Mithali 18:10-14 “Jina la Bwana ni ngome
imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama. Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa
nguvu; Ni kama ukuta mrefu katika mawazo yake. Kabla ya uharibifu moyo wa
mwanadamu hujivuna; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu. Yeye ajibuye
kabla hajasikia, Ni upumbavu na aibu kwake. Roho ya mtu itastahimili udhaifu
wake; Bali roho iliyovunjika nani awezaye kuistahimili? ”
Utangulizi:
Kifungu cha mistari ya msingi kwa
ujumla kinazungumzia ulinzi unaopatikana kwa Mungu jinsi ulivyo Muhimu kuliko
ulinzi wa matajiri, au moyo wa mwanadamu
ulioharibika au wenye kiburi na majivuno, Mwenye Hekima hapa anataka kufafanua jambo la
muhimu na la msingi kwamba usalama na ulinzi unaopatikana kwa Mungu ni wa
msingi sana kuliko ule tunaoufikiria kibinadamu na moyoni mwetu! Na kwa sababu
hiyo kulitumainia Jina la Mungu ni kwa Muhimu zaidi ya marafiki, mioyo yetu na
kiburi cha kibinadamu! Lakini hakuna mtu anayemtegemea Mungu au jina lake kisha
Mungu akamuacha aaibike ona
Yeremia 17:5-9 “Bwana asema hivi,
Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake
Na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona
yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi
isiyokaliwa na watu. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni
tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi
yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa
bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa
matunda. Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani
awezaye kuujua? ”
Kwa msingi huo ni wazi kuwa
maandiko yanatuasa kuwa kumtumainia Mungu na jina lake ni jambo la msingi na la
muhimu sana kuliko kuitegemea Hekima ya kibinadamu au kujivunia mitazamo ya
kibinadamu na utajiri wa Dunia hii.
Maana ya Neno Ngome!
Nyakati za Biblia watu walipokuwa
wanajenga miji, walihakikisha kuwa miji yao vilevile inazungukwa na kuta kubwa
ngumu na imara kwa kusudi la kuhakikisha ulinzi na usalama wa watu wote pamoja
na mfalme wa mji ule ili ustawi wa watu uweze kuendelea kuwepo, aidha juu ya
kuta hizo askari walikuwa wakizunguka zunguka kufanya matembezi ya kiulinzi na
pia kulikuwa na minara mirefu ambayo pia ilikuwa na walinzi waliokaa kwa zamu
kwaajili ya kuangalia usalama wa mji na wakati mwingine kutoa taarifa kwa
wananchi na serikali kuhusiana na usalama wao, kwa msingi huo uimara wa mji ulitegemea
sana na Ngome za miji hiyo zikoje Miji mingi katika nchi ya Kanaani ilikuwa
imejengwa kwa ngome imara zisizopenyeka kwa ulaini ambazo pia ziliitwa boma kwa
jina lingine ona
Yoshua 19:35-39 “Na miji yenye boma ilikuwa
ni hii, Sidimu, na Seri, na Hamathi, na Rakathi, na Kinerethi; na Adama, na
Rama, na Hazori; na Kedeshi, na Edrei, na Enhasori; na Ironi, na Migdal-eli, na
Horemu, na Bethanathi, na Bethshemeshi; miji kumi na kenda, pamoja na vijiji
vyake. Huu ndio urithi wa kabila ya wana wa Naftali kwa kuandama jamaa zao;
miji hiyo pamoja na vijiji vyake.”
Ngome au boma katika miji ilikuwa
ni alama kubwa sana ya kuonyesha ulinzi na nguvu kwaajili ya miili, akili,
uwezo, utajiri, ushawishi, ulinzi, uadilifu, nguvu, uthabiti, afya, uwezo wa
kutokuvamiwa na kuonewa, uhakika, uimara, na uwezo wa kutoa mahitaji ya watu,
na usalama, kwa hiyo kila kitu ambacho
kilikuwa kinahifadhiwa na wenye miji yenye boma ndio katika Jina la Mungu navyo
vinapatikana endapo kila mwanadamu atalitumainia na kulikimbilia.
Jina la Bwana ni ngome Imara.
Mfalme Sulemani anaposema Jina la
Bwana Ni ngome imara mwenye haki hukimbulia akawa salama ana maanisha nini? Nyakati za Biblia jina lilikuwa lina maana pana
sana kuliko tunavyoweza kufikiri katika siku za leo, jina lilikuwa
linatambulisha uwezo na mamlaka ya kila kitu alichokuwa nacho Mtu, au mwenye
jina, Jina la bwana ni Ngome imara neno Bwana hapo lilikuwa linasomeka kama YAHWEH na hii ilikuwa inafunua uhalisia
na ukweli wote kuhusu sifa zake zote alizokuwa nazo Mungu, kwa hiyo jina
lilifunua tabia na sifa alizokuwa nazo, kwa hiyo jila la Mtu lilikuwa linauwezo
wa kukupa picha nzima ya anayetajwa katika jina hilo, kwa mfano Mungu
alipojifunua kwa Musa kuhusu jina lake alikuwa anamaanisha maswala kadhaa
yafuatayo:-
Kutoka 34:5-7 “BWANA akashuka ndani ya lile
wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la BWANA. BWANA akapita
mbele yake, akatangaza, BWANA, BWANA, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili,
si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; mwenye kuwaonea huruma watu
elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia
mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao,
na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne.”
Jina la Mungu wetu linafunua
uwezo wake na mamlaka yake na yale yote ambayo Mungu wetu anaweza kutufadhili
kwayo, kwa msingi huo kama Mungu ana uwezo wote ni wazi kuwa jina lake linapita
vyote ni jina ambalo liko juu mno kwa uweza na mamlaka na kwa msaada wowote ule
1. Jina
hili lilo juu mno Zaburi 148:11-13 “Wafalme wa dunia, na watu wote, Wakuu, na makadhi wote wa
dunia. Vijana waume, na wanawali, Wazee, na watoto; Na walisifu jina la Bwana,
Maana jina lake peke yake limetukuka; Adhama yake i juu ya nchi na mbingu.”
2. Jina
hili linafunua ya kuwa yeye anamiliki na kuwa hakuna mfalme wala taifa
linaloweza kusimama mbele yake kila anayesikia matendo yake anatetetmeka Yoshua 2:9-11 “akawaambia
wale wanaume, Mimi najua ya kuwa Bwana amewapa ninyi nchi hii, na ya kuwa hofu
imetuangukia mbele yenu, na ya kuwa wenyeji wote wa nchi wanayeyuka mbele yenu.
Maana tumesikia jinsi Bwana alivyoyakausha maji ya bahari ya Shamu mbele yenu,
hapo mlipotoka Misri, tena mambo hayo mliyowatendea wafalme wawili wa Waamori
waliokuwa huko ng'ambo ya Yordani, yaani, Sihoni na Ogu, mliowaangamiza kabisa.
Na mara tuliposikia hayo mioyo yetu iliyeyuka, wala haukusalia ujasiri wo wote
katika mtu awaye yote, kwa sababu yenu; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu,
katika mbingu juu na katika nchi chini.”
3. Ni
jina ambalo kwalo linaokoa Yoeli 2:32
“Na itakuwa
ya kwamba mtu awaye yote atakayeliita jina la Bwana ataponywa; kwa kuwa katika
mlima Sayuni na katika Yerusalemu watakuwako watu watakaookoka, kama Bwana
alivyosema; na katika mabaki, hao awaitao Bwana.” Warumi
10:13 “kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana
ataokoka.” Matendo 2:21 “Na itakuwa kila
atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa.”
4. Ni
jina ambalo ukilitumia kwenye maombi kuomba lolote utajibiwa ona Yohana 14:12-14 “Amin,
amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye
atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba.
Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani
ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.”
5. Ni
jina lenye uwezo wa kutiisha kila kitu chini yake Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu
alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la
Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya
nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu
Baba.”
6. Jina
hili ni ngome ya kumfanya adui asikupate
Zaburi 61:2-3 “Ee Mungu, ukisikie kilio changu,
Uyasikilize maombi yangu. Toka mwisho wa nchi nitakulilia nikizimia moyo,
Uniongoze juu ya mwamba nisioweza kuupanda. Kwa maana ulikuwa kimbilio langu,
Ngome yenye nguvu adui asinipate.”
Hitimisho
Kwa msingi huo sasa iwapo
unakabiliwa na hali yoyote ya hatari, iwe ya kimwili au kiroho, kiakili au
kisaikolojia na hatari nyingine za aina
yoyote maandiko yanatushauri kuwa ni hekima kulikimbilia jina la Bwana kwani
jina hilo linatoa usalama, usalama maana yake ni kuwa katika ulinzi, kulindwa
na madhara, au kuawa, au kujeruhiwa, au kupotea, na nhatari nyingine yoyote,
Jina la Mungu wetu liko juu ya kila jina
maana yake liko juu ya mamlaka zote, ni salama kwa ulinzi, ni salama kwa
kulikimbilia ni salama kwa kulitegemea, ni nguvu yetu, ni katika jina hili
ndiko kuliko na usalama wa kweli na ulinzi wa uhakika, jina la Bwana ni ngome
imara maana yake hatupaswi kuogopa kama tunaumwa, hatupaswi kuchanganyikiwa
kama tuna huzuni, hatupaswi kuogopa wakitutisha, hatupaswi kuhofia tuwapo,
dhaifu, tunapolemewa na au tunapokuwa na uchumi dhaifu, tunapopatwa na matisho
ya aina yoyote ukweli ni kwamba wakati wowote hatuna budi kukumbuka ya kuwa ni
jina la Yesu ndilo ngome imara hapo ndipo tunapoweza kukimbilia na kuliitia
jina lake kwa msaada tunaouhitaji, Jina lake linawakilisha kila tunachokihitaji,
iwe, Upendo, Rehema, Neema, Nguvu, Haki, na zaidi, Watakatifu waliotutangulia
walilitegemea na kuliitia wakati wote na Mungu akawasaidia ni hekima kubwa
kumkimbilia Mungu, ni ujinga kutegemea wanadamu, na tujiachie katika mikono
yake ili tuwe salama kwani hakuna sababu ya kuogopa
Mithali 29:25 “Kuwaogopa wanadamu huleta
mtego; Bali amtumainiye Bwana atakuwa salama.”
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima !
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni