1Samuel 24:9-13 “Daudi akamwambia Sauli, Kwa nini unasikiliza maneno ya watu wasemao, Tazama, Daudi anataka kukudhuru? Tazama, leo hivi macho yako yameona jinsi Bwana alivyokutia mikononi mwangu pangoni, na watu wengine wakaniambia nikuue; lakini nikakuacha; nikasema, Sitaki kuunyosha mkono wangu juu ya bwana wangu; kwa maana yeye ni masihi wa BWANA.Tena, baba yangu, tazama, tafadhali, tazama upindo wa vazi lako mkononi mwangu; maana ikiwa nimeukata upindo wa vazi lako, nisikuue, ujue, na kuona ya kuwa hakuna uovu wala kosa mkononi mwangu, wala sikukukosa neno; ingawa wewe unaniwinda roho yangu ili kuikamata. Bwana atuamue, mimi na wewe, na Bwana anilipizie kisasi changu kwako; lakini mkono wangu hautakuwa juu yako. Kama vile walivyosema watu wa kale katika mithali yao, Katika waovu hutoka uovu; ila mkono wangu hautakuwa juu yako.”
Utangulizi:
Wote tunakuwa tunakumbuka
jinsi ambavyo Sauli alikuwa anamfuatilia sana Daudi akiwa na majemadari zaidi
ya 1000 makomandoo walioteuliwa ili ikiwezekana aweze kumuangamiza hata ingawa
Daudi hakuwahi kumkosea kitu Sauli
1Samuel 24:1-2 “Ikawa,
Sauli aliporudi baada ya kuwafuatia Wafilisti, aliambiwa ya kwamba, Daudi yuko
katika nyika ya Engedi. Ndipo Sauli akatwaa watu elfu waliochaguliwa katika
Israeli wote, akaenda kumtafuta Daudi na watu wake juu ya majabali ya
mbuzi-mwitu.”
Wakati majeshi ya Sauli
na Sauli mwenyewe wanaelekea huko Engedi kumtafuta Daudi, Sauli aliingia katika pango mojawapo peke yake na Daudi
alikuwako katika Pango lile pamoja na watu wake na akawa ana nafasi ya kumuua,
watu wake Daudi walimshawishi na kumtia moyo Daudi ammalize Sauli na inaonekana wazi kuwa huenda kulikuwa na
neno la kinabii kwa Daudi kuwa siku mmoja Bwana atamtia adui yake chini ya
mikono yake na anaweza kumfanya kama atakavyo, Hata hivyo Daudi alikataa
kufanya jambo hilo na badala yake aliukata upindo tu wa vazi la Sauli na hata
kwa tendo hilo moyo wake ulimshitaki.
1Samuel 24:3-7 “Akafika
penye mazizi ya kondoo kando ya njia, na huko kulikuwa na pango; Sauli akaingia
ndani ili kuifunika miguu. Na Daudi na watu wake walikuwa wakikaa mle pangoni
ndani sana. Nao watu wa Daudi wakamwambia, Tazama, hii ndiyo siku ile
aliyokuambia Bwana, Angalia, nitamtia adui yako mikononi mwako, nawe utamtenda
yo yote utakayoona kuwa mema. Basi Daudi akainuka, akaukata upindo wa vazi lake
Sauli kwa siri.Lakini halafu, moyo wake Daudi ukamchoma, kwa sababu amekata
upindo wa vazi lake Sauli. Akawaambia watu wake, Hasha! Nisimtendee bwana
wangu, masihi wa BWANA, neon hili, kuunyosha mkono wangu juu yake,kwa maana
yeye ni masihi wa BWANA. Basi Daudi akawazuia watu wake kwa maneno hayo,
asiwaache kumwondokea Sauli. Kisha Sauli akatoka pangoni, akaenda zake.”
Baadaye Daudi akasimama
mbali na kumuita Baba yangu akamwonyesha pindo hilo kama ushahidi kwamba hakuwa
na nia ya kumuua kama jinsi alivyokua anafikiri au watu wanavyomdanganya na
kisha akampa somo kutoka katika mithali ya wazee isemayo Katika waovu hutoka
uovu! Na hili ndilo somo tunalojifunza leo, tutajifunza somo hili Katika
waovu hutoka uovu kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya maneno Katika waovu hutoka uovu!
·
Mifano ya watu waliofanya uovu na kupata uovu
·
Katika waovu hutoka uovu!
Maana ya maneno Katika waovu hutoka uovu!
Maneno katika waovu
hutoka uovu yanatokana na mithali ya wazee wa Kiebrania ambayo inasomeka
“Mershaim yetse resha” ambayo kwa kiingereza “Out of the wicked comes
wickedness” kwa Kiswahili Katika waovu hutoka uovu, yakimaanisha kuwa
matendo mabaya yanatoka kwa wabaya wenyewe, au mtu anayekusudia mabaya atapatwa
na mabaya yeye mwenyewe, kwa hiyo maana yake mtu awaye yote mwenye nia ya
kumdhuru mtu mwenye haki atadhurika mwenyewe, ni Kama wazee walikuwa wanasema
kuwa atendaye uovu ataangamia kwa uovu wake mwenyewe, Kauli hii pia ina pande
kuu nne zinazoshikamana ambazo zote zinatufundisha kitu kinafanana
-
Kimjazacho mtu ndicho kimtokacho, Kile kilichojaa katika moyo wa mtu ndicho kinachojitokeza
katika maneno na matendo, ni kama Daudi alikuwa anamwambia Sauli kuwa kama mimi
ningekuwa mwovu ungekuwa umekwishakufa leo, kwa kuwa sina uovu moyoni mwangu na
ndio maana sikuweza kukufanyia maovu, Yesu alifundisha kuwa mtu mwovu katika
hazina mbovu ya moyo hutoa yaliyo maovu
Luka 6:44-45. “kwa
kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi
tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu. Mtu mwema katika hazina njema ya
moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake
hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.”
-
Kila anayechimba shimo atatumbukia mwenyewe, Usemi huu naonyesha kuwa unapoandaa njama au mpango
wa kumfanyia ndugu yako jambo baya unatengeneza sumu kwenye mikono yako
mwenyewe, ambayo mwishoni itakugusa wewe mwenyewe, maandiko yanaonyesha hivyo
na shuhuda za kibiblia zinaonyesha kuwa watu wengi ambao walikuwa wakiwaandalia
wenzao au waliowafanyia wenzao mambo mabaya walipatwa na mabaya pia
Mithali 26:26-27 “Ingawa
chuki hufunikizwa kwa hila; Uovu wake utadhihirika mbele ya kusanyiko.
Achimbaye shimo atatumbukia mwenyewe; Naye abingirishaye jiwe litamrudia.”
Zaburi 7:14-16 “Tazama,
huyu ana utungu wa uovu, Amechukua mimba ya madhara, amezaa uongo. Amechimba
shimo, amelichimba chini sana, Akatumbukia katika handaki aliyoifanya! Madhara
yake yatamrejea kichwani pake, Na dhuluma yake itamshukia utosini.”
-
Yeye aushikaye upanga ataangamia kwa upanga, Usemi unamaanisha pia watu wanaotegema njia za uasi
nguvu au za kikatili kutatua changamoto au wanaojipatia mamlaka au madaraka kwa
nguvu wataangamia kwa jinsi ile ile ya nguvu uasi na ukatili, Daudi hakutaka
kuingia madarakani kwa njia ya kumwaga damu au kuua mtu mwingine kama Mungu
amempaka mafuta basi yeye mwenyewe ndiye atakayemuweka madarakani, lakini vile
vile kile anachikifanya Sauli kutaka kumzima kwa kutumia upanga basi kitamrudia
mwenyewe kwani naye atazimwa na upanga wa watu wengine Japokuwa usemi huu
ulitamkwa na Yesu lakini unamfanano mkubwa na kile tunachojifunza hapa kuwa
katika waovu hutoka uovu!
Mathayo 26:51-52 “Na
tazama, mmoja wao waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono wake, akaufuta
upanga wake, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. Ndipo Yesu
akamwambia, Rudisha upanga wako mahali pake, maana wote waushikao upanga,
wataangamia kwa upanga.”
1Samuel 31:1-6 “Basi
Wafilisti wakapigana na Israeli; nao watu wa Israeli wakakimbia mbele ya
Wafilisti, wakaanguka wameuawa katika mlima wa Gilboa. Wafilisti wakamfuatia
sana Sauli na wanawe, Wafilisti wakawaua Yonathani, na Abinadabu, na Malkishua,
wana wa Sauli. Tena vita vilikuwa vikali sana juu ya Sauli, na wapiga upinde
wakampata; hata akafadhaika sana kwa sababu ya wapiga upinde. Ndipo Sauli
akamwambia yule mchukua silaha zake, Futa upanga wako, unichome nao; wasije
watu hawa wasiotahiriwa wakanichoma, na kunisimanga. Lakini huyo mchukua silaha
zake akakataa; kwa sababu aliogopa sana. Basi Sauli akautwaa upanga wake,
akauangukia. Na mchukua silaha zake alipoona ya kuwa Sauli amekufa, yeye naye
akauangukia upanga wake, akafa pamoja naye. Hivyo Sauli akafa, na wanawe
watatu, na mchukua silaha zake, na watu wake wote pamoja siku iyo hiyo.”
-
Ogopa mtu anayesema anamwachia Mungu – Daudi hakukubali ushauri wa watu wala unabii
uliomhakikishia kuwa iko siku Bwana atamtia adui yako mikononi mwako nawe utamtenda
uonalo jema badala yake alisema Bwana na ahukumu kati yangu na yako lakini
mkono wangu hautakuwa juu yako, aliomba Mungu amlipie kisasi, kwa hiyo usemi
katika waovu hutoka uovu maana yake kwa kuwa Mungu ni Mungu wa haki ukimkabidhi
yeye njama na nia za watu waovu na kumwachia basi hukumu ya Mungu ni tamu zaidi
ya hukumu ya kibinadamu
1Samuel 24:12-15 “Bwana
atuamue, mimi na wewe, na Bwana anilipizie kisasi changu kwako; lakini mkono
wangu hautakuwa juu yako. Kama vile walivyosema watu wa kale katika mithali
yao, Katika waovu hutoka uovu; ila mkono wangu hautakuwa juu yako. Na mfalme wa
Israeli ametoka ili kumfuatia nani? Unamwinda nani? Ni kuwinda mbwa mfu, au
kiroboto. Basi Bwana atuamue, akatuhukumu mimi na wewe, akaone, akanitetee neno
langu, akaniokoe na mkono wako.”
Mifano ya watu waliofanya uovu na kupata uovu
Biblia imejaa mifano ya
watu kadhaa ambao historia ya maandiko inaonyesha kuwa walikuwa wakatili na
watu waliofanyia wengine mabaya au kuwalipa mabaya badala ya mema, maandiko
yanaonyesha jeuri zao na mwisho wao namna ulivyokuwa, walijisahahu na kufanya maovu
na maovu hayo yakawarudia mifano hii inatuthibitishia kweli katika wawovu
hutoka uovu na sisi tusiwaige, wala tusijaribu kuwatendea watu wengine uovu
yasije yakatukuta:-
Nabali – Daudi na timu
yake walimtendea wema walipokuwa nyikani na wachungaji wa Nabali, Mtu huyu
alikuwa tajiri sana Daudi na timu yake waliwahakikishia usalama walipokuwa
nyikani, waliwalinda wachungaji wake dhidi ya uonevu na mifugo yao na huenda
taarifa zilimfikia mzee huyu, hata hivyo siku moja wakati Daudi akiwa na shida
aliagiza kuomba mikate yeye na timu yake waliokuwa nyikani na kumkumbusha
Nabali wema wote waliomtendea mtu huyu hata hivyo kwa ujeuri alijifanya
hatambui mchango wowote wa Daudi wala hamjui hata Daudi mwenyewe
1Samuel 25:4-11 “Basi
Daudi akasikia huko nyikani ya kuwa Nabali alikuwa katika kuwakata manyoya
kondoo zake. Daudi akatuma vijana kumi, Daudi naye akawaambia hao vijana,
Kweeni mwende Karmeli, na kumwendea huyu Nabali ili mnisalimie; na hivi ndivyo
mtakavyomwambia huyu aishiye salama, Amani na iwe kwako, na amani nyumbani
mwako, na amani kwao wote ulio nao. Nami sasa nimesikia ya kuwa una watu
wanaokata manyoya kondoo zako; haya! Wachungaji wako wamekuwa pamoja nasi, wala
hatukuwadhuru, wala hawakukosa kitu wakati wote walipokuwako huko Karmeli.
Waulize vijana wako, nao watakuambia; basi na wakubaliwe vijana hawa machoni
pako; maana tumekujia katika siku ya heri; uwape, nakusihi, cho chote
kitakachokujia mkononi, uwape watumwa wako na mwanao Daudi. Basi walipofika
vijana wake Daudi, wakamwambia Nabali sawasawa na maneno hayo yote kwa jina la
Daudi, kisha wakanyamaza. Naye Nabali akawajibu wale watumishi wa Daudi,
akasema, Huyu Daudi ni nani? Na mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumwa
wengi wanaomtoroka kila mtu bwana wake! Basi mimi je! Nitwae mkate wangu, na
maji yangu, na machinjo yangu niliyowachinjia hao watu wangu wakatao manyoya
kondoo zangu, na kuwapa watu ambao siwajui wametoka wapi?”
1Samuel 25:36-38 “Kisha
Abigaili alimjia Nabali; na tazama, alikuwa amefanya karamu nyumbani mwake,
kama karamu ya kifalme; na moyo wake huyo Nabali ukafurahiwa ndani yake, kwa
maana amelewa kabisa. Kwa sababu hiyo hakumwambia neno, dogo wala kubwa, hata
kulipopambazuka. Ikawa asubuhi, divai ilipokuwa imemtoka Nabali, mkewe alimwambia
mambo hayo, na moyo wake ukafa ndani yake, akawa kama jiwe. Tena ikawa, yapata
siku kumi baadaye, Bwana alimpiga huyo Nabali, hata akafa.”
Adoni-Bezeki – Alikuwa
mfalme katili sana mara kadhaa alipokuwa akipigana na wafalme wa mataifa
mengine akiwakamata wafalme wale na alikuwa akiwakata vidole gumba huu ndio
ulikuwa mfumo wake wa mateso na ukatili na jumla ya wafalme aliowahi kuwakata
vidole gumba wanafikia 70, ukataji wa dole gumba ilikuwa njia ya kikatili sana
ya zamani ya kumpunguzia mtu uwezo wa kufanya kazi zozote za kijeshi kwa sababu
asilimia 50% ya utendaji wa mkono hutegema kidole gumba kwa hiyo mtu akitaka
kukuharibiwa uwezo wako wa kutenda kazi alikukata kidole gumba (an ancient
method of Physical incapacitation) lakini pia njia ya kudhalilisha hadharani
public humiliation ona
Waamuzi 1:4-7 “Yuda
akakwea; naye Bwana akawatia Wakanaani na Waperizi mkononi mwao; nao wakawapiga
huko Bezeki watu elfu kumi. Wakampata huyo Adoni-bezeki huko Bezeki; wakapigana
naye, nao wakawapiga Wakanaani na Waperizi. Lakini Adoni-bezeki akakimbia; nao
wakamwandamia na kumshika, wakamkata vyanda vyake vya gumba vya mikono na vya
miguu. Adoni-bezeki akasema, Wafalme sabini, waliokuwa wamekatwa vyanda vyao
vya gumba vya mikono na vya miguu, waliokota chakula chao chini ya meza yangu;
kama nilivyofanya mimi, Mungu amenilipa vivyo. Wakamleta Yerusalemu naye akafa
kuko.”
Farao – Mfalme
katili sana aliyekuwa na mipango ya hila ya kuwaangamiza wana wa Israel kwa
kuwaua watoto, kuamuru watoto wa kiume wa kiebrania watupwe kwenye maji ya mto
Nile, na kuwatesa wana wa Israel kwa utumwa mzito sana, yeye na majeshi
yake yote siku yao ya kufa walikufa katika maji ya bahari ya Shamu
Kutoka 1:22 “Kisha huyo Farao akawaagiza watu
wake, akisema, Kila mtoto mwanamume atakayezaliwa mtamtupa mtoni, na kila mtoto
mwanamke mtamhifadhi hai.”
Kutoka 14:27-28. “Musa
akaunyosha mkono wake juu ya bahari, na kulipopambazuka, bahari ikarudi kwa
nguvu zake; Wamisri wakakimbia mbele yake; na BWANA akawakukutia mbali hao Wamisri
kati ya bahari. Yale maji yakarudi yakafunikiza
magari na wapanda farasi, hata jeshi lote la Farao lililoingia katika bahari
nyuma yao; hakusalia hata mtu mmoja.”
Ahabu na Yezebeli – Walikuwa na tamaa kwaajili ya shamba la mizabibu la
Nabothi, Alipowakatalia kwa sababu za kisheria kwamba Torati haikuruhusu kuuza
urithi, walikasirika na Yezebeli alitengeneza mashahidi wa uongo na wakamuua
Naboth mtu huyu mwenye haki aliuawa kwa kupigwa mawe kwamba eti amemtukana
mfalme na Mungu, na mbwa waliiramba damu yake, jambo hili lilimuudhi Mungu na
Mungu aliwahukumu viongozi hao kuwa pale ambapo Mbwa waliramba damu ya Nabothi
na ya kwao itarambwa na kwa hakika ikawa vilevile ilivyosemwa!
1Wafalme 21:19 “Ondoka,
ushuke, ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko katika
shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukia ili alitamalaki. Ukamwambie,
ukisema, Bwana asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki? Nawe utamwambia, kusema,
Bwana asema hivi, Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa
watairamba na damu yako, naam, damu yako.”
2Wafalme 9:32-36 “Akainua
uso wake kulielekea dirisha, akasema, Aliye upande wangu ni nani? Matowashi
wawili watatu wakachungulia. Akasema, Mtupeni chini. Basi wakamtupa chini; na
damu yake ikamwagika nyingine juu ya ukuta, na nyingine juu ya farasi, naye
akamkanyaga-kanyaga. Alipoingia, akala, na kunywa; kisha akasema, Haya!
Mwangalieni mwanamke huyu aliyelaaniwa, mkamzike; kwa maana ni binti mfalme.
Wakaenda ili kumzika; lakini hawakuona kitu ila kifuvu cha kichwa chake, na
miguu yake, na vitanga vya mikono yake.Basi wakarudi, wakampasha habari.
Akasema, Hili ndilo neno la Bwana, alilolinena kwa kinywa cha mtumishi wake
Eliya, Mtishbi, kusema, Katika kiwanja cha Yezreeli mbwa wataila nyama ya
Yezebeli.”
Hamani maarufu kama adui wa Wayahudi alimchukia sana Mordekai na Wayahudi wote na pamoja
na kupitisha mswada ili kwamba Wayahudi wote wakaao Shushani Ngomeni na nchi
nzima wauawe, pia alikuwa akiandaa msalaba kwa kusudi la kumtundika Mordekai
lakini katika namna isiyoweza kuelezeka Mungu aliingilia kati na mtu huyu
alitundikwa yeye katika msalaba ule ule aliomwandalia mwenzake!
Esta 7:8-10. “Kisha mfalme akarudi kutoka katika
bustani ya ngome hata mahali pa karamu ya divai. Ikawa Hamani amejitupa chini
penye kitanda alipokuwapo Esta. Mfalme akasema, Namna gani! Je! Atamfanyia
malkia jeuri hata machoni pangu nyumbani mwangu? Na neno lilipotoka kinywani
mwa mfalme, wakamfunika uso Hamani.Ndipo aliposema Harbona, msimamizi-wa-nyumba
mmojawapo wa wale waliohudhuria mbele ya mfalme, Tazama, basi, mti wa mikono
hamsini urefu wake, Hamani aliomwekea tayari Mordekai, ambaye alinena vema kwa
ajili ya mfalme, upo umesimamishwa nyumbani kwa Hamani. Mfalme akasema,
Mtundikeni juu yake. Basi wakamtundika Hamani juu ya mti aliomwekea tayari
Mordekai. Ghadhabu ya mfalme ikatulia.”
Maandiko haya ndugu yangu
na dada yangu ni ushahidi tosha ya kuwa Katika waovu hutoka uovu, Mungu
anatufundisha hapo ya kuwa tujihadhari sana kuwatendea watu mabaya na pia
tukitendewa sisi Mungu muhukumu mwenye haki yupo na atahukumu kwa haki nadhani
hukumu ya Mungu ni bora sana kuliko hukumu za wanadamu.
Zaburi 7:11-13 “Mungu
ni mwamuzi mwenye haki, Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku. Mtu asiporejea
ataunoa upanga wake; Ameupinda uta wake na kuuweka tayari; Naye amemtengenezea
silaha za kufisha, Akifanya mishale yake kuwa ya moto.”
Katika waovu hutoka uovu!
Ni muhimu kujikumbusha
tena na tena Mungu anataka tuwe watu wa haki duniani, tuache kiburi na kujiamini
kulikopitiliza kutakakotufanywa tuwe na uonevu kwa wengine neno la Mungu
limetuthibitishia kauli ya Daudi iliyonenwa na wazee kuwa ni kweli katika waovu
hutoka uovu, Mungu hadhihakiwi chochote apandacho mtu hapa duniani atavuna unapowatendea
wengine ukatili nawe utatendewa au watoto wako watatendewa acha uovu wako
Wagalatia 6:7-8 “Msidanganyike,
Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.Maana
yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye
apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.”
Sauli alipoelezwa maneno
yale ni kweli kuwa alilia na kukiri kuwa Daudi ni mwenye haki kuliko yeye,
lakini hata hivyo hakuacha uovu wake kwani muda mfupi baadaye aliendelea
kumsaka Daudi kwa kusudi lile lile la Kumwangamiza tena sasa akaongeza kikosi
kutoka askari 1000-3000 kumsaka Daudi,
1Samuel 24:16-20 “Ikawa,
Daudi alipokwisha kumwambia Sauli maneno hayo Sauli alisema, Hii ndiyo sauti
yako, Daudi, mwanangu? Naye Sauli akapaza sauti yake, akalia. Akamwambia Daudi,
Wewe u mwenye haki kuliko mimi; maana wewe umenitendea mema, nami nimekutenda
mabaya.Nawe umeonyesha leo jinsi ulivyonitendea mema, kwani Bwana aliponitia
mikononi mwako, hukuniua. Maana mtu akimwona adui yake, je! Atamwacha aende
zake salama? Basi Bwana na akulipe mema kwa haya uliyonitendea leo.Na sasa,
angalia, najua ya kuwa hakika utakuwa mfalme, na ufalme wa Israeli utafanyika
imara mkononi mwako.”
1Samuel 26:2 “Basi hao Wazifi wakamwendea Sauli
huko Gibea, wakasema, Je! Yule Daudi hakujificha katika kilima cha Hakila,
kuelekea Yeshimoni? Basi Sauli akaondoka, akashuka nyikani kwa Zifu, naye
alikuwa na watu elfu tatu, wateule wa Israeli, pamoja naye, ili kumtafuta Daudi
katika nyika ya Zifu.”
Mikono ya Sauli tayari
ilikuwa imejaa damu, kwa kuwaua makuhani wa Bwana huko Nobu wapatao 85 pamoja
na wanawake na watoto wakati akimtafuta Daudi, mtu huyu alikuwa tayari amejaa
maovu na alitaka kuendeleza uovu wake kama desturi yake, mikono yake ilikuwa
imejaa damu ya makuhani 85 na familia zao ambao hawakuwa waovu
1Samuel 22:17-21. “Kisha
mfalme akawaambia askari walinzi waliosimama karibu naye Geukeni, mkawaue hao
makuhani wa Bwana, kwa sababu mkono wao u pamoja na Daudi, na kwa sababu
walijua ya kuwa amekimbia, wasiniarifu. Lakini watumishi wa mfalme walikataa
kunyosha mkono na kuwaangukia makuhani wa Bwana.Basi mfalme akamwambia Doegi,
Geuka wewe, ukawaangukia hao makuhani. Basi Doegi, Mwedomi, akageuka,
akawaangukia makuhani, akaua siku ile watu themanini na watano wenye kuvaa
naivera ya kitani. Kisha akaupiga Nobu, mji wa makuhani, kwa makali ya upanga,
wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, na ng'ombe, na punda, na kondoo. Na
katika wana wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, akaokoka mtu mmoja tu, aliyeitwa
jina lake Abiathari, akamkimbilia Daudi. Naye Abiathari akamweleza Daudi ya
kwamba Sauli amewaua makuhani wa Bwana.”
Unapata picha jinsi gani
Sauli alikuwa mwovu, kwaajili ya kumsaka Daudi aliua watu wengi sana na hivyo
kuifanya mikono yake kuwa yenye Damu, muuaji huyu hatimaye, Mungu akawa hajibu
maombi yake kwa njia zote na akajikuta anawaendea wenye pepo, moyo wake haukuwa
na toba wala hakuwa imara kwa Bwana Mungu wake, Upanga wake aliouchomoa
kumtafuta Daudi ulimgeukia yeye mwenyewe na kumuua, na ufalme aliokuwa
akiulinda kwa damu ukachukuliwa na Daudi. Kwa Amani kweli Kila aushikaye upanga
ataangamia kwa upanga!
1Samuel 31:1-6 “Basi
Wafilisti wakapigana na Israeli; nao watu wa Israeli wakakimbia mbele ya
Wafilisti, wakaanguka wameuawa katika mlima wa Gilboa.Wafilisti wakamfuatia
sana Sauli na wanawe, Wafilisti wakawaua Yonathani, na Abinadabu, na Malkishua,
wana wa Sauli.Tena vita vilikuwa vikali sana juu ya Sauli, na wapiga upinde
wakampata; hata akafadhaika sana kwa sababu ya wapiga upinde. Ndipo Sauli
akamwambia yule mchukua silaha zake, Futa upanga wako, unichome nao; wasije
watu hawa wasiotahiriwa wakanichoma, na kunisimanga. Lakini huyo mchukua silaha
zake akakataa; kwa sababu aliogopa sana. Basi Sauli akautwaa upanga wake,
akauangukia. Na mchukua silaha zake alipoona ya kuwa Sauli amekufa, yeye naye
akauangukia upanga wake, akafa pamoja naye. Hivyo Sauli akafa, na wanawe
watatu, na mchukua silaha zake, na watu wake wote pamoja siku iyo hiyo”
Hitimisho!
Tunajifunza nini katika
somo hili Katika waovu hutoka uovu, tutende mema ndugu zangu, tuache kuwa
sababu ya mbegu mbaya, wakati wote tuilinde mioyo yetu na mambo maovu,
tumwambie Mungu atuumbie moyo safi kama alivyoomba Daudi, Daudi alikuwa mtu
mwenye Moyo safi na aliisikiliza dhamiri yake na kulitii neno la Mungu, Moyo
wake ulimchoma pale tu alipokata upindo wa vazi la Sauli na hakutaka
kujichukulia sheria mikononi je dhamiri yako hukuambia nini pale unapowatendea
wenzako yasiyo haki Je huoni hata dhamiri inakusuta? Unafanyaje kuhusu ushauri
wa rafiki zako? Daudi alishauriwa kuwa afanye kitu kwa sababu Mungu alimtia
Sauli katika mikono yake? Hata hivyo Daudi aliona aliachie jambo hilo katika
mikono ya Mungu mwenyewe tuwe makini na wanaotushauri na ushauri unaotusukuma
katika uovu, wivu, wizi, ulevi, ujambazi, ushirikina na chuki, heshimu uhai wa
wengine, familia zao na majukumu waliyo nayo, usikimbilie kunyoosha mkono wako
hata kama mtu huyo humpendi, jitafute katika tiba kwani kuacha na Mungu ni
jambo baya kuliko yote, ukipanda mbegu ya wema unapanda mbegu ya kudumu kwako
na uzao wako! Sauli kwa kuwa alichagua
upanga akafa kwa upanga, yeye na familia yake, Daudi alimchagua Mungu akawa
mfalme mkao wa moyo wetu ndio unaoamua uhusiano wetu kwa Mungu na Baraka zake!
Jilinde sana
Rev. Innocent Samuel Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.
