Ijumaa, 25 Desemba 2020

Upendo mwingi!

Yoahan 15:13 “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.”



Utangulizi:

Moja ya maagizo ya mwisho kabisa ya Yesu Kristo kwa wanafunzi wake kabla ya kuteswa, kufa na kufufuka ilikuwa ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wake wanakuwa na upendo, wote tunafahamu kuhusu kupenda, lakini Yesu hakutaka tu tuwe tunapenda lakini alitaka wawe na upendo mwingi sana, unaweza kujiuliza upendo mwingi ni upendo wa namna gani? Biblia nyingine za Kiswahili zinatumia neno upendo mkuu, biblia ya kiingereza inatumia neno “The Great love” ambalo ka Kiswahili ni Upendo mwingi au upendo mkuu! Kwanini Yesu anazungumzia upendo mwingi kwani kuna upendo kidogo au mchache ndio kuna upendo kamili “Perfect Love au “sacrificial love” na upendo mwingine wenye upungufu!

Katika Lugha ya kiyunani neno upendo linaelezewa vizuri, sana kwa kuzingatia maeneo manne

1.       Phileo – Huu ni upendo au uhusiano wa kirafiki, unampenda mtu kwa sababu ni rafiki yako mahusiano yenu ni ya kirafiki, upendo huu una mipaka, kwa sababu unaweza kufa unaweza kuharibika ndio maana unaweza kuona watu wanafarakana na wanaweza hata kusalitiana na urafiki ukageuka kuwa uadui mkubwa

2.       Storge – Huu ni Upendo au uhusiano wa kindugu, unampenda mtu kwa sababu ni ndugu yako, mna uhusiano wa damu, uhusiano wa kubaiolojia ni babam ni mama, ni mama mdogo ni baba mdogo, ni binamu, ni shangazi, ni babu, ni bibi na kadhalika upendo huu pia una mipaka na unaweza kuharibika na ndugu wakageuka kuwa maadui wakubwa sana

3.       Eros – Huu ni upendo au uhusiano wa kimapenzi, ni upendo wa asili ya kibinadamu ambao mvutio wake unatokana na mapenzi, so unaweza kumpenda mtu kwa sababu ana usio mzuri, hana malolo, Yakobo alimpenda Raheli kuliko Leah kwa sababu Lea alikuwa na macho dhaifu alikuwa na malolo, unaweza kumpenda mtu kwa sababu ana makalio makubwa, mazito, hips za kutikisa dunia, ana chuchu zilizosimama, saa sita ni mkwaju wa nguvu umbo namba nane, potable au ana mzigo mzito wa kitikisa dunia na kadhalika huu ni upedno wenye hisia za kimapenzi

4.       Agape – Upendo huu sasa ndio unaoitwa upendo mwingi, ni upendo wenye kujitoa sacrificial love , upendo huu ni mgumu kuwa nao, ni watu wachahce sana wanaweza kuwa na upendo kama huu, Yesu aliuita upendo huu kuwa ni upendo mkuu, ni upendo mwingi, unahusisha kupenda mpaka kuyatia maisha yako kwaajili yaw engine Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele upendo huu mtu akiwa nao ndio tunasema amekomaa kiroho, ni upendo ambao una sifa za kipekee 1Wakoritho 15:1-13Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu. Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika. Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika. Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto. Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana. Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.”

 

Ukomavu wetu wa juu sana Kiroho utajulikana pale tunapokuwa tayari kuyatoa maisha yetu kwaajili ya wengine 

 

Yuda - Mwanzo 44:1-34,·  Alikuwa mwenye upendo mwingi sana alikuwa tayari kufa kwaajili ya kuitunza familia yake na baba yake na kwaajili ya ndugu zake

Daudi - 2Samuel 18:31-33·   alikuwa na upendo mwingi kiasi ambacho alilia kwaajili ya Absalom mwanaye japokuwa yeye alikuwa amekusudia kumuua baba yake

 

Yesu Kristo Yohana 15:13:- “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake· kwa ajili ya rafiki zake”.

 

1. Daktari mmoja wa Uingereza aitwaye Will Pooley alikuwa ni moja ya madaktari waliokuwa mstari wa mbele Nchini “Sierra Leone” huko walikuwa na wenzake wengi wakipambana na wagonjwa wa EBOLA na virusi vyake katika harakati hizo Madaktari wengi sana na Manesi wengi sana wakiwemo wa Afrika Magharibi waliambukizwa virusi vya ebola wakati walipokuwa wakiwauguza wagonjwa na wengi wao walikufa Ugonjwa utokanao na kirusi cha Ebola ni ugonjwa hatari wenye uwezo wa kusababisha kifo kwa asilimia 90. Shirika la afya duniani, WHO katikatovuti yake inasema kwa mara ya kwanza ulibainika mwaka 1976 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Sudan. Chanzo cha kirusi hiki hadi sasa hakijulikani lakini popo aina ya (Pteropodidae) wanaonekana kuwa wabebaji wa kirusi hicho, kwa mujibu wa ushahidi uliopo sasa. Maambukizi hupatikana kwa kila aina ya majimaji yanayotoka katika mwili wa binadamu ni ugonjwa hatari na unaoua kwa haraka na hauna tiba Will Pooley alipoupata ugonjwa huu alirejeshwa katika ndege maalumu na kuanza kutibiwa chini ya uangalizi maalumu huko uingereza Jambo la kushangaza ni kuwa baada ya kupona kwa bahati tu Will Pooley alitangaza nia yake ya kurudi tena Sierra Leone kusaidiana na wenzake kupambana na ugonjwa huo. Mtu huyu aliwashangaza wengi sana na kuwaogopedha wengi sana akiwa amepona kwa asilimia 100%alisema atarudi Africa kusaidia zaidi maana alizaliwa kwaajili ya hayo, jambo hili lilimfanya aandikwe kama shujaa na mwanadamu mwenye uwezo wa kujitoa kwa kiwango cha juu.

 

2. Maximilian Kolbe alikuwa ni Padre aliyetokea Poland aliuawa kama mfungwa tarehe 14 August 14,1941, Jeshi la wa NAZI waligundua kuwa baadhi ya wafungwa wamejaribu kutoroka na hivyo waliamua kuwaua wafungwa kadhaa, walijaribu kuwaua kwa njia mbalimbali, na hivyo walichagua wafungwa 10 ili wauawe na kifo chao kiliamuriwa kuwa kifo cha njaa, wafungwa waliamuriwa kujitoa mmoja mmoja yeye mwenyewe na mfungwa wa kwanza kuchaguliwa alijulikana kama Franciszek Gajowinczek mfungwa huyu alipochaguliwa alilia kwa huzuni kubwa akimtaja mkewe, watoto wake na familia yake na kusikitika kuwa hatowaona tena kutokana na swala hili Maximillian alisimama na kusogea mbele na kuomba afe yeye kwa niaba ya Franciszek ombi lake lilikubaliwa, wafungwa waliwekwa kizuizini kwa muda wa siku kadhaa bila kula wengine walikunywa mikojo yao ili waweze kuishi, Maximillian alikaa kwa wiki mbili bila kufa huku wengine wote wakiwa wamekufa, walimchoma sindano ya kufa hakufa na hivyo waliamua kukata kichwa Pope John Paul II alimtangaza kuwa Mtakatifu kutokana na moyo wake

 

3. Mifano hii inatusaidia kujua kile ambacho Bwana wetu Yesu amekifanya Pale alipojibu kuwa kwaajili ya haya Nalizaliwa alikuwa akimkumbusha Pilato kuwa yeye amekuja kuwafia wanadamu, amekuja kuwaonyesha upendo wa Mungu jinsi ulivyo Isaya 53:1-5 “Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.” Huu ni upendo mkubwa sana Yesu alikufa kwaajili yetu, Hatuna budi kuhakikisha kuwa tunasimama upande wake siku zote za maisha yetu, tusihesabu damu yake ya thamani kuwa kitu cha hovyo tudumu katika wokovu na kuwa wavumilivu kwaajili ya Mungu wetu.”

Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: