Jumamosi, 25 Mei 2019

Nguvu ya Neno la Mungu

Yeremia 23:28-29 . “Nabii aliye na ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu. Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema Bwana. Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?”

 
Askari wa Israel pamoja na mbinu za kimapigano pia hutumia neno la Mungu kwa vita

Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa kama tunataka kufanikiwa katika maisha yetu na kusitawi, Hatuna budi kuhakikisha kuwa tunaliangalia neno la Mungu, siri zote za mafanikio yote ya mwanadamu zimefungwa katika neno la Mungu, nje ya kanuni na njia za Mungu hatuwezi kufanikiwa, kwa nini tunapaswa kuliangalia neno la Mungu ni kwa sababu nje ya neno la Mungu hatuwezi kuzijua Nguvu zake, Yeremia alikuwa ni nabii aliyetumwa kuwaonya wayahudi kwa miaka mingi kuhusu hukumu itakayokuja kwa sababu ya dhambi yakuabudu sanamu na dhuluma, hata hivyo watu walimdharau, walimpinga na kumtesa, na hata manabii wa uongo waliojichagua wenyewe waliamka na kuhubiri kintume na Yeremia wakiwaahidi watu kuwa kutakuwa na amani na Mafanikio, Mwitikio wa Yeremia ulikuwa “Kila nabii na aeseme alichopewa kama ni ndoto zungumza ndoto zako lakini mimi nitalizungumza neno la Mungu kwa sababu Yeremia alijua kuwalina nguvu, lina uweza, ni Neno la kweli la Mungu linalozungumzwa kwa uaminifu ndilo linaloweza kuleta Mabadiliko makubwa kwa wanadamu na nguvu yake kuonekana. Historia ilionyesha kuwa Maneno ya Yeremia yalikuja kutimia kwa sababu alikuwa akizungumza neno la Mungu sawa na jinsi Mungu alivyotaka. Ni kweli ya neno la Mungu pekee inayoweza kutupeleka kwenye ujuzi na uelewa wa nguvu zake.

·         Ujuzi wa kisayansi hauwezi kutusaidia
·         Ujuzi wa dini mbalimbali hauwezi kutusaidia
·         Ujuzi kuhusu Mungu hauwezi kutusaidia
·         Kwenda vyo vya biblia na kuwa na madegree ya Kitheolojia hayawezi kutusaidia

Ni ujuzi wa neno la Mungu uliokaa katika ufunuo wa kweli yake ndio unaoweza kutusaidia  kumjua Mungu na Nguvu zake, Hivyo neno la Mungu ni la Muhimu sana kama Mungu mwenyewe anavyoliheshimu na kutushauri.

Yoshua 1:8 “itabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.”

Hakuna siri nyingine yoyote ya mafanikio ya maisha yetu kama sio kuliangalia neno la Mungu, Yoshua alipewa siri hii na Mungu mwenyewe kwamba ili aweze kufanikiwa na kusitawi sana hana budi kuliangalia neno la Mungu, kulitafakari, kulisoma, kulielewaq, kulijadili, na hapo ndipo tukilifanyia kazi tutaweza kuona mafanikio makubwa sana katika maisha yetu, Daudi alikuwa ni mfalme aliyepata mafanikio makubwa sana wakati anakaribia kufa alimuhusia Daudi kwamba ili aweze kufanikiwa hana budi kuliangalia neno la Mungu, na wakati ule neno la Mungu lililokuweko ilikuwa ni torati iliyoandikwa na Musa.

1Wafalme 2:3 “3. uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako;

·         Mafanikio ya kila mtu mmoja mmoja
·         Mafanikio ya Kifamilia
·         Mafanikio ya kijamii
·         Mafanikio ya kitaifa
·         Mafanikio ya kijeshi
·         Mafanikio ya kiafya

Yote yamefungwa katika neno la Mungu, Mtu awaye yote anayetaka kufanikiwa katika jambo lake lolote hana budi kujiweka katika mazingira ya kujifunza na kulielewa na kulitafakari neno la Mungu.

Neno la Mungu lina uhai kama Mbegu kwamba ikipandwa inaongezeka,mbegu ikitulia mahali na kuhifadhiwa haiwezi kuonekana kuwa na maana lakini ikitumiwa na kupandwa huleta mazao makubwa sana ndivyo lilivyo neno la Mungu, Luka 8:11Na huo mfano, maana yake ni hii; Mbegu ni neno la Mungu”., Yohana 12:24Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.

Kama tukikaa hivi hivi katika maisha yetu bila kulitendea kazi neno la Mungu, Hatutaweza kuona uweza wa Mungu ukitenda kazi katika maisha yetu, ili tuweze kuona matokeo chanya katika maisha yetu hatuna budi kuhakikisha kuwa tunalifanyia kazi neno, lazima tulisome, lazima tulijadili, lazima tujifunze, lazima tulitafakari na kulitendea kazi, nguvu za Mungu na utendaji wake utadhihirika kwa uwazi katika maisha yetu.

Yesu alimuita mtu anayesikiliza neno la Mungu na kulifanyia kazi kama mtu mwenye akili na mtu asikilizaye kisha asilifanyie kazi kama mtu mpumbavu Mathayo 7:24-27Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa” Kama tunataka kuishi maisha ya ushindi na mafanikio kamwe tusimlaumu Mungu maelekezo yote Mungu ameyaweka katika neno lake, hatuna budi kuhakikisha kuwa tunajisomea neno la Mungu kila mara tunalikariri,tunalielewa, tunajifunza, tunalijadili kwa kusudi la kulielewa na tutaweza kuona mafanikio makubwa sana katika kupitia neno la Mungu.

Nguvu ya neno la Mungu

Ni muhimu sasa kujiuliza kwamba, kwa nini neno la Mungu ni ni muhimu sana katika maisha yetu? Je tunawezaje kufanikiwa na kufaidika kwa neno la Mungu, nikilisoma na kulielewa na kulikariri itanifaidia nini?

1.      Neno la Mungu linafaa kwa Mafundisho

2Timotheo 3:14-17Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.” Nyakati hizi tulizo nazo watu wanapata shida sana na namna na jinsi tunavyoweza kuwalea watoto wetu katika ustahivu, dunia ya leo inaonekana kama kuna tatizo kubwa sana la uadilifu! Unajua ni namna gani tunaweza kuwasaidia watu, ni namna gani tunaweza kuwaongoza watu, ni namna gani tunaweza kuwakemea watu ni namna gani tunaweza kuwaonya watu na ni namna gani watu wanaweza kuwa wakamilifu ni kwa kuwajuza neno la Mungu hakuna njia ya mkato, Zaburi 119:9 “Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako.” Kila kijana na jamii itakuwa safi kama watu watafundishwa neno la Mungu na kujifunza kulitii, wat7u wakilipa kipaumbele neno la Mungu watafaa kwa kila tendo jema , watu wengi leo hawafai sehemu mbalimbali kwa sababu hawajaandaliwa katika neno la Mungu, Bwana amope neema kila mmoja wetu kulitii na kulifanyia kazi neno la Mungu.

2.      Neno la Mungu ni upanga wa roho.

Waefeso 6:17 “Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;” Katika fungu la silaha za kiroho zinazotajwa katika Waefeso 6:10-18, Neno la Mungu ni moja ya silaha kali za mashambulizi, silaha nyingi zinazotakwa kwa mkristo ni za kujilinda, na silaha chache sana ni za mashambulizi, Neno la Mungu ni silaha ya mashambulizi, katika vita ka katika michezo kujihami sana hakusaidii, kujilinda na kujihami ni kuzuri lakini hakuwezi kumfukuzia mbali adui, nafikiri kama ningelikuwa mwalimu wa vita au kocha wa Mpira ningewafundisha watu wangu kushambulia zaidi, kushambulia ndiko kutakako mfanya adui akimbie na kwenda mbali sana au afanye kazi ya kujihami na kujilinda, ushindi wetu katika maandiko unatajwa kuwa katika neno la Mungu na Damu ya Yesu, Ufunuo 12:10-11Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku. Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.”    Wote tunafahamu kuwa Yesu wakati wa Majaribu aliweza kumshinda shetani kwa sababu alikuwa na ujuzi wa ajabu kuhsu neno la Mungu, ujuzi kuhusu neno la Mungu na kujaa kwake maandiko kulimfanya ibilisi kumkimbia, kushindwa kwa Eva katika Bustani ya Edeni ni wazi kunaonekana kulitokana na kushindwa kuhifadhi na hata kulielewa agizo la Mungu na neno la Mungu kwamba wasile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, Lakini hali hiihaikuwa hivyo kwa Yesu yeye alikuwa amejaa nneno na ufahamu kuhusu neno la Mungu ulikuwa juu yake naye alifanikiwa Luka 4:1-13 “Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa. Ibilisi akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate. Yesu akamjibu, Imeandikwa ya kwamba mtu hataishi kwa mkate tu. Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako. Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake. Akamwongoza mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake wakulinde; na ya kwamba,mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu akajibu akamwambia, Imenenwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako. Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda.” Watu wengi wanashindwa na hali zinazowazunguka leo kwa sababu hawana ujuzi wa neno la Mungu katika vita vyao, Neno la Mungu lina nguvu unapolisema na kulitaja kazi za adui zinashambuliwa vibaya na shetani anapata tabu sana, unawezaje kuwa mshindi katika maisha yako uwe na neno la Mungu kwa kila hali inayokuzunguka, uwe na neno la Mungu kwa kila vita inayokuzunguka, mkumbushe Mungu hali unayokutana nayo na mtamkie shetani hali anayokujaribu nayo na hapo ndipo utakapoona uweza mkubwa wa neno la Mungu.

3.      Neno la Mungu lina Nguvu ya kuhekimisha (power to make you wise)

Mithali 3:13 “Heri mtu yule aonaye hekima, Na mtu yule apataye ufahamu.” Biblia ya kiingereza inasema “Blessed is the man who finds wisdom, the man who gains understanding” kwa Kiswahili kizuri tungeweza kusema heri mtu yule atafutaye hekima, na mtu yule apataye ufahamu”

Ni muhimu kufahamu kuwa kuna ujuzi na hekima kubwa sana katika neno la Mungu kuliko katika maandiko mengine yoyote yale, mtu anayejisomea neno la Mungu hata asiposoma vitabu vingine anauwezo wa kuitambua Hekima ya kweli kuliko wenye hekima wa dunia hii Katika macho ya Mungu hekima ya dunia hii ni upuuzi 1Wakoritho 1:20 “Yu wapi mwenye hekima? Yu wapi mwandishi? Yu wapi mlete hoja wa zamani hizi? Je! Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa ni upumbavu?” 3:19 “Maana hekima ya dunia hii ni upuzi mbele za Mungu. Kwa maana imeandikwa, Yeye ndiye awanasaye wenye hekima katika hila yao.Katika historia ya ulimwengu watu ambao wameweza kuutikisha ulimwengu, watu ambao wameweza kuupindua ulimwengu, watu ambao wameweza kusimamia uadilifu na kusimamia mafundisho sahihi ya biblia ni watu ambao wanalijua neno la Mungu, watu wasio na tamaduni zozote na wakaweza kufaidika kwa ujuzi ni wale ambao wallifahamu neno la Mungu wale wanaoisoma na kuijua Biblia, ujuzi katika neno la Mungu, Kaka zangu dada zangu kama tunataka kuwa na uelewa wa kupita kawaida katika maswala ya ulimwengu huu suiache kujifunza neno la Mungu, Hekima inajenga Nyumba inaimarisha Mithali 14:1 “Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.

4.      Neno la Mungu hupandisha Imani

Warumi 10:17 “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” Ni muhimu kukumbuka kuwa hatuwezi kuwa na imani kamwe kwa kuomba pekee, wala imani haiji kwa kujitahidi, Imani inakuja kwa kusikia, kwa kusoma kwa kuliamini neno la Mungu, Mkuu wa Gereza pale Filipi aliuliza afanyeje ili aweze kuokoka na Mtume Paulo alimjibu kuwa lazima amuamini Bwana Yesu Matendo 16:30-31,32 na hawakuishia hapo bali aliendelea kumueleza neno la Mungu na ndipo alipoweza kuokoka yeye na nyumba yake yote Matendo 16:30-32 “kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako. Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake.”  Maombi yetu nili yaweze kuwa na nguvu vilevile yanahitaji imani Marko 11:24 “Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.”           Yohana 20: 31 Neno la Mungu liliandikwa ili tupate kusadiki ya kuwa Yesu ni mwana wa Mungu Yohana 20:31 “Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.” Unaweza kuona kama sasa tunahitaji imani katika kila eneo na katika maisha yetu hatuna budi kulisoma neno la Mungu, hatuna budi kuliamini, iliimani zetu ziweze kupanda na kutusaidia kutuletea wokovu, kuleta majibu ya maombi yetu na kutusaidia kumjua Yesu na kumuamini tunahitaji neno la Mungu na ni neno la Mungu pekee linaloweza kutusaidia kuwa na imani.

5.      Neno la Mungu lina Nguvu.

Ni muhimu kufahamu kuwa Neno la Mungu lina nguvu na uweza wa ajabu, wakati ambapo tunapitia haki ngumu mno na haki za kukata tamaa au magumu ya aina yoyote tusisite kulitamka neno la Mungu kwa sauti, litamke neno kwa mamlaka kila hali inayokukabili kinyume na neno la Mungu itawekwa sawa, Isaya 55:10-11Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma       Neno la Mungu lina Nguvu  kama mstari wa msingi usemavyo, Lina nguvu kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande, lina nguvu kama moto, lolote na hali yoyote inayoonekana kuwa ngumu katika maisha yetu, inaweza kusambaratishwa kupitia neno la Mungu, Yeremia 23:28-29 . “Nabii aliye na ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu. Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema Bwana. Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?”

6.      Neno la Mungu lina nguvu ya kusafisha.

Yohana 17:17Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.” Mungu husafisha na kutakasa kupitia neno lake Waefeso 5:26-27. “ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa, Yohana 15:3 “Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. Neno lina uwezo wa kusafisha maisha yetu, ikiwa tuna tatizo lolote neno la Mungu linatuagiza kutubu kuungama na kuacha maovu yetu 1Yohana 1;9,Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.” na hali kadhalika tunapaswa kuruhusu neno la Mungu kutusafisha na kututakasa.

7.      Neno la Mungu lina nguvu ya kujenga (the power to build up).

Matendo 20:32 “Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa.Tunajifunza hapa kuwa kumbe neno la Mungu lina uwezo mkubwa sana wa kutujenga, neno la Mungu linanguvu ya kutujenga katika tabia na mwenendo wetu, Mungu anataka watu wake wajengwe kupitia neno lake na ndio maana ametoa karama mbalimbali katika kanisa ili kila mmoja ajengwe, kujengwa kwetu kuna mpango wa kutupeleka katika ukamilifu “Maturity” hata tuweze kumfikia Yesu Kristo Waefeso 4:11-13 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;  ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.” Mungu anataka tuondoke katika hali ya uchanga na kufikia ngazi ya kuwa walimu wa neno la Mungu, kamwe sio mpango wa Mungu sisi tudumae Waebrania 5: 12-14 “Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia. Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya.Tunawezaje kuondoka katika uchanga na kuelekea katika ukomavu ni kwa kukubali kujifunza neno la Mungu, tukiwa wavivu kujifunza neno la Mungu tutadumaa na hatutaweza kujengeka.Kwa msingi huo tunapaswa kulitamani neno la Mungu kama tunavyotamani maziwa ili tuweze kukua 1Petro 2:2Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;ili tuweze kukua na kujengeka vema tunapaswa kulitamani nenola Mungu, Mkristo wa kweli anapaswakujua kuwa hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu, Neno la Mungu lina virutubisho vya kutosha kutufanya kukua na kujengeka na kufikia kiwango ambacho Mungu amekusudia katika maisha yetu.

8.      Neno la Mungu lina Nguvu ya kitupa furaha na amani.

Maisha yetu duniani yana changamoto nyingi sana, kama hakungekuwa na neno la Mungu watu nwengi wangeweza kukata tamaa na wasingeliweza kupata faraja ya aina yoyote, lakini ni kupitia neno la  Mungu tunakuwa na amani na furaha, ya kweli ujuzi wa kweli katika neno la Mungu unaweza kutusaidia na kutufanya tuwe na amani wakati wote Yeremia 15:16Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana, Mungu wa majeshi.” Neno la Mungu liliandikwa ili kutupa Matumaini kutufunza uvumilivu na kutuletea faraja Warumi 15:4 “Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya maandiko tupate kuwa na tumaini”. Unaona ndani ya maandiko kuna faraja na matumaini, tunapopita katika wakati mgumu na wenye kukatisha tamaa tunaweza kukubaliana wazi kuwa Mungu hufanya mambo yote katika kutupatia mema sisi tumpendao Warumi 8: 28 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.” Zaburi 85:8 Biblia inasema “Na nisikie atakavyosema Mungu Bwana, Maana atawaambia watu wake amani, Naam, na watauwa wake pia, Bali wasiurudie upumbavu tena.”

9.      Neno la Mungu li hai tena lina nguvu (the word of God is alive and active)

Moja ya sifa kubwa  na ya kipekee kuhusu neno la Mungu ni pamoja na kuwa na uhai na tena lina nguvu, Kwa wayahudi ilikuwa inaeleweka wazi kwamba ukitaja neno la Mungu ni sawa na kumtaja masihi mwenyewe Yohana 1;1Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu” Neno la Mungu lina uhai maana yake ndani yake kuna uwezo wa kumfanya mwanadamu aishi, maisha yetu na kuwepo kwetu hakutegemei tu nguvu ya chakula bali tunaweza kuishi kwa neno la Mungu Mathayo 4:4 “Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.”  Neno la Mungu halitakuja kufa wala halitachakaa kila kitu kitapita lakini neno la Mungu halitapita kamwe Mathayo 7:24 “Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.” Ni neno la Milele, ndani yake iko pumzi ya Mungu na hivyo linafanya kazi ndani ya walioamini 1Wathesalonike 2:13 “Kwa sababu hiyo sisi nasi twamshukuru Mungu bila kukoma, kwa kuwa, mlipopata lile neno la ujumbe la Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na ndivyo lilivyo kweli kweli; litendalo kazi pia ndani yenu ninyi mnaoamini.Neno la Mungu lina uhai, lina nguvu, lina na lina uwezo wa kuponya Zaburi 107:19-20 “Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao.Kwa sababu hiyo kuna umuhimu mkubwa sana kwetu, kulitegemea, kuliamini, kulisoma na kulitumia litumie katika hali yoyote na mazingira yoyote kwa changamoto zozote zinazokukabili.

10.  Neno la Mungu lina Nguvu ya kutufunulia siri kuu za ulimwengu (Reveal philosophical question)

Mtaifahamu kweli nayo itawaweka huru Yohana 8:32tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru”
Neno la Mungu lina nguvu ya kutufunulia na kutujuza maswala makubwa ya kifalsafa ambayo tusingeweza kuyajua kwa akili za kawaida za kibinadamu, Maswali makubwa ya ki-falsafa ni kama vile
a.      Ulimwengu uliumbwa na nani (Mwanzo 1-2, Waebrania 11:3)
b.      Kwa nini wanadamu wako hivi walivyo (Zaburi 146:6, Isaya 45:12)
c.       Mungu ni nani
d.      Nini kinatokea baada ya kifo (Waebrani 9:27)
e.      Kwa nini mwanadamu yuko Duniani
f.        Mwanadamu anawezaje kuishi duniani (Kumbukumbu la Torati 10:12)

Maswali haya ya kifalsafa tungeweza kusoma na kusoma miaka na miaka, na mawazo mengi yangetengenezwa kama “EVOLUTION THEORY” na nyingine nyingi lakini zoyte zingebaki kuwa upuuzi kwa sababu zinashindwa kutujulisha ukweli, Ni neno la Mungu tu linaloweza kutusaidia kujua na kujibu maswali yote ambayo ulimwengu wa kawaida.

11.  Neno la Mungu lina nguvu ya kufuta Makosa (the Power to refute).

Dunia imaejaaa utetezi mwingi wa kijinga, wako wanaotetea Pombe, wako wanaotetea zinaa, wako wanaotetea ushoga, wako wanaotetea uongo, wako wanaotetea, dhuluma, wako wanaoona mambo yasiyo sawa kuwa yako sawa, katika ulimwengu hu tulio nao wa sasa kamwe hatupasi kukubaliana na kila kinachopendekezwa na ulimwengu, ni lazima tuliangalie neno la Mungu linasema nini na kukemea na kukaripia na kuvunjialia mbali kila kinachoonekana kuwa sio tatizo wakati ni tatizo 2Timotheo 4:1-4 “Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake; lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongoMitume walilitumia neno la Mungu kuilinda na kuitetea imani na kuwakemea kwa nguvu kubwa manabii au walimu wa uongo, pia walilitumia kung’oa falsafa na imani potofu dhidi ya kanisa 2Petro 1:19-21 “Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing'aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu. Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.” Unaweza kuona hivyo wanafunzi wa Yesu wana kila sababu ya kuliangalia neno na kuyatatuta mapenzi yake na kilitafasiri kwa halali baada bya kulijifunza kwa kina ili hatimaye waweze kuishindania imani Yuda 1:3-4 “Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu. Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo”. 

12.  Neno la Mungu lina nguvu ya kutuandaa kwa wakati ujao “get us ready for the feature      
Maandiko yana nguvu  ya kutuandaa kwa wakati ujao  Yesu Kristo mwenyewe alisema ni lazima tujiweke tayari Luka 12:40 “Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu.” Neno la Mungu linaelezea wazi kuwa kuna siku tutasimama mbele za nkiti cha hukumu ya Mungu, na kwa sababu hiyo hatuna budi kuwa na ufahamu  wa namna gani tunaweza kujiandaa kukutana na Mungu, kwa hukumu,  tunawezaje sasa kujiandaa vema ni kwa kuliangalia neno, ni neno la Mungu pekee lenye uwezo wa kutusaidia katika maandalizi yetu
Neno la Mungu linaonyesha mpango wa Mungu wa ukombozi kupitia mwana wa Mungu Yohana 3:16
Neno la Mungu linatuonyesha namna tunavyoweza kuwa na uzima wa milele na kuhukumiwa Yohana 3:17-18
Neno la Mungu linatuelekeza namna tunavyoweza kumrudia Mungu kwa toba Matendo 2:37-38
Neno la Mungu linatuandaa kwa kifo na ufufuo
Ni neno la Mungu pekee linaloweza kutusaidia kutuandaa katika hali zote za maisha yetu, swala kubwa la msinhgi na la muhimu sasa ni jinsi gani tunaweza kufurahia nguvu za Neno la Mungu?

1.      Ni lazima tulisome  Yoshua 1:5-8
2.      Ni lazima tulitii Zaburi 119:9
3.      Ni lazima tulihubiri na kulieneza Warumi 1:16
Neno la Mungu lina nafasi pana ya kutusaidia na kutufanikisha katika maisha yetu

Rev. Innocent Kamote 
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!.

Hakuna maoni: