Mathayo 5:20 “*Maana nawaambia
haki yenu isipozidi Hiyo haki ya waandishi na mafarisayo hamtaingia kamwe
katika ufalme wa Mbinguni*”
Utangulizi:
Waandishi na Mafarisayo ni akina nani
?
Ni
muhimu kufahamu kuwa nyakati za
ulimwengu wa agano jipya yaani wakati wa Yesu Kristo katika Dini ya kiyahudi
kulikuwa na Makundi (Madhehebu) mbalimbali ya watu mbalimbali wenye misimamo
kadhaa ya kidini lakini makundi makubwa yaliyojulikana zaidi walikuwa
Mafarisayo na Masadukayo, lakini kulikuwa na kundi lingine maarufu
lililojulikana kama waandishi au wanasheria, na mengineyo yenye misimamo ya
kisiasa na kidini lakini hapa nitawazungumzia Waandishi na mafarisayo tu kwa
sababu ndio ambao wametajwa katika mstari wa Msingi kwamba “Haki yetu (Wakristo au wanafunzi wa Yesu)
isipozidi hiyo haki ya Waandishi na mafarisayo Hatutaingia kamwe katika ufalme
wa Mungu” kwanza tuwajue hao ni kina nani:-
Waandishi
Waandishi
ni kundi la jamii katika dini ya kiyahudi waliokuwepo wakati wa Agano jipya
ambao walikuwa ni walimu na watafasiri wa Sheria ya Musa Yesu alilitaja kundi
hili kwa sababu walikuwa wasomi na watu waliobobea katika ujuzi wa torati, kazi
yao kubwa pia ilikuwa kunakili sheria kutoka katika magombo ya chuo
yanayochakaa au ya zamani na kuyanakili katika magombo mapya aidha watu hawa
pia walijikita katika kusoma na kuielewa sheria ili kuwafundisha au
kuwafafanulia watu.
•
Walijulikana pia kama wanasheria
•
Ni kundi la uamsho wa kimaandiko lililoanza
wakati wa Ezra mwandishi baada ya watu kurejea kutoka uhamishoni Babeli
•
Waliitwa “SOFERIM”
Kwa Kiebrania, maana yake watu wanaojua maandiko lakini pia waliitwa wenye
hekima.
Ezara 7:10 “Kwa
maana huyo Ezra alikuwa ameuelekeza moyo wake kuitafuta sheria ya Bwana, na
kuitenda, na kufundisha maagizo na hukumu katika Israeli”.
Mafarisayo.
Kundi
lingine la kidini katika dini ya kiyahudi waliokuwepo pia wakati wa agano jipya
na wakati wa Yesu walijulikana kama Mafarisayo hawa walikuwa watu walijitahidi
sana kuishi kwa haki na kuitii sheria ya Mungu kivitendo na kwa kujiamini na
kujivunia Yesu alilitaja kundi hili kwa sababu lilikuwa na bidii katika utii wa
torati lakini sio kwa moyo mweupe na hata wale waliokuwa na moyo mweupe
waliishika sheria katika misingi ya kujipatia haki nje ya neema ya Mungu Matendo
26:4-5 “Kwa
maana Wayahudi wote wanajua maisha yangu tangu ujana, yaliyokuwa tangu mwanzo
katika taifa langu huko Yerusalemu, wakinijua sana tangu mwanzo, kama wakipenda
kushuhudia, ya kwamba nalikuwa Farisayo kwa kuifuata madhehebu ya dini yetu
iliyo sahihi kabisa”
•
Pamoja na Torati ya Musa pia waliamini
maandiko mengine ya manabii na masimulizi ya kale ya kiyahudi kuwa ni neno
kamili la Mungu
•
Walikazia sana maswala ya uadilifu kuliko
Theolojia
•
Waliamini kuwa kuna maisha baada ya kufa, na
pia wafu watafufuliwa
•
Wakliamini uwepo wa malaika, maono, na kuwepo
kwa pepo wabaya
Haki yenu isipozidi hiyo haki ya
waandishi na mafarisayo!
Moja
ya maandiko ambayo hutumiwa vibaya na wahubiri wengi wa injili ni na walimu wa
Biblia ni pamoja na andiko hili *Mathayo
5;20*
Maana nawaambia haki yenu isipozidi Hiyo haki ya waandishi na mafarisayo
hamtaingia kamwe katika ufalme wa Mbinguni*”
kimsingi kutokana na maandiko haya wakristo waliookoka na hata wale wasiookoka
wametengenezewa makongwa mengi na mazito
sana siku zote watafasiri wa neon la
Mungu au maandiko wakikosea hata kidogo tu katika kuitafasiri maandiko wanaweza
kusababisha tatizo kubwa sana sawa na Daktari kuzidisha dozi au kutoa dozi
iliyo chini ya kiwango na ndivyo ilivyotokea kwa miaka mingi katika tafasiri ya
mstari huu hebu sasa tuuangalie tena mstari huu kwa kina kwa kawaida mstari huo
unasomeka hivi “*Maana nawaambia haki yenu isipozidi Hiyo haki ya waandishi na
mafarisayo hamtaingia kamwe katika ufalme wa Mbinguni*” ndugu msomaji wakristo wengi narudia tena wamefanywa kuwa watumwa na kubeba
mizigo isiyowahusu kupitia andiko hili jinsi andiko hili lilivyo na kile
kinachotafasiriwa au kukaziwa na wahubiri na badhi ya walimu wa maandiko ni tofauti sana
na hata na jinsi Kristo alivyokusudia
andiko hili kutumika.
Kwa
ujumla kile ambacho wahubiri na waalimu
wengi wa neon la Mungu wengi wanakimaanisha katika maandiko haya ni kama
maandiko haya yanasomeka hivi “*Maana nawaambia Matendo yenu yasipozidi Hayo Matendo ya
waandishi na mafarisayo hamtaingia kamwe katika ufalme wa Mbinguni*”
nimewahi kuwasikia wahubiri wakikazia wakristo kuwa na matendo yanayowazidi
mafarisayo na waandishi yaani waalimu wa sheria tunapounganisha na swala zima
la wokovu mafundisho ya aina hiyo sio injili sahihi tuliyoipokea toka kwa
Bwana,
Wakati
Fulani kwa sababu ya mafundisho ya aina hiyo nilikuwa nimejipangia kuwa ni
lazima niamke kuomba Alfajiri kama vile waislam wafanyavyo na kwakuwa niliamini
kuwa wao hawana Mungu wa kweli na aliye hai kama niliye naye, Na kutokana na msisitizo wa
mahubiri ya wachungaji wengi nilijifunza kuwa ninalazimika kuamka kabla ya
Waislamu hawajaamka na kumuomba Mungu ili
matendo yangu yazidi hayo matendo ya mafarisayao na kwakuwa maisha yangu ya
mwanzo kabla ya kumjua Mungu nilikuwa nikilala na kuamka kwa saa nilizotaka
uamkaji wa Alfajiri lilikuwa jambo jipya katika maisha yangu na halikuwa jambo
jepesi kusema ukweli. niliambiwa kuwa huko Korea ya kusini wakristo huamka
alifajiri na kumuomba Mungu na wamepata mafaniko makubwa sana lakini sisi
Afrika Mashariki wamishionari wetu waliokuja mapema na kuleta Ukristo hawakuwa
wametufunza kuamka alfajiri kwa Msingi
huo mwanzoni nilichapa usingizi lakini nilipomjua Mungu na kujifunza kuhusu
kuamka alifajiri niligundua kuwa ninapaswa kuwawahi waislamu na siku kama
ikitokea nimechelewa kuamka na wakanitangulia nilijihisi vibaya na kuonakama kuwa siku hiyo ni chungu na sio siku nzuri na labda imeharibika na nilihisi au niliiishi
kwa maumivu ambayo sikuwa nayo kabla ya kuokoka kwa nini nilijifunza kuwa
matendo yangu lazima yazidi yale ya Mafarisayo.
Kumbe
nilikuja kugundua siri kutoka kwa Roho wa Mungu kuwa Mungu hakumaanisha kile
nilichokifanya kimsingi Yesu alikuwa akizungumzia “*HAKI*” na sio “*MATENDO*”
nililazimika kujifunza kuhusu haki kama mstari halisi unavyosema na niligundua
kuwa kwanza hakuna mwanadamu mwenye haki hata mmoja *Warumi 3:10-12, Biblia inasema hivi “Kama ilivoandikwa ya kwamba hakuna mwenye
haki hata mmoja hakuna afahamuye, Hakuna amtafutaye Mungu Wote wamepotoka
wameoza wote pia hakuna mtenda mema la! Hata mmoja”* nilijiuliza kama hakuna mwenye haki hata mmoja
inakuwaje Yesu aseme haki yetu isipozidi haki ya mafarisayo hatutauona ufalme
wa Mbinguni?
Nikagundua
kuwa kumbe Mafarisayo hawakuwa na haki hawakuwa na haki ya kweli haki
waliyokuwa nayo ilikuwa haki ya nje tu, Yesu aliwataja waandishi kwa sababu
walikuwa wasomi waliobobea katika maandiko na aliwataja mafarisayo kwa kuwa
walikuwa na juhudi ya kutafuta haki kwa nguvu zao, Makundi haya yalikuwa na
haki ya nje ya kidini tu na haikuwa haki yenye faida yoyote kwa ufalme wa Mungu
haki yao iliwekwa katika misingi ya matendo ya nje yasiyotoka moyoni na yenye
kubeba utukufu wa kibinadamu tu na zaidi sana waliwadharau watu wengine
wakifikiri kuwa watu hao ni wenye dhambi na wasiofaa au ambao hawawezi
kukubaliwa na Mungu kwa sababu ya kujifikiri kuwa waio ni bora zaidi ona kwa mfano Luka 18:10-14 “Akawaambia
mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine
wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili
mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu,
nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu,
wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa
zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala
hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema,
Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda
nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye
atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.” Unaweza kuona kwa hiyo kwa
mtazamo wa nje na wa kibinadamu waandishi na Mafarisayo waliokuwa wenye haki
iliyochanganyika na kiburi, wakijidhani kuwa wao ni watakatifu na wenye kibali
kwa Mungu kuliko wengine walikuwa hawana ujuzi kuwa Mungu ndiye mwenye
kutuhesabia haki na kuwa ni Mungu ndiye anayeujua moyo wa Binadamu.
“*Mathayo
23;25-28* “Ole
wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na
bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema,
na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache.Viongozi
vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia. Ole wenu waandishi na Mafarisayo,
wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa
unyang'anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya
kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi. Ole wenu, waandishi na Mafarisayo,
wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje
yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote.Vivyo
hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani
mmejaa unafiki na maasi”.
Yesu
anawaonya mafarisayo “*Ole wenu waandishi na Mafarisao wanafiki …..*” kumbe
mafarisayo walikuwa wanafiki hawakuwa na haki ya kweli, Haki yao ilikuwa haki
ya nje walifanya mambo ili waonekane na watu *Mathayo 23;5a* “*Tena matendo
yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu*;” kumbe mafarisayo haki yao ilikuwa ni haki ya nje haki ya
kujionyesha tu walionekana na watu kuwa ni wenye haki lakini kwa kweli hawakuwa
na haki ya kweli na ndio maana na sio hivyo tu walikuwa na dhambi ya dharau au
walikuwa na kiburi wakijifikiri kuwa waoa ni watakatifu au wana kibali kwa
Mungu kuliko watu wengine waliowadhani kwa akili zao na mawazo yao kuwa ni
wenye dhambi ona maneno haya Luka 18:9 “Akawaambia
mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine
wote.” Ni
kwaajili ya haya utaweza kuona kuwa Yesu alisisitiza kuwa ni lazima iwepo haki
mbadala, haki ambayo ni tofauti na haki na ile ya waandishi na mafarisayo ambayo kimsingi ni haki ya nje. Sasa ili mtu aweze kuingia katika ufalme wa
mbinguni hawezi kuingia kwa haki kama ile ya waandihi na mafarisayo ambayo
ilikuwa ya nje ni kweli walionekana wanashika sheria walionekana wanaomba,
walisifu na kufunga walisoma neno la Mungu
na hata kuhudhuria ibada hata
hivyo walifanya hayo ili waonekane na watu wasifiwe waonekane kuwa wao ni wa
kiroho na washika dini wakubwa huu haukuwa mtazamo sahii, haki mbadala ni haki
ambayo haitokani na matendo ya sheria ni
haki kutoka moyoni ni haki itokanayo na imani
ni neema ya kukubali kazi aliyoifanya Yesu Kristo kwaajili yetu
Msalabani ni haki itokanayo na Kristo *Warumi
3;21-26*Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria;
inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani
katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; kwa sababu wote wamefanya dhambi, na
kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa
njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe
upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake,ili aonyeshe haki yake ,kwa
sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa MUNGU dhambi zote zilzotangulia
kufanywa.apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye
kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu.*
Angalia pia Waefeso 2;1-9 *Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo
mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme
wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi; ambao
zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu,
tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa
hasira kama na hao wengine. Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa
mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya
makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema.
Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho,
katika Kristo Yesu; ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa neema
yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu. Kwa maana
mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu,
ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu”
hii ndio haki mbadala aliyoizungumzia Bwana
Yesu kwa hiyo Kristo hajatuita katika mashindano ya kuwazidi wale tunaowaita
mafarisayo kwa matendo kama ukifanya hivyo wakikushinda unakuwa chini ya kongwa
ambalo hata kabla ya kuokoka hukuwa nalo, Mtu anapomuamini Yesu mara moja Yesu
anafanyika kuwa haki yetu ipatikanayo kwa neema na wala sio kwa matendo neema ya Kristo ndani yetu inatugeuza na
kutufanya kuwa wema yenyewe na hivyo kutupelekea katika Tito 2:11-12 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo
yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na HAKI,
na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;” Kwa
hiyo Yesu hakumaanisha kuwa matendo mema ni mabaya la hasha matendo mema
yanakubalika kwake ykihusisha imani na rehema kutoka kwake Yesu yeye ndiye
anakuwa haki yetu ambayo ni zawadi kutoka kwake ni neema kutoka kwake Biblia inasema hivi
1Wakoritho
1:30 -31 “Bali
kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima
itokayo kwa Mungu, na HAKI, na utakatifu, na ukombozi; kusudi, kama
ilivyoandikwa, Yeye aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana.”
2Wakoritho 5:21 “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili
yetu, ili sisi tupate kuwa HAKI ya Mungu katika Yeye.”
Kumbe
unaweza kuona haki halisi haitokani na nafsi zetu haki halisi ni ile tunayopewa
kwa imani kwa kumuamini Yesu na kukubali kazi yake aliyoifanya pale msalabani,
ni aina hii ya haki ndiyo ambayo Yesu alikuwa anaizungumzia na manabii
walitabiri kwa kumuamini Mungu yeye sasa anafanyika kuwa haki yetu
Yeremia 23:5-6 “Tazama siku zinakuja, asema Bwana, nitakapomchipushia
Daudi Chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye
atafanya hukumu na haki katika nchi. Katika siku zake Yuda ataokolewa, Na
Israeli atakaa salama, Na jina lake atakaloitwa Ni hili, Bwana ni haki yetu.”
Kujaribu
kwa njia za kibinadamu kuishi maisha ya kujitafutia haki bila imani kwa Yesu
Kristo kutatufabya tuishi katika Kongwa kubwa sana la matendo yatakayotufanya
tuuone wokovu kuwa ni kitu kigumu sana na kumbe wokovu ni mwepesi na raha
nafsini mwetu
Ukiyajua hayo heri wewe ukiyatenda
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!
Maoni 2 :
Kazi Yako siyo Bure Mwalimu wangu .. Let the fire burning 🔥🔥
Kazi Yako siyo Bure Mwalimu wangu.. 🔥🔥🔥 Mchungaji Joshua Mapamba
Chapisha Maoni