Marko 10:46-50 “Wakafika Yeriko; hata
alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano
mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando
ya njia. Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti
yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu. Na wengi wakamkemea ili
anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu
akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo;
inuka, anakuita. Akatupa vazi lake,
akaruka, akamwendea Yesu.”
Utangulizi:
Moja ya stori zenye mvuto mkubwa
sana katika maandiko ya neno la Mungu (Biblia) ni pamoja na stori ya kuponywa
kwa kipofu Batimayo, Katika stori hii kuna mambo mazuri sana ya msingi
yakujifunza lakini kwa bahati mbaya wakati mwingine tunakosa kuyagundua mambo
hayo, kuna kitu kikubwa na cha ziada cha kujifunza katika mwenendo mzima wa
stori hii ukiacha uponyaji wenyewe! Lakini kuna mambo ya msingi ambayo Kristo
anatufundisha kupitia tukio hili, kipofu mwenyewe na jamii ya watu waliokuwa
wana mzunguka na kisha tutaweza kujiona sisi wenyewe tunapokuwa katika uhitaji,
tabia ya uungu katika kushughulika na changamoto zetu na tabia ya watu wakati wa
changamoto zetu, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuwa na macho ya rohoni
tunapojifunza somo hili katika jina la Yesu Kristo amen!, tutajifunza somo hili
kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo;-
Dhana potofu wakati wa changamoto!
Tabia ya Mungu wakati wa changamoto
Mambo ya kujifunza kutoka kwa Batimayo
Dhana potofu wakati wa changamoto!
Stori ya uponyaji wa kipofu Batrimayo
inaenda pamoja na ukweli kuwa mwandishi alikusudia chini ya uwongozi wa Roho
Mtakatifu kutufungua macho, ili hatimaye tuweze kuona moja ya changamoto
iliyojengeka katika jamii ya watu wanayoyajua maandiko kama ilivyokuwa kwa
wayahudi dhana hii iko hata leo, hii ni ile dhana ya kufikiri kuwa kila
changamoto inayomtokea mtu katika maisha yake imesababishwa na dhambi, katika
kipindi cha muujiza huu kulikuwa na dhana potofu miongoni mwa wayahudi ya kuwa
watu wenye changamoto kama hii ya kipofu Batrimayo labda huenda imesababishwa na
dhambi, aidha ya mtu mwenyewe au wazazi wake kwa hiyo analipia, hivyo mtu kama
Batrimayo licha ya kuwa na tatizo la upofu lakini vilevile alikuwa amekataliwa
na jamii kwa kufikiri ya kuwa anastahili kubaki katika hali kama hiyo kwa vile
yeye au wazazi wake wanalipia hali anayoipitia ona
Yohana 9:1-3 “Hata alipokuwa akipita
alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa. Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi,
ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu? Yesu
akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu
zidhihirishwe ndani yake.”
Unaona? Ni ukweli ulio wazi
kitheolojia kuwa dhambi ina changamoto zake inazoweza kusababisha majanga
katika maisha yetu, lakini ni muhimu kuweka uwiano kuwa sio kila changamoto
inaweza kuwa na uhusiano na dhambi, hapo wanafunzi pamoja na jamii walihesabu
watu waliokuwa vipofu walikuwa na laana Fulani au malipo Fulani kutokana na
dhambi walizozifanya, sio hivyo tu hata kulipotokea majanga ya asili
yaliyosababisha tatizo katika jamii Fulani haraka sana ilifikiriwa kuwa huenda
ni kwaajili ya dhambi nyingi huku wale walio salama wakidhani wako sawa na
Mungu ona mfano
Luka 13:1-5 “Na wakati uo huo walikuwapo
watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao
na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia,
Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya
wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi
nyote mtaangamia vivyo hivyo. Au wale
kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya
kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? Nawaambia,
Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.”
Unaweza kuona! majanga
yanapotokea na kuwapata watu haimaanishi kuwa wale waliopatwa na majanga ni
waovu kuliko wale waliokuwa salama dhana hii Yesu alikuwa akiifundisha na
kuwaelekeza watu kuwa wanapaswa kumzalia bwana matunda na kuacha kufikiri kuwa
changamoto wanazozipitia watu wengine zimetokana na dhambi, Yesu alionyesha
kuwa hitaji la toba ni hitaji la kila mmoja na hitaji la kuzaa matunda ni la
kila mmoja na hivyo majanga yanaweza yasiwe na uhusiano wa moja kwa moja na
hali ya dhambi au kiroho cha mtu husika
Ni katika dhana hiyo hiyo tunaona
kuna jambo ambalo lilijitokeza hali kadhalika wakati wa uponyaji wa kipofu
Batimayo wakati kipofu huyu alipokuwa anamuita Yesu na ikaonekana kana kwamba
Yesu anapita au kama hajali makutano waliokuwa wakifikiri vibaya waliona kuwa
Kipofu huyo anatakiwa kupambana na hali yake na kuwa hapaswi kumsumbua Yesu
wala Yesu hajali hali yake, Maandiko yanatutaarifu kuwa wakati Yesu anapita na
kipofu huyu anapaaza sauti yake kumuita makutano walimweleza wazi kwa kumkemea
anyamaze ni kama walikuwa wanamwambia acha usumbufu wako, Yesu hawezi
kushughulika na watu kama wewe pambana na hali yako ona
Marko 10:46-48a “Wakafika Yeriko; hata
alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano
mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando
ya njia. Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti
yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu. Na wengi wakamkemea ili
anyamaze,…..”
Unaona kutokana na dhana ya
kufikiri kuwa watu wenye ulemavu na changamoto mbalimbali na hata walio na
magonjwa ni kama wanaadhibiwa na Mungu kwaajili ya dhambi zao au za wazazi wao
au babu zao na kadhalika kwa hiyo maandiko yanaonyesha kuwa wengi wakamkemea acha
kelele zako, acha ujinga acha usumbufu hana mpango na wewe pambana na hali yako
katika lugha ya kiingereza tunaweza kusema hivi “A BLIND BEGGAR WAS HUSHED BY THE CROWD” ni kama sio kunyamazishwa
tu bali kunyamazishwa kwa ukali,kunyamazishwa kwa kunyanyaswa, ni ili unyamaze,
ukae kimya usisumbue, uache fujo tulia, shiiiiii, funga domo lako, nyamaza!
Katika hali moja ama nyingine katika maisha yetu inawezekana tumewahi kunyamazishwa
katika namna ya ukali kama ilivyotokea kwa kipofu Batrimayo, unaonywa kuto
kudai chochote kunyamaza na kulazimika kupitia au kipitishwa katika hali ambayo
watu wanataka, ni katika hali kama hiyo Batimayo alikuwa anakutana na
kipingamizi kikubwa cha kubakizwa katika hali ileile na jamii, hawataki asonge
mbele wanaona kama wale walio na miguu na macho wao ndio wanaostahili,
kuendelea mbele na Yesu na sio watu hovyo na wenye kutupwa na kudharaulika kama
kipofu Batrimayo! Jambo moja kubwa la msingi ni kuwa yeye
aliendelea kupaza Sauti akimuita Yesu! Akihitaji rehema zake !
Tabia ya Mungu wakati wa changamoto!
Ni muhimu kufahamu kuwa katika
mchakato mzima wa uponyaji wa Batimayo Yesu alionekana kama anapita na ni
kutokana na hali hii nadhani hata makutano waliomkemea Batimayo walikuwa
wanadhani kuwa hata Yesu hakuwa anajali hali aliyokuwa anaipitia kipofu, Yesu
ni mwana wa Mungu kufikiri ya kuwa Yesu hangemjali Batimayo ni kufikiri vibaya,
kufikiri kuwa Mungu hatujali ni fikra mbaya, ambayo iko kinyume na ukweli
kuhusu wema wa Mungu, wakati tunapoliitia jina lake na kuhitaji rehema zake na
kuona kama amekawia kuitikia na kudhani kuwa hajishughulishi tena na mambo yetu
ni dhana isiyofaa kitu kabisa; Mungu ni mwema wakati wote maandiko
yanatuthibitishia wazi ya kuwa anajishughulisha sana na mambo yetu ona
1Petro 5:6-7 “Basi nyenyekeeni chini ya
mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye
fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.”
Tofauti na mawazo ya Mwanadamu
Yesu alikuwa anapita huku anamwazia mema kipofu Batrimayo, kimsingi hata kupita
njia ile ilikuwa ni maalumu sana kwa Batimayo wala sio kwaajili ya umati
uliokuwa unamfuata, Ni huyu kipofu ndiye aliyekuwa amelengwa na Yesu siku ile
kwanini unawezaje kujua ? Yesu alisimama na alisimama maalumu kwaajili ya huyu
mtu mtu dhaifu, aliyekataliwa katika jamii na kudharauliwa masikini asiye na
msaada, Yesu alimjua alijua historia yake alifahamu mahitaji yake kamwe
hangeweza kumpita, wale watu kimsingi ndio waliokuwa vipofu hawakuweza kujua
imani ya Batrimayo wala hawakuweza kujua namna Mungu anavyoshughulika na
mahitaji ya watu wake. Mungu ana njia
zake na namna yake jambo jema hapa ni kuwa watu hawakumlaumu Yesu kama wakati
alipokuwa amelala katika boti ambapo wanafunzi walimlaumu kuwa Mwalimu si kitu
kwako kuwa tunaangamia? Na ni tofauti kiasi na alivyokuwa akishughulika na
mwanamke aliyekuwa akitoka na damu kwa kumgusa katika upindo, wanafunzi
walimshanga kuwa tunazungukwa na umati mkubwa je si rahisi kwako kuguswa rabbi?
Hapa Yesu alisimama na kuamuru kuwa mwiteni! kuna kitu kimejificha hapa kwenye
neno YESU AKASIMAMA katika lugha ya
kiyunani kusimama kwa Yesu nenola kiyunani linalotumika ni “HISTEMI” ambalo ni neno lililovutwaa kutoka kwenye
neno la kiyunani STAO katika lugha nzuri ya kuelewa kusimama kwa
Yesu hapa neno la kiingereza linaloweza kutumika hapa ni ESTABLISH STAND STILL, kwa hiyo neno STAO ni sawa na neno STAND
na neno HISTEMI ndio ESTABLISH STAND STILL kwa hiyo kwa Kiswahili kizuri ni kuwa YESU AKATAFUTA MAHALI PAZURI PANAPOFAA
KUSIMAMA, hivyo kimsingi sio kuwa Yesu alikuwa amekusudia kumpita Batimayo
lakini Yesu alikuwa anatafuta mazingira mazuri ya kusimama na kipofu ili aweze
kumuhudumia vizuri, Haleluya! Mwandishi
maarufu wa karne za mwanzoni mwa kanisa Mtakatifu Jerome anaeleza kuwa
Mazingira ya Yeriko ni yenye miamba na mawe ambayo yangeweza kusababisha
kujikwaa au kuanguka hivyo ni kweli kuwa
Yesu alikuwa anaangalia mazingira mazuri ya kusimama na mtu asiyeona ili waweze
kuzungumza vizuri na kwa kufanya hivi
alikuwa akiitimiza sharia ya Musa katika
Walawi 19:14 “Usimlaani kiziwi, wala usitie
kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi BWANA.”
Unaona wakati Mungu anaandaa
mazingira mazuri ya kushughulika na mtu huyu duni mwenye imani na utambuzi
mkubwa kuwa Yesu ni mwana wa Daudi, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa Batimayo
alikuwa ameamini kuwa Yesu ni Masihi, Unadhani Yesu angemuachaje? Yanenaje maandiko? na kila amwaminiye
hatatahayarika! katika wakati huo tayari
watu wameshapata dhambi kwa kufikiri kuwa (Yesu) Mungu alikuwa hamjali na wala
hakuwa na mpango naye, au kusaidia kumnyamazisha Batrimayo. Mungu alikuwa anaandaa mazingira, acha kuimba
usinipite mwokozi, yeye huwa hampiti Mtu mwenye uhitaji na anayemuamini na watu
wanyamaze kimya wakati Bwana anashughulika na watu wake maana unaweza kujikuta
unatengeneza dhambi wakati Kristo anaandaa mazingira mazuri ya kusema na mtu
wake, kwa muda sahihi na mahali sahihi ili akutane na mahitaji yake, watu wale
wale waliokuwa wakimkemea na kumwambia nyamaza ni hao hao waliomwambia
changamka jipe moyo inuka anakuita, Kwa kawaida kuna watu wengi sana vipofu
walioponywa na Yesu lakini hawakutajwa kwa majina yao Huyu alikuwa anatupa somo
muhimu sana ndio maana anatajwa kwa jina lake alimuamini Yesu kuwa ni Masihi,
Yesu alitengeneza mazingira ya kuzungumza na mtu huyu muhimu kwake kuliko wote
wakati wao walikuwa wakimuona hana maana hana faida, Yesu aliwafunga mdomo nao
wakamwambia jipe moyo inuka anakuita haleluya ! Yesu ni Mungu mwenye moyo wa
ajabu na huruma sana! Anajali, alimjali.
Mambo ya kujifunza kutoka kwa Batimayo
Kuna mambo mengi ya kujifunza
kutoka katika muujiza huu yako mengi, habari hii inatufunza mengi kwanza wako
marafiki au watu ambao sio wazuri kwetu na wasiotutakia mema wanataka
tusifanikiwe na tubaki katika hali ile ile tuliyo nayo, watatusaidia kutoa
majibu ambayo wala sio majibu ya Mungu,
wanatuzuia kwenda kwenye mwelekeo sahihi wakijua wazi kabisa kuwa ndio
mwelekeo wa mafanikio yetu, je unadhani watu wale walikuwa hawajui kuwa Yesu
anaponya vipofu? Unadhani walikuwa hawajui kuwa Yesu ameponya vipofu wengi
sana? Na je unadhani walikuwa hawaoni ya kuwa Batrimayo ni Kipofu na unadhani
walikuwa hawajui kuwa siku ile ilikuwa siku nzuri sana kwa Batrimayo kuponywa
kwa vile Yesu alikuwa Yeriko siku ile?
Kumbuka watu ni wale wale ambao tunapolia wanatuambia nyamaza, ashukuriwe Mungu na aendelee kuwatunza kwani
Mungu atageuza mambo hao hao waliokuwa wakikuambia nyamaza ndio watakaokuja
kusema jipe moyo inuka anakuita ! Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Batrimayo!
Usikubali mtu yeyote
akunyamazishe au akuhesabu kuwa wewe ni wa kutupwa wakati Yesu Kristo amekuja
kwaajili yako. Batrimayo ashukuriwe Mungu hakuwajali watu wanamwambia nini yeye
aliendelea kumtazama Yesu tu na kulilia Rehema kutoka kwa Masihi mwana wa
Mungu!
Uhusiano wako na Yesu ni wa
tofauti haufannani na wa mwingine wengine wanafikiria kuwa hakujali! wewe
endelea kumtazama kama mwenye kujali na utangundua kuwa kumbe yuko kwaajili
yako
Linapokuja swala la wewe na
maisha yako na Mungu usiangalie umati unasemaje, Mungu haabudiwi kwa mkumbo uwe
na msimamo wako wa kipekee kuhusu Mungu, Batrimayo kwake Yesu ni mwana wa Daudi
nani pekee mwenye kutoa rehema
Watumishi wa Mungu ni lazima
waandae mazingira mazuri kwaajili ya huduma za uponyaji, nguo za kuwafunika
wanaoangushwa na mapepo, wahudumu watakaosaidia kuwahifadhi wanaodondoshwa,
mazingira yatakayosaidia kutunza usafi wao na kadhalika Yesu hakutaka Batrimayo
ajikwae kwenye mawe alitafuta mazingira mazuri.
Mungu habadiliki, yeye ni yule
yule jana, leo na hata milele, yeye ndiye mwenye kipimo cha wema wetu, matendo
yetu yawe sawa na kile anachotuelekeza yeye na sio kwenye dhana za watu na yale
wanayoyafikiri, wakatim Batrimayo akiwa katika changamoto hii ni ukweli ulio
wazi kuwa walioelewana Lugha pale alikuwa Yesu mwenyewe na Batrimayo wengine
walitoka kappa, ninapopita katika mapito ninayoyapitia na hali yoyote ile
ninayoipitia anayeweza kunielewa vizuri mi Mungu na mimi ninayeipitia ile hali
ninyi wengine kaa kimya msininyamazishe ninapomtafuta Bwana wangu,
msininyamazishe ninapopiga kelele wala Mungu wangu hanipiti anaaandaa mazingira
salama na ya utulivu nipige naye stori nimueleze ninayo yahitaji ana rehema
hataniacha yatima hali hii baadaye utakuja kugundua kuwa kumbe mimi na Yesu
tunaelewana vizuri sana kuliko umati huu. Yawezekana unapitia katika changamoto kadhaa
wa kadha na unadhani Yesu amekupita au hakujali na watu wanapata nafasi ya
kukudhihaki wanatamani ubakie katika hali hiyo hiyo, hawataki ukutane na Yesu
akusaidie nataka nikuambie wewe endelea kupiga kelele na kumwambia mwana wa
Daudi unirehemu, ususeme usinipite mwokozi kwani yeye hapiti mtu anayemwangalia
na kumlilia Rehema zake naye ataandaa mazingira na watu wale wale wanaosema
nyamaza watapiga kelele Jipe moyo inuka anakuita! haleluyaa
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni