Andiko la Msingi: Luka 2:41-49 “41.
Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. 42.
Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi
ya sikukuu; 43. na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule
mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari.
44. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa,
wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; 45. na walipomkosa, wakarejea
Yerusalemu, huku wakimtafuta. 46. Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni,
ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47. Nao wote
waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. 48. Na walipomwona
walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama,
baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni.49. Akawaambia, Kwani
kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu?”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa mara baada ya sikukuu ya krismas Kanisa huwa linasheherekea siku ya familia takatifu, Tayari Yesu Kristo amezaliwa na tayari imekuwa familia kamili, Yenye baba, Mama na mtoto, hii sasa ni familia ya watu wanaomcha Mungu, Familia ndio asili ya kila kitu, hakuwezi kuwa na taifa pasipo familia, hakuwezi kuwa na kabila pasipo familia, hatuwezi kuwa na viongozi wazuri wasiotoka katika familia, hatuwezi kuwa na watetea haki, waamuzi, wanamapinduzi, manabii, na wachungaji ambao kwa namna moja ama nyingine hawajatokana na familia, hivyo familia ndio taasisi ya kwanza kabisa kabla ya kuweko kwa taasisi nyingine, Kwa msingi huo basi ili tuweze kuwa na kila jambo zuri, lazima jambo hilo lianzie katika familia, Leo tutachukua muda kujifunza namna familia ya Yesu, ambayo ilimjumuisha Mariamu, mama yake na Yusufu Baba yake mlezi na kijana mtoto Yesu. Hii ilikuwa ni familia ambayo imeleta Baraka kubwa sana duniani na hivyo kuna mambo ya kujifunza
1.
Hakuna
familia isiyokuwa na Changamoto.
Ni muhimu kufahamu kuwa kila familia inapitia changamoto zake, Familia ya Yesu ilipitia changamoto za aina mbalimbali, Lakini kutokana na kumtanguliza Mungu, Mungu aliwatoa katika changamoto hizo:-
a. Walipitia katika umasikini uliokithiri ;-
Kabla ya Yesu kuzaliwa ni wazi kabisa kuwa Yusufu na
Mariamu hawakuwa na uchumi mzuri, walikuwa na ukata, usafiri waliotumia ulikuwa
usafiri wa punda, sadaka walizokuwa
wakitoa Hekaluni ilikuwa ni njiwa wawili ambayo ni sadaka ya chini mno iliyotolewa
na watu waliokuwa masikini, Hata hivyo umasikini huu haukuwa sababu ya
manung’uniko kwao, wala sababu ya kuiba, au kutapeli, au kukopa na
kutokurudisha, au kuomba omba, waliweza kuvumilia na kuendelea kumtegemea Mungu
huku wakifanya kazi kwa bidii, Maisha yao yalibadilika baadaye baada ya sadaka
ya Mamajusi waliotoa dhahabu, uvumba na manemane hivyo ndio viliweza kuibadili
hali ya familia hii iliyomtegemea Mungu, Wakristo lazima tujifunze kuwa
wavumilivu na kuusubiri wakati wa Mungu wa kutufanikisha bila kupitia short cut
kwani Mungu ana majira na nyakati za kutubariki, Familia hii ilivumilia magumu
na changamoto walizozipitia mpaka Mamajusi walipotoa zawadi zilizowatajirisha
sana ona
Mathayo 2:10-12 “10. Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno.
11. Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka
wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na
uvumba na manemane. 12. Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie
Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.”
Tunaimba kwamba mjini
mwaka mfalme Daudi palikuwa zizi nyoge... Yesu alizaliwa katika hali ya unyonge
lakini maisha ya uvumilivu na subira ilibadilisha maisha ya familia yake na
wakawa sasa wana uwezo wa kwenda Misri na kuishi huko kwa muda wakijikimu
maisha yao, Lazima kila familia iwe na uvumilivu, usijilinganisha na watu
wengine mtegemee Mungu, na Mungu atawabariki
b. Walimsikiliza Mungu (Walitii mapenzi ya
Mungu):-
Familia takatifu lazima iwe na uwezo wa kumsikiliza
Mungu, Kumsikiliza Mungu ni kulisikiliza neno lake, kusikiliza watumishi wake
na kuhudhuria ibada, Familia hii iliweza kudumu kwa sababu ilikuwa familia ya
wazazi ambao wote walikuwa na uwezo wa kumsikiliza Mungu, kuliko kusikiliza
maneno ya watu wa mtaani, Yusufu alipoona Mariamu ana Mimba biblia inasema
aliamua kumuacha kwa siri! Unaona lakini mapema sana Malaika wa Bwana alimuonya
Yusufu asimuache mariamu mkewe, ona katika
Mathayo
1:19-21 “19. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile
alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. 20.
Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto,
akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba
yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 21. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina
lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.”
Unaona
Kama Yusufu angekuwa ni mwenye kusikiliza maneno ya watu wa mitaani ndoa yake
ingevunjika mapema na familia hii isingekuwa Baraka kwa dunia, Familia takatifu
ni lazima iwe familia inayosikiliza maneno ya Mungu na kufuata uongozi wa Mungu,
ni kwa kujua unyenyekevu na usikivu wa Yusufu, Mungu alisema na Yusufu tena
kupitia malaika wake ili kukimbilia Misri na kuyalinda au kuyatunza maisha ya
Yesu asiuawe na Herode ona
Mathayo 2:13-14 “13.
Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu
katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri,
ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize.
14. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri;”
Unaona
ni maisha ya usikivu wa Yusufu ulioweza kumfanya Mariamu na mtoto Yesu kuwa
salama kule misri na kuepuka kifo kutoka kwa Herode, Leo hii familia nyingi
zinaharibika na watoto wanaenea mitaani wakipoteza muelekeo, au hata wakikosa
kusoma kwa sababu ya wazazi waliokosa usikivu kwa Mungu na kwa wazazi, vijana
wengi wanaishi vile wanavyojisikia na kujibu kile wanachojisikia na hata wazazi
wamekosa kuwa mfano bora kwa kuigwa na watoto wao kwa sababu ya kutikumcha
Mungu, Yusufu, na Mariam na Yesu walikuwa ni familia ya mfano katika kumcha
Mungu.
c. Walimuabudu Mungu;’-
Mstari wa msingi tuliousoma unasema “Basi, wazee
wake huenda Yerusalemu kila mwaka,” Unajua maana yake nini
hawakukosa ibada kuu katika hekalu lililokuwako Yerusalem, wazee wake maana
yake wazazi wake kila mwaka walikwenda Hekaluni kusali na hawakuenda wenyewe
walikwenda na vijana wao akiwemo Yesu, wao wenyewe walimuabudu Mungu lakini
waliwafundisha watoto wao kumuabudu Mungu na kumpenda jambo hili lilijenga
uhusiano mkubwa wa Yesu na Mungu baba wa Mbinguni, kiasi ambacho licha ya Yesu
kuwaheshimu wazazi wake alimuona Mungu baba wa Mbinguni kuwa baba yake
Luka 2:48-49 “48.
Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda
hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. 49.
Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba
ya Baba yangu?”
tuwafunze watoto wetu wajue kuwa japo sisi ni wazazi
wao lakini wanaye baba wa Mbinguni wamsikilize, wamtiii wampende wamuabudu
familia takatifu lazima wajijenge tabia ya kuabudu. Kuimba, kuomba, kusoma neno
la Mungu na kuhudhuria makusanyiko ya ibada na kujifunza na kudumisha uhusiano
na Mungu ni jukumu la kila familia kuhimizana na kutiana moyo, kumuheshimu
Mungu.
d. Walipeleka watoto shule
Katika desturi za kiyahudi kijana aliyefikisha miaka
12 alikuwa tayari amefunzwa kuijua Torati na kufanya kazi za kujitegemea,
wengine walijivunza uvuvi, wengine ukulima, wengine ujenzi na wengine kushoma
mahema kama Paulo mtume, Yesu alikuwa na ujuzi wa torati na alikuwa amejifunza
ujenzi “Carpenter” hii iliwajengea watoto uwezo wa kujiamini na
kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha Hivyo Yesu alijengewa kupenda kujifunza
na alikuwa msikivu kwa walimu wake na alikuwa mdadisi aliuliza maswali ona
“Luka 2:45-47 45.
na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. 46. Ikawa baada ya siku
tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza
maswali. 47. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake.”
Familia takatifu na iliyo njema inapaswa kuhakikisha kuwa watoto wao
wanapata Elimu nzuri, na wanakuwa na uwezo wa kujitegemea wanaweza kufanya kazi
mbalimbali, na wanakuwa na ujuzi wa maadili na sheria za ukoo na familia zao,
leo hii tunaona kuna mmomonyoko mkubwa wa uadilifu lakini ni kwa sababu tatizo
kubwa limeanzia katika ngazi ya familia, wazazi wanapaswa kuwa kitu kimoja na
kuhakikisha kuwa wote kwa pamoja wanawajengea watoto uwezo wa kijitegemea ili
watoto hao wasigeuke kuwa mzigo kwetu endapo hatutawaandaa vema Yesu alijengewa
uwezo mkubwa sana na hatimaye akawa Mwalimu mwema alikuwa na wanafunzi 12
maalumu na wanafunzi wengine wengi, aliuitwa RABBI yaani Mwalimu, uwezo wake
mkubwa wa kufundisha ulitokana na uwezo wake mkubwa wa kujifunza, kawaulize
walimu hakuna Mwalimu mzuri ambaye sio mwanafunzi mzuri, Lazima tuwajengee
uwezo wa kielimu watoto wetu
e. Waliwalea watoto wao katika uadilifu
Tunasoma hivi katika Luka 2:52 “Naye Yesu akazidi kuendelea
katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.”
Swali jepesi
la kujiuliza je watoto wetu leo na familia zetu leo zinampendeza Mungu na
wanadamu? Tunaambiwa Yesu alizidi kukua akiwa na hekima lakini vilevile
akimpendeza Mungu na wanadamu, Je tunampendeza Mungu na wanadamu, hii haiwezi
kutokea kama hatutakuwa chuo cha maadili kwa vijana wetu, ni muhimu kuwafunza
watoto wetu, na kuwalea katika uadilifu, tikifanya hivi tutakuwa na watoto
wenye muelekeo thabiti katika taifa letu, leo hii tujnashuhudia mmomonyoko
mkubwa waa maadili lakini sababu kubwa ni kuanzia ngazi ya familia kutokujali
uadilifu na mwenendo mwema kwa watoto wetu.
f.
Walijali
Ndugu jamaa na kule walikozaliwa/kulelewa
“Human being is a
social being” Mungu hakutuuumba tuishi kama kisiwa, aluiposema si vema mtu
huyu awe peke yake alimaanisha wanadamu tunahitajiana wakati mwingine ili uweze
kujengeka unapaswa kuwa na muda wa kusikiliza wengine na hapo ndipo tunapoweza
kujengwa na kukua au kutiana moyo, Mariam alipopata ujauzito wa ajabu malaika
alimueleza kuwa jamaa yako Elizabeth pia
ana mimba ya mtoto wa kiume, kusudi kubwa ilikuwa ili Mariamu aweze kutiwa moyo
kustahimili kile kilichomtokea hivyo Mariamu alimtembela Elizabeth ona
Luka 1:36-44 “36.
Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume
katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; 37. kwa
kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. 38. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni
mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka
akaenda zake. 39. Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya
milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, 40. akaingia nyumbani kwa Zakaria
akamwamkia Elisabeti. 41. Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake
Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho
Mtakatifu; 42. akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika
wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. 43. Limenitokeaje neno hili,
hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? 44. Maana sauti ya kuamkia kwako
ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya
tumbo langu.”
Unaoma Mariamu anamtembelea Elizabeth anajifunza mambo
mablimbali kutoka kwa mwanamke mzee mwenye uzoefu wa kutembea na Mungu, na
hivyo anajifunza mambo mbalimbali Mariamu kutoka kwa watu wa rika linguine je
leo hii wanawake watu wazima huwafunza wanawake vijana ? je watu hutembeleana
nyakati za leo? Je watu hutembelea kule
walikozaliwa au kulelelwa familia zenye upendo hutembeleana Yesu pia
alitembelea Nazareth kule alikolelewa na kuwafundisha mambo makubwa ya Mungu
ona
Luka 4:16-21 “16. Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato
akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome.17.
Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa,
18. Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini
habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu
kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, 19. Na kutangaza mwaka wa Bwana
uliokubaliwa. 20. Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote
waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. 21. Akaanza kuwaambia, Leo
maandiko haya yametimia masikioni mwenu.”
Yesu alienda Nazareth kule
alikolelewa, Ni muhimu kukumbuka na nyumbani, watu wengi sana wanapofanikiwa
hawakumbuki nyumbani, watu wengi wa Tanga waliosoma zamani walitawanyika huko
na huko na kusaidia watu wengine na kuwaelimisha lakini waliisahau Tanga, wabunge wengi
hukumbuka nyumbani wajkati wa kupiga kura, Yesu pamoja na umaarufu wake
wote na alikuwa Mungu hakuweza kusahau kule alikolelewa, tunawashangaa wachaga
tu wanapoenda nyumbani msimu wa sikukuu, hebu na sisi tujifunze na kukumbuka
kuenda kule tulikolelelwa na kukulia na kuwa Baraka kwao pia
Tuwe tayari kujitoa kwa wengine
Kusudi kubwa la Yesu kuzaliwa ni
ili awaokoe watu wake na dhambi zao Yusufu alielezwa hili mapema ona
Mathayo 1:20-21 “20.
Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto,
akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba
yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 21. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina
lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.”
Yusufu alielezwa mapema kuwa Yesu ni mwokozi, familia ina wajibu wa kulea
vijana na kukuza viongozi ambao watakuwa faida si kwaajili yao tu bali kwaajili
ya ulimwengu mzima Mariamu pia alijulishwa kuwa mtoto wake sio wake pekee bali
amewekwa kwaajili ya wenginona
Luka 2:34-35
“34. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama
yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli,
na kuwa ishara itakayonenewa. 35. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako,
ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.”
Ilikuwa wazi kuwa Mungu
aliwaamini Mariamu na Yusufu kuwa walezi wa kiongozi mkubwa ambaye atakuwa
Baraka kubwa kwa ulimwengu ni mwokozi wa ulimwengu, kama familia hatuna budi
kuwatunza wanafamilia wote na kuwasaidia kutimiza ndoto zao ili makusudi yote
ya Mungu yapate kutimizwa ndani mwao, nani ajuaye kuwa mtoto uliyembeba ni
Raisi ajaye, ni Mwalimu ajayem, ni daktari ajaye, Mungu ana makusudi na kila
aliyezaliwa na hakunanayezaliwa kwa bahati mbaya hivyo tuendelee kuwa na ustawi
katima familia zetu ili Mungu ajiinulie watumishi wake kutioka katika familia
zetu watakaokuwa Baraka kwa wengine
Yohana 13:17 “Mkiyajua hayo heri ninyi
mkiyatenda!”
Bwana Mungu awabariki na kuwafadhili tunapoadhimisha siku ya familia
takatifu katika jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu amina
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!
0718990796
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni