Alhamisi, 21 Novemba 2019

Ni zaidi ya Ukarimu!



Warumi 8:32Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?”


Utangulizi:

Moja ya sifa kubwa sana ya Mungu wetu ni pamoja na kuwa Mkarimu, Maandiko yanatufunza sisi nasi kuwa wakarimu,

Waebrania 13:2
Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua.”  Lakini hata hivyo yanamfunua kuwa Mungu ni zaidi ya Ukarimu, hii inapimwa na andiko hili katika Warumi 8:32  Mstari huu unaakisi kinabii tendo lililofanywa na Abrahamu aliyekuwa na upendo mkubwa sana kwa Mungu kiasi cha kuwa tayari kumtoa Isaka.

Kimsingi na kinabii Ibrahimu alikuwa anamwakilisha Mungu na Isaka anamwakilisha Yesu, Tendo la Ibrahimu kuwa tayari kumtoa mwana wake wa pekee Isaka kwa Mungu, Hali kadhalika ni picha halisi ya namna na jinsi Mungu alivyokuwa mkarimu kiasi cha kuwa tayari kutoa  mwanaye wa pekee Yesu Kristo kwetu, na kwa ulimwengu mzima kwa ujumla  Yohana 3:16Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Mungu yu aonyesha zaidi ya ukarimu kwa kumtoa mwanae wa Pekee Yesu Kristo kuja ulimwenguni kwa watu wasiofaa ili awaokoe huu ni zaidi ya ukarimu Yesu Kristo ni zawadi ya juu na kubwa mno ambayo tumepata kupewa kama wanadamu Isaya nabii anaielezea zawadi hii namna na jinsi Yesu alivyo zawadi kubwa mno na yenye thamani na nguvu ona!

Isaya 9:6-7 “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda hayo.” 

    
Tumepewa Isaya anasema tumekarimiwa ni zawadi ya mtoto wa kipekee mwanamume, ni mfalme serekali iko mabegani mwake ni mshauri wa ajabu, ni Mungu mwenye nguvu na baba wa milele na mfalme wa amani, hana mwanzo wala mwisho ataketi katika kiti cha enzi cha Daudi, Huyu ni Yesu Kristo ni zawadi kubwa mno ni zawadi ya kipekee sana ni zawadi kubwa Mungu kutupa Yesu ameonyesha zaidi ya Ukarimu

Huu ni upendo mkubwa mno kwa kupewa Yesu Kristo kuwa zawadi kubwa kwetu:-
·         Hakuna wa kutushitaki
·         Hakuna wa kutuhukumu
·         Hakuna wa kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Bwana wetu
Orodhesha chochote unachoweza kuorodhesha hakuna kinachoweza kulinganishwa na upendo wa Mungu kwetu na ukarimu wake wa kupita kawaida


Warumi 8:33-39 inasema “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.  Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

Sasa basi ikiwa upendo wa Mungu kwetu ni mkubwa namna hii Paulo mtume anasema kwamba Kama Mungu alimuachilia mwana wake wa pekee kwaajili yetu atashindwaje kutukirimia na mambo mengine? Atatukarimia mambo yote pamoja naye, kama ametupa Yesu Kristo ni rahisi, kupewa  Mume, ni rahisi kupewa mtoto, ni rahisi kupewa ufaulu katika mitihani yako, ni rahisi kupewa gari, ni rahisi kupewa nyumba, ni rahisi kupewa Hekima


1Wafalme 3:5-13 “Na huko Gibeoni Bwana akamtokea Sulemani katika ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo nikupe. Sulemani akasema, Umemfanyia mtumwa wako Daudi baba yangu fadhili kuu, kadiri alivyoenenda mbele zako katika kweli, na katika haki, na katika unyofu wa moyo pamoja nawe; nawe umemwekea na fadhili hii kubwa, maana umempa mwana wa kuketi kitini pake kama ilivyo leo. Na sasa, Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi. Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi? Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili. Mungu akamwambia, Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu; basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe. Na mambo yale usiyoyaomba nimekupa, mali na fahari, hata hapatakuwa na mtu katika wafalme kama wewe, siku zako zote.”

Suleimani aliomba Hekima lakini Mungu alimuongezea Utajiri na heshima kubwa sana, Mungu alidhihirisha kuwa yeye ni zaidi ya ukarimu, yeye anaweza kutupa lolote tuliombalo na tulitakalo kwa kadiri ya wingi wa rehema zake na neema yake,  Yesu ni zaidi ya Hekima, Yesu ndio Hekima yenyewe kutoka Mbinguni unapokuwa naye unakuwa na kila kitu, Ukimtafuta yeye mambo mengine yote utazidishiwa, Yesu ndio zawadi ya juu kabisa ambayo Mungu amepata kuwapa wanadamu, nyingine ni ndogo Yesu ni zawadi kubwa mno sasa  Kama Mungu ametupa Yesu Kristo ni wazi kuwa ametupa kila kitu hatatuzuilia maswala mepesi tuyaombayo kwa kuwa amekwisha tenda jambo zito kuliko yote kutupa Yesu Kristo kama zawadi ya pekee ni kwaajili ya sababu hii nzito Paulo mtume anahoji kuwa kama Mungu hakumuachilia Yesu Kristo mwana wake wa pekee alimtoa kwaajili yetu, atakosaje atashindwaje atasitaje kutukirimia mambo yote pamoja naye kumbuka kuwa mambo yote pamoja naye yaani ukisha kuwa na Kristo ambaye ndiye mfalme wa Ufalme wa mbinguni hutakosa kamwe kupewa mengineyo huu ni zaidi ya ukarimu!


Warumi 8:32Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?”

Ni zaidi ya Ukarimu
Na Mkuu wa wajenzi mwenye hekima
Rev. Innocent Kamote
0718990796.