Jumatatu, 25 Februari 2019

Tukalia tulipoikumbuka Sayuni!

Zaburi 137: 1-4 “Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati yake Tulivitundika vinubi vyetu. Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni. Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika nchi ya ugeni?

 
Utangulizi: 
  
Kila mwanadamu katika maisha yake ana historia ambayo imejaa milima na mabonde katika mapito mbalimbali ya maisha, Ukimuuliza mtu swali akuelezee au akuandikie siku ambayo hatakuja kuisahau katika maisha yake kwamba siku ambayo ilimpa furaha kubwa sana (Golden Age) au siku ambayo aliwahi kuuzunika sana (Ashes Age) utaweza kugundua kwamba wengi wataandika siku zao ambazo hawatazisahahu katika maisha yao kutokana na huzuni na mapito mazito waliyoyapitia.
Wengine wataeleza siku yao wasioweza kuisahahu kama siku ya harusi yake, au siku ya msiba wa mtu wake aliye karibu, au siku timu yake ilipofungwa, au siku timu yake ilipopata ushindi, au siku alipopata kazi, au siku alipofukuzwa kazi, kila mmoja anaweza kuelezea siku yake ya huzuni za wakati wake wa furaha hii ni hali ya kawaida katika maisha ya mwanadamu, na ndio maana waswahili wanasema maisha ya mwanadamu yana milima na mambonde. Halii hii pia inaweza kugusa hata taifa fulani au bara fulani na kadhalika. 

Zaburi hii ya 137:1-9 imegawanyika katika sehemu kuu tatu. 

·         Mstari wa 1-4 inaelezea hali halisi ya huzuni waliyokuwa nayo wayahudi huko utumwani, walilia na walivitundika vinubi vyao juu ya miti kwa sababu wasingeliweza kuimba wimbo wa kumuabudu Mungu ugenini 

·         Mstari 5-6 inaelezea jinsi walivyojipa moyo na kujiapiza juwa haitakuja itokee waisahau Sayuni yaani Yerusalem yaani uwepo wa Mungu, na ni afadhali kusahahu mkono wa kulia au kuwa bubu kuliko kuisahai Sayuni 

·         Mstari 7-9 jamaa anaomba kwamba Mungu ashughulike na Babeli pamoja na Edomu ambao walishangilia kuangamia kwa Wayahudi na kuboibmolewa kwa Yerusalem    

Katika kifungu za Zaburi hii leo tunaweza kupata picha ya wana wa Israel waliorejea kutoka utumwani, ambao walishuhudia uzuri wa Taifa lao lilipokuwa chini ya uongozi wa Mungu na baadaye lilipoadhibiwa na kuruhusiwa kwenda utumwani 

Zaburi 137:1-4Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati yake Tulivitundika vinubi vyetu. Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni. Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika nchi ya ugeni?

Mwandishi wa zaburi hii japokuwa wengine wanadhani ni Yeremia lakini mimi bila shaka naamini atakuwa Ezra au mojawapo ya watu waliorejea kutoka uhamishoni  kwa sababu anajaribu kuelezea hali halisi waliyoipitia walipokuwa nje ya Israel yaani utumwani huko Babeli, na historia haionyeshi kuwa yeremia alikwenda uhamishoni Babeli kama ilivyo kwa Ezekiel na Daniel, kwani inasemekana huenda yeye Yeremia alikwenda Misri.  Ingawa nchi ya Babeli yaani Iraq na Iran ya leo zilikuwa na mito mkubwa na mizuri na yenye matawi mengi sana yaliyochangia taifa hilo kuwa na uwezo mkubwa wa kujitosheleza kwa chakula na umwagiliaji na ujenzi ulioruhusu maji kupita katikati ya majiji yao mito kama Mto Kebari, Mto Frati na mto Tigris na ustaarabu mkubwa na wa hali ya juu, Babeli ulikuwa mji wa kifahari sana ndio ulikuwa mji wenye bustani zinazoelea angani na kuingizwa katika moja ya maajabu saba ya kale ya dunia (The Seven wonders of the ancient world ) ukiacha pyramid la Chiops lililoko Gezer nchini Misri hata leo, Bustani na uzuri wa jiji la Babeli lilikuwa linashika nafsi ya pili kwa ajabu zake duniani, Mfalme Nebuchadnezar aliwahi kujisifia kuhusu ujenzi wa mji huu na akaadhibiwa na Mungu kwa kiburi chake akidhani kuwa alifanya kwa nguvu zake na utukufu wake  

Daniel 4:29-33 “Baada ya miezi kumi na miwili, alikuwa akitembea ndani ya jumba la kifalme katika Babeli. Mfalme akanena, akasema, Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi, uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu? Hata neno lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme, sauti ilikuja kutoka mbinguni, ikisema, Ee mfalme Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe; Ufalme huu umeondoka kwako. Nawe utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni; utalishwa majani kama ng'ombe, na nyakati saba zitapita juu yako, hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote. Saa iyo hiyo jambo hilo likatimizwa, likampata Nebukadreza; alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ng'ombe, na mwili wake ulilowa maji kwa umande wa mbinguni, hata nywele zake zikakua, zikawa kama manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege.” 

Unaweza kuona Babeli kulikuwa ni kuzuri sana kuliko hata Sayuni, lakini wana wa Israel walilia walipoikumbuka Sayuni kwanini? Unaweza kuwa na ndoa ya kifahari sana lakini huo sio uthibitisho wa furaha ya kweli, unaweza kuwa na kila kitu lakini kama Mungu hamo haiwezi hiyo kitu kukupa furaha ya kweli unaweza kuwa katika nchi iliyoendela sana lakini hili sio suluhisho la furaha ya kweli ya mwanadamu, unaweza kuwa na mume mzuri na mke mzuri lakini bila uwepo wa Mungu ni sawa na shamba la miwa karibu na shule ya msingi, wako watu wengi wanalia japokuwa wanaishi katika mageti, na nyumba nzuri, na magari mazuri si dhambi kuwa navyo lakini the best ni kuwa na uwepo wa Mungu, Mungu ndiye furaha yetu ya kweli, Elimu na ujuzi na maendeleo hayatupi guarantee ya uhakika wa furaha yetu.

Kwa nini walilia walipoikumbuka sayuni?

Wayahudi waliketi na kutafakari, kwamba wao ingawa walikuwa katika nchi nzuri sana yenye mito mingi, Machozi yaliwatoka kwa sababu sasa walikuwa wametengwa mbali na uwepo wa Mungu, walipotafakari juu ya Nyumba ya Mungu iliyokuwako Sayuni yaani Yerusalem, walipokumbuka makaburi ya baba zao, walipokumbuka sikukuu zao namna na jinsi walivyokuwa wakipanda kwenda kumuabudu Mungu wa baba zai Ibrahim na Isaka na Yakobo, Jinsi walivyokuwa na fahari kuu wakati wa utawala wa Daudi na Solomon, walikumbuka walivyokuwa wakikwea kwenda kuabudu na makuhani wakiwaongoza, walivyokuwa wakitoa sadaka za kuteketeza na kumuabudu Mungu wa kweli kwa furaha na uhuru wao waliokuwa nao, jinsi walivyotumia vinubi na vinanda kumsifu na kumuheshimu Mungu huu ulikuwa ni wakati ambao ni kama golden age kwao, ulikuwa ni wakati wa furaha

Sasa Israel wako utumwani hawana uhuru wao wenyewe, hawawezi kuabudu kama walivyozoea, wanapangiwa kila kitu, waliowachukua mateka wanawasanifu wanasema wawaimbie kama walivyokuwa wakiimba huko sayuni, wakati wao wakiwa na huzuni waliowateka kama mateka wanataka waimbiwe wanataka wafurahie, wao kwao ilikuwa ni swala gumu, uzuri wa Babeli haukuwa na maana kwao, walikumbuka misiba mikubwa, walikumbuka walivyoamuriwa wawaue ndugu zao kwa upanga, wamepoteza mali zao, hawana mashamba yao, hawana nyumba zao,  hawana serikali yao, hawana wafalme wao matumaini waliyokuwa nayo yametokweka, walikumbuka mateso waliyoyapata, walikumbuka walivyochomwa moto, walikumbuka manabii waliokuwa nao, walikumbuka jinsi Mungu alivyowadekeza na kuwapa kila walichokihitaji, sasa ni kama mbingu zimefungwa, ni kama wameondolewa kwenye uwepo wa Bwana, hakuna tena hekalu kubwa kama lile la Sulemani,Unawezaje kuimba wimbo wa Bwana katika nchi ya Ugenini

Waliikumbuka Sayuni waliikumbuka Yerusalem, waliweka nadhiri na kujiapisha kuwa hawatakuja waisahau Yerusalem na kama ikitokea ni sawa na kusahahu mkono wa kulia au mdomo ugande kwa kushikana na ulimi kuliko kuisahau Israel, lakini pia walikumbuka jinsi wakati wanaondoka watu wa Edomu walikuwa wakishangilia kuharibiwa kwa mji huo Bomoeni bomoeni bomoeni walisema na pia waliomba kisasi dhidi ya Babeli kwamba isiachewe salama 

Zaburi 137:5-9 “Ee Yerusalemu, nikikusahau wewe, Mkono wangu wa kuume na usahau. Ulimi wangu na ugandamane Na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka. Nisipoikuza Yerusalemu Zaidi ya furaha yangu iliyo kuu. Ee Bwana, uwakumbuke wana wa Edomu, Siku ya Yerusalemu. Waliosema, Bomoeni! Bomoeni hata misingini! Ee binti Babeli, uliye karibu na kuangamia, Heri atakayekupatiliza, ulivyotupatiliza sisi. Heri yeye atakayewakamata wadogo wako, Na kuwaseta wao juu ya mwamba.” 

Hivi ndivyo inavyotokea katika maisha yetu na maisha ya kanisa la Mungu, hakuna jambo ba ya sana kama kutengwa mbali na uwepo wa Mungu, hatuwezi kufurahia fahari za dunia na dhambi, hatuwezi kuabudu kwa uhuru ikiwa tumechukuliwa mateka, aidha inatia uchungu sana wakati unapopitia mambo magumu kisha wakawepo kando watu wa kufurahia unayoyapitia au kuunga mkono kile unachokipitia, Maandiko yanaonyesha kuwa mwandishi aliomba Mungu akutane na watesi na mashabiki wao pia awalipize kisasi, hatuwezi kuwa na furaha kamili kama maadui zetu wanaisshi na wanashangilia kuangamia kwetu, ni lazima Mungu afanye kitu ili yamkini hata kama wanaishi waweze kuona na kujua kuwa Mungu hawatupilii mbali watu wake, ni lazima wasikie na wajue, Mungu awapatilize,  Natangaza habari njema kwako ya kuwa uko wakati wako wa golden age unakuja ikiwa utakubali Yesu Kristo akutawale, jitegemeze kwake yeye atakutetea anatayafuta machozi yako yote nawe utapata raha nafsini mwako, jitie katika utawala wake nawe utaonja ya kuwa Yesu hatakuacha yeye ni mwema katika maisha yako, hatakusahau kamwe. Kumbuka kurudi katika uwepo wa Mungu, usikubali kutengwa mbali na uwepo wake, uwepo wa Mungu ndio furaha ya kweli, ndio ushindi wa maisha yetu, kila kitu kitakuwa na maana kwetu iwapo tutajikinga katika uwepo wake Zaburi 27:1-4, wale wote wanaotazamia kuwangamia kwetu lazima wajue na wasikie kuwa Mungu wetu yu hai nay a kuwa anafanya kazi kubwa ya kutukomboa pale tunapojitegemeza kwake.

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!.

Maoni 1 :

Shalom alisema ...

Asante mtumishi