Jumapili, 27 Desemba 2020

Usimwambie Yakobo neno la heri wala la Shari!

Mwanzo 31:24 “Mungu akamjia Labani, Mshami, katika ndoto ya usiku, akamwambia, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari.     


Utangulizi:

Je umewahi kupitia mambo magumu katika maisha yako mpaka unaamua kukimbia? Umewahi kupitia mitihani mizito mpaka unaamua kufanya maamuzi magumu?  Maisha ya Yakobo yaani Israel duniani hayakuwa mepesi kama tunavyoweza kufikiri, alipitia mambo magumu mno, alipitia maisha ya taabu na dhiki kuliko Ibrahimu na Isaka baba zake ona

Mwanzo 47:7-9 “Yusufu akamleta Yakobo babaye ndani akamweka mbele ya Farao Yakobo akambariki Farao.  Farao akamwuliza Yakobo, Je! Siku za miaka ya maisha yako ni ngapi? Yakobo akamjibu Farao, Siku za miaka ya kusafiri kwangu ni mia na thelathini; siku za miaka ya maisha yangu zimekuwa chache, tena za taabu, wala hazikufikilia siku za miaka ya maisha ya baba zangu katika siku za kusafiri kwao.”

Moja ya maeneo ambayo huenda Israel aliyakumbuka katika taabu alizozipitia ni pamoja na maisha yake  ya ujombani, alikokuwa akimtumikia Laban Mjomba wake, Hatimaye Yakobo na wake zake na wanae waliamua kuondoka kwa mjomba kwa kutoroka bila hata kuaga kwa kuhofia kuwa huenda Labani atamuonea tena Yakobo kama alivyomuonea siku zote za maisha yake, Hata hivyo Labani aligundua kutoroka kwa Yakobo na kuwa msafara wake ulikuwa ukielekea Gilead akamuwahi na kumkuta baada ya wiki nzima

Mwanzo 31:21-23 “Basi akakimbia yeye na yote aliyokuwa nayo; akaondoka akauvuka mto, akaelekeza uso wake kwenda mlima wa Gileadi. Hata siku ya tatu Labani akaambiwa ya kwamba Yakobo amekimbia, akatwaa ndugu zake pamoja naye, akamfuata mwendo wa siku saba. Akampata katika mlima wa Gileadi.”

Hatuwezi kujua kuwa Labani alikusudia kumfanya nini Yakobo? Hatujui nini kilikuwa katika akili zake lakini bila shaka alikuwa amenogowa na utumishi wa Yakobo, alitamani kuendelea kumfanya yakobo kuwa mtumwa wake siku zote, hakufikiri wala kutamani kuona kuwa siku moja Yakobo anakuwa huru, anamuabudu Mungu wa baba zake kwa uhuru, ana kuwa na kabila zake mwenyewe, anajitawala na kutimiza hivyo kusudi la Mungu, labani alikuwa ni muabudu miungu, hakuweza kujua kusudi la Mungu ndani ya Yakobo. Lakini alikuwa na hisia zilizowazi kuwa mtu huyu anaye Mungu aliye hai, anajua na kufahamu kuwa Yakobo alitajirika kwa jasho lake huku Mungu wa baba zake akiwa ameweka mkono wake kumbariki mtu huyu aliyeonewa na kupangiwa maisha tangu siku ya kwanza, Labani asingeweza kukubali hata kidogo kumuachia Yakobo kama farao alivyokataa kuwaachia wana wa Israel Kule misri baadaye, Yako mambo ambayo ulimwengu hauwezi kukubali kutuachia wala shetani hakubali kukuachia kwa sababu uweza wa Mungu uko juu yako na adui zako wanafaidika na uwepo wako, Africa wazungu hawawezi kukubali kukuachia ujitawale hawawezi kukuacha uchakate kila ulicho nacho kwa sababu wanafaidika na utumwa wako, wakati mwingine ili tuweze kuwa huru katika eneo Fulani ni mpaka Mungu aingilie kati, na Mungu huingilia kati pale anapoona tu mechoshwa na hali hiyo, hata hivyo Labani hangekubali na hivyo Mungu wa Israel aliingilia kati na kumuonya katika ndoto kwamba Usimwambie Yakobo neno la heri wala la Shari!

Kwa Lugha nyingine usiiingilie kati kusudi la Mungu lililoko ndani yakem usimzuie, Yakobo ni lazima aishi kanaani, ni lazima aende katika nchi ya ahahdi ndani yake kuna kusudi Yeye anajua na Mungu anajua kwa hiyo umemtafuta umemuona lakini lazima umuache aende zake usmwambie la heri wala la shari katika uamuzi wake huu unasikia labani? Labani alikuwa amefikisha Hatua ambayo angeingia kwenye ugimzi na Mungu, alikuwa akimuonea Yakobo mara kadhaa na inawezekana kabisa pia alitaka kumdhuru wakati ulikuwa umefika sasa Yakobo lazima awe huru, na Labani achague kurejea katika nchi yake ama akutane na mkono wa Mungu! Ona

Mwanzo 31:6-16 “Nanyi mmejua ya kwamba kwa nguvu zangu zote nimemtumikia baba yenu. Na baba yenu amenidanganya, akabadili mshahara wangu mara kumi; lakini Mungu hakumwacha kunidhuru. Aliposema, Walio na madoadoa watakuwa mshahara wako, wanyama wote wakazaa madoadoa. Aliposema, Walio na milia watakuwa mshahara wako, ndipo wanyama wote wakazaa wenye milia.  Hivi Mungu akamnyang'anya mali yake baba yenu, na kunipa mimi. Ikawa, wakati wale wanyama walipochukua mimba, naliinua macho yangu nikaona katika ndoto, na tazama, mabeberu waliowapanda hao wanyama walikuwa na milia, na madoadoa, na marakaraka. Na malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, Yakobo! Nikasema, Mimi hapa. Akasema, Inua, basi, macho yako, ukaone; mabeberu wote wanaopanda wanyama wana milia, na madoadoa, na marakaraka; maana nimeona yote aliyokutendea Labani. Mimi ni Mungu wa Betheli, huko ulikotia mafuta nguzo, na kuniwekea nadhiri. Sasa ondoka, toka katika nchi hii, urudi mpaka nchi ile uliyozaliwa. Raheli na Lea wakajibu, wakamwambia, Je! Imetubakia sehemu au urithi katika nyumba ya baba yetu? Hakutufanya kama wageni, maana ametuuza, naye amekula fedha zetu kabisa? Maana mali yote ambayo Mungu amemnyang'anya baba yetu, mali hiyo ndiyo yetu na ya wana wetu. Basi yo yote Mungu aliyokuambia, uyafanye.

Unaona unaposoma kifungu hicho unaweza kuona  na kupata picha ya kuwa maisha ya Yakobo, hayakuwa rahisi, kulikuwa na kila aina ya ukatili   na uonevu kutoka ujombani,  Labani alijaribu kwa kila namna kumfanya yakobo awe mtumwa wake wa kudumu, mtumwa wa maisha yake yote, Mungu alikuwa ni shahidi wa kile Labani alikuwa anamfanyia Yakobo, ni jambo la kushangaza kwamba mjomba wako mwenyewe kaka wa mama yako anakuwa kikwazo cha kusudi la Mungu maishani mwako sasa ilikuwa lazima Yakobo aende Nyumbani, aende alikozaliwa arudi Betheli kwenye nyumba ya Mungu, anede kwenye kusudi la Mungu, aende kwa baba yake aende akamuabudu Mungu wa baba yake katika nchi ya ahadi, Mungu mwenyewe alisema aende na kuwa atakuwa pamoja naye

Mwanzo 31:2-3 “Yakobo akaona uso wa Labani, ya kuwa hakumtazama vema kama jana na juzi. BWANA akamwambia Yakobo, Urudi mpaka nchi ya baba zako na kwa jamaa zako, nami nitakuwa pamoja nawe.”

Inaonekana kulikuwa na hali ngumu katika nyumba ya labani na ni wazi kuwa Israel alikuwa mvumilivu mno, ziko hali zinaweza kukuta mpaka majirani wakaona jinsi unavyoteseka na kuvumilia, ziko hali zinaweza kukukuta mpaka Mungu mwenyewe anakuambia sasa toka na kuwa nitakuwa pamoja nawe

Ni Mungu pia aliyemshauri Yakobo kurejea na ni Mungu aliyemuahidi atakuwa pamoja naye, yakobo alitoroka kama mahusiano yalikuwa mema haiwezekani kutoroka kwa mjomba lakini kutoroka huku kimya kimya kunaashiria kuwa hakli haikuwa nzuri ujombani, Labani anagundua bila shaka anamfuatilia Yakobo akiwa na hasira kali, akiwa amekusudia kumdhuru na kumfanyia jambo baya sana Lakini Mungu wa wote wenye mwili alimkemea Labani alimuonya katika ndoto alimtokea na kumueleza waziwazi Usimwambie Yakobo neno la heri wala la Shari! Ndio  kuna watu ni wakorofi, hatuwawezi kwa akili zetu na unyonge wetu, ndio wenye nguvu, ndio waliotuajiri ndio wajomba zetu lakini Mungu akiwa upande wako hatakuacha uonewe, atamkemea kila mtu anayesimama kinyume na kusudi la Mungu ndani yako kumbuka

Zaburi 105:14-15 “Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao.  Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.

Haijalishi audi zako wana uwezo kiasi gani, wana nguvu kiasi gani, wana uzoefu kiasi gani wana mali kwa kiasi gani vyovyote iwavyo Bwana atawakemea Mungu alimkemea Labani  kwaajili ya Yakobo, Mungu atamkemea kila mmoja anayesimama kinyume nawe kwa kuwa wewe umtumishi wake, Labani ni lazima akumbuke kuwa hawezi kushindana na kusudi la Mungu lililo ndani yako Lazima akumbuke jinsi Mungu alivyomuonya na kusema naye, ana nguvu ana uwezo anaweza kukudhuru lakini Bwana amesema naye ajihadhari asiseme le heri wala la shari nini kingemtokea unajua unaelewa hakuna mtu anaweza kushindana na kusudi la Mungu hata kidogo Labani angeshughulikiwa lakini afadhali alikumbuka maonyo ya Mungu ona

Mwanzo 31:25-29. “Labani akamfikia Yakobo, na Yakobo alikuwa amepiga hema zake katika mlima, na Labani na ndugu zake wakapiga hema zao katika mlima wa Gileadi.Labani akamwambia Yakobo, Umefanya nini? Umenihadaa, ukawachukua binti zangu kama mateka waliotwaliwa kwa upanga. Mbona umekimbia kwa siri ukanihadaa, wala hukuniambia, nipate kuagana nawe uende zako kwa furaha, na nyimbo, na ngoma, na kinubi?Wala hukuniacha niwabusu wanangu, na binti zangu; basi umetenda upumbavu. Ninao uwezo mkononi mwangu wa kukufanyia madhara; lakini Mungu wa baba yako usiku huu ameniambia, akisema, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari.

Nakuombea neema kwa Mungu, wewe unayeteseka kwa sababu mbali mbali, natamka maneno ya kinabii juu yako dhidi ya adui zako dhidi ya wanaokuonea dhidi ya wenye kutunga hila juu yako, kwamba wakuache wajihadhai wasinenen neno la Kheri wala la shari juu yako!  Wewe una Mungu aliye hai, wewe hauabudu vinyago, wewe una kusudi la Mungu ndani yako nasema wakuache nasema wakuache nasema wasikusimange nasema wasikusengenye nasema kwa lugha ya kinabii nawakemea wenye kukusudia mdhara juu yako wasinene wasipange la kheri wala la shari wakumbuke neno hili kwani Mungu yule yule wa Israel Mungu yuleyule wa Yakobo na baba yetu Isaka na Ibrahimu huyu huyo ndiye mtetezi wetu, huyo huyo ndiye atakayefanya njia , huyo huyo ndiye  jemedari wetu, huyo huyo hataacha mtu atuoneee hata kama ni wenye uwezo na mamlaka atawakemea

Baraka za Mungu yule nimuabuduye na ziwe na kila aneysoma waraka huu, Bwana kubariki na kuwa upande wako, wasinene la Kheri wala la shari dhidi yako katika jina la Yesu Kristo wa Nazareth amen

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Maoni 1 :