Wana wa Israeli wakafanya hivyo, wakaokota wengine zaidi, wengine kupungua. Nao walipoipima kwa pishi, yeye aliyekuwa ameokota kingi hakubakiwa na kitu, na yeye aliyekuwa ameokota kichache hakupungukiwa; wakaokota kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa. Musa akawaambia, Mtu awaye yote asikisaze hata asubuhi. Lakini hawakumsikiza Musa; wengine miongoni mwao wakakisaza hata asubuhi, nacho kikaingia mabuu na kutoa uvundo; Musa akawakasirikia sana. Basi wakaokota asubuhi baada ya asubuhi, kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa; na hapo jua lilipokuwa ni kali, kikayeyuka.”

Watu wengi sana wanahofu kuhusu maisha ya baadaye kuwa yatakuwaje kiasi ambacho wanaweza kusahahu kuhusu mapenzi ya Mungu, jambo hili ni hatari, kujiandaa kwa maisha ya baadaye ni kwa muhimu sana, na biblia haikatazi hilo lakini ni uzembe mkubwa kumsahahu Mungu kwaajili ya maisha haya kwa sababu yeye ndiye mwenye kuutunza uzima wetu, watu wanaoogopa kesho pia wanakuwa wachoyo Luka 12: 15-26 “1Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu.  Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.Akawaambia wanafunzi wake, Kwa sababu hiyo nawaambia, Msisumbukie maisha yenu, mtakula nini; wala miili yenu, mtavaa nini. Kwa kuwa maisha ni zaidi ya chakula, na mwili ni zaidi ya mavazi. Watafakarini kunguru, ya kwamba hawapandi wala hawavuni; hawana ghala wala uchaga, na Mungu huwalisha. Bora ninyi mara nyingi kuliko ndege!  Na yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Basi, ikiwa hamwezi hata neno lililo dogo, kwa nini kujisumbua kwa ajili ya yale mengine?” Unaona Mungu hataki tusumbukie maisha Mungu hataki tuwe na hofu kuhusu kesho yeye ndiye anayejua maisha yetu na hivyo anataka tuwe na furaha, furahia kila unachokikamilisha kwa siku ile,  na usiogope kuhusu kesho itakuwaje Mungu anajua.

3.       Rizika na ulichonacho.

Waebrania 13:5-6 “.Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?”

Tamaduni za dunia ya sasa zinafikiri kuwa na furaha ni kuwa na vitu vingi au kuwa na kila kitu lakini ukweli umedhihirika kuwa wale wanaoishi maisha rahisi ndio wenye furaha kubwa duniani kuliko wengine wote, utafiti umethibitisha kuwa watu wanaoishi muda mrefu zaidi kuliko wote duniani ni Mabedui wanaishi jangwani hawa wanauwezo wa kufikisha hata miaka 200 ya maisha yao, sababu kuu ni kuwa wameridhika na maisha yao, Maisha yamebadilika sana kwa sababu watu wameharibu tamaduni zao kuanzia namna mtu anapozaliwa mpaka namna mtu anavyozikwa. leo hii hata kuzika mtu imekuwa ni gharama kubwa sana, Mungu anataka watu wafurahie maisha na hivyo ni muhimu kuridhika na kile ulicho nacho Wafilipi 4:11-13Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo. Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.” Kumbuka kuwa sio dhambi kuwa na vitu lakini ni dhambi kumezwa na tamaa, ni kwa sababu ya kutokuridhika watu wengi wameingia katika mateso makubwa sana na hata kufarakana na imani, mioyo tetu inapofungamanisha na maswala ya vitu vya dunia inaweza kutuletea maumivu makubwa sana na tukafikia ngazi ya kutokuyafurahia maisha 1Timotheo 6:6-10Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.”  Kama tutajifunza kumfurahia Mungu kwa kile alichotupa tutaishi maisha ya raha na amani, hakuna sababu ya kushindana na awaye yote, kila mtu ana maisha yake na hatuwezi kufanana kwa sababu ninachikiwaza sio unachokiwaza, ninachoamini sio unachokiamini kwa hiyo kila mmoja aepuke maisha ya mashindano na ajifunze kuridhika na kile alicho nacho. Watu wakiishi hivi hakutakuwa na wizi na maisha yatakuwa mazuri.

4.       Muweke Mungu mbele.

Mathayo 6: 31-33 “Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Yesu anatupa kanuni nyingine ya namna ya kuishi bila kuhangaika au kusumbuka anatoa maangizo ya aina mbili kwa wakati mmoja kumtafuta Mungu kwanza na haki yake na mengine yote tutazidishiwa;  maana yake ni nini? kama tuko duniani kwa makusudi ya Mungu na kila tunachokifanya ni kwaajili ya kutimiza kusudi hilo basi ni vema tukamtafuta Mungu kwanza, yaani “kama Mungu ni chanzo cha kila kitu ni vema tukaacha kutafuta au kuhangaika na kila kitu na tukampata  Yeye aliye chanzo” Chakula na mavazi pamoja na mahitaji yetu mengine ni jukumu la kawaida la baba mwenye upendo, Yesu anaweka wazi kuwa ni afadhali kuhangaika na kumtafuta yeye au kumsikiliza yeye inaweza kuwa muhimu zaidi kuliko kusumbuka na maswala mengineyo Luka 10:38-42 “Ikawa katika kuenenda kwao aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie.Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.”
Unaona mtu anapochagua kumsikiliza Mungu amechagua fungu lililojema, ni muhimu sana kupata ujuzi kuhusu nini ni mapenzi ya Mungu na kuyafanya kwa wakati huo, na ni muhimu kuwa na ushirika na Mungu kwanza kabla ya kuanza kusumbuka na kutimiza kusudi lake, wakati mwingine tunaweza kusumbuka bila mafanikio kwaajili ya kujishughulisha kutafuta mafanikio bila kusikia neno la mfanikishaji

Kwa akili zetu wakati mwingine tunaweza kusumbuka sana kufanya mambo bila kufanikiwa lakini kwa kutii na kufuata au kuomba uongozi wa Mungu tunaweza kupata mafanikio makubwa katika jambo lilelile ambalo limeshindikana mwanzoni Luka 5:4-7 “Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki. Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu. Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama.” Unaona tunapomtanguliza Mungu na kumtii yeye kwanza kwa kuwa yeye ndio chanzo cha mambo yote hutupa maelekezo stahiki yanayoweza  kutupa mafanikio tunayoyataka    

Biblia inaonyesha kuwa kama tukimtumikia Mungu yaani kumuabudu na kumuweka yeye Mstari wa mbele atatuponya Magonjwa, ataondoa utasa, na kutimiza siku zako za kuweko duniani Kutoka 23:25-26 “Nanyi mtamtumikia BWANA, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza.” Torati inaonyesha kuwa kuna Baraka nyingi sana kama watu wataitii sauti ya Mungu na kumuweka yeye mbele, Neno la Mungu moja tu kwetu linaweza kubadilisha kabisa mfumo wa maisha yetu na tukaishi maisha ya furaha.

5.       Sahahu yaliyopita.

Wafilipi 3:13 “Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele;”
               
Moja ya kikwazo kikubwa sana katika maisha ya watu wengi kinachowakosesha wasiweze kuwa na furaha au kusumbuka ni kutokusahau Historia, ingawa Historia ni nzuri lakini wote tutakubaliana kuwa ziko historia nyingine haziwezi kutupa maisha yenye furaha, kwa msingi huo Biblia inatutaka tusahau yakiyo nyuma na kuchuchumilia yaliyo mbele, historia yetu ya maisha ya nyuma ni ya kuitupa.

Mara kadhaa wana wa Israel walijikosesha Baraka za Mungu kwa sababu walikumbuka Misri katika inchi ya utumwa na kudharau uhuru ambao Mungu alikuwa amewazawadia, Mungu alikuwa amewapa ukombozi mkuu lakini mara kwa mara walimuhuzunisha kwa kukosa shukurani Hesabu 14:1-4 “Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule. Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri?  Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri.” Kutokana na kuwa na hali ya manunguniko na kukosa shukurani kwa Mungu ugumu uliongezeka katika maisha yao safari ya jangwani ilikuwa ndefu na yenye misiba Mingi inakisiwa kuwakila siku waisrael 70 walikufa, ni lazima tusahahu tulikotoka na nkuendelea kumtumikia Mungu kwa nguvu na kumuabudu yeye kwa nguvu, kamwe tusiangalie nyuma kule alikotutoa Bwana Luka 17:32-33 “Mkumbukeni mkewe Lutu. Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote atakayeiangamiza ataiponya.” Yesu alikumbusha juu ya kujikana nafsi na kuendelea kumcha yeye na kutimiza wajibu wetu kwa Mungu bila kugeuka nyuma, Yesu alitumia mfano wa mkewe Lutu, na kuonya juu ya jkutaka kuiokoa nafsi yetu, Yesu anazungumzia juu ya kujihurumia na kutokujikana kwa Mungu, wengi kwaajili ya kujihurumia wamepoteza Baraka na uwepo wa Mungu Paulo Mtume alikuwa ni mtume aliyepata neema kubwa ya Mungu kuliko mitume wote, alipelekwa mpaka mbigu ya tatu na kupewa mafunuo makubwa sana hata hivyo hakuwahi kuridhika wala kuangalia historia yake yeye alijua kuwa furaha yake inapatikana kwa kuendelea kusahau yaliyo nyuma na kuchuchumilia yaliyo mbele, aliwataka kanisa la kolosai kuangalia Wakolosai 3:1-2 “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.   Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi.” Ni Muhimu kujifunza kuangalia mbele ondoa uchungu wote na hakikisha kuwa unasamehe wote waliokukosea uchungu una tabia ya kutufungia Baraka na uwepo wa Mungu hivyo kusahau  yaliyopita ni pamoja na kusamehe wale waliotukosea Hesabu 4:13 “Nao watayaondoa hayo majivu madhabahuni; na kutandika nguo ya rangi ya zambarau juu yake;” Kusamehe na kuondoa kila aina ya uchungu ni sawa na kazi za makuhani ambao walitakiwa kuhakikisha wanaondoa majivu katika madhabahu ili moto uendelee kuwaka.

6.       Fanya kila kitu kwa utukufu wa Mungu.

1Wakoritho 10:31 “Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.” Moja ya mambo ambayo yanawaumiza watu wengi sana duniani ni kufanya mambo kwa mashindano au kwa kutaka kushindana au kujilinganisha, watu wengi sana wanakosa amani na kusumbuka katika maisha haya kwa sababu wanajilinganisha na wengine, hawafanyi mambo kwa nia njema nia ya Mungu kutukuzwa.

Mara zote mashindano yameleta kiburi, yameleta dharau yameleta maumivu na majuto,siku hizi kuna mashindano mpaka ya kutoa sadaka tabia ya aina hii imeumiza wengi Mungu hatahukumu kile tunachokifanya bali atahukumu kwa nini tumefanya, ni muhimu nia yetu nadhamiri zetu za kutenda lolote tunalolitenda ikawa ni kwaajili ya Mungu kutukuzwa, kamwe neno la Mungu haliitii moyo kufanya jambo kwa mashindano, Wafilipi 2:3Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.” Unaweza kuona tabia ya kushindana ikiingia kanisani au kwa watu wa Mungu inaweza kuleta vita na magomvi hata kuomba kwetu kunaweza kugeuzwa kuwa kuomba kubaya kuomba kwa tamaa kwa sababu ya mshindano na sio kwaajili ya utukufu wa Mungu Yakobo 4:1-3 “Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu? Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi! Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.” Kama kila kitu tukifanyacho hakifanyiki kwaajili ya utukufu wa  Mungu maisha yetu yatakuwa yenye uchungu mwingi, na hata kuomba kwetu kutaathiriwa tutakuwa tunaomba kwa sababu ya kutaka kitu fulani kwa tamaa na sio kwaajili ya utukufu wa Mungu kanuni kuu ya msingi hapa ni kufanya kila jambo kwaajili ya utukufu wa Mungu.

7.       Jifunze kukataa.

Mathayo 5:37 “Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.”

Yakobo 5:12 “Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho chote; bali ndiyo yenu na iwe ndiyo, na siyo yenu iwe siyo, msije mkaangukia hukumu.”

Nyakati za Biblia hususani wakati wa Yesu Kristo wayahudi wengi sana walikuwa wakiogopa sana kuapa au kujifunga katika ahadi yoyote kwa kumuhusisha Mungu hii ni kwa sababu waliogopa kuwa endapo watashindwa kutimiza ahadi basi watakuwa wamejifunga kwa Mungu, hivyo hawakutaka kumuhusisha Mungu ili hata wakivunja ahadi wasiweze kuwajibika kwa Mungu wakijua kuwa hawafungwi, swala hili lilipunguza uaminifu wa watu na kuwanyima raha, tatizo la kutokuwa wakeli linawatesa sana hata wafrika wengi wanaogopa kusema Ndio au sio inayotoka Moyoni wanaweza kusema Ndio lakini kumbe moyonimwao hawako radhi na hilo, au wanaweza kusema sio kumbe kuna kitu wanakihitaji

Neno la Mungu kupitia Yesu Kristo linatutaka tuwe watu wenye maamuzi yaliyo wazi tu kuwa kama jambo ni ndio iwe ndio kivitendo maana sisi ni wa Mungu na kama jambo sio iwe sio kwa maana sisi ni watu wa Mungu hakuna sababu ya kupiga siasa, wengi wanaogopa kusema sio kwa wake za, mabosi wao kwa kuogopa kuuwaumiza mioyo lakini baadaye wanajuta kwa nini sikukataa au kwanini nilikubali Heri kama ningelikataa

Kutokusema HAPANA ni tatizo kubwa sana la kisaikolojia wana saikoloji wanaliita tatizo hilo “CANT SAY NO SYNDROM  wengi wanaoogopa kusema hapana wanafikiri kwamba labda wao sio Bora sana, hivyo wanafikiri kuwa wanaweza kuwapendeza wengine kwa kuwakubalia kila wanachokitaka, au wanafikiri kuwa wanapaswa kuwatumikia wengine na kuwa wema sana kiasi wakisema hapana watawaudhi, au anafikiri kuwa akisema hapana atakataliwa, wanafikiri kuwa watu watawapenda wakiwakubalia kila kitu, wanadhani kusema hapana ni swala la kikatiali sana, wanafikiri kuwa wataonekana kuwa wabinafsi wakisema hapana, au wanafikiri kuwa wengine hawatakiwi kuona yeye kuwa ni mkaidi, na tafasiri mbaya ya maandiko heri wenye upole maana watairithi inchi.

Biblia imatupa kweli muhimu au kanuni ya muhimu ya kuyafurahia maisha ambayo ni kusema Ndio au Hapana
Vijana wengi wa kiume wakiombwa na wasichana kuwa wapenzi inakuwa vigumu kwao kusema hapana kwa sababu ya kuwaonea huruma biblia inatutaka tuseme hapana kwa hapana kweli na ndio kwa ndio kweli na sio kutoa maelezo.
Kusema hapana sio swala rahisi, wengi wanaogoipa kusema hapana, kiroho kutokusema hapana kuna maanisha kuwa tuna roho ya woga; 2Timotheo 1:7 “Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.Kutokana na woga huu hususani woga wa kuumiza wengine kwa sababu kusema hapana mara nyingi kunaumiza wengine watu wengi sana wamejikuta au tumejikuta katika matatizo ya aina mbali mbali
·         Dereva anaweza akawa anaendesha kwa kasi sana na kuhatarisha maisha lakini ukaogopa kumwambia punguza mwendo
·         Jambo linaweza likawa liko kinyume cha Sheria.lakini kwa vile wengine wanafanya ukashidwa kusema hapana
·         Jambo linaweza kuwa hukubaliani nalo, lakini kwa vile wengi wamelikubali hutaki kuonekana tofauti

Inahitajika roho ya ujasiri, bila kuumiza moyo wa mtu mwingine kusema Hapana tofauti na mtazamo wake, au wakati mwingine kusema hapana hata kama jambo hilo litamuumiza muhusika Daniel 3:13-18Basi Nebukadreza akatoa amri kwa hasira na ghadhabu, waletwe hao Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Basi wakawaleta watu hao mbele ya mfalme. Nebukadreza akajibu, akawaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu? Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha”.  Shadraka na Meshaki na Abednego walijifunza kusema hapana katikakweli waliweza kumkatalia mfalme katika kile walichokiamini, kuwa kwao na kwa imani yao hakiko sahihi.

1Wafalme 21: 1-4 “Ikawa baada ya hayo, Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria. Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake. Nabothi akamwambia Ahabu, Bwana apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu. Basi Ahabu akaenda nyumbani kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno lile aliloambiwa na Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba zangu. Akajilaza kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula.”  Unaona Nabothi pia alikuwa mtu mwenye ujasiri wa kusema hapana katika jambo alilokuwa anaamini kuwa ni sahihi kwa utamaduni wake na kwa mujibu wa mila zao.

Unaona kutokuwa na uwezo wa kusema hapana ni tatizo linalowasumbua watu wengi duniani kwani wanaogopa kuumiza wengine, wengi tunaogopa kusema hapana kwa viongozi wetu, kwa wake zetu, kwa waume zetu, kwa wachumba zetu kwa wazazi wetu na kadhalika na kutokna na hayo wengi wameishi maisha ya kinafiki au kufanya mambo yanayoweza kumiza nafsi zao.

Matendo ya Mitume 5:27-29 “Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza, akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.” 

8.       Kataa kufanya jambo ambalo hutalikamilisha.

Luka 14:28-32Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza. Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali.”

Maandiko yanatufundisha kuwa ni tabia ya uungu kuanza jambo na kulikamilisha, Mungu hana kigeugeu kama ameanza kazi njema mioyoni mwetu atahakikisha kuwa anaikamilisha Wafilipi 1:6  “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu;”
Yesu Kristo pia anaitwa katika maandiko mwanzilishi na mwenye kutimiza imani yetu hii inatukumbusha kuwa Mungu akianza jambo huwa haliachii njiani kwa msingi huo ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa hauishii njiani katika maswala ya aina mbalimbali, kuanzia maswala ya imani, miradi na lolote lile unalolianzisha ni muhimu kuhakikisha kuwa haliishiinjiani, “Mtu atakumbukwa kwa kila alichokamilisha na sio kwa kile alichojaribu”    Waebrania 12:2 “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.”

Mambo mengi sana hapa duniani yanahitaji subira na uvumilivu, hakuna kitu kinaweza kutokea mara moja tu vingine vinahitaji subira, watu wasio na subira hawawezi kukamilisha mambo, kukomaa kwetu pia kiroho na kitabia na mwenendo hakutokei kwa usiku mmoja tu ni mchakato, watu wengi wanaoshindwa kiroho ni wale ambao wanatarajia kitu kitokee mara moja tu na kufanikiwa kwa haraka yako mambo buna budi kuwa na subira na uvumilivu. Usianzishe jambo kwa msukumo wa kihisia tu hapana lazima ufikiri kwa kina namna utakavyokamilisha mambo uwe na busara kama mkulima ambaye analima na kisha anasubiria mavuno yake Yakobo 5:10-11 “Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu. Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.”

9.       Mwachie Mungu Mizigo yako.

Ni muhimu kufahamu kuwa ingawa tunamwanini Mungu na tunamwamini Yesu, hii haimaanishi kuwa hatutapitia changamoto za namna mbalimbali, madamu tumo ulimwenguni bado tunaweza kupitia dhiki na vikwazo na changamoto mbalimbali Yohana 16:33 “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” Kwa nini Yesu anatuambia kuwa duniani tunayodhiki? Yesu hataki tushangae tunapopitia majaribu ya namna mbalimbalia hata kama sisi ni watu wake, Majaribu yanatufundisha kuvumilia na kutuleta katika ukamilifu Yakobo 1:2-4 2. “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno”. Hata hivyo pamoja na faida hizo za majaribu Mungu anataka tumtike yeye fadhaa zetu zote

Zaburi 55:22 “Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza, Hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele.”

 1Petro 5:6-7 “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;  huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.”

Kwa mujibu wa maandiko hayo tunapata picha iliyo wazi  na ukweli kuhusu Mungu, kwamba yeye hatatuacha tuondoshwe, yaani ahatatuachan tuaibike, Yeye anatujalia Mungu anaonyesha wazi kuwa anauwezo wa kutusaidia kiakili, kihisia, kiroho na kimwili, yuko tayari na anauwezo kama alivyoahidi katika neno lake Mungu huruhusu au hufanya mambo yote yaani magumu na mepesi kwa kusudi la kutupatia mema sisi tumpendao Warumi 8:28 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.” Kwa msingi huo ni muhimu kupeleka kwake kila jamnbo linalosumbua maisha yetu, hata wakati wa shida na tunapokuwa na mashaka hata ya kumuamini yeye , Yeye hubaki mwaminifu na anafanya kazi kwaajili yatu kwa utukufu wake, na ametuahidi kuwa hatatuacha tujaribiwe kuliko tuwezavyo na kwamba kwa kila jaribu ameweka mlango wa kutokea  kwa msingi huo hatatuangusha kama ilivyo ahadi yake 1Wakoritho 10:13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.”

10.   Wewe ni zaidi ya Mshindi.

Warumi 8:37 “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.”
Wakristo wengi sana wanaufahamu mstari huu au andiko hili na hulitaja mara kwa mara kwa tafasiri mbalimbalui, kwa mujibu wa somo hili kuwa zaidi ya mshuindi maana yake ni kuwa na ujasiri kwa jambo lolote linalokutokea katika maisha kupitia Yesu Kristo au kwaajili ya Yesu Kristo tunaweza kabisa kulikabili kwa ushindi, hatutaogopa na hatutaishi kwa kusumbuka kwa vile tunajua hata kama tutazamishwa katika hali ngumu kwa kiwango chochote kila Kristo atatusaidia na kutupa ushindi

Mungu ni mkuu kuliko Hofu zetu, kwa msingi huo maandiko yanatutaka

1.       Tuwe na furaha hata wakati wa taabu na masumbufu ya ulimwengu huu tukijua ya kuwa Mungu anaweza kuyatumia kuzalisha uvumilivu, kututunza, kuwa na tabia njema , sifa njema na matumaini Warumi 5:3-4Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini;”              
2.       Kwamba tutumia masumbufu yetu kama njia ya kutukuza kiimani na ya kutupeleka katika ngazi nyingine ya kumtumaini Mungu kuliko njia zetu na akili zetu kwaajili ya utukufu wake Mithali 3:5-6 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.”               
3.       Njia ya kutii na kutufanya tuwe wema kwa kila mtu, uwezo wa kusamehe na kuchukuliana Waefeso 4:31-32 “Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.”     
4.       Kwaajili ya kutuleta katika toba ili tushughulikie dhambi zetu na kuwa wakeli na kuishi maisha ya haki 1Yohana 1:9 “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.”

Maombi:
Mungu baba uliyejaa upendo na fadhili, rehema zako zina wakuchao kizazi na hata kizazi, ututie nguvu wakati wote wa masumbufu ya ulimwengu huu, uwe pamoja nasi hata tuwapo na mashaka, utupe kujificha kwako wakati wa shida namasumbufu ya ulimwengu huu, utupe kukukimbilia wewe ili tusiaibike kweli wanaokutumaini wewe ni kama mlima wa Sayuni  hawatatikisika milele, Katika jina la Yesu Kristo mwana wako ninakurudishia sifa na utukufu, Amen

Na mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima

Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni: