Jumapili, 24 Novemba 2019

Je mtu kama mimi Nikimbie?


Nehemiah 6:11Nami nikasema, Je! Mtu kama mimi nikimbie? Naye ni nani, akiwa kama nilivyo mimi, atakayeingia hekaluni ili kuponya maisha yake? Sitaingia.”



Utangulizi:

Nehemiah alikuwa moja ya viongozi  Muhimu sana aliyepewa Mzigo na Mungu wa kuujenga ukuta wa Yerusalem, Nehemia alikuwa ni kiongozi wa Pili aliyefanya kazi kubwa na ya muhimu ya kurejesha heshima ya mji wa Yerusalem, Mojawapo wa viongozi wakubwa waliotangulia alikuwa ni Zerubabel, Yeye alijenga Hekalu, na Ezra alikuja baadaye kwaajili ya kuwajenga watu kiroho, Lakini Nehemia alikuwa na kazi ya kuujenga ukuta wa Yerusalem kazi iliyokuwa muhimu kwaajili ya usalama wa watu wa Mungu na mji wa Mungu, Unaposoma kitabu hiki unaweza kudhani mwanzoni kuwa kazi hii ilikuwa Rahisi kwa sababu ilitoka kwa Mungu na Nehemiah alipewa kibali na Mungu


Nehemia 1:2-6 “Hanani, mmoja wa ndugu zangu, akanijia, yeye na watu wengine waliotoka Yuda; nami nikawauliza habari za Wayahudi waliopona, hao watu wa uhamisho waliosalia; na habari za Yerusalemu. Wakaniambia, Watu wa uhamisho, waliosalia huko katika wilaya ile, wamo katika hali ya dhiki nyingi na mashutumu; tena ukuta wa Yerusalemu umebomolewa, na malango yake yameteketezwa kwa moto. Hata ikawa niliposikia maneno hayo, nikaketi, nikalia, nikaomboleza siku kadha wa kadha; kisha nikafunga, nikaomba mbele za Mungu wa mbinguni; nikasema, Nakusihi, Ee Bwana, Mungu wa mbinguni, Mungu mkuu, mwenye kuogofya, mwenye kutimiza agano lake na rehema zake kwa hao wampendao na kuzishika amri zake; tega sikio lako, macho yako yakafumbuke, upate kuyasikiliza maombi ya mtumishi wako, ninayoomba mbele zako wakati huu, mchana na usiku, kwa ajili ya wana wa Israeli


Nehemia alikuwa ni mtu mwenye mzigo kwaajili ya Yerusalem, na alimuomba Mungu kwaajili ya Mzigo uliokuwa ndani yake na Mungu alimpa kibali, Biblia inaeleza kuwa mkono wa Mungu ulikuwa mwema juu yake Nehemia 2:18a “Nikawaeleza habari ya mkono wa Mungu wangu ulivyokuwa mwema juu yangu; yaani Mungu alikuwa amempa kibali kwaajili ya kazi ile na mfalme alimruhusu Nehemia na kumpatia kila kilichohitajika kwa ajili ya nyumba mji wa Yerusalem, hii ilikuwa ni kazi ngumu ni wito kwaajili yake


Hata hivyo kazi hii ilikuwa na vikwazo vingi na haikuwa rahisi, Shetani aliipinga kazi hii akitumia watu mbalimbali, kuitukana, kuidharau, kuinena vibaya na kuwatishia kina Nehemia ili yamkini aache kazi hii, wakatimwinguine walitaka kuwakatisha tamaa na kuwanenea maneno mabaya sana ya kudhoofisha pasipo sababu


Angalia


1.       Maadui walinena maneno ya kipuuzi mno kuhusu ujenzi wa ukuta ule Nehemia 4:1-3 “Lakini ikawa, Sanbalati aliposikia ya kwamba tulikuwa tukiujenga ukuta, akaghadhibika, akaingiwa na uchungu sana, akawadhihaki Wayahudi. Akanena mbele ya nduguze na mbele ya jeshi la Samaria, akisema, Wayahudi hawa wanyonge wanafanyaje? Je! Watajifanyizia boma? Watatoa dhabihu? Au watamaliza katika siku moja? Je! Watayafufua mawe katika chungu hizi za kifusi, nayo yameteketezwa kwa moto? Basi Tobia, Mwamoni, alikuwa karibu naye, akasema, Hata hiki wanachokijenga, angepanda mbweha, angeubomoa ukuta wao wa mawe.”


Nehemia alichokifanya wakati huu ilikuwa ni kuomba na kusonga mbele kwa kufanya kazi Nehemia 4:4-6 “Sikia, Ee Mungu wetu; maana tunadharauliwa; ukawarudishie mashutumu yao juu ya vichwa vyao, ukawatoe watekwe katika nchi ya uhamisho; wala usiusitiri uovu wao, wala isifutwe dhambi yao, mbele zako; kwa maana wamekukasirisha mbele ya hao wanaojenga. Basi tukaujenga ukuta; nao ukuta wote ukaungamanishwa kiasi cha nusu ya kimo chake; maana watu walikuwa na moyo wa kufanya kazi.”



2.       Maadui walipoona kuwa jamaa hawajakata tamaa bali waliendela na kazi wakashuriana kunazisha vita Nehemia 4:7-8 “Lakini ikawa, Sanbalati, na Tobia, na Waarabu, na Waamoni, na Waashdodi, waliposikia ya kuwa kazi ya kuzitengeneza kuta za Yerusalemu inaendelea, na ya kuwa mahali palipobomoka panaanza kuzibwa, basi wakaghadhibika mno; wakafanya shauri wote pamoja kuja kupigana na Yerusalemu, na kufanya machafuko humo.”



Nehemia alichokifanya sasa aliweka walinzi., na kazi iliendelea usiku na mchana walijenga huku kukiwa na walinzi kwaajili ya kuwapinga maadui Nehemia 4:9 “Bali sisi tulimwomba dua Mungu wetu, tena tukaweka walinzi, mchana na usiku, kwa sababu yao, ili kuwapinga.”



3.       Maadui walikusudia kuwashambulia wayahudi ili kuikomesha kazi ile kabisa Nehemia 4:10-12 Wakasema Yuda, Nguvu zao wachukuao mizigo zimedhoofika, na kifusi tele zipo; tusiweze kuujenga ukuta. Nao adui zetu wakasema, Hawatajua wala kuona, hata tutakapokuja kati yao, na kuwaua, na kuikomesha kazi hiyo. Kisha ikawa, Wayahudi walipokuja, wale waliokaa karibu nao, wakatuambia mara kumi, Kutoka kila mahali mtakaporejea watatushambulia.”



Nehemia hakukata tamaa yeye na watu wake waliendelea kujipanga waliweka ulinzi na kuhakikisha kuwa kazi inafanyika usiku na Mchana Nehemia 4:13-23.


4.       Baada ya Ibilisi kuona kuwa amewashindwa kwa namna hii alileta njaa, Familia za wayahudi wanawake na watoto walikopa fedha ili wapate chakula kwa sababu wanaume walikuwa na kazi ya kuujenga ukuta kule walikokopa walishikwa riba na hivyo umasikini mkubwa na njaa vikawapata Nehemia 5:1-6 “Ndipo kukatokea kilio kikuu cha watu, na wake zao, juu ya ndugu zao Wayahudi. Maana, walikuwako watu waliosema, Sisi, na wana wetu na binti zetu, tu wengi; na tupate ngano, tule, tukaishi. Tena walikuwako wengine waliosema, Tumeweka rehani mashamba yetu, na mizabibu yetu, na nyumba zetu; tupate ngano, kwa sababu ya njaa. Tena walikuwako wengine waliosema, Tumekopa fedha ili kulipa kodi ya mfalme kwa kuweka rehani mashamba yetu, na mizabibu yetu. Walakini miili yetu ni kama miili ya ndugu zetu, na watoto wetu kama watoto wao; kumbe! Mnawatia utumwani wana wetu na binti zetu kuwa watumishi, na baadhi ya binti zetu wamekwisha kutiwa utumwani; wala hatuwezi kujiepusha na hayo; maana watu wengine wana mashamba yetu na mizabibu yetu. Nami nilikasirika sana, niliposikia kilio chao, na maneno hayo.”


Nehemia hata hivyo tena aliwakemea viongozi kuwatoza riba wayahudi wenzao na kuamuru kuwarejeshea mashamba yao na kila kitu walichoweka Reheni Nehemia 5:7-19

5.       Mbinu ya mwisho kabisa shetani aliyoitumia ili sasa aweze kummaliza Nehemia ilikuwa ni kumtumia manabii wa uongo ili kwamba wamshawishi Nehemia avunje sheria za Kiyahudi na sheria za Kisrrikali wapate namna ya kumaliza, walituma watu nkumuita Nehemia mara kadhaa ili ikiwezekana akikubali kushuka waweze kumuua Nehemia 6:1-14, Hata hivyo Nehemia alikuwa na uwezo mkubwa mno wa kujijua mitego ya ibilisi na kuiepuka, Mungu alikuwa amempa Hekima ya kushinda vikwazo vyoye adui alikuwa amevikusudia, mwisho walipoona kuwa hawafanikiwi kumpata Nehemia wakamtumia Nabii wa uongo akamwambia kuna njama za wewe kutaka kuuuawa na Mungu anakutaka ukimbilie Hekaluni kujisalimisha  na walimshauri akimbilie Hekaluni akajifungie huko maana angauawa wakati wa usiku 

     Nehemia 6:8-12 “Ndipo mimi nikatuma kwake wajumbe, kusema, Hakukufanyika mambo kama hayo uyasemayo, lakini kwa moyo wako wewe mwenyewe umeyabuni. Kwani hao wote walitaka kutuogofisha, wakisema, Italegea mikono yao katika kazi, isifanyike. Lakini sasa nitaitia mikono yangu nguvu.  Nikaingia nyumbani kwa Shemaya, mwana wa Delaya, mwana wa Mehetabeli, aliyekuwa amefungwa; naye akasema, Tukutane nyumbani mwa Mungu, ndani ya hekalu, tukaifunge milango ya hekalu; kwa maana watakuja kukuua; naam, wakati wa usiku watakuja kukuua. Nami nikasema, Je! Mtu kama mimi nikimbie? Naye ni nani, akiwa kama nilivyo mimi, atakayeingia hekaluni ili kuponya maisha yake? Sitaingia. Nikatambua, na tazama, siye Mungu aliyemtuma; lakini amefanya unabii huu kinyume changu; nao Tobia na Sanbalati ndio waliomwajiri.”

      Nehemia alikuwa anajua sherai za Nchi na vilevile alikuwa anazijua sheria za Mungu Yeye alikuwa mtu wa kawaida tu na mtu wa kawaida kwa mujibu wa Torati hakupaswa kuingia Hekaluni na kujifungia kitendo hicho cha kuinhgia hekaluni na kujifungia katika chumba cha hekalu kilikuwa ni halali kwa Makuhani na ukoo wa kikuhani yaani walawi tu na mtu wa kawaida kama angeingia Hekaluni kwa mujibu wa Torati alitakiwa kuuawa Hesabu 18:7 “Nawe na wanao pamoja nawe mtautunza ukuhani wenu, kwa ajili ya kila kitu cha madhabahu, na kwa ajili ya vile vilivyomo ndani ya pazia, nanyi mtatumika. Nawapeni ukuhani kuwa utumishi wa kipawa; na mgeni akaribiaye atauawa.” 


Majaribu ya Nehemia yanatufundisha wazi kuwa shetani ataendela kutupinga kila wakati akitumia njia na mbinu na mashambulizi ya aina mbalimbali, ni lazima uelewe kuwa hata kama tuko katika mapenzi ya Mungu mambo hayawezi kuwa rahisi, kila wakati tuaona upinzani mkubwa adui atajaribu kutukatisha tamaa, atataka tushindwe atataka tuache kumuamini Mungu, ni muhimu kwetu kufahamu kuwa hatuna budi kusonga mbele, kuendela kuomba na kufanya kazi kwa bidii, na kumpuuzia ibilisi na kazi zake na wajumbe wake, Mungu anajua kile tunachokifanya kwamba twakifanya kwaajili ya utukufu nwake, hatutafuti sifa kwa wanadamu, Bali afadhali kupata sifa kwa Mungu, Mungu hataondoa upinzani kama ambavyo hakuondoa kwa Nehemia lakini wakati wote tukumbuke kuwa upinzani utatupeleka katika kiwango kingine, utatufanya tumtegemee Mungu zaidi kuliko akili zetu, tukikata tamaa tutakuwa tumeishia njiani, washndani wazuri ni wale wanaopambana mpaka dakika ya mwisho 

Tukifahamu kuwa shetani anatumia nini kutushambulia tutashinda kila aina ya kikwazo kinachokuja mbele yetu

Shetani atatumia 

1.       Hasira za wengine juu yako
2.       Dharau na kejeli
3.       Vitisho na mikwara
4.       Kukukatisha tamaa na kukuvunja moyo
5.       Kukuzungumzia kinyume
6.       Kukutisha
7.       Kuishiwa kiuchumi na kuwa na Madeni
8.       Kukutaka uvunje sheria  za nchi au shuleni
9.       Kukufanya ufanye dhambi


Hizi ndio mbinu alizozitumia kutaka kumkatisha tamaa Nehemia, lakini Nehemia alizijua zote alikaa katika maombi, alikaaa katika wito wake alioitiwa, Walijilinda na adui na walimtazama Mungu, Kama unamjua Yesu na unatimiza majukumu yako sawa na mapenzi yake ni lazima ujue kuwa utakutana na vikwazo,Kama umeitwa katika wito wowote au wewe ni kiongozi huna budi kufahamu kuwa kitakachokuokoa ni kuwa kama Nehemia kuomba, kuangalia kile ulichoitiwa, kujilinda na maadui na kumwangalia Mungu aliyekuita katika hilo uliloitiwa. Je mtu kama Mimi nikimbie? Naye ni nani atakayekuwa kama nilivyo atakayekimbia?


Nchi yetu hivi karibuni imeshuhudia upinzani wa kiuchumi hasa katika ameneo ya kuzuiwa kwa ndege zetu mara kwa mara na madui wa uchumi wa Taifa letu, jambo hili lisitukatishe tamaa, tuendelee kusonga mbele na kusimama na Mungu naye ataupigania. 

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote
0718990796

Hakuna maoni: